Tuesday, May 14, 2013

ZITTO KABWE AZILIPUA KAMPUNI ZA SIMU KUHUSU WIZI WA RINGBACK TONES.

 
Mbunge wa Kigoma Kaskazini Mh.Zitto Zuberi Kabwe (CHADEMA) ametoa pendekezo binafsi kuhusu miito ya simu na kusema kuwa ni wizi kama ifuatavyo:-
#RBT #COSOTA #Transparency #FairRevenueShare kesho Bajeti ya Wizara ya Biashara ambapo COSOTA ipo. Pendekezo langu kuhusu biashara ya Ringtone

PENDEKEZO BINAFSI LA MBUNGE KUHUSU KUZUIA UNYONYAJI DHIDI YA WASANII WA TANZANIA KATIKA BIASHARA YA MIITO (RING BACK TONES)

Kwenda kwa: DR ABDALLAH KIGODA, Waziri wa Viwanda na Biashara

Kuhusu: BIASHARA YA MIITO YA SIMU (RINGBACK TONES)

Kumekuwa na malalamiko makubwa sana kuhusu biashara ya mauzo ya nyimbo kama miito kwenye simu. Malalamiko haya yalianzia kwa wasanii wenyewe na baadaye mimi binafsi niliwasilisha hoja zao Bungeni mwaka 2012. Hata hivyo, hadi sasa malalamiko haya bado hayajapatiwa ufumbuzi na hivyo wasanii kuendelea kunyonywa. Tatizo kubwa katika biashara hii ni USIRI na UNYONYAJI kwa wasanii wa Tanzania. Suala la USIRI lipo Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia. Suala la Unyonyaji lipo Wizara ya Viwanda na Biashara.

USIRI
Biashara hii ya “Ring Back Tones” (RBT) hufanywa na Kampuni za simu (Network providers) kwa kununua maudhui kutoka wachuuzi (Content Providers) ambao nao huingia mikataba na Wasanii (Content Creators).
Hakuna sheria yoyote au Kanuni hapa nchini inayoongoza biashara hii na hivyo “Network providers” na “Content Providers” kuwa watu pekee wenye taarifa zote za biashara hii. Kampuni za simu hujumuisha mapato ya biashara hii na mapato yake mengine (Not Ringfenced), hawatoi taarifa za manunuzi ya nyimbo (au ‘content’ nyingine yeyote) kwa wadau na hasa wasanii. Wachuuzi (Content Providers) nao hawatoi taarifa za mauzo kwa wasanii na wanatumia uelewa mdogo wa wasanii kuwasainisha mikataba inayowanyonya. Matokeo yake ni kwamba msanii hupata kiasi cha asilimia mbili tu (2.5%) ya mapato ghafi ya kazi yake. Hivi sasa biashara hii inathamani (turnover) ya takribani shilingi 44 bilioni kwa mwaka.

Suluhisho:
Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano iandike kanuni (regulations) zitakazolazimisha makampuni ya simu kuweka wazi mapato yatokanayo na biashara ya RBT (Miito ya simu) kila baada ya miezi 4 (disclosure rules). Kanuni hizi zielekeze makampuni kutoa taarifa za mauzo kwa kila kazi (nyimbo/vichekesho etc.)

UNYONYAJI
Kutokana na usiri ulioelezwa hapo juu, wasanii wamekuwa wakinyonywa kimapato. Kwa mfano Msanii hulipwa mapato yatokanayo na ununuzi wa awali wa kazi yake (wimbo) katika mwezi (downloads).

Lakini mapato yatokanayo na “subscriptions” ambapo mlaji hukatwa shilingi 30 kila siku msanii hapati chochote. Hivyo katika mapato ya sh. 1,300 kila mwezi kwa kila mteja kwa kila wimbo, msanii hupata mgawo wake kutoka shilingi 400 tu za ‘downloads’ na ndio maana wasanii wote nchini hupata 2.5% ya shilingi 44 bilioni zinazokusanywa na Kampuni za Simu.

Nchini Marekani biashara ya miito ya simu (RBT) imetafsiriwa kama maonyesho (Public Performances) na hivyo “copyright Association” ya Marekani imeweka kiwango cha chini cha mrahaba (royalty) ambacho msanii hulipwa. Marekani msanii hulipwa asilimia 10 ya patoghafi linalozalishwa na kazi yake kama muito wa simu.

SULUHISHO
Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara iandike kanuni kwamba mauzo ya kazi za wasanii kama miito ya simu inachukuliwa kama ‘performance’ na kwamba Kampuni za simu zitalipa sio chini ya asilimia 12 (12%) ya mapato ghafi, ambapo asimilia 10% itakwenda kwa msanii na asilimia 2% COSOTA kwa ajili ya usimamizi na Ulinzi wa kazi za Wasanii.

HITIMISHO
Kanuni za Uwazi (disclosure rules) katika biashara hii ya ‘Ring Back Tones’ na mgawo wa haki wa mapato (fair and just revenue share) ndio suluhisho endelevu na litakaloleta tija kwa wasanii wa Tanzania na hata Serikali kukusanya mapato stahili. Kanuni (Regulations) zinazopendekezwa zianze kutumika kuanzia tarehe 1/7/2013

Kabwe Z. Zitto, Mb
Kigoma Kaskazini
Dodoma, 13 Mei 2013.
 
Source:Zitto's social media

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...