Mh.Tundu Lissu. |
MAONI
YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA KATIBA NA SHERIA,
MHESHIMIWA
TUNDU A.M. LISSU (MB.)
KUHUSU
MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA
WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KWA MWAKA 2013/2014
(Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2013)
UTANGULIZI
Mheshimiwa
Spika,
Ofisi
ya Waziri wa Katiba na Sheria imeanzishwa kwa mujibu wa kipengele cha 12 cha
Nyongeza ya Waraka wa Rais uliochapishwa kama Tangazo la Serikali Na. 494 la tarehe 17 Desemba 2010. Majukumu ya
Ofisi hii yameainishwa katika Tangazo la
Ukasimishaji wa Majukumu ya Kiuwaziri la mwaka 2010 (The Ministers [Assignment
of Ministerial Functions] Notice, 2010) lililochapishwa katika Gazeti la Serikali kama Tangazo la Serikali Na. 494A la tarehe 17
Desemba 2010. Kwa mujibu wa Nyongeza ya Pili ya Tangazo hilo, pamoja na
mengine, Ofisi ya Waziri wa Katiba na Sheria imekasimiwa majukumu ya masuala ya
kikatiba, uendeshaji na utoaji wa haki, uendeshaji mashtaka na haki za binadamu. Kwa sababu ya matukio ya
hivi karibuni yanayohusu utendaji wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika
mchakato wa Katiba Mpya na kwa kuzingatia umuhimu wake katika mustakbala wa
taifa letu, tunaomba kuanza na masuala yanayoihusu Tume na uendeshaji wake wa
mchakato huo.
TUME
YA MABADILIKO YA KATIBA NA MCHAKATO WA KATIBA MPYA
Mheshimiwa
Spika,
Katika
mwaka wa fedha 2012/2013, Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliidhinishiwa jumla ya
shilingi bilioni 33.944 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya
83 ya Sheria za Tanzania. Kwa mujibu wa Maelezo
ya Makadirio ya Matumizi Mengineyo kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014 yaliyoletwa
mbele ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala mwezi uliopita, hadi kufikia
tarehe 25 Februari, 2013 Tume ilishapokea shilingi bilioni 18.473 kutoka Hazina
na ilikwishatumia shilingi bilioni 14.968, sawa na 81% ya fedha zilizopokelewa.
Kwa mujibu wa Maelezo hayo, shilingi
bilioni 3.504 ambazo hazijatumika zimetengwa kwa ajili ya kulipia madeni
kutokana na huduma za uchapishaji wa Mwongozo wa Mabaraza ya Katiba, uratibu wa
mchakato wa kupatikana Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba na gharama nyingine za
uendeshaji wa Ofisi.
Maelezo
ya Tume yanaonyesha kwamba shillingi bilioni 15.471 ambazo hazijatolewa na
Hazina zitatumika kwa ajili ya kusambaza nakala milioni moja za Rasimu ya
Katiba Mpya (shilingi bilioni 3.848); elimu kwa umma juu ya Rasimu ya Katiba
Mpya (shilingi milioni 400); kuratibu na kuendesha Mabaraza ya Katiba kwa nchi
nzima (shilingi bilioni 4.734); na shilingi bilioni 6.488 kwa ajili ya matumizi
mengine pamoja na ‘stahili za Wajumbe na Sekretarieti.’
Mheshimiwa
Spika,
Katika
Maoni yetu ya mwaka jana, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ililalamikia kile
ilichokiita “... matumizi yasiyoelezeka na yasiyokubalika ya fedha za umma hasa
hasa katika mazingira ambayo wananchi wanahubiriwa na watawala kwamba miradi ya
maendeleo yao ya kiuchumi na kijamii haitekelezeki kwa sababu ya ufinyu wa
bajeti ya Serikali.” Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilidai kwamba shilingi
bilioni 14.633 zilizotengwa kwa ajili ya kuwalipa wajumbe na watendaji wa Tume
posho mbali mbali zilikuwa zinatishia kuigeuza “heshima ya kutumikia waliyopewa
wajumbe wa Tume kuwa hongo ya Serikali.” Madai ya Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni kuitaka Serikali ieleze Bunge hili tukufu gharama zote za kila Mjumbe
wa Tume, Sekretarieti na watumishi wengine wote wa Tume “ili Wabunge na
wananchi wa Tanzania wafahamu kodi wanazolipa zinavyotumika katika mchakato wa
Katiba Mpya” yalikataliwa na Serikali kwa hoja kwamba taarifa hizo ‘ni siri
kati ya mwajiri na mwajiriwa.’
Mheshimiwa
Spika,
Kuendelea Bonyeza Read More
Bunge lako tukufu linaombwa kuidhinisha shilingi bilioni 33.944, kiasi kile kile kilichoidhinishwa mwaka jana, kwa ajili ya matumizi ya Tume kwa mwaka wa fedha 2013/14. Kiasi hiki ni pamoja na shilingi bilioni 12.193 kwa ajili ya “... kulipia posho za vikao kwa Wajumbe wa Tume 34 na Sekretarieti 160 ...”; shilingi bilioni 1.728 ambazo “... zitalipia posho ya kujikimu kwa ajili ya Wajumbe na Sekretarieti wanaposafiri ndani ya nchi kikazi”; na shilingi bilioni 1.650 kwa ajili ya “... kulipa gharama za nyumba za Wajumbe na Sekretarieti wanaotoka nje ya Dar es Salaam.”
Aidha,
kuna shilingi milioni 18 zinazoombwa “... kwa ajili ya kugharamia chakula kwa
Wajumbe wa Tume na Sekretarieti watakaokuwa wamepata maambukizi ya ukimwi”;
shilingi milioni 60 kwa ajili ya usafiri wa ndani; shilingi milioni 50 kwa
ajili ya gharama za malazi kwa Wajumbe wa Tume na Sekretarieti ‘wanaposafiri
kikazi’; shilingi milioni 423 kwa ajili ya ‘chai na vitafunwa’; na shilingi milioni
50 kwa ajili ya “... wahudumu wanaosaidia kazi za Tume wakiwa mikoani wakati wa
kushiriki kwenye Mabaraza ya Katiba na zoezi la upigaji kura ya maoni.”
Vile
vile, Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu linaombwa kuidhinisha shilingi
milioni 60 ya kulipia maji kwa matumizi ya ofisi za Tume; shilingi milioni 30
“... kwa ajili ya kulipia gharama za usafiri wa basi na taxi kwa Wajumbe na
Sekretarieti watakaposafiri ndani ya nchi kikazi”; na shilingi milioni 103 kwa
ajili ya kulipia gharama za simu za mikononi.
Mheshimiwa
Spika,
Bunge
lako tukufu linaombwa kuidhinisha posho na ulaji zaidi ya huu kwa ajili ya
wajumbe na Sekretarieti ya Tume. Ulaji huu mwingine unajumuisha shilingi
milioni 604 “... kwa ajili ya posho kwa Wajumbe wa Tume na Sekretarieti wakati
wa Bunge Maalum la Katiba.” Maelezo ya
Tume yamejaribu kuhalalisha matumizi ya fedha hizi za ziada kwa kuzibatiza jina
la ‘hardship allowances’, yaani ‘posho ya mazingira magumu’, wakati vikao vya
Bunge Maalum la Katiba vitafanyika Dar es Salaam au hapa Dodoma!
Vile
vile, katika ulaji huu mpya zipo shilingi milioni 266 zinazoombwa “... kwa
ajili ya chakula na viburudisho wakati wa vikao vya Bunge Maalum la Katiba”; shilingi
milioni 12 nyingine “... kwa ajili ya huduma za chakula na viburudisho kwa
shughuli zinazohusiana na Tume”; na shilingi milioni 185 kwa ajili ya kulipia
“... usafiri wa basi na taxi....” Aidha, kuna shilingi milioni 30 za “...
utengenezaji wa T-shirts na kofia kwa Wajumbe wa Tume na Sekretarieti wakati wa
kushiriki kwenye zoezi za uhamasishaji kuelekea upigaji wa kura ya maoni”;
shilingi milioni 40 nyingine kwa ajili ya “... utengenezaji wa sare wakati wa
maadhimisho mbali mbali ya kitaifa”; na shilingi milioni 12 “... kwa ajili ya posho
za kujikimu kwa watumishi wa Tume watakaohudhuria kwenye maadhimisho mbali
mbali ya kitaifa....” Zaidi ya hayo, kuna shilingi bilioni 1.307 zinazoombwa kwa
ajili ya “... posho za kujikimu kwa ajili ya Wajumbe na Sekretarieti ya Tume
wanaposafiri ndani ya nchi wakati wa kushiriki kwenye zoezi la upigaji wa kura
ya maoni”; na shilingi milioni 218 kwa ajili ya “... ununuzi wa mafuta ya
magari ya Tume wakati wa kushiriki zoezi la uhamasishaji kuelekea upigaji wa
kura ya maoni.”
Kwa
ujumla, Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu linaombwa kuidhinisha jumla ya
shilingi bilioni 19.039 kwa ajili ya posho za aina mbali mbali na malipo
mengine yanayowahusu Wajumbe na Sekretarieti ya Tume kwa mwaka wa fedha
2013/14. Hii ni zaidi ya 56% ya bajeti yote inayoombwa kwa ajili ya Tume. Kwa
ulinganisho, posho na malipo mengine yanayowahusu Wajumbe na Sekretarieti ya
Tume yalikuwa shilingi bilioni 14.633 au 43% ya bajeti yote ya mwaka wa fedha uliopita.
Hii ina maana kwamba gharama za moja kwa moja za Wajumbe na Sekretarieti ya
Tume zitaongezeka kwa zaidi ya shilingi bilioni 4.406 au zaidi ya 30% ya
gharama za mwaka jana kama Bunge lako tukufu litaidhinisha maombi haya!
Mheshimiwa
Spika,
Maombi
haya ya mabilioni ya fedha za wananchi yanatoa uvundo na harufu mbaya ya
ufisadi, na hayaelezeki na wala kukubalika kwa misingi ya kisheria, na kwa
rekodi ya utendaji kazi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kwanza kabisa, kwa
mujibu wa kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Mabadailiko ya Katiba, Tume ina
Wajumbe wasiozidi thelathini pamoja na Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wake.
Kwa maana hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua uhalali wa maombi
ya shilingi bilioni 12.193 kwa ajili ya posho za vikao kwa Wajumbe 34 wa Tume
wanaotajwa katika kijifungu 210321 cha kasma 210300 kwenye randama ya Fungu 08
linalohusu Tume. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua Wajumbe hawa
wanne wa ziada ni akina nani na wameteuliwa lini kuwa Wajumbe wa Tume? Aidha, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kuelezwa, inakuwaje Tume iwe na Wajumbe 34
wakati Sheria iliyoiunda inataka Tume yenye Wajumbe wasiozidi thelathini?
Pili,
kwa mujibu wa kazi za Tume kama zilivyoainishwa katika kifungu cha 9 cha Sheria;
na kwa mujibu wa utaratibu wa utendaji kazi wa Tume kama ulivyofafanuliwa
katika Sehemu ya Nne ya Sheria; na kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 22(1)
cha Sheria hiyo, Wajumbe na Sekretarieti ya Tume sio wajumbe wa Bunge Maalum la
Katiba. Badala yake, uhusiano pekee wa kisheria uliopo kati ya Tume na Bunge
Maalum ni ule uliotajwa katika vifungu vya 20(3), 20(4) na 25(2) vya Sheria
vinavyomruhusu Mwenyekiti wa Tume kuwasilisha Rasimu ya Katiba Mpya kwenye
Bunge Maalum, na kuwaruhusu Mwenyekiti na wajumbe “... kutoa ufafanuzi
utakaohitajika wakati wa majadiliano katika Bunge Maalum.”
Hii
ina maana kwamba mara baada ya kuwasilisha Rasimu ya Katiba Mpya, Mwenyekiti wa
Tume anakuwa functus officio, yaani
hana kazi nyingine yoyote ya kufanya kwenye Bunge Maalum. Aidha, Mwenyekiti na
Wajumbe wa Tume hawana kazi nyingine yoyote ya kufanya katika Bunge Maalum hadi
hapo watakapohitajika na Bunge Maalum kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa jambo
lolote linalohusu Rasimu ya Katiba Mpya. Wakishatoa ‘ufafanuzi utakaohitajika’
walioitiwa, nao pia wanakuwa functus
officio. Kwa sababu hizo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua uhalali
wa shilingi bilioni 1.055 ambazo Bunge lako tukufu linaombwa kuziidhinisha kwa
ajili ya posho, chakula na viburudisho na usafiri wa basi na taxi kwa Wajumbe
wa Tume na Sekretarieti wakati wa vikao vya Bunge Maalum la Katiba.
Tatu,
kwa mujibu wa kifungu cha 33(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, jukumu
pekee la Tume katika hatua ya uhalalishaji wa Katiba Mpya ni “... kutoa elimu
ya uraia na uhamasishaji juu ya Katiba inayopendekezwa kwa muda usiozidi siku
thelathini kuanzia siku ya kuchapishwa katika Gazeti la Serikali.” Kwa kazi ya
mwezi mmoja tu Wajumbe na Sekretarieti ya Tume wanaombewa shilingi bilioni
1.307 kwa ajili ya posho za kujikimu. Kwa mahesabu hayo, kila Mjumbe wa Tume,
Katibu na Naibu Katibu pamoja na wakuu wa vitengo saba vya Tume na madereva wa
kila mmoja wao watalipwa wastani wa shilingi milioni 16.756 kwa mwezi huo mmoja,
au shilingi 558,547 kama posho ya kujikimu kwa kila siku moja!
Mheshimiwa
Spika,
Katika
nchi ambayo wauguzi katika hospitali za umma wanalipwa mshahara wa kuanzia wa takriban
shilingi 360,000 kwa mwezi; na walimu wa shule za msingi wanaanzia shilingi
laki mbili na nusu na wale wa sekondari shilingi 325,000 kwa mwezi, malipo haya
kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba yana uvundo na harufu mbaya ya rushwa kwa
Wajumbe wa Tume! Hivyo basi, kwa vile kifungu cha 14(2) cha Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba kinatamka kwamba Wajumbe wa Tume na Sekretarieti
“watalipwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi”, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM iliambie Bunge lako tukufu ni sheria na
kanuni zipi za nchi yetu ambazo zimetumika kuhalalisha malipo haya makubwa kwa
Wajumbe na Sekretarieti ya Tume.
Aidha,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM itoe kauli rasmi
mbele ya Bunge lako tukufu kama kuna uhalali wowote wa kutumia fedha za
wananchi wa Tanzania ili kununua ‘chakula maalum’ (special foods) kwa ajili ya
Wajumbe na Sekretarieti ya Tume watakaopata ukimwi kwa sababu ya kuendekeza
ngono zembe na starehe zao binafsi wakati wanatakiwa wafanye kazi ya Tume!
Vinginevyo, Bunge lako tukufu lielezwe kwa ufasaha ni kwa namna gani mchakato
huu wa Katiba Mpya unatazamiwa kusababisha maambukizi ya ukimwi kwa Wajumbe na
Sekretarieti ya Tume!
Kwa
Serikali kujificha nyuma ya pazia la ‘siri ya mwajiri na mwajiriwa’ hakutoshi
tena, kwani ni kulizuia Bunge lako tukufu kutekeleza wajibu wake kikatiba wa
kuisimamia Serikali chini ya ibara ya 63(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sura ya 2 ya Sheria za
Tanzania. Aidha, ni haki kwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kujua uhalali
wa malipo haya kwani, kwa mujibu wa ibara ya 63(3)(a) ya Katiba, Bunge lako
tukufu “laweza kumuuliza Waziri yeyote swali lolote kuhusu mambo ya umma katika
Jamhuri ya Muungano ambayo yako katika wajibu wake....”
Mheshimiwa
Spika,
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua shilingi milioni 218 kwa ajili ya
ununuzi wa mafuta ya magari ya Tume zitatumikaje ndani ya kipindi cha siku
thelathini za uhamasishaji na kuelimisha wananchi kupiga kura ya maoni kwa
Katiba Mpya. Hii ina maana kwamba hata kama kila Mjumbe wa Tume, Katibu, Naibu
Katibu na wakuu wa vitengo saba vya Tume watapewa gari moja kwa kila mmoja wao
kwa kipindi hicho, kila gari itatumia wastani wa shilingi 186,325 kwa siku kwa
ajili ya mafuta tu! Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni safari
zipi hizo za Tume ambazo zitalazimu matumizi ya full tank ya mafuta kila siku kwa mwezi mzima? Huu, kama Baba wa
Taifa Mwalimu Nyerere alivyowahi kusema, ni ‘wizi mtupu’!
Mheshimiwa
Spika,
Amlipaye
mpiga zumari ndiye achaguaye wimbo. Baada ya Tume kulipwa mabilioni yote
tuliyoyapigia kelele kwenye Maoni yetu ya mwaka jana, kuna ushahidi kwamba Tume
imekuwa inacheza wimbo uliochaguliwa na CCM na Serikali yake. Mwezi Februari ya
mwaka huu, Tume ilichapisha Mwongozo
Kuhusu Muundo, Utaratibu wa Kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya
(Mamlaka za Serikali za Mitaa) na Uendeshaji Wake. Mwongozo huo ulisainiwa
na Mwenyekiti wa Tume Jaji Joseph Sinde Warioba na ulianza kutumika tarehe 1
Machi, 2013. Ingawa Tume imedai kwamba Mwongozo huo ulitolewa kwa kuzingatia
matakwa ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inaamini kwamba Mwongozo ulitolewa kinyume na matakwa ya Sheria hiyo na kwa
lengo la kuinufaisha CCM na washirika wake.
Mheshimiwa
Spika,
Kifungu
cha 17(8) cha Sheria kinailazimu Tume kubuni “... utaratibu unaofanana ambao
utatumika katika kila upande wa Jamhuri ya Muungano katika ukusanyaji na
uchambuzi wa maoni ya wananchi, uendeshaji wa mabaraza na uandaaji wa ripoti.”
Katika utekelezaji wa majukumu yake, Tume inatakiwa kufuata msingi huu mkuu
“isipokuwa kama mazingira yatahitaji vinginevyo....” Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inatambua kwamba, kwa kiasi kikubwa, Tume iliweka utaratibu unaofanana
ambao ulitumika katika hatua ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi katika kila
upande wa Jamhuri ya Muungano.
Kwanza,
Tume haikuweka utaratibu wowote wa maana wa kutoa elimu kwa wananchi juu ya
masuala yote yanayohusu Katiba Mpya ili kuwaandaa wananchi kuchangia maoni yao
kwa Tume wakiwa na uelewa wa kutosha. Badala yake, wakati wa mikutano ya Tume
ya kupokea maoni ya wananchi, wajumbe wa Tume walipewa jukumu la kuwaeleza
wananchi juu ya Katiba Mpya kwa muda usiozidi nusu saa. Hii ilifanyika katika
mikutano yote ya Tume katika kila upande wa Jamhuri ya Muungano.
Pili,
muda uliowekwa na Tume wa kukusanya maoni ya wananchi ulikuwa mdogo sana
ukilinganisha na ukubwa wa nchi yetu na wingi wa Watanzania. Katika Majimbo
karibu yote ya uchaguzi, Tume iliendesha wastani wa mikutano saba kwa kila
jimbo kwa lengo la kukusanya maoni ya wananchi. Lakini huu ni wastani tu,
katika majimbo mengi, Tume ilifanya mikutano minne au mitano tu. Hili pia
lilifanyika katika kila upande wa Jamhuri ya Muungano.
Tatu,
katika mikutano yote ya ukusanyaji maoni, wananchi walitakiwa kutoa maoni yao
kuhusu Katiba Mpya kwa muda wa dakika tano kila mmoja na mikutano yenyewe
ilichukua muda wa masaa matatu ikiwa ni pamoja na muda wa kutambulishana
wajumbe wa Tume na mambo mengine yaliyo nje ya kuchukua maoni ya wananchi. Hii
ilifanyika hata kwa Wabunge wakati Tume ilipokuja kuchukua maoni ya Wabunge
hapa Dodoma. Utaratibu huu ulitumika katika kila upande wa Jamhuri ya Muungano.
Aidha, utaratibu unaofanana katika kila upande wa Jamhuri ya Muungano ulitumika
pia kukusanya maoni ya makundi maalum kama vile vyama vya siasa, taasisi
zisizokuwa za kiserikali, mashirika ya kidini na hata taasisi za kiserikali na
viongozi wake, wa sasa na waliostaafu.
Mheshimiwa
Spika,
Wakati
Tume iliweka utaratibu unaofanana katika kila upande wa Jamhuri ya Muungano
wakati wa zoezi la kukusanya maoni ya wananchi, Tume hiyo hiyo iliweka
utaratibu tofauti na wa kibaguzi katika hatua ya kuunda Mabaraza ya Katiba ya
Wilaya. Kwanza, Tume iliweka ngazi mbili za uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza kwa
upande wa Tanzania Bara wakati kwa upande wa Zanzibar Tume iliweka ngazi moja
tu ya uchaguzi.
Hivyo,
kwa mfano, aya ya 6.1.4 ya Mwongozo wa Tume imeweka Mkutano Mkuu Maalum wa
Kijiji au Mtaa “ambao utakuwa na agenda moja tu ya kuwapendekeza kwa kuwapigia kura watu wanne ambao majina yao
yatawasilishwa kwenye Kamati ya Maendeleo ya Kata.” Hii ni ngazi ya kwanza ya
uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza kwa upande wa Tanzania Bara na kazi yake ni
kupendekeza tu. Baada ya hapo majina ya watu walioshinda katika uchaguzi wa
ngazi ya Kijiji au Mtaa yatawasilishwa kwa Afisa Mtendaji wa Kata “ambaye
ataitisha Kikao Maalum cha Kamati ya Maendeleo ya Kata, ambacho ... kitachagua
majina manne ...” ya wajumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya. (aya ya 6.1.8,
6.1.9 na 6.1.10) Hii ni ngazi ya pili na ndiyo inayoamua nani awe mjumbe wa
Baraza la Katiba la Wilaya kwa upande wa Tanzania Bara na nani asiwe.
Kwa
upande wa Zanzibar, ngazi ya uchaguzi ni moja tu, Mkutano wa Shehia ambao, kwa
mujibu wa aya 6.3.4 ya Mwongozo wa Tume, “... utakuwa na agenda moja tu ya
kuwapigia kura ya siri watu watatu ... ambao majina yao yatawasilishwa kwa
Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa au Katibu wa Halmashauri ya Mji au Wilaya
ambapo Shehia hiyo ipo.” Kwa utaratibu huu, wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya
Wilaya kwa upande wa Tanzania Bara wamechaguliwa na watu wanne au watano tu ambao
ni wajumbe wa WDC wakati wajumbe wa Mabaraza ya hayo kwa upande wa Zanzibar
wamechaguliwa na watu wote walioshiriki katika Mkutano wa Shehia.
Wajumbe
wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa upande wa Zanzibar wana uhalali wa kisiasa
kwa sababu wanawakilisha matakwa ya wananchi waliowachagua moja kwa moja bila
mchujo, wakati wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa upande wa Tanzania
Bara hawana uhalali wowote wa kisiasa kwa sababu wanawakilisha maslahi ya CCM
ambayo ndiyo inayotawala asilimia zaidi ya themanini ya WDC zote ambazo ndio
zilizowachuja wajumbe hao.
Mheshimiwa
Spika,
Eneo
la pili linalothibitisha kwamba utaratibu wa Tume ni wa kibaguzi ni katika
uendeshaji wa mikutano ya uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.
Kwa mujibu wa aya ya 6.1.4 ya Mwongozo wa Tume, kwa upande wa Tanzania Bara
Mkutano Maalum wa Kijiji au Mtaa “... utaendeshwa na Mwenyekiti wa Kijiji au
Mtaa, ambapo Afisa Mtendaji wa Kijiji au Mtaa atakuwa Katibu wa Mkutano na
ndiye atakayewasilisha majina ya wananchi walioomba kuingia kwenye Baraza la
Katiba la Wilaya.”
Hata
hivyo, kwa upande wa Zanzibar kwa mujibu wa aya ya 6.3.5 ya Mwongozo wa Tume,
“Mkutano wa Shehia utachagua Mwenyekiti na Katibu wa Mkutano huo kutoka
miongoni mwa wananchi waliohudhuria Mkutano. Katibu ndiye atakayewasilisha
kwenye Mkutano majina ya wananchi wote walioomba kuwa wajumbe wa Mabaraza ya
Katiba ya Wilaya....” Karibu Maafisa Watendaji wa Vijiji na Mitaa wote wa
Tanzania Bara ni wanachama na makada wa CCM, ilhali zaidi ya 90% ya Wenyeviti
wa Vijiji na Mitaa wote ni wanachama na makada wa chama hicho.
Kwa
maana hiyo, mikutano ya uchaguzi wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa upande wa
Tanzania Bara imeendeshwa na makada wa CCM wakati kwa upande wa Zanzibar
mikutano imeendeshwa na viongozi waliochaguliwa na wananchi walioshiriki katika
mikutano hiyo bila kujali itikadi au uanachama wao katika vyama vya siasa.
Ndiyo maana, karibu nchi nzima ukiacha Zanzibar, kwa mujibu wa taarifa ilizo
nazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, wananchi wengi wasiokuwa wanachama wa CCM
ambao walipata kura nyingi katika kura za mikutano ya uchaguzi ya Vijiji na
Mitaa walienguliwa kwenye michujo iliyofanyika katika Kamati za Maendeleo za
Kata zilizowekwa kwa mujibu wa Mwongozo wa Tume.
Mheshimiwa
Spika,
Hata
mahali ambapo wananchi wasiokuwa wanaCCM walifanikiwa kupenyeza katika
chekecheke la mchujo wa WDC wamefanyiwa mizengwe na wanaCCM ili waondolewe
katika orodha ya wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya. Mfano mzuri ni
yaliyomkuta Bw. Beatus Kipeya aliyechaguliwa mjumbe wa Baraza la Katiba la
Wilaya ya Arusha Mjini kwa kupitia Kata ya Sombetini. Mara baada ya Bw. Kipeya
kuchaguliwa kwenye kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Sombetini cha
tarehe 8 Aprili, 2013, siku hiyo hiyo Katibu wa CCM Wilaya ya Arusha Allan G.
Kingazi alimwandikia Mkuu wa Wilaya ya Arusha barua ya malalamiko juu ya
kuchaguliwa kwa Bw. Kipeya.
Pamoja
na kumpa Mkuu wa Wilaya ‘salaam za Chama’ chao, Katibu wa CCM Kingazi
alilalamika kwamba Afisa Mtendaji wa Kata ya Sombetini amemruhusu “... raia wa
Burundi Bwana Beatus Ndanyahubwi Kipea (ambaye katika kugombea ametumia jina la
Beatusi Kipea ili asijulikane kama ni Mrundi – ila mtu wa Kigoma yaani Muha)
kugombea nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya na akashinda, kinyume na
maagizo ya Tume ya Katiba, kwamba Mjumbe ni lazima awe Raia wa Tanzania.”
Baada
ya maelezo mengi kuhusu ‘Urundi’ wa Bw. Kipeya, Katibu wa CCM Kingazi
anamwambia Mkuu wa Wilaya yafuatayo: “... (N)ashauri matokeo ya Uchaguzi wa
Wajumbe wa Baraza la Katiba ufutwe na utangazwe upya. Aidha, Afisa Mtendaji
huyo achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kuvuruga kwa makusudi Uchaguzi wa Muundo
wa Baraza la Katiba la Wilaya.”
Mheshimiwa
Spika,
Kitu
cha kwanza cha kushangaza kuhusu barua ya Katibu wa CCM Kingazi ni kwamba
aliyetumiwa malalamiko ni Mkuu wa Wilaya ambaye, kwa mujibu wa ibara ya 42(3),
44(3) na 46(3) ya Katiba ya CCM Toleo la
1982, Mkuu wa Wilaya ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya, Halmashauri
Kuu ya CCM Wilaya na Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya. Kwa
mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Mwongozo wa Tume, Mkuu wa Wilaya
hana mamlaka yoyote kushughulikia jambo lolote linalohusu uchaguzi wa Wajumbe
wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya. Kwa maana hiyo, sababu pekee ya Mkuu wa Wilaya
ya Arusha kuandikiwa malalamiko haya ni kwa sababu ni kada wa CCM!
Mheshimiwa
Spika,
Ukiacha
Afisa Uhamiaji wa Mkoa wa Arusha, watu wengine wote walionakiliwa barua ya
malalamiko ya Katibu wa CCM Kingazi ni makada wa CCM. Hivyo basi, nakala za
malalamiko hayo zinaonyeshwa kupelekwa kwa Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Katibu wa
CCM Mkoa, Mkuu wa Mkoa (ambaye pia ni mjumbe wa vikao vyote vya kikatiba vya
CCM katika ngazi ya mkoa), Afisa usalama wa Taifa na Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Jiji la Arusha. Wote hawa hawahusiki kisheria kwa namna yoyote ile
katika mchakato wa uundaji wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya. Chombo pekee
ambacho kinahusika kisheria na mchakato wa kuunda Mabaraza hayo na ambacho kilitoa
Mwongozo wa namna ya kuyaunda, yaani Tume, haikuandikiwa wala kunakiliwa barua
ya malalamiko ya Katibu wa CCM Kingazi!
Mheshimiwa
Spika,
Mara
tu baada ya Afisa Uhamiaji Mkoa wa Arusha Bw. R. Gowelle kupata nakala yake, alimwandikia
Bw. Kipeya barua ya ‘wito wa kufika ofisi ya uhamiaji Mkoa wa Arusha’, ambapo
alimtaka kufika ofisini kwake ‘bila kukosa wala kutuma mwakilishi.’ Cha
kushangaza ni barua hiyo imenakiliwa kwa Afisa Mtendaji Kata ya Sombetini,
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kirika A, Sombetini na Balozi wa Mtaa wa Zurich,
Sombetini. Mbali na Afisa Mtendaji Kata ambaye alikuwa mlalamikiwa, wengine
wote walionakiliwa barua ya Afisa Uhamiaji Mkoa ni makada wa CCM na, kwa
taarifa za Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ndio walikuwa chanzo cha malalamiko
ya Katibu wa CCM Kingazi. Kwa taarifa za Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Bw.
Kipeya ni raia halali wa Tanzania anayetoka katika Jimbo la Muhambwe katika
Wilaya ya Kasulu ya Mkoa wa Kigoma. Dhambi pekee na kubwa aliyoifanya na
kustahili kusumbuliwa na Idara ya Uhamiaji ni kugombea na kuchaguliwa kuwa
mjumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya ya Arusha wakati yeye sio mwanachama wa CCM.
Mheshimiwa
Spika,
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni ina ushahidi unaoonyesha kwamba njama za kuhakikisha
kwamba wanaCCM pekee ndio watakaochaguliwa kuwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba
ya Wilaya kwa upande wa Tanzania Bara zilipangwa katika ngazi za juu kabisa za
CCM. Mnamo tarehe 3 Machi, 2013, siku mbili tu baada ya Mwongozo wa Tume kuanza
kutumika, Katibu wa NEC ya CCM, Uhusiano wa Kimataifa Dr. Asha-Rose Migiro
alituma barua pepe kwa wajumbe na watendaji wa Sekretarieti ya NEC ya CCM yenye
kichwa cha habari: ‘MUHIMU!! MABARAZA YA KATIBA YA WILAYA.’
Barua
pepe ya Dr. Asha-Rose Migiro inasema: “Naandika kuhimiza kazi ya kuwatia hamasa
Makatibu wa Mikoa wasimamie kikamilifu mchakato wa kuundwa kwa Mabaraza ya Wilaya
ya Katiba. Kama mnavyofahamu Tume ya Katiba imeshatoa taarifa rasmi kwenye
vyombo vya habari ... kuhusu zoezi hili muhimu. Sambamba na hatua za awali
tulizochukua baada ya kupata rasimu ya mwanzo ya Mwongozo wa Tume, hivi sasa
tunatakiwa tuongeze juhudi za ushiriki wetu na kutayarisha makundi husika kama
tulivyokwishaongea.”
Baada
ya kuagiza ‘mawasiliano kati ya SUKI na Makatibu wa Mikoa’ kuhusu mambo ya
kufanya, Dr. Asha-Rose Migiro alimalizia barua yake kwa maneno yafuatayo:
“Tafadhali wanakaliwa msisite kutoa maoni, ushauri na mbinu bora zaidi za
kutimiza azma yetu katika suala hili muhimu.” ‘Wanakiliwa’ wa barua pepe ya Dr.
Asha-Rose Migiro ni pamoja na Mh. Mwigulu Nchemba, Mh. Zakhia Meghji, Mh.
Muhamed Seif Khatib na Bw. Nape Nnauye, Katibu Mwenezi wa NEC ya CCM.
Siku
moja baadaye, Nape Nnauye aliwaandikia ‘wanakiliwa’ wenzake kama ifuatavyo:
“NASHAURI ikiwezekana kwa sababu ya unyeti wa swala hili tupate taarifa kila
siku/au walau siku tatu ya HALI HALISI inavyoendelea katika kila mkoa, ni
vizuri idara ikaandaa checklist ya mambo muhimu ya kupima kama mchakato
unakwenda vizuri au la! Mfano ... idadi ya walioandaliwa kugombea katika kila
eneo, idadi ya waliohamasishwa kuhudhuria na kupiga kura, n.k.”
Mheshimiwa
Spika,
Njama
za CCM kuteka nyara mchakato wa Katiba Mpya zinahusu pia mchakato wa uhalalishaji
wa Katiba Mpya kwenye kura ya maoni. Mnamo tarehe 18 Desemba mwaka jana, Katibu
wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Francis K. Mwonga, aliwaandikia
barua Makatibu wote wa CCM wa Mikoa kuwapa ‘Maelekezo ya Kikao cha Sekretarieti
ya Halmashauri Kuu ya Taifa na Makatibu wa CCM wa Mikoa Kilichofanyika Dar es
Salaam Tarehe 10/12/2012.’
Sehemu
ya Maelekezo hayo inasema: “Wakati wa kupiga kura ya maoni kuhusu Katiba Mpya
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mawasiliano yafanywe na wahusika ili vituo
vya kupigia kura visiwe mbali sana na wananchi.” Maneno haya yameandikwa hata
kabla Tume haijamaliza zoezi la kukusanya maoni ya wananchi na tayari
Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM inawaelekeza makada wake mikoani kufanya
mawasiliano na ‘wahusika’ juu ya namna ya kupanga vituo vya kupigia kura.
Mheshimiwa
Spika,
Kwa
mujibu wa kifungu cha 56(a) cha Sheria ya
Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 ya Sheria za Tanzania, mamlaka inayohusika kupanga
vituo vya kupigia kura ni Msimamizi wa Uchaguzi, yaani Mkurugenzi wa Jiji, Mkurugenzi
wa Manispaa, Mkurugenzi wa Mji na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya.
Wasimamizi hawa wa uchaguzi wamelalamikiwa kwa miaka mingi na vyama vya upinzani
kwa kupendelea CCM na wagombea wake katika chaguzi mbali mbali. Hawa ndio
wanaotakiwa wawasiliane na Makatibu wa CCM Mikoa ili wapange vituo vya kupigia
kura ya maoni juu ya Katiba Mpya!
Mheshimiwa
Spika,
Mawasiliano
haya ya viongozi wa ngazi za juu za CCM yanathibitisha kwamba mchakato wa
Katiba Mpya umeiingiliwa na kuhujumiwa kwa kiasi kikubwa na CCM. Aidha,
mawasiliano haya yanathibitisha kauli iliyotolewa mbele ya Bunge lako tukufu na
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakati wa mjadala wa hoja ya Ofisi
ya Waziri Mkuu kwamba “...viongozi wa kiserikali kama vile Wakuu wa Wilaya na
wa Mikoa waliwahamasisha wenyeviti wa vijiji, mitaa na madiwani kuhakikisha
kwamba wagombea wote wasiokuwa wa CCM, hasa wa CHADEMA, wanaenguliwa katika
chaguzi za vijiji, mitaa au kata.” Aidha, mawasiliano haya yanathibitisha kauli
ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwamba Mabaraza ya Katiba ya Wilaya
yaliyochaguliwa kwa utaratibu “...ni mabaraza ya CCM na sio mabaraza ya katiba
ya Watanzania wote.”
Mheshimiwa
Spika,
Yote
ambayo tumeyasema hapa yanathibitishwa pia na Tume yenyewe. Tarehe 29 Aprili,
2013 Mwenyekiti wa Tume Jaji Warioba alikiri kwenye mkutano wa waandishi habari
kwamba “... sehemu kubwa ya matatizo yaliyojitokeza yalisababishwa na misukumo
na misimamo ya kisiasa na kidini.” Mwenyekiti Warioba amekiri kwamba kuna
wajumbe wamejazwa katika Mabaraza ya Katiba ya Wilaya: “‘Hao waliojazana kwenye
mabaraza wanadhani wanakuja kupiga kura, hapana.... Tume inazingatia uzito wa
hoja zilizotolewa na wananchi na si idadi ya watu waliotoa maoni.’” Kwingineko,
Mwenyekiti Warioba amekaririwa na vyombo vya habari akikiri kwamba kulikuwa na
rushwa katika mchakato wa uchaguzi wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya. Hata hivyo,
licha ya kukiri kuwepo kwa matatizo makubwa kama haya katika mchakato wa kuunda
Mabaraza hayo, Mwenyekiti Warioba na Tume yake wamekataa madai ya kufutwa kwa
matokeo ya uchaguzi wa Mabaraza kwa hoja kwamba kufanya hivyo kutachelewesha
kupatikana kwa Katiba Mpya!
Mheshimiwa
Spika,
Kauli
ya Mwenyekiti wa Tume ni ya kinafiki na ya kujikosha kutokana na makosa ya Tume
yenyewe. Hii ni kwa sababu Tume yake ilitahadharishwa mapema juu ya uwezekano
mkubwa wa matatizo hayo kujitokeza. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kiliitahadharisha Tume mapema mwezi Februari ya mwaka huu kwamba rasimu ya
Mwongozo wa Tume itazaa mabaraza ya kiCCM na italeta manung’uniko mengi ya
wadau ambao wataenguliwa kwenye ngazi ya WDC ambazo zinatawaliwa na CCM kwa
kiasi kikubwa.
CHADEMA
iliishauri Tume iachane na mapendekezo ya kuziweka WDC kuwa ni kikao cha
uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na badala yake wajumbe wa
Mabaraza wachaguliwe moja kwa moja na wananchi kama ilivyopendekezwa kwa upande
wa Zanzibar. Jaji Warioba na Tume yake walikataa kata kata mapendekezo haya ya
CHADEMA. Kama alivyosema Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni: “... (L)icha
ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kupatiwa maoni ya wadau kwamba utaratibu huo
utaharibu mchakato wa Katiba Mpya, Tume ilikataa kata kata kuubadilisha Muundo
wa Mabaraza haya. Ni wazi kwamba Tume inafahamu inachokifanya. Ni wazi vile
vile kwamba Tume inafahamu matokeo ya hicho inachokifanya, yaani kuundwa kwa
Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ambayo ni ya wanaCCM.”
Mheshimiwa
Spika,
Jaji
Warioba na Tume yake hawawezi wakasikika sasa hivi wakisema kwamba vyama vya
kisiasa na taasisi za kidini ndio zenye makosa kwa kuvurugika kwa mchakato wa
Mabaraza ya Katiba ya Wilaya! Aidha, Tume iliyotengeneza Mwongozo uliosababisha
wanachama wa CCM ‘kujazana’ katika Mabaraza ya Katiba ya Wilaya haiwezi sasa
ikalalama na kudai kwamba haitaangalia idadi ya waliotoa maoni bali itaangalia
uzito wa hoja! Katika hili Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali
iwaeleze Watanzania kama kuna uhalali wowote kutumia shilingi bilioni 4.734 kwa
ajili ya kuratibu na kuendesha Mabaraza ambayo Tume imesema maoni ya wengi
katika Mabaraza hayo hayatafuatwa.
Zaidi
ya hayo, kukataa kwa Tume kufuta matokeo ya uchaguzi wa Mabaraza ambayo Tume
yenyewe inakiri umevurugwa ni uthibitisho tosha kwamba ndivyo Tume
ilivyodhamiria tangu mwanzoni. Mabaraza haya ya kiCCM ni matunda ya moja kwa
moja ya Tume kukiuka utaratibu uliowekwa na kifungu cha 18(3) cha Sheria ulioilazimu
Tume kuunda Mabaraza ambayo “... yatashirikisha na kuwakutanisha wawakilishi
toka makundi mbali mbali ya wananchi katika jamii.”
Mheshimiwa
Spika,
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli mbele ya Bunge lako
tukufu kama CCM au viongozi na makada wake wamefanya mawasiliano yoyote na
vyombo vitakavyosimamia kura ya maoni juu ya Katiba Mpya kama zinavyoashiria
nyaraka za CCM ambazo tumezielezea hapa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inaitaka Serikali hii ya CCM itoe kauli juu ya uhalali wa mawasiliano haya
wakati mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya haujakamilika na wala sheria husika
za uchaguzi hazijafanyiwa marekebisho ili kuruhusu kura ya maoni kufanyika
kihalali, hasa kwa upande wa Tanzania Bara.
Mheshimiwa
Spika,
Kifungu
cha 10 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinafafanua kwamba “Tume itakuwa na
mamlaka na uhuru kwa kadri itakavyokuwa muhimu kwa ajili ya utekelezaji wa
majukumu na mamlaka yake chini ya Sheria hii na haitaingiliwa na mtu au mamlaka
yoyote.” Nyaraka za CCM ambazo tumezielezea hapa zinaonyesha dhahiri kwamba CCM
imeingilia uhuru na mamlaka ya Tume. Kwa uchache kabisa, nyaraka hizi
zinaonyesha viongozi wa ngazi za juu kabisa wa Sekretarieti ya NEC ya CCM
wamefanya makosa ya kula njama kutwaa mamlaka ya Tume kwa kuwatumia Makatibu wa
Mikoa wa CCM ‘kusimamia kikamilifu mchakato wa kuundwa kwa Mabaraza ya Wilaya
ya Katiba.’ Kwa mujibu wa kifungu cha 21(2)(b) cha Sheria, “mtu yeyote ...
atakayejifanya kuwa mjumbe wa Tume au Sekretarieti ... atakuwa ametenda kosa.”
Kifungu cha 21(3) kinaelekeza adhabu ya faini isiyopungua shilingi milioni
mbili na isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo kwa muda usiopungua mwaka
mmoja na usiozidi miaka mitatu au adhabu zote mbili, kwa mtu yeyote
atakayepatikana na hatia na kosa hilo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
Serikali hii ya CCM itoe kauli mbele ya Bunge hili tukufu kama iko tayari sasa kuwachukulia
hatua tajwa za kisheria Dr. Asha-Rose Migiro, Mh. Mwigulu Nchemba, Mh. Zakia
Hamdani Meghji, Mh. Muhamed Seif Khatib, Nape Nnauye na wengine wote waliotajwa
katika nyaraka za CCM kwa uhalifu walioufanya dhidi ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba.
Mheshimiwa
Spika,
Baada
ya ushahidi wote huu, hakuwezi kuwa na ubishi kwamba utaratibu mzima wa kuundwa
kwa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ni haramu. Hakuwezi kuwa na ubishi tena kwamba
uharamu huu una lengo moja tu: kuhakikisha kwamba Katiba Mpya itakayopatikana
kwa mchakato huu haramu “... itakuwa ni Katiba Mpya kwa jina tu, mambo mengine
ya msingi yatabaki vile vile (yalivyo katika Katiba ya sasa). Kwa maneno
mengine, itakuwa ni Katiba ile ile, ya watu wale wale, wa chama kile kile.”
Kama
alivyosema Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni: “Katika mwaka wa kwanza
wa mchakato wa upatikanaji Katiba mpya, Tume ya Mabadiliko ya Katiba
imethibitisha hofu tuliyokuwa nayo toka mwanzo kwamba lengo la mchakato wa
Katiba Mpya uliowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ni
kuhakikisha kwamba mabadiliko pekee yakayokuwepo ni yale yenye kulinda matakwa
ya CCM na Serikali yake au yale pekee yatakayokuwa na baraka za “‘status quo.’”
Mheshimiwa
Spika,
Katika
Maoni ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu hoja ya Ofisi ya
Waziri Mkuu, tulitangaza kwamba CHADEMA itajitoa ushiriki wake katika mchakato
wa Katiba Mpya endapo mambo yafuatayo hayatapatiwa ufumbuzi hadi kufikia mwisho
wa mwezi huu, yaani tarehe 30 Aprili, 2013:
1.
Kufutwa kwa uchaguzi wa wajumbe wa
mabaraza ya wilaya ya Katiba uliofanywa na Kamati za Maendeleo za Kata, na
badala yake wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya wachaguliwe moja kwa moja
na wananchi wa Kata husika bila kuchujwa na WDC;
2.
Serikali ilete mbele ya Bunge hili
tukufu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
yatayofanyia maeneo yafuatayo marekebisho:
(a)
Vifungu vyote vinavyohusu uwakilishi
katika Bunge Maalum la Katiba wa taasisi zilizoainishwa katika Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba ili kuweka wazi namna wawakilishi wa taasisi hizo
watakavyopatikana kutoka kila taasisi na idadi yao kwa kila taasisi;
(b)
Vifungu vyote vinavyohusu
ushirikishi wa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka Zanzibar katika
mijadala inayohusu mambo yasiyokuwa ya muungano ya Tanzania Bara ili
kuhakikisha kwamba wajumbe wa Zanzibar ambao hawatakuwa pungufu ya theluthi
moja ya wajumbe wote watashiriki katika mijadala inayohusu mambo ya Muungano tu
na sio mambo ya Tanzania Bara yasiyokuwa ya Muungano;
(c)
Vifungu vyote vinavyohusu mamlaka ya
Rais kuitisha tena Bunge Maalum la Katiba baada ya Bunge hilo kuwa
limeshapitisha Rasimu ya Katiba Mpya kwa lengo la kufanya marekebisho katika
Rasimu kabla haijapelekwa kwenye kura ya maoni ili kumwondolea Rais uwezo wa
kubadilisha maamuzi yaliyopitishwa na Bunge Maalum;
(d)
Vifungu vyote vinavyohusu mamlaka ya
kikatiba na ya kisheria yatakayoiwezesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuendesha na
kusimamia kura ya maoni ili kurekebisha hali ya sasa ambayo Katiba na Sheria za
Uchaguzi za nchi yetu hazitambui uwepo wa kura za maoni na utaratibu wa namna
ya kuiratibu, kuisimamia na kuiendesha;
Mheshimiwa
Spika,
Madai
ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni hayajatimizwa hadi tunatoa Maoni haya.
Mwenyekiti wa Tume Jaji Warioba amesema wazi wazi kwamba uchaguzi wa Mabaraza
ya Katiba ya Wilaya, ambayo Tume inakiri ulivurugwa na mivutano ya kisiasa na
kidini, hautarudiwa na Mabaraza hayo yataendelea. Aidha, Mwenyekiti wa Tume
amewaasa wale wanaolalamikia uchaguzi wa Mabaraza hayo wapeleke malalamiko yao
kwenye Tume ili yashughulikiwe. Ushauri huu wa Tume hauna maana yoyote kwa
sababu Mwongozo uliotolewa na Tume yenyewe haujaweka utaratibu wowote wa
kufungua na kushughulikia malalamiko yoyote yanayotokana na uchaguzi wa
Mabaraza hayo!
Mheshimiwa
Spika,
Kwa
upande wa Serikali, Waziri Mkuu aliahidi – wakati wa kuhitimisha hoja ya Ofisi
ya Waziri Mkuu – kwamba Serikali italeta Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba kabla ya mwisho wa Mkutano huu wa Bajeti. Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni imetafakari sana ahadi hii ya Waziri Mkuu. Pamoja na kwamba ni ahadi ya
maneno tu, kama ilivyokuwa ahadi ya Mheshimiwa Rais Dokta Jakaya Mrisho Kikwete
kwamba marekebisho yote yanayohitajika katika Sheria hiyo yatakamilika hadi
kufikia Novemba 2012, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeona ni vema iipe muda
Serikali wa kuleta marekebisho tajwa ndani ya Mkutano huu wa Bunge la Bajeti.
Kipindi hiki pia kitaenda sambamba na Tume kutoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba
Mpya kwa ajili ya kuanza kujadiliwa na Watanzania.
Mheshimiwa
Spika,
Endapo
hadi kufikia mwisho wa kipindi hicho Serikali itakuwa haijaleta Muswada wa
marekebisho yanayotakiwa; au endapo Muswada utakaoletwa hautakidhi matakwa ya
kuboresha mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya, basi CHADEMA itawaalika
wanachama, wafuasi na mashabiki wake Tanzania nzima, pamoja na taasisi za
kiraia na za kidini, vyama vya siasa na Watanzania wote wenye nia njema na
taifa hili kuhamasisha Watanzania kuikataa Rasimu ya Katiba Mpya kwenye kura ya
maoni itakayofanyika kwa ajili ya kuihalalisha Katiba hiyo.
Mheshimiwa
Spika,
Nchi
ya Kenya imepata Katiba Mpya mwezi Agosti 2010 baada ya mchakato uliochukua
zaidi ya miaka kumi na moja. Kwa mujibu wa Dr. Patrice L.O. Lumumba[i]
aliyekuwa Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Kenya, kwanza Serikali ya
KANU chini ya Rais Daniel arap Moi, na baadaye Serikali ya NARC chini ya Rais
Mwai Kibaki, zilijaribu kuteka nyara mchakato wa Katiba Mpya ya Kenya kwa
kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya ambayo ilipopelekwa kwenye kura ya maoni mwaka
2005 ilikataliwa na wananchi wa Kenya.
Kama
inavyojulikana, baadaye Kenya ilifanya Uchaguzi Mkuu wa Desemba 2007 kwa mujibu
wa Katiba ya zamani ya Kenya ya mwaka 1969. Matokeo ya uchaguzi huo chini ya
Katiba ya zamani yaliingiza Kenya katika machafuko makubwa ya kisiasa yaliyosababisha
mauaji ya maelfu ya Wakenya. Kwa sababu ya machafuko hayo, Kenya imeingia
katika vitabu vya historia kuwa nchi ya pili katika Bara la Afrika, baada ya
Hassan al-Bashir wa Sudan, yenye Rais na Naibu Rais walioko madaraka lakini
wanakabiliwa na mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu (crimes against
humanity) katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.
Mheshimiwa
Spika,
Jamhuri
ya Zimbabwe nayo imepata Katiba Mpya mwezi Februari ya mwaka huu baada ya
mchakato uliochukua zaidi ya miaka kumi na sita. Mwaka 2000, Chama tawala cha
ZANU PF cha Rais Robert Mugabe kiliwapelekea wananchi wa Zimbabwe Rasimu ya
Katiba Mpya iliyotokana na mchakato uliotawaliwa na chama hicho kuanzia mwanzo
hadi mwisho. Katika kura ya maoni iliyofanyika mwaka huo, Rasimu hiyo ya Katiba
Mpya ilikataliwa kwa kura nyingi na wananchi wa Zimbabwe.
Matokeo
yake, Zimbabwe iliingia katika giza kuu la machafuko ya kisiasa na kijamii
yaliyopelekea ukiukwaji wa kutisha wa haki za binadamu na hatimaye Zimbabwe kutengwa
kimataifa kwa kufukuzwa katika Jumuiya ya Madola na kuwekewa vikwazo vya
kiuchumi na kidiplomasia. Baadaye, ZANU PF iliyofikiria kwamba inaweza kutawala
kwa mabavu ya kijeshi, ilipoteza wingi wake Bungeni na hatimaye ililazimika
kufanya maridhiano na vyama vya upinzani na makundi mengine ya kijamii
yaliyopelekea kusainiwa kwa Makubaliano Makuu ya Kisiasa (Global Political
Agreement). Chini ya Makubaliano hayo, Bunge la Zimbabwe liliunda Kamati ya
Katiba ya Bunge iliyokuwa na wajumbe sawa kwa kila kimoja cha vyama vikuu vya
kisiasa vya nchi hiyo. Kamati hiyo ya Bunge, iliyokuwa na Wenyeviti Wenza
Watatu, Makamu Wenyeviti Wenza Watatu na wajumbe tisa kwa kila chama, ndiyo
iliyoandaa Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Zimbabwe iliyopigiwa kura ya maoni
na kupitishwa na wananchi wa Zimbabwe mwezi Februari ya mwaka huu. Baadhi ya
wabunge wa Bunge lako tukufu walishiriki katika kura ya maoni hiyo kama sehemu
ya ujumbe wa waangalizi wa Chama cha Mabunge ya SADC.
Mheshimiwa
Spika,
Mifano
ya Kenya na Zimbabwe inatosha kuwaonyesha kwamba wanajidanganya wale wote
wanaodhani kwamba kuwa chama tawala chenye wabunge wengi na mabavu ya kijeshi
inatosha kubaki madarakani hata kwa hila na uchakachuaji. Saa ya mabadiliko
inapogonga, hakuna mabavu ya kijeshi wala usalama wa taifa wala mapesa mengi
wala ukatili wa aina yoyote unaoweza kuzuia wimbi la mabadiliko hayo! Bunge
lako tukufu litafanya vema kujifunza kutokana na historia ya wenzetu.
HIFADHI
YA HAKI ZA BINADAMU
Mheshimiwa
Spika,
Katiba
ya nchi yetu inatambua na kuhifadhi haki za binadamu na wajibu muhimu. Sehemu
ya Tatu ya Katiba yetu imefafanua haki hizo kwa kirefu. Kama sehemu ya jumuiya
ya kimataifa, Tanzania vile vile imeridhia mikataba mbali mbali ya haki za
binadamu kama vile Tangazo la Ulimwengu la Haki za Binadamu (Universal
Declaration of Human Rights – UDHR), 1948; Mkataba wa Kimataifa wa Haki za
Kiraia na Kisiasa (International Covenant on Civil and Political Rights –
ICCPR), 1966 na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na
Kiutamaduni (International Covenant on Economic, Social and Cultural Rights –
ICESCR), 1966. Aidha, Tanzania ni mwanachama wa Mkataba wa Afrika wa Haki za
Binadamu na za Wananchi (African Charter on Human and Peoples Rights – ACHPR),
1981.
Mheshimiwa
Spika,
Licha
ya kuwepo kwa msingi huu wa kikatiba na kisheria, hali ya haki za binadamu
imezidi kuzorota kwa kiasi kikubwa katika nchi yetu kama ambavyo Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni imeelezea mara nyingi katika Bunge lako tukufu. Kwenye Maoni
haya, Mheshimiwa Spika, tunaomba tufanye marejeo ya taarifa rasmi za kitafiti
za mamlaka za umma za kiserikali na za taasisi zisizokuwa za kiserikali
kuhusiana na matumizi ya nguvu za vyombo vya dola na jinsi ambavyo
zinahatarisha haki za binadamu zilizohifadhiwa na Katiba yetu. Taarifa hizi
rasmi zinahusu uchunguzi wa kifo au mauaji ya mwandishi wa habari Daudi
Mwangosi katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa mnamo
tarehe 2 Septemba, 2012, wakati akifanya kazi ya kukusanya habari kwa niaba ya
Kituo cha Televisheni cha Channel Ten katika mkutano wa ndani ulioandaliwa na
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Mheshimiwa
Spika,
Ibara
ya 18(b) na (d) ya Katiba inahifadhi haki ya kila mtu “... kutafuta, kupokea na
kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi”; na “... haki ya kupewa taarifa
wakati wowote kuhusu matukio mbali mbali muhimu kwa maisha na shughuli za
wananchi na pia kuhusu masuala muhimu ya jamii.” Aidha, kwa mujibu wa ibara ya
22(1) inatamka bayana kwamba “kila mtu anayo haki ya kufanya kazi.” Kwa misingi
hii ya kikatiba, Marehemu Daudi Mwangosi alikuwa na haki zote kisheria
kukusanya habari katika mkutano wa CHADEMA katika Kijiji cha Nyololo siku
alipouawa.
Mheshimiwa
Spika,
Katiba
yetu pia inatambua na kuhifadhi “... uhuru wa kukutana na watu wengine kwa
hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine, na kwa
ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani na kuanzisha na kujiunga na vyama au
mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi na kuendeleza imani au
maslahi yake au maslahi mengineyo.” (ibara ya 20(1) Ni muhimu kutambua hapa
kwamba ‘aya nyakuzi’ (clawback clauses) zilizokuwa zinaweka masharti na
vizingiti vya ‘kwa mujibu wa sheria’ vilivyokuwa vinazuia raia kufaidi haki na
uhuru unaotambuliwa na ibara za 18 na 20 viliondolewa na Sheria ya Marekebisho
ya Katiba, Sheria Na. 1 ya 2005. Kwa maana hiyo, hakuna sheria nyingine yoyote
inayoweza kufunga au kupunguza uhuru na haki zilizotolewa na vifungu hivi
isipokuwa masharti yaliyoko kwenye ibara ya 30 ya Katiba yenyewe.
Mheshimiwa
Spika,
Sehemu
ya Kwanza ya Sura ya Sita ya Katiba inaunda Tume ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora na kuipa majukumu na mamlaka ya kuyatekeleza majukumu hayo. Kwa mujibu wa
ibara ya 130(1) ya Katiba, majukumu ya CHRAGG ni pamoja na kuhamasisha hifadhi
ya haki za binadamu na wajibu kwa jamii; kupokea malalamiko ya uvunjaji wa haki
za binadamu na kuyachunguza; na, kama itabidi, kufungua mashauri mahakamani ili
kuzuia uvunjaji wa haki za binadamu. Mara baada ya mauaji ya Marehemu Mwangosi
kutokea, Tume ya Haki za Binadamu ilifanya uchunguzi wa mazingira na sababu za
mauaji hayo. Baada ya uchunguzi huo, Tume iliandaa Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ya Uchunguzi wa
Tukio Lililopelekea Kifo cha Daudi Mwangosi Kilichotokea Septemba 2, 2012 Kijijini
Nyololo. Taarifa hiyo ilitolewa
hadharani na kwa vyombo vya habari tarehe 10 Oktoba, 2012.
Mheshimiwa
Spika,
Taarifa
ya Uchunguzi inaeleza kwamba “... Tume ilizingatia zaidi masuala ya uvunjwaji
wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora. Hivyo basi, Tume
ilitilia maanani Katiba ..., sheria mbali mbali na mikataba ya kimataifa na ya
kikanda inayohusu haki za binadamu ambayo Tanzania imeridhia.” Katika uchunguzi
wake Tume ilibaini mambo yafuatayo:
1)
Tarehe 2 Septemba,
2012 CHADEMA kiliruhusiwa na Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Mufindi kufanya
mikutano ya ndani na kuzindua matawi mapya. Lakini jioni ya tarehe 1 Septemba,
2012 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa Michael Kamuhanda alizuia CHADEMA
kufanya mikutano iliyoruhusiwa. Kwa mujibu wa Tume ya Haki za Binadamu, Kamanda
wa Polisi wa Wilaya ndiye ‘“Officer in charge” wa polisi wa eneo husika kama
sheria inavyotaka.’
2)
Viongozi wa CHADEMA
kilifanya mazungumzo na Mkuu wa Upelelezi wa Jinai Mkoa wa Iringa “... na
kuruhusiwa kufungua matawi yao bila ya kuwa na mikutano ya hadhara.”
3)
Msajili wa Vyama
vya Siasa aliwaandikia barua viongozi wa vyama vya siasa kuwataka kusitisha
shughuli zao kwa sababu ya sensa ya watu na makazi iliyokuwa inafanyika wakati
huo.
4)
Wakati shughuli ya
uzinduzi wa tawi la Nyololo ukiendelea, Kamanda Kamuhanda alifika eneo hilo na
kuamuru viongozi wa CHADEMA wakamatwe, na wafuasi wa CHADEMA walipinga
kukamatwa kwa viongozi wao.
5)
Kamanda Kamuhanda
aliamuru kupigwa kwa mabomu ya machozi ili kuwatawanya wananchi waliokusanyika
katika ofisi za tawi hilo la CHADEMA.
6)
Baada ya mabomu ya
machozi kupigwa, wananchi walitawanyika na kukimbia ovyo, lakini Marehemu
Mwangosi “... alizingirwa na askari, aliteswa na hatimaye inadaiwa alipigwa
bomu na kufa papo hapo.
7)
Marehemu Mwangosi
aliuawa umbali wa takriban mita 100 kutoka ilipo Ofisi ya CHADEMA tawi la
Nyololo.
8)
Katika tukio hilo
wananchi kadhaa walijeruhiwa kwa mabomu, wakiwemo mwandishi wa habari wa gazeti
la Nipashe Godfrey Mushi, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake CHADEMA Wilaya ya
Mufindi, Winnie Sanga, na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mufindi Asseli Mwampamba “aliyekuwa
akifanya jitihada za kumuokoa marehemu Daudi Mwangosi.”
Kwa
mujibu wa Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu, “... Tume imejiridhisha kuwa
tukio la lililopelekea kifo cha Daudi Mwangosi limegubikwa na uvunjwaji wa haki
za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.” Taarifa ya Tume
inafafanua kuwa, “... Tume imejiridhisha kuwa Jeshi la Polisi limevunja haki ... ya kuishi, haki ya kutoteswa na
kupigwa, haki ya usawa mbele ya sheria na haki ya kukusanyika na kutoa maoni.”
Kuhusiana
na amri ya Kamanda Kamuhanda ya kupiga marufuku mkutano wa CHADEMA, Taarifa ya
Tume inasema kwamba katika utekelezaji wa majukumu yake, Kamanda Kamuhanda “...
alikiuka Sheria ya Vyama vya Siasa ... kifungu cha 11(a) na (b) na Sheria ya
(Jeshi la) Polisi ... kwa kuingilia kazi za OCD wa Mufindi na kutoa amri ya
kuzuia shughuli za CHADEMA wakati yeye hakuwa ‘Officer in-charge’ wa polisi
eneo husika. Kwa maana hiyo amri aliyoitoa haikuwa halali kwa kuwa ilitolewa na
mtu ambaye hakuwa na mamlaka kisheria kutoa amri hiyo. Haya ni matumizi mabaya
ya madaraka, hivyo ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.”
Mheshimiwa
Spika,
Tume
ya Haki za Binadamu ilihoji pia hatua ya Msajili wa Vyama vya Siasa John Tendwa
kuwaandikia barua viongozi wa vyama vya siasa kuwataka kusitisha shughuli zao
kwa sababu ya sensa. Kwa mujibu wa Taarifa ya Tume, hatua hiyo “... ilikiuka
misingi ya utawala bora kwani maelekezo yaliyotolewa ndani ya barua hiyo
yanakinzana na Sheria ya Takwimu, Na. 1 ya mwaka 2002 inayotoa fursa kwa
wananchi kuendelea na kazi zao wakati wa sense....” Barua hiyo pia “... ni
kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa ... inayotoa fursa kwa vyama vya siasa kufanya
shughuli zake bila kuingiliwa.”
Katika
hili ni muhimu kunukuu mapendekezo ya Tume ya Haki za Binadamu kwa kirefu:
“Jeshi la Polisi na Msajili wa Vyama vya Siasa waepuke kufanya maamuzi au
matendo yanayoibua hisia za ubaguzi au upendeleo miongoni mwa jamii wakati
wanapotekeleza majukumu yao kisheria. Mfano, Jeshi la Polisi lilizuia mikutano
ya CHADEMA kwa sababu ya sensa wakati huo huo ... CCM walikuwa wakifanya
uzinduzi wa kampeni huko Zanzibar. Aidha, rai ya Msajili wa Vyama vya Siasa
haikuzingatiwa kwa upande wa CCM Zanzibar huku CHADEMA walishurutishwa na
polisi kutii rai hiyo.” Aidha, Taarifa ya Tume inasisitiza kwamba “demokrasia
ya mfumo wa vyama vingi iheshimiwe na kulindwa.”
Mheshimiwa
Spika,
Sio
Tume ya Haki za Binadamu pekee iliyofanya uchunguzi wa mauaji ya Marehemu
Mwangosi. Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),
taasisi mbili huru zinazojihusisha na masuala ya habari Tanzania, nazo
zilifanya uchunguzi wa pamoja. Taarifa yao inayojulikana kama Ripoti ya Timu Maalum ya Uchunguzi
Iliyoteuliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania
(TEF) Kuchunguza Mazingira Yaliyopelekea Kuuawa kwa Mwandishi wa Habari Daudi
Mwangosi Septemba 2, 2012 Katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoani
Iringa, imeunga mkono Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu juu ya jambo
hili.
Kwa
mujibu wa Ripoti ya MCT/TEF, matokeo ya uchunguzi wao “... yanadhihirisha bila
wasi wasi kwamba polisi kwa makusudi waliwavurumisha waandishi waliotoka Iringa
wakati wakikusanya habari za shughuli za CHADEMA katika kijiji cha Nyololo.
Zaidi ya hapo, Daudi Mwangosi mwenyewe aliuawa akiwa mikononi mwa polisi huku
wakisimamiwa moja kwa moja na Kamanda ... Kamuhanda.” Ripoti inakubaliana na
Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu kabla ya Mwangosi kuuawa, “... maelewano
yalifikiwa katika ya RCO na maofisa wa CHADEMA, na kamanda (RCO) (aliwa)amuru
maofisa wake kutotumia nguvu dhidi ya watu waliokusanyika kwenye ofisi ile.
Hata
hivyo, hali hiyo maelewano ilibadilika mara baada ya Kamanda Kamuhanda kufika
katika eneo la tukio. Kwa mujibu wa Ripoti ya MCT/TEF, “mashuhuda wanaeleza
kuwa RPC alimwita RCO na kumuonya wazi kuhusu kushughulikia kwa amani masuala
ya CHADEMA katika eneo la awali la utulivu.” Baada ya hapo, “inaelekea RCO
alijitoa kuelekea eneo la umwagaji damu ... na hivyo usimamizi wa utoaji amri
katika eneo la umwagaji damu ... ulibakia kwa mkuu wake ambaye ni RPC Michael
Kamuhanda.”
Sawa
na Taarifa ya Tume, Ripoti ya MCT/TEF inaweka lawama za vurugu zilizotokea
Nyololo kwenye miguu ya Kamanda Kamuhanda: Vurugu zilianza pale Kamanda
Kamuhanda alipoamuru kukamatwa kwa viongozi wa CHADEMA waliokuwepo. “Kufuatia
amri hiyo ... polisi ... waliingia kwa nguvu katika ofisi ya CHADEMA wakipiga
mabomu ya machozi na kuwaamuru viongozi hao wajisalimishe.” Kwa mujibu wa
Ripoti ya MCT/TEF, viongozi wa CHADEMA walitii amri hiyo na “... kujisalimisha
kwa kuketi na kuinua mikono yao juu.” Hata hivyo, “... wakati makada wa CHADEMA
walitii maagizo ya viongozi wao ya kuketi chini na kuinua mikono yao juu,
polisi walifyatua risasi na mabomu ya machozi, na kuwapiga makada hao na
waandishi kwa virungu.”
Mheshimiwa
Spika,
Ripoti
ya MCT/TEF inakubaliana na Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu juu ya jinsi
Marehemu Mwangosi alivyouawa. “Alipoangalia nyuma, Daudi Mwangosi aliona
kikundi cha polisi wakimpiga mwandishi mkuu wa gazeti la Nipashe wa Iringa, Godfrey Mushi.... Wakati mwandishi Godfrey Mushi
akiwa bado anapigwa na polisi, marehemu Mwangosi aliwakimbilia akiwaomba waache
kumdhuru zaidi Mushi kwa kuwa alikuwa mwandishi tu. Polisi hawakumsikiliza. Badala
yake wakamburuta mwandishi huyo ambaye tayari alikuwa amepoteza fahamu na
kumweka kwenye gari lao na wakamgeukia Daudi Mwangosi mwenyewe, wakampiga kwa
nguvu mpaka akapoteza fahamu.”
Hata
amri ya Mkuu wa Kituo cha Polisi Mafinga Mwampamba kuwataka askari polisi
waache kumpiga marehemu Mwangosi haikusikilizwa na askari hao. Ili kujiokoa,
marehemu Mwangosi alimkumbatia OCS Mwampamba na “baadaye kumwangukia miguuni
mwake kuepuka kipigo zaidi.” Kwa mujibu wa Ripoti ya MCT/TEF, “picha za mgando
zinaonyesha polisi mmoja akipiga bomu la machozi tumboni mwa marehemu Mwangosi
kwa karibu kabisa.” Bomu hilo liliusambaratisha mwili wa marehemu Mwangosi
aliyekufa papo hapo. Kwa sababu marehemu Mwangosi alikuwa chini ya miguu ya OCS
Mwampamba, “naye pia alijeruhiwa vibaya.”
Mheshimiwa
Spika,
Siku
moja baada ya mauaji ya Daudi Mwangosi, Kamanda Kamuhanda alinukuliwa na vyombo
vya habari akidai kwamba marehemu Mwangosi alifariki “kutokana na kitu kizito
kilichotupwa na waandamanaji.” Aidha, siku iliyofuata Kamishna wa Operesheni wa
Jeshi la Polisi Paul Chagonja alidai kwamba baada ya ghasia kudhibitiwa,
marehemu Mwangosi alikimbilia walipokuwa polisi na “kitu kama bomu kikarushwa
na kundi la watu wanaokimbia hovyo na kumlipua Mwangosi.”
Madai
haya yanakanushwa na Ripoti ya MCT/TEF inayomnukuu shuhuda mwanamke aliyeshuhudia
mauaji hayo na kubainisha kwamba marehemu Mwangosi “aliuawa chini ya usimamizi
wa moja kwa moja wa RPC Michael Kamuhanda.” Ripoti hiyo pia imeelezea kwa
kirefu jinsi Jeshi la Polisi lilivyotoa taarifa zinazokinzana juu ya kuhusika
kwake na mauaji ya Mwangosi. Hivyo, kwa mfano, wakati Waziri wa Mambo ya Ndani
Mheshimiwa Emmanuel Nchimbi alidai tarehe 4 Septemba 2012 kwamba marehemu
aliuawa na bomu la machozi ambalo ‘halikulipuliwa kitaalamu na polisi’, Kamanda
Kamuhanda alitokea kwenye televisheni siku iliyofuata “akitangaza habari za
kuwatupia lawama wafuasi wa CHADEMA kwa kutupa kitu kizito kilicholipuka na
kumuua Mwangosi....”
Mheshimiwa
Spika,
Kwa miaka miwili
mfululizo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imezungumzia kwa kirefu vitendo vya
mauaji ya raia wasiokuwa na hatia ambavyo vimekuwa vinafanywa na vyombo vya
dola hasa Jeshi la Polisi. Kama
tulivyowahi kusema kwa kunukuu matokeo ya utafiti uliofanywa katika nchi za
Afrika Mashariki na Mradi wa Haki za
Binadamu wa Jumuia ya Madola na kuchapishwa mwezi Juni 2006, ‘“watu wa
Tanzania … wanakabiliwa na tatizo la kuwa na jeshi la polisi ambalo mara nyingi
lina sifa ya ulaji rushwa, matumizi ya mabavu na kuwa na chombo katili cha
serikali.” Kwa mujibu wa utafiti huo, “aina hii ya uendeshaji wa shughuli za
polisi inapingana na madai ya kuwepo kwa demokrasia yanayotolewa na serikali ya
Tanzania.”
Mheshimiwa Spika,
Sasa Taarifa
ya Uchunguzi wa Kifo cha Mwandishi wa Habari wa Channel Ten Bw. Daudi Mwangosi,
iliyoandaliwa na Kamati iliyoundwa na Mheshimiwa Nchimbi na kuchapishwa tarehe
9 Oktoba 2012 imethibitisha ukweli wa kauli hii na ukweli wa madai ya Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni juu ya matumizi ya nguvu ya Jeshi la Polisi. Baada ya
kuzunguka huku na huko ikijaribu kulisafisha Jeshi la Polisi, Taarifa ya Kamati
hiyo inasema: “Hapakuwepo na uhalali wa kutumia Bomu la Kishindo kwani lengo la
ulipuaji wake ni ili watu waogope na kukimbia.” Aidha, Kamati hiyo iliyoongozwa
na Jaji Mstaafu Stephen Ihema, inakiri kwamba “hapakuwepo umuhimu wa kutumia
Bomu la Kishindo kwa sababu hata ingekuwa ukamataji tayari askari polisi
wapatao sita walikuwepo eneo la tukio.” Kwa misingi hiyo, “… Kamati imeona
kwamba … tukio la kuuawa Bw. Daudi Mwangosi na kuumizwa baadhi ya askari polisi
halikustahili kabisa.”
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
Serikali itoe kauli kama inakubaliana na matokeo ya taarifa hizi tatu
zilizoandaliwa na taasisi za kiserikali kama vile Tume ya Haki za Binadamu,
Kamati ya Jaji Ihema na MCT/TEF juu ya kuhusika kwa Jeshi la Polisi na mauaji
ya marehemu Daudi Mwangosi. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
Serikali iteo kauli mbele ya Bunge lako tukufu kama inakubaliana na Taarifa ya
Tume ya Haki za Binadamu kwamba kitendo cha Kamanda Kamuhanda kupiga marufuku
mkutano halali wa CHADEMA kilikuwa ni kinyume cha Sheria ya Jeshi la Polisi,
Sheria ya Vyama vya Siasa na ukiukwaji wa haki za binadamu na misingi ya
utawala bora.
Vile vile, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inaitaka Serikali itoe kauli kama – baada ya ushahidi wa taarifa hizi tatu -
iko tayari kuiomba radhi CHADEMA kwa kuisingizia kuhusika na kifo cha marehemu
Daudi Mwangosi. Na mwisho, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali
itoe kauli mbele ya Bunge lako tukufu kama iko tayari kuilipa familia ya
marehemu Mwangosi fidia kwa mujibu wa sheria kwa kitendo cha Serikali
kusababisha mauaji yake bila ‘uhalali.’
Mheshimiwa
Spika,
Serikali
na chama ambacho sera zake zinakiuka haki za binadamu na misingi ya utawala bora
inapoteza uhalali (legitimacy) ya kuendelea kutawala. Hapa ndipo CCM na
Serikali yake ilikoifikisha nchi yetu: waandishi wa habari wanauawa kwa sababu
ya kufanya kazi yao halali ya kutafuta habari za mambo yanayohusu umma kama
mikutano ya vyama vya siasa. Watanzania hawastahili Serikali ya aina hii. Kama
alivyosema Baba wa Taifa katika kitabu chake Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania: “Hatulazimiki kuendelea na uongozi mbovu wa Chama na Serikali. Wala
tukiendelea na hali hii, bila kubadili uongozi wa Chama na Serikali, sina
hakika kama tutafika huko salama. Masuala muhimu ya nchi yetu
hayatashughulikiwa.... Na masuala mengine muhimu ... yataachwa yajitatue
yenyewe. Nasema katika hali kama hiyo sina hakika kama tutafika salama; na
tukifika salama tukiwa na uongozi huu huu wa Chama na Serikali mbele kutakuwa
ni giza tupu. Majuto ni mjukuu, huja baadaye.”
Mheshimiwa
Spika,
Baada
ya maelezo haya marefu, naomba kukushukuru na wewe binafsi na naomba
kuwasilisha.
---------------------------------------------------------------
Tundu
Antiphas Mughwai Lissu
MSEMAJI
& WAZIRI KIVULI, SHERIA, KATIBA NA UTAWALA
KAMBI RASMI
YA UPINZANI BUNGENI
[i] Kenya’s Quest for a Constitution: The Postponed Promised, The Jomo Kenyatta Foundation, Nairobi, 2008
Source: CHADEMA social media.
No comments:
Post a Comment