HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHESHIMIWA SAID AMOUR ARFI (MB), WIZARA YA UJENZI, KUHUSU MAPITIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014 (Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) toleo la mwaka 2013)
1.0
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
jukumu la msingi la Wizara hii ni kusimamia kukamilifu tasnia ya ujenzi kwa
ukamilifu wake ili kutoa matokeo bora na kuchochea uchumi wa nchi yetu na
kuwaletea maendelo watu wetu na kupunguza umasikini kwa kuwa na miundombinu
yenye kukidhi viwango, ubora na Usalama.
2.0
MAPITIO
YA UTEKELEZAJI WA BAJETI 2012/2013
Mheshimiwa Spika,
ukusanyaji wa vyanzo vya mapato katika idara na vitengo vya Wizara ya Ujenzi
kwa mwaka 2012/13 ulivuka lengo la mwaka hadi kufikia Februari 2013 walikusanya
zaidi ya mara mbili ya lengo la makusanyo kwa mwaka. Halikadhalika mfuko wa
Barabara ulikusanya takriban asilimia 70 hadi februari 2013 ni dhahiri mfuko wa
barabara nao utafikia lengo uliokusudia kwa mwaka 2012/13 na kuvuka lengo, haya
si mafanikio haba, hata hivyo hayajakidhi wala kupunguza changamoto za Wizara
hii.
Mheshimiwa Spika,
matumizi ya kawaida na maendeleo, wizara imeendelea kupokea fedha kwa mtiririko
unaoridhisha, matumizi ya kawaida hadi
februari 2013 ilipokea 69% ya fedha za matumizi na 100% kwa miradi ya maendeleo
kwa fedha za ndani zilikuwa zimepokelewa.
Mheshimiwa Spika, yapo
matukio kadhaa yaliyotokea ambayo Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Maelezo ya
kina na kutosheleza na hatua zilizochukuliwa ili kuzuia hali hii isijirudie
tena na kuleta maafa kwa watanzania. Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua majukumu
ya Wizara hii pamoja na kuzisimamia taasisi zilizopo chini ya Wizara hii
ikiwemo Baraza la Ujenzi (NCC), Bodi ya Usajili wa Wahandisi(ERB), Bodi ya
Usajili wa Wabunifu majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQSRB), Pia Bodi ya Usajili
wa Makandarasi (CRB) na vyombo hivi kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na
taratibu za miundo yake.
Mheshimiwa Spika,
yamekuwepo matukio ya kujirudia ya kuanguka kwa majengo ya magorofa
yaliyokamilika na yanayoendelea kujengwa katika jiji la Dar es Salaam na tukio
la hivi karibuni jengo lililokuwa linaendelea kujengwa katikati ya jiji la Dar
es Salaam, mtaa wa Indira Ghandi na kupoteza maisha ya Watanzania kadhaa, Kambi
Rasmi ya Upinzani inatoa pole kwa wale wote waliopoteza ndugu na marafiki zao katika tukio hilo
Mwenyezi Mungu awapumzishe kwa amani. Aidha,tukio la kuanguka kwa ukuta katika
kituo cha Mabasi Ubungo na kuharibu magari na mali za watanzania ambao walifika
katika kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo kwa kujipatia huduma. Kambi Rasmi ya
Upinzani inasikitishwa kwa tukio hilo ambalo lingeweza kuzuilika iwapo
mkandarasi angezingatia kanuni za usalama. Tunapenda kuwapa pole watanzania
wenzetu waliokumbwa na mkasa huo.
Mheshimiwa Spika,
pole na kufarijiana pekee haitoshi bado tunajiuliza kama nchi ni lini viongozi
wetu wataheshimu, kuwajibika na kutekeleza majukumu yao na kuwa na ujasiri wa
kutafuta mbinu za kutatua matatizo pindi tunapokutana na mambo magumu katika
utendaji wetu na si kukimbia matatizo
kwa kujificha chini ya migongo ya watendaji
wengine na kutowajibika na uozo unaotokea katika wizara tunazozisimamia na
tukisubiri kusifiwa kwa mazuri yanayofanywa na watendaji haohao na kukwepa
lawama kwa mambo ya ovyo.
Mheshimiwa Spika,
wakati waziri anawasilisha hotuba yake ya bajeti kwa mwaka wa fedha uliopita
alisema kuwa, naomba kunukuu “Bodi itafanya ukaguzi wa kina katika
taasisi za elimu ya juu zinazofundisha uhandisi ili kubaini kama vyuo hivyo
vina sifa stahiki za kufundisha wahandisi na iwapo wahadhiri wanaofundisha
wahandisi wamesajiliwa na Bodi” (Hotuba
ya bajeti ya waziri wa ujenzi 2012/2013, uk 162).
Kuendelea bofya Read More
Mheshimiwa Spika, kutokana na nukuu hiyo hapo juu ni dhahiri kuwa wizara na waziri wana hofu na aina ya vyuo vinavyotoa elimu ya uhandisi na pia wana hofu na wahadhiri ambao wanajukumu la kufundisha wahandisi hapa nchini kuwa hawana viwango vinavyotakiwa , Kambi rasmi ya upinzani , tunataka kujua ukaguzi huo ulifanyika katika vyuo gani na hali ikoje na ni hatua gani zilichukuliwa dhidi ya vyuo ambavyo wahandisi na wahadhiri walikutwa hawana sifa sitahiki , kwani tumeendelea kushuhudia maafa yanayotokana na kazi mbalimbali zinazofanywa na wahandisi hapa nchini mwetu.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inahitaji kujua taarifa za uchunguzi ya kuanguka kwa
magorofa Dar es Salaam ya mwaka 2006 na hatua zilizochukuliwa baada ya ukaguzi
na nyumba ngapi zilizopaswa kuvunjwa.
Kwa maelezo ya Waziri Mkuu mstaafu rejea gazeti la Nipashe la 03 April 2013
ilionekana takriban magorofa 100 katika jiji la Dar es Salaam yalitakiwa
kuvunjwa kwa mapungufu na kutokidhi viwango ni magorofa mangapi hadi sasa
yamevunjwa?
Mheshimiwa Spika,
hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekezaa mambo yafuatayo:-
1. Hatua
stahiki za kinidhamu na kisheria zichukuliwe kwa wahusika wa maafa haya na
zionekane zimetendeka ili kujenga imani
kwa watanzania.
2. Bodi
zote nilizozitaja hapo juu ziwajibike ipasavyo kila moja katika eneo lake na
kusimamia kikamilifu wajibu wao kwa mujibu wa sheria na taratibu, vinginevyo
hatuna sababu ya kuwa na Bodi za kitaalam ambazo haziwezi kusimamia wanachama
wao.
3. Tuangalie
upya sheria zetu na ikiwezekana tuwe na mamlaka mahususi ya ukaguzi (Inspection
Authority) inayosimamia majengo hususan magorofa yenye kuwa na wataalamu wa
fani zote kwa miji na majiji yetu badala ya Halmashauri zetu zinazotoa vibali
na kushindwa kusimamia kutokana na ukosefu wa wataalamu ili tuweze kujua ni
nani wa kuwajibishwa.
4. Ukaguzi
wa kina na wa kitaaluma ufanywe katika vyuo vyote vinavyotoa elimu ya uhandisi
na kuona kama vyuo hivyo vina sifa za kutoa elimu hiyo kwa mujibu wa sheria na
kama wahitimu wake wanasifa za kuwa wahandisi.
3.0
MATUMIZI
MABAYA YA FEDHA ZA BARABARA
Mheshimiwa Spika, katika
hotuba ya kambi rasmi ya upinzani bungeni kwenye bajeti ya mwaka 2011/2012
tulihoji kuhusiana na fedha zilizokuwa zimetengwa chini ya fungu lililojulikana
kama “special
road construction project” , na tulisema ifuatavyo; Nanukuu
hansard ya tarehe 01.08.2011 “Mheshimiwa Spika, Miradi maalum ya
ujenzi wa barabara (kasma 4168).kitabu cha Miradi ya Maendeleo (sehemu-A juzuhu
iv) katika fungu 98, kasma 4168 utaona kuwa mradi unaitwa “Miradi ya ujenzi wa
barabara maalum” (special road
construction projects) na fungu hili limetengewa kiasi kikubwa kuliko
miradi mingine yoyote ya ujenzi wa barabara katika mwaka huu wa fedha kwani zipo
jumla ya sh. 348,075,000,000/= na hizi zote ni fedha za ndani. Kwa hakika hizi
ni fedha nyingi sana na hasa ikizingatiwa kuwa kitabu hicho kimeonesha miradi
yote ya ujenzi wabarabara ambayo itatekelezwa katika mwaka huu wa fedha, ila
hii miradi maalum haijaoneshwa ni miradi ya barabara gani na zitajengwa wapi. (Makofi)
Mheshimiwa
Spika, kasma hii kwa mwaka wa fedha 2009/2010 na 2010/2011 haikuwa imetengewa
kiasi chochote cha fedha na ndio maana imetustua kuona mwaka huu fedha nyingi
kiasi hicho zinatengwa kwa miradi isiyojulikana kuwa itajengwa wapi. (Makofi)
Mheshimiwa
Spika, hata ukiangalia maelezo yaliyotolewa kwenye Kamati ya Bunge ya
Miundombinu juu ya mpango na bajeti ya mwaka 2011/2012, kasma 4168 haipo kwenye
randama na hakuna maelezo yoyote ambayo yametolewa kuhusiana na fedha hizo
ambazo zimetengwa. (Makofi)
Kambi
ya Upinzani, tunataka kupata maelezo ya kina ni miradi gani hii ambayo haiwezi
kuandikwa na inatengewa fedha nyingi kiasi hicho? Kwani hii italiwezesha Bunge
kuweza kupitisha bajeti inayoifahamu na kuisimamia Serikali kwa kuweza
kufuatilia utekelezaji wa miradi husika”.
Mheshimiwa Spika,
wakati wa mjadala kuhusiana na hotuba ya wizara ya uchukuzi 2011/2012 ilipowasilishwa , Mhe.Mbunge wa Ukerewe
Salvatory Machemli alihoji fedha hizi na kusema , naomba kunukuu Hansard ya
tarehe 03.08.2011 “Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaja
mwanzoni kwamba reli inakufa wakati watu wanaiangalia na Serikali haisemi kitu
chochote kazi yao kuomba Miongozo tu hapa, pesa zipo nyingi. Wakati mimi
nawasilisha hotuba yangu kwa Wizara ya Ujenzi, nilihoji kiasi cha pesa shilingi
bilioni 348 ambazo hazikuonyeshwa zinafanya kazi gani kwenye Wizara ile.
Mheshimiwa Magufuli jana wakati anafanya majumuisho hakutaja, amemeza tu
japokuwa aliona ni chungu lakini akameza kama chloroquine, nataka sasa hizi shilingi bilioni 348 ambazo
zimeonyeshwa kwenye vote 4168
ambazo matumizi yake hazikuonyeshwa basi wapelekewe reli ili tuimarishe reli,
tuweze kuokoa barabara zetu kuliko kuziacha tu, jamaa wanatia mfukoni,
wanachukua wanaweka waa, kama ilivyo kawaida yenu Chama cha Mapinduzi,
mnakwenda kujenga masinagogi Ulaya. (Makofi)”
Mheshimiwa
Spika, katika mjadala huo
aliyekuwa naibu waziri wa Ujenzi Mhe.Dr.Harison Mwakyembe alijibu kuhusiana na
hoja hiyo na kusema , nanukuu hansard ya tarehe 03.08.2011 “NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ili Mheshimiwa Mbunge asiendelee kupotosha na kujenga mahekalu
hewani, nilitaka kumueleza kwamba hizo pesa zilizopitishwa hapa jana ni za
Mfuko Maalum ambao unaisaidia Serikali pale ambapo mfadhili wa nje kwa mfano,
anaamua kufadhili ujenzi wa barabara fulani na anasema Serikali ichangie ten bilioni, utaitoa wapi kama wewe
huna Mfuko Maalum? Serikali ikaona logic
ya kuweka Mfuko Maalum ili isitulazimu tena kuitisha Bunge kupitisha
pesa hizo, sasa zianze kuleta maneno, kutufanya wote ni wahuni kama yeye na hii
siyo vizuri kusema kwamba tutapeleka hizo pesa wapi? Ahsante. (Makofi)
Mheshimiwa
Spika, mnamo tarehe 04.08.2011
wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Mhe.waziri Mkuu alitoa kauli
ya serikali kuhusiana na fedha kuongezwa wizara ya uchukuzi na alisema, nanukuu
hansard ya tarehe husika…..’Kwa hiyo, baada ya Kamati ya
Miundombinu kupitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kuishauri
Serikali kuongeza bajeti hiyo kwa shilingi bilioni 95, jambo ambalo
tuliliridhia na kulikubali, lakini hatukuweza kufikia kiwango hicho kama
ilivyokuwa imeombwa. Kikao cha jana kimewezesha Serikali kufanikiwa kupata
fedha hizo ambazo zitatumika kwenye maeneo matatu yafuatayo: Reli ya Kati, Kampuni
ya Ndege Tanzania na Usafiri wa Majini yaani Meli katika Maziwa ya Victoria,
Tanganyika na Nyasa. Kiasi hicho cha shilingi bilioni 95 ni kiasi ambacho
Wizara ilikuwa imeji-commit au
imejiahidi mbele ya Kamati kwamba, zikipatikana zitawezesha huduma za msingi
katika maeneo hayo matatu kuweza kuendelea bila matatizo makubwa. (Makofi)’
Mheshimiwa
Spika, wakati Bunge
likiwa limekaa kama kamati ya matumizi wakati wa kupitisha mafungu ya wizara ya
uchukuzi Mhe. Tundu lissu aliomba ufafanuzi kama ifuatavyo, nanukuu hansard “ …..Mheshimiwa
Mwenyekiti, mimi naomba nifafanuliwe, kama Bajeti ya Wizara ya Ujenzi
ilishapitishwa mafungu yote yalishapitishwa, hii bilioni 95 iliyochotwa kutoka
fungu la miradi maalum ya barabara na kuletwa kwenye miradi ya maendeleo ya Wizara
ya Uchukuzi ambayo ni Vote tofauti
kabisa zimechotwa kwa idhini ya Kanuni ipi, mimi naomba nipewe angalau msingi
wa Kikanuni au wa kisheria wa kuchota fedha ambazo tayari zimeshatengwa na
Bunge hili bila kupata authorization ya
Bunge hili. Ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa
Spika, majibu
yafuatayo yalitolewa,kwa mujibu wa Hansard “ WAZIRI WA NCHI OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA,
URATIBU NA BUNGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu alichokisema Mheshimiwa
Tundu Lissu kipo ukurasa 276, Kifungu kidogo cha 4168. Hizi ni fedha ambazo
zimewekwa katika Kifungu hiki katika Bajeti hii ya ujenzi lakini ni mfuko maalum,
hela hizi hazijawa committed kama
unavyoziona. Ukiangalia miradi yote iliyomo katika kfungu hiki ina barabara
tayari. Fedha hizi ziliwekwa maalum kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya miundombinu
hasa katika maeneo ambayo ipo miradi kadhaa ambayo tuna uzoefu, imekuwa inachangiwa
inatolewa na wafadhili, lakini hii tulifikiri sehemu nyingine miradi hii
imekwama kwa sababu sisi tulikuwa hatujajitayarisha kuweka counterpart fund. Kwa hiyo, hizi
fedha zimewekwa hapa kwa ajili hiyo, miradi yote ambayo Serikali ya Tanzania
itafanya kutoka kwenye fedha za wafadhili hizi ni fedha ambazo zimewekwa, ni
fungu ambalo haliko committed.
(Makofi)
Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwa hiyo hizi fedha zimechukuliwa hapa zimepelekwa ujenzi kwa maana
ya kwamba ni fedha ambazo ziliwekwa kwa ajili ya mfuko wa miundombinu. Zimekuwa
voted lakini Mheshimiwa Tundu
Lissu atakuja kupata ukweli wa mambo haya yote wakati wa Appropriation Bill. (Makofi)
Mheshimiwa Spika,
baada ya fedha hizi kupunguzwa kiasi cha shilingi bilioni 95 na kupelekwa wizara ya uchukuzi zilibakia kiasi cha
shilingi bilioni 252.975 katika
kifungu hiki, leo tumelazimika kulikumbusha Bunge kuhusiana na suala hili kwani
kwa mujibu wa ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ya mwaka
husika wa fedha kuhusiana na kifungu hiki alisema, naomba kunukuu “malipo
ya madeni ya mwaka wa nyuma yaliyolipwa kwa fedha za 2011/2012 kwa kutumia jina
la mradi usiohalisi shs.252,975,000,000. Miradi katika wizara ilipewa namba
4168 kwa ajili ya kupitisha malipo ya madeni ya miaka ya nyuma kwa miradi
inayotekelezwa na TANROADS. Namba hii sio halisi” (chanzo: taarifa ya CAG
uk.160,fungu 98)
Mheshimiwa
Spika, fedha hizi “zilizopotea”au
“kulipwa kifungu hewa” ni sawa na fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya
barabara zifuatazo kwa mwaka huu wa fedha 2013/2014;
i.
Barabara
ya Usagara-Geita-Kyamyorwa (KM 422)
ii.
Barabara
ya Kigoma-Kidahwe-Uvinza-Kaliua-Tabora (KM 443)
iii.
Barabara
ya Nangurukuru-Mbwemkulu (KM 95)
iv.
Barabara
ya Sumbawanga-Matai-Kasanga Port (KM 112)
v.
Barabara
ya Manyoni-Itigi-Tabora (KM264)
vi.
Barabara
ya Tabora-Ipole-Konga-Mpanda (KM 359)
vii.
Barabara
ya Kidatu-Ifakara-Lupilo-Malinyi-Londo-Lumecha/Songea(KM- 396)
viii.
Kuondoa
msongamano barabara za Dar (KM- 102.15)
Aidha,
ni sawa na kusema kuwa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 316.218 imepotea kwa kutumia mahesabu ya wizara ya ujenzi
kuwa kilomita moja ya lami inajengwa kwa kiasi cha shilingi milioni mia nane (800,000,000), hii ni sawa na kusema
kuwa barabara ya kutoka Manyoni-Itigi-Tabora
(KM 264) Changanya na barabara ya kutoka Chunya –Makongorosi (KM 43) na
Barabara ya Tangi Bovu –Goba (KM 9), zimepotea kutokana na ufisadi huu.
Kambi
rasmi ya upinzani, inataka kupata majibu yafuatayo kuhusiana na suala hili;
i.
Fedha
hizi zilizokuwa zimetengwa zilitumika kwa ajili ya kufanyia shughuli gani?
Kwani majibu yaliyotolewa na wizara na serikali Bungeni sio yaliyotolewa kwa mdhibiti
na Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali
ii.
Ni
madeni gani yalilipwa kama kweli yalikuwepo?au wajanja wachache walijinufaisha
? na wahusika wamechukuliwa hatua gani mpaka sasa.
iii.
Nini
kauli ya serikali kuhusiana na Ufisadi huu, mbele ya Bunge na watanzania kwa
ujumla .
iv.
Je,
Tunaweza kuendelea kuamini kauli za viongozi wa serikali hii ndani ya Bunge
kama hii ndio hali halisi ?
v.
Nini
kauli ya serikali kuhusiana na Ufisadi huu.
4.0
MFUKO
WA BARABARA
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inatoa pongezi kwa Mwenyekiti, Bodi na Watendaji wa Mfuko wa
Barabara kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa uwazi na uwajibikaji. Kambi Rasmi ya
Upinzani inapendekeza kutafuta njia bora ya kuongeza mapato kwa mfuko huu ili
uongeze kasi ya kusaidia Ujenzi wa Barabara zetu na matengenezo. Aidha, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kukusanya fedha za tozo kutoka makampuni ya uchimbaji wa madini ambayo
ndio waaribifu wakubwa wa barabara zetu kwa kusafirisha mizigo mizito na magari
makubwa na kufutiwa msamaha wa tozo hilo kama watumiaji wakubwa wa mafuta, huku
wafanyakazi na wafanyabiashara wanatozwa tozo hilo kila wanaponunua mafuta, kwa
kutoa msamaha kwa makampuni haya yanaukosesha mfuko wa Barabara kiasi kikubwa
cha fedha.
4.1
Matumizi
mabaya ya fedha za Mfuko wa barabara.
Mheshimiwa Spika,
pamoja na mfuko wa barabara kujitahidi kukusanya mapato kwa wingi, ila pia kasi
ya matumizi ya fedha hizo kwa ajili ya masuala ambayo sio ya kujenga barabara moja
kwa moja imeongezeka sana, kwa mfano kwa mwaka huu wa fedha kwa mujibu wa
randama kiasi cha shilingi bilioni 9.126 zilizotengwa (tazama
kiambatanisho A ni Jedwali na 4) ni kwa ajili ya miradi inayotekelezwa kwa
kutumia fedha za mfuko wa barabara (5.5.2.1
Barabara Kuu), kati ya fedha hizo Kiasi
cha shilingi bilioni 2.460 kitatumika kwa ajili ya matumizi ambayo siyo ya
kujenga barabara moja kwa moja kama ifuatavyo;
i.
kifungu cha 2326,training and Technical
assistance TANROADS Shilingi milioni
300.00 , hizi ni kwa ajili ya kutoa mafunzo ya kitaalam kwa wafanyakazi 100
wa TANROADS
ii.
Kifungu 2326, updating of draft design
manual 1989 and economic analysis manuals for TANROADS ,shilingi milioni 300.00
iii.
Kifungu 2326,vifaa vya maabara,ufuatiliaji
na usimamizi wa kazi za ujenzi wa barabara shilingi milioni 500.00
iv.
Kifungu 2326, kuandaa mpango mkakati wa
TANROADS kwa kipindi cha miaka mitano shilingi milioni 100.00
v.
Kifungu 2326,ufuatiliaji na usimamizi wa
kazi za ujenzi wa Barabara TANROADS shilingi milioni 400.00
vi.
Kifungu 2326, ufuatiliaji na usimamizi wa
miradi (monitoring and other related activities ) shilingi milioni 860.00
Mheshimiwa Spika, Aidha,
kwa upande wa barabara za mikoa Fedha za mfuko wa barabara ambazo zitatumika
kwenye mambo ambayo sio kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa moja kwa moja wa
barabara ni kiasi cha zaidi shilingi bilioni
2.465 ,tazama kiambatanisho B uk. 26
&27
Kambi rasmi ya Upinzani,
inataka kujua mambo yafuatayo;
i.
Kwanini fedha za mfuko wa barabara
hazielekezwi zote kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara ?
ii.
Mbona fedha kwa ajili ya kufuatilia na
kusimamia miradi ni nyingi sana wakati kwenye mikataba ya ujenzi fedha za
usimamizi wa mradi huwa zipo?
iii.
Je? Ni kwanini fedha kwa ajili ya mafunzo,
uandaaji wa nyaraka mbalimbali za wizara zisitokane na fungu la serikali kuu na
fedha za mfuko wa barabara zikawa ni kwa ajili ya kuwekezwa zote kwenye sekta
husika , yaani ujenzi na ukarabati wa barabara na si matumizi mengine.
5.0
MSONGAMANO
JIJI LA DAR ES SALAAM
Mheshimiwa Spika,
kama Taifa tunapoteza wastani wa masaa 4 kila siku za kufanya kazi ukiwa
barabarani sawa na siku 112 za kazi kwa mwaka, hiki si kiasi kidogo katika nchi
maskini inayohitaji maendeleo kwa haraka kuzipoteza barabarani badala ya
kutumika katika uzalishaji, na wafanyakazi kulipwa mshahara kamili wa masaa 8
ya kazi wakati amefanya kazi kwa masaa 4 tu, Taifa linapoteza kiasi kikubwa
katika ujira, watumiaji wa barabara wanatoa fedha zaidi kufika mahali
anapokwenda kwa kuchoma mafuta akiwa amesimama barabarani muda mrefu sana na
hasara hii haipimiki.
Mheshimiwa Spika,
hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza yafuatayo:-
1. Kasi
ya Ujenzi wa Mradi wa DART(Mabasi yaendayo kasi Dar) iongezwe ili mradi huu
ukamilike kwa haraka kupunguza tatizo la
msongamano Dar.
2. Miradi
ya barabara za viungo (Ring Roads) ikamilishwe na kutazama barabara mpya
zitakazosaidia kupunguza msongamano.
3. Kutafuta
fedha maalum(Special fund) hata kwa kukopa kwa ajili ya barabara za Dar es
Salaam na kuzijenga upya na kujenga barabara za juu (Fly overs) badala ya
kusubiri wahisani hata kujenga KM 3 toka UDA depot/Kamata junction tunasubiri
fadhila na hisani, hii ni aibu kwa Taifa letu.
4. Upanuzi
wa barabara unaooendelea sasa uzingatie mahitaji ya baadae na si sasa. Kila
panapostahili tujenge njia zaidi ya mbili kila upande, tuachane na mazoea ya
njia 2 twende njia 3 au 4 kila upande wa barabara na Jambo hili lianze sasa.
Mheshimiwa Spika,
kwa fedha zinazotengwa katika bajeti za kila mwaka ya Wizara hatuwezi kumaliza
tatizo la barabara za Dar es Salaam, Serikali ichukue maamuzi magumu ya kuwa na
fedha za kutosha (special fund) kwa tatizo la Dar es Salaam mji unakua kwa kasi
kubwa.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali na Wizara hivi sasa kuwasilisha
Bungeni mipango ya muda mfupi/Kati/ mrefu wa kukabiliana na changamoto za kukua
kwa miji ya Arusha, Mwanza na Mbeya na tatizo la msongamano ambao umeanza
kujitokeza katika miji hiyo, ili tuweze kujiandaa mapema badala ya kusubiri
mpaka hali iwe mbaya ndipo tuanze kuchukua hatua za dharura.
6.0
DARAJA
LA KIGAMBONI
Mheshimiwa Spika,
katika ujenzi wa daraja hili la
Kigamboni Kambi Rasmi ya Upinzani inaipongeza NSSF na wadau wengine kwa kuona
umuhimu wa daraja hili na kuchukua tahadhari ya mahitaji ya baadae kwa kuongeza
njia katika kila upande wa Barabara hiyo lakini Wizara inapaswa kujipanga sasa
namna ya kukabiliana kuyaondoa magari mengi yatakayokuwa yanatumia barabara
hiyo, vinginevyo itakuwa haina tija kwa
maana utakwenda kasi darajani unakuja kukwama uhasibu junction (Mandela/Kilwa
Rd) na Uda Depot(Mandela road)
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kupata maelezo, ratiba na maandalizi ya
kukabiliana na changamoto hiyo ili mradi huu uweze kuleta tija kwa taifa.
7.0
MIRADI
YA UJENZI WA BARABARA
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa taarifa ya Wizara, Wizara ilipokea fedha zote 100% kwa ajili ya
miradi ya maendeleo kwa mwaka 2012/13, hata hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani
inasikitishwa kwamba fedha iliyoombwa haikutumika katika miradi mingi
iliyoombewa fedha mwaka 2012/13 na kutokamilika kwa miradi hiyo hususan
barabara za Dar es Salaam kama vile barabara ya Kimara-Kilungule,Mbezi-malamba
mawili-Kinyerezi, Banana-Tegeta, Kibaoni-Wazo-Goba, Mbezi
Morogoro-Tangibovu-Goba na Kimara Baruti.
Mheshimiwa Spika,
wananchi wamechoshwa na hotuba za Mawaziri zenye matumaini,ahadi na maneno
mengi huku wakijua na kuamini kwamba hawatatimiza wajibu wao na kulidanganya
Bunge na kuwapa wananchi matumaini yasiyotekelezeka. Kambi Rasmi ya Upinzani
inashauri miradi inayoombewa fedha na kuidhinishwa na Bunge itekelezwe kwa
mujibu wa mpango wa bajeti na si vinginevyo.
Mheshimiwa Spika,
miradi ya barabara kuu, kadhalika haijengwi kwa kasi inayotakiwa, miradi mingi
ambayo ilikuwa ikamilike mwaka 2012, 2013 na mapema 2014 bado haijakamilika
hadi sasa. Ujenzi wa barabara nyingi kati ya hizo umefikia chini ya asilimia
50% ya ujenzi, kama Barabara ya Sumbawanga/Kibaoni, Sumbawanga/Kasanga, Tabora/Nzega,
Tabora/Ndono, Ndono/Urambo, Kyaka/Bugene/Kasulo. Manyoni/Itigi/Chaya,Tabora/Nyahua,
Korogwe/Handeni, Korogwe/ Mkumbara, Mkumbara/Same, Mbeya/Lwanjilo, Lwanjilo/Chunya,Chalinze/
Kitumbi, Mhe Spika, orodha ni ndefu, lakini zipo pia ambazo
zimejengwa kwa kiwango cha kati ya 45%-70% kadhalika orodha ni ndefu kwa ujumla
miradi yetu yote ya barabara haikamiliki kwa wakati ni pamoja na barabara ya
Iringa/ Dodoma/Kondoa/Babati.
Mheshimiwa Spika,
hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani na
watanzania kwa ujumla wanataka kujua juu ya masuala yafuatayo:
a. Kwa
nini miradi hii haijakamilika kwa mujibu wa mikataba iliyopo, aidha wanataka
kujua hasara inayopatikana kutokana na kutokamilika kwa miradi hii kwa wakati.
b. Gharama
halisi ya miradi hii hadi sasa imeongezeka kwa kiasi gani kulinganisha na
gharama za awali kutokana na kuchelewa kwa miradi hii ?
c. Zipo
taarifa kuwa baadhi ya miradi iliyokamilika na kutumika bado ina madeni, je? inadaiwa
kiasi gani na lini italipwa?
d. Watanzania
wanataka kujua jumla ya riba na deni tunalodaiwa katika miradi ya barabara ni
kiasi gani mpaka sasa na kuna mkakati gani wa kulipa deni hilo?
e. Serikali
itoe maelezo ya kina ni sababu zipi zilizopelekea kampuni ya Progressive
kupewa mkataba wa kujenga barabara ya Tunduma/Matemanga/
Kilimasera/Namtumbo ambayo iligawanywa lot 3 na zote kupewa kampuni moja, mbaya
zaidi kampuni hiyo haikuwa na sifa ya
kujenga barabara, katika nchi za Afrika, nani aliitambua, nani aliileta nchini,
nani aliwasaidia kupata kazi na kwanini wameshindwa. Je muda na hasara
tunayopata na kuchelewa kwa mradi kwa hatua zilizochukuliwa nani analipa na
nani kawajibishwa kwa uzembe huu.
f. Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Wizara kutoa ratiba na mpango mkakati wa kufungua
kanda ya Kusini na Magharibi kwa barabara ya Masasi hadi Mbamba-bay.
Tabora/Mbeya, Tabora/Mpanda, Mpanda/Kogoma na Kigoma/Biharamulo.
g. Ujenzi
wa barabara uzingatie michoro, sheria za ujenzi wa barabara na kuondosha mara
moja matuta madogo madogo katika barabara kuu, maarufu kama Rasta zinaleta
uharibifu mkubwa kwenye vyombo vya
usafiri na inapokuwa lazima, wajenge Bumps zenye uwiano kwa barabara zote na kuwepo alama za barabarani. Hakuna barabara
kuu (Highway) yeyote duniani iliyo na rasta na
Bumps ila Tanzania, tunaona BUMPS katika barabara za mijini na si high way.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
miradi yetu yote izingatie mpango wa Taifa wa miaka 5, na uwezo wa kifedha wa nchi.
Wataalam watimize wajibu wao na wasiwe
watumwa wa kauli na ilani za kisiasa-Mwalimu alisema, “Kupanga ni
kuchagua” –ukishindwa kuchagua huwezi kupanga.
8.0
TANROADS
Mheshimiwa Spika,
wakala huu ni muhimu sana katika kusimamia na kuendeleza ujenzi wa Barabara
nchini, kwa mujibu wa Taarifa ya ukaguzi wa utendaji ya PPRA kwa 2011/2012
inasema kuwa Tanroads kwenye kipengele cha kusimamia ubora (compliance level and Quality
Control) imepewa alama 45 kati ya 100, PPRA imeshindwa kupata taarifa
za kumbukumbu kwamba Tanroads ina mpango wowote wa kusimamia ubora wa kazi
kwenye mikataba inayotolewa. Aidha kwenye kipengele cha mikataba (compliance
on contracts Management) imepewa alama 0 kati ya alama 100, kwa maana
kwamba PPRA hawakuona ushahidi wowote kwamba Mamlaka imekuwa ikisimamia
mikataba kwa bidhaa na huduma zinazotolewa kwa mujibu wa mikataba na
wakandarasi
Mheshimiwa Spika, ni
dhahiri kwamba kwa hali hii bado tutaendelea kushuhudia mikataba mibovu, ujuzi
chini ya kiwango, hasara kwa taifa na kupungua kwa kasi ya maendeleo ya nchi.
Mheshimiwa Spika,
hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Wizara ya Ujenzi kushughulikia
mapungufu hayo na kuondoa dosari zilizopo kwa kupata wataalam wenye sifa, uwezo
na weledi katika maeneo yenye mapungufu na kutoa fursa za mafunzo kwa wataalam
waliopo, aidha uongozi na utawala uimarishwe.
9.0
WAKALA
WA BARABARA VIJIJINI
Mheshimiwa Spika,
tunatambua barabara vijijini zinasimamiwa na Halmashauri zetu ambazo nyingi hazina
uwezo mkubwa wa kifedha na pia hutengewa fedha kidogo na mfuko wa barabara
kulingana na kazi kubwa wanayotakiwa kufanya ya kuhakikisha kuwa barabara
zinapitika katika kipindi chote cha mwaka mzima, Aidha wana ukosefu mkubwa wa
nyenzo na wataalam. Kutokana na umuhimu wa barabara hizi kwa uchumi wa wananchi
wetu ambao wanaishi vijijini , kwa mara nyingine tena Kambi Rasmi ya Upinzani
inapenda kuishauri Serikali na kupendekeza kuwepo na WAKALA WA BARABARA VIJIJINI (RURAL ROADS AGENCY) kwa ajili ya usimamizi,
ufanisi na ujenzi wa barabara bora vijijini.
Mheshimiwa Spika, Kwa
kufanya hivyo tutaweza kufungua uchumi wa vijijini kwani kutakuwa na wakala
ambaye atakuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa barabara zinafanyiwa matengenezo
na ukarabati kwa wakati na hivyo kurahisisha uchukuzi wa mazao ya vyakula
kutoka maeneo ya uzalishaji na kuweza kuwafikia watumiaji wa mazao hayo yakiwa
katika hali ya ubora zaidi na hivyo yataweza kuongezewa thamani kulingana na
ubora wake .Aidha, tutaweza kuchochea uzalishaji kwa kiwango kikubwa kwani
maeneo mengi ya vijijini mazao huharibika kutokana na kukosekana kwa barabara
na hivyo kuwakatisha tamaa wakulima/wazalishaji, pia Taifa litakuwa na uhakika
wa barabara/madaraja yatajengwa katika kiwango cha kuridhisha na thamani ya
fedha(value for money) kuonekana na kupimika.
10.0 VIVUKO NA MADARAJA
Mheshimiwa Spika,
katika eneo hili juhudi zimefanyika kwa kiwango ambacho si cha kuridhisha sana
pamoja na changamoto zake, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Wizara kuagiza na
kusimamia kwa uangalizi mahususi kuhakikisha madaraja yote yanayojengwa
yanakamilika kwa wakati. Ubora na usalama kwa vivuko vyetu vyote nchini
uimarishwe, matengenezo yafanyike kwa wakati, vifaa vya usalama viwepo vya
kutosha, pia ukaguzi wa mara kwa mara uimarishwe na uthibiti wa idadi ya abiria
na mizigo uzingatiwe.
Mheshimiwa
Spika, kwa umuhimu wa mahitaji ya kipekee na haraka, Mv Ilagala ni kidog na chakavu kimekuwa kikiharibika
mara kwa mara ni lini kivuko cha uhakika kitapelekwa licha ya kuwepo kwa ahadi
nyingi, au kujenga daraja katika mto Malagarasi kama mto Kilombero ili kuondoa
adha hiyo?
Mheshimiwa Spika,
katika hotuba yetu ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa tulishauri kwamba, “Kikosi cha Wanamaji (Navy)
kinatumika chini ya Kiwango. Licha ya kikosi hiki kuwa na wahandisi wa usafiri
majini waliobobea, Serikali hii ya CCM imekuwa ikitoa zabuni za kutengeneza
vivuko kwa wakandarasi wengine kwa gharama kubwa wakati wanajeshi wenye taaluma
hiyo wapo.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa zabuni za kutengeza
vivuko kwa kikosi cha wanamaji kwa kuwa wana taaluma hiyo, na pia kwa kufanya
hivyo wanapata nafasi ya kufanyia mazoezi taaluma zao”.
Mheshimiwa Spika,
kwa kuwa jukumu la vivuko, madaraja na barabara liko chini ya Wizara hii ya
Ujenzi, hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Wizara kulifanyia kazi pendekezo
hilo ili kuangalia ni kwa jinsi gani kamandi hii ya navy itakavyoweza kutekeleza
jukumu hilo la utengenezaji na ukarabati wa vivuko.
11.0 TAMESA
Mheshimiwa Spika,
kitengo hiki ni muhimu sana katika kuthibiti matumizi bora ya fedha za umma
katika matengenezo ya magari ya Serikali kuu na Serikali za mitaa. Sehemu kubwa
ya matumizi ya Serikali yanagusa usafirishaji na upo mwanya wa ubadhirifu, wizi
na matumizi mabaya katika gharama za uendeshaji wa sekta ya usafiri katika Serikali
na kulipa gharama kubwa za matengenezo katika karakana na makampuni binafsi.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kwamba:
i.
Serikali ifanye maamuzi bila ya kuchelewa
kukiimarisha kitengo hiki kwa raslimali fedha na watu (wataalamu), nyenzo na
majengo ya karakana ili magari yote
yatengenezwe kupitia wakala huu kama ilivyokuwa zamani na kupiga marufuku
magari ya Serikali kufanyiwa matengenezo katika karakana binafsi.
ii.
Wakati Serikali inajipanga kutekeleza hilo,
kama imeweza kusimamia kuagiza mafuta
nchini kwa utaratibu wa Bulk Procurement, Serikali iiwezeshe TAMESA
kufanya “Bulk Procurement” ya Matairi ya magari kwa ajili ya Serikali. Jambo
hili si gumu hata kidogo ili kuwepo na bei inayofanana, na ubora wa matairi kwa
magari ya Serikali/Halmashauri badala ya kila idara, Wizara, Taasisi kununua
kwa bei wanayoikuta sokoni na yenye kupishana kwa kiwango kikubwa na ubora.
12.0 WAKALA WA MAJENGO(TBA)
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka wa fedha uliopita 2012/2013 waziri wakati anawasilisha hotuba yake
ya bajeti alisema kuwa wakala wa majengo uko katika mchakato wa ujenzi wa
nyumba 10,000 katika mikoa yote kwa
ajili ya kuishi watumishi wa umma .Aidha , alisema kuwa katika mwaka huo wa
fedha wizara kupitia wakala wa majengo ilikuwa imepanga kujenga nyumba 2,500 katika mikoa yote ya Tanzania
Bara na fedha kwa ajili ya kukamilisha mradi huo zilikuwa tayari zimepatikana,
kama mkopo kutoka kwenye Mabenki ya ndani ambayo TBA ilikuwa imeomba .
Mheshimiwa Spika,
waziri alisema katika hotuba yake ya bajeti kwamba, naomba kunukuu “Aidha
katika mwaka wa fedha 2012/2013 wizara kupitia wakala wa majengo Tanzania
imepanga kujenga nyumba 2,500 katika mikoa yote ya Tanzania Bara”(ukurasa
159 aya 230), hakika maneno haya yalikuwa faraja kwa
watumishi na matumaini kwa watanzania.
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni,
inataka kujua majengo hayo 2,500 ambayo yalikuwa tayari yametengewa fedha
kwenye bajeti iliyopita yamejengwa katika mikoa gani na maeneo gani hapa nchini,
Je? Nyumba hizo wamepewa watumishi wa kada gani na ni vigezo gani vilitumika
katika kugawa nyumba hizo kwa watumishi
hao.
13.0 HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
kumekuwepo malalamiko na kutokuridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Wizara na
Taasisi zake hususan Tanroads kutowalipa wananchi fidia stahiki, za haki na kwa
wakati wananchi hawaridhishwi na kauli za viongozi wa Wizara hususan katika
suala la kuwalipa wananchi fidia kwa mali zao wakipisha miradi mbalimbali za
ujenzi nchini.
Mheshimiwa Spika, miradi
ya ujenzi, na hasa barabara za lami ni maendeleo kwa jamii pana na Taifa, kwa
mwananchi wa kawaida maendeleo kwetu ni nyumba/shamba/ardhi yake hata kama
nyumba ni ya miti, tofali za tope na kuezekwa kwa nyasi kwake ni maendeleo na
si barabara ya lami, unapomvunjia/kunyang’anya ardhi yake unamzidishia
mtanzania huyo umaskini kwa gharama ya maendeleo ya jamii pana. Kwa sababu
yoyote ile, kwa namna yoyote ile haki yake ni lazima narudia ni lazima alipwe,
kitendo chochote cha kuvunja au kunyang’anya mali ya mtu yeyote ni dhulma kama
inafanywa na mtu au Serikali ni dhulma.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani kamwe haiwezi kukubali, kushangilia au kushiriki katika
dhulma hii, tunasema walipeni haki zao hawa watanzania maskini ambao mali
mnazoziharibu na kunyang’anya ndio maendeleo na ustawi wa maisha ya familia
zao, na kama kweli Serikali ya CCM inavyodai maisha bora kwa kila mtanzania,
basi boresheni maisha ya watanzania hawa kwa kuwalipa stahiki zao ili waweze
kupata makazi/Ardhi mbadala, waondoleeni watanzania hawa mifadhaiko ya maisha
na chuki dhidi ya Serikali.
Mheshimiwa Spika,
chakula, nguo, malazi ni haki za msingi kwa kila binadamu, hata kama ni kibanda
ndiyo makazi yake, hakuna mtu yeyote mwenye haki ya kumnyang’anya mwingine
haki hizo bila ya kufidia au kumpatia makazi mbadala. Kilio cha fidia, fidia
zisizostahiki, fidia za upendeleo na kutokulipwa ndio kilio cha watanzania kila
kwenye mradi wa ujenzi hususan Barabara. Orodha ni ndefu ya wananchi
wanaolalamika kila palipo na mradi na hata waliokuwa tayari kupisha mradi kwa
ahadi ya kulipwa wanaendelea kusumbuliwa na urasimu wa Tanroads, Wizara na
Hazina, walipeni wananchi haki zao mapema.
Mheshimiwa Spika,
mihimili ya dola kila mmoja ufanye kazi bila kuingiliwa na kuheshimika. Wizara
hii na Tanroads haipo juu ya sheria na inatakiwa kuheshimu sheria hata pale
panapotolewa tangazo (notice) ya kukusudia kuishtaki Serikali kabla serikali
haija wasilisha majibu katika vyombo vya haki. Wakala wa barabara anavunja
nyumba za watanzania maskini tena wenye hati miliki ya viwanja zilizotolea na
mamlka za Serikali hii kabla shauri kusikilizwa mahakamani, huu ni ukiukwaji
mkubwa wa haki za raia, kuheshimiwa utu wake na kusikilizwa. Wizara hii
isiwaongezee watanzania umaskini. Wakaazi wa Minsukumilo/Mpanda Hotel ni
wahanga wa ubabe huu wa kutoheshimu mamlaka nyingine.
Mheshimiwa Spika,
kuwepo kwa sheria ni jambo moja, kusimamia sheria ni jambo lingine. Uungwana na lugha njema ni zaidi ya hayo, kwa
kuwa Wizara ilishindwa kutambua na kuweka mipaka ya maeneo yao toka sheria
ilipotungwa mwaka 1926, leo wanamlaumu nani kuvamia maeneo yao, sasa ndio
wanakumbuka kwamba wanamaeneo ambayo tayari ni makazi ya wananchi si kisingizio
cha kuwapora haki zao, wangeliweka mapema mipaka ya hifadhi ya barabara
wananchi wasingelijenga wangeheshimu mipaka hiyo iliyokuwepo vingenevyo wizara
inakwepa uzembe wake kwa kuwaadhibu watanzania maskini.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulipa fidia kwa wote sio watu wa Dar
es Salaam walipwe fidia. Watanzania wote wanahaki sawa mbele ya sheria, Kambi
Rasmi ya Upinzani hairidhiki na watanzania maskini kutolipwa fidia katika
miradi mbalimbali ya barabara nchini, fidia stahiki na kwa wakati.
Mheshimiwa Spika,
baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.
…………………………………..
Said A. Arfi (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani-
Wizara ya Ujenzi
13.05.2013Source:CHADEMA social media.
No comments:
Post a Comment