Friday, May 31, 2013

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHE. SYLVESTER MHOJA KASULUMBAYI (MB) KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2012/13 NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA WIZARA YA MAENDELEO YA MIFUGONA UVUVI KWA MWAKA WA FEDHA 2013/14 (Inatolewa chini ya Kanuni ya 99 (9), ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Mwaka 2013)

A: UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, dira ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ni kuhakikisha kuwa raslimali za mifugo na uvuvi zinaendelezwa na kutunzwa katika mazingira endelevu kwa ajili ya ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.  Aidha dira inalenga kuhamasisha ufugaji wa kisasa na uvuvi endelevu ili kujenga uchumi endelevu kwa jamii nzima ya wafugaji na wavuvi na taifa kwa jumla.
Mheshimiwa Spika, Licha ya ukweli kwamba wafugaji na wavuvi wana mchango mkubwa katika uchumi wetu, Serikali hii ya CCM imeshindwa kuwapatia maeneo maalum kwa ajili ya malisho kwa maendeleo ya mifugo yao. Wafugaji wamekuwa wakihamishwa na au wakifukuzwa kutoka eneo moja la nchi hadi eneo lingine kama vile hawana haki ya kufanya shughuli za kiuchumi kama ufugaji katika nchi yao. Ni aibu kwa  Serikali kushindwa kuwapatia wafugaji mahitaji muhimu ambayo yangepelekea ufugaji wao kuwa wa kisasa, kibiashara na endelevu kama ilivyobainisha katika dira ya Wizara hii.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, haioni sababu ya Serikali kuwapatia wafugaji maeneo ya kufugia  kwa kuwa wafugaji wangeweza  kuingia ubia na mashamba makubwa ya mifugo ambayo yalikuwa yanamilikiwa na Ranchi za Taifa, lakini kutokana na ubinafsi na ufisadi uliofichwa kwenye kivuli cha cha sera ya ubinafsishaji,  Serikali ya CCM imesimamia zoezi la  viongozi wa serikali na Chama cha Mapinduzi wakigawiana ranchi hizo na kuwaacha wafugaji wakifukuzwa ovyo na kupewa jina la wachungaji.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa wavuvi hali ni hiyo hiyo,  kwani mapato mengi ya Serikali  yanayokusanywa kutoka katika sekta ya uvuvi yanatokana na wavuvi wadogo ambao mara zote wao ndio waathirika wa mfumo kandamizi wa Serikali.  Zana za uvuvi zinapokamatwa, wao ndio wanapata hasara, lakini wauzaji wa zana hizo za uvuvi  wala hawaulizwi na wala hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi yao.
 Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa inayozikabili sekta hizi za ufugaji na uvuvi ni kwamba sekta  zote mbili hazina bima dhidi ya  majanga ambayo yanaweza kutokea.  Katika mazingira kama haya, dhana ya kuwa sekta za kisasa, kibiashara na endelevu inakuwa ngumu sana.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa mwaka wa fedha 2012/2013 liainisha mapungufu makubwa katika ya kiutendaji na kiuwajibikaji kwa wizara hii na kuitaka Serikali kufanya mambo yafuatayo:
1.      Kuwajibika kwa uzembe wa kuitelekeza meli ya uvuvi ya Tawariq iliyokamatwa ikifanya uvuvi haramu katika ukanda wa bahari ya hindi hadi meli hiyo kuharibika kabisa na kuanza kuzama bila faida yoyote?
2.      Kuchukua hatua dhidi ya mwekazaji wa Kagera Sugar kwa kushindwa kuendeleza shamba la ukubwa wa hekta 45,000 (sawa na ekari 112,500) kinyume na mkataba.
3.      Kueleza sababu za kuwapa mashamba makubwa wawekezaji wa kigeni na kuwanyanyapaa wafugaji wa asili kinyume cha sheria.
4.      Kutatua migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji ambayo mara kadhaa imesababisha uvunjifu wa amani na umwagaji damu miongoni mwa wananchi.
5.      Kujenga viwanda vya kusindika nyama katika mikoa ya wafugaji ili kuongeza thamani ya bidhaa ya nyama na hivyo kukuza uchumi.
6.      Kuweka wazi kiasi cha fedha kinachopatika kama mrahaba kutokana na uvuvi katika bahari kuu, pamoja na fedha za leseni kwa meli zinazofanya uvuvi katika ukanda wa bahari kuu.




  1. SEKTA YA MIFUGO
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Mifugo ina nafasi kubwa katika kujenga uchumi imara wa Taifa, kuongeza kipato kwa Watanzania wanaotegemea mifugo, na kutoa fursa za ajira sanjari na kuhifadhi rasilimali za Taifa. Sera ya mifugo inaeleza nia ya Serikali na wadau wengine katika kukabiliana na changamoto zinazokabili Sekta ya Mifugo. Lengo kubwa ni kujenga mazingira mazuri yatakayotoa fursa za kuongeza kipato na ajira kwa wafugaji wadogo, kufuga kibiashara na kuongeza ajira. Ili kufikia haya Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutekeleza, malengo makuu matatu ya kisera kama ifuatavyo:-
  1. Kuendeleza Sekta ya Mifugo itakayokuwa na mwelekeo wa kibiashara, yenye ufanisi na itakayohimili ushindani wa kimataifa;
  2. Kuibua mifumo bora ya uzalishaji itakayoongeza tija miongoni mwa wafugaji wadogo na wa asili.
  3. Kuhifadhi rasilimali za mifugo na kuunda sera na taasisi zitakazosimamia maendeleo na matumizi endelevu ya rasilimali hizo n.k.
Mheshimiwa Spika, Sera hiyo ya mifugo imeweka wazi azma ya Serikali ya kuboresha sekta hii ya mifugo, lakini kutokuwepo na mkakati madhubuti wa kufanikisha yale yote yanayohitajika kufanyika na sera hii ya Mifugo ya mwaka 2006, kunaendeleza matatizo katika sekta hii mpaka sasa.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Mifugo hapa nchini ina nafasi kubwa katika ujenzi wa uchumi wa Taifa. Kwanza kwa kuthamanisha kiwango cha nyama kinachotumika kila siku hapa nchini ikiwa  kiwango hicho kingekuwa kinaagizwa toka nje ya nchi. Pili ni kuongeza kipato kwa Watanzania wanaotegemea mifugo, na kutoa fursa za ajira sanjari na kuhifadhi rasilimali za Taifa.
Mheshimiwa Spika, Mashamba makubwa ya mifugo yana uwezo wa kuongeza viwango vya uzalishaji na uuzaji wa mifugo na mazao yake nje ya nchi, ajira na kuboresha maisha ya wafanyakazi wake. Mkakati umetumika wa kugawa mashamba makubwa ya Kampuni ya Ranchi za Taifa KARATA (NARCO) na yale yaliyokuwa chini ya Kampuni ya Ng’ombe wa Maziwa (DAFCO) kuwa mashamba yenye ukubwa wa kati kwa ajili ya ufugaji wa kibiashara unaolenga kutekeleza dhana hii. Mkakati huu umeongeza upeo wa umilikaji mashamba na pia kuwawezesha Watanzania kuingia katika ufugaji wa kibiashara. Maeneo ya ranchi za KARATA (NARCO) yaliyobaki yataendelea kutumika kama ranchi za mfano na maeneo yasiyo na magonjwa ya mifugo kwa ajili ya soko la nje ya nchi[1].
Mheshimiwa Spika, ilani ya CCM ya mwaka 2005-2010 aya ya 32 inasema kwamba,  Pamoja na kwamba Tanzania ina mifugo mingi sana; mchango wa mifugo kwenye uchumi wa Taifa ni mdogo. Kwa lengo la kuendeleza Sekta ya Mifugo ili ichangie zaidi ukuaji wa uchumi wa Taifa na kuwaongezea kipato wafugaji, Serikali za CCM zitaendeleza kwa msisitizo zaidi lengo la kuzingatia zaidi ubora kuliko wingi pekee katika ufugaji. Ili kufikia lengo hilo, hatua zifuatazo zitachukuliwa katika kipindi cha 2005-2010:-
(a)               Kujenga mazingira ya kuvutia uwekezaji katika viwanda vya kuongezea thamani mazao ya mifugo kama vile ukataji nyama, usindikaji wa maziwa, utengenezaji wa bidhaa za ngozi n.k.”
Mheshimiwa Spika, na katika Ilani ya CCM ya mwaka 2010-2015 aya ya 38 inasema  kwamba; Katika kipindi cha Ilani hii ya miaka 2010-2015, Chama Cha Mapinduzi kitazielekeza Serikali kuiendeleza sekta ya mifugo kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi ili kuiwezesha kutoa mchango mkubwa kwenye pato la Taifa kwa kuchukua hatua zifuatazo:-
(a) Serikali iandae programu kabambe ya kuendeleza sekta ya mifugo na ufugaji. Programu hiyo ijumuishe pamoja na mambo mengine masuala ya uendelezaji wa maeneo ya malisho, kuchimba na kujenga malambo, mabwawa, majosho na huduma za ugani ili hatimaye wafugaji waondokane na ufugaji wa kuhamahama.
(b) Benki ya Kilimo itakayoanzishwa iwe pia Benki ya Mifugo ili iweze pia kutoa mikopo kwa wasomi wenye nia ya kufuga na kuwawezesha kuingia kwa wingi katika ufugaji wa kisasa.
(c) Kuelimisha wafugaji uwiano kati ya idadi ya mifugo na eneo.”
Mheshimiwa Spika, katika kuonyesha kuwa CCM yale wanayoandika sio wanayosimamia katika kuinua sekta ya ufugaji hasa wa asilia ambao unachangia zaidi ya asilimia 85 ya ufugaji wote, Kambi Rasmi ya Upinzani, inauliza kwa mkakati huo wa CCM dhidi ya wafugaji na Ufugaji ni kwa vipi ufugaji unaweza kuwa endelevu na wa kisasa wakati wafugaji wanaporwa maeneo ya kulishia mifugo yao, hawapewi maeneo ya malisho, hawapati huduma za ugani, hawapati mikopo na hawana soko la uhakika wa bidhaa zinazotokana na mifugo. Kambi Rasmi ya Upinzani, inauliza kwa makati huo wa CCM dhidi ya wafugaji na ufugaji ni kwa vipi ufugaji unaweza kuwa endelevu na wa kisasa wakati wafugaji wanaporwa maeneo ya kulishia mifugo yao?. Hawapewi maeneo ya malisho, hawapati huduma za ugani, hawapati mikopo, hawana soko la uhakika. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa kauli juu ya ni wapi wafugaji wa asili watafugia mifugo yao ili kuwa endelevu nay a kisasa?
 jumla ya wafugaji wakulima wa vijiji vinne vya Makuyuni, Loikisale, Naiti na Mswakini katika Wilaya ya Monduli wanatishiwa kuhamishwa kutokana na mkakati mahususi ulioasisiwa na Mheshimiwa Waziri Kagasheki wa kutangaza maeneo hayo kuwa ni Wildlife Management Area (WMA). Uhakika ni kwamba WMA hiyo ni hewa haipo na ukweli ni kwamba eneo hilo kinapewa kikundi kinachoitwa ELEWANA AFRIKA.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwaeleza Wafugaji hao, ni wapi wanakwenda na mifugo yao? Aidha, kwa kuwa utaratibu wa kuanzisha WMA huwa inaanzishwa kwa kupata ridhaa za wanavijiji ambao kwa hiari yao wanatoa maeneo ya vijiji vyao kuwa WMA na ndipo kazi ya Waziri husika inafuata ya kutoa idhini ya uanzishwaji wa hiyo WMA.  Kwa kuwa huo ndio utaratibu wa kuanzisha WMA, Je, ni kwanini vijiji hivyo havikupewa fursa hiyo?
Mheshimiwa Spika, Mgogoro wa ardhi katika eneo la Loliondo ni taswira nyingine ya jinsi ambavyo Serikali ya CCM imekiuka haki za wafugaji wa Kimaasai kwa manufaa ya wawekezaji wa kigeni katika sekta ya uwindaji wa kitalii.
Mheshimiwa Spika, mgogoro wa Loliondo bado haujapatiwa ufumbuzi na sasa umeanzishwa mgogoro mwingine Wilaya ya Monduli. Hii ni kwa makusudi kuhakikisha wafugaji wa asili wanakwisha kabisa?
Mheshimiwa Spika, hapo kabla ya uhuru  Serikali ilitenga eneo la zaidi ya hekta 18,000 sawa na ekari 45,000 wilayani Maswa lililojulikana kama SHISHIYU Holding ground kwa ajili ya kunenepesha mifugo kabla ya kusafirishwa kwenye kiwanda cha Nyama cha Tanganyika Packers, ambacho kimekufa, cha ajabu ni kwamba katika eneo hilo bado hadi sasa wafanyakazi wa Idara ya mifugo wapo pale lakini mifugo hainenepeshwi. Je, hii si hujuma kwa sekta ya mifugo na wafugaji hasa wa wilaya ya Maswa?
Mheshimiwa Spika, si hilo tu bali pale Ipala wilaya ya Nzega Mkoa wa Tabora kuna kituo cha treni kilichokuwa kikitumika kupakia ng’ombe kwenda Dar es Salaam. Eneo hilo lilikuwa limetengwa rasmi kwa ajili ya mifugo na kuna miundombinu ya kupakia mifugo kwenye treni, jambo la ajabu ni kwamba serikali imeligeuza eneo lile kuwa hifadhi ya misitu. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwa wafugaji wanaoishi eneo hilo waachiwe eneo litumike kwa malisho na miundombinu iliyopo.
Mheshimiwa Spika, aidha, kitendo kinachofanywa na Wakuu Wilaya na Wakurugenzi wa Halimashauri kuwahamisha wafugaji kwa nguvu katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kuwalipisha mamilioni ya fedha wafugaji hao (Mfano mfugaji mmoja wa mikumi alitozwa faini ya shilingi milioni 42.78 kwa kukamatwa ng’ombe wake, mfugaji wa chunya million 19 n.k) nao ni ushahidi wa dhahiri kwamba Serikali hii ya CCM haina dhamira ya dhati katika kuhakikisha wafugaji na ufugaji unakuwa na tija katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, wafugaji wa asili ya kisukuma,kimasai,wairaq na wabarbaig katika wilaya za Kilombero, Ulanga, Kilosa, Mbarali, Chunya, Kilindi, Handeni,Mpanda, Rufiji n.k  wamepata matatizo makubwa sana na wengine wameuawa na vyombo vya dola, kosa lao kubwa ni kuwa na mifugo mingi iliyosababisha wahame toka mikoa ya kanda ya ziwa kwa sababu za malisho. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge, je kosa la ndugu zetu hao ni kuwa na utajiri wa mifugo mingi au nini hadi wanadharauliwa na kunyanyaswa na kufanywa kuwa watanzania wa daraja la nne katika nchi yao?
Mheshimiwa Spika, kutokana na ukweli kwamba Wizara imeshindwa kuwatetea na kuwalinda wafugaji wa asili, hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali iwaeleze wafugaji ni wizara gani itakayosikiliza na kutatua matatizo yao?
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo imekuwa ikitokea katika maeneo ya Ranchi zilizokuwa za mkoa wa Kagera, Rukwa, Morogoro, Tanga, Pwani watu waliopewa 4000 ha au ekari 10,000 za maeneo ya Ranchi za Taifa kama wawekezaji, watu hao wameshindwa kuziendeleza ranchi hizo kwa vile wengine hawana hata mifugo ya kuweka katika maeneo hayo. Kukosa mifugo ya kuendeleza eneo hilo kwa makusudi watu hao huona kuwa mbadala unaobakia ni kupangisha maeneo hayo kwa wawekezaji kutoka nchi jirani.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona lingekuwa ni jambo la busara kama ushirika wa wafugaji au mwekezaji mmoja mmoja kupewa  ekari 1000  ikiwa eneo lote la  ekari 10,000 lingegawanywa ili kurahisisha uwekezaji wake na kufanya kuwa endelelevu. Kwa eneo dogo uwezekano wa kupata mkopo toshelezo kwa uwekezaji toka benki zetu na asasi zingine za fedha ni rahisi kwani hata investiments risks inakuwa ni ndogo na inakuwa imesambaa kwa wawekezaji wengi.
Mheshimiwa Spika, wakati Waziri akijibu swali Na. 26 kuhusu maeneo ya Ranchi za Mkoa wa Kagera, “Je, kwa nini Serikali isiyarudishe maeneo hayo kwani waliopewa wanayakodisha kwa wafugaji toka nchi jirani?  Je, ni Watanzania gani kwa majina waliogawiwa maeneo kwenye ranchi hizo? Mheshimiwa Spika, orodha ya majina ya Wawekezaji Watanzania waliogawiwa maeneo hayo ya ranchi ipo, nitaomba kukutana na Mheshimiwa Mbunge baada ya hapa ili nimkabidhi orodha hiyo”.
 Mheshimiwa Spika, hadi sasa hivi majina hayo ya wamiliki, Waziri ameshindwa kuitoa kama alivyoahidi ndani ya Bunge, hoja ni kama kweli wamiliki ni watanzania ni kwanini wanashindwa kuweka majina hadharani? Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Waziri kutoa kwa wabunge majina hayo ya wamiliki na uraia wao hadharani.
Mheshimiwa Spika, ili kuiwezesha sekta ya mifugo kutoa mchango stahiki kwa Taifa hili ni lazima uboreshaji katika sekta ya mifugo wetu ufanyike kwani wanachokosa wafugaji wetu ni Ardhi na elimu ya ufugaji yenye mafanikio kutokana na kutumia mbinu za zamani za kuzalisha mifugo. Changamoto kubwa katika sekta hii ni kukosekana kwa mbinu za kisasa, vifaa na madawa ya uhakika kuhudumia wanyama. Aidha, mifugo mingi inatunzwa kienyeji na matokeo yake kukosa soko la kimataifa kama zilivyo nchi nyingine. Kama elimu ya kutosha itatolewa na kuruhusu wawekezaji wa ndani katika sekta ya mifugo changamoto hizo zitapungua kwa kiasi kikubwa na hivyo kutoa nafasi ya ongezeko la bidhaa zitokanazo na mifugo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema wawekezaji wa ndani, kwa maana kwamba wafugaji wa asili wao mtaji wao mkubwa ni mifugo na NARCO wao mtaji wao ni utaalam na miundombinu iliyopo tayari. Hivyo basi, ni rahisi wa ubia huo kati ya wafugaji wa asili na NARCO kuleta tija zaidi kuliko mwekezaji toka nje.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu, kipato na ukuaji wa miji kwa nchi zinazoendelea Duniani, Tanzania ikiwa ni mojawapo, mahitaji ya bidhaa za mifugo nayo yamekuwa yakiongezeka pia. Takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania pekee itaongeza mahitaji mara nne kwa mwaka 2030. Hivyo ni jukumu la Serikali sasa kulieleza Bunge hili ni kwa vipi Wizara imejipanga kukabiliana na changamoto ya ongezeko hilo la mahitaji ya nyama kwa muda huo?
Mheshimiwa Spika, hivi sasa ni 2% tu ya mifugo yote inayozalishwa na kufugwa kibiashara, hivi sasa Tanzania ina machinjio ya kisasa manne (4) ambayo hayatoshelezi kwani mahitaji ya nyama safi na salama yanaongezeka kila siku. Aidha, inaonyesha kuwa chini ya 1% ya nyama yote iliyosindikwa ndiyo inazalishwa hapa nchini na sehemu yote iliyobaki inaagizwa na kuingizwa nchini kutoka Kenya. Vile vile taarifa hiyo inaonyeshwa kuwa zaidi ya tani 700 ya nyama safi inaaagizwa toka nje ya nchi kila mwaka wakati mahitaji ya nyama ndani ya nchi na Kanda yetu ya ushirikiano yanazidi kuongezeka[2].
Mheshimiwa Spika, Tanzania ni nchi ya pili nyuma ya Ethiopia kwa kuwa na mifugo wengi katika Bara la Afrika, sasa kwa hali ya kawaida tu inakuwaje nchi yetu inaagiza nyama kutoka nje ya nchi?
Mheshimiwa Spika, Tanzania ina rasilimali kubwa ya maliasili ikiwemo ardhi, malisho na idadi kubwa ya mifugo. Kati ya jumla ya hekta milioni 94 za rasilimali ya ardhi, hekta milioni 60 ni nyanda za malisho zinazofaa kwa ufugaji. Kwa sasa kuna ng’ombe milioni 21.3, mbuzi milioni 15.2 na kondoo milioni 6.4.  Mifugo wengine ni pamoja na nguruwe milioni 1.9, kuku wa asili milioni 58[3].
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa mpango na bajeti ya mwaka 2012/2013 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2013/2014 kiambatanisho Na.3 kinaonyesha kuwa kwa mikoa 21 wilaya 69 na vijiji vilivypimwa 479 eneo la malisho ambalo linasadikiwa kuwa limetengwa kwa ajili ya wafugaji kuwa ni hekta milioni 1.28. Hii ni sawa na asilimia 2.13 ya hekta million 60 za nyanda za malisho katika nchi hii.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Mhe Waziri awaeleze wafugaji kwa ng’ombe milioni 21.3 na mbuzi na kondoo milioni 21.5 wanatakiwa wachungwe kwenye eneo la ukubwa gani?
Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa mifugo umegawanyika katika mifumo mikuu miwili ambayo ni ufugaji huria na ufugaji shadidi. Mfumo wa ufugaji shadidi japo sio mkubwa nchini, unatiliwa mkazo zaidi katika kuendeleza ufugaji na uwekezaji kwani unachangia zaidi kwenye uchumi wa soko.
Mheshimiwa Spika,  kwa upande mwingine, mfumo wa ufugaji huria ambao hufanywa na wakulima-wachungaji na wachungaji -wahamaji, ni mfumo unaotegemea upatikanaji wa malisho na maji kwa msimu na matokeo yake husababisha wafugaji kuhamahama. Mfumo huu unakabiliwa na matatizo ya utunzaji duni wa mifugo, matumizi duni ya teknolojia za kisasa, kuhodhi mifugo wengi zaidi ya uwezo wa ardhi na ukosefu wa mazingira mazuri ya masoko.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa tafiti uliofanywa na asasi ya kiraia ya Tanzania Pastoralists, Hunters and Gatherers Organization(TAPHGO) kuhusu mfumo wa biashara ya mifugo Tanzania inaonyesha kwamba sekta ya ufugaji Tanzania inachangia asilimia 18 ya pato la Taifa,  uzalishaji wa nyama kwa mwaka unakadiriwa kuwa ni tani 259,800, kwa mifugo inayofugwa kwa ajili ya nyama pekee huchangia tani 181,800.
Mheshimiwa Spika, aidha mchango wa wafugaji ambao pia ni wakulima huchangia asilimia 98 ya uhitaji wote wa nyama hapa nchini, huku asilimia 2 hutoka kwenye ranchi za taifa. Wakati mbuzi na kondoo huchangia tani 75,800. Thamani ya nyama inayozalishwa  inakadiriwa kuwa ni shilingi bilioni 727.44, kati ya hizo shilingi bilioni 537.94 zinachangiwa na nyama ya ng’ombe na zilizobaki shilingi bilioni 189.5 ni kwa mbuzi na kondoo.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Rais wakati wa kufungua  mkutano wa uwekezaji kwa shabaha ya kuibua maendeleo ya Mkoa wa Mara kwa kutumia rasilimali na utajiri uliopo mkoani Mara “Lazima tuanze kutekeleza misingi ya ufugaji wa kisasa na tujipange vizuri kwa uwekezaji kwenye sekta hii. Naomba tutenge maeneo maalum ya ufugaji wa kisasa. Kwa mfano, tukigawa maeneo ya ukubwa wa hekta 2,000 kila moja na tukawagawia watu kwa ajili ya kufuga kisasa. Watakaopewa maeneo hayo wahimizwe na kusaidiwa wayaendeleze kwa malisho na huduma muhimu za maji, majosho pamoja na za matibabu kwa mifugo. Maeneo hayo yakatumiwa kunenepesha ng’ombe wa nyama tunawezesha kuwepo kiwanda cha nyama kitakachonunua toka kwao mifugo ya kuchinja. Kiwanda hicho kitatengeneza soko la uhakika kwa wafugaji”.
Mheshimiwa Spika, kauli hiyo ya Mhe Rais imekuja muda ambao tayari maeneo mengi mazuri yaliyokuwa yanamilikiwa na Serikali tayari yamekwishachukuliwa, na kama utaratibu ambao tumejaribu kuutolea maelezo kwa kuangalia Ranchi za Mkoa wa Kagera jinsi gani migogoro iliyopo haimaliziki kutokana na ukweli kwamba wahusika wakuu katika migogoro hiyo ni watendaji wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, Changamoto kubwa inayoikabili tasnia ya mifugo ni namna ya kufikia viwango vya ubora wa mifugo na mazao yake vitakavyokidhi mahitaji ya soko la kikanda na kimataifa.
Mheshimiwa Spika, katika kuonyesha kuwa watendaji wanashindwa kutenganisha kati ya machinjio ya kisasa na viwanda vya kusindika ni pale, Waziri alipokuwa anajibu swali namba 27 kwa mujibu wa Hansard, “Je, hivi sasa kuna viwanda vingapi vya nyama na vinasindika kiasi gani cha nyama?” Jibu la Waziri lilikuwa “Mheshimiwa Spika, Tanzania inahitaji viwanda ama machinjio makubwa takribani 16 yenye uwezo wa kuzalisha nyama tani 133 kwa siku kwa kila kiwanda au kila machinjio”
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasisitiza tena ni kwa njia zipi utekelezaji wa Ilani unaweza kufikiwa kama tafsiri ya kiwanda cha kusindika nyama na machinjio inaonekana kuwa ni kitu kimoja?
Mheshimiwa Spika, kwa hali ya kawaida ng’ombe wa asili hutoa maziwa 0.5ltr kwa siku wakati yule wa kisasa anatoa kati ya lita 7-30ltrs kwa siku kutegemea na matunzo na elimu ya ufugaji aliyonayo mfugaji.  Hivyo basi ili mfugaji wa ng’ombe za asili aweze kupata lita 30 za maziwa kwa siku atahitaji kuwa na ng’ombe 15. Mbali na mambo hayo yote ambayo yataenda na uwiano huo lakini jambo la muhimu kwa mfugaji wa asili ni kwamba madawa yanayohitajika kwa  chanzo, kuosha na kutibu magonjwa ni zile zile kwa ng’ombe wote wa asili na wa kisasa.
  1. HUDUMA ZA UGANI
Mheshimiwa Spika, ili sekta hii ya mifugo iweze kuleta tija inayokusudiwa huduma ya ugani ni muhimu sana, lakini kwa mtindo wa utendaji kazi kwa watoa huduma hiyo ulivyo ni dhahiri tija inayotegemewa ni vigumu kupatikana.
Mheshimiwa Spika, kutokana na watoa huduma kutokuwa na idadi maalum ya wafugaji wanaowahudumia, eneo maalum na hivyo kuweza kuwajibika kwa matokea yatakayopatikana katika eneo husika ni tatizo kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona itakuwa ni vyema kama kila afisa ugani atakuwa na orodha kamili ya wafugaji anaofanya nao kazi katika eneo maalum, kwani utaratibu huo utarahisisha upatikanaji wa kumbukumbu sahihi na pia kuweza kupima utendaji wa afisa huyo.
Kwa mfano kwa maafisa ugani wanaofanyakazi mkoa wa Kagera  ambao ni watumishi wa Serikali (Ndg. Patrick, Kashankoro, Kanyambo na Mutabazi), hawa wote wanamiliki vitalu vya Ranchi. Hoja ni je utaratibu wa watendaji wa Serikali kujimilikisha mali za wananchi unaendelea hata kwenye ngazi ya chini? Na mgongano wa maslahi katika suala hili unashughulikiwa vipi?
  1. SEKTA YA NGOZI
Mheshimiwa Spika, wakati waziri kivuli wa fedha akiwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani kwenye muswada wa fedha, tarehe 16.08.2012 alisema yafuatayo “Mheshimiwa Spika, katika kifungu cha 12 cha muswada, serikali inatoa pendekezo la kufanyia marekebisho sheria ya kodi ya mauzo ya nje ya nchi sura 196 kwa kuweka jedwali jipya ambalo linaongeza viwango vya tozo kwenye ngozi ghafi inayosafirishwa kwenda nje ya nchi. Kama serikali ina mpango madhubuti wa kuendeleza sekta ya viwanda nchini na kuleta tija kiuchumi ni dhahiri kuwa inatakiwa kusitisha uamuzi huu.
Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba yetu ya bajeti tulipendekeza kuwa serikali izuie kabisa ngozi ghafi kusafirishwa nje ya nchi na badala yake ijikite kutafuta uwezekano wa kuitumia ngozi hiyo hapa nchini na kuanzisha viwanda vya kutengeneza bidhaa zitokanazo na ngozi hiyo. Hata Kamati ya fedha na uchumi ilikuwa na mapendekezo hayahaya. Hii ni kutokana na manufaa makubwa ya kiuchumi wanayopata wenzetu hasa nchi ya Ethiopia.
Mheshimiwa Spika, hata katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki wenzetu wa Uganda na Rwanda nao wamezuia ngozi ghafi kuuzwa nje ya nchi. Mapendekezo haya ya serikali yakibaki kama yalivyo hayataifanya serikali kupata mapato yanayostahili kwa sababu wafanyabiashara wengi wanatoa takwimu zisizo sahihi kuhusu mauzo halisi watakayokuwa wanauza nje ya nchi (under invoicing).
Mapato ambayo serikali inahofia kuyapoteza kwa kupiga marufuku uuzaji wa ngozi ghafi nje ya nchi yatapatikana tena kwa kiasi kikubwa kutokana na ajira zitakazopatikana katika viwanda vya kusindika ngozi, kodi ya mapato kama vile PAYE n.k. Ni wakati muafaka sasa tuchukue hatua hii kwani hata nchi ya Pakistani ambao ndio wanunuzi wa ngozi yetu wamepiga marufuku kabisa uuzaji wa ngozi ghafi nje ya nchi yao”.
  1. SEKTA YA MAZIWA
Mheshimiwa Spika, Taarifa ya uwezo wa viwanda na hali halisi ilivyo sasa hivi Inayonyesha kuwa hadi sasa hivi kuna viwanda 35 vyenye uwezo wa kusindika zaidi ya lita 1000 kwa siku kwa kila kimoja. Kati ya hivyo ni viwanda 28 tu ambavyo vinazalisha hadi sasa na vingine 7 ama vimefungwa au kusimamisha uzalishaji. Kuna baadhi ya viwanda vinatumia hadi zaidi ya 80% ya uwezo wake na vingine chini ya 16%. Kwa vile kuna viwanda visivyozalisha kabisa, wastani wa matumizi ya uwezo wa kusindika ni 12% tu.
Mheshimiwa Spika, Uwezo wa jumla wa viwanda vyote ni kusindika, lita 428,500 kwa siku lakini hali halisi ni kusindika lita 52,330 kwa siku. Hali hii inaonyesha kuwa juhudi kubwa zinahitajika ili kuwezesha sekta ya viwanda vya maziwa kuwa na uwezo wa ushindani na kutoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa taifa.
  1.  MATATIZO YANAYOATHIRI USINDIKAJI WA MAZIWA
Mheshimiwa Spika, Matatizo yanayovikabili viwanda vya maziwa ni mengi na yanahitaji uchunguzi wa kina katika kila kiwanda ili kutoa ushauri kwa kila kiwanda husika, lakini matatizo yaliyotajwa na viwanda vyote ni kama yafuatayo:
  1. Ukosefu wa maziwa ya kutosha.
Mheshimiwa Spika, Ingawa Tanzania inakadiriwa kuzalisha lita 1,400 milioni za maziwa kila mwaka kiasi cha maziwa yanayopatikana kwa ajili ya kusindika ni kidogo sana. Hali hii inatokana na maziwa mengi kuzalishwa na wafugaji wa jadi ambayo kiasi kikubwa kinatumika na wafugaji wenyewe, uzalishaji ni wa msimu na ukusanyaji ni mgumu. Wafugaji hawa ndio huzalisha 70% ya maziwa yote nchini.
Upungufu wa maziwa ya kusindika ambao huwa zaidi wakati wa kiangazi unachangiwa na sababu nyingi ambazo ni:
  1. Gharama kubwa na ugumu wa kukusanya maziwa ya wafugaji
waliosambaa maeneo ya mbali
  1. Ushindani na wachuuzi wadogo wadogo.
  2. Faida ndogo kutokana na matumizi kidogo ya uwezo wa viwanda.
  3. Uzalishaji wa msimu ambapo maziwa mengi hupatikana msimu wa mvua na kidogo sana wakati wa kiangazi na hivyo kushindwa kutosheleza[4]
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa viwanda vya maziwa vilivyopo vinapata maziwa ya kutosha, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuhakikisha kwamba  maziwa yanayozalishwa na wafugaji wadogo au wa asili yanauzwa kwenye vituo maalum vya kukusanyia maziwa, na pia maziwa yasiuzwe kwa wanunuzi bila ya kuyasindika. Kufanya hivyo kutaondoa kwanza matatizo ambayo yanayoweza kutokana na magonjwa ya kuambukizwa kati ya mifugo na binadamu (zoonotic deseases).
Mheshimiwa Spika, pia liwe ni jukumu la Halmashauri kulinda soko la maziwa yaliyosindikwa, na kwa njia hiyo wafugaji wadogo na wale wa asili maziwa yao yatakuwa na uhakika wa soko badala ya sasa ambapo wakati wa msimu wa mvua maziwa yanakosa soko na hivyo kumwagwa.
Mheshimiwa Spika,  kwa kuwa maziwa kuuzwa moja kwa moja na wafugaji wadogo na wakubwa ni upotevu wa mapato, hivyo basi  Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwa, liwe ni jukumu la Halmashauri kutunga kanuni ndogo za kuhakikisha viwanda vya maziwa vinalindwa kwa kupata maziwa muda wote ili kiwanda kiweze kulipa kodi kwa halmashauri.
  1. Matatizo ya kimfumo na sera
Mheshimiwa Spika, mbali ya matatizo hayo pia kuna matatizo ya kimfumo na sera. Katika kundi hili kuna matatizo kama urasimu katika vyombo vya kudhibiti ubora kama TBS, kuwa na vyombo vingi vya uthibiti, wadau kutoshirikishwa katika maandalizi ya sera, migogoro kati ya wafugaji na wasindikaji na vyama vya wadau visivyo imara.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwepo uwajibikaji kwenye vyombo vya udhibiti na vyombo hivi madhumni yake, yawe ni kuwezesha na siyo kukwamisha. Inapendekezwa kuwa shughuli zote za udhibiti wa sekta ya maziwa zifanywe na Bodi ya Maziwa tofauti na sasa ambapo vyombo vingi hufanya hivyo. Aidha, Bodi ya Maziwa iliyoanzishwa kisheria iwezeshwe kufunya shughuli zake kwa kupewa rasilimali zinazotakiwa tofauti na sasa ambapo Bodi ipo kwa jina tu.
Mheshimiwa Spika, aidha, wadau washirikishwe katika utayarishaji wa sera zinazohusu sekta ya maziwa, kwani sasa wanaohusishwa ni wale wenye viwanda vya maziwa, je wafugaji wa asili wanahusishwa vipi?
  1. Matatizo mengineyo:
Mheshimiwa Spika, Haya ni kama kipato kidogo cha wananchi, wawekezaji kuwa na miradi mingi kwa pamoja, sekta ya maziwa kutokuwa na mvuto kwa wawekezaji, ukosefu wa vyombo vya mikopo ya muda mrefu na riba ndogo na kutokuwa na maeneo maalum yenye miundombinu ya kutosha ya kujenga viwanda.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi Upinzani inaitaka pia Serkali itafute njia ya kuimarisha vyama vya kitaifa vya wadau (TAMPA, TAMPRODA) ili viwe kweli vya kitaifa na vyenye uwezo wa kushirkiana na Serikali kundeleza sekta.
Mheshimiwa Spika, nguzo ya 7 aya ya 7.2.3 ya kilimo kwanza  inayosema kwamba “Kuainisha na kuimarisha uwezo unaohitajika kwa kuendeleza sekta ya mifugo-  Kwa mwaka 2010 serikali  pamoja na TPSF ilitakiwa Kukarabati viwanda vyote vya maziwa vilivyopo nchini na kuanzisha vituo vya kukusanyia maziwa”. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge na wadau kwenye sekta hii ya maziwa utekelezaji wa nguzo hii ya Kilimo kwanza imetimizwa kwa kiasi gani?
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano inaonyesha ili sekta ya Mifugo iweze kuleta tija tarajiwa ilitakiwa kwa mwaka wa fedha 2013/14 ipewe shilingi bilioni 275.98 kama fedha za maendeleo. Lakini kwa masikitiko makubwa  mwaka huu  wa fedha Wizara imetengewa jumla ya shilingi bilioni 8.97. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge ni kwanini imeshindwa kutekeleza matakwa ya mpango wa maendeleo ambao ulipitishwa na Bunge?
  1. SEKTA YA UVUVI
Mheshimiwa Spika, Tanzania inamiliki maeneo makubwa ya maji ambamo rasilimali za uvuvi hupatikana kwa wingi. Maeneo hayo ni pamoja na Ziwa Vctoria, Ziwa Tanganyika Ziwa Nyasa, Mabwawa
(Nyumba ya Mungu, Mtera na mengine mengi ya asili), mito (Rufiji, Ruvu, Kilombero n.k.), malambo na maeneo oevu ambayo yana fursa kubwa ya uvuvi hapa nchini. Aidha, kuna Bahari ya Hindi ambayo ina maeneo mawili ya Bahari ya Taifa (Territorial Sea) na Ukanda wa Uchumi wa Bahari (Exclusive Economic Zone - EEZ).
Sekta ya uvuvi inatoa mchango mkubwa katika kuwapatia wanachi ajira, lishe, kipato, na kuingizia nchi fedha za kigeni. Uvuvi nchini huendeshwa na wavuvi wadogo takriban 200,000 ambao huvua asilimia zaidi ya 90 ya samaki wote wanaovuliwa nchini. Zaidi ya wananchi 4,000,000 hujishughulisha na kujikimu kutokana na shughuli zinazoendana na uvuvi hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Kutokana na uharibifu uliopo katika uvuvi umesababisha kuwepo kwa upungufu mkubwa wa rasilimali ya uvuvi, hususan katika Ziwa Victoria ambalo huongoza kwa upatikanaji wa samaki aina ya Sangara ambao wamepungua kutoka tani 676,000 mwaka 2006 hadi tani 331,000 mwaka 2009. Hali hii imetokana na sababu zifuatazo:-
  1. Ongezeko la kasi ya matumizi ya zana haramu pamoja na ongezeko la idadi ya wavuvi kutoka 92,529 mwaka 2000 hadi 105,016 mwaka 2008;
  2. Ongezeko la vyombo vya kuvulia samaki kutoka vyombo 30,171 (2000) hadi vyombo 52,174 (2008); na
  3. Ongezeko kubwa la mahitaji ya samaki na mazao yake katika soko la samaki ndani na nje ya nchi na hivyo kuwa kichocheo kikubwa cha samaki wachanga kuvuliwa. Kwa upande wa Bahari ya Hindi, mathalani rasilimali ya kambamiti imepungua kiasi cha kusababisha uvuvi wake kwa meli kubwa kufungwa hadi sasa. Aidha, rasilimali ya Kambamiti (Prawns) imepungua kutoka tani 1,320 kwa mwaka 2003 hadi kufikia tani 205 mwaka 2007[5].
Mheshimiwa Spika, pamoja na uwepo wa ongezeko la mahitaji ya samaki na mazao yake katika soko, wavuvi wamekuwa wakiilalamikia Serikali kuwa inakwamisha au kuwahujumu kwa uchomaji wa nyavu za wavuvi ambao hata hawaelewi ni kwanini wanauziwa nyavu zisizostahili kwa mujibu wa Watendaji. Lakini ukweli ni kuwa nyavu zote kustahili au kutostahili inategemea unavua samaki wa aina gani na nyavu hizo zinatumika namna gani, hivyo basi kitendo cha kuchoma nyavu (Zana za uvuvi) za wavuvi bila ya kuhakiki matumizi yake na bila ya kutoa nyavu (zana mbadala) ni hujuma kwa sekta hii ya uvuvi na wavuvi wenyewe. Kumekuwepo na tabia ya kufunga ziwa au kusitisha shughuli za uvuvi kiholela, bila taarifa au sababu za kisayansi zinazotolewa kwa wavuvi.
Mheshimiwa Spika, Mfano wa tabia hii yenye kujenga hisia ya chuki za wananchi kwa Serikali yao ni Ziwa Basotu. Hili ziwa limeingizwa kwenye mitego, chambo na chuki/ulipazaji visasi vya kisiasa tu kumewekupo na shinikizo la ulipazaji kisasi ya kisiasa kwa kufungiwa ziwa mara kwa mara ili wataabike, wasipate kitoweo na kipato na kuvuruga mfumo wao wa maisha ya kila siku lakini sio ukweli wa hali halisi kuwa kuna uvuvi usiofaa. Je, haya ndo mandeleo ya sekta ya uvuvi? Hivi jambo la kisayansi linaendeshwaje kisiasa? Nadhani haya si maendeleo tuliyotarajia kwa mujibu wa ilani za CCM za mwaka 2005-10 na 2010-15 bali ni  hujuma na upandikizwaji wa mbegu mbaya za chuki ya kisiasa tu.
Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Waziri awaeleze wananchi wa BASOTU kwanza ni nani mwenye mamlaka ya kusitisha uvuvi katika ziwa na hatua zipi ambazo pia zinashirikisha wadau zinapaswa kufuatwa?
a.      UFUGAJI WA SAMAKI
Mheshimiwa Spika, shughuli za ufugaji wa samaki unafanywa na wafugaji wadogo. Hata hivyo, ufugaji wa samaki lazima ishindane na shughuli zingine za vijijini kwa eneo la ardhi, maji, nguvu kazi na vyakula. Hali hii hupelekea umuhimu wa kutathmini gharama na faida ya ufugaji samaki na mchango wake kwa maisha ya wakazi wa vijijini kulingana na shughuli zao zingine.
Mheshimiwa Spika, zaidi ya hayo, ufugaji wa samaki hukabiliwa na matatizo na changamoto zingine kama ukosefu wa sera thabiti ya ufugaji samaki; mabadiliko katika sera za uchumi; ukosefu wa teknolojia bora; upungufu wa vifaranga bora; miundombinu duni ya usafiri; utafiti usiokidhi mahitaji; ukosefu wa takwimu za uzalishaji; upungufu wa taarifa sahihi za utunzaji wa bwawa la samaki.
Mheshimiwa Spika, ili kuwa na uwezo wa kufanya shughuli kwa mafanikio, ni muhimu kuwa na takwimu ya utendaji na shughuli husika. Vivyo hivyo, ili kuendesha shughuli za ufugaji samaki kibiashara, mfugaji analazimika kuchukua na kutunza takwimu kwa hatua zote au shughuli yoyote anayoifanya ikiwemo ya kutunza matumizi na mapato ya fedha.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano, sekta ya Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2013/2014 ilitakiwa itengewe jumla ya shilingi  bilioni 60.896 ili sekta nzima ya uvuvi iweze kuleta tija stahili pamoja na faida zingine ni kwamba kama uwekezaji kwa mujibu wa mpango hadi 2015. Makusanyo ya Serikali kwa mwaka katika sekta hii yalitakiwa kukua kutoka shilingi bilioni 6.58 hadi shilingi bilioni 12.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali iwaeleze watanzania ni kwanini Serikali imekinzana na mpango wa Maendeleo ambao ulipitishwa na Bunge?
  1.  MAPITIO YA BAJETI YA UTEKELEZAJI KWA WIZARA
Mheshimiwa Spika, Ukiangalia mwenendo wa bajeti ya wizara kwa miaka minne inaonyesha kuwa bajeti ambayo imekuwa ikitolewa kwa wizara hii imekuwa ikishuka, mwaka wa fedha 2010/2011 zilitengwa shilingi bilioni 58.8, mwaka 2011/2012 zilitengwa shilingi bilioni 57.2, mwaka wa fedha 2012/2013 zilitengwa shilingi bilioni 54.6 na kwa mwaka huu wa fedha 2013/2014 zimetengwa shilingi bilioni 47.18
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa tafsiri ya kupungua huko kwamba ni fundisho kwa watendaji wizara kuangalia fursa za mapato ambazo zipo katika wizara hiyo zifanyiwe kazi na ziweze kuwekezwa kwa maendeleo ya sekta hizi mbili-(Mifugo na Uvuvi), na kwamba kutokana na ukweli ulipo wa fursa hizo wizara imelala na hata kusimamia sheria na kanuni zilizopo za kuhakikisha mirabaha ya uvuvi inalipwa imeshindwa na wajanja wanavuna raslimali yetu bila nguvu yoyote ya ziada.
  1. HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inasema kwamba, wizara hii kwa kipindi kirefu imekuwa kama nyumba isiyokuwa na msimamizi kiasi kwamba raslimali za nchi hii zimekuwa zikigawiwa, zikivunwa na kutumiwa bila kufuatwa kwa sheria na kanuni, mfano mmojawapo ni ugawaji wa mashamba ya Ranchi za Taifa na kilichofuata ni nchi kuingia kwenye migogoro mikubwa kati ya wafugaji na wakulima.
Mheshimiwa Spika, katika kuonyesha kuwa Serikali imeshindwa kuthamini sekta ya mifugo kwa ujumla, mwaka 1981, Morogoro Muasisi wa nchi hii Mwalimu J.K Nyerere alisema “tumetenga, kwa mfano, maeneo maalum kwa ajili ya mazao kama pamba, kahawa, tumbaku na katani lakini hatujatenga maeneo kama hayo kwa ajili ya mifugo.Tumetenga maeneo maalum kwa ajili ya pundamilia (hifadhi za taifa) lakini wafugaji wananing’inia hewani tu”.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kama kungekuwa na umakini katika serikali hii ya CCM ni dhahiri kuwa makosa ambayo yalikuwa yametendeka huko nyuma ulikuwa ni muda mwafaka wa kurekebisha makosa katika sekta hii ya mifugo na hivyo yanayopelekea wafugaji kuwa wahamiaji au watu wasiohitajika katika nchi yao kama ilivyo sasa.
Mheshimiwa Spika, mwisho lakini kwa umuhimu mkubwa ni shukrani kwa wanachama na wapenzi wote wa Wilaya ya Maswa kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa katika kujenga na kuimarisha chama chetu.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.
………………………………………..
Slyvester Mhoja Kasulumbayi (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-
Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
                                                                  31.05.2013

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...