Friday, May 24, 2013

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHE . EZEKIAH DIBOGO WENJE (MB)

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHE . EZEKIAH DIBOGO WENJE (MB) KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI KWA MWAKA 2012/2013 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA AFRIKA MASHARIKI KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014


1.0       UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Jumuiya ya Afrika Mashariki imeundwa na Ibara ya 2(1) ya Mkataba wa kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki kufuatia makubaliano ya wakuu wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Aidha Ibara ya 8(3) (a) ya Mkataba wa kuanzishwa kwa  Jumuiya ya Afrika Mashariki imezipa mamlaka nchi wanachama kuanzisha Wizara mahsusi,  itakayoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki. Kwa mujibu wa ibara hiyo,  Tanzania, ilianzisha  Wizara ya Afrika Mashariki ambayo  majukumu yake ni pamoja utekelezaji wa Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mikataba Midogo (Protocols)  Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja la Afrika Mashariki  na Mazungumzo ya uundwaji wa Shirikisho la kisiasa la  Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika, ni mategemeo ya Watanzania kwamba, Wizara hii ya Afrika Mashariki italitendea haki taifa hili, kwa kuwashirikisha wananchi kwenye kila hatua na kwa kusimamia kwa dhati na kikamilifu michakato yote ya mtangamano wa Afrika Mashariki, kwa maslahi ya nchi yetu, ili kuhakikisha kwamba Tanzania inanufaika vilivyo na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani kipindi hiki itajielekeza kwenye mambo machache ambayo tunaamini yakizingatiwa, Jumuiya ya Afrika Mashariki itakuwa imara, na nchi zote wanachama watafurahia matunda ya jumuiya hiyo.
2.0 MADAI YA MAFAO YA WASTAAFU WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI ILIYOVUNJIKA 1977
Mheshimiwa Spika, madai ya mafao ya wazee wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki sasa ni aibu kwa Taifa. Wastaafu hawa wameyumbishwa kiasi cha kutosha, wamepuuzwa kiasi cha kutosha, wamedhalilishwa kiasi cha kutosha na wameonewa kiasi cha kutosha na serikali hii ya CCM inayojiita sikivu.  Hakika  laana ya wastaafu hawa wanaodhulumiwa haki yao wazi wazi namna hii  itaendelea kulitafuna taifa hili kwa kwa miaka mingi ijayo kama Serikali haitawatendea haki.
Mheshimiwa Spika, Baada ya Jumuiya hiyo kuvunjika ghafla tarehe 30 Juni, 1977 ulizuka mgogoro wa mgawanyo wa mali na madeni yake. Ili kuumaliza mgogoro huo, Umoja wa Mataifa uliiteua Benki ya Dunia kusuluhisha mgogoro huo. Benki ya dunia ilimteua mtaalamu wake, mwanadiplomasia, Dkt. Umbricht (sasa marehemu) ambaye alifanikisha kuwanzishwa kwa Mkataba wa Kimataifa uliojulikana kama “East African Community Mediation Agreement 1984” kuhusu mgawanyo wa mali na madeni ya Jumuiya yakiwemo mafao ya wafanyakazi wa Jumuiya hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa tulizo nazo, kazi kubwa aliyofanya msuluhishi, Dkt. Umbritch ilikuwa ni kuzigawanya fedha za pensheni na provident funds za Jumuiya kwa nchi tatu wanachama yaani Kenya, Uganda na Tanzania kulingana na idadi ya raia wake katika Jumuiya, kwa madhumuni ya kuwalipa mafao raia wake. Katika mgawo huo, Tanzania ilikabidhiwa paundi za Uingereza milioni 14 kwa ajili ya kulipa mafao ya wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza bunge hili na wananchi wote fedha hizo zilitumika kufanyia nini­ kama walengwa hawakulipwa mafao yao?
Mheshimiwa Spika, nchi za Kenya na Uganda tayari zilishawalipa wastaafu wa Afrika ya Mashariki stahili zao na hali huko ni shwari, lakini kwa Tanzania jambo hili limegubikwa na wingu zito la ufisadi kwa kuwa fedha ya kuwalipa wastaafu hao ilishatolewa. Kwanini wastaafu hao hawakulipwa, na wale waliolipwa, walipewa cheki za silingi 10 na shilingi 130 za kitanzania jambo ambalo ni aibu na fedheha kwa Serikali hii ya CCM inayojiita sikivu kwa wananchi wake.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali hii ya CCM inayojiita sikivu, kutoa tamko leo,  mbele ya bunge hili kuhusu mafao ya wastaafu hao ili wajue moja: kama wanalipwa au hawalipwi. Kama Serikali haitatoa tamko leo,  kuhusu unyanyasaji wanaofanyiwa wastaafu wa Afrika Mashariki, basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni italazimika kuleta hoja binafsi bungeni kwa hatua za kibunge kuhusu mafao ya wastaafu wa iliyokuwa Afrika Mashariki.


3.0 SARAFU YA PAMOJA
Mheshimiwa Spika,  katika  hotuba ya  bajeti ya Wizara ya Afrika Mashariki kwa mwaka wa fedha 2012/2013, Kambi Rasmi ya Upinzani ilinukuu sehemu ya hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa wakati wa uzinduzi wa Bunge la Kumi tarehe 18 Novemba, 2010 kwamba mchakato wa kuanzisha Umoja wa Sarafu ulikuwa ukiendelea kwa kasi na kwamba  ulikuwa unategemewa kukamilika mwaka 2012. 
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuhoji hatua iliyofikiwa katika kuanzisha umoja wa Sarafu kwa mwaka ule wa 2012/2013,  Kambi Rasmi ya Upinzani vilevile iliitaka Serikali kulieleza Bunge kama ilikuwa imefanya utafiti wa kina juu ya suala hilo kwa kuwa tayari kulikuwa na mvutano  katika  nchi za Jumuiya ya Ulaya kuhusu kujiunga na umoja huo au kutojiunga nao.
Mheshimiwa Spika, mgogoro uliopo katika “EURO ZONE” ni kwamba;  pamoja na kuwa na sarafu moja ya “EURO”  bado kuna   nchi wanachama ambao wanaendelea kutumia sarafu yao, lakini pia kuna nchi nyingine zinaonekana kuwa mzigo katika umoja huo wa EURO kama ilivyo Ugiriki.
Mheshimiwa Spika, Tarehe 28 Aprili mwaka 2013, wakuu wa nchi za Afrika Mashariki, akiwemo Rais Kikwete walikutana Arusha na kuagiza pamoja na mambo mengine, kusainiwa kwa mkataba wa sarafu ya pamoja kabla ya mwezi Novemba 2013.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaihoji Serikali kwa mara nyingine tena, hivi imefanya utafiti wa kina na kujiridhisha kwamba umoja huu wa sarafu hautakumbwa na dhoruba kama ilivyotokea kwa umoja wa sarafu wa nchi za Jumuiya ya Ulaya (Eurozone)? Pili, kwa kuwa shilingi ya Tanzania imekuwa ikishuka thamani dhidi ya shilingi ya Kenya na Faranga ya Rwanda, na kwa kuwa kuna tofauti kubwa za hali ya uchumi baina ya nchi wanachama huku Tanzania ikiwa nyuma ukilinganisha na nchi nyingine za Jumuiya, Je, kuna mkakati gani wa kuimarisha hali ya uchumi wetu ili tusiburuzwe katika Shirikisho?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haipingi kuwa na Umoja wa Sarafu (Monetary Union), lakini inataka kama taifa, tuwe na maandalizi ya kutosha na tukidhi vigezo ili tusiwe mzigo au watumwa katika umoja huo. Hii ni kwa sababu kila nchi mwanachama inataka kutumia fursa za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuimarisha uchumi wake wa ndani, na kwa maana hiyo kama hatutakuwa na maandalizi ya kutosha, tutaishia kuwa soko la bidhaa za wenzetu.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa angalizo kwa Serikali, isiharakishe kusaini mkataba wa sarafu ya pamoja. Serikali iweke nguvu zaidi katika kujenga uchumi wa ndani. Serikali ikipuuzia ushauri huu, kuna kila dalili kwamba Tanzania itakuwa nyenzo ya kujenga uchumi wa nchi nyingine wanachama na yenyewe ikibaki kama mzalishaji wa malighafi ya kulisha viwanda vya wenzetu na kuwa soko la bidhaa zao kama ilivyokuwa enzi za ukoloni. Jambo hili likitokea ni kwamba matumaini ya Kauli Mbiu ya Serikali ya Tanzania ya “Maisha bora kwa kila Mtanzania” itakuwa imezikwa.
4.0 WABUNGE WA AFRIKA MASHARIKI
Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya bajeti ya Wizara hii mwaka 2012/2013, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilishtushwa sana na maamuzi mazito yanayofanywa, sheria mbalimbali zilizotungwa, na maridhiano na mikataba mbalimbali inayofanywa na Bunge la Afrika Mashariki bila bunge letu kuwa na taarifa. Miongoni mwa mikataba iliyoridhiwa na bunge la Afrika Mashariki na sheria mbali mbali zilizotungwa bila bunge letu kuwa na taarifa rasmi ni kama ifuatavyo:
i.                    Jumuiya ilisaini  mkataba na Jumuiya ya wafanya biashara wa Uturuki chini ya umoja unaojulikana kama “Africa-Turkey Partinership” mkataba ambao ulitegemewa kuingiza zaidi ya dola za kimarekani 350 bilioni kutokana na biashara mbalimbali.
ii.                  Uandaaji wa sheria ya kuthibiti uhalifu wa kimtandao “cyber laws”
iii.                Uandaaji wa itifaki ya pamoja kuhusiana na kuwa na kituo kimoja cha utalii “Single Tourist Destination Protocol” na uwepo wa hati ya kusafiria na visa moja ya utalii “Single Tourist Visas” kwa nchi wanachama wa Jumuiya.
iv.              Kuandaa mfumo mmoja wa mitaala ya elimu ili kuweza kukidhi haja ya soko la pamoja la ajira la Jumuiya.
v.                Kusainiwa makubaliano ya pamoja (MOU) juu ya ushirikiano wa masuala ya kiulinzi.
vi.              Kuanzishwa kwa umoja wa wafanyabiashara wa samaki ukanda wa Ziwa Victoria “The Lake Victoria Fisheries Organization” (LVFO)  ambacho ni chombo chenye mamlaka juu ya usimamizi wa shughuli zote za uvuvi katika ziwa Victoria
vii.             Kuandaliwa kwa miswada mbalimbali ya sheria ambayo inasubiri kupitishwa kuwa sheria: Miswada hiyo ilikuwa ni:
The East African Community Human and Peoples’ Rights Bill, 2012;
The East African Legislative Assembly Elections Bill, 2011;
The East African Customs Management (Amendment) Bill, 2012;
The East African Community Trans-Boundary Ecosystems Management Bill, 2010;
The East African Community Polythene Materials Control Bill, 2011;
The East African Community Elections Bill, 2012;
The Administration of the East African Legislative Assembly Bill, 2011; na
The East African Parliamentary Institute Bill, 2011.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani iliona kwamba ni busara mambo haya yakawa wazi kwa bunge letu na kwa wananchi wote pia, kwa kuwa ni maamuzi na sheria ambazo zitakuwa na athari ya moja kwa moja kwa nchi yetu kama vile kusimamia chaguzi zetu, Majeshi yetu, Rasilimali zetu kama samaki wa ziwa Victoria, utalii, elimu yetu, na maisha yetu kwa jumla.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia uzito wa jambo hili, na ili kuhakikisha kwamba nchi yetu inapata taarifa muhimu na kushiriki kikamilifu kila hatua katika michakato mbalimbali ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kambi ya upinzani Bungeni, ilipendekeza mambo yafuatayo:
i.        Kuundwa kwa Kamati Mpya ya Kudumu ya Bunge ya Afrika Mashariki, ambayo itakuwa inapokea na kujadili miswada , itifaki   na mwenendo mzima wa Jumuiya na iwe na wajibu wa kutoa taarifa yake kwenye vikao vya Bunge mara kwa mara ili Bunge letu liweze  kuzijadili na kuishauri serikali kikamilifu. Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilishauri Kamati hiyo iwe na jukumu la kushughulikia nidhamu ya Wabunge wa Afrika Mashariki.
ii.      Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni pia ilipendekeza Pawepo na vikao vya pamoja baina ya wabunge wa Bunge la Afrika mashariki wanaotoka Tanzania na Kamati ya Afrika Mashariki (itakayoanzishwa) ili kuweza kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusiana na utendaji wao wa kazi na masuala mbalimbali ya Jumuiya.
iii.     Vilevile Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilipendekeza uwepo  utaratibu wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na kila hatua ambayo imefikiwa kuelekea kwenye Shirikisho la Afrika Mashariki  ili kuepusha kuwa na Jumuiya ya viongozi peke yao na badala yake iwe ni Jumuiya ya wananchi kwani watakuwa na taarifa za kina kuhusiana na kila hatua iliyofikiwa.
iv.  Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni pia ilipendekeza kuwa, kabla ya itifaki mbalimbali kuridhiwa na Bunge la Afrika Mashariki,  ni vema wabunge wa Afrika Mashariki wakishirikiana na Wizara ya Afrika Mashariki  kuziwasilisha itifaki hizo, kwenye Bunge letu ili ziweze kujadiliwa na kupitishwa au kukataliwa na Bunge kama ambavyo tumekuwa tukifanya kwa maazimio, mikataba na itifaki  za Kimataifa.
Mheshimiwa Spika, Waziri wa Afrika Mashariki alikubaliana na mapendekezo haya wakatika akifanya majumuisho ya hoja yake ya bajeti ya wizara ya Afrika Mashariki 2012/2013. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inachotaka kujua sasa ni hatua gani imefikiwa katika utekelezaji wa mapendekezo hayo? Aidha, tunatambua kuwa kamati ya Bunge ya mambo ya nje ndio imekuwa na jukumu la kusimamia masuala yote yahusuyo Afrika Mashariki.
4.1  Uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ibara ya 50 ya mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mabunge ya nchi wanachama wana haki ya kuchagua wabunge wa wa Bunge la Afrika Mashariki.  Aidha, ibara hiyo imeelezea utaratibu wa jinsi ya kuwapata wabunge hao kuwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa wabunge hao wanawakilisha makundi mbalimbali kama vile uwiano wa vyama vya siasa vyenye uwakilishi Bungeni, jinsia na makundi mengine maalum.
Mheshimiwa Spika,  kutokana na ibara hiyo  ya 50 (1)  kutoa haki  kwa mabunge ya nchi wanachama kuweka utaratibu wa kufuatwa katika kuwachagua wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki, jambo hili  limetoa mwanya kwa kila nchi kuweka utaratibu wake wa ndani ambao hauheshimu ibara hii kama ambavyo Tanzania na Uganda walivyofanya, kwa kuhakikisha kuwa vyama vikuu vya Upinzani katika mabunge yao, yaani CHADEMA kwa Tanzania, na FDC kwa Uganda  hawana uwakilishi, pamoja na ukweli kuwa ndio vyama vya upinzani  vyenye wabunge wengi kwenye mabunge ya nchi zao.
Kambi rasmi ya upinzani, inaitaka serikali kuwasilisha mapendekezo ya mabadiliko ya vifungu vya mkataba kwenye Jumuiya na kuweka kifungu cha adhabu ya moja kwa moja kwa nchi mwananchama ambaye kwa makusudi anakiuka baadhi ya ibara za mkataba huu ili liwe fundisho kwa kila mmoja kuheshimu mkataba huu.
Aidha, tunataka pawepo na utaratibu wa kufanana katika Jumuiya linapokuja zoezi la kuchagua wabunge hao katika nchi wanachama ili kuondoa udhaifu wa Mabunge husika kutokutenda haki.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuitaka Serikali kutekeleza mapendekezo haya, bado Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kwamba uwakilishi wa Bunge la Afrika Mashariki kwa wananchi ni mdogo sana au pengine haupo kabisa. Kimsingi Bunge la Afrika Mashariki linawakilisha mabunge ya nchi wanachama ambayo ndiyo yaliwapigia kura wabunge wa Afrika Mashariki. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inakubaliana na ripoti ya timu ya wataalamu ya Oktoba 2011 (Report of the team of Experts on addressing the Fears, Concerns and Challenges of the East African Federation) kuhusu hofu na changamoto za kujiunga na shirikisho la Afrika Mashariki kwamba wabunge wa Afrika Mashariki wawe wanachaguliwa na wananchi moja kwa moja.  Hata hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri utaratibu huo ufanyike tutakapokuwa kwenye shirikisho kamili la kisiasa .
5.0 HOFU NA CHANGAMOTO ZA KUJIUNGA NA SHIRIKISHO LA AFRIKA MASHARIKI
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa taarifa ya timu ya wataalamu juu ya kutoa ufumbuzi wa hofu, na changamoto zinazozikabili nchi wanachama katika  kuelekea Shirikisho la Kisisasa la Afrika Mashariki ya Oktoba, 2011, ni kwamba,  pana hofu kubwa miongoni mwa wananchi wa nchi wanachama kuhusu mchakato wa  kuingia kwenye Shirikisho la Afrika Mashariki kwa sababu mbali mbali kama ifuatavyo:
                             i.        Kupoteza Mamlaka ya Dola kwa nchi husika.
Mheshimiwa Spika, taarifa ya wataalamu inaweka bayana kwamba ili shirikisho la kisiasa liwepo lazima kutakuwa na  kupotea kwa kiwango fulani cha mamlaka ya Dola (Sovereignty) lakini taarifa hiyo inashauri kwamba watu waangalie mbele ya pazia la “upofu wa mamlaka” (beyond the curtain of power blindness) na kuona faida na fursa nyingi zitakazopatikana kutokana na shirikisho hilo. Ili kuondoa hofu hii, Jumuiya ya Afrika Mashariki inashauriwa kukamilisha kwa ufanisi itifaki na michakato yote ya mwanzo kuelekea kwenye shirikisho,  ili nchi wanachama weweze kuona faida halisi (tangible benefits) za Jumuiya kwa hali ilivyo sasa, ili kuwaondolea nchi wanachama na wananchi wao woga wa kuingia katika shirikisho la Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza bunge hili kwamba Tanzania imenufaika kwa kiasi gani kwa hatua ya sasa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuwaondolea hofu wananchi ya kuingia katika Shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika, mambo mengine yaliyotajwa kuleta hofu miongoni mwa wananchi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kuelekea kwenye Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki, ni pamoja na mfumo wa Utawala (Governance) baada ya shirikisho. Taarifa hiyo ya timu ya wataalamu ilishauri kwamba ili kuondoa hofu hiyo kila nchi mwanachama iandae ‘utaratibu wa kikatiba’ wa kutambua maandalizi ya shirikisho hilo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua kuwa mchakato wa kupata katiba mpya unaendelea ila tunasikitishwa na kitendo cha serikali kutokuitoa ripoti hii mapema ili wananchi waweze kuelimishwa kuhusiana na pendekezo hili katika kuta maoni yao kwa tume ya Katiba. Aidha tunaitaka wizara na Serikali kulielieleza bunge hili, imewaelimisha wananchi kwa kiwango gani ili kutoa maoni juu ya mfumo wa utawala wa Shirikisho la Afrika Mashariki katika mchakato katiba mpya unaoendelea?.
                           ii.        Hofu ya Kukosa Ajira kutokana na Mitaala na Viwango  Tofauti vya Elimu na Taaluma   
Mheshimiwa Spika, taarifa ya timu ya wataalamu imebaini kwamba tofauti ya mitaala ya elimu na viwango vya ubora wa elimu miongoni mwa nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki imesababisha kutokuwa na uwiano na fursa sawa za ajira hasa kwa nchi ambazo zina uwezo mdogo wa rasilimali watu,  jambo ambalo linalowatia hofu wananchi wa nchi hizo kuingia katika Shirikisho.
Mheshimiwa Spika, ili kuondokana na hofu hiyo, Jumuiya ya Afrika Mashariki imeshauriwa kwamba ianzishe uratibu wa kuwa na mitaala ya elimu inayofanana ili kuondoa ubaguzi wa vigezo vya kielemu katika fursa za ajira katika Shrikisho la Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilipendekeza katika bajeti ya Wizara hii kwa mwaka wa fedha unaomalizika 2012/2013 kuhusu kuanzishwa kwa mfumo mmoja wa Elimu Afrika Mashariki ili kuondoa ubaguzi kutokana na tofauti ya mitaala na viwango vya ubora wa elimu katika fursa za ajira. Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilipendekeza kuwa kuwe na mfumo wa pamoja wa udahili kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, ili mwanafunzi mwenye sifa ya kujiunga na chuo kikuu awe na uhuru wa kuchagua chuo chochote ndani ya Jumuiya Afrika Mashariki na adhaminiwe na bodi ya mikopo kutoka nchini mwake.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali hii ya CCM kulieleza bunge hili kuwa imefanya jitihada zipi ikishirikiana na nchi wanachama kuanzisha mfumo mmoja wa elimu ili kuwaondolea hofu wananchi wetu kuhusu unyanyapaa katika ajira unaotokana na tofauti za kielimu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali kuhimiza Baraza la  Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki ( The East African Universities Council) liwezeshwe ili liweze kuendesha udahili kwa wanafunzi wanaotaka kujiunga na chuo kikuu chochote katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, na kuwa kiungo kati ya  tume za vyuo vikuu na bodi za mikopo za nchi wanachama ili kuwawezesha wanafunzi wa vyuo vikuu katika Jumuiya kupata elimu kwa uhuru na bila bugudha.
6.0 SEKTA YA BIASHARA NA UWEKEZAJI
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kukuza uchumi wa nchi yetu, Tanzania inajitahidi kuvutia wawekezaji wa nje. Ili kufikia malengo ya kuvutia wawekezaji wengi kadiri iwezekanavyo, Serikali inatoa motisha mbalimbali ikiwemo misamaha ya kodi . Hata nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki halikadhalika zinafanya vivyo hivyo . Kwa mantiki hiyo, kunakuwa na ushindani mkubwa baina ya nchi wanachama wa Afrika Mashariki kutoa misamaha ya kodi kwa wingi ili kuwavutia wawekezaji.
Mheshimiwa Spika, japo kanuni za uchumi wa kisasa zinaongozwa na nguvu ya soko ambayo msingi wake ni ushindani katika ubora wa bidhaa na huduma, Kambi Rasmi ya Upinzani haioni wala haishawishiki kama ushindani katika kutoa misamaha ya kodi una tija katika kujenga uchumi imara. Hii ni kwa sababu rahisi kabisa kwamba: “ni ushindani unaopoteza mapato”
 Mheshiwa Spika, twakwimu zilizopo ni kwamba: Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi kwa pamoja zinapoteza Dollar za Kimarekani bilioni 2.8[1]  kila mwaka kutokana na mashindano ya msamaha wa kodi ili kuvutia wawekezaji. Kambi Rasmi ya Upinzani haiungi mkono jambo hili kwani ni mashindano ya kuwania nafasi ya kwanza ya kuwa masikini na fukara zaidi jambo ambalo halikubaliki.
Mheshimiwa Spika, ili kuondokana na hasara hii kubwa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kuanzishwa kwa kituo cha Uwekezaji cha Afrika Mashariki (The East African Investment Center) kitakachoratibu viwango vya motisha wa kodi (tax incentives) kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuweka uwiano wa viwango hivyo na kuepusha upotevu wa mapato kama ilivyo sasa.
          6.1. Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika, Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki ni taasisi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya zamani ambayo haikuvunjika wakati jumuiya hiyo ilipovunjika mwaka 1977. Pamoja na kuendelea na shughuli zake kwa muda mrefu, benki hii haionekani kama ina nguvu kiuchumi na mchango wake katika maendeleo ya kiuchumi ya Afrika mashariki hali kadhalika hauonekani.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ya Tanzania kuzishawishi nchi wanachama kuwekeza katika benki hii kwa kuichangia fedha na kuiombea mikopo kutoka benki ya dunia au Shirika la Fedha Duniani ili kuipa nguvu benki hii na kuifanya iweze kutoa mikopo ya riba nafuu kwa nchi wanachama na pia kugharamia miradi ya maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
7.0 UTALII WA PAMOJA
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kumekuwa na malalamiko mengi toka kwa makampuni ya utalii na hata  kwa watalii wenyewe kutokana na kulipa pesa nyingi kwa ajili ya viza za kutoka nchi moja na kuingia nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa madhumuni ya utalii,   na kwa kuwa kutokana na tatizo hilo watalii wengi wanachagua kufanya utalii wao Kenya zaidi kwa kuwa kuja Tanzania kutawalazimu kulipa gharama zaidi za viza  jambo ambalo linaikosesha Tanzania mapato yatokanayo na utalii, na kwa kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ilishaanza mchakato wa kuandaa itifaki  ya pamoja ili kuwa na kituo kimoja cha utalii “Single Tourist Destination Protocol” na uwepo wa hati ya kusafiria na visa moja ya utalii “Single Tourist Visas” kwa nchi wanachama wa Jumuiya, Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuhimiza ukamilishaji wa haraka wa mchakato huo wa kuwa na utalii wa pamoja ili kuondoa adha iliyopo sasa hivi ya watalii kutembelea nchi moja zaidi na nyingine kukosa mapato.
8.0 BIASHARA HARAMU YA PEMBE ZA NDOVU AFRIKA YA MASHARIKI
Mheshimiwa Spika, biashara haramu ya pembe za ndovu katika ukanda wa Afrika ya Mashariki inakuwa kwa kasi sana jambo ambalo linatishia kutoweka kabisa kwa wanyama hao ambao ni kivutio kikubwa cha utalii. Taarifa katika mtandao wa habari wa “Annamiticus” (www.annamiticus.com) zinasema kwamba mwaka jana 2012, makontena mawili kutoka Kenya na Tanzania yalikamatwa huko HongKong yakiwa yamebeba tani 4 (Kilo 4,000) za pembe za ndovu.  
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa hiyo, kontena lililotoka Tanzani lilikuwa limeandikwa “plastic scrap” ikimaanisha kuwa lilikuwa na vifaa ya plastiki lakini baada ya kufunguliwa kulikuwa na vipande 972 vya pembe halisi za ndovu zenye uzito wa kilogramu 1,927 pamoja na kilo moja na nusu ya unga wa pembe za ndovu zilizosagwa. Kontena lililotoka Kenya lilikuwa limeandikwa “roscoco beans” yaani maharage aina ya roscoco, lakini lilipofunguliwa kulikuwa na vipande 237 vya pembe za ndovu sawa na kilogramu 1,884.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa hiyo, wingi wa pembe hizi za ndovu zilizokamatwa, unadhihirisha kwamba tembo 600 kwa uchache waliuwawa.
Mheshimiwa Spika,  mwezi uliopita   kontena lingine limekamatwa lililosheheni pembe za ndovu 113 huko China zenye thamani ya Dola za Kimarekani 400,000. Kontena hili liliandikwa kwamba limebeba vipuri (spareparts) toka Burundi .
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Burundi haina bandari, kuna uwezekano mkubwa kwamba kontena hilo lilipitia bandari ya Tanzania, na hivyo kuna uwezekano pia kwamba pembe hizo zinatokana na tembo waliouwawa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua kama Serikali ya Tanzania imefanya mawasiliano na Serikali ya Burundi ili kujua ukweli kuhusu kontena lililosheheni pembe za ndovu lililokamatwa huko China. Hii ni kwa kuzingatia utekelezaji wa  Mpango Mkakati wa Amani na Usalama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (The Strategy for Regional Peace and Security) wa kubadilishana taarifa za uhalifu na usalama.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kuna watanzania walioshutumiwa na kusutwa kuhusika na mtandao huu wa biashara hii haramu ya pembe za ndovu  akiwemo Katibu Mkuu wa CCM, ndugu Abdulrahman Kinana, na kwa kuwa Serikali ya Tanzania inaonekana dhahiri kumtetea na kumlinda mtu huyu kwa kuwa ni kiongozi mkubwa wa chama tawala, kama alivyofanya waziri wa mambo ya ndani Mhe. Emmanuel Nchimbi alipokuwa anatoa mchango wake kwenye bajeti ya wizara ya maliasili na utalii mnamo tarehe 30.04.2013, na kwa kuwa tembo wengi wa Afrika Mashariki wanazidi kupotea kila siku kutokana na biashara hii haramu ya pembe za ndovu jambo ambalo linaikosesha Jumuiya ya Afrika Mashariki mapato yatokanayo na utalii na hivyo kuiweka hatarini sekta ya utalii ya Afrika Mashariki.
Na  kwa kuwa Waziri wa mambo ya ndani Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi alipokuwa anachangia hotuba ya Maliasili na utalii na kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi za Bunge (Hansard) alisema kuwa kesi Na.3 na 4 ya mwaka 2009 kuhusu pembe za ndovu na meli iliyokamatwa Vietnam iliyokuwa mahakama ya Kisutu ilifutwa kutokana na Tanzania kutokuwa na mkataba wa kubadilishana wahalifu na Vietnam na hivyo kukosekana kwa ushahidi Mahakamani, (hansard ya tarehe 30.04.2013, uk.141) .
 Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inamtaka Mwendesha Mashtaka wa Jumuiya ya Afrika Mashariki  kumfungulia mashtaka ndugu Abdulrahman Kinana katika mahakama ya Afrika Mashariki kwa madhumuni ya kuubaini na kuudhibiti mtandao wa majangili na wafanya biashara haramu ya pembe za ndovu katika ukanda huu wa Afrika ya Mashariki kutokana na Meli anazosimamia kama wakala wa meli mojawapo kukamatwa na shehena za pembe za ndovu huko Vietnam mwaka 2009.
Aidha, tunaitaka serikali iombe msaada kutoka nchi mwanachama ya Kenya ambayo ina ubalozi wa Vietnam ili kurahisisha upatikanaji wa ushahidi badala ya kutegemea ubalozi wetu ulioko China kama ilivyosemwa na hivyo kesi hii iweze kuendelea ili wahujumu hawa wa uchumi  na washirika wao waweze kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria.
9.0 UHURU WA VYOMBO VYA HABARI AFRIKA YA MASHARIKI
Mheshimiwa Spika, sasa hivi kumezuka wimbi la kukandamiza uhuru wa habari katika ukanda wa Afrika Mashariki. Matukio ya kuvifungia vyombo vya habari, na kuwadhuru waandishi wa habari kwa sababu za kulinda maslahi ya watawala yanazidi kuongezeka kwa kasi kubwa katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ya tarehe 20 Mei, 2013, Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameamuru kufungiwa kwa gazeti la kila siku la nchi hiyo la “The Daily Monitor”, na gazeti lingine la “Red Pepper” kwa kuchapisha habari iliyofichua njama za Rais Museveni za kumuandaa mtoto wake Muhoozi Kainerugaba ambaye ni brigedia wa jeshi la nchi hiyo kuwa Rais wa nchi hiyo baada ya yeye kuondoka madarakani. Katika sakata hilohilo, redio mbili za Dembe FM na KFM zilivamiwa na askari polisi zaidi ya 50 wenye silaha na kuamrisha kufungwa kwa vituo hivyo kwa madai kwamba vipo katika eneo moja na ofisi za magazeti yaliyofungiwa.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Tanzania hakuna asiyejua jinsi tasnia ya habari inavyodhibitiwa ili kulinda maslahi ya wakubwa. Licha ya kufungia gazeti la ki-uchunguzi la Mwanahalisi kwa muda usiojulikana kwa kusema ukweli, watanzania pia wameshuhudia waandishi wa habari wakitekwa, kuteswa na hata kuuwawa huku serikali  ikiwaachia huru baadhi ya maafisa wake walioshiriki katika unyama huo wakiendelea na kazi katika ofisi za serikali.  Jambo hili limeichafua taswira ya nchi yetu mbele ya Jumuiya na mbele ya ulimwengu.
Mheshimiwa Spika,  matukio haya ya kufungiwa na kuumizwa na kuuwawa kwa waandishi wa vyombo vya habari ndani ya Jumuiya ya Afrika yasiposhughulikiwa sasa, yataongeza hatari na hofu ya wananchi kutoka nchi wanachama na hivyo kupinga  kuingia katika Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki .
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka Serikali na wizara hii kulieleza Bunge na watanzania nini kauli yake na msimamo wake kuhusiana na suala la uhuru wa vyombo vya habari na usalama wa wanahabari ndani ya Jumuiya hii ya Afrika Mashariki.
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inapendekeza kuwa kutokana na tishio hili la uhuru wa habari na wanahabari katika nchi wanachama wa Jumuiya ni vyema sasa tukawa na itifaki ya pamoja “Protocol” na sheria moja ya kusimamia uhuru na haki ya kupata habari ndani ya Jumuiya ili kuzuia serikali na viongozi wasiopenda kukosolewa ndani ya Jumuiya kuwa na haki ya kuvifungia vyombo vya habari kwa kutumia sheria kandamizi za nchi wanachama, hii ni hatua muhimu sana katika kuelekea kwenye Shirikisho la Afrika ya Mashariki.
 10.0 ITIFAKI MBALIMBALI ZA USHIRIKIANO WA KIKANDA
Mheshimiwa Spika, bila shaka wananchi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wanataka kuona matunda ya ushirikiano na sio kuona utitiri wa taasisi na itifaki mbalimbali zinazoanzishwa bila mafanikio.
Mheshimiwa Spika, hotuba ya Waziri wa Afrika Mashariki ya mwaka 2012/2013 ilitaja itifaki na mikakati  kadhaa ya ushirikiano wa kikanda.  Itifaki na mikakati hiyo ni pamoja na Mkakati wa Kikanda wa kusimamia amani na usalama, uwianishaji wa shughuli za kipolisi, kupambana na madawa ya kulevya, mapambano dhidi ya ugaidi, itifaki ya amani na usalama, itifaki ya ushirikiano katika ulinzi, mazoezi ya pamoja ya kijeshi na ushirikiano katika siasa.
Mheshimiwa Spika, pamoja na utitiri huu wa mikakati na itifaki, bado Afrika ya Mashariki imekuwa mhanga (victim) mkubwa wa matukio ya kigaidi, biashara haramu ya madawa ya kulevya, biashara haramu ya pembe za ndovu.  Kambi Rasmi ya Upinzani ya Upinzani inataka kujua kama itifaki na mikakati hiyo ina nia ya dhati ya kukabiliana na matatizo yaliyotajwa au  ni miradi ya ulaji ya wakubwa na kuanzisha nafasi za ajira kwa watoto wa wakubwa bila ufanisi wa vyombo hiyo.
11.0 UTEKELEZAJI WA SHERIA KATIKA JUMUIYA
Mheshimiwa Spika, shirikisho la Afrika Mashariki limesababisha mwingiliano wa kijamii katika nchi wanachama kwa kiwango kikubwa ambapo raia wa nchi wanachama wana fursa ya kuoana na kuanzisha familia. Tatizo linaloibuka katika mahusiano haya ni kwamba hakuna utaratibu wa utekelezaji wa hukumu iliyotolewa katika nchi moja mwanachama katika nchi nyingine  mwanachama kuhusu masuala ya ndoa, talaka wala malezi ya watoto.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, sheria ya utekelezaji wa hukumu katika nchi jirani (The Judgement Extension Act) haihusishi hukumu zinazohusu mambo ya ndoa, talaka wala  malezi ya watoto na hivyo kutoa wakati mgumu kwa wananchi wanapotaka kukazia hukumu kwenye nchi wanachama za Kenya na Uganda. Mbaya zaidi ni kwamba, sheria hiyo haina kabisa mamlaka katika nchi nyingine wanachama za Jumuiya kama vile  Rwanda na Burundi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo imepelekea wananchi katika nchi wanachama kukosa haki zao na hasa kuhusiana na mambo ya ndoa , malezi na hata haki za watoto inapotokea kuwa mzazi mmojawapo anatokea nchi nyingine na wanapokuwa ama wamekosana na kutalikiana na mmojawapo kuamua kurejea kwenye nchi yake zile haki za mhanga zinakuwa zimepotelea ama kuishia hapo kwani hawezi kwenda kukazia hukumu huko kwa mujibu wa sheria na hii imeleta usumbufu mkubwa sana kwa wananchi wetu waliooa ama kuolewa katika nchi wanachama .
 Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwana CHADEMA inataka kujua Serikali na wizara ina mpango gani wa kuondoa utata huu wa kisheria ili haki za kifamilia ziweze kulindwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya kambi rasmi ya upinzani Bungeni naomba kuwasilisha.
………………………………..........................
Raya Ibram Khamis (Mb)
Kny. MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
WIZARA YA AFRIKA MASHARIKI
24 Mei, 2013

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...