Friday, May 3, 2013

MBOWE:MAJANGILI WANASAGA MENO YA TEMBO HAPA NCHINI.

 
Mh.Freeman Mbowe.

Mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ilizidi kulitikisa Bunge baada ya jana Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kusema kwamba kuna kwa viwanda vinavyosaga meno ya tembo kabla ya kuyasafirisha nje.
Akichangia hotuba ya wizara hiyo, Mbowe alisema majangili wamekuja na mbinu hiyo mpya kwa lengo la kukwepa kunaswa na vyombo vya dola.
Alisema hivi sasa meno hayo hayasafirishwi kwa meli kama zamani na badala yake kuna viwanda nchini ambavyo huyasaga meno hayo na kisha kusafirishwa kama unga kupitia viwanja vya ndege.
“Watu hawa wamekuwa wajanja, wameona kupitisha meno kama unga ni rahisi kwani hakuna mashine za kung’amua unga huo,” alisema Mbowe.
Mbowe alisema Serikali inapaswa kuwa na mikakati ya kukabiliana na biashara hiyo ambayo inaweza kuwamaliza tembo wa Tanzania.
Mbowe alisema kwa sasa kilo moja ya meno ya ndovu inauzwa mpaka Dola 5,000 (Sh7.9 milioni), jambo linalofanya majangili kubuni njia mbalimbali za kufanikisha njama zao.
Alishauri kuwa Serikali inapaswa kuchukua hatua kali dhidi majangili ikiwamo ya kuwanyonga wanapopatikana na hatia.
“Tatizo wahusika wakubwa wa biashara hii ni watu wenye uhusiano mkubwa na viongozi wa Serikali lakini dawa yao ni kunyonga tu,” alisema.
Kauli hiyo ya Mbowe imekuja siku chache baada ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani katika Wizara ya Maliasili, ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa kutoa tuhuma nzito kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwamba anahusika na biashara ya meno hayo.
Jana, akichangia mjadala wa bajeti hiyo, Msigwa alimjia juu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi kwa kitendo chake cha kumtetea Kinana badala ya kumtaka kumpa ushahidi wa tuhuma alizotoa.
“Nilitarajia Nchimbi angenitaka nimpelekee ushahidi badala yake, anamkingia kifua mtuhumiwa, lakini sishangazwi na maelezo yake kwa sababu aliweza kuitwa Dokta kabla hajapata shahada,” alisema.
Alisema badala ya wapinzani kuitwa wahuni, wabunge wa CCM walitakiwa kufanya kazi pamoja kuhakikisha wanalinda masilahi ya nchi.
Hata hivyo, akichangia hoja hiyo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye alimtetea Kinana na kuiomba Ofisi ya Bunge kuielekeza wizara inayohusika na usafirishaji kutoa semina kwa wabunge wa upinzani akisema wengi hawajui taratibu za kusafirisha mizigo.
“Sikufurahishwa kabisa na kauli ya Mchungaji Msigwa kwa kuwataja viongozi kuhusika na biashara ya meno ya tembo licha ya ukweli kuwa kuna mfumo wa mambo ya usafirishaji,” alisema Medeye.


Source:CHADEMA social media.

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...