HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHESHIMIWA JOSEPH O. MBILINYI (MB) KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA KAZI NA AJIRA KWA MWAKA 2013/2014 (Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya kanuni za Bunge toleo la mwaka 2013)
1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa spika, mwaka jana nilianza
hotuba yangu kwa kutoa pole kwa ndugu jamaa na marafiki wa wale wote waliofariki dunia kwa ajali ya mv
skagit, mwaka huu naomba nianze hotuba yangu kwa kutoa pole kwa ndugu jamaa na
marafiki wa wale waliofariki kwa ajali nyingine ya kizembe ya kuanguka kwa
ghorofa la Dar Es Salaam. Aidha, mwaka jana nilianza kwa kutoa pole kwa Mh.
Joseph selasini kwa kufiwa na baba yake na mwaka huu nianze pia kwa kutoa pole
kwa Mh. mchungaji Israel Natse kwa kufiwa na baba yake mzee Yohana Natse.
Mwenyezi Mungu ailaze roho yake , mahali pema peponi.
Mheshimiwa Spika, hakuna ubishi wala
ushindani kuwa Serikali yoyote makini duniani huweka sera na mifumo thabiti ya
kuhakikisha kuwa ajira za kutosha zinatengenezwa, mazingira ya kazi yanaboreshwa
na wafanyakazi wanalipwa ujira na mishahara yenye staha, si tu kwaajili ya
kuwawezesha kumudu gharama za maisha, bali pia kuwapa morali wa kutekeleza
majukumu yao kwa ufanisi zaidi kwa maendeleo ya taifa.
Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza
kuwa Taifa lolote duniani ambalo haliwezi
kutengeneza ajira na hivyo kuwafanya vijana wake wengi wenye uwezo wa kuajiriwa
kuzurura mitaani, na wale walio vyuoni wanashindwa kusoma kwa sababu ya
Serikali kushindwa au kupuuza kugharamia masomo yao; sote tunatambua kuwa Taifa
hili limejaliwa rasilimali nyingi za
utalii na madini ya thamani, lenye vyanzo vingi vya kodi na mapato, lakini
limegubikwa na migogoro mingi, ya mara kwa mara na isiyokwisha, ya wafanyakazi
wanaodai haki na mafao yao halali, huku wakiishia kunyamazishwa kwa kauli laini
zenye matumaini hewa; Kwa namna yoyote ile taifa hilo, ni kielelezo cha nchi
inayoongozwa na Serikali isiyo na vipaumbele, yenye viongozi wasiojali na
wanaotekeleza sera wasizozijua au zilizoshindwa.
2.0 MIFUKO YA HIFADHI YA
JAMII
Mheshimiwa Spika, katika Maoni yetu ya
mwaka jana, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilituhumu kwamba Serikali hii ya
CCM haiijatekeleza ahadi zake kwa Watanzania kuhusu mifuko ya hifadhi ya jamii
kama zilivyotajwa katika Ilani ya
Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya 2010 – 2015. Katika Maoni hayo tulidai
kwamba ahadi ya “… kurekebisha viwango vya mafao ili visipishane mno
haijatekelezwa hadi sasa kwani viwango vya mafao vinavyotolewa na Mifuko mbali
mbali ya Hifadhi ya Jamii ni vile vile vya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2010.”
Aidha, tulifafanua jinsi ambavyo ahadi ya “… ya kupanua wigo wa kinga ya
hifadhi ya jamii ili Watanzania wengi zaidi wafaidike na huduma hiyo nayo
haijatekelezwa.” Vile vile, tulionyesha jinsi ambavyo ahadi ya “kuelimisha jamii … juu ya umuhimu wa
hifadhi ya jamii kwa maendeleo ya wafanyakazi na ya nchi kwa ujumla”, nayo
haikutekelezwa kwa sababu Serikali yenyewe imekiri kwamba ‘“… bado kuna uelewa mdogo wa masuala ya hifadhi
ya jamii kwa watunga sera, waajiri, waajiriwa, wanachama na wananchi kwa
ujumla.”’
Mheshimiwa Spika, katika Maoni yetu
hayo tulionyesha kwamba ahadi pekee ambayo Serikali hii ya CCM imeitekeleza ni “… kuendelea kutumia fedha za wafanyakazi
zilizomo katika Mifuko mbali mbali ya Hifadhi ya Jamii kuwekeza katika miradi
ambayo haina manufaa yoyote kwa wafanyakazi wenyewe.” Tulifanya rejea pana
ya Taarifa Kuu ya Mwaka ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Kuhusu Hesabu za Mashirika ya Umma na
Taasisi Zingine kwa Mwaka 2010/2011, iliyoonyesha kwamba “… kuna udhaifu
mkubwa katika vitega uchumi vinavyosimamiwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.”
Hivyo, kwa mfano, ukaguzi wa vitega uchumi vya NSSF
ulionyesha kwamba licha ya Mfuko huo kuwekeza zaidi shilingi bilioni 269.272 za
wafanyakazi katika ujenzi wa Awamu ya Kwanza na ya Pili ya Chuo Kikuu cha
Dodoma (UDOM), sio tu Mfuko huo ‘“… ulikuwa haujasaini mkataba na Serikali juu
ya fedha za mradi huo”’, bali pia ulikuwa ‘“…
haujapokea fedha ya pango, au malipo ya mkopo kutoka Serikalini ambao tayari
umelimbikiza riba ya shilingi bilioni 14.157.”’
Mheshimiwa Spika, kwa kutumia Taarifa
ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu tulionyesha kwamba sio fedha za NSSF tu ambazo
zimetumiwa na Serikali hii ya CCM kwenye UDOM. Kama tulivyosema, “… PPF
imekwishazamisha jumla ya shilingi bilioni 39.987; PSPF imechakachuliwa
shilingi bilioni 105.921; LAPF imepoteza shilingi bilioni 22.030; wakati ambapo
NHIF imekwishaunguza shilingi bilioni 13.403 za wanachama wake. Jumla ya fedha
za wafanyakazi wanachama wa Mifuko hii mitano ambazo zimeunguzwa katika ujenzi
wa UDOM ni shilingi bilioni 450.615…. Vitega uchumi vyote hivi katika UDOM …
havirudishi fedha za mikopo ya Mifuko
husika.” Hali kadhalika, tulionyesha
jinsi ambavyo ujenzi wa Jengo la Idara ya Usalama wa Taifa ulivyotafuna
shilingi bilioni 11.83 za NSSF na PSPF ambazo hadi tunaandika Maoni yetu ya
mwaka jana zilikuwa hazijaanza kulipwa pamoja na riba yake! Vile vile,
tulionyesha kwamba jumla ya shilingi bilioni 19.77 zilitolewa kama mikopo na
NSSF, PPF na LAPF kwa ajili ya ujenzi wa Ukumbi huu wa Bunge lako tukufu “…
hazijalipwa hadi sasa.” Aidha, zaidi ya shilingi bilioni 152.6 zilizotolewa
kama mikopo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Jeshi la Polisi, Machinga Complex,
Continental Venture Tanzania Ltd., Meditech Industrial Co. Ltd., General Tyre,
Dar es Salaam Cement Co. Ltd., Kagera Sugar, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa
Elimu ya Juu (HESLB) na Kiwira Power Ltd. haikuwa imelipwa. Kwa sababu hizo,
tulimnukuu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali akisema “… ukubwa wa biashara inayofanywa baina ya
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na taasisi za Serikali na malipo yasiyokuwa na
uhakika ya mikopo hiyo yanatia shaka juu ya uendelevu wa Mifuko husika katika
siku chache zijazo.”
Mheshimiwa Spika, licha ya kuwa
yalitokana na Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambaye
ni mteuliwa wa mhe. Rais Mheshimiwa Dokta Jakaya Mrisho Kikwete, Maoni ya Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni yalishambuliwa sana na Wabunge wa CCM na wawakilishi
wa Serikali yake humu bungeni. Hata hivyo, facts
are very stubborn things, kama mwanamapinduzi mmoja wa karne iliyopita
alivyokuwa anapenda kusema. ‘Ukweli ni vitu vikorofi sana’! Na ukweli juu ya
afya ya Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii ni vitu vikorofi kweli kweli, ambavyo
haviwezi kuzimwa na propaganda nyepesi nyepesi za watawala na wawezeshaji wao
ndani na nje ya Bunge hili tukufu.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba yake
wakati wa Sherehe za Mei Mosi mwaka huu kule Mbeya, Rais Kikwete alielezea
‘tathmini ya afya ya kifedha’ ya Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii nchini kama
sehemu ya ‘maboresho’ ya sekta hiyo. Tunaomba kumnukuu Rais in extenso: “Tathmini hiyo imeonesha kuwa mifuko yetu ya hifadhi ya jamii ipo kwenye
hali nzuri kifedha na ni endelevu. Kwa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma
(PSPF), Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya malipo ya michango ya
watumishi waliokuwepo kabla ya mwezi Julai 1999 mfuko ulipoanzishwa rasmi. Kwa
hiyo, katika mwaka ujao wa fedha, Serikali italipa shilingi bilioni 50 ikiwa ni
sehemu ya malipo hayo. Napenda kuwatoa hofu wanachama wa Mfuko huo kuwa mafao
yao yako salama. Hakuna atakayestaafu akakosa kulipwa mafao yake.
“Vile vile Mamlaka ya
Udhibiti na Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kwa kushirikiana na
Benki Kuu wameandaa na kutoa miongozo … yenye lengo la kuiwezesha mifuko ya
hifadhi ya jamii kufanya uwekezaji ulio bora na wenye tija unaomnufaisha
mwanachama na taifa kwa ujumla. Tangu kuanza kutumika kwa miongozo hiyo Mei
2012, uwekezaji wa mifuko hiyo umeongezeka kutoka shilingi trilioni 3.38 mpaka
shilingi trilioni 4.24. Pia mali za mifuko hiyo zimeongezeka kutoka shilingi
trilioni 3.74 hadi kufikia shilingi trilioni 4.73.”
Mheshimiwa Spika, matrilioni haya ya
Rais Kikwete yanahitaji kuchukuliwa kwa tahadhari kubwa na Bunge lako tukufu.
Hii ni kwa sababu takwimu hizi zimetiliwa na shaka na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Kuhusu Ukaguzi
wa Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012 iliyowasilishwa kwa Rais
tarehe 28 Machi, 2013. Tunaomba kuiacha Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
ijisemee yenyewe: “Ukaguzi wa Mfuko wa
Pensheni kwa Wafanyakazi wa Serikali Kuu (PSPF) ulibaini kwamba ‘actuarial
valuation’ iliyofanyika … tarehe 30 Juni, 2010 … ilionyesha kuwa hali ya
kifedha ya Mfuko iliendelea kuwa mbaya. Ukadiriaji thamani ulibaini hasara
halisi ya shilingi trilioni 6.487 kwa mwaka unaoishia tarehe 30 Juni, 2010.
“Pia nilibaini kwamba
katika mwaka wa fedha 2011, Serikali ilikubali kuanza kurejesha mafao
yaliyolipwa na Mfuko kuanzia mwaka 2004 hadi 2010 kiasi cha shilingi za Kitanzania
bilioni 716. Kiasi hiki kilipaswa kurejeshwa kidogo kidogo na Serikali kila
mwaka katika mgawanyo wa shilingi bilioni 71.6 kwa muda wa miaka kumi kuanzia
mwaka 2010. Kufikia mwaka unaoishia tarehe 30 Juni, 2012 kulikuwa na
malimbikizo ya marejesho katika kipindi cha mwaka 2011 hadi 2012 na kufikia
kiasi cha shilingi bilioni 133. Vile vile, ilibainika kwamba, Serikali ya
Tanzania haikuweza kutoa fedha za kuziba pengo la upungufu uliojitokeza …
ikiashiria kuwepo kwa shaka kuhusiana na uwezo wa Mfuko kuendelea kulipa madeni
yake yanapokuwa tayari kwa kulipwa.”
Mheshimiwa Spika, ripoti ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu kwa mwaka wa fedha uliopita inafichua ‘ukweli korofi’ zaidi kuhusu
afya ya kifedha ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii hapa nchini. Hivyo basi, Ripoti hiyo
inaonyesha kwamba PSPF imetoa mikopo ‘isiyolipika’ ya jumla ya shilingi bilioni
67. 179 kwa Serikali na taasisi zisizo za kiserikali “… na hakuna malipo yoyote yalifanywa kwa Mfuko katika kipindi chote cha
mwaka. Hii inaweza kuharibu mtiririko wa fedha za Mfuko na matokeo yake
kushindwa kulipa mafao yanapofika wakati wa kulipwa.” Taasisi zisizokuwa za
kiserikali zilizofaidika na mikopo ‘isiyolipika’ ya fedha za watumishi wa
Serikali hii ya CCM ni pamoja na Tan Power Resources, kampuni iliyokuwa inamilikiwa
na familia ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa na ya swahiba wake Daniel Yona ambayo
iliwahi kumilikishwa Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira kwa njia za kifisadi. Kwa
mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, Tan Power Resources ina ‘madeni
yasiyolipika’ kwa PSPF ya jumla ya shilingi bilioni 5.421! Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu inaeleza
kwamba PSPF imeingia mkataba na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kutoa
fedha za kujenga Chuo Kikuu cha Elimu Dodoma. Hata hivyo, “mapitio ya mkataba
yalibaini mkanganyiko wa tafsiri ambao unahitaji kutatuliwa mapema. Kutokuwa na
mkataba sahihi kunafanya kuwa na tafsiri mbali mbali ambazo matokeo yake ni
hasara kwa Mfuko iwapo mgogoro utajitokeza.”
Mheshimiwa Spika, PSPF sio Mfuko wa
Hifadhi ya Jamii pekee ambao afya yake ya kifedha ni ya mashaka. Kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu, PPF imetoa shilingi bilioni 71 katika ujenzi wa UDOM “… ingawa mkataba wa
kutoa fedha kwa ajili ya mradi huu kati ya Mfuko na Serikali … bado
haujakamilika hadi ripoti hii inaandaliwa.” Kwingineko katika Ripoti hiyo,
inasemekana kwamba majengo ya UDOM yenye thamani shilingi bilioni 452
‘zilizofadhiliwa’ na Mifuko ya Jamii ‘chini ya maelekezo ya Serikali’ “… hayajakabidhiwa
rasmi kwa Chuo Kikuu Dodoma na Serikali ambayo ilisaini mkataba na Mifuko ya
Jamii ya NSSF, PSPF, LAPF na PPF.”
Kwa kuhofia kwenda kinyume na matakwa ya kanuni ya
64(1)(d) na (e) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inachelea kumwita Rais Kikwete muongo kutokana na kauli yake juu ya afya ya
kifedha ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Hata hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inataka kujua, na Watanzania wanataka kujua, kati ya Rais na Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ni yupi anayesema ukweli kuhusu hali ya
kifedha ya Mifuko ya Hifadhi ya Afya ya Jamii katika nchi yetu? Ni nani
aaminiwe na Watanzania kati ya Rais Kikwete anayesema kwamba “… mifuko yetu ya hifadhi ya jamii ipo kwenye
hali nzuri kifedha na ni endelevu”; na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali anayesema kwamba “… hali ya
mfuko wa hifadhi ya jamii uko katika hatari ya kutoendelea kama hatua madhubuti
hazitachukuliwa na pande zinazohusika”? Aidha, wafanyakazi wa Serikali ya
Tanzania wampuuze yupi kati ya Rais ‘anayewatoa hofu’ kwamba “hakuna atakayestaafu akakosa kulipwa mafao
yake”; na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu anayedai kuwa kuna “… shaka kuhusiana na
uwezo wa Mfuko kuendelea kulipa madeni yake yanapokuwa tayari kwa kulipwa.”
Mwisho, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
Serikali hii ya CCM iwaambie Watanzania nani ni mkweli kati ya Rais Kikwete
anayedai kuwa mali za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imefikia shilingi trilioni
4.73; na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu anayetuambia kwamba ukaguzi wake wa PSPF
pekee unaonyesha ‘hasara halisi’ ya shilingi trilioni 6.487!
Mheshimiwa Spika, katika mazingira ya
kiza na utatanishi kama haya, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inarudia wito
wake wa mwaka jana kwa Serikali “…
kusitisha mara moja matumizi haya makubwa ya fedha za wafanyakazi katika miradi
ambayo inaelekea kuifilisi Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na hivyo kuhatarisha
maslahi ya moja kwa moja ya wafanyakazi wa Tanzania.”
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inarudia kauli
yake ya mwaka jana: “… Ni wazi kwamba
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya Tanzania inaongozwa, kuendeshwa na kusimamiwa na
watu ambao hawana uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ujuzi na uadilifu
unaohitajika kwa maslahi ya wafanyakazi wanachama wa Mifuko hiyo. Ni wazi, kwa
ushahidi huu, kwamba mabadiliko makubwa ya kimfumo na kiutendaji katika Mifuko
hii yanahitajika na kwa haraka kabla mifuko hii haijafilisika kabisa.” Vile vile, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inawataka wastaafu na wafanyakazi wa Tanzania sasa waelewe chanzo halisi cha
mafao yao ya uzeeni kucheleweshwa ama kutokuongezeka ama kutokulipwa kabisa na
Serikali hii ya CCM! Na wakishafahamu sababu halisi za mateso yao, wastaafu na
wafanyakazi wa Tanzania wachukue hatua stahiki dhidi ya wale wote ambao kwa
sera zao na utekelezaji wao wa sera hizo, wamesababisha mateso hayo kwa
wastaafu na wafanyakazi wetu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba
bila wafanyakazi kuchukua hatua hizo, maneno ya ibara ya 11(1) ya Katiba yetu
kwamba “mamlaka ya nchi itaweka utaratibu
unaofaa kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa haki ya mtu … kupata msaada
kutoka kwa jamii wakati wa uzee, maradhi au hali ya ulemavu, na katika hali
nyinginezo za mtu kuwa hajiwezi …” yatabaki dhihaka ya kikatili kwa
wastaafu na wafanyakazi wetu.
Mheshimiwa Spika, aidha Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kurejea
pendekezo letu tuliloishauri katika bajeti ya Wizara hii ya mwaka 2011/2012
katika kuona umuhimu wa kuiunganisha mifuko yote ya hifadhi za jamii na kubaki
katika wizara moja ambayo ni ya Kazi na Ajira. Kambi rasmi ya Upinzani
inasisitiza kuwa lengo kuu la kuunganisha mifuko hii ya hifadhi za jamii ni
katika kuirahisishia Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi za Jamii
(SSRA) katika kutekeleza Sheria moja na kuunda vifungu sawa vya kisheria
vitakavyosimamia utekelezaji na uendeshaji wa mifuko hii ambapo kwa sasa mifuko
hii imekuwa chini ya wizara tofauti na hivyo hata utekelezaji wake unakua mgumu
na kuleta ukinzani kwa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi za Jamii.
Tunasisitiza kuwa pendekezo letu ni kuifanya PPF na NSSF iunganishwe na kuwa
mfuko mmoja kwaajili ya Sekta Binafsi vilevile LAPF, PSPF na GEPF iunganishwe
na kuwa mfuko mmoja kwaajili ya Sekta ya Umma. Pia, kambi ya Upinzani
inapendekeza mifuko yote isimamiwe chini ya Wizara ya Kazi na Ajira.
3.0 NYONGEZA YA
MISHAHARA YA WAFANYAKAZI NCHINI
Mheshimiwa Spika, Katika hotuba yake
ya Mei Mosi mwaka huu, Raisi Kikwete alisema kuwa " ........Kwa upande wa makusanyo ya kodi kwa mfano,mapato yameongezeka kutoka
wastani wa shilingi bilioni 541 kwa
mwezi mwaka 2011/12 hadi kufikia shilingi
bilioni 637 kwa mwezi
mwaka 2012/13, ikiwa ni ongezeko la
asilimia 18. Mapato yanapoimarika kama hivi, Serikali inakuwa na uwezo mkubwa wa kuwahudumia
wananchi wake, kutekeleza miradi ya maendeleo na wakati huo huo kuboresha zaidi maslahi ya wafanyakazi........
Pamoja na mafanikio hayo,
lakini bado hatujafikia mahali ambapo tunaweza kuongeza mishahara kama vile
ambavyo tungependa sote tupate.
Hata kwa kiwango cha sasa ambacho sote tunakubaliana hakitoshi bado mishahara inachukua sehemu kubwa ya mapato ya
Serikali."
Mheshimiwa Spika, kitendo
cha Raisi kusema kuwa mishahara itaongezwa bila ya kutaja kiwango kama ilivyo
desturi ya mei mosi haitoshi. Ni lazima Serikali iseme kiwango cha nyongeza
ya mshahara kwa wafanyakazi nchini kwa
mwaka ujao wa fedha wa 2013/2014 ni kiasi gani, na je nyongeza hiyo itatatua
matatizo ya wafanyakazi kwa kiwango gani? Aidha, kambi rasmi ya Upinzani
Bungeni, inaiona kauli ya Mheshimiwa Raisi kuwa, Serikali imedhibiti ubadhirifu
wa umma, ni lazima ionekane katika mishahara ya wafanyakazi wa sekta zote za
umma na za binafsi.
4.0 PUNGUZO LA KODI YA MAPATO KWA WAFANYAKAZI PAYE)
Mheshimiwa Spika,Pamoja na ugumu wa
mazingira ya kazi, mishahara duni na hali ngumu ya maisha nchini, bado
mfanyakazi anaendelea kunyonywa kwa kiwango kikubwa cha PAYE , ambacho ni moja
ya vyanzo vya Serikali katika mapato, huku Serikali ikishindwa kutafuta njia
nyingine mbadala za kukusanya kodi ikiwemo
kufuta misamaha ya kodi isiyo na tija kwenye uchumi wa taifa letu.
Mheshimiwa Spika, katika maoni
yetu ya mwaka jana, tulipendekeza kwamba kiwango cha PAYE ishuke kutoka
asilimia 14 za sasa hadi asilimia 9 kwa kiwango cha chini kinachotozwa na
asilimia 27 kwa kiwango cha juu kinachotozwa.Katika hotuba yake ya mei mosi,
zaidi ya kusema kwamba serikali imekamilisha uchambuzi wa maombi ya wafanyakazi
na kwamba waziri wa fedha atayafafanua zaidi katika hotuba yake ya bajeti,
Raisi Kikwete hakusema kodi ya pato la mfanyakazi itapungua kwa kiasi gani. Kwa
kuzingatia mapendekezo ya TUCTA kwamba kima cha chini cha mfanyakazi wa
Tanzania kiwe 350,000, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba
kiwango cha chini cha mshahara kitakachotozwa PAYE kiwe shilingi 350,000. Hii
itawezesha wafanyakazi wote wanaopata kiwango hicho cha mshahara au pungufu
yake kuwa na mapato zaidi na kukabiliana na mfumuko wa bei wa mara kwa mara na
kupanda kwa gharama za maisha.
Mheshimiwa Spika,wakati Serikali
hii ya CCM ikisita kupunguza mzigo wa maisha magumu unaowakabili wafanyakazi,
kwa kuwaongezea mshahara au kuwapunguzia PAYE , Serikali hiyohiyo haijawahi
kusita kutoa misamaha ya kodi kwa waajiri matajiri wa wafanyakazi. Ukweli ni
kwamba katika baadhi ya sekta
zinazoongoza kwa mauzo ya fedha za nje waajiri wamelipa kodi ya mapato
ya chini kuliko kodi ya PAYE wanayolipa wafanyakazi wao licha ya waajiri hao
kuwa na vipato vikubwa kutokana na mauzo ya bidhaa zao nje ya nchi. Kwa mfano,
kwa mujibu wa hotuba ya bajeti waziri wa nishati na madini iliyowasilishwa
na waziri mwenye dhdamana, Mh. Prof. Muhongo, katika kipindi cha miaka 14
(1992-2012), makampuni ya madini yalilipa jumla ya shilingi bilioni 468 kama
kodi ya mapato. Katika kipindi hicho hicho, wafanyakazi wao walilipa jumla ya
shilingi bilioni 506 kama PAYE na tozo ya kuendeleza ujuzi (Skills Development Levy) inayolipwa
VETA. Takwimu hizo zinaonesha kwamba, katika miaka sita ya kwanza (1999-2004)
makampuni ya madini yalilipa shilingi 0 kama kodi ya mapato, wakati waajiriwa
wao wa kitanzania walilipa shilingi bilioni 52 kama PAYE na SDL (Skills
Development Levy).Aidha,katika miaka 8 iliyofuata ,makampuni ya madini
yalilipa kodi ya mapato ya shilingi bilioni 468 wakati waajiriwa wao walilipa
shilingi bilioni 454. Kwa kipindi chote hicho kwa mujibu wa takwimu hizo za Mh. Prof Muhongo,thamani ya madini
yaliyouzwa nje ya Tanzania na makampuni hayo ilikua ni shilingi Trilioni
19.278. Kwa takwimu hizi, sio tu kwamba Serikali hii ya CCM imeruhusu utajiri
wa nchi hii kutajirisha makampuni ya kigeni bali pia imewanyonya waajiriwa wa
kitanzania wa makampuni hayo kwa kuwatoza kodi kubwa ya mapato kuliko
inayolipwa na waajiri wao wa kigeni.
4.1 Serikali na kima cha chini cha mishahara sekta binafsi Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa
fedha 2012/2013 katika kifungu 2001 wizara ilitenga jumla ya shilingi 60,000,000 kwa ajili ya kuratibu na
kuwezesha utafiti wa kima cha chini cha mshahara katika sekta binafsi , na pia
zilitengwa shilingi 55,000,000 kwa
ajili ya vikao vya bodi 12 za kisekta za kima cha chini cha mshahara katika
seka binafsi na mwaka huu wa fedha 2013/2014
katika fungu hilo hilo zimetengwa kiasi cha shilingi 60,600,000 kwa ajili ya ‘kuratibu na
kuwezesha utafiti wa kima cha chini cha mshahara katika sekta binafsi’, vile
vile zimetengwa tena shilingi 22,325,000
kwa ajili ya ‘kuwezesha vikao vya Bodi 12 za kisekta za kima cha chini cha
mshahara katika sekta binafsi’. Yaani kwa miaka 2 tumetumia jumla ya shilingi 197,925,000 kwa ajili ya kufanya
kinachoitwa utafiti na vikao kwa ajili ya kujua kama sekta binafsi inahitaji
kuongezewa mishahara ama laa na kama ipo haja iwe ni kiasi gani .
Kambi rasmi ya upinzani , inasikitishwa sana
na mtindo wa serikali hii sikivu ya CCM ambayo inasema kuwa inasikia lakini
inaendelea kutenga fedha za kufanya utafiti kuhusiana na kima cha chini cha
mishahara ya wafanya kazi, hivi ni kweli kuwa serikali hii haijui wafanyakazi
wanastahili kulipwa nini , hivi ni kweli kuwa hamkuwasikia TUCTA tangu mwaka
2010 walipopendekeza kuwa kima cha chini cha mshahara kiwe kiasi gani? Hivi
hamjui kuwa gharama za maisha zimepanda sana na hivyo huhitaji kufanya utafiti
kujua kama wafanyakazi wa sekta binafsi wanahitaji kuongezewa mishahara?
Aidha kwa maombi mapya
ya kutengwa kwa kiasi hiki cha fedha kinatoa taswira kuwa, hata kauli aliyoitoa
Mhe. Raisi kwenye maadhimisho ya Mei Mosi mwaka huu kwa kusema nanukuu " Katika kikao chetu tulichokutana na viongozi wa
TUCTA tarehe 27 Februari, 2013 tulijadili suala hili na kukubaliana kwamba
Serikali iendelee kulichambua zaidi ili kutoa unafuu zaidi kwa wafanyakazi kila
mwanya unapopatikana. Nafurahi kuwaarifu kuwa kazi ya uchambuzi
imekamilika na maombi yenu yamesikilizwa." Hii ni fedheha kwa
Serikali makini na sikivu ya CCM, ambayo
utendaji wake na kauli za viongozi wake wakuu ni wazi zinalenga kuwalaghai
wafanyakazi na kuwanyonya kupitia matumizi mabaya ya kodi zao!
5.0 TATIZO LA UKOSEFU
WA AJIRA NCHINI
Mheshimiwa Spika, Tatizo la ukosefu wa
ajira limeendelea kukua kila kukicha huku likiambatana na ugumu wa maisha.
Upatikanaji wa ajira katika soko la ajira nchini ni wa kusikitisha na jambo la
kushangaza ni kuwa Serikali haitaki kukubali kuwa tatizo hili ni kubwa sana na
lina athari kubwa si kwenye jamii ya kitanzania bali hata kwenye uchumi wa
taifa hili.
Leo hii tukiwa tumefungua milango ya ushirikiano baina
ya nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki, kama taifa hatujaweka mikakati
ya jumla ya kukabiliana na changamoto za soko la ajira katika Jumuia. Kambi
rasmi ya Upinzani Bungeni, inajiuliza kuwa wakati leo mfumo wa elimu wa
Tanzania ukiwa katika hali tete yenye kuzalisha kizazi kisichoweza kushindana
na nchi za Kenya, Rwanda, Uganda ambapo wazazi wengi wenye uwezo wanapeleka
watoto wao huko, je nchi ipo tayari kukabiliana na vigezo takwa vya soko la
ajira la ujumla? Ndio maana leo hii si ajabu kukuta katika soko la ajira, hasa
katika utalii kwenye mikoa ya kaskazini kama Kilimanjaro na Arusha, wakenya
wameweza kuliteka soko la ajira ya utalii kama waongoza watalii, wafanyakazi wa
mahoteli makubwa ya kitalii huku watanzania wakishindwa kutumia fursa hizo
kutokana na changamoto za kitaaluma ambazo zimesababishwa na mfumo duni wa
elimu nchini.
Mheshimiwa Spika, Ili nchi iweze kufanya
mabadiliko makubwa katika sekta ya ajira, lazima Serikali ikubali kuwa mfumo wa
elimu uliopo sasa haukidhi matakwa ya soko la ajira duniani. Mfumo wa elimu
uliopo hauzalishi wataalamu wa kutosha wa fani mbalimbali wanaoweza kufanya
kazi kwa weledi katika sekta mbalimbali ndio maana hata kwenye sekta ya madini
nchini, leo hii asilimia kubwa ya kazi zenye kuhitaji ujuzi na sifa za juu,
zimeendelea kufanywa na wageni na bila kufuata sheria za nchi.
Mheshimiwa Spika, Ili tufanikiwe katika soko la ajira
hatuna budi kufumua mfumo mzima wa elimu yetu. Hakuna mabadiliko magumu
duniani, kama madadiliko ya mfumo wa elimu kwa kuwa unahusisha gharama kubwa,
wakati na hata kuleta mtikisiko kwa kuwa utaathiri hata ajira za wale waliopo;
lakini pia wataalamu wanakiri kuwa mabadiliko ya mfumo wa elimu ndio njia pekee
ya kuweza kukabiliana na changamoto kubwa za kiuchumi, kijamii, kisiasa na hata
kiutamaduni. Lazima kama taifa , tukubali kufanya maamuzi magumu ili kuokoa
nchi yetu ambayo sasa imekosa mikakati endelevu ya kukabiliana na tatizo la
ajira. Kambi rasmi ya Upinzani inajua kuwa jibu la Serikali katika kupambana na
tatizo la ukosefu wa ajira litakua "mtikisiko wa uchumi duniani umeathiri
nchi nyingi hata zilizoendelea nazo lina tatizo la ukosefu wa ajira".
Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukishuhudia
serikali ikiwatimua wafanya biashara wadogo walioamua kujiajiri wenyewe na
hivyo kuwakosesha amani na kuwakatisha tamaa.Cha kusikitisha zaidi ni kwamba; Serikali
imekuwa ya kwanza kuzikimbia bidhaa zinazozalishwa na watanzania hawa
wanaojitahidi kutatua tatizo (la ukosefu wa ajira kwa kujiajiri wenyewe), na
kukimbilia bidhaa za nje licha ya kuwa bidhaa zinazozalishwa na watanzania zipo
za kutosha na zenye hadhi na ubora wa kutosha.Hivi serikali haioni
tunawakatisha tamaa hawa watanzania ambao wameamua kujiajiri?
6.0 UKOSEFU WA AJIRA
KWA VIJANA NCHINI
Mheshimiwa Spika, Tanzania, tumebarikiwa
kwa kuwa na rasilimali nyingi, lakini asilimia kubwa ya watanzania imeendelea
kuishi katika umasikini mkubwa , huku soko la ajira kila mwaka likikua katika
upande wa sekta ya kilimo na sekta isiyo rasmi ambapo kuna kiwango kidogo cha
ujira na uzalishaji.
Mheshimiwa Spika,tatizo la ajira nchini
limeendelea kukua, huku viongozi wa Serikali wakiendelea kupoza wananchi kuwa
tatizo la ajira si kubwa na kuwa Serikali imefanya jitihada katia kuongeza
ajira nchini. Leo hii, tunashuhudia ongezeko la ajira , lakini ajira zisizo na
tija kwa taifa, ajira zisizo za staha kwa watanzania na ajira zisizo na ujira
wa kuridhisha kwa watanzania, Je tuendelee kujisifia kuwa tunajenga jamii yenye
usawa na kuheshimu utu na thamani ya mtanzania?
Mheshimiwa Spika, Serikali ya CCM
iliahidi mambo mengi kwa mbwembwe ili kupata kura mwaka 2010, wakati ahadi zake
kwa wananchi walizotoa kwa mwaka 2005 zikiwa zimetekelezwa kwa kiwango kidogo.
Mojawapo ya ahadi hizo ni pamoja na ajira milioni moja za Raisi Kikwete
alizowaahidi wapiga kura. Serikali inayoongozwa na CCM haina budi kutambua kuwa
ari na mwamko wa watanzania leo hii si kama wa wakati ule wa "Ndiyo
mzee", kwa kuwa watanzania sasa wamenguka na wanaelewa wajibu wao katika
kuisimamia Serikali.
Mheshimiwa Spika, tatizo la ajira
nchini ni kubwa sana na Serikali isipokubali wazi kuwa hali ni mbaya na kuamua
kuweka mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na tatizo hili, ni wazi kuwa,
tunajichimbia kaburi , kwa kuwa uchumi wetu utaendelea kuporomoka huku asilimia
kubwa ya watanzania wakiishi katika maisha magumu yanayoambatana na maumivu ya
kupanda kwa gharama za maisha. Leo hii, tunasema zamani mtu akiokota chupa na
makopo ya plastiki barabarani ama kwenye majalala, ni mwendawazimu, ila
tulipofikia hata wazazi wetu, wazee ambao hawana pensheni na wanaishi kwa
mazingira magumu, wameingia mitaani na kuanza kuokota makopo kama sehemu ya
ajira kwao. Wazee wetu wanaokota makopo, vijana wanaokota makopo, watoto
wanaokota makopo, kwa kuwa taifa sasa limekosa mwelekeo wa kuweza kuandaa
mazingira kwa wazee, vijana na watoto katika kujikwamua kimaisha kwa mipango
endelevu ya kazi na ajira nchini.
Mheshimiwa Spika, kati ya mambo ambayo
yamesababisha ukosefu wa ajira nchini ni pamoja na kutolingana kwa uhitaji
na upatikanaji wa wa ajira katika soko
lo ajira, uanzilishwaji wa ajira katika shughuli za uchumi unaotokana na
sera zisizotekelezeka za uwekezaji,
kutokuwepo kwa programu mbalimbali za ajira zinazoweza kuchangia upatikanaji wa
ajira katika sekta mbalimbali kuanzia ngazi ya taifa mpaka serikali za mitaa.
Mheshimiwa Spika, Moja ya changamoto
kubwa ambayo vijana wengi wa kitanzania tunakutana nazo ni pamoja na kukosa
elimu, maarifa, mafunzo na ujuzi unaotakikana katika soko la ajira hapa nchini
na katika jumuia ya Afrika mashariki. Wakati huohuo, kazi nyingi zinatoa na
ajira zisizoleta tija zenye masharti magumu. Kiuhasilia, kuna matatizo mengi ya
kimuundo na vikwazo vinavyofanya ajira kwa vijana na uwezekano wa vijana
kuajiriwa kuwa mgumu. Waajiri wengi, kwa mfano wanatoa matangazo ya nafasi za
kazi na ajira kwa kuweka vigezo kama ujuzi wa kazi wa kuanzia miaka mitano na
kuendelea, wakati vijana wengi, kama inavyjulikana, hawana uzoefu wala ujuzi
katika ajira hizo zinazotangazwa ingawa wana uwezo wa kuzifanya na
kuzitekeleza. Ingawa , waajiri wote katika sekta binafsi na umma, wanaweka
masharti au vigezo vya ujuzi na uzoefu kuwa moja ya masharti magumu ya ajira
kwa vijana, wanasahau kuwa Tanzania
tumekosa mpango maalumu wa mafunzo yanayoendana sambamba na elimu ya kijana,
ili kumfanya kijana apate ujuzi katika taaluma yake na katika sekta
inayohusika. Hali hii inasababisha ugumu kwa waajiri, katika kutoa nafasi za
kwa kazi kwa vijana, kwa kuwa kuajiri mtu asiye na ujuzi au uzoefu inachukuliwa
kama ni gharama, kwa kuwa mwajiri lazima aingie gharama za kutoa mafunzo ya
awali tena kwa vijana atakaoajiri. Hii inasababisha waajiri wengi kukwepa
kuwaajiri vijana kwa kigezo cha kupunguza gharama za mafunzo.
Mheshimiwa Spika,
tatizo la ajira kwa
vijana pia linachangiwa zaidi kwa
kutokuwa na uoanishaji mzuri na
ushirikiano kati ya taasisi za elimu na mafunzo kwa upande mmoja na
viwanda au
soko la ajira kwa upande mwengine. Na hii ni kwa kuwa, mitaala ya sasa
ya elimu
na mafunzo haindeshwi kwa kushirikisha wadau wengine, hasa katika
masuala ya
kazi na ajira. Mabadiliko makubwa ya kisera yanatakiwa kufanyika katika
sekta
mbalimbali ambazo zina msukumo katika kuongeza thamani ya ya mtafuta
kazi
kwenye soko la ajira . Kati ya maeneo ya muhimu ambayo yanatakiwa
kufanyiwa
mabadiliko ni pamoja na kuazimia kufanya mabadiliko katika mfumo wa
elimu
uliopo sasa kwa kufanya maboresho kwanza;
kwa kuhakikisha kuwa elimu ya msingi na sekondari inatolewa bure kwa
watanzania wote. Pili mfumo na mtaala wa
elimu uliopo sasa urekebishwe ili uweze kukidhi mahitaji ya soko la
ajira
ambalo huwa linabadilika. Lazima Serikali kwa kupitia wizara ya elimu na
mafunzo ikubali kufanya mapinduzi ya sera ya elimu itakayomfanya kijana
wa
kitanzania aweze kuajiriwa popote pale hasa katika jumuia ya Afrika
Mashariki.
Lakini pia ni kwa Serikali kuhakikisha mipango na mikakati ya ukuzaji
wa sekta mbalimbali inaambatana na uanzishwaji wa kazi na ajira kwa
vijana wa
kitanzania. Kila sekta iendane na mipango endelevu ya kukuza ajira kwa
vijana.
Kwa mfano ukuzaji wa sekta ya miundombinu, uendane na kutoa nafasi za
ajira kwa
vijana wa kitanzania pamoja na kuwalipa mishahara na posho zenye staha,
zitakazowezesha vijana kujikwamua na hali ngumu ya kiuchumi na maisha.
Mheshimiwa Spika, ushindani wa kidunia,
unafanya uchumi wa nchi mbalimbali kuendana na mabadiliko mbalimbali, hasa
mabadiliko ya teknolojia. Hapa nchini, tumeshuhudia mabadiliko makubwa na
mapinduzi ya teknolojia kuanzia kwenye uzalishaji, kilimo, habari na
mawasiliano. Mabadiliko makubwa yanayoendelea katika vigezo na masharti ya
kazi, ni kiashiria kikubwa kuwa vijana lazima wasaidiwe katika kukabiliana na
changamoto za ukuaji wa kasi wa
teknolojia. Hata vijana ambao wanapata fursa ya ujasiriamali lazima wapate
mafunzo ya kukabiliana na ukuaji wa teknolojia.
Mheshimiwa Spika, kutokana na ahadi
mbalimbali ambazo zilitolewa kipindi cha uchaguzi wa mwaka 2010 za kuongeza ajira kwa vijana na
kukabiliana na tatizo la ukosefu kwa ajira za vijana, ikiwemo kutatua
changamoto za vijana waliopo katika sekta isiyo rasmi ;wamachinga, wachuuzi wa
bidhaa ndogondogo,wakulima wadogowadogo,wasanii,wavuvi,wajasiriamali,mamalishe,
wafanyabiashara ndogondogo, wachimba madini, waliopo kwenye sekta ya utalii;
matumaini ya vijana wengi yalikua ni utekelezaji wa ahadi za Serikali kwa
wakati. Pamoja na taifa kuwa na takribani ya vijana milioni 16, ambapo katika
kupitisha bajeti ya vijana, fedha zilizotengwa kwa ajili ya vijana zilikua ni
kiasi kidogo cha bilioni 3.
Mheshimiwa Spika, Katika kuweka fursa
sawa kwa wote na kuleta usawa katika mgawanyo wa rasilimali za nchi hii, kwa
tengo hilo la fedha za kiasi cha bilioni 3 kwa vijana milioni 16 wa kitanzania,
basi kila kijana ana uwezekano wa kupata kiasi cha shilingi za kitanzania 187.5
kama mtaji.
Mheshimiwa Spika, Huu si upotoshaji kama mnavyouita bali ni
ukweli halisi ambao watanzania leo wanakumbana nao kwa kuwa na Serikali ambayo
haina vipaumbele katika kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana. Kumekua na
ongezeko la vijana wanaojihusisha na biashara za madawa ya kulevya, ujambazi,
ukahaba, hali inayochangiwa na fursa chache za kufikiwa kwa malengo na miradi
mbalimbali ya programu za vijana.
Mheshimiwa Spika, jitihada za
kutengeneza mazingira kwa vijana na watanzania kwa ujumla hasa wanaofanya
biashara katika maeneo yasiyo rasmi maarufu kama wamachinga, unaleta changamoto
katika uchumi wa taifa letu na katika utatuzi wa migogoro inayotokana na
ukosefu wa ajira nchini. Serikali inatakiwa kuweka mpango mkakati wa kuoanisha
idadi ya vijana ambao wamekuwa wakifanya biashara zao katika maeneo
yasiyokubalika,na kuwatengea maeneo
ambayo yatawakutanisha na wateja wao ili waendeshe biashara zao bila bughuza
kwa wengine. Hii iambatane na mifumo dhabiti ya kuhakikisha kuwa vijana
wanapata fursa ya mikopo katika taasisi za fedha nchini yenye masharti nafuu.
Mheshimiwa Spika, kuna haja ya Serikali
kuanzisha mpango wa kuwadhamini vijana waliotimiza masharti ya kibiashara
inayoambatana na michanganuo kwa kushirikiana na Benki ambazo zina matawi mpaka
sehemu za vijijini, ili mipango ya kifedha ya kuwanufaisha vijana iwafikie kwa
ukaribu na kwa wakati ili kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana hapa
nchini.
Mheshimiwa Spika, tatizo la ajira
nchini bado ni kubwa sana na linazidi kuwa siku hadi siku huku kukiwa hakuna
ufumbuzi wa kuaminika unaotolewa na viongozi wa nchi.Vijana wamekuwa
wakiendelea kuhitimu katika vyuo mbali mbali nchini huku wakiwa wanakosa kazi
maalum za kufanya na hivyo kujikuta wakiishi maisha ya dhiki na yasiyotamanika
huku wakiwa wamekata tamaa. Katika jitihada za kutatua tatizo la ukosefu wa
ajira nchini,wataalam mbalimbali wamekuwa wakishauri kwamba suluhisho la kuwanusuru
vijana ni kuwahamasisha na kuwajengea mazingira ya kujiajiri wenyewe kwenye
sekta binafsi kama ufundi,kilimo, ujasiriamali na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni dhahiri
kuwa vijana wengi wameendelea kuhitimu elimu ya juu nchini kila mwaka katika fani
mbalimbali. Pamoja na ugumu wa soko la ajira nchini,lazima Serikali iweke
mikakati ya kuhakikisha kuwa kundi hili linapewa elimu na mafunzo ya
kuwawezesha kutumia taaluma zao ili waweze kusaidia kada mbalimbali nchini.Moja
ya mikakati ambayo Serikali inaweza kuitumia ni pamoja na kuingia ubia na
makampuni yaliyo katika sekta mbalimbali nchini ambazo zitakua zinatoa nafasi
za mafunzo ya kazi 'internship' kwa muda utakaopangwa kama moja ya wajibu wa
mashirika kwa umma 'Corporate Social
Responsibility'. Hii si tu itawajengea vijana uwezo wa kujifunza bila pia
italisaidia taifa kutunza thamani ya mtaji rasilimali watu(Human Capital Value) na kuwa taifa lenye ujuzi na maendeleo ya
nguvu kazi (human resoures development ).Lazima
serikali sasa itambue kuwa kundi vijana ndilo chachu ya mabadiliko ya kila kitu
hivyo wakishirikishwa ipasavyo katika sekta mbalimbali wanao uwezo wa kuliletea
maendeleo ya kweli taifa hili.Kama serikali haitakuwa makini katika kuutafutia
ufumbuzi mgogoro huu wa ajira, ni wazi kuwa
vijana wataendelea kudai mabadiliko hata kwa kutumia nguvu pale
inapobidi kutokana na ugumu wa maisha na ufinyu wa fursa za kuwakwamua
kimaisha.
6.1 UKOSEFU WA AJIRA
KWA MAKUNDI MAALUMU NA CHANGAMOTO ZAKE ZA KISERA.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya
upinzani inaendelea kuitaka Serikali kuboresha sera za kazi na ajira, sera za
usalama wa mahali pa kazi pamoja na sheria mbalimbali ambazo zitatoa nafasi na
fursa kwa makundi maalumu yalipo katika jamii yetu. Ukiangalia mifumo
mbalimbali ambayo ipo nchini, kuanzia mifumo ya elimu, mifumo ya kifedha na
mifumo ya uendelezaji wa mtaji watu, makundi maalumu hasa walemavu wamekua
wakikumbana na changamoto nyingi ambazo zimewakatisha tamaa. Soko la ajira na
kazi leo, halijawekea mfumo utakaohakikisha kuwa unatoa fursa kwa walemavu ili
nao wapate nafasi zaajira na majukumu ya kazi yatakayoweza kuwaendeleza na
kujikwamua kiuchumi.
Mheshimiwa Spika,katika mawasilisho ya
bajeti kwa wizara hii kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013 , waziri alieleza kuwa
kwa jumla ya watu wenye ulemavu 308[1]
walipatiwa mafunzo ya ujuzi wa fani
mbalimbali kwa kupitia mafunzo ya ujuzi kwa kushirikiana na wadau kama
CCBRT(Comprehensive Community Based Rehabilitation in Tanzania), CEFA na Radar
Development ambapo kati ya wahitimu hao 145 wameajiriwa na 163 wamejiajiri.
Mheshimiwa Spika, idadi hii haileti
taswira halisi ya makundi maalumu katika jamii ambayo yana watanzania wenye
elimu, ujuzi na utaalamu katika fani mbalimbali lakini wamekosa fursa za ajira
kutokana na hali zao. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka wizara kutoa
takwimu ya jumla ya watanzania walio kwenye makundi maalumu walioajiriwa katika
sekta mbalimbali na waliojiajiri pamoja na kutoa tathmini ya ufuatiliaji wa
utekelezwaji wa Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008 katika kuhakikisha kuna
usawa wa fursa za ajira na kipato kwa makundi yote. Kambi rasmi ya upinzani
inataka kujua ni kiasi gani cha fedha za maendeleo amacho wizara imetenga kwa
mwaka huu katika kuwawezesha walemavu nchini katika kukabiliana na changamoto
za maisha aidha kwa kuwaanda kujiajiri ama kwa kuwaongezea ujuzi na maarifa ili
waweze kuajiriwa.
6.2 TATIZO LA AJIRA
MBAYA KWA WATOTO NA ATHARI ZAKE
Mheshimiwa Spika, kwa miaka mingi haki
za watoto zinakiukwa hasa katika suala la kuwaajiri kinyume cha umri wao,
ambapo kimsingi ni kosa na ni kinyume na sheria na taratibu za nchi.Hali hii
inachangiwa na ugumu wa maisha hasa kwa watoto wanaoishi vijijini na wale ambao
wamekumbana na athari mbalimbali ikiwemo wale ambao wazazi wao wamefariki
kutokana na ugonjwa wa UKIMWI. Zaidi pia inatokana na hali mbaya ya umasikini
uliokithiri katika familia nyingi za kitanzania, hali inayomnyima mtoto kufanya
maamuzi sahihi kutokana na umri wake na hivyo kukimbilia kwenye ajira hatarishi
kwa misingi ya kujikomboa kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, lakini ni wazi kuwa
watoto walio katika ajira mbaya wananyimwa elimu na fursa ya kukua na kujenga
vipaji na uwezo utakaoweza kuwakwamua wao, familia na jamii zao kutoka kwenye
mzunguko wa umaskini. Tumeshuhudia ajira mbaya za watoto ambao wengi wanafanya
ajira hatarishi na zenye kuleta madhara si tu ya kiafya bali kisaikolojia
ikiwemo ajira za kwenye mashamba makubwa ya kahawa, chai, tumbaku; ajira za
viwandani; ajira za kazi za nyumbani; ajira hatarishi kwenye migodi ya madini
na machimbo na kadhalika. Hii si tu ni hatari kwa taifa ambalo tunasema watoto
ni taifa la kesho, bali kwa mustakabali wataifa ambalo lina amini katika
misingi ya haki na usawa pamoja na kuwalinda watoto dhidi ya mazingira
hatarishi.
Mheshimiwa Spika,katika kukabiliana na
tatizo la ajira mbaya kwa watoto,mwezi Machi mwaka huu , Marekani ilitoa ruzuku
ya Sh. bilioni 16 kwa Kamati ya Uokoaji wa Kimataifa nchini (IRC) kwa ajili ya
kukabiliana na ajira mbaya kwa watoto katika mikoa ya Kigoma na Tanga ambapo
fedha hizo zitatumikakupitia kwenye mradi mpya ujulikanao kama ”Wekeza” na kuwa
IRC itashirikiana na wabia wake kukabiliana na ajira kandamizi na za kinyonyaji
dhidi ya watoto.
Mheshimiwa Spika, Balozi Lenhardt
alikaririwa akisema kuwa “Mradi utalenga wilaya sita katika mikoa ya
Kigoma na Tanga ambako kuna tatizo
kubwa la utumikishwaji wa watoto
katika ajira mbaya kwenye shughuli za kilimo na kazi za majumbani
na utawahudumia waathirika pamoja na kujenga uwezo wa serikali
kulishughulikia
tatizo hilo,”
Mheshimiwa Spika, pamoja na msaada wa
Marekani katika kukabiliana na ajira mbaya kwa watoto, Serikali kwa kupitia
wizara itupatie majibu ni mkakati gani uliowekwa katika kukabiliana na ajira
mbaya kwa watoto katika sehemu mbalimbali za taifa hili tofauti na wilaya hizo
6 zilizofadhiliwa na Marekani.
7.0 PENSHENI KWA WAZEE WOTE NCHINI
Mheshimiwa Spika; katika maoni yake kuhusu bajeti ya Serikali
na Ofisi ya Waziri na Wizara ya Kazi na Ajira ya mwaka 2011 na 2012 kwa nyakati
mbalimbali Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA imeitaka Serikali
kuharakisha kuanza kutoa pensheni kwa wazee wote nchini.
Mheshimiwa Spika; majibu ya Serikali
hii inayoongozwa na CCM yamekuwa ni ahadi kwa wazee kwamba pensheni hiyo
itaanza kulipwa kwa kuwa serikali iko katika hatua ya mwisho ya kufanya utafiti
na kuandaa mfumo wa kisheria.
Mheshimiwa Spika; tarehe 6 Agosti 2012
wakati akijibu maswali bungeni hatimaye Waziri wa Kazi na Ajira Gaudencia
Kabaka akatoa ahadi mahususi kwamba mwanzoni mwa mwaka 2013 ingetungwa sheria
ya wazee ambayo pamoja na mambo mengine ingeweka mfumo madhubuti wa wazee wote
kuanza kulipwa pensheni kuanzia mwaka huu wa 2013. Waziri alilihakikishia Bunge
kwamba Serikali iko katika hatua za mwisho za kuandaa mpango madhubuti wa
ulipaji wa pensheni kwa wazee nchini kuanzia mwaka 2013.
Mheshimiwa Spika; badala ya kutimiza
ahadi hiyo huku mwanzoni mwa mwaka 2013 ukiwa umepita bila sheria husika
kutungwa wala pensheni kuanza kulipwa, Rais Jakaya Kikwete akihutubia kilele
cha wiki ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Mkoani Dodoma tarehe 17 Mei 2013
aliagiza Wizara ya Kazi na Ajira kuanza ‘kufikiria’ kuwalipa pensheni wazee
wote na kujiridhisha kabla ya kuanza kutoa mafao hayo.
Mheshimiwa Spika; kufuatia agizo hilo
la Rais, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inaitaka
Wizara ya Kazi na Ajira itoe taarifa ya kina kwa Bunge kueleza Mpango Madhubuti
ambao ilijibu bungeni kwamba uko katika hatua za mwisho umeishia wapi na
kuwasilisha bungeni rasimu ya mpango huo iliyokuwa tayari mpaka wakati Waziri
alipojibu bungeni mwaka 2012. Aidha, Wizara ya Kazi na Ajira ieleze juu ya
matumizi ya fedha za umma zilizotumika kufanya tathmini na utafiti ambao Wizara
ilieleza katika majibu yake ya wakati uliopita iwapo ni sasa ndipo wizara hiyo
imeagizwa ianze ‘kufikiria’.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya
Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inaona kauli hizo za Serikali inayoongozwa na
CCM ni za kutowajali wazee na za kuwepwa kuwajibika kutimiza ahadi kwamba kuwa
tathmini na tafiti zimefanywa mpaka na asasi za kiraia na Serikali kupewa
nakala. Aidha, kufuatia tafiti hizo Wizara iliahidi bungeni kwamba wameanza
kuandaa mfumo wa kuorodhesha wazee ikiwa ni sehemu ya kuanza kuandaa mchakato
wa malipo ya pensheni hizo.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya
Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali inayoongozwa na CCM kuanza
kutoa kauli ya kuanza kulipa pensheni hiyo kwa Wazee mwaka huu 2013 na kuingiza
katika bajeti ya mwaka wa fedha 2013/2014 kwa kuzingatia maoni na mapendekezo
tuliyotatoa mwaka 2011 na 2012.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani
inayoongozwa na CHADEMA inaitahadharisha Serikali inayoongozwa na CCM kwamba
ahadi hii isipotekelezwa, tutawakumbusha wazee wote juu ya ahadi alizotoa
Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika kilele cha siku ya Wazee duniani tarehe 1
Oktoba 2010 alipotumia vibaya nafasi ya
kiserikali kutafuta kura za wazee kwa niaba ya CCM ili wazee wafanye maamuzi
sahihi ya kukikataa chama hicho. Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na
CHADEMA inawakumbusha wazee wote nchini kwamba miaka takribani kumi imepita
toka sera ya wazee itungwe mwaka 2003 hata hivyo utekelezaji wake chini ya
Serikali inayoongozwa na CCM umekuwa ni wa kusuasua.
8.0 SHERIA ZA KAZI NA
HAKI ZA WAFANYAKAZI
Mheshimiwa Spika, tumeendelea
kushuhudia kuwepo na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika maeneo mengi
ya kazi. Tatizo hili limechangiwa kwa kiasi kikubwa na wafanyakazi kutosimamia
au kutojua haki zao za msingi kama wafanyakazi na hivyo kusababisha waajiri
kutumia fursa hiyo ya wafanyakazi kutozijua sheria, kuvunja sheria na haki
nyinginezo za kibinadamu.
Mheshimiwa Spika, Ni muhimu kwa mfanyakazi wa sekta
yoyote ile kujua haki zake za msingi kama mfanyakazi na mwajiri kuziheshimu
haki za kila mfanyakazi kama zilivyoainishwa katika sheria ya kazi namba 6 ya
mwaka 2004 na Sheria za Taasisi za kazi Na.7 ya mwaka 2004. Sote tunatambua
kuwa mfanyakazi ni mtu ambaye ameingia mkataba na mtu, taasisi au
serikali.Kimantiki, mkataba, kulingana na Sheria ya Ajira Na. 6 ya mwaka 2004
kifungu cha 14 ambayo imetoa aina tatu za mikataba ambayo ni mkataba usio na muda
maalum kwa ajili ya watalaam.Mkataba wenye muda maalum kwa ajili ya wafanyakazi
wasio kwenye taaluma ya utawala na mikataba kwa ajili ya shughuli maalum kwa
muda muafaka na kifungu cha 15 cha Sheria ya Ajira imefafanua kwamba, mikataba
yote lazima iwekwe katika maandishi.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo kuna pengo
kubwa la sheria katika kulinda haki za wafanyakazi pindi kunapotokea uhamisho
wa shughuli yaani(Transfer of Undertakings) kwa upande wa muajiri hususani
kwenye sekta binafsi ambapo kumekuwa na migogoro mingi baina ya pande mbili
hizi inayotokana na mapungufu sheria
hii.
Mheshimiwa Spika, aidha wakati
nikiwasilisha hotuba ya kambi ya upinzani ya wizara hii kwa mwaka 2012/2013
kambi rasmi ya upinzani iliishauri serikali kuleta muswada wa sheria bungeni
utakaosimamia maslahi ya wafanyakazi katika suala hili, jambo ambalo
linaonekana ni kitendawili mpaka sasa kwa serikali inayojiita siikivu masikioni
pa watanzania.
9.0 HAKI NA WAJIBU WA MFANYAKAZI
Mheshimiwa Spika, mwajiriwa ana haki ya kupata likizo ya siku
28- ambapo kifungu cha 31 kinamtaka mwajiri kutoa likizo ya siku 28 mfululizo
kwa kila mwaka wa ajira.Siku 28 hizo zinajumuisha sikukuu iwapo zitaangukia
ndani ya siku hizo, na siku za mwisho wa juma. Mwajiri anaweza kupunguza siku za likizo iwapo
mwajiriwa aliomba mwenyewe likizo fupi za muda na ambazo alipokea malipo.
Mheshimiwa Spika, Ikumbukwe kuwa katika
Sheria Ajira, likizo ni suala la lazima kwa kila mfanyakazi na tabia ya
kuzuiana likizo kati ya mwajiri na mwajiriwa hairuhusiwi kwani sheria
inamlazimisha mwajiri kumlipa mwajiriwa au mfanyakazi fedha ya likizo, ambayo
ni nauli ya mfanyakazi, mke wake na watoto wasiozidi wanne na wategemezi
wawili, Katika sheria hiyo ya kazi kuna
likizo ya uzazi, kifungu 33, ambapo mfanyakazi atakayekuwa mjamzito anapaswa
kutoa taarifa ya maandishi ya miezi mitatu kabla ya kuanza likizo yake ya uzazi
na taarifa hiyo ni lazima iambatanishwe na cheti cha daktari. Mjamzito anaweza
kuanza likizo yake wakati wowote, ilimradi tu yawe yamebaki majuma manne kabla
ya kujifungua .
10.0 MALIPO BAADA YA KUACHISHWA KAZI
Mheshimiwa Spika, mara baada ya
kuachishwa kazi, mfanyakazi anatakiwa kulipwa mafao yake yote yanayotokana na
ajira yake kwa kipindi chote cha ajira. Malipo hayo ni pamoja na mapunjo ya
mshahara, kiinua mgongo na nauli ya kumsafirisha hadi kituo cha karibu na
nyumbani kwake. Hata hivyo kumekuwepo na usumbufu mkubwa kwa wafanyakazi wa
sekta binafsi na serikali mara baada ya
kustaafu katika kufuatilia na
hata kulipwa stahili hizo jambo ambalo ni ukiukwaji wa sheria ambazo zipo kwa
ajili ya kulinda na kuhifadhi haki za wafanyakazi hao
11.0 VYAMA VYA
WAFANYAKAZI NCHINI
Mheshimiwa Spika, uhuru wa vyama vya wafanyakazi nchini unatambuliwa na Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kwa uangalizi wa sheria za kazi na Mahusiano ya kazi ya
mwaka 2004. Uhuru huu una umuhimu sana katika maeneo ya kazi na historia yake
ipo tangu Mapinduzi ya viwanda nchini Uingereza karne ya 19, katika bara la
Ulaya na Marekani. Uhuru wa vyama vya wafanyakazi ni msingi muhimu wa haki za
binadamu kwa kutoa haki za kila mmoja, kuunda na kujiunga na vyama vya
wafanyakazi katika eneo lake la kazi, haki ya kugoma na kuandamana na maridhiano /matakwa ya
kitaifa na kimataifa.
Mheshimiwa Spika, Hata hivyo hali hii ni tofauti kwani vyama hivi vimeendelea kupigia
kelele madai na maslahi mbalimbali kupitia vyama vyao lakini Serikali
imeendelea kuwa kimya na kukimbilia mahakamani kunyamazisha madai/malalamiko
yao, jambo ambalo si suluhisho la masuala hayo bali ni sawa na kujifunika shuka
katikati ya mvua kubwa ya mawe huku ukidhani utaikwepa mvua hiyo.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya upinzani tunaitaka na kuishauri serikali kushughulikia kwa
dhati masuala yote ya wafanyakazi ikiwa ni malimbikizo ya mishahara, kuboresha mazingira
mahali pa kazi na bima za afya kwa wafanyakazi.
12.0 TAKWIMU ZA
RASILIMALI WATU NCHINI
Mheshimiwa Spika, katika mkutano wa mwaka wa 47 wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB), uliofanyika juni 2012 jijini Arusha,[2]
Waziri wa kazi na ajira alisema tatizo la ajira kwa vijana limepungua kutoka
asilimia 12.9 mwaka 2000/2001 hadi asilimia 11.7 mwaka 2006. Waziri Kabaka
alisema kitendo cha wanasiasa kuendelea kusema tatizo la ajira kwa vijana ni
bomu linalosubiri kulipuka, siyo kweli kwani utafiti uliofanywa na wizara yake
kwa kushirikiana na Taasisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), unaonyesha kuwa tatizo
hilo limepungua kwa asilimia 1.2. Waziri aliendelea kueleza kuwa, utafiti
uliofanywa na NBS mwaka 2006, kwa kushirikiana na wizara hiyo umebainisha kuwa
nguvu kazi ya Tanzania ni milioni 20.6 kati ya watu milioni 37.5, kwa wakati
huo.
Mheshimiwa Spika, Ni wazi hali ya uchumi duniani kwa
sasa si nzuri hasa kwa nchi zinazoendelea, na changamoto kubwa ni hali ya
uchumi pamoja na kubadilika kwa vigezo na masharti katika soko la ajira. Majibu
ya serikali kuwa tatizo la ajira kwa vijana limepungua, kwa kuangalia takwimu
za mwaka 2006 halitoi taswira halisi ya tatizo hili, hivyo kutoa majibu kwa
makadirio ya takwimu kuwa tatizo la ajira limepungua si sahihi. Katika hotuba
ya wizara ya kazi na ajira kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013 waziri wa kazi na
ajira alikiri kuwa tatizo la takwimu za ajira ni changamoto kwa kuwa linaleta
picha hasi na aliahidi kuwa wizara yake
kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO) imempata mshauri mwelekezi
anaye andaa mfumo wa taarifa za soko la ajira utakaokamilika katika mwaka
2012/2013.[3] na
kwa kuwa wakati akijibu swali la Mheshimiwa Naomi Kaihula, tarehe 13 aprili
2011,mheshimiwa naibu waziri wa kazi na ajira alikiri kuwa ni vigumu kupata
taarifa za uwiano wa vijana wanaomaliza shule na vyuo na wanaopata ajira
kutokana na kukosekana mfumo wa utuatiliaji (Trace Study) kamilifu, ambao
ungetuwezesha kufahamu ni vijana wangapi kati ya waliomaliza shule au vyuo
wameweza kuajiriwa. Kutokana na upungufu huo, naibu waziri aliahidi kuwa wizara
inaandaa mfumo wa upatikanaji wa taarifa za soko la ajira,ambao ungeanza
kufanya kazi mwishoni mwa mwaka 2011 na kusaidia kupatikana kwa taarifa hizo.[4]
13.0 WAKALA WA USALAMA
NA AFYA MAHALI PA KAZI (OSHA)
Mheshimiwa Spika,OSHA ilianzishwa kwa kutumia Sheria
ya Executive Agencies Act, No 30 ya
mwaka 1997. Na wajibu wa OSHA ni kufanya kaguzi na kufuatilia uzingatiaji wa
masuala ya usalama na afya na kuhakikisha kuwa waajiri wanazingatia sheria na
kanuni za usalama mahali pa kazi hasa Sheria ya Afya na Usalama katika Maeneo
ya Kazi (OHS)Na. 5 ya mwaka 2003. Mpaka kufikia Mei 2012, jumla ya kesi 16[5]
zilikua mahakamani. Tunaitaka wizara itupe mrejesho wa kesi hizo dhidi ya
waajiri waliokiuka sheria na kanuni za
usalama mahali pa kazi.
Kambi rasmi ya upinzani inaitaka Serikali kupitia
wizara kuiwezesha OSHA kwa kuipatia rasilimali za kutosha ili iweze kufanya
kaguzi zake ikiwemo kutekeleza wajibu wake wa uainishaji na usajili, ukaguzi wa
usalama na afya,tathmini za maafa yawezayo kutokea mahali pa kazi na athari
zake.
Mheshimiwa Spika, kumekua na matukio mbalimbali ambayo
yanatokea nchini ambayo yanasababisha athari si tu kwa raia wengine bali kwa
wafanyakazi ambao wanakua ni wahanga wa matukio hayo. Katika kuporomoka kwa
jengo la ghorofa 16, jijini Dar Es Salaam ni kielelezo cha kutofanyika pia
kaguzi za usalama na afya mahali pa kazi. Lazima Serikali ya CCM ikiri kuwa
imeshindwa kuhakikisha kuwa mahali pa kazi ni salama kwa kila mtanzania. Ni
fedheha kuwa na wakala wa Serikali mwenye dhamana ya kuhakikisha usalama na
afya mahali pa kazi unazingatiwa lakini inashindwa kuwa na vitendea kazi pamoja
na rasilimali za kutosha kwa ajili ya kulinda usalama na afya za mahali pa kazi
kutokana na ufinyu wa bajeti na rasilimali kazi.
Idadi ya Mahali pa
kazi zilizosajiliwa kulinganisha na zisizosajiliwa nchini[6]
Year
|
Makadirio ya Mahali pa Kazi nchini
|
Sehemu za Kazi zilizosajiliwa
|
%ya sehemu za kazi zilizosajiliwa
|
2009
|
6,825
|
1,747
|
25
|
2010
|
11,691
|
2,069
|
22
|
2011
|
21,068
|
5,045
|
24
|
2012
|
27,500
|
6,599
|
24
|
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka wizara,
kulipatia Bunge majibu ya maswali yafuatayo kutokana na takwimu zilizopo hapo
juu. Je , ni sababu zipi ambazo zimeifanya OSHA ifanye kaguzi za usalama wa
afya na mahali pa kazi bila ya kufikia nusu ya sehemu hizo? Na kwa kutumia
takwimu ambazo waziri alizitoa katika Bunge hili wakati wa mawasilisho ya
bajeti kwa mwaka wa 2012/2013 kwa kutoa taswira kuwa OSHA imefanya asilimia
85.6% ya kazi zilizopangwa kufanyika mahala pa kazi, ni wazi kuwa waziri alikua
anaupotosha umma kuwa OSHA imefanikiwa kwenye kusimamia usalama na afya kwa
mahali pa kazi, huku ukweli ukiwa kuwa wizara imeshindwa kwa asilimia 76%
kusajili mahali pa kazi nchini, hali ambayo inaonesha kuwa si kipaumbele cha
Serikali hii ya CCM katika kujali usalama wa watu wake sehemu za kazi.Kambi
rasmi inataka kujua ni hatua gani za kisheria ambazo asilimia 75 ya mahali pa
kazi ambazo hazijasajiliwa zitachukuliwa kama ambavyo sheria inaelekeza kutoa
adhabu? Na je Serikali imeweka mkakati gani wa kuhakikisha kuwa kila mahali pa
kazi nchini panasajiliwa? Na kwa kuwa inakadiriwa kuwa kiasi cha shilingi
milioni 600 zinahitajika kwa OSHA ili
kuweza kusajili sehemu zote za kazi nchini, je wizara imetenga kiasi gani kwa
mwaka huu wa fedha wa 2013/2014?
Mheshimiwa Spika, aidha kambi rasmi ya
upinzani inataka kujua pia kama wizara imefanya usimamizi na tathmini ya kaguzi
zinazofanywa na OSHA na kama wamefanya tathmini ya shughuli za OSHA, ni vigezo
vipi vya ambavyo vimetumia katika kupima na kusimamia utendaji wa OSHA?
14.0 MAPITIO YA UTEKELEZAJI BAJETI 2012/2013
NA MAKADIRIO YA MWAKA 2013/2014
Mheshimiwa Spika, katika fungu 1001
utawala na rasilimali watu katika mwaka wa fedha 2012/2013 zilitengwa jumla ya
shilingi 2,780,306,000, aidha kwa
mujibu wa randama ya wizara ni kuwa jumla ya shilingi 705,400,000 zilikuwa ni kwa
ajili ya kulipia pango la ofisi ya wizara ,maji,umeme na simu na hii ni kwa
mujibu wa randama ya wizara shughuli namba D03S01.
Kambi rasmi ya upinzani, inaona kuwa fedha hizi
ni nyingi sana kutengwa kila mwaka kwa ajili ya kulipia pango la ofisi ya
wizara na ikizingatiwa kuwa ni wizara ambayo inasimamia haki za wafanyakazi
ambao kila leo wanalia kutokana na kiwango kidogo cha mishahara , tunataka
kujua wizara ina mpango gani wa kujenga ofisi zake ili iachane na mpango wa
kulipia mamilioni ya walipa kodi kila mwaka kama pango na ofisi hizo zijengwe
Dodoma kama ambavyo serikali mara zote imekuwa ikisisitiza kuwa ofisi zake
zitajengwa Dodoma kama sehemu ya maandalizi ya kuhamia Dodoma.
Mheshimiwa Spika, katika fungu hilo
hilo la 1001, namba ya mradi D03S08
randama ya wizara inaonyesha kuwa jumla ya shilingi 8,000,000 zilitengwa kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kwa ajili ya
gharama za safari za waziri na Naibu waziri kwenda Majimboni na hadi mwezi Mei
2013 jumla ya shilingi 5,600,000
zilikuwa zimetumika kwa ajili ya safari tatu za Majimboni kwa Mhe.Waziri na
Mhe.Naibu Waziri .
Aidha , kwa mwaka huu
wa fedha wizara imeomba kutengewa kiasi cha shilingi 16,710,000 (randama uk 21) kwa ajili ya kuwezesha safari nne za
majimboni kwa Mhe.Waziri na Naibu Waziri ,maana yake ni kuwa kila safari moja
inatumia wastani wa shilingi milioni nne (4,000,000)hata kwa Naibu waziri
ambaye Jimbo lake lipo Ukonga Dar Es Salaam .
Kambi rasmi ya upinzani, inataka kujua kuhusiana
na safari ya waziri Jimboni kwani tunajua kuwa huyu ni Mbunge wa Viti maalum na
hana jimbo hiyo ziara alifanya kwenye Jimbo gani na fedha za mwaka huu
anategemea kwenda kufanya ziara jimbo gani? Aidha , tunataka kujua fedha
wanazolipwa kama posho ya mafuta na Bunge kwa ajili ya kufanya ziara majimboni
huwa wanazitumia kufanya nini wakati wizarani nako wanajitengea fedha kwa ajili
ya kwenda majimboni, ni kwanini wao Mawaziri na Manaibu wawe wanalipwa mara
mbilimbili fedha kwa ajili ya kazi moja ? Pia ni mamlaka gani huwa inapanga na
kuidhinisha viwango hivyo, au kila wizara inajipangia kutokana na wanavyotaka .
Mheshimiwa Spika, Baada ya kusema hayo
kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.
.......................................
Cecilia Daniel Paresso (Mb)
k.n.y Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-
Wizara ya Kazi na Ajira.
29.05.2013
shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa wema wake na wema juu ya maisha yangu nini i wamefanya kama si kwa Bibi Kate Lisa ambaye i daima kuona kama Mungu alimtuma mwanamke ambaye Mungu wamechagua kuwasaidia watu walio katika haja ya fedha kama mimi maskini mjane ambaye alikuwa short waliotajwa, na short wa fedha mwanamke ambao wana watoto wawili na ana majukumu mengi mwanamke ambaye alipoteza mume wake na ina kulipa bili yenye kodi ya nyumba na umeme bili zote mbili na ilikuwa scammed Jumla ya $ 4,000 uSD i kamwe kuamini kwamba bado kuna legit mkopo kampuni online ambao bado wanaamini kwamba watu ni katika tatizo la kifedha na tayari kusaidia baada ya kuwa scammed $ 450,000 uSD i kamwe kuamini kwamba bado kuna legit mkopo kampuni ya mpaka i alimkuta baada ya kuwa alikuwa posted na moja Bibi Luis juu ya jukwaa hiyo yeye alielezea jinsi yeye alipata mkopo wake kutoka Bibi Kate Lisa ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji Bibi Kate Lisa nyumbani mkopo na kisha i mara baada ya hakuna chaguo zaidi kuliko kujaribu bahati yangu kwa wakati wa tatu ili kuepuka kupoteza nyumba yangu (malazi ) ili i kufikiri juu yake i alikuja na hitimisho kwamba i unapaswa kujaribu tena hivyo i kuwasiliana Bibi Kate Lisa kupitia barua pepe wao walihudhuria kwangu katika chini ya 10mins i kutumika kwa ajili ya mkopo jumla ya $ 95,000,00 dola mkopo kupitishwa na ya chini kiwango cha riba na baada ya usindikaji i got mkopo wangu katika akaunti ya benki yangu jana hivyo i unataka haraka kutumia kati ya ushauri yoyote mtafuta mkopo huko nje kuwasiliana na Bibi Kate Lisa email mrskatelisaloanhome1@gmail.com yeye dhahiri kukupa mkopo unahitaji bila matatizo yoyote kwa mara nyingine tena , shukrani kwa Mungu kwa huruma yake juu ya maisha yangu. i itakuwa kuangalia mbele na kusikia ushuhuda wako mwenyewe tu kama yangu.
ReplyDeleteBibi Sarah .