SIKU moja
baada ya serikali kufuta matokeo ya mtihani wa kidato cha nne na kuamuru
yaandaliwe upya, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ameshangaa kuona Waziri Kawambwa hajiuzulu na
ametaka wazazi wa wanafunzi waliojinyonga kwa matokeo hayo walipwe
fidia.
Wakati
akitaka wanafunzi hao walipwe fidia, pia Mbatia alimshangaa Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, akihoji anasubiri nini
kung’atuka wakati kuna wanafunzi wamepoteza maisha kwa uzembe wao.
Alisema
Kawambwa anapaswa kujiuzulu kwani Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani
nchini, Joyce Ndalichako, hawezi kufanya mabadiliko makubwa ya aina hiyo
bila kuishirikisha wizara.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana mjini hapa, Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa
kuteuliwa alisema serikali imekuja na majibu rahisi kwenye jambo gumu,
kwani uamuzi wa kufuta na kuandaa upya matokeo hayo kwa utaratibu wa
mwaka 2011, hauleti ufumbuzi wa mfumo wa elimu.
“Tume
imekuja na majibu mepesi sana kwenye tatizo kubwa. Wanafunzi wamejiua
kwa msongo wa mawazo, wengine wamekata tamaa na kuamua kuolewa, wengine
kupata ujauzito, leo kwa uzembe wao wanataka kuwafaulisha wanafunzi ili
kupata sifa kisiasa, haiwezekani,” alisema.
Akichambua
maoni ya tume hiyo, alisema imeibua hoja ambazo yeye aliziwasilisha
bungeni kupitia hoja yake binafsi ambayo ilizimwa na wabunge wa CCM kwa
sababu za kulinda masilahi ya chama chao.
Alilishambulia Bunge kuwa limekuwa chanzo cha matatizo mengi kutokana na ubinafsi wa vyama bila kujali masilahi ya taifa.
“Bunge
linaangamiza taifa kwa sababu ya itikadi. Hizi itikadi za vyama
zinaliangamiza taifa. Kuna umimi, ubinafsi kwenye mambo ya masilahi ya
taifa. Nawataka wabunge watoke usingizini,” alisema Mbatia.
Juzi serikali ilitangaza kufuta matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2012 na kuagiza yaandaliwe upya.
Uamuzi huo mgumu ulitangazwa bungeni na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
Akisoma
tamko hilo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Lukuvi alisema
uamuzi huo wa serikali umetokana na mapendekezo ya tume ya waziri mkuu
iliyoundwa kuchunguza chanzo cha matokeo ya kidato cha nne mwaka jana
kuporomoka kwa kiwango cha kutisha.
Matokeo ya
mitihani ya kidato cha nne mwaka 2012 yalionesha kuwa kiwango cha ufaulu
kimeshuka kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miaka ya hivi karibuni.
Matokeo
yaliyotangazwa hivi karibuni, yalionesha kwamba kati ya wanafunzi
367,756 waliofanya mtihani huo, watahiniwa 126,847 ndio waliofaulu.
Katika idadi
hii, wanafunzi waliofaulu katika daraja la kwanza hadi la tatu ni
23,520, sawa na asilimia 6.4 na daraja la nne ni 103,327, sawa na
asilimia 28.1.
Watahiniwa
240,909, sawa na asilimia 65.5 ya wanafunzi wote, waliofanya mtihani wa
kidato cha nne mwaka 2012, walipata daraja sifuri.
Kuendela,bofya Read More
Lucy Ngowi
anaripoti kuwa, Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA), limemtaka Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na wasaidizi wake
kujiuzulu mara moja ili kupisha wenye uwezo wa kusimamia sekta hiyo.
Katibu Mkuu
wa BAVICHA, Deogratias Munishi, alisema hayo katika tamko alilolitoa
jana baada ya Tume ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutoa ripoti ya awali
kuhusu sakata la kufeli vibaya kwa wanafunzi waliofanya mtihani wa
kidato cha nne mwaka jana.
Akinukuu
moja ya sababu za kushindwa kwa wanafunzi hao, Munishi alisema ni
kutumika kwa alama mpya tofauti na miaka ya nyuma bila taarifa kwa
walengwa.
Alisema kuwa huo ni muendelezo wa siasa na mzaha kwa Watanzania kunakofanywa na serikali ya CCM kwenye masuala nyeti.
“BAVICHA
inasisitiza Waziri Kawambwa na wasaidizi wake wajiuzulu nyadhifa zao ili
kupisha watu wenye uwezo wa kusimamia sekta hii na taasisi zilizo chini
yake,” alisema Munishi.
Aliongeza
kuwa viwango hivyo vipya vilivyowekwa na Baraza la Mitihani bila
kushirikisha wadau ni kiashiria cha uzembe uliokithiri.
“Kama Baraza
lilifanya maamuzi hayo bila waziri kujua nako kunaashiria uzembe
uliobobea wa waziri huyu wa kushindwa kujua kinachofanyika na taasisi
zilizo chini yake na kwa maana hiyo ni mzigo kwa taifa,” alisema.
Kwa mujibu wa Munishi, suala hilo limeleta athari kwa wanafunzi, kwani baadhi yao wamepoteza maisha kwa kujinyonga.
SOURCE: chadema SOCIAL MEDIA.
No comments:
Post a Comment