TAARIFA KWA UMMA
TAHADHARI LA TISHIO LA MLIPUKO WA UGONJWA WA KUPOOZA (POLIO)
Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii imepokea taarifa mnamo tarehe 22 Mei 2013
kutoka Shirika la Afya Ulimwenguni, (WHO) ya kuwepo kwa mlipuko wa
ugonjwa wa kupooza (Polio) katika Wilaya ya Fafi nchini Kenya. Mpaka
sasa kuna mgonjwa mmoja bila kifo.
Ugonjwa wa Polio ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na virusi vijulikanavyo kama “Polio Virus”.
Ugonjwa huu unaathiri misuli na mfumo wa fahamu hivyo kusabisha kupooza
kwa viungo hasa miguu na hata kifo. Ulemavu huu ukishajitokeza huwa ni
wa kudumu. Waathirika wakuu wa ugonjwa huu ni watoto hasa walio na umri
chini ya miaka mitano. Hata hivyo ugonjwa huu unazuilika kwa chanjo ya
Polio ambayo ni salama na inatolewa bure na Serikali katika vituo vyote
vya huduma ya afya. Mtoto aliyepata chanjo ya Polio anakuwa amekingwa na
ugonjwa wa Polio kwa maisha yake yote.
Kutokana
na taarifa hiyo ya kutoka nchini jirani ya Kenya, baadhi ya mikoa ina
uwezekano mkubwa wa kupata maambukizo ya ugonjwa huo kufuatia ushauri wa
kitaalam. Aidha, mikoa hii mingine inapakana na nchi jirani ya Kenya na
mingine ina mapungufu yaliyopo katika hali ya chanjo ya Polio. Mikoa
hii ni pamoja na Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Arusha, Manyara,
Kilimanjaro, Mara na Mwanza.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imechukua hatua zifuatazo katika kukabiliana na tishio la ugonjwa huu:
· Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya.
· Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipaka
· Kufuatilia kwa karibu hali ya chanjo mikoani na wilayani hususan ya Polio hususani iliyo katika hatari ya maambukizi
· Kuhamasisha
watoto ambao hawajakamlisha ratiba yao ya chanjo hususani ya Polio au
ambao hawajapata ya chanjo hii waweze kwenda vituo vya karibu vya afya
vya kutolea chanjo
Wizara
inapenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa Viongozi na Watendaji wa
ngazi zote kutoa ushirikiano ili kuhakikisha kila mtoto mlengwa anapata
chanjo ya Polio. Aidha Wizara inatoa rai kwa wadau wetu, taasisi za
dini, taasisi zinazofanya kazi katika jamii na vyombo mbalimbali
kuhamasisha watu wapeleke watoto wao kwenye vituo vya huduma wakapewe
chanjo hii muhimu. Chanjo hii ni salama na inatolewa bila malipo.
Wananchi wanashauriwa kutoa taarifa kwenye kituo cha huduma za afya kilicho karibu mara wanapoona au kupata taarifa
ya mtoto yoyote anayepata ulemavu wa ghafla pasipo sababu yoyote. Mtoto
huyo apelekwe katika kituo cha huduma za afya kwa uchunguzi na hatua za
haraka.
Imetolewa na;
Nsachris Mwamwaaja
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
30/05/2013
No comments:
Post a Comment