HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHE. HALIMA JAMES MDEE (MB) KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA 2012/2013 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI KWA MWAKA WA FEDHA 2013/14
I. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, hakuna
ubishi kwamba ardhi ndio msingi mkuu wa uchumu wa taifa lolote, na kwa maana
hiyo ardhi ni msingi maisha ya mwanadamu.
Ardhi ni miongoni mwa vitu vikuu vine vinavyohitajika ili taifa
liendelee. Hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere aliwashi kusema “Ili taifa
liendelee linahitaji watu, ardhi, siasa
safi na uongozi bora”
Mheshimiwa Spika,
nimekuwa nikijiuliza kuhusu chimbuko la umasikini uliokithiri Tanzania kwa
kuzingatia vigezo vya maendeleo alivyotoa Hayati Mwalimu Nyerere. Baada ya kufanya marejeo ya machapisho
mbalimbali lakini pia baada yakupata uzoefu wa uongozi kama Mbunge wa Wananchi
na hasa kama Waziri Kivuli kwa Arhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, na kwa
kuzingatia mwenendo halisi wa watawala hapa Tanzania nimegundua kuwa kiwazo
kikubwa kwa maendeleo ya nchi yetu sio watu (watu wapo wengi sana takribani
milioni 45), tatizo sio ardhi (hiyo ipo ya kutosha na ziada takribani hekta
milioni 94.3[1]).
Mheshimiwa Spika,
tatizo ni “siasa safi na uongozi bora”. Tofauti na Kauli Mbiu
mkakati za kisiasa enzi za Mwalimu, kwamba Sisa ni kilimo, Uhuru na Kazi, Kilimo cha Kufa na Kupona,
sasa hivi tunashuhudia siasa za watawala za kuongeza umasikini wan chi hii “kwa
ari na kasi zaidi, tunashuhudia watawala wakijigamba kwamba “wamethubutu
na wameweza” kuwa mafisadi wa rasilimali za nchi hii.
Mheshimiwa Spika,
maneno niliyoyatumia hivi punde hayanifurahishi hata kidogo, lakini
nimelazimika kuyasema kwa kuwa sioni watawala wa nchi hii wakifikiri namna ya
kumkomboa mtanzania kutoka kwenye wimbi la umasikini, bali kila mmoja
anajitahidi kujilimbikizia mali hasa kwa hofu ya kuondolewa madarakani (akakosa
namna ya kuishi) kutokana na kuenea kwa kasi na kuungwa mkono kwa wingi na
wananchi kwa chama kikuu cha upinzani nchini cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA).
Mheshimiwa Spika,
nasikitika sana kwamba badala ya Serikali ya CCM kutumia muda na rasilimali
ilizo nazo kutatua matatizo sugu ya kiuchumi ya taifa hili (hususan uporaji wa
ardhi ya wananchi), inatumia fedha nyingi za umma kupambana na CHADEMA ambayo
inatetea maslahi ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, Nchii hii ina rasilimali nyingi sana ikiwemo
ardhi ambazo zingeweza kuifanya Tanzania
kuwa miongoni mwa nchi za ulimwengu wa pili kiuchumi, lakini tuna tatizo la uhaba wa viongozi wenye “ufahamu, maadili na busara” ya kutumia rasilimali
hizi kwa maslahi ya taifa.
Mheshimiwa Spika,
kutokana na ombwe la uongozi katika taifa hili, na kutokana na “ubinafsi,
ulafi na ufisadi” wa viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali
za nchi yetu, leo taifa hili ni masikini, miaka hamsini na mbili baada ya
uhuru.
Mhshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA imekuwa ikibainisha mapungufu
na kasoro nyingi katika masuala ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi tangu
mwaka 2011 hadi leo, lakini Serikali hii ya CCM imeendelea kuwa na shingo ngumu
kuyafanyia kazi mapendekezo ya Kambi ya Upinzani jambo ambalo linaendelea
kusababisha migogoro mingi na ufisadi katika umiliki na matumizi ya ardhi hapa
nchini
Mheshimiwa Spika,
katika hotuba ya msemaji mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani katika bajeti ya
wizara hii kwa mwaka wa fedha 2011/2012, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
ilianisha matatizo makubwa ya ardhi
nyumba na maendeleo ya makazi na kuitaka Serikali kutafuta ufumbuzi kwa kuchukua
hatua za haraka. Matatizo hayo yalikuwa kama ifuatavyo:-
1.
Uporaji wa ardhi ya Tanzania unaofanywa chini ya
usimamizi wa Serikali kwa mbinu au hila ya uwekezaji,
2.
Ufisadi wa ardhi unaofanywa na viongozi wa Serikali na
Chama cha Mapinduzi kwa kuuziana ardhi
kwa bei ya kutupwa,
3.
Ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka
1999 na Sheria namba 5 ya ardhi ya vijiji ambapo viongozi wa Serikali walikuwa
wakigawa ardhiki holela bila kuzingatia matakwa ya sheria hizo,
4.
Migogoro mikubwa ya ardhi baina ya wakulima na
wafugaji ambayo kwa nyakati tofauti imepelekea umwagaji wa damu miongoni mwa
wananchi,
5.
Matatizo makubwa katika tathmini ya malipo ya fidia
kwa wananchi wanaotakiwa kuondoka katika maeneo yao kupisha matumizi mapya ya
ardhi,
6.
Kuendelea kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi jambo
ambalo limesababisha wananchi kuendelea kuishi katika makazi duni na hivyo
kuhatarisha usalama wao na kutweza utu wao,
7.
Serikali na
taasisi zake kutolipa kodi za pango kwa wakati kwa Shrika la Nyumba la Taifa na
hivyo kulirudhisha nyuma kimaendeleo, na
8.
Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba bora na Vifaa vya
Ujenzi kushindwa kuleta mabadiliko
kutokana na kuongezeka kwa nyumba zisizo bora ( kama vile nyumba za tembe, tope
na nyasi) na kuongezeka kwa bei ya vifaa vya ujenzi
Mheshimiwa Spika,
Aidha, katika bajeti ya wizara hii kwa mwaka 2012/2013, Kambi Rasmi ya Upinzani
iliendelea kuipigania ardhi ya watanzania inayoporwa kwa kuitaka Serikali
kufanya yafuatayo:-
1.
Kuyarejesha kwa wananchi, mashamba yote
yaliyobinafsishwa ambayo wawekezaji wameshindwa kuyaendeleza,
2.
Kutatua mgogoro wa ardhi kati ya Hifadhi ya Taifa ya
Tarangire na vijiji vya Gijedabung,
Ayamango[2] na Gedamar[3] katika
Wilaya ya Babati Mkoani Manyara ambapo mamlaka ya hifadhi ilitoa amri kwa
wananchi wa vijiji hivyo kuondoka kwa kuwa walikuwa wako ndani ya hifadhi,
3.
Kutatua migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima
hasa katika Wilaya ya Karagwa na Biharamulo
Mkoani Kagera ambapo wananchi walifukuzwa kwenye maeneo yao ya kilimo na
maeneo hayo kugawiwa kwa wafugaji matajiri bila wananchi kuhusishwa,
4.
Kulipa fidia stahiki kwa wananchi wanaotakiwa kuondoka
katika maeneo yao kupisha matumizi mapya ya ardhi hasa katika maeneo ya Kibamba
–Luguruni, Kwembe Kati na Kigamboni Mkoa wa Dar es Salaam,
5.
Kuandaa mpango mkakati na endelevu wa kukomesha
uvamizi wa ardhi (hasa katika Manispaa ya Kinondoni ) unaofanywa na magenge ya
watu wenye silaha wanaovamia maeneo ya
watu, kuharibu mali na kuyakalia maeneo hayo kwa nguvu jambo linalosababisha
uvunjifu wa amani na hatimaye vifo,
6.
Kubatilisha mkataba wa kifisadi kati Kampuni ya
Uwindaji ya Game Frontiers of Tanzania Limited na Kampuni mbili za nje za
uchimbaji madini za Uranium Resourses PLC na Western Metals, kufanya utafiti wa
uchimbaji wa madini ya Uranium kwenye kitalu cha uwindaji katika kijiji cha
Mbarang’andu kinyume cha sheria.
7.
Kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Kodi za Nyumba (Real
Estate Regulatory Authority) ili kuratibu, kuweka viwango na miongozo ya kodi
za nyumba ili kuwaondolea wananchi wapangaji wa nyumba adha kubwa ya gharama
kubwa za pango zisizo na viwango.
Mheshimiwa Spika, baada
ya Serikali hii ya CCM kuoneka kutojali maslahi ya wananchi katika kumiliki na
kutumia ardhi yao, na baada ya kuongezeka kwa kasi ya kugawa ardhi kwa wageni
kwa hila ya uwekezaji, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA
iliendelea kupambana kuitetea ardhi ya Tanzania ili wananchi wawe wanufaika wa
kwanza wa rasilimali ardhi.
Mheshimiwa Spika, Safari
hii, Kambi Rasmi ya Upinzani ilileta hoja binafsi bungeni tarehe 8 Novemba, 2012
kwa ajili ya hatua za kibunge baada ya Serikali kuoneka kutojali uporaji wa
ardhi ya wananchi unaofanywa kwa kisingizio cha uwekezaji.
Mheshimiwa Spika, katika hoja hiyo, Bunge liliazimia
kwamba :
- Zoezi la ugawaji ardhi kwa wawekezaji wa nje na ndani lisitishwe hadi hapo tathmini ya kina itakapofanyika kubaini ni kiasi gani cha ardhi kipo mikononi mwa wawekezaji na wasio wawekezaji.
- Tathmini ya kina ifanyike kuweza kubaini raia wa kigeni na wa ndani waliojipatia ardhi kinyemela kupitia serikali za vijiji kinyume na matakwa ya sheria ya ardhi Na. 5 ya mwaka 1999.
Mheshimiwa Spika, baada ya mvutano mkali kati ya
wabunge wa CCM wakiisaidia Serikali yao dhidi ya Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, hatimaye Serikali ilikubali kwa shingo upande kufanya tathimini ya
ardhi iliyoko mikononi mwa wageni lakini
ilikataa kusitisha uwagaji wa ardhi kwa wageni. Hata hivyo, Serikali ilitakiwa
kuleta ripoti ya tathmini hiyo bungeni mwezi Aprili, 2013, lakini mpaka sasa Serikali haijafanya hivyo.
Mheshimiwa Spika, kabla sijajielekeza katika mambo
mahsusi yanayohusu wiza hii kwa mwaka wa fedha 2013/2014 napenda kuchukua
nafasi hii kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuitaka Serikali
ilieleze Bunge hili na wananchi wote, kwamba imetatua kwa kiasi gani matatizo
yaliyoainishwa hapo juu na imetekeleza kwa kiasi gani mapendekezo ya Kambi
Rasmi ya Upinzani yaliyoorodheshwa hapo juu (moja baada ya jingine) ya tangu
mwaka 2011 hadi leo?. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inayoongozwa na
CHADEMA inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili imetekeleza vipi maazimio ya
bunge ya tarehe 8 Novemba, 2012 yaliyoitaka Serikali kufanya tathmini ya ardhi
iliyopo chini ya umiliki wa wageni (wawekezaji) na kuleta taarifa ya tathmini
hiyo bungeni mwezi Aprili, 2013?[
Mheshimiwa Spika, ni masikitiko
yangu kwamba mpaka nawasilisha bajeti hii, licha ya kupeleka taarifa ya
maandishi kwenye ofisi yako nikikutaka uielekeze serikali kuwasilisha ripoti
husika mbele ya Bunge hili tukufu ,ili kuliwezesha Bunge kufanya maamuzi ya
msingi/muhimu katika sekta ya ardhi sioni jitihada zozote za kuleta ripoti hiyo
katika mkutano huu wa bunge.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Taarifa
ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imezipata,
ambazo tunaamini ndicho chanzo cha serikali kushindwa kuleta ripoti kwa
wakati ni kushindwa kwa timu iliyopewa jukumu la kuzunguka nchi nzima kufanya
tathmini kushindwa kumaliza kazi ndani
ya muda iliyopewa, sambamba na kukumbana na upinzani mkubwa wa kupata taarifa
kutoka kwenye mashamba ambayo yanamilikiwa na viongozi na vigogo wakubwa
serikalini!
II. UWEKEZAJI
KATIKA ARDHI YA TANZANIA
Mheshimiwa Spika, Tanzania ina ukubwa wa Zaidi ya Km2 940,000. Kwa
mujibu wa sheria za ardhi na 4 na 5
za 1999 ardhi ya Tanzania imegawanyika
katika makundi 3 ambayo ni ardhi ya Jumla, ardhi ya kijiji na ardhi ya
hifadhi. Hadi sasa ardhi ya hifadhi
inaelezewa kufikia zaidi ya 30% ya ardhi yote. Ardhi yenye rutuba na inayofaa
kwa kilimo cha aina mbali
mbali inakadiriwa kufikia hekta milioni
80, eneo linalotumika kwa sasa
linakadiriwa kufika 10% tu.
Mheshimiwa Spika, shughuli za
uwekezaji huongozwa na sheria ya
uwekezaji ya mwaka namba 26 ya 1997.
Hata hivyo sheria ya ardhi inatamka wazi
kuwa wasio raia wa Tanzania hawaruhusiwi kumiliki ardhi
isipokuwa kwa matumizi ya uwekezaji
ambapo hupewa hati hafifu kupitia kituo cha uwekezaji (TIC)
Mheshimiwa Spika, pamoja na
katazo hili la kisheria, tumeshuhudia mara nyingi
wawekezaj wasio watanzania wakimiliki ardhi,wakiwaondoa wamiliki wa asili katika maeneo yao na
kuharibu kabisa mifumo yao ya maisha.Hii mara nyingi imetokea kwa sababu ya
kukiuka kwa makusudi sheria na taratibu zilizopo , udhaifu wa mifumo ya
utekelezaji wa sheria na dharau kwa vyombo vya ngazi za chini za
utawala na wananchi wao kwa kuwa maamuzi hufanywa na ngazi za juu.
Mheshimiwa
Spika, ingawa karibu kila eneo limevutia wawekezaji wa aina fulani
katika ardhi, lakini maeneo ya uchimbaji madini, shughuli za wanyhama pori
(kama vile uwindaji, mahoteli, na utalii) pamoja na kilimo yameonekana
kuwavutia zaidi wawekezaji.
Mheshimiwa
Spika, katika Kilimo, ambako kuna wazalishaji wadogo,
shabaha ya hivi karibuni imekuwa ni kuwekeza kwenye kilimo cha “nishati uoto” kwa ajili ya mafuta ya magari na mitambo. Jambo la
kutilia shaka ni kwamba; wawekezaji wengi sasa wanaenda vijijini kutafuta ardhi
wenyewe badala ya kupewa na kituo cha uwekezaji kama sheria inavyotaka. Kutokana
na wanavijiji kutokuwa na uwezo wa
kimaarifa na ujuzi wa kujadiliana na wawekezaji kwa mizania sawa, wamekuwa
wakitoa ardhi kiholela bila kufuata
taratibu za kisheria .Pale ambapo
wanavijiji wamethubutu kuhoji, sheria
imetafsiriwa vibaya kuwapora ardhi na haki yao. Kwa mfano; sheria ya ardhi namba
4 ya 1999 inaeleza kwamba: ardhi ya
kijiji isiyotumika, wala kukaliwa, ni ardhi ya jumla na hivyo inaweza kuchukuliwa
na serikali kuu wakati wowote ingawa ukweli unabaki pale pale kuwa ni ardhi ya
kijiji.
III. UKADIRIFU NA TATHMINI YA
WAMILIKI WA MASHAMBA TANZANIA BARA 2013[4]
Mheshimiwa Spika, kikosi kazi
kilichopewa kazi na Wizara ya Ardhi , kilipewa jukumu la kufanya tahmini nchi
nzima ya watu wanaomiliki mashamba makubwa .Mashamba yaliyofanyiwa tathmini ni
yale tu yenye ukubwa zaidi ya ekari 50 (Hekta 20).
Malengo ya Tathmini:
i)
Kufanya uchunguzi wa
mashamba ya wawekezaji wa ndani na wa nje yaliyopatikana kwa njia halali na ambazo sio halali,
ii)
Utaratibu uliotumiwa na wawekezaji kupata mashamba
iii)
Kuangalia uhalali wa umiliki (kwa wenye hatimiliki)au ukodishaji wa
mashamba,
iv)
Kutambua tozo mbali mbali (land rent,fees,levies) za
ardhi au malipo mengine yeyote yananayotakiwa kulipwa kutoka katika mashamba
husika,
v)
Kutambua matumizi ya ardhi, kama yanaendana na matakwa ya
Mkataba,
vi)
Kutambua maendelezo yaliyofanywa katika mashamba husika,
kama yapo!
vii)
Kutambua migogoro ya ardhi (kama ipo) kati ya wamiliki wa
mashamba na wanavijiji na hatua ambazo zimeshachukuliwa/zinazochukuliwa kutatua
migogoro husika
viii)
Kutambua faida iliyotokana na uwekezaji na kwa namna
vijiji vinavyowazunguka wawekezaji
vimenufaika kutokana na uwekezaji huo!
Mheshimiwa Spika, tathmini hii
ilikuwa muhimu kutokana na ukweli kwamba
ongezeko la mahitaji ya chakula
duniani, nishati mbadala, mali ghafi, mbao na uhifadhi wa misitu imesababisha
ongezeko kubwa la uhitaji wa ardhi duniani . Uhitaji huu[5] ndio unazisukuma kwa kasi
kubwa nchi zilizoendelea kuja Afrika
kutafuta ardhi.[6]
Mheshimiwa Spika, watafiti
hawakutembelea nchi nzima, walitembelea wilaya 79 tu! na kukagua mashamba 763 tu (sampling). Licha uchache wa
maeneo yaliyotembelewa ripoti hii sio ya kupuuzwa kwa kuwa inatoa sura ambayo,yawezekana
ikawa ndio hali halisi ya maeneo mengine ya nchi.
Utafiti umegundua yafuatayo:
1) Umiliki.
Imegundulika kwamba katika mashamba
makubwa 763 yaliyotembelewa, mashamba 455 sawa na 65.8% yalikuwa
yanamilikiwa na watanzania wenyewe (individual ownership), ikilinganishwa na 14 (2%) yaliyokuwa chini ya umiliki wa raia wa
kigeni . Mashamba yaliyokuwa yanamilikiwa kwa ubia kati ya watanzania na
wageni yalikuwa 31 (4.4%).
Hata hivyo, licha
ya raia wa kigeni kuwa na mashamba
machache kiidadi walikuwa wanamiliki
maeneo makubwa ya ardhi
ukilinganisha na watanzania. Timu ya
uchunguzi imebainisha kwamba hali hii inatakiwa iangaliwe kwa jicho pana!
Kielelezo Na. 1
Aina ya
umiliki
|
Wastan wa ukubwa wa shamba
|
Idadi ya Mashamba
|
Jumla (Ekari)
|
% ya eneo lote
|
|||
Kampuni zinazomilikiwa na
watanzania
|
2,972.03
|
72
|
213,986.38
|
23.71
|
|||
Kampuni zinazomilikiwa kwa ubia
kati ya watanzania na wageni
|
3,091.66
|
31
|
95,841.37
|
10.62
|
|||
Kampuni za Kigeni
|
6,301.55
|
31
|
195,348.04
|
21.65
|
|||
Mashamba yanayomilikiwa na watanzania (individuals)
|
280.59
|
455
|
127,669.61
|
14.15
|
|||
Mashamba yanayomilikiwa na wageni (individual)
|
2,547.18
|
14
|
35,660.50
|
3.95
|
|||
Mashamba yanayomilikiwa na
Taasisi
|
2,049
|
63
|
129,108.09
|
14.31
|
|||
Mashamba ambayo hayajulikani ya nani
|
4,191.58
|
25
|
104,789.39
|
11.61
|
|||
Jumla
|
1,305
|
691
|
902,403.38
|
100
|
Mheshimiwa
Spika, utafiti
umeonyesha kwamba kuna tofauti kubwa sana ya umiliki wa mashamba makubwa kati
ya raia wa kigeni na watanzania. Wakati watanzania (mmoja mmoja) wanaonekana kumiliki 60% ya ‘mashamba’ yote
yaliyotembelewa, mgao wao katika jumla kuu ni ekari 127,670 ambayo ni sawa na 14% ya eneo lililofanyiwa utafiti. Wakati
huo huo, makampuni yanayomilikiwa na
wageni, ambayo wana miliki asilimia
4% tu ya idadi ya mashamba yaliyotembelewa, lakini wanahodhi/miliki eneo
lenye ukubwa wa Zaidi ya 21% (ekari 195,348 ) ya ardhi yote
iliyofanyiwa utafiti. Mashamba
yanayomilikiwa na makampuni ya kitanzania ni ekari 213, 986 tu.
Mheshimiwa Spika, kwa wastani makampuni ya
kigeni wana maeneo makubwa ya mashamba ,
yakifuatiwa na makampuni yanayomilikiwa kwa ubia baina ya watanzania na raia wa
kigeni. Ni muhimu hapa ikaeleweka kwamba, katika makampuni ambayo watanzania
inasemekana wana ubia, hisa zao ni finyu sana kati ya (1%-10%)..ya hisa zote.
Mheshimiwa
Spika, utafiti umeonyesha pia kwamba;
wakati raia wa kigeni kwa wastani
wanamiliki shamba lenye ukubwa wa ekari 6,302, raia wa kitanzania kwa
wastani wanamiliki shamba lenye ukubwa wa ekari 280 tu!
Aidha, mashamba mengi ya raia wa kigeni yalikuwa na ukubwa unaokaribia ekari 1,526,
ambao ni mara 18 zaidi ya mashamba yanayomilikiwa na watanzania. Wataalam
hao wanazidi kusisitiza kwamba: ni
ukweli usiofichika kwamba: umiliki wa
mashamba makubwa umetawaliwa na raia wa kigeni.
Mheshimiwa
Spika, ni muhimu
wabunge na wananchi wakaelewa kwamba; kinachozungumziwa hapa ni mashamba ambayo tayari yana hati miliki (miaka 33, 66 au 99) na sio ardhi za vijiji ambazo ( kisheria ziko
chini ya vijiji)lakini zinaweza
kubadilishwa wakati wowote na kupangiwa matumizi mengine pasipo kijiji kuwa na
mamlaka ya kuzuia. Hii inashabihiana
kabisa na utafiti uliofanywa na Oxfarm
uliobainisha kwamba katika nchi zinazoendelea kuna zaidi
ya ekari 203 milioni ambazo ziko
chini /zimechukuliwa na raia/wawekezaji wa kigeni.
Mheshimiwa
Spika, baadhi ya
mashamba yaligundulika kwamba
yanamilikiwa na maafisa waandamizi wa serikali, ambao taarifa za
mashamba yao zilishindwa kupatikana katika utafiti huu wa serikali,
chini ya usimamizi wa wizara ya ardhi
kwa sababu wamiliki husika hawakuwepo kwenye mashamba yao na walinzi
wao
hawakuwa tayari kutoa taarifa za
mashamba husika zaidi ya kutaja majina
ya wamiliki wa mashamba!hii ilitokea Dakawa, na ilihusisha mashamba 28! Ni azma ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
kuwataja wamiliki wa mashamba hayo, kama serikali itagoma kufanya hivyo!
Mheshimiwa
Spika, katika
kile ambacho hakikutarajiwa uchunguzi umebaini kwamba kuna makampuni ya kigeni na raia wa kigeni wanaomiliki ardhi kimila (customary land right) ambayo kwa
mujibu wa sheria za nchi, ni maalum/
mahsusi kwa raia wa Tanzania pekee mpaka pale ambapo ardhi husika itahuilishwa
(transferred from one category to another). Huu ni uvunjwaji mkubwa sana wa sheria ya
umiliki ardhi kimila… Aidha, utafiti
umegundua pia kwamba; wageni wanamiliki ardhi ambayo haijulikani iko kwenye
kundi gani (‘the unspecified category’) la ardhi ambayo ina ukubwa wa ekari
94,360 (10%ya ardhi iliyofanyiwa utafiti).
Mheshimiwa
Spika, ni jambo
la kusikitisha na kushtua sana kama ardhi yenye ukubwa kiasi hicho iko mikononi
mwa wawekeaji wa kigeni. Aidha, ni jambo
la kushangaza sana kama Wizara haifahamu kiasi kikubwa hivyo cha ardhi kiko
katika himaya ya nani? Kama wizara au mamlaka zilizo chini yake hazijui jambo
hili , ni nani atakaye jua?
IV. MUDA WA UMILIKI
WA MASHAMBA
Mheshimiwa Spika, utafiti umeonyesha sehemu kubwa ya makampuni ya kigeni au
raia wa kigeni wanaomiliki ardhi ndio
wanaoongoza kwa kuwa na mikataba ya muda mrefu ya umiliki wa ardhi, yaani miaka 99! (ekari 500,135 kati ya 902,403 zilizofanyiwa utafiti). Halika
dhalika utafiti umegundua pia kuna wawekezaji ambao wana umiliki wa ardhi wa
kimila (Customary Right of Occupancy).
Kitu aambacho ni kinyume kabisa na sheria za nchi , ambazo zinampa fursa
Mtanzania tu kuwa na umiliki wa aina hiyo!
V. UPORAJI WA ARDHI
Mheshimiwa Spika, imebainika
pia
kwamba watu wenye fedha na watu wenye ushawishi wa kisiasa wamekuwa
wakitumia nguvu zao kushawishi na kupoka ardhi za vijiji , katika
mazingira
ambayo hakuna ushirikishwaji wa wanakijiji (55.11% ya maeneo
yaliyotembelewa,
wanakijiji waliohojiwa walikiri hakukuwa na ushirikishwaji wakati ardhi
yao
inapochukuliwa). Ushawishi husika ni pamoja na kutoa ahadi za uongo na
hongo
kwa viongozi wa serikali za vijiji kama ilivyotokea kwa makampuni ya
Bioshape (Wilaya ya Kilwa na Sun Biofuels- Wilaya ya Kisarawe). [7]
Mheshimiwa Spika, utafiti pia iligundua kwamba fidia kwa wananchi wanaoondolewa
kwenye maeneo yao ili kupisha uwekezaji kama
ilivyoelekezwa na kifungu
34(3)b cha sheria ya ardhi, namba 4 ya 1999 hailipwi.
VI. TOZO ZA ARDHI ( LAND RENT ,
FEES,LEVIES AND OTHER PAYMENTS)
Mheshimiwa Spika, kifungu cha 33 cha
Sheria ya Ardhi (Sheria na 4,ya mwaka 1999) kinatamka kwamba , mwenye hati
miliki anatakiwa, pamoja na masharti ya
vifungu vingine vya sharia, kulipa kodi
ya mwaka
kama ilivyoelekezwa na Sheria ya Fedha za Umma (Public Finance Act). Utafiti
umegundua kwamba kati ya mashamba 763 yaliyotembelewa, ni mashamba 278 (36.4%)
tu ndio yaliyolipa kodi ya ardhi (2012) kama sheria inavyotaka. Wamiliki wa
mashamba 432 (56.6%) waliohojiwa walikiri kwamba hawajalipa kodi husika. Halikadhalika utafiti umegundua kwamba 43.47%
ya wenye mashamba waliohojiwa walikiri
kwamba hawajawahi kulipa kodi ya ardhi toka
walipomilikishwa mashamba hayo!. Hii inaonyesha kwamba , hata wale watu
ambao wanamiliki ardhi kihalali, uhalali
wa umiliki wao una mashaka kutokana na
kutokidhi takwa muhimu la kumiliki ardhi husika ambalo ni ulipaji wa kodi ya
ardhi. Zaidi ya hayo, utafiti umeonyesha pia kwamba; mashamba 643 kati ya 763 yaliyotembelewa yalishindwa kutoa
ushahidi (risiti) kuonyesha kama ni kweli walikuwa wanalipa kodi za ardhi kama
matakwa ya kisheria yanavyoelekeza.
VII. UWEKEZAJI
KATIKA NISHATI UOTO (BIOFUELS) NA MUSTAKABALI WA ARDHI YA WATANZANIA
Mheshimiwa
Spika, kupanda
kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na mabadiliko hasi ya hali ya
hewa duniani vimechangia kwa kiasi kikubwa wimbi la utafutaji nishati
mbadala ili kukabiliana na uchafuzi wa hali ya hewa na pia kuleta
uhuru katika matumizi ya nishati. Kuanzia
miaka ya 2000, matumizi ya nishati yalianza kushika kasi sana katika
maeneo
mbali mbali duniani. Kwa Tanzania,
tangu nishati hiyo ianze kuchukua mkondo
wake ikiwahusisha wawekezaji wakubwa na wadogo , ujio wake
umeshuhudia kiasi kikubwa cha ardhi kikichukuliwa kwa ajili ya mashamba ya kuzalisha nishati
hiyo.
Mheshimiwa
Spika, watetezi wa Nishati
Uoto, wamekuwa wakiipigia chapuo aina hiyo ya nishati kwa kutaja faida zake
ambazo ni pamoja na kuzalisha na kukuza ajira kwa wananchi waishio maeneo
yalipo mashamba au viwanda vinavyozalisha aina mbalimbali za nishati hiyo,
kuongeza mapato kwa wakulima wadogo na
kupambana na gesi zijulikanazo kama Green house gases (GHG). (Wizara ya
Nishati na Madini, 2006)[8]
Mheshimiwa
Spika, maeneo kadhaa nchini yamekuwa katika utekelezaji wa
miradi ya mashamba ya kuzalisha Nishati Uoto kama vile Kilwa, Kisarawe,
Bagamoyo, Arusha, Manyara, Shinyanga, Singida na Mwanza. Tokea makampuni haya
ya kigeni,yalipokabidhiwa ardhi ya watanzania kama njugu, na katika mazingira
mengine chini ya ukuwadi wa Kituo cha uwekezaji nchini hakuna faida “endelevu”
iliyopatikana zaidi ya kuongezeka kwa migogoro ya ardhi kati ya wawekezaji na
wanavijiji na kutamalaki kwa rushwa, udanganyifu, hadaa na mizengwe miongoni mwa watendaji wa vyombo
vinavyosimamia masuala ya ardhi, wananchi na
wawekezaji.
Mheshimiwa
Spika, taratibu nyingi za ugawaji na uhawilishaji wa ardhi
zilikiukwa makusudi kwa lengo la kuwapendelea wawekezaji hasa wa kigeni. Katika
maeneo ya uwekezaji, mifumo ya maisha ya wananchi imehatarishwa kwa
kunyang’anywa ardhi walizokuwa wakitumia kwa shughuli za kilimo, malisho na
shughuli nyinginezo za uzalishaji na za kijamii. Wale waliobahatika kupata
ajira katika kampuni za wawekezaji nao wameachwa njiani hawajui kesho yao baada
ya wawekezaji kuwaachisha kazi na wengine
kususa miradi yao, kuwatelekeza
wafanyakazi na kutokomea kusikojulikana.
Mheshimiwa
Spika, kwa kuwa
taratibu za kisera na kisheria nchini ni dhaifu katika usimamizi wa
Nishati Uoto, uanzishwaji wa miradi ya nishati hii nchini kwa kiwango
fulani umesababisha kuwapo kwa unyonyaji
wa rasilimali muhimu za taifa ambazo ni ardhi, maji,misitu na nguvu kazi
ya watanzania.
VIII. HALI
YA MASHAMBA WALIYOPORWA WANANCHI NA KUKABIDHIWA WAWEKEZAJI KWA KILIMO CHA MAZAO
YA NISHATI UOTO (BIOFUEL)
Mheshimiwa
Spika, uchunguzi
umebaini kuwa katika wilaya ya Kilwa,mwekezaji alikuwa kampuni iitwayo Bioshape
kutoka nchini Uholanzi. Kampuni hii ilipewa ardhi yenye ukubwa wa hekta 80,000
kwalengo la kulima zao la mbono kaburi.Ardhi hiyo ilihusisha vijiji vine ambavyo ni Mavuji,
Migelegele,Liwiti na Inokwe. Mwekezaji
hakuwahi kulima eneo lote bali alilima
hekta 800 ambazo ni shamba la mfano lililopo katika kijiji cha Mavuji.
Mheshimiwa
Spika, dhana ya uwekezaji
ni jitihada za kugeuza mali
asili za nchi kuwa katika rasilimali kwa kutumia nyenzo kama
mtaji , teknolojia na nguvu kazi. Ziada inayotokana na
uzalishaji hurejeshwa katika kuimarisha
miundombinu , mitaji, teknolojia na
rasilimali watu ( watu, fedha, malighafi ) ili faida iweze kupatikana na pale inapopatikana faida ndipo
matunda ya maendeleo huonekana!
Mheshimiwa
Spika, kama ambavyo tulifanya makosa ya kutokulinda maslahi
ya watanzania katika uvunaji wa madini mbali mbali yanayopatikana nchini, na
kama ambavyo tunaelekea kufanya makosa katika uvunaji na nishati muhimu ya gesi
, ama kutokana kuwa na viongozi wasio na upeo/wabinafsi/wanaoendekeza
njaa/waliokosa uzalendo kutokana na nchi yetu kutokuwa na intelijensia ya kiuchumi,
nchi yetu imejikuta ikikaribisha wawekezaji wa hovyo,wasio na mitaji,
teknolojia wala nguvu kazi!
Mheshimiwa
Spika, serikali ilikaribisha makampuni ya kigeni pasipo hata kuandaa sera kwa ajili ya nishati
uoto. Sote tunafahamu fika kwamba sera
ndio dira, na mwongozo utakaoelekeza
nini kifanyike,kwa namna gani na malengo yapi. Uzembe huu umelisababishia Taifa
na vijiji vilivyoporwa mashamba yao hasara kubwa. Ikumbukwe kwamba katika
maeneo mengi kama sio yote wananchi walipoteza ardhi yao pasipo kulipwa
fidia,waliolipwa fidia walilipwa kidogo sana,ajira zilizopatikana katika
mashamba hazikuwa endelevu. Maeneo yaliyokuwa mapori huku yakiwanufaisha wananchi kwa kufanya shughuli
za kijamii kama kupata miti ya dawa ,kuchota maji,kukata kuni na
shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi, hivi sasa yamegeuka kuwa majangwa ). Na katika
mazingira mengine vijiji vilikumbwa na njaa kwa sababu ardhi waliyokuwa wakiitumia kwa uzalishaji wa mazao
ya kilimo, walipewa wawekezaji ambao
walijikita katika uzalishaji wa mibono!
Mheshimiwa
Spika, kutokana na uzembe wa serikali, wawekezaji waliokuja
kwa ahadi kemkem waliiishia kutelekeza mashamba. Mheshimiwa Spika, kwa ufupi naomba Bunge lako tukufu lipate taarifa
juu ya hali ya maelfu ya hekta ya ardhi zilizoporwa kwa wanakijiji, kwa mabavu
kulikoenda sambamba na kuvunjwa kwa sheria kwa makusudi : Naamini taarifa hii
itapelekea Bunge lako tukufu, kutoa au kufanya maamuzi yenye busara kwa manufaa
ya taifa na wananchi wake:
1. Sun
Biofuel (Mwekezaji toka Uingereza) alipewa eneo la – Kisarawe ardhi ya
vijiji 11 ( hekta 8200-9000) kwa
miaka 99, akiahidi kutengeneza
ajira 5000 [9]. Walianza
kusafisa eneo kwa ajili ya kupanda mazao mwezi Juini, 2009,na kufanikiwa
kupanda hekta 600 ilipofika Novemba,
2009. Waliahidi kusaidia wakulima wadogo wadogo wa pembezoni, ahadi ambayo
haikutimia mpaka walipositisha shughuli za uwekezaji (HAKIARDHI). Mwaka 2011
eneo husika liliuzwa kwa mwekezaji mpya
30 Degree ( ubia kati ya Raia wa Mauritania 90% na Mtanzania 10%. Mwaka 2012
kampuni ilifilisika .Imeachisha kazi ghafla wafanyakazi 750..ahadi zake zote za
kiuchumi na kijamii zilizoahidiwa zikaishia hapo…
2. Africa Biofuel & Emmission Reduction Co. (Tanzania
Ltd).[10]Ardhi
waliyopewa hekta 60,000 , wilaya ya Biharamulo (Biofuel)[11] Taarifa
za serikali zinaonyesha ,kampuni ilisimamishwa
na ofisi ya makamu wa Rais
kutokama na masuala yanayohusiana na masuala ya ardhi ( locher 2010)/wako kwenye hatua za mwisho
za kumilikiswa eneo na walitaraji ingia
mkataba 2010.
3. Agrisol energy Tanzania ( ubia kati ya Serengeti Adivisors ltd na Agrisol
Energy LLC / group (IOWA based ) . Mshirika: Pharos Global
Agricultures Fund, chini ya usimamizi wa Pharos
Financial Group (Dubai), wilaya ya Mpanda –Rukwa na Kigoma (Oakland
Institute) Mchakato wa kupata eneo la Rukwa bado unaendelea ( 325117 ha). Eneo ambalo limeshakabidhiwa
kwa mwekezaji hekta10,000( Lugufu) na
3250 (Basansa)- kigoma .Agrisol Energy Tz inamiliki 25% ya hisa za kampuni. Kampuni hii imeungana
na Kampuni ya Kitanzania the Serengeti
Advisors (Inayoundwa na vigogo/viongozi wastaafu wa serikali wenye
ushawishi mkubwa sana kwenye serikali ya CCM)
ili kuhakikisha kampuni inapata ardhi
kutoka Halmashauri ya wilaya ya Mpanda ( Baha 2011).
4. Agro Forest Plantation ( Misri), Rufiji ,(kilimo cha sukari kwa soko la Misri na la
ndani) ardhi waliyoomba ni hekta 10,000 iliyopo ni hekta 8,000 (RUBADA) ,
Ilikuwa ardhi ya Kijiji (Mojoro,Chumbi A,B,C na Ruma Villages
,imeasjiliwa na TIC Desemba, 2011, na inatarajiwa kuanza kazi Desemba 2014
5. Arkadia Ltd (Italia),
imesajiliwa
Brela Septembe 2007 , Wilaya ya Mkinga( jatropha ), Wilaya iliidhinisha
hekta 500, wizara ya adhi
imesajili/register hekta 25,000 ( Project bado ina utata ,maofisa wa
wilaya hawaelewi ni vigezo gani na kwa utaratibu upi kampuni iliweza
kupewa na
wizara ya ardhi hekta 25,000
(Sulle 2012)
6.Bagamoyo Eco Energy Ltd. (Eco Energy
Tanzania Ltd). Kampuni hii ina mchanganyiko wa wamiliki toka mwaka
2009. Eco Energy Bagamoyo[12]
inamilikiwa kwa 100% na Agro EcoEnergy Tanzania (ambayo nayo inamilikiwa 93.5% na EcoEnergy Africa AB, na 5%
Tanzania Petroleum Development
Co Ltd.(TPDC ) na 1.5% Community Finance
Corporation Ltd(CFC).
EcoEnergy Africa nayo inamilikiwa na Eco Development Europe AB , mwanahisa mdogo
wa SEKAB (SEKAB ndiye alikuwa mmiliki wa awali ,kabla ya kushindwa kuendelea na
uwekezaji kisha kuikabidhi ardhi kwa kampuni nyingine ya Sweden EcoEnergy
October 2009 , mwaka 2010 Eco Energy
inaunda Kampuni nnyingine, Bagamoyo EcoEnergy Ltd-Kampuni tajwa hapo juu!).
TPDC inamilikiwa kwa 100% na serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na CFC ina
milikiwa na watanzania watatu. Kampuni
inamiliki hekta 8000. Kwa makubaliano ya
sasa Eco Energy watapata mkataba wa
miaka 99 na fursa ya kutumia ardhi kwa uhuru kwa kuipatia serikali 25% ya hisa
za Kampuni na ujumbe wa Bodi.
7. Bio shape
Tanzania ltd (Dutch)- Kilwa-Lindi
(Jatropha),
hekta 81, 000. Kampuni imefilisika mwishoni mwa mwaka 2009, imefanikiwa kusafisha
eneo lenye ukubwa wa hekta 70 (Simeye 2011). Kampuni ilianza kufanya biashara
ya Magogo badala ya kulima. Baada ya shughuli zenye utata na hatimaye
kufilisika kwa kampuni hii, inasemekana kuwa wawekezaji wapya toka Netherlands, Uingereza, Marekani na
Italia wanataka kuuziwa eneo husika na
BIOSHAPE (Valentino 2011).
8.Bio Energy Tanzania ( Mtanzania na Mcanada), amepewa hekta 4500[13]. Kilimo
cha Jatropha , ardhi ya vijiji (Vigwaza
na Kidogozero). Bado haijaanza uzalishaji kicha ya kukabidhiwa ardhi,pia
kuna mgogoro mkubwa wa ardhi baada kijiji cha awali kugawanywa mara mbili
,kijiji kipya hakikuhali eneo lake kuchukuliwa na mwekezaji (Sulle 2012)
9. CAMS Agrienergy Tanzania Ltd.[14] Inamiliki
hekta 45000 .Katika maeneo ya Handeni na Bagamoyo . Mpango ukia ni kuzalisha lita 250 milioni za Ethanol na umeme wa 120MW
(Oakland Institute 2011a) .Kutokana na mgogoro
wa fedha mpango ulipunguzwa kukiwa na malengo ya kuzalisha lita milioni
20 kwenye hekta 18,000. Kampuni iko kwenye mipango wa kuanza uzalishaji. Kwa
sasa nguvu wamezielekeza miradi yao huko Uganda na Kenya!
10. Eco Carbon (French) - Zamani ikiitwa (Diligent Tanzania Ltd)- Bagamoyo
kilimo cha Jatropha .Waliomba hekta
75000, bado hawajakabidhiwa ardhi.
11.Euro Tech ( ya Korea). Ina mpango
ya kulima hekta 100,000 za Jatropha na Castor Oil for biodiesel , wanaanza na hekta 10,000 na
wana mpango wa kuwekeza dola za kimarekani milioni 20[15]
12. Eurovista Trading Co. Ltd ( ya India), Kampuni hii
imepewa hekta 6,000 za ardhi ya Kijiji[16], kwa ajili ya kilimo cha mahindi.
(Inasemekana kwamba alikuwa kwa madhumuni ya kulima pamba, lakini amekuwa akilima mahindi toka 2006).
13. FELISA (Farming for energy for better Livelihoods in
Southern Africa)
Kampuni hii ni ubia kati ya Tanzania na Ubeligiji. Hawa walipewa hekta 4,258
huko Kigoma kwa ajili ya kilimo cha nishati joto kwa soko la ndani. Wananchi hawakushirikishwa
ipasavyo katika suala hili na matokeo yake ni kwamba vyanzo vya maji vimezuiwa na mwkezaji (LEAT 2011).
14. FJS African
Starch Development Ltd. ( ya Kimarekani), Hawa waliomba hekta 5,000 za
ardhi ya vijiji vya Nyambili na Nyambunda huko Rufiji kwa ajili ya Kilimo cha Mihongo. (Rubada 2012).
15.Green Resourses
Ltd ( Subsidiary of Green
Resources SA (ya
Norway),
mwekezaji huyu anamiliki hekta 20,434 zikiwa
ni ardhi ya kijiji huko Mufindi, kwa ajili ya
upandaji wa misitu, uzalishaji wa nishati , na uuzaji wa mbao.
16. Green Resources Ltd. (ya Norway), hawa wanamiliki shamba kubwa la Kilombero
Forest Plantation, lenye ukubwa wa hekta 12,121. Wamepeleka maombi ya ziada hekta 10,000, na maombi hayo yamepata
Baraka za Halmashauri ya Wilaya, ila kibali cha Kamishna wa ardhi kinasubiriwa
(Sulle 2012)
17.Kagera Sugar Plantation (Mhindi na Mtanzania), hawa wamepewa hekta 7,000
huko Misenyi kwa ajili ya kuzalisha sukari, hata hivyo kiasi cha ardhi
kinachotumika ni hekta 300 tu
18. KYC Mpanga Co. Ltd (Kilimo cha Yesu) ya Switzerland, Kampuni hii
ilipewa hekta 3,000 za ardhi ya kijiji huko Kilombero kwa ajili ya Kilimo cha
Mpunga. Baada ya kupata hasara mwaka 2004, kampuni hii ilianza kukodisha
mashamba kwa wakulima wadogowadogo kwa shilingi 170,000/= kwa heka moja.
19. Kilimanjaro Aloe Vera Plantation Ltd (Mwingereza), huyu alipewa hekta 400 kwa ajili
ya kulima jatropha lakini baadaye alibadili mpango na kuanza kulima Aloe Vera.
(Mwamila et al. and Bengesi et.al 2009)
20.Kilombero Plantations Ltd (KPL), subsidiary fo AGRICA
Ltd. Kampuni
hizi zilipewa hekta 8,000 katika bonde la Mto Rufiji kwa ajili ya kilimo cha
Mpunga (Chachage 2010). Mwaka 2010, AGRICA ilipewa tuzo ya Mwekezaji
wa Kimkakati wa Kitaifa na Serikali. Ni kampuni inaoongoza Afrika Mashariki kwa
uzalishaji wa mchele.
21.Kilombero Sugar Company
Ltd.
(Afrika Kusini hisa 55% - Ilovo Sugar Plantation , mwingereza hisa 20% ED
&F Man, na Serkali ya Jamhuri ya Muungazo –Tanzania, hisa 25%). Hawa wana
hekta 8,000 za ardhi ya vijiji vya Msolwa Station, Hifadhi ya Selous, Gombala
na Nyange.
22. Kilomero Valley Teak Co. (Finland), hekta 4,748 - Kilombero –Ulanga [17].
23. Korean Rural Community Cooperation (KRC) ( Korea Kusini
na RUBADA). Hawa
wana hekta 15, 000 za ardhi kwa ajili ya kilimo cha Mpunga huko Rufiji (Oakland Institute 2011a;Daily
News & RUBADA 2012). Mwaka 2010,
kampuni hii ilipanga kuwekeza Dola za
Kimarekani 50 milioni.
24. Lindi Forests LTD (Subsidiary of Green Resources
SA(Norwegian). Kampuni
hii inamiliki hekta 13,000 za ardhi huko Lindi. Kiasi cha hekta 600 tu zilikwa
zimelimwa na kupandwa mazai mpaka 2009.
25. Lukulilo Farm Holdings (ya Uingereza) ina jumla ya hekta 5,000 za ardhi
ya vijiji vya Ndundunyikanza, Nyaminywili na Kipo – Rufiji. Kampuni imesajiliwa na TIC, 10/11/2011 na Itaanza kazi
Novemba 2014.
26.Mufindi Paper Mills
(Mhindi),
huya amepewa kibali cha kumiliki hekta
10,000 na Halmashauri ya Wilaya kwa
ajili ya Kilimo cha Mbao laini huko Kilombero,
27.Nava Bharat
Africa Resources PVT Ltd. (NBAR) (Mhindi), huya ameomba hekta
10,000 za ardhi ya kijiji huko kwa ajili ya kilimo cha Michikichi ili kuzalisha
mafuta ya Mawese,( RUBADA 2012- Sulle).
28. Pharos Financial Group ( Kampuni binafsi UAE)-Pharos Miro Agriculture Fund – hawa wamepewa hekta
50,000 kwa ajili ya kilimo cha Mpunga ila Kampuni hii haijasajiliwa Brela (Bakr
2010- Reuters article )
29.Rufiji Sugar Plant (mwekezaji wa nje, asili yake
haifahamiki,
(RUBADA 2012), hawa wana hekta 12,132
ikiwa ni ardhi ya vijiji vya Tawi, Nyamwange na Utunge – Rufiji. Wanatumia
ardhi hii kwa kilimo cha sukari, Kampuni imesajiliwa na TIC 9/5/2012. Itaanza
ifikapo shughuli zake Mei, 2015 (DAO 2012- Sulle2012)
30.SAP Agriculture Ltd.(Uturuki), Kampuni hii ina hekta 5,000 za
ardhi ya kijiji (Nyamwange na Ikwiriri) – Rufiji. Wananchi wamelalamikia sana
utarajibu wa utwaaji wa ardhi husika uliotawaliwa na ubabe na vurugu( Sulle
2009 field visit: Kweka 2012). Mpaka mwaka
2006, kampuni ilifanikiwa kuendeleza
hekta 500-600 tu. Kwa mujibu wa Uongozi wa Halmashauri ya kijiji, ardhi
husika amepewa mwekezaji mwingine
anayetambulika kwa jina la Majani ya Chai (Mwami & Kamata 2011), Kampuni
haijasajiliwa Brela.
31. Shanta Estate Ltd. (Mkenya na Mhindi) Hawa wa jumla ya
hekta 14,500 huko Bagamoyo
kwa ajili ya Kilimo cha Jatropha Eneo
hili limetolewa kwa makubaliano baina ya
mwekezaji na wanavijiji wa Kibindu,Mkange na Miyono, (Mwamila et.al). TIC haina taarifa kususiana na huyu mwekezaji
(Locher 2010). Sehemu ya eneo ambalo mwekezaji huyu analimiliki hekta 2000 , mwekezaji mwingine
Eco Energy naye anadai analimiliki
kutokana na makubaliano waliyoingia na wizara
ya Ardhi (Sulle 2012).
32.Sun BioFuels (
huyu alibadilisha jina na sasa inaitwa
30 Degree East). Shamba
lipo Kisarawe kwa kilimo cha Jatropha.
33.SyEnergy – hekta 30,000 za ardhi ya kijiji kwa ajili ya kilimo cha
mpunga – Kilombero (sulle 2012 interview
with District land Officer).
34. The New Forest company (NFC)(Uingereza na Afrika ya
Kusini). Hawa wana hekta 6,000 za ardhi huko Kilolo - Iringa kwa ajili ya upandaji miti kwa ajili ya mbao kupunguza hewa
ukaa (Chachage & Baha 2010) . Mchakato huu ulivihusisha vjiji 11, hata
hivyo mchakato wa kuhamisha ardhi kwa mwekezaji ulifanikiwa katika vijiji sita
( hekta 4800, mchakato ulifanyika 2009 ukihusisha vijiji vya Isele, Ukwega,Ipalamwa na Magome na
hekta 1,175 ukihusisha
vijiji vya Kisang’a na Iselemwaka
mwaka 2010 (Locher 2011). Mwekezaji anaendelea kupora ardhi ya wananchi, hali
iliyopelekea kuibuka kwa mgogoro mkubwa katika
kijiji cha Kidabaga na Kilawamo ambacho kinapinga ardhi yao kuchukuliwa
kimabavu pasipo wananchi kushirikishwa
wala kutoa ruksa!. Wananchi wamelazimishwa kutia sahihi nyaraka za fidia
kuonyesha kwamba wamehalalisha uporaji huo! Mwekezaji huyu anaendelea kuhodhi ardhi
kwa kununua rdhi kutoka kwa mwananchi mmoja mmoja katika vijiji husika(Locher
2010/2011).
35. TPC Ltd (CUEL Agro – Industry, Mauritius & Group
Quartier –France),
- Kampuni hii inahodhi hekta 15,000 za ardhi ya vijiji huko Moshi vijijini kwa
ajili ya kilimo cha miwa (uzalishaji wa sukari).Hata hivyo ni hekta 7,700 tu
zilizolimwa.
36.Vita Grain Ltd/GK Farm Ltd (RUBADA 2012- Sulle 2012 ) Kampuni
hizi zina hati ya Makubaliano (Memorandum Of Understanding) na RUBADA na mchakato ulikuwa katika hatua za mwisho,
mwaka 2012 (RUBADA 2012).
IX. MASHAMBA AMBAYO TAARIFA ZA
WAWEKEZAJI HAZIKO WAZI/HAZIELEWEKI
1.CHAWAGWA – hekta 200 za ardhi ya Kijiji[18], lipo
Kisarawe. Lilikuwa ni kwa ajili ya kilimo cha Jatropha lakini halijaendelezwa
2 . Euro Mine Export
Ltd – Kampuni
hii ina shamba Mikese- Morogoro kwa ajili ya kilimo cha Jatropha. Hali ya sasa
ya kampuni haijulikani (Sulle 2012)
3. Oxman Tanzania Ltd – Shamba lipo Rufiji, ni kwa ajili ya Kilimo cha Mpunga.
Halijaendelezwa[19]
4. RUBANA - Shamba lipo Mwanza, ni kwa ajili ya kilimco
cha Jatropha, ila halijulikani kwa
maafisa kilimo wa ardhi wa Wilaya[20]
5.SYNERGY Tanzania Ltd - Kampuni hii ina shamba la hekta 20,000 huko
Rufiji kwa ajili ya kilimo cha Mpunga [21]
6. Tanzania Biodiesel Plant – hekta 16,000 za shamb, lipo Bagamoyo, ( Halmashauri ya wilaya
iliidhinisha mwaka 2008[22] Mpaka Novemba 2012 Rais bado
alikuwa hajaibadilisha toka ardhi ya kijiji (village lands) kwenda general lands[23].
X. BAADHI YA
MAKAMPUNI AMBAYO YAMETELEKEZA MASHAMBA/YAMEACHA KUFANYA KAZI
1. African Green Oils Ltd Kampuni hii imetelekeza hekta 5,000ha[24] huko
Rufiji. Kwa sasa kampuni haifanyi kazi [25]
2.Bio diesel East Africa Ltd - Bahi, hekta 10000ha [26]zimetelekezwa.
3. Bio Massive – hekta 7500 zimetelekezwa huko Lindi Vijijini. Kampuni ilisitisha shughuli zake kutokana na
mtikisiko wa kiuchumi na mgomo wa
wanakijiji kutoa ardhi yao kwa
mwekezaji.[27]
4.Boleyn International (T) Ltd. Ilisajiliwa na Brela 2012 ila haifanyi kazi
kwa sasa.
5.CAMS AGRI-Energy Tanzania - Rufiji
6. Clean Power Tanzania - Bagamoyo
7.Donester - Bagamoyo
8.J &J group - Tabora Kaliua
9.JCJ
Co. Ltd- Mwanza, Mara,
Shinyanga ,Tabora
10.Kitomondo Ltd - Bagamoyo (Shamba la Makurange)
11.Safe Production Ltd - Rufiji.
12.Savannah Biofuels Ltd - Handeni
13.Savannah Biofuels Ltd. - Kongwa
14.Sekab Bioenergy Tanzania - Rufiji
15.Tanga
Forest(s) - Handeni
16. Tanga
Forest(s) - Mkinga
17.Tanga
Forest(s) - Pangani
XI. NTELIGENSIA
MBOVU YA KIUCHUMI
Mheshimiwa
Spika, kama ilivyojidhihirisha hapo juu wanaojiita au kutambulishwa kama wawekezaji,
ambao wametawaliwa la lugha tamu ,zilizojaa hadaa na matumaini makubwa, wengi
wao hawana mitaji au wamefilisika huko waliko toka,wakitarajia kutumia mtaji wa
ardhi ya Tanzania kwenda kutafuta/kukopa fedha nje. Na mbaya Zaidi , baadhi yao
badala ya kutumia mikopo kwa manufaa ya kuendeleza kilimo, wamekuwa na mtindo
wa kuzihamishia fedha kwenye miradi yao
mingine. Hali iliyopelekea miradi mingi kushindwa kuanza wakati tayari miliki
ya ardhi imeshapokwa toka kwa wanakijiji.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya upinzani inaitaka serikali, kurejesha
mashamba yote ambayo hayajaendelezwa/yametelekezwa chini ya miliki ya vijiji
vilivyoathirika .
Mheshimiwa Spika, wakati
taarifa
za kiuchunguzi naonyesha kwamba hakuna
uwiano wa miliki za mashamba makubwa kati ya wawekezaji wa nje na raia
ya watanzania, ripoti ya hivi karibuni
ya Kaimu Mkurugenzi wa kituo cha
uwekezaji Tanzania (TIC) Raymond Mbilinyi
wakati akitoa taarifa ya uwekezaji nchini, alisema kuwa Tanzania ina
hazina kubwa ya ardhi kwa shughuli za uwekezaji kwa kuwa mpaka sasa ni
wawekezaji 52 pekee ndio waliopewa hati ya kumiliki ardhi nchini,
akiwataka watanzania kuondokana na dhana
kwamba ardhi yao inaporwa! Alibainisha
hayo alipozungumza katika
kikao cha kikundi kazi kilichojadili
umuhimu wa kuwa na Bank ya ardhi nchini.
Alisisitiza kuwa kampuni za uwekezaji zinazokuja kuwekeza nchini
zinahitaji ardhi hivyo ni lazima
Tanzania kuweka mazingira kulingana na
hali ilivyo na kwenda na wakati[28].
Mheshimiwa Spika, hawa ndio
watendaji wa serikali ambao kutokana na kuzoea kufanyia kazi makaratasi hawana
uelewa wa kile kinachoendelea DUNIANI! Ni rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni kwa TIC kabla haijaendelea na utaratibu wake wa kupiga mnada ardhi ya
Tanzania, wafanye tathmini ya uendelezaji
wa ardhi ambayo mpaka sasa wamewapa wawekezaji. Inakadiriwa kwamba zaidi
ya hekta 640,000 zilitolewa kwa
kilimo cha mazao ya nishati pekee...ardhi ambayo ilipatikana kwa kuhawilisha ardhi ya vijiji . Mengi ya mashmba hayo
yameendelezwa kidogo au hayajaendelezwa kabisa!
XII. SHERIA
NO. 5 NA MUSTAKABALI WA TAIFA
Mheshimiwa Spika, katika
hotuba yetu ya Bajeti ya mwaka mwaka 2011/12, pamoja na mambo mengine
tuliieleza Serikali juu ya haja ya kuifanyia marekebisho sheria ya Sheria ya
Ardhi ya Kijiji ambayo inatoa mamlaka kwa Halmashauri ya kijiji kusimamia ardhi yote ya kijiji, na imepewa mamlaka ya
kugawa ardhi isiyozidi heka 50 baada ya kuruhusiwa na Mkutano Mkuu wa Kijiji.
Kambi ya upinzani ilitoa mapendekezo hayo kutokana na uchunguzi wa kitaalam
iliyoufanya na kugundua kwamba kutokana na kutokuwa na ufahamu mpana wa sheria,
watu wenye fedha wamekuwa wakitumia
fursa hii ya kisheria vibaya kwa kuwarubuni viongozi wa vijiji, na
hatimaye kugawa maeneo ya kijiji kwa watu wachache wenye fedha /ushawishi wa
kisiasa, huku ikiwaacha wanakijiji bila
ardhi kinyume na matakwa ya kisheria.
Mheshimiwa Spika,hali inakuwa
mbaya zaidi pale ambapo watu ambao sio watanzania wanatumia upenyo huu wa
kisheria ,na kumilikishwa maeneo makubwa ya kijiji kinyemela! Hakuna ubishi kwamba kuna wageni
wengi waliopata maeneo ya vijiji
kinyemela kwa kutumia upenyo huo ,wakati sheria ya Ardhi No.4 , kifungu na 20 kinakataza
wageni kumiliki ardhi nchini isipokuwa kwa malengo ya uwekezaji tu, na ambao
umiliki wake lazima upitie Kituo cha uwekezaji Tanzania na si vinginevyo.
Mhesimiwa Spika,kama ilivyo
kawaida,maoni ya Kambi ya Upinzani yalipuuzwa...miaka mitatu baadae utafiti wa
chombo kilichopewa kazi na serikali kufanya tathmini ya ardhi nchini, pamoja na
watafiti wengine wamethibitisha kile ambacho Kambi ya Upinzani ilikisema, kwa
vielelezo zaidi ya miaka mitatu iliyopita!
Kambi Rasmi Upinzani
Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inaitaka
serikali ilieleze Bunge hili tukufu...ni
lini sheria hii itafanyiwa mabadiliko? Aidha, ni lini serikali itawanyang’anya
ardhi watu wote (watanzania na wageni) ambao wamemilikishwa ardhi za vijiji
kinyume na sheria ya ardhi namba 4 na 5 ya mwaka 1999?.
XIII. UKOMO WA ARDHI KWA WAWEKEZAJI WA
KILIMO- MKANGANYIKO NA KAULI ZA SERIKALI .
Mheshimiwa Spika, tarehe 28/11/2012 (Kufuatia hoja binafsi ya
Ardhi Bungeni tarehe 8/11/2012) Serikali
ilitangaza ukomo wa ardhi kwa wawekezaji kwenye sekta ya kilimo nchini, ambao
utakuwa kati ya hekta 5,000 hadi 10,000 ili kutoa nafasi kwa wawekezaji wengi
na kuongeza ushindani katika sekta hiyo.
Serikali pia imeweka masharti kwa kila mwekezaji anayekuja nchini, kulazimika kumsaidia mkulima mdogo katika uwekezaji, ili kumwinua kiuchumi na kumfanya awe sehemu ya uwekezaji huo.
Serikali pia imeweka masharti kwa kila mwekezaji anayekuja nchini, kulazimika kumsaidia mkulima mdogo katika uwekezaji, ili kumwinua kiuchumi na kumfanya awe sehemu ya uwekezaji huo.
Mheshimiwa Spika, kauli hiyo ilitolewa na Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano
maalumu wa wadau wenye ari ya kuwekeza katika sekta ya kilimo kupitia Mpango wa
Ukuzaji wa Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
Waziri Mkuu alisisitiza kwamba si busara kwa Serikali kutoa eneo kubwa la zaidi ya hekta 60,000 au 100,000 kwa mwekezaji na badala yake, uwepo ukomo wa ardhi.
“Moja ya mambo ambayo ni ya msingi ni hili la kupunguza ukubwa wa eneo kwa mwekezaji, kwa mfano kama mwekezaji wa mpunga, tumeona hekta 5,000 ni nyingi kuzimaliza mapema, zinamtosha hivyo tunaanza na kiasi hicho,”
Waziri Mkuu alisisitiza kwamba si busara kwa Serikali kutoa eneo kubwa la zaidi ya hekta 60,000 au 100,000 kwa mwekezaji na badala yake, uwepo ukomo wa ardhi.
“Moja ya mambo ambayo ni ya msingi ni hili la kupunguza ukubwa wa eneo kwa mwekezaji, kwa mfano kama mwekezaji wa mpunga, tumeona hekta 5,000 ni nyingi kuzimaliza mapema, zinamtosha hivyo tunaanza na kiasi hicho,”
Mheshimiwa Spika, Waziri Mkuu alisema uchunguzi wa Serikali umebaini kuwa
wawekezaji wenye maeneo makubwa hawajayafanyia kazi na hivyo kuwanyima nafasi
wengine na kuongeza kuwa kwa upande wa mashamba ya sukari, hekta 10,000 zinatosha
kuanzia.
Mheshimiwa
Spika, wakati Waziri Mkuu akitoa
taarifa juu ya ukomo wa ardhi kwa wawekezaji, Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais , Mahusiano na Uratibu, Mheshimiwa Stephen Wassira (Mb)
akiwasilisha katika Kamati ya Bunge
Mapendekezo ya mpango wa maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2013/14 (Ofisi ya rais Tume ya
Mipango, Machi 2013[29] alisema katika
kuendeleza kilimo cha ‘miwa’ kwa mwaka 2012/13 , mashamba kwa ajili ya uwekezaji katika mabonde ya Wami, Ruvu,Kagera,kilombero na Malagarasi
kiasi cha Hekta 277,000 yametambuliwa na uhakiki wake unaendelea
kwa ajili ya kuwezesha uwekezaji
. Wawekezaji walioonesha nia ni:- Kampuni ya Ecoenergy[30] (Bonde la Ruvu-
hekta 20,000); Agroforestry (Muhoro Rufiji- hekta
20,000). Wawekezaji
hawa wanatarajia kushirikiana na ‘wakulima
wadogo’ (rejea taarifa ya tathmini ya ardhi juu ya nafasi ya wazawa katika
kuhodhi ardhi). Aidha shamba la ukubwa
wa hekta 50,000 katika eneo la Mkulazi (Morogoro) limepatikana na utafiti wa maji unaendelea!
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kupitia waziri wa ardhi
,ilieleze Bunge lako tukufu, utekelezaji wa kauli ya Waziri Mkuu juu ya ukomo
wa ukomo wa ardhi ya kilimo kwa wawekezaji unaanza lini? Mipango na kauli za
waziri Mkuu zina uhusiano na Mpango wa Taifa wa
Taifa wa miaka mitano kama ulivyowasilishwa na Mhe. Wassira au kila mtu
ana jipangia mipango yake kwa kadiri atakavyoona inafaa? Kauli ipi hasa ni
msimamo wa serikali: Kauli ya Waziri Mkuu au kauli ya Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais – Mahusiano na Uratibu?
XIV. UPANGAJI
WA MATUMIZI YA ARDHI
Mheshimiwa Spika,
katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia migogoro ya
ardhi isiyokwisha. Migogoro ikiwahusisha wakulima na wafugani, vijiji na vijiji
, wawekezaji na wananchi wenyeji n.k . Migogoro hii mara nyingi inachangiwa na
serikali ya CCM kutokuwa na mipango thabiti ya matumizi bora ya ardhi.
Mheshimiwa
Spika, miaka 52 baada ya uhuru, Wizara
imeandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji takriban 1,300
tu (sawa na asilimia 11 ya vijiji vyote nchini) kati ya vijiji 12,000. Hadi
mwaka 2011 kwa upande wa mijini, miji
mikuu ya mkoa , yenye mipango ya uendelezaji (master plans) iliyo hai ilikuwa
10 tu kati ya miji 25. Miji mikuu ya
wilaya yenye mipango ya matumizi ya ardhi ni 20 kati ya miji zaidi ya 110, na
miji midogo yenye mipango ni 25 tui kati ya miji 95 !Mwisho lakini nsio kwa umuhimu....miaka
52 baada ya uhuru viwanja
vilivyopimwa ni laki tisa na tisini na
tano elfu tu ( 995,000).
Mheshimiwa Spika, kwa kasi hii ,
hatutaweza kumaliza squatters, hatutaweza kumaliza migogoro ya ardhi ambayo imekuwa donda ndugu
katika Taifa hili...donda ambalo halina dalili yoyote ya kupata tiba !!! Kwa
kuonyesha ni kwa kiwango gani serikali haina mpango kabisa wa kuhakikisha
vijiji vinakuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi ,sambamba na kuhakikisha
kwamba kasi ya upimaji wa ardhi inaongezeka, serikali imekuwa na mkono wa
birika katika kutenga fedha mahsusi kwa
ajili ya upimaji wa viwanja hususan kuwezesha ujenzi wa kituo cha satelite
ambacho kingekuwa mhimili wa kupima
viwanja haraka na kwa njia ya kisasa!
Mheshimiwa Spika, kwa miaka
miwili mfululizo (mwaka 2010/11 (bilioni 3), 2011/12 (bilioni 4)) Bunge lako
tukufu limekuwa likitenga fedha imekuwa
ikitenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo husika, lakini ama kwa dharau ama
kwa kutokuona umuhimu wizara ya fedha
(hazina) wamekuwa wagumu kutoa fedha....na kwa taarifa iliyonayo Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, mwaka huu hakuna fedha iliyotengwa kwa ajili ya kupima viwanja !
Mheshimiwa Spika,taarifa za
kitaalam zinaonyesha kwamba kama wizara wangepewa shilingi bilioni 12 tu,
wangeweza kupima viwanja visivyopungua milioni 5. Ni rai yangu kwa wabunge, tunaokabiliwa na
changamoto ya migogoro ya ardhi inayotishia amani na ustawi wa nchi
yetu,tuungane kwa pamoja kuhakikisha kwamba kwa mwaka huu wa fedha zinapatikana
fedha kwa ajili ya maandalizi ujenzi wa kituo cha satelite, na fedha kwa ajili
ya upimaji viwanja.
XV. VIONGOZI
WA CCM NA UJAMBAZI WA ARDHI
Mheshimiwa Spika, dhuluma hii
inalihusisha shamba namba 24 Lorkisalie
( OLDUPAI SEED CO. LTD) ,lililopo Wilayani Simanjiro, Jimbo la Simanjiro ,
Kitongoji cha Lemooti, Kijiji cha
Loiborsoit A.
Kwa mujibu wa
barua ya ofisi ya Msajili wa Hati Kanda
ya Kaskazini- Moshi ya tarehe 1/3/2010 yenye kumbukumbu namba
LR/MS/T/1127 4/15 inaonyesha kwamba
shamba husika lilisajiliwa tarehe
28/11/1994 na kupewa hati namba 11274.
Mheshimiwa Spika, mhusika mkuu
katika mgogoro huu ni bwana Brown Mathew Oleseya, Mwenyekiti wa CCM Wilaya
ya Simanjiro, ambaye amejimilikisha kiujanja-ujanja hekta za kijiji 3,425 ambazo ni sawa na ekari
8,562.5. Licha ya kujipatia eneo husika
kimizengwe, Mheshimiwa huyu wa Chama Tawala
amefungia wananchi njia zote za
chemchem za maji na malisho ya mifugo.
Mheshimiwa Spika, barua yake ya
maombi ya shamba ya tarehe 14/4/1978 ,
yenye kumb Na:PF/MI/40 inaonyesha kwamba
aliomba eneo tofauti
na analolitumia kwa sasa. Barua inaonyesha aliomba eneo la LESHUTA,
ambayo ipo katika kijiji cha Engonongoi Kata ya Terat na Shamba
’analolimiliki’ kwa sasa lipo
eneo la LEMOOTI kijiji cha Loiborsait A.
Mheshimiwa Spika, muhtasari wa
kikao cha kamati ya maendeleo ya Kata kilichoketi tarehe 26/4/1978.
kilichohudhuriwa na wajumbe 19 kinachosemekana kilimpatia Mwenyekiti huyu wa
CCM Ardhi (ekari 5000, ekari 2000 za kulima na 3000 kwa ajili ya mifugo ),
haujaidhinishwa na mamlaka yoyote na
hakuna muhuri wala sahihi ya Mwenyekiti , Katibu wala wajumbe. Barua pekee yenye sahihi, bila muhuri
wowote ni ya Katibu Kata ya tarehe
26/4/1978 ikimtaarifu kwamba amepewa shamba husika.
Mheshimiwa Spika, Kamati ya
Ushauri wa ardhi ya Wilaya ya Kiteto Ilioketi
tarehe 16 Januari 1979 iliyohudhuriwa
pia na na Mwenyekiti wa CCM wa wilaya kipindi hicho , Ndugu Ole Kone na katibu wa
CCM (W) ,ndugu P.Bura , pamoja na mambo mengine
walijadili maombi ya mashamba , yaliyopitishwa na ngazi ya Kata pamoja
na shamba la Bwana Brown Mathew Ole
Suya. Kikao husika kiliamua kwamba
katika ekari 5000 zilizoombwa , eka 2000
za kilimo atazitumia kwa miaka 5 kisha zirejeshwe kijijini, na ekari 3,000
apewe lease ya miaka 33. Lakini asiingilie
Hifadhi , sehemu ya jeshi na wilaya ya Monduli. Kama ilivyo nyaraka
zilizotangulia Muhtasari wa kikao husika,hakikuwa na sahihi ya Mwenyekiti wala
Katibu!
Mheshimiwa Spika, licha ya
kwamba nyaraka husika (anazozitumia kiongozi huyu kama ushahidi wa kupewa
shamba) hazina uhalali wowote kisheria , kwa mujibu wa makabidhiano ya ardhi
husika,kama ilivyoamauliwa na kamati ya ardhi ya Wilaya, Bwana Brown alitakiwa arejeshe ardhi ya kijiji( ekari 2000 za kilimo)
mwaka 1985, na ardhi ya mifugo (ekari
3000 kwa ajili ya malisho ) mwaka 2011! Mwaka 1985, shamba la kijiji halikurudishwa (ekari 2000), mwaka 1991 kada huyu aliendelea
kupora ardhi ya kijiji kwa kuongeza ukubwa wa eneo lake kutoka!
Hekta 2000 za awali mpaka hekta 3,425 (Ekari 8,000)!, ambayo ni hekta 1425
zaidi ya kiasi ’alichopewa’. Eneo hilo
jipya liliingia kwenye kijiji cha Lolksale
wilaya ya Monduli !
Mheshimiwa Spika, kada huyu wa CCM, licha
ya kutokuwa mmiliki halali wa eneo husika ,tarehe 31/8/ 2009 kwa kushirikiana na watumishi wa serikali
wasio waaminifu walibadilisha matumizi
ya shamba kutoka kilimo na ufugaji
na kuwa Hifadhi ya kitalii.[31]
Uhalali wa Kubadilisha Matumizi ya Ardhi na Mwenye
Mamlaka ya Kubadilisha Matumizi
Mheshimiwa Spika, Kanuni na na taratibu
za kubadilisha matumizi hazikufuatwa:
i)
Bango kwa lengo la
kukusanya maoni ya wananchi majirani kuhusu
nia ya mmiliki kutaka kuongeza
matumizi kama inavyotakiwa kwenye
waraka wa kitaalam Na.1 wa mwaka 2006
ii)
Kibali cha Mkurugenzi wa mipango Miji na vijiji kama inavyotakiwa kwenye Sheria ya Mipango miji Na.8
ya mwaka 2007 kifungu 32(1) na
6(3)
iii)
Kibali cha nyongeza ya matumizi katika Miliki ( Land Form
na. 28) kimetolewa na kusainiwa Paulo E .Kibona ambaye hana mamlaka kisheria kusaini Fomu hiyo. Fomu hiyo
husainiwa na Kamishna wa ardhi kwa mujibu wa sheria ya ardhi na.4 ,1999 kifungu
35(4)
Nyaraka
ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani inazo zinaonyesha
kwamba Wizara ya Ardhi, kupitia kwa
Kamishna Msaidizi Kanda ya Kaskazini kwa barua yenye kumbukumbu Na. LD
/NZ/6014/22/DW ya tarehe 22/09/2010
ilimtaka arejeshe hati iliyoofanyiwa mabadiliko ya matumizi....lakini
alipuuza amri ya mamlaka halali! Hali iliyoilazimu Kamishna
msaidizi kuandaa hati ya marekebisho
ya mabadiliko ya matumizi (deed of rectification) na kuiwasilisha kwa
Msajili wa hati msaidizi kanda ya Moshi ili afanye marekebisho kwenye
daftari lake .
Marekebisho yalifanyika tarehe 26/01/2011 na kusajiliwa kwenye FD.
No. 29828 ambapo matumizi kwenye
hati yalitakiwa yabaki yale ya awali (japokuwa hakuwa na uhalali wowote
wa
umiliki)
Mheshimiwa Spika, licha ya kuwa
na uelewa wa mgogoro husika bado Kada
huyu wa CCM aliuza eneo husika (ardhi ya
kijiji) kwa raia wa kigeni , mmiliki wa Kampuni
Maasai steppe Conservancy limited mnamo tarehe 14/12/2010.
Kwa mujibu wa Taarifa za BRELLA , kampuni ya Maasai
Steppe Conservancy limited ina jumla ya hisa 10,000, kama ilivyoainishwa hapa chini:
i)
BCZV Holdings limited
ni kampuni inayomilikiwa na
Baastian bruins 9Mdachi) na Jerome Bruins (Mdachi) wana hisa 9700
ii)
John warren (Mwingereza ) ana hisa
100
iii)
Brown Mathew Ole suya ( Mtanzania)
ana hisa 200.
Kutokana na hisa nyingi ( 9800) za
kampuni ya Maasai Steppe Conservancy kumilikiwa na wageni ni dhahiri
kwamba kampuni hiyo ni ya kigeni.
Kwa mujibu wa sheria ya ardhi Na.
4 ya mwaka 1999, fungu la 20 : Kampuni
/raia wa kigeni kabla ya kumiliki
ardhi wanatakiwa wapate kibali
( Cerificate of incentives) kutoka TIC. Utaratibu huu haukufuatwa!
Wakati nchi inakabiliwa na changamoto kubwa ya ardhi kumilikiwa na wageni!
Kada/kiongozi wa chama cha mapinduzi
amegeuka kuwadi namba moja wa kuuza nchi
kwa wageni! Waziri wa ardhi ana taarifa zote kuhusiana na uvunjwaji huu
wa sharia kuanzia na uporaji wa wa eneo la kijiji, kubadilishwa kwa matumizi ya
ardhi pasipo kufuata sharia na taratibu na kuuza ardhi kwa raia wa kigeni
kinyume na sharia za nchi! Waziri aliahiidi kwenda kulishughulikia toka mwaka 2011 mpaka sasa hajatia mguu.
Kambi ya upinzani inataka kupata majibu ya maswali
yafuatayo:
I)
Wizara ya ardhi ilitumia vigezo gani kumpatia hati?
II)
Wizara ilitoaje uhalali wa kubadilisha matumizi ya ardhi
III)
Wizara imeafiki vipi wa umiliki wa ardhi kwa raia wa kigeni (Mdachi)
IV)
Hatua gani zitachukuliwa kwa kada huyu wa CCM kwa kukiibia kijiji na watanzania ardhi yao na kwa kuvunja
sheria?
XVI. UVAMIZI
WA MAENEO YA WAZI MKOA WA DAR ES SALAAM
Mheshimiwa Spika, Rais,
Mheshimiwa
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete wakati
akifanya majumuisho ya ukaguzi wa hali ya maji katika mkoa wa Dar es
salaam tarehe 24 Mei, 2010 alitoa hoja ya kuvamiwa kwa maeneo mengi
ya wazi katika Mkoa wa Dar es
salaam,ambapo alilalamikia baadhi ya Madiwani kuhusika na uvamizi huo.
Halikadhalika aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. William Lukuvi,
alipotembelea Manispaa ya Kinondoni tarehe 15 Juni 2010 alibaini mapungufu husika hali
iliyopelekea kuunda kamati
maalum ya kuchunguza maeneo yote
ya wazi yaliyovamiwa katika Mkoa wa Dar es salaam. Kamati ambayo
iliundwa tarehe 18 Juni, 2010 lengo la kazi
likiwa ni kuchunguza maeneo ya
wazi yaliyomo katika Jiji la Dar es salaam, ambayo yamevamiwa, kuendelezwa au kuuzwa
kinyume na taratibu za mipango miji. Kamati ambayo ilikamilisha kazi
yake tarehe 13/7/2010 (taarifa ya Kamati
husika,pamoja na mapendekezo tunayo).
Mheshimiwa Spika,Kambi ya upinzani inaitaka serikali itueleze, baada
ya miaka 4 kupita tokea Kamati husika
imalize kazi yake;
1)
Ni hatua gani
zimeshachukuliwa ili kuyarudisha maeneo husika?
2)
Ni maeneo mangapi
kati ya yaliyobainishwa yamesharudishwa?
3)
Ni Hatua gani
zimechukuliwa dhidi ya maafisa waliohusika na ubadhirifu huu na kwa kiwango
gani?
4)
Ni lini serikali inatarajia kukamilisha
utekelezaji wa mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati husika?
5)
Je serikali itakuwa tayari kuvunja majumba makubwa makubwa
ya watu wenye fedha waliouziwa maeneo ya wazi kinyume na utaratibu na kupewa hati na maafisa wasio waaminifu ?
6)
Serikali inatoa tamko
gani juu ya Kiwanja namba 856
Msasani beach, ambacho kwa mujibu wa Ramani ya
upimaji iliyosajiliwa namba 29331
ilikuwa ni kwa matumzi ya wazi, lakini baadae
kilimilikishwa kwa mtu binafsi. Matokeo yake njia ya mkondo wa maji kuelekea baharini imezibwa,na mvua ikinyesha
maeneo ya kwa Warioba, mpaka njia panda ya kuelekea Clouds FM yanajaa maji.
7)
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi
ya Upinzani inaitaka serikali itoe
maelezo kuhusiana na viwanja
namba 9 & 10 Kitalu ’S’ Tabata Segerea. Mgogoro huu ni wa muda mrefu sana,
Waziri wa Ardhi anayo taarifa. Barua ya mwisho kwa waziri iliandikwa tarehe 2/5/2013 ,ilikuwa na viambatanisho
kumi. Viwanja husika vilivyotengwa mahsusi kwa matumizi ya Umma (soko).
Tume ya Ardhi iliyoundwa tarehe 23/9/2008 kuchunguza mgogoro husika ilibaini kwamba viwanja husika vilimilikishwa
kimakosa kwa Walter
Camilius na Rose Samwel Binagi.
8)
Kambi Rasmi ya Upinzani
bungeni, inataka Serikali itoe maelezo
juu eneo la wazi la Kitalu D, Registered Plan namba
8750, mtaa wa Mikumi na
Makongoro, Magomeni , lango la JIJI , ambalo licha wa maelekezo na kauli mbali
mbali za serikali,bado linaendelea kuendelezwa!
XVII. SHIRIKA
LA NYUMBA LA TAIFA
SERIKALI NA TAASISI ZAKE KUTOLIPA KODI ZA PANGO
KWA WAKATI
Mheshimiwa Spika, ’Katika
kipindi
cha Julai 2011 shirika lilikusanya kodi
za pango pamoja na malimbikizo
kiasi cha shilingi bilioni 31.Pamoja na na jitihada za kukusanya
kodi na malimbikizo na hasa yale yanayodaiwa serikali na taasisi zake,
malimbikizo bado ni
makubwa . Hadi machi 2011, Serikali
na taasisi zake ilikuwa
ikidaiwa kiasi cha shilingi bilioni 1.543, baada ya kupunguza
malimbikizo kwa kiasi cha shilingi
milioni 115 ,sawa na asilimia 8 tu!’ hii ilikuwa hotuba yetu
ya mwaka 2011...miaka mitatu baadae taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya wizara
katika mwaka 2012/13 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2013/14 kwa
kamati ya kudumu ya Bunge ardhi , maliasili na mazingira inaonyesha kwamba madeni[32] ya serikali na taasisi zake
yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 2.8 mwaka 2011/12 mpaka bilioni 3.4 mwezi Februari 2013!
Kambi ya upinzani
inataka serikali ieleze ni kwa nini
imekuwa ni mdaiwa sugu , na kwa nini
hailipi madeni ya shirika la nyumba?
XVIII. MIKOPO
YA UNUNUZI NA UJENZI WA NYUMBA
Mheshimiwa Spika,Pamoja na
kuwepo kwa sheria ya Mikopo ya nyumba
(Mortgage Financing Act) ya mwaka
2008 na sheria ya umiliki wa
sehemu ya majengo ( Unit Titles Act)
ya mwaka 2008, masharti ya mikopo hii
bado ni magumu. Mfano, kwa sasa benki
zanazotoa mikopo ya nyumba masharti yake ni pamoja na muda wa marejesho ya kati
ya miaka 6 mpaka 15 na riba kati ya asilimia 17 mpaka 22 kwa mwaka .
Mheshimiwa Spika, Iwapo hali hii haitabadilika , itakuwa vigumu kwa
wananchi , halikadhalika shirika letu la
nyumba kujenga nyumba za gharama
nafuu na kwa wananchi walio
wengi kuweza kumudu mikopo
ya ununuzi wa nyumba.
XIX. SERIKALI
KUVUNJA AHADI YA KUWAUZIA NYUMBA (KWA BEI NAFUU) WAPANAGAJI WA SHIRIKA LA
NYUMBA KINYEMELA.
Mheshimiwa Spika, Serikali, tangu mwaka 1996, ilpitisha
maamuzi ya kuliruhusu Shirika la Nyumba kuwauzia wapangaji wake nyumba za
gharama ndogo na gharama ya kati zilizojengwa na Shrika lenyewe. Hata hivyo,
nyumba zilizotaifishwa hazihusiki na uamuzi huu.
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2008,
Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa Ziarani Manispaa ya Iringa kuzindua
majengo ya SNT/NHC (Agosti, 07 2008) alikazia uamuzi wa Serikali kwa
kusema ”Sheria ya Mikopo ya Nyumba
inatarajiwa kuwasilishwa Bungeni Oktoba mwaka huu, ambapo ikipitishwa,
itawezesha Watanzania wanaoishi kwenye nyumba za Shirika la Taifa, kununua nyumba
hizo” Rais aliongeza kuwa ”MTU HAWEZI
KUISHI NDANI YA NYUMBA ZA NHC KWA MIAKA 30 BILA KUFAIDIKA”.
Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko
makubwa, Sheria ilitungwa lakini Serikali imeamua kubadili mwelekeo kimyakimya.
Serikali imesema kwamba jukumu la msingi la Shirika la Nyumba litakuwa ni
kufanya bishara ya kujenga na kuuza nyumba badala ya jukumu la sasa la
kupangisha nyumba na kukusanya kodi kwa mwezi. Hata hivyo, bei ya nyumba
inazingatia bei ya soko la sasa hivi ambapo gharama ni kubwa sana na kihalisia
hakuna mtanzania masikini anayeweza kununua nyumba hizo.
Kwa mfano: UNUNUZI WA NYUMBA UBUNGO KN 242/1-242/12
BEI YA UNUNUZI BILA VAT TSHS 67,946,567.86
VAT 18%
TSHS 12, 230,382.21
BEI YA UNUNUZI PAMOJA NA VAT TSHS. 80,176,950.07
RIBA YA BENKI 18% TSHS. 144,318,510.234
MUDA WA KULIPA NI MIAKA 15
TSHS 800,000 KWA MWEZI XMIAKA 15 =
144,000,0000
MAJI TAKA 3000X48 DEPARTMENT BLOC 1 =TSHS. 144,000
BLOCK 9X 144,000 BLOCK 9= MWEZI TSHS. 1,296,000
KWA MWAKA TSHS. 15,552,000
PARKING – HAKUNA
VIWANJA VYA MICHEZO – HAKUNA
Mheshimiwa Spika, kwa hali
hiyo, ni mtanzania gani ataweza kununua nyumba ya Shirika la Nyumba la Taifa?
Hakika huu ni ubaguzi mkubwa kwa kuwa sasa hivi wenye uwezo ambao wengi ni
wageni (wahindi, wachina na wazungu) ndio wameanza kujaa katika nyumba hizo.
Haki ya Mtanzania iko wapi?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi
ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa kauli mbele ya bunge hili leo hii kama bado
ina mpango wa kuwauzia nyummba za bei nafuu wapangaji wa shirika la nyumba la
taifa. Aidha, Kambi ya upinzani , inaitaka Serikali itueleze ni
kwa namna gani imejipanga kuweza kutatua tatizo hili ! Lazima
Serikali iweke Mazingira ya kuziwezesha Benki kutoa mikopo yenye
masharti nafuu kwa wawekezaji na wanunuzi wa nyumba.!!!!
XX. KODI YA
ONGEZEKO LA THAMANI (VAT) NA
ONGEZEKO LA MTAJI (CAPITAL GAIN
TAX) KWENYE MAUZO YA NYUMBA ZINAZOJENGWA NA SHIRIKA
Mheshimiwa Spika, Shirika la
Nyumba la Taifa, lilipoanzishwa mwaka
1962 , moja kati malengo yake ilikuwa ni
kujenga nyumba nafuu kwa ajili ya watanzania
wafanyao kazi mijini . Hata hivyo
kwa kadiri siku zilivyosonga mbele, Shirika hili liligeuka kutoka
kuwahudumia masikini na watu wenye kipato cha kati na badala yake kuwahudumia
watu wa kipato cha juu.
Mheshimiwa Spika, kodi
ambazo Shirika hulipa
pale linapouza nyumba: Uwepo wa
kodi hizi huzifanya nyumba zinazojengwa na shirika kuwa ghali na hivyo
zisiweze kushindana kwenye soko
na kuwa mzigo mkubwa sana kwa wananchi wanaotaka kununua nyumba . Mfano
dhahiri, kwa mwaka wa fedha 2010/11 shirika lilitarajia kujenga nyumba 49 , zenye jumla ya
thamani ya shilingi bilioni
4.08. Kwa gharama iliyotumika, wastani
wa nyumba moja ililigharimu shirika shilingi milioni 83.4,
Mheshimiwa Spika,kwa mujibu wa
Taarifa ya utekelezaji wa Kazi za Shirika la Nyumba la Taifa kuanzia Julai 2010 hadi Mei 2011 wanatarajia
kupata shilingi bilioni 6.3 kutokana na mauzo ya nyumba hizo , yaani faida ya shilingi bilioni
1.9
Kwa tafsiri nyingine nyumba moja itauzwa na shirika la nyumba kwa
shilingi milioni 129.2, wakati
gharama halisi za ujenzi ni shilingi milioni 83. Kwa kila nyumba iliyounzwa
shirika limepata faida ya shilingi milioni
46.
Mheshimiwa Spika, Kwa hali hii,
inawezekana kweli Shirika hili kujenga nyumba kwa ajili ya wananchi wa
kawaida ,kuweza kumudu? Kama kweli
tatizo ni kodi la ongezeko la thamani na
kodi ya ongezeko la mtaji, serikali haioni kwamba ina wajibu wa kuondoa hizi kero ili shirika
lifanye kazi kwa maslahi ya wengi, na sio kwa maslahi ya wachache?
XXI. KODI KWA VIFAA VYA UJENZI
Mheshiwa Spika,gharama za vifaa vya ujenzi imekuwa ni kero kubwa sana
kwa wananchi wengi, tumekuwa
tukilizungumzia hili kwa kipindi kirefu sasa na serikali imekuwa ikiahidi
kulitafutia ufumbuzi ili kuwapungumzia
raia wake mzigo katika ujenzi wa nyumba..ili hatimaye makazi na
nyumba za wananchi wetu ziakisi maendeleo na mafanikio yanayotokea nchini na kuondokana kabisa na nyumba za matope, fito
na nyasi ifikapo 2020.
Mheshimiwa Spika ,Kambi ya upinzani inaitaka serikali
ilieleze Bunge lako tukufu ni lini kodi
katika vifaa vya ujenzi wa nyumba kama saruji, mabati, nondo nk. itaondolewa ili kuweza kufanikisha dhamira
hii?
XXII. KODI ZA
PANGO
Mheshimiwa Spika, eneo lingine
ambalo ni kero ,ni kodi za nyumba. Kila
mwenye nyumba katika nchi hii amekuwa akijipangia kodi , kwa kadiri atakavyoona
inafaa. Ni kwa bahati mbaya sana wamiliki wa nyumba licha ya kupata mapato (ya kibiashara),hawalipi
kodi serikalini. Kambi ya upinzani imelizungumza hili kwa kipindi kirefu sana,
hivyo tunaitaka Serikali ianzishe Taasisi itakayosimamia na kudhibiti kodi za
pango la nyumba ambazo hivi sasa ni kubwa mno! zinatozwa kwa mwaka mzima, hivyo kuwatesa
wapangaji husan wa kipato cha chini.
XXIII. UENDELEZAJI MAJENGO MIJINI
Mheshimiwa spika, yamekuwepo
matukio ya kujirudia ya kuanguka kwa majengo ya maghorofa
yaliyokamilika na yanayoendelea kujengwa
katika jiji la Dar es salaam, na
tukio la hivi karibuni jengo
lililokuwa linaendelea kujengwa katikati ya jiji la Dar es salaam, mtaa wa Indira Ghandi,kiwanja
namba 2032/73 na kupoteza maisha ya
watanzania wasiopungua 36. Kambi ya upinzani inasikitishwa kwa tukio hilo ambalo lingeweza kuzuilika
iwapo mkandarasi angezikatia kanuni za usalama, halikadhalika kama mamlaka
zenye jukumu ya kusimamia sekta hii ya ujenzi zingetekeleza wajibu wao
ipasavyo!
Mheshimiwa Spika, kama ilivyo
kawaida yetu , pale ambapo panatokea tatizo watu wenye dhamana ya kutafuta
mbinu za kutatua matatizo wamekuwa ni mabingwa ya kujificha kwenye vivuli vyao!
Mheshimiwa spika,
hakuna ubisihi
kwamba Waziri pekee aliyeonekana japo kuguswa kilichotokea na hata kutoa
maelekezo ya kiutendaji kwa mamlaka za chini kwa utekelezaji ni waziri
wa
ArdhiM(japokuwa mpaka sasa kauli yake haijafanyiwa kazi) mawaziri
wengine
walidiriki, kukana mbele ya Bunge lako tukufu ( akiwemo waziri wa
Ujenzi,
Mhe.John Pombe Magufuli wakati akijibu hoja za wabunge ,wakati wa wa
mawasilisho ya Bajeti ya wizara ya Ujenzi na wengine walikuja
kuchungulia
kwenye kamati ya ardhi na maliasili,walipopewa maelekezo ya nini
wanatakiwa
walete kwenye kamati,waliingia mitini – Mhe Aggrey Mwanri, naibu waziri
TAMISEMI) huku kiti cha Spika kikiwalinda kwamba hawahusiki kwa namna
yoyote,na hoja zote za wabunge zikatupiwa kapuni!
Mheshimiwa Spika, ni muhimu
Bunge lako tukufu likaelewa kwamba kuna mamlaka zaidi ya moja katika suala zima
la uendelezaji wa majengo mjini. Ni muhimu mamlaka zote hizi zielewe wajibu
wake,na ziwajibike ipasavyo kwa mema na mabaya!Katika sakata hili,wizara
zifuatazo haziwezi kukwepa uwajibikaji:
1) Wizara ya
Ardhi
2) Ofisi ya
Waziri Mkuu (TAMISEMI)
3) Wizara ya
Ujenzi na
4) Wiza ya Kazi
na Ajira
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa
sheria ya mipango miji , No.8 ya mwaka
2007,Wizara ya ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi ina jukumu
la kusimamia upangaji na uendelezaji wa maeneo ya mjini(Kisera).
Mheshimiwa Spika,
Mamlaka
zinazohusika na kutekeleza sheria ya Mipango Miji , namba 8 ya mwaka
2007 ni Halmashauri za Jiji, Miji na Wilaya pamoja na kampuni au
taasisi yeyote itakayopewa
hadhi ya kuwa mpangaji . Sheria ya serikali za mitaa( Local government
Act
number 3 of 1982)inazipa mamlaka
halmashauri zote nchini kuandaa mipango
ya uendelezaji maeneo yaliyomo kwenye
eneo lililotangazwa kuwa la upangaji
kisheria (kulingana na sheria ya mipango miji
namba 8 ya 2007).
Mheshimiwa spika, kimsingi
usimamizi wa uendelezaji wa majengo
mijini uapaswa kusimamiwa chini ya
wizara ya Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (TAMISEMI).Maeneo muhimu
yanayosimamiwa na Halmashauri ili kuhakikisha majengo yanayopjengwa yanakuwa
katika ubora stahiki ni pamoja na:
i)
kukagua ramani zinazowasilishwa kwao kutumia wataalam mbali
mbali,
ii)
kutoa vibali kwa
waombaji ambao ramani zao zimebuniwa na kampuni zilizosajiliwa ,
iii)
kufanya ukaguzi wa majengo kwa kutumia timu ya wakaguzi wa majengo ili kubaini kama majengo yanayojengwa kwa kufuata sheria,
iv)
Kukagua na
kujiridhisha kama wajenzi wanaojenga
ndani ya Halmashauri wamesajiliwa na Bodi husika !
Mheshimiwa Spika, Wizara
ya
Ujenzi inawajibIka kwa kupitia vyombo mbali mbali ambavyo viko chini
yake,
ambavyo kisheria vinawajibuka katikasuala zima la usimamizi wa majengo:
Bodi ya
wabunifu wa majengo na wakadiriaji Majenzi
ni mamlaka iliyoanzishwa na
sheria Na. 16/1997 ( the Architects and Quality
Surveyors (Registration) Act { Cap. 269 R.E 2002) na mwaka 2010. Fungu
la 4 la sheria hii linaweka majukumu kuwa ni pamoja na :
i)
Kusimamia shughuli na utendaji kazi wa wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi , pamoja na
kampuni zinazofanya kazi ya utaalam ushauri katika kusimamia miradi ya ujenzi
ii)
Kuingia na kukagua
shughuli zote za ujenzi unaofanyika hapa nchini kwa madhumuni ya
kujiridhisha na kuhakikisha kama kazi ya ujenzi inayofanyika inafanywa na mtu
ambaye amesajiliwa na Bodi na anazingatia taratibu, kanuni na sheria zote
zinazosimamia ujenzi mijini
iii)
Kuhakikisha kuwa maeneo yote ambako ujenzi unafanyika
kumewekwa mabango yenye kuonyesha jina
na anwani ya mradi,jina la mmiliki ,wataalam wahsauri kwa maana
wabunifu majengo ,wakadiriaji majenzi ,wahandisi pamoja na mkandarasi
endapo atakuwa hakufanya hayo atachukuliwa hatu za kisheria
Mheshimiwa Spika,Chombo
kingine
ambacho kiko chini ya wizara ya ujenzi
ni Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB). Bodi hii ilianzishwa chini ya
Fungu la 4 la sheria Na .15 ya mwaka 1997 (The Engineers registration
Act [Cap . 63 R.E 2002]. Sheria hii imeainisha wajibu na
majukumu ya Bodi mbali mbali kama
ifuatavyo:
i)
Kufuatilia na kusimamia shughuli za utendaji kazi wa
wahandisi ikiwa ni pamoja na kampuni zinazofanya kazi ya utaalam ushauri wa
usimamizi wa miradi ya majenzi mijini,
ii)
Kuingia na Kukagua
shughuli zote za ujenzi
unaofanyika hapa nchini kwa madhumuni ya kujiridhisha na kuhakikisha
kama kazi ya ujenzi inafanyika /inafanywa na mtu ambaye amesajiliwa na bodi na
anazingatia taratibu, kanuni na sheria
zote zinazosimamia ujenzi nchini,
iii)
Kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo ujenzi unafanyika
kumewekwa mabango yenye kuonyesha jina na anwani ya mradi ,jina la mmiliki
,wataalam washauri kwa maana wabunifu
majengo , wakadiriaji majenzi ,wahandisi
pamoja na mkandarasi endapo
atakuwa hajafanya hivyo,atachukuliwa hatua za kisheria.
Mheshimiwa Spika, Chombo kingine ni bodi ya wakandarasi (CRB) ,imeanzishwa na sheria Na. 17/ 1997 (The Contractors
Registration Act [ Cap. 234 R.E 2002.Fungu la 4 la sheria hii imekipa chombo hichi majukumu yafuatayo:
i)
Kusimamia shughuli
za utendaji kazi wa wakandarasi katika kujenga majengo imara yenye kufuata
viwango kwa mujibu wa michoro ya majengo hayo
ii)
Kuingia na kukagua shughuli zote za ujenzi unaofanyika
hapa nchini kwa madhumuni ya kujiridhisha na kuhakikisha kama kazi ya ujenzi inayofanyika inafanywa na
mtu ambaye amesajiliwa na bodi na anaingatia
taratibu ,kanuni na sheria zote
zinazosimamia ujenzi mijini,
Wizara ya Kazi na ajira , inabeba dhamana kwa
kupitia chombo chake cha wakala wa
afya na usalama kazini (OCCUPATIONAL,SAFETY
AND HEALTH AGENCY –OSHA). Chombo hiki kinasimamia usalama mahali pa kazi ,pia
kinashiriki kusimamia miradi ya ujenzi mijini. Mamlaka hii hutoa kibali na
kusajili mradi kama ambavyo mamlaka nyingine zinafanya kwa kutoa sticker.
Mheshimiwa Spika, Wizara zote
hizi zinawajibika kwa namna moja au nyingine kwa maisha ya watanzania 36 yaliyoteketea
kutokana tu na uzembe! Ni TAMISEMI kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Ilala
iliyohusika moja kwa moja na kubadilisha
kibali cha awali cha ghorofa tisa ( 10 storeys) ilichokitoa 4/12/2007[33] na
kutoa kibali kingine cha kuongeza sakafu
saba ,kufikia ghorofa 16!Kinyume na matakwa ya Mpango wa Uendelezaji upya wa
eneo la Kati la jiji la Dar es salaam wa
mwaka 2000. Mpango ambapo unaainisha
kuwa ujenzi kwenye viwanja vilivyoko eneo hilo uwe wa
uwiano wa jengo 2.0, ujazo wa kiwanja wa
asilimia 60 hadi 70 na sakafu kati ya 7 na 10 . Na kama kuna nyongeza yotote
inayotaka kufanyika, lazima kibali kitolewa na Wizara yenye dhamana, suala
ambalo halikufanyika. Halikadhalika wizara ya ujenzi na wizara ya kazi na ajira
kwa vyombo vilivyo chini ya wizara husika, kama ilivyoainishwa hapo juu vyenye mamlaka ya kisheria ya usimamizi
kushindwa kufanya hivyo!
Mheshimiwa Spika, licha
ya
uthubutu ulioonyeshwa na waziri wa ardhi , kulishughulikia suala hili,
Shirika
la nyumba la Taifa haliwezi kukwepa wajibu kama mbia. Mbali na kwamba
Sera ya Ubia ya NHC na Mkataba wa Ubia baina ya pande mbili(NHC na M/S
LADHA
CONSTRUCTION LTD),inabainisha kwamba NHC itatoa Kiwanja na mbia
atagharamia
mradi husika kwa 100%. Na kwamba Mbia ana wajibu wa kuteua wakandarasi
na washauriwa ujenzi na kulipia gharama zao zote, Ni ukweli
usiopingika kwamba baad ya jengo
kukamilika, NHC angekuwa na umiliki wa 50% ya Jengo lote. Jengo ambalo (
kama
yalivyo majengo mengine ya NHC) ni kwa ajili ya makazi au biashara!
Mheshimiwa Spika, kwa namna
yeyote ile , shirika la nyumba lilikuwa na wajibu wa kuhakikisha kwamba
linafuatilia kwa ukaribu(kama ambavyo taasisi nyingine za serikali zinazoingia
ubia na zinavyofanya) ili kuwa na uhakika na usalama wa majengo kwa watumiaji! Shirika
lina wajibu wa kufuatilia kila hatua ya
ujenzi. Ni muhimu ikaeleweka kwamba
miradi ya ubia ni mhimili muhimu sana wa shirika, ikumbukwe kuwa hadi
Februari ,2013 miradi na majengo 11
ilikamilika na miradi ya majengo 19
iliendelea na mradi wa jengo 1 ulianza! Hii ni miradi inayogharimu si tu
mabilioni ya shilingi ,bali yanahusisha maelfu ya watanzania ambao wanatarajia
kuishi au kufanya biashara katika nyumba husika!
XXIV. KIWANJA
NAMBA 1662 INDIRA GHANDI /ASIA
Mheshimiwa Spika,kufuatia
kuporomoka kwa jengo kiwanja namba 2032/75 tarehe 29/ March 2013 ilibainika kwamba jengo lililoko mkabala na
eneo hilo lenye kiwanja na 1662/75 chenye mita za mraba 150 nalo limejengwa kwa
viwango visivyokidhi kanuni za upangaji
miji kama zilivyoainishwa kwenye Mpango
wa Uendelezaji Upya eneo la Kati la jiji la Dar es salaam ! ( Rejea Mpango
unasemaje katika maelezo ya kiwanja 2032/75).
Mheshimiwa Spika, TAMISEMI-
kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, iliendelea na mtindo ule ule wa
kukiuka sheria baada ya kupokea maombi
ya kibali cha ujenzi wa michoro ya ghorofa
kumi na nne (15 Storeys yenye sakafu ya wazi (Terrace) tarehe 21 Mei
,2009 kwa ajili ya biashara na makazi
yaliyosajiliwa kwa plan na.
ILA /213/2009, maombi ammbayo yalipishwa
na kamati ya vibali vya ujenzi iliyoketi
tarehe 20/07/2009 na kuthibitishwa
kwenye kikao cha tarehe 24/08/2009. Na kupewa kibali Na.0398 cha tarehe
12/08/2009.[34]
Mheshimiwa Spika,licha ya
Mamlaka husika kutakiwa kuvunja jengo husika ili kuepuka madhara mengine
kutokea, kwa barua ya 5/04/2013,kutoka kwa Mkurugenzi wa Mipango Miji na Vijiji
, Bibi albina Bura ...katika muktadha ule ule wa baadhi ya watendaji kujificha katika vivuli vyao..mpaka leo jengo
husika bado halijavunjwa. Taarifa zilizopo ni kwamba imebidi wakazi wa eneo
hilo kwa gharma zao watelekeze nyumba zao na kutafuta makazi mapya,nyumba ya
ibada iliyokuwa inahudumia waumini imefungwa, kituo cha afya nk..
Mheshimiwa Spika, Kambi ya
upinzani inatambua juhudi kubwa inayofanywa na kamati ya Bunge ya ardhi na mazingira
katika kushughulikia hili suala, licha ya kutokupata ushirikiano kutoka kwa
baadhi ya mawaziri!Kambi ya upinzani haitarajii kwamba Mhe. Waziri mkuu,
ambaye,wizara ambayo iko chini yake inahusika moja kwa moja na akiwa kama kiongozi wa shughuli za serikali Bungeni
ataruhusu uzembe huu uendelee: Tunaitaka serikali ichukue hatua zifuatazo :
i)
Hatua stahiki za
kinidhamu za kisheria zichukuliwe kwa wahusika wa maafa haya
ii)
Itoe Bungeni Taarifa ya uchunguzi ya kuanguka kwa magorofa Dar es salaam ya mwaka 2006 na
hatua zilizochukuliwa na baada ya ukaguzi nyumba ngapi zilitakiwa kuvunjwa
.Taarifa tulizonazo ile taarifa iko kwenye makabati,imejaa vumbi!
iii)
Bodi zote zilizotajwa hapo juu ziwajibike ipasavyo kila
moja katika eneo lake iliyotakiwa kuwajibika kisheria
iv)
Ukaguzi ufanyike kwenye majengo yote yaliyojengwa na
Ladha Construction LTD, taarifa ambazo kambi ya upinzani inazo mbia amekuwa na
mahusiano ya kikazi ya muda mrefu na NHC na kuna nyumba alizozijenga ambazo
kuna wapangaji ndani yake
v)
Takukuru ichunguze mchakato mzima wa utoaji wa vibali
uliotawaliwa na ukiukwaji wa sheria ili kujiridhisha kama hakukuna na harufu ya
rushwa katika mchakato mzima. Kamati zilizohusika na utoaji vibali zinahusika
hapa.
vi)
Sheria ziangaliwe upya na ikiwezekana tuwe na chombo mamlaka mahsusi ya ukaguzi
(Inspection Authority ) inayosimamia
majengo hususan maghotofa ambayo
itakuwa na wataalam wa fani zote kwa miji na majiji yetu badala ya halmashauri zinazotoa vibali na kushindwa kusimamia
kutokana na ukosefu wa wataalamu.
vii)
Serikali iongeze
idadi ya wataalam katika Halmashauri zetu ili waweze kukidhi mahitaji na ukuaji
wa kasi wa mji.
XXV. MSISITIZO
KUHUSU MIGOGORO YA ARDHI
- FIDIA ZA ARDHI
Mheshimiwa
Spika; Mfano mwingine wa mgogoro na madai
ya muda mrefu ya fidia ni ya wananchi wa Kata ya Kwembe hususan wanaoishi
katika maeneo ya Mloganzila. Tarehe 1 Julai 2011 wakati Bunge lilipokaa kama
Kamati kupitia makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya Waziri Mkuu,
Serikali iliulizwa kuhusu fidia ya wananchi wa eneo la Kwembe Mlonganzila
wanaopaswa kuhama kupisha ujenzi wa majengo ya Chuo cha Afya Muhimbili (MUHAS).
Serikali ilitoa majibu siku hiyo
kuhusu wananchi ambao walibaki baada ya wananchi 1919 kupewa fidia ya
maendeleo na mimea. Hata hivyo Serikali haikutoa majibu yoyote juu ya madai ya
fidia ya ardhi ambao wananchi hao walipewa.
Mheshimiwa
Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani
inaikumbusha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi izingatie kwamba
izingatie kwamba Rais Jakaya Kikwete aliahidi Julai, 2008 kuwa wananchi wa eneo
hilo wangelipwa fidia stahiki pamoja na kupewa viwanja mbadala (rejea Daily
News – 22 Julai, 2008). Aidha, Waziri Mkuu aliwahi kuandika barua kwa
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
tarehe 21 Aprili, 2010 yenye Kumb. Na. PM/P/1/569/29 ya kuelekeza mgogoro
wa fidia ya ardhi umalizwe.
Mheshimiwa
Spika; Ikumbukwe pia kwamba Tarehe 22
Novemba, 2010 katika kikao na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Serikali iliahidi kulipa fidia zote stahiki ikiwemo fidia
ya ardhi. Hii ni baada ya Wizara kuzingatia historia ya eneo husika tangu
wakati wa uhuru na uwepo wa hati ya kijiji cha Kwembe kilichosajiliwa na kupewa
hati No.DSM VC 40 ya tarehe 22 Februari, 1980.
Maeneo mengine yote yanayozunguka eneo hili yalipotwaliwa na mamlaka
mbalimbali yalilipwa fidia ya ardhi,
mfano viwanja 600 Kwembe, Dampo Kisopwa, ekari 200 za wasioona, na mji wa mdogo
Luguruni.
Mheshimiwa Spika;
Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali hii
inayojiita sikivu ya CCM; ni sababu zipi zinazofanya mpaka sasa Chuo Kikuu cha
Sayansi ya Tiba na Afya (MUHAS) pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi kutokulipa wananchi hao fidia ya ardhi mpaka hivi sasa kama Serikali
ilivyoahidi? Je, serikali hii inayojiita inajali inaona fahari gani kuwa na
wakimbizi wa ndani (internally displaced persons) wanaoishi baadhi katika
mahema katika eneo hilo na wengine wengi wakitangatanga katika maeneo mengine
baada ya kukosa walau kupewa viwanja mbadala kama Serikali ilivyowaahidi?
- VIWANJA VYA WAZI
Mheshimiwa Spika; Kwa nyakati mbalimbali kambi rasmi ya Upinzani
Bungeni imekuwa ikihoji juu ya hatua zilizochukuliwa kurejesha viwanja vya umma
(public spaces) vilivyouzwa au kubadilishwa matumizi kinyume cha sheria. Kambi
Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali kueleza ni lini
hasa itakamilisha kuchukua hatua na ni kwanini Serikali inashindwa kusimamia
utawala wa sheria na hivyo kuachia viwanja vingine zaidi kuvamiwa?
Mheshimiwa Spika; Itakumbukwa kwamba Tarehe 1 Julai 2011 katika
mkutano wa nne wa Bunge kikao cha kumi na saba, Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi wakati akijibu maswali bungeni aliahidi kuweka wazi kupitia
kwa Manispaa za Dar Es Salaam taarifa ya kamati ya uchunguzi ya mwaka 2010
iliyoundwa na aliyekuwa mkuu wa mkoa wakati sasa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) William Lukuvi. Aidha, Waziri aliahidi kupitia
kada ya askari wa ardhi (land rangers) kuhakikisha maeneo hayo yanarejeswa na
pia maeneo mengine mapya hayavamiwi. Tangu wakati huo mpaka hivi mabango
yamesimikwa katika baadhi ya maeneo mapya yaliyovamiwa na wahusika kupewa
notisi bila kuvunjika huku maeneo mengine mapya yakiendelea kuvamiwa.
XXVIMUHSTASARI
WA MATUMIZI YA FEDHA ZA KAWAIDA NA
MAENDELEO
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13 wizara
iliidhinishiwa jumla ya shilingi 101,731,722,000 , kati ya fedha hizo shilingi 10,422,891,000 zilitengwa kwa ajili
ya mishahara shilingi 20,308,831,000 kwa
ajili ya matumizi mengineyo na shilingi 71,000,000,000 kwa ajili ya miradi ya
maendeleo… hadi februari 2013 wizara ilipokea jumla ya shilingi 30,991,919,144. Kati ya
fedha hizo shilingi 15,505,928,393 ni fedha za matumizi mengineyo, shilingi 6,773,240,751
ni fedha za mishahara na shilingi 8,712,750,000 kwa ajili ya maendeleo..
Hata hivyo ,mpaka Februari
2013 ni shilingi 2,465,731,973 kwa ajili ya miradi ya maendeleo !
Mheshimiwa Spika, niliwahi kusema hapa Bungeni, na ninarudia kusema; kama
kuna eneo ambalo linaweza kutuletea uvunjifu wa Amani,kama lisipofanyiwa kazi
kwa umakini mkubwa ni ardhi . Migogoro ya ardhi inachangiwa kwa kiasi kikubwa
kwa sababu hakuna mipango utekelezaji wa mipango ya matumizi bora ya
ardhi!Wizara hii licha ya unyeti wake ,ni kati ya wizara ambazo kwa miaka 5
mfululizo,mbali na kutengewa fedha kidogo sana za miradi maendeleo,pamoja na
ufinyu wa fedha husika zimekuwa zikitolewa kidogo sana…wakati mwingine chini ya
20% ya fedha zote . Ni jukumu letu wabunge kulisimamia hili.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, inayoongozwa na CHADEMA, naomba kuwasilisha.
______________________________________
Halima
James Mdee (Mb)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA
UPINZANI BUNGENI
NA
WAZIRI KIVULI WA ARDHI, NYUMBA NA
MAENDELEO YA MAKAZI
No comments:
Post a Comment