Balozi
wa Tanzania nchini Ethiopia, Joram Biswaro amewataka wachezaji wa Taifa
Stars kuhakikisha wanaipeleka timu hiyo kwenye fainali za Kombe la
Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil.
Ametoa
changamoto hiyo wakati alipotembelea mazoezi ya timu hiyo jana (Mei 29
mwaka huu). Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager
imepiga kambi nchini Ethiopia na inafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Addis
Ababa.
“Watanzania
tunafurahi kutokana na uwezo mnaouonyesha, hasa baada ya kuifunga
Morocco mabao 3-1. Kama mliwafunga nyumbani hata kwao mnaweza kuwafunga.
Tunataka kuwaona Maracana (Brazil) mwakani, mimi tayari ninayo tiketi
mtanikuta kule,” amesema Balozi Biswaro ambaye enzi zake aliwahi
kuichezea timu ya Yanga.
Taifa
Stars ambayo iko Addis Ababa tangu Jumatatu (Mei 27 mwaka huu) imeweka
kambi katika hoteli ya Hilton ambapo Jumapili (Juni 2 mwaka huu)
itacheza mechi ya kirafiki na Sudan (Nile Crocodile) kwenye Uwanja wa
Addis Ababa.
Balozi
Biswaro ameikaribisha Taifa Stars ubalozini Addis Ababa mara baada ya
mechi dhidi ya Sudan ambapo itakutana na baadhi ya Watanzania wanaoishi
Ethiopia kabla ya kuondoka alfajiri kwenda Marrakech, Morocco kwa
kupitia Cairo, Misri.
Kocha
Kim Poulsen amesema kikosi chake kinaendelea na mazoezi vizuri na
kitaimarika zaidi baada ya wachezaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu
wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC)
kujiunga nacho Juni 3 mwaka huu jijini Marrakech kwa ajili ya mechi
dhidi ya Morocco itakayochezwa Juni 8 mwaka huu.
Wachezaji
walioko katika kikosi cha Stars jijini Addis Ababa ni Juma Kaseja,
Aggrey Morris, Mwadini Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin
Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo,
Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva,
John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd, Haruni
Chanongo na Zahoro Pazi.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Addis Ababa
+251 919910240
No comments:
Post a Comment