Msimamo huo
umetolewa jana bungeni na baadhi ya wabunge wa chama hicho walipokuwa
wakichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
iliyowasilishwa na Waziri Emmanuel Nchimbi.
Mbunge wa
Mbozi Magharibi, David Silinde, alisema Jeshi la Polisi limeoza, kwa
sababu limeshindwa kutekeleza wajibu wake kikamilifu, ikiwamo kuwakamata
wahalifu mbalimbali wanaoshiriki kwenye matukio ya kihalifu.
“Napendekeza
Jeshi la Polisi livunjwe na liingizwe ndani ya Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) liwe sehemu ya kitengo katika jeshi hilo.
“Naamini kwa
kufanya hivyo tutaboresha utendaji wake, silaha kubwa iliyobaki
kulinusuru taifa hili kwa sasa ni kusema ukweli, kwani bila kufanya
hivyo miaka sita ijayo hali itakuwa mbaya,” alisema.
Bofya read more kuendelea.
Aliongeza
kuwa lazima Watanzania wakubali kuwa nchi imegubikwa na matukio ya udini
na ukabila, ingawa serikali ama kwa kufanya makusudi au rais na Waziri
Nchimbi kudanganywa wamekuwa wakishindwa kuchukua hatua.
Silinde
alisema kuwa kama ilivyoandikwa kwenye maandiko matakatifu kuwa itafika
wakati wenye macho hawataona na wenye masikio kutosikia, na kuifananisha
hali hiyo na CCM ya sasa.
Mbunge huyo
aligusia tukio la Arusha akisema huo ni mwendelezo wa kile
walichokipanda CCM kwa kutochukua hatua kwa watu wanaochochea vurugu
hizo za udini.
“Serikali ya CCM haioni tena, haisikii wala haiwezi kunusa tena, hili ndilo anguko la serikali hii,” alisema.
Hata hivyo
alimshangaa Waziri Nchimbi kwa kumtaja mtuhumiwa mmoja kwa jina na
kuwaacha wengine watano aliodai ni raia wa kigeni, akisema huo ni
mwendelezo wa kuficha maovu.
“Kama huyu
mmoja katajwa, kwanini hao wengine wasitajwe? Tunaficha nini? Ama ndio
mwendelezo huo huo wa kutaka kupindisha ukweli wa tatizo na kuibua mambo
mengine?
Mbunge wa
Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu ‘Sugu’ alisema serikali imekosa
mikakati ya kutuliza vurugu hizo na badala yake inakuja na maneno ya
kisiasa yasiyo na ufumbuzi wa tatizo.
Mbunge wa
Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), alisema vitendo vya vurugu za
kidini vinavyoendelea nchini ni matunda ya serikali ya CCM.
Lissu alianza kujenga hoja yake akitumia usemi wa mwanafalsafa mmoja kuwa hakuna uchochezi mkubwa kama kukaa kimya.
Alisema kile
kilichotokea Arusha juzi pamoja na matukio ya kuvamiwa kwa viongozi wa
kidini visiwani Zanzibar ni ukimya wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) ikiwa ni pamoja na kuchochea matendo hayo.
“Nchi hii
imeshuhudia baadhi ya watu wakifanya mihadhara ya kidini na kuhamasisha
uchochezi, magazeti yanaandika kuchochea udini, zipo radio zinatangaza
kashfa mbalimbali dhidi ya dini nyingine, lakini serikali hii iko kimya.
“IGP Omar
Mahita, alitangaza mchana kweupe kuwa Chama cha Wananchi (CUF) ni cha
kigaidi, akaonesha na visu kwenye vyombo vya habari, lakini serikali
hadi leo haijasema kitu juu ya hilo,” alisema.
Lissu
aliongeza kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, CCM iliweka kwenye
ilani yake kuwa itawapatia Waislamu Mahakama ya Kadhi na ilipoona
haiwezi kufanya hivyo ikawasingizia maaskofu kuwa ndio hawataki mahakama
hiyo iwepo.
Lissu
alifafanua kuwa hali imekuwa mbaya kutokana na uchochezi huo ulioasisiwa
na serikali ya CCM halafu sasa inageuka na kuanza kutaka kujinasua.
“Tumeambiwa
tusimlaumu mtu katika tukio hili la Arusha, nami nakubali ila
ninachosema ni kwamba huu ni wakati wa Waziri Nchimbi kuachia ngazi
mwenywewe kutokana na kushindwa kazi ama awajibishwe.
“Huu ni wakati wa IGP Said Mwema kujiuzulu na akishindwa awajibishwe kwa kushindwa kazi,” alisema.
Lissu
alisema kuwa serikali ya CCM ndiyo imepalilia uchochezi wa udini na
ukabila nchini kama kinga ya kujilinda na kasi ya vyama vya upinzani.
“Serikali
hii ndiyo ilisema CHADEMA ni chama cha Wachaga, serikali hii ndiyo
ilisema CHADEMA ni chama cha Wakristo, ni chama cha Wakatoliki. Leo
wanajigeuza na kuanza kujifanya wanachukia vitendo hivi.
“Mheshimiwa
Spika lazima tuambiwe kwanza CUF imeacha lini kuwa chama cha kigaidi na
Uislamu wenye itikadi kali, CHADEMA kimeacha lini kuwa chama cha
Wachaga, Wakristo na Wakatoliki?” alihoji Lissu.
Nchimbi atoa kauli
Mapema
akisoma kauli ya serikali bungeni kueleza mlipuko huo wa Arusha, Waziri
Nchimbi alisema idadi ya watu waliokufa ni wawili baada ya mmoja
kuongezeka usiku wa kuamkia jana.
Aliwataja
marehemu hao kuwa ni Regina Kurusei (45) aliyefariki juzi akipatiwa
matibabu katika Hospitali ya Mount Meru na James Gabriel (16)
aliyefariki dunia usiku wa kuamkia jana huku watu wengine 59 wakiachwa
majeruhi, ambapo miongoni mwao watatu ni mahututi.
Dk. Nchimbi
alisema kuwa uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mlipuko huo ni bomu na
kwamba uchunguzi wa kubaini aina ya bomu lililotumika unaendelea
kufanywa na Jeshi la Polisi na wataalamu wa JWTZ.
“Hadi sasa
watuhumiwa sita wanashikiliwa na polisi. Miongoni mwao ni Victor Ambrose
(20) dereva wa bodaboda, mkazi wa Kwa Mrombo, Arusha ambaye anatuhumiwa
kurusha bomu hilo. Watuhumiwa wengine watano waliokamatwa ni raia wanne
wa kigeni na Mtanzania mmoja, ambao wanashikiliwa kwa mahojiano,”
alisema.
CCM yanena
Nacho Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana,
kimeeleza kusikitishwa na kitendo hicho cha kulipuliwa kwa kanisa mjini
Arusha.
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Kinana alisema kuwa CCM
imeguswa na tukio hilo na kwamba wanalilaani kwa nguvu zote pamoja na
kuitaka serikali kufanya kila mbinu kuwakamata wahusika na kuwachukulia
hatua.
Kinana
alitoa pole kwa waathirika wa tukio hilo wakiwamo wafiwa, majeruhi
pamoja na Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, akisema kuwa wanaamini
kuwa serikali itachukua kwa karibu kila taarifa kuhusiana na tukio hilo.
Chanzo: Mtandao wa kijamii wa CHADEMA.
No comments:
Post a Comment