HOTUBA YA MHESHIMIWA DR ANTONY GERVAS MBASSA (MB) MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014 (Inatolewa kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge kanuni ya 99(9) toleo la mwaka 2013).
1.0 RASILIMALI WATU
KATIKA SEKTA YA AFYA
Mheshimiwa Spika,
hatuwezi kuongelea au kuzungumzia hali ya sekta afya nchini bila ya kuangalia
mambo makuu mawili yanayoifanya sekta hiyo kuonekana na kuiwezesha kuwa na
tija. Mambo hayo makuu kwanza ni rasilimali watu katika sekta hiyo na pili
madawa na vifaa vya kutolea tiba. Wizara ya afya na ustawi wa jamii ilianzisha
mpango mkakati wa rasilimali watu wa mwaka 2008-2013 unaoitwa 'Human
Resources Strategic Plan' unaolenga kutoa muongozo jinsi gani ya
kupanga na kupambana na tatizo la rasilimali watu katika sekta ya afya lakini
mpaka hivi sasa tatizo la rasilimali watu limekuwa likiongezeka kwa kasi ya
ajabu na halijapatiwa ufumbuzi wa kutosha.
Mheshimiwa Spika,
taarifa iliyotolewa na McKinsey & Company mwaka 2006 kufuatia tafiti uliofanywa
na McKinsey & Company’s Global Public Health
practice, hasa kufuatia taarifa yao waliyoito hapo mwaka 2003 inayoitwa, “ Acting
Now to Overcome Tanzania’s Greatest Health Challenge: Addressing the Gap in
Human Resources for Health”. Mapungufu
ya rasilimali
watu katika sekta ya afya inaonyesha kuwa Tanzania ina upungufu mkubwa wa raislimali
watu, na pia hakuna mfumo au kanuni maalum inayotumiwa na Wizara katika kugawanya rasilimali watu chache iliyopo katika mikoa
na wilaya mbali mbali hapa nchini. Jambo hili limepelekea wilaya nyingi hapa
nchini kukosa kabisa madaktari katika
hospitali za wilaya.
Mheshimiwa Spika,
taarifa iliyotolewa na wizara ya afya kuhusu rasilimali watu katika kada ya
afya kwa mwaka 1999 ilionyesha kuwa
jumla ya watumishi wenye sifa 46,868 kwenye sekta ya afya walihitajika, lakini
waliokuwepo ni 15,060 ambao ni sawa na
asilimia 32.1% ya mahitaji yote, Upungufu wa watumishi 31,808 ambao ini sawa na
asilimia 67.9%. Mchanganuo huo ulihusu mfumo mzima wa afya kuanzia ngazi ya
chini hadi ya juu ya huduma za afya.[1]
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali iwaeleze watanzania toka taarifa
imetolewa na Wizara na kuonyesha upungufu wa watumishi katika sekta ya afya wa
asilimia 67.9% kwa mwaka 1999, sasa ni miaka 14, je ni kwa kiasi gani imekabiliana na upungufu huo? Au taarifa zake
za tafiti zinasomwa kwa wadau wa maendeleo na kuwekwa makabatini tu?
Kuendelea,Bofya Read More
Mheshimiwa Spika,
Taarifa ya utafiti uliofanywa na taasisi inayojihusisha na afya ya SIKIKA, “HRH
TRACKING STUDY 2012” kuhusu mahitaji ya watumishi wa afya inaonyesha
kuwapo kwa upungufu mkubwa na kwamba idadi ya watumishi wanaopangiwa vituo vya
kazi na kuripoti ni asilimia 70% kwa wilaya za vijijini na asilimia 93% kwa wilaya
za mijini, na pia wilaya zingine hazipati watumishi kulingana na mahitaji
yao. Aidha, utafiti unaonyesha kuwa wilaya nyingi zilipata asilimia 35% tu ya
watumishi katika maombi yao. Hoja hapa ni je hiyo asilimia 30% ya wanaopangiwa vijijini na asilimia 7% ya
wanaopangiwa mijini inakwenda wapi na kwa nini? Je Serikali ina mkakati gani wa
kuhakikisha watumishi hao wanaripoti na kufanya kazi katika mazingira rafiki?
Mheshimiwa Spika,
Taarifa hiyo inaonyesha kuwa kati ya
madaktari 2252 waliopo ni asilimia 60.3% tu ndio wanajihusisha na utabibu na
asilimia 39.7% wanafanya kazi tofauti kabisa na utabibu. Sambamba na hilo,
inaonyesha kuwa mgawanyo wa madaktari
wahitimu (MD Graduates) ambao tafiti hiyo iliwaangaza inaonyesha kuwa ni
asilimia 41.6% ya madaktari wanafanya kazi katika majiji (Mbeya, Mwanza, Arusha
na Dar) na asilimia 11.3% mikoa mingine,
asilimia 36.6% haijulikani wanajihusisha na nini. Asilimia 8.2% wanafanyakazi nje ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu takwimu zilizotolewa na shirika la
afya la dunia (WHO) na kuchapishwa na
jarida la “Joint Learning Initiative” mwaka 2009 , inaonyesha kuwa kwa wastani Tanzania kila mwaka takriban wanafunzi waliotimiza
vigezo zaidi ya 1,000 wanaomba kujiunga
na masomo ya udaktari, lakini nafasi zilizopo ni 200 tu. Kulingana na taarifa kutoka kwenye utawala wa
Chuo cha Afya Bugando ni kuwa kila mwaka wanapokea maombi yapatayo
500 kwa ajili ya AMO lakini nafasi
zilizopo ni 50 tu kila mwaka.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa kwa
mgawanyo huu wa madaktari ni kweli kwamba ule Mpango wa
Maendeleo wa Afya ya Msingi (MMAM) ambao ulianza rasmi mwaka 2007 na unatarajia
kumalizika mwaka 2017 kila kata iwe na kituo cha afya na kila kijiji kiwe na
Zahanati, ni dhahiri lengo hilo haiwezi kufikiwa.
Mheshimiwa Spika, kuna idadi kubwa ya watumishi wa afya (AMOs)
ambao hufanya kazi katika Hospitali za mikoa,wilaya na mpaka vituo vya afya.
Kundi hili muhimu stahili zake katika muundo wa utumishi hauonekani upo wapi,
kundi hili ndio uti wa mgongo katika utoaji wa huduma za afya ukizingatia
majukumu yao ya kila siku kadri wanavyoongozwa na “job description”.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaita Serikali
kueleza wazi ni nini stahili za kundi hili katika ngazi za utumishi na maslahi
yao ni yapi?
Mheshimiwa Spika, aidha, kuna tatizo la wafanyakazi
wanaojiendeleza mahali pa kazi wanapohitimu, kwani hawapandishwi madaraja au
kulipwa stahili zao kulingana na ngazi mpya ya madaraja yao, Suala
linalokatisha tama kwa wafanyakazi katika sekta ya afya. Je Serikali ina mpango
gani katika kuhakikisha suala hili linapatiwa ufumbuzi wa haraka ili kutokuzidi
kuleta madhara katika utoaji huduma kwenye sekta ya afya?
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Munga na
Mbilinyi (2009)[2] kuhusu sababu zinazo wafanya watumishi katika
sekta ya afya kukimbilia nje ya nchi au kuhama serikalini ni utawala mbovu
uliopo katika sekta ya afya ikiwa ni pamoja na upendeleo katika upandishwaji wa
madaraja ya kazi, upendeleo katika kutoa fursa mbalimbali za kujiendeleza
kimasomo na kimafunzo, kukosekana kwa vitendea kazi, malipo duni yasiyoendana
na kazi inayofanyika.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inaliona
tatizo la kutokuwepo kwa usimamizi dhabiti wa sekta ya afya, kwa msingi kwamba
Mganga Mkuu wa Wilaya ndiye mtawala mkuu wa sekta ya afya katika wilaya. Hili
ni tatizo kubwa kwani mganga mkuu hana taaluma stahiki katika utawala wa
Rasilimali watu hali inayoleta changamoto za kiutawala na usimamizi wa
rasilimali watu. Ipo haja kubwa ya kuhakikisha kuwa wataalamu hawa wanapata
mafunzo yatakayowawezesha kusimamia rasilimali watu.
Kambi ya upinzani inahitaji maelezo ya kutosha ni jinsi gani mpango wa rasilimali
watu kwa sekta ya afya kwa mwaka 2008-2013 umeweza kutatua matatizo ya raslimali watu hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, changamoto
kubwa kwa upande wa rasilimali watu ambayo ni lazima ipewe kipaumbele ni pamoja
na kuwa na Succession Plan ambayo itasaidia katika kuandaa madaktari, wauguzi
na wahudumu pale ambapo wale waliopo wanakua wamestaafu, kupata matatizo,
kuacha kazi ama kushindwa kuendelea na nafasi walizo nazo. Vituo vingi vya afya
pamoja na hospitali, zimekumbwa na uhaba wa watumishi pale panapokua na pengo
la madaktari, wauguzi ama wahudumu.
Mheshimiwa Spika,
kuna suala ambalo linawasumbua sana wauguzi ambao kwa idadi kubwa ni waajiliwa
wa Serikali, lakini watumishi hawa inawabidi kila mwaka katika utendaji wao
walipie leseni inayowawezesha kufanyakazi zao.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kufahamu hizi leseni zinazokatwa kila mwaka
fedha za leseni hizo zinapelekwa kwenye fungu lipi na ni kwanini iwe ni kada
hiyo ya utumishi wa umma inayotakiwa kuwa na leseni?
2.0 HALI YA VYUO
VYA MAFUNZO YA AFYA
Mheshimiwa Spika,
kutokana na utafiti uliofanywa na taasisi hiyo ya SIKIKA katika vyuo vya mafunzo vya afya hamsini na moja
vilivyofanyiwa utafiti mwaka 2012, inaonyesha kwama katika vyuo 30, asilimia 59
ya vyuo hivyo vilibainika kuwa na upungufu wa malazi. Na vyuo 26, asilimia 51
ya vyuo hivyo ilibainika kuwa na upungufu mkubwa wa madarasa. Aidha vyuo 24
kati ya 51, asilimia 47 vilibainika kuwa na upungufu mkubwa wa
wakufunzi/walimu. Katika mtiririko huo vyuo katika 23, asilimia 45 yake
vilionekana kuwa na ukosefu wa vifaa vya kufundishia.
Mheshimiwa
Spika, Pamoja na mapungufu
haya yanayovikabili vyuo vya mafunzo ya
watumishi wa afya, bado fedha iliyotengwa kwa maendeleo ya mafunzo ya
rasilimali watu katika sekta ya afya kwa mwaka 2013/14 imepungua kwa
asilimia 54 ukilinganisha na mwaka uliopita.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kulieleza Bunge hili ni kwa vipi mpango wa kuongeza raslimali watu kwenye sekta
ya afya utaweza kufanikiwa ikiwa raslimali fedha inashindwa kuelekezwa kwenye
Nyanja hiyo ya uzalishaji wataalam?
3.0
BUDGET YA MAFUNZO IDARA YA AFYA
Mheshimiwa
Spika, Katika kutekeleza mpango mkakati wa rasilimali
watu afya ya 2008/2013, zaidi ya shilingi bilioni 400 zilihitajika, kwa wastani
kwa mwaka zinahitajika jumla ya shilingi bilioni 80. Katika mwaka wa fedha wa
2012/13 kitengo cha mafunzo afya kilitengewa jumla ya shillingi bilioni 47.6 Ambapo
jumla ya shilingi Bilioni 24.3 zilitengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na
shilingi Bilioni 23.3 kwa ajili ya maendeleo. Mheshimiwa Spika, Kiwango hiki ni
cha chini ya kiwango kilichohitajika
Mheshimiwa
Spika, Katika mwaka 2013/14, serikali imepanga
kutumia shilingi 33.9 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo; hii ni pungufu kwa
asilimia 29 ukilinganisha na mwaka wa fedha uliopita, Matumizi ya kwaida katika
2013/14 yatakuwa ni billion 23.2 (pungufu ya asilimia 5 ukilinganisha na
2012/13).
Mheshimiwa
Spika, fedha za matumizi ya maendeleo kwa mwa wa
fedha 2013/14 ni shilingi billion 10.7
(pungufu ya asilimia 54 ukilinganisha na mwaka wa fedha uliopita). Kambi Rasmi
ya Upinzani inauliza, ikiwa fungu la fedha zinazotengwa kwa ajili ya maendeleo
ya mafunzo ya rasilimali watu katika sekta ya afya zinapungua kwa kiasi hicho,
Je wafanyakazi wa kuhudumia vituo vya huduma za afya watapatikana kwa njia
gani?
UAJIRI WA WATUMISHI WA AFYA
UKILINGANISHA NA VIBALI VYA AJIRA
Mheshimiwa
Spika, Pamoja na upungufu wa wafanyakazi, bado Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii imekuwa ikiajiri wafanyakazi wachache ukilinganisha
na vibali vya ajira vinavyotolewa na Ofisi ya Rais– Utumishi wa umma kama inavyoonekana katika mchoro wa umbo hapo
juu.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia mahitaji ya watumishi walioidhinishwa kwa ajili ya kuajiriwa na
idadi iliyoajiriwa toka mwaka 2005/06
hadi 2010/2011 utaona upungufu mkubwa uliopo. Katika mwaka wa fedha 2009/10,
jumla ya wafanyakazi 4,090 waliajiriwa. Idadi hii ni sawa na asilimia 65 tu ya
wahitimu wa kada za afya kwa mwaka husika. Pamoja na upungufu mkubwa wa
wafanyakazi, bado asilimia kubwa ya wahitimu hawakupata ajira serikalini.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona sasa ni muda
mwafaka kwa Mheshimiwa Waziri akaeleza watanzania hasa wadau wa sekta ya afya ni
sababu zipi zimepelekea kutolewa kwa ajira kidogo kulinganisha na idadi ya
ajira ambazo zinatolewa kibali na Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa umma.
4.0 AFYA YA MAMA NA
MTOTO
Mheshimiwa
Spika, Sera ya afya ya mwaka 2007 inasema
afya ni ukamilifu wa binadamu kimwili, kiakili na kijamii na kutokuwepo kwa
maradhi. Changamoto mbalimbali zinawakumba kina mama hasa inapokuja kwenye
suala zima la uzazi. Kuna uhaba mkubwa wa vifaa tiba
katika hospitali na vituo vya afya katika sehemu kubwa ya Tanzania hasa vifaa vya
kusaidia wajawazito wakati wa kujifungua.
Mheshimiwa Spika, aidha
kuna tatizo kubwa linaloikabili nchi, ambapo wagonjwa wengi wanahitaji damu salama
lakini baadhi hawapati kutokana na kutokuwepo watu wa kujitolea damu. Wagonjwa
au ndugu zao hutozwa sh 2,500 kwa ajili ya kununulia mifuko ya kukusanyia damu,
mirija ya dripu ya kumwingizia mgonjwa sh 2,000 na kama atakuwa anatakiwa
kufanyiwa upasuaji anatoa pesa ya nyuzi sh 5,000 na kumshona ni sh 8,000,’’[3] na
baadhi ya wagonjwa wanakufa baada ya kukosa msaada wa damu. Hivyo katika baadhi
ya vituo vya afya na hospitali wanaamua kuokoa maisha ya wagonjwa hao kwa
kuwatoa damu watu wanaokubali hasa ndugu wa wagonjwa na kuwaongezea wagonjwa
bila uhakika wa vipimo vya virusi vya ukimwi (VVU) na UTI (magonjwa ya zinaa)
na ini. Moja ya sababu za ukosefu wa damu kwa baadhi ya wanawake hasa kinamama
wajawazito ni pamoja na ukosefu wa lishe bora ikiwamo vyakula vya virutubisho
vya kuongeza damu mwilini ambapo kwa watoto ni kutokana na homa kali na
malaria.
Mheshimiwa Spika, Katika
kulinda afya ya mama na mtoto, kuna dawa zinazohitajika kwa wajawazito ambazo
ni pamoja na za malaria, dawa za kuharakisha kupona vidonda au maumivu, SP na
mseto lakini wajawazito wengi wamekuwa wakipewa dawa aina ya SP pekee huku
katika baadhi ya maeneo wakinunua hata kadi za kliniki ingawa zimeandikwa kuwa
haziuzwi.
Mhemshimiwa Spika, Katika
kukabiliana na changamoto mbalimbali za uzazi,wajawazito wengi wamekua
wakikumbana na kauli pamoja na huduma duni toka kwa wauguzi huku wauguzi
wengine wakitoa kauli za kukebehi na za kukwaza ambapo kutokana na kauli za wauguzi hao imefikia
mahala wajawazito wanaona ni bora kujifungulia nyumbani au kwa wakunga wa jadi
kuliko kwenda sehemu ya kutolea huduma za kisasa na kwamba watalazimika kwenda
hospitali kama watakuwa na matatizo makubwa katika ujauzito wao ingawa kliniki
wanahudhuria kila tarehe wanayopangiwa.
Mheshimiwa Spika, Katika
karne hii ya 21, lazima Serikali iweke mikakati ya kuweza kuwaokoa wananchi
wake hasa kina mama na watoto kwa kukabiliana na changamoto za sekta ya afya
hasa kwa kukabiliana na upungufu wa
wauguzi na kuwatumia ipasavyo wakunga. Takwimu zilizochapishwa na ripoti ya Hali ya Wakunga
Ulimwenguni (State of the World’s Midwives) zinaonyesha kuwa Tanzania inahitaji
wakunga 9,941 zaidi ili kufikia lengo ifikapo mwaka 2015 la kuwa na asilimia
95% ya wajawazito wanaozalishwa na wahudumu wenye taaluma. Na kwa mujibu wa
taarifa hii akina mama 5,000 na watoto wachanga 32,000 wangeweza kuokolewa
ifikapo 2015. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kueleza mipango
mikakati madhubuti itakayohakikisha kuwa wakunga wanapewa nafasi katika kulinda
afya ya mama na mtoto.
Mheshimiwa Spika,
Kuhusu afya ya mama na mtoto, Kambi Rasmi ya Upinzani katika hotuba yake hapa
bungeni 2011/2012 tulionesha wazi kutoridhika na zoezi la ununuzi wa pikipiki
za miguu mitatu ambazo zilinunuliwa kwa bei ghali kwa mchakato ambao
tuliulalamikia kuwa unatumia vibaya fedha za walipa kodi, masikini wa nchi hii ambao
wanajitahidi kulipa kodi hizi kwa maendeleo ya taifa letu. Tulibezwa na kuitwa
adui wa maendeleo. Lakini kwa wingi wa uwakilishi na demokrasia ya wengi wape
hata pale maslahi ya taifa hili yanapowekwa rehani.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani bungeni inaelekeza masikitiko yake makubwa kwa Serikali kwa
kununua pikipiki zaidi ya 372 kama Mheshimiwa Waziri alivyotamka wakati wa
bajeti ya afya mwaka 2012/13 lakini ukiangalia asilimia kubwa ya hizo
pikipiki zimetelekezwa katika hospitali
za wilaya ama zimeshindwa kabisa kupelekwa kwenye vituo vya afya kwa kuwa
miundombinu hairuhusu hizo pikipiki kutumika katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inashindwa kuamini kuwa wakati zoezi hili la kununua pikipiki
hizo wahusika wa zoezi hilo walikuwa wageni hapa nchini au kwa kuwa masuala
yote yanafanyika Dar es salaam bila kujua kuna maeneo mengi ya nchi hii pamoja
na miaka 51 ya uhuru bado hayawezi kufikika kwa urahisi, liwe jua au iwe mvua. Suala hili linazidi kutia shaka kwani
linapekelea uwapo wa hisia za rushwa katika zoezi hilo kutokana na msukumo
ulioonyeshwa na wasimamizi wakuu wa Wizara wakati huo.
Mheshimiwa Spika, aidha, tuna inaishauri Serikali kufanya
utafiti wa kutosha kabla ya kufanya maamuzi na tuache kufanya maamuzi kwa
kuangalia nchi ya India au China wanafanyaje. Tukumbuke mazingira ya nchi yetu
na yao nitofauti. Maamuzi kama haya mwisho wa siku yamepelekea kutumia rasilimali
na kodi za walalahoi kwa vitu ambavyo havitoi tija na tatizo kuendelea kuwa
sugu.
5.0 MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA
Mheshimiwa Spika,
kumekuwepo na ongezeko kubwa sana la magonjwa ya mioyo,shinikizo la
damu,saratani mbalimbali n.k. Haya
magonjwa kwa kiasi kikubwa
yanatokana na kubadilika kwa hali ya maisha, aidha kwa kutokuzingatia lishe
bora, kwa maana ya kutotumia vyakula asili na hatimaye kutumia vyakula
vilivyosindikwa na baadhi ya kemikali.
Mheshimiwa Spika,
kumekuwepo na hali ya baadhi ya watu kutopenda kufanya uchunguzi wa afya zao mara
kwa mara na na pale wanapopata maradhi
hayo ambayo hutokea ghafla na kujikuta wamefikishwa hospitalini, hali inakuwa
mbaya sana kwa mgonjwa.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa elimu na mwongozo juu ya lishe
bora na si bora lishe kuhimiza umuhimu wa watu kupima afya zao na pale
inapobainika basi wapatiwe huduma za afya zinazostahili.
5.1Huduma za Macho:
Mheshimiwa Spika,kuna
takriban watu milioni 285 ambao wana
matatizo ya kuona Duniani. Watu milioni 39 wana upofu, watu milioni 246 wana
uono hafifu, 80% ya matatizo haya yanaweza kuzuilika na 90% wapo kwenye nchi
zinazoendelea.
Mheshimiwa Spika,
kulingana na taarifa za shirika la afya la Dunia (WHO), Tanzania inakadiriwa
kuwa na watu 992,250 sawa na 3.15% wana matatizo ya uono ambapo kati yao
wasioona ni 315,000 sawa na 0.7% ya watanzania wote. Watu wenye uono hafifu
wanakadiliwa kuwa 787,000, na sababu zinazoongoza ni kuwa na mtoto wa jicho (cataract),
shinikizo la jicho(Glaucoma), matatizo ya retina ambayo yanatokana na sukari na
umri mkubwa n,k
Mheshimiwa Spika,
shughuli za utibabu huu huendeshwa na madaktari bingwa, madaktari wasaidizi au
wauguzi wenye fani ya macho, na hii ni pamoja na mtaalam wa kupima upeo wa
macho na miwani (optometrist).
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza ina mpango gani wa
kuongeza
nafasi za madaktari ambao wanajiunga na vyuo vinavyotoa au kufundisha
fani hii?
Aidha serikali ina mpango gani wa haraka
kufanikisha uwepo wa vifaa tiba na upasusaji wa jicho katika hospitali
zetu za wilaya na mikoa? Pia Serikali ina mkakati gani wa haraka
kupitia
kamati za afya ya msingi kutoa elimu sahihi ya afya katika suala la
kudhibiti upofu?
6.0
UPATIKANAJI WA DAWA, VITENDANISHI, VIFAA NA VIFAA TIBA
Mheshimiwa Spika, Suala
la upatikanaji wa dawa, vifaa, vitendanishi na vifaa tiba limeendelea kuwa
taizo sugu sana. Na hii inatokana na mfumo uliopo wa bohari ya madawa kufanya
kazi aidha chini ya kiwango au kuendelea kufanya kazi kwa mazoea yaleyale.
Sehemu nyingi upatikanaji wa dawa muhimu umekuwa ni kitendawili kisicho na jibu
na hususan kwa mazingira ya vijijini na hii upelekea usumbufu mkubwa kwa
wananchi wengi wasio na kipato kukosa dawa jambo ambalo ni stahili ya msingi
kwa kila mwananchi. Mfano halisi ni katika hospitali ya wilaya
Biharamulo, Pamoja na hoja za Serikali kuwa kumekuwa na ucheleweshaji wa maombi
ya dawa, vifaa na vifaa-tiba ni ukweli usiopingika kuwa mfumo uliopo hauendani
na kasi ya mahitaji ya dawa na vifaa katika maeneo mbalimbali ya nchi kutokana
na ukiritimba kwenye mfumo mzima wa upatikanaji wa dawa, viaa na vifaa tiba.
Mheshimiwa Spika, Tatizo
la ucheleweshwaji wa dawa pamoja na kutopatikana kwa dawa stahiki kwa wagonjwa,
zimewafanya wauguzi na madaktari kubeba mzigo mzima wa lawama kutoka kwa
wananchi. Mara kadhaa ucheleweshwaji wa dawa na vifaa katika vifaa vya afya
umesababisha madaktari na wauguzi kuandika ununuzi wa dawa nje ya vituo vya
afya. Hali hii imezua migogoro ya mara kwa mara na malalamiko mengi kwa wauguzi
na madaktari kuwa wanazuia upatikanaji wa dawa, na huku serikali inaendelea
kujikwepesha lawama kuwa vituo vya afya vimekua vinachelewa kuagiza dawa na
hivyo mzigo wa lawama umekua mkubwa kwa wauguzi na hivyo kuleta uhasama kwao na
wananchi na mpaka sasa ni ukweli kuwa wananchi hawana imani na vituo vya afya
pale wanapoambiwa kuwa dawa na vifaa havipatikani.
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa taarifa ya utafiti iliyotolewa mwezi wa march 2012 na taasisi isiyo ya kiserikali inayojihusisha
na afya ya SIKIKA kuhusu, “Availability of Essential Medicines,Medical Supplies
and Bed Capacity in Hospitals in Tanzania Mainland”
ambao ulihusu hospitali
54 za Serikali uligundua kwamba kati
hospitali hizo 43 zilikuwa ni hospitali
za wilaya na kati ya hospitali hizo za
wilaya 40 zilichaguliwa “randomly” na tatu
zilizobaki zilichaguliwa kwa vigezo maalum
kwenye maeneo ambayo taasisi hiyo inafanyia kazi. Aidha, 11 zilizobaki
zilikuwa ni hospitali za rufaa za mikoa.
Mheshimiwa Spika,
matokeo ya utafiti huo ni kwamba 94% ya hospitali hizo zilionyesha kukosekana kwa
madawa na vifaa tiba “out of stock of
one or more essential medical supplies”, 96% ya
hospitali zilionyesha kukosekana kwa madawa muhimu. Aidha,taarifa hiyo
inaonyesha kuwa vifaa tiba ambavyo vimekuwa ni tatizo kwa takriban hospitali
zote ni: gloves imeonyesha 83% , sutures (48%), gauze (39%) for medical supplies, and quinine
(43%) and metronidazole (31%) for medicines. Asilimia , 52% na 59% ya hospitali zilionyesha kuwa zilikuwa
zinaishiwa madawa na vifaa tiba
muhimu kwa kipindi kinachozidi
majuma manne.
Mheshimiwa Spika, kwa kuangalia takwimu za utafiti huo
ni dhahiri sekta hiii ya madawa na vifaa tiba kwa hospitali zetu bado ni tatizo
kubwa, na Kambi ya Upinzani inashindwa kuelewa kwa mwendo huo ni kwa jinsi gani
malengo ya millennia yatafikiwa? Tunamtaka Mhe Waziri awape ufafanuzi
watanzania tatizo hilo kwa sasa limetatuliwa kwa kiwango gani.
Mheshimiwa Spika,
Kwa upande wa dawa na vifaa tiba hali ni
mbaya zaidi kutokana na ukweli kwamba kutokana na makadirio ya fedha shilingi
bilioni 198 katika mwaka wa fedha 2012/13 zilizotakiwa kwenda Bohari kuu ya
madawa kwa ajili ya kufanya manunuzi ya dawa na vifaa hadi mwezi Desemba 2012 zilikuwa zimetolewa
shilingi bilioni 3 sawa na takriban asilimia 3; na hadi mwezi Machi 2013 zilikuwa zimetolewa shilingi
bilioni 28.3 ambayo ni takribani asilimia 27 ya bajeti iliyokuwa imetengwa kwa
taasisi hiyo.
7.0 BOHARI YA DAWA
YA TAIFA (MSD)
Mheshimiwa Spika, Tunataka
taifa lijue kuwa Serikali ya CCM inacheza na uhai na afya zao. Pamoja na
changamoto mbalimbali ambazo MSD inakumbana nazo, pamoja na makelele ya taifa
kuwa hakuna dawa za kutosha kwenye vituo vya afya huku viongozi wa Serikali
wakiendelea kufanya manunuzi kwa magari yenye thamani kubwa na safari za nje
zisizo kuwa na uratibu au tija. Huku wakielewa kuwa Bohari ya Dawa inaidai
Serikali kiasi cha sh. bilioni 52 ambazo zimelimbikizwa kutokana na madeni ya
muda mrefu ya huduma za dawa, vifaa, na vifaa tiba ambavyo taasisi hiyo ilitoa
kwa vituo vya afya vya Serikali pamoja na hospitali zake.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni inaishauri Serikali kuangalia upya vipaumbele vyake kwani
afya ya watanzania inatakiwa kuwa ni kipaumbele cha msingi badala ya utaratibu
mpya wa ulaji kwa ofisi ya Rais wa uanzishwaji wa kinachoitwa Presidential
Delivery Bureau, na kutenga shilingi bilioni 28 kwa ajili ya vikao tu.
Mheshimiwa Spika, Leo
tunaongelea ucheleweshaji wa utoaji wa fedha kwa MSD unaosababisha pia kuharibu
na kucheleweshwa kwa mfumo mzima wa
manunuzi na usambazaji wa madawa na vifaa tiba kwa nchi. Aidha, kwa mfuatano
huo ni kwamba uboreshwaji mzima wa sekta ya afya unazidi kuwa mgumu sana na
hivyo kushindwa kutimiza malengo ambayo tunajiwekea kama nchi. Afya za wananchi
wa taifa hili, Serikali ya CCM imeziweka rehani. Lazima kama taifa tuseme, lazima
tukatae ujanja ujanja wa Serikali hii.
Mheshimiwa Spika, Bohari ya Dawa ina changamoto mbalimbali inazokumbana nazo, zikiwemo za
vyombo vya dola kuwafumbia macho baadhi ya wafanyabiashara wanaouza dawa za
serikali kiholela pamoja na wanaokamatwa kwa kutorosha dawa hizo nje ya nchi.
Taasisi zilizomwagiwa lawama hizo ni baadhi ya maofisa kutoka vyombo vya dola,
serikalini na wafanyabiashara. Hayo yalisemwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
Bohari ya Dawa (MSD), Cosmas Mwaifwani
wakati wa Kongamano la Nane la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) la
kujadili tafiti zilizofanywa na wanahabari kuhusu matumizi ya fedha
zinazochangwa na wananchi kwa ajili ya masuala ya afya katika halmashauri 26
nchini.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na hayo bado kuna tatizo
kubwa la kutoainisha pesa inayotengwa kwa ajili ya madawa, vifaa tiba
vitendanishi inayopelekwa Tamisemi. Kumekuwapo utendaji ambao ki-msingi unaongiliana
lakini hakuna usimamizi wa jumla wa wizara hizi mbili. Kambi Rasmi ya Upinzani
inatoa wito kuwepo na Afisa wa Wizara ya afya atakaye simamia mipango ya Afya
upande wa TAMISEMI.
8.0 MAMLAKA YA
CHAKULA NA DAWA TANZANIA (TFDA)
Mheshimiwa Spika, Mamlaka
ya chakula na dawa, iliyopo chini ya wizara hii, ilianzishwa kwa ajili ya
kuimarisha udhibiti wa ubora na usalama wa vyakula, vipodozi na vifaa tiba
nchini ili kulinda afya za watumiaji. Kati ya majukumu yake ni pamoja na kudhibiti
utengenezaji, usambazaji na uuzaji wa dawa, vipodozi na vifaa tiba; ukaguzi wa
viwanda vya utengenezaji; kufuatilia madhara yatokanayo na matumizi ya dawa
zinazodhibitiwa; kufanya uchunguzi na uhakiki wa ubora na usalama wa bidhaa na
kadhalika.
Mheshimiwa Spika, Katika
kutekeleza wajibu wake wa uchunguzi wa sampuli za bidhaa kimaabara, jumla ya
asilimia 83.5 zilifaulu uchunguzi. Pamoja na TFDA kuzuia bidhaa zilizoshindwa
vigezo kuingia nchini au kusitishwa matumizi ya bidhaa na kuondolewa kwa bidhaa
hizo sokoni, haijatoa taarifa rasmi ya uchunguzi wa madhara ya bidhaa ambazo
tayari zilikua sokoni na kusababisha madhara kwa watumiaji, na kama watumiaji
walioathirika na bidhaa zisizokidhi vigezo. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
inaitaka wizara kulieleza Bunge lako jumla ya idadi ya waathirika wa bidhaa
zisizokidhi vigezo ambao wamelipwa fidia kufikia Machi mwaka huu.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaendelea kusisitiza kuwa ili kuwe na na mfumo
udhibiti bora wa dawa, chakula, vipodozi na vifaa tiba lazima kuwe na sheria
madhubuti zenye kuendana na uhalisia wa hali ya sasa yenye changamoto nyingi.
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inaishauri Serikali kuharakisha marekebisho ya
Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya mwaka 2003 ambayo imepitwa na wakati
hivyo kuleta changamoto katika utendaji wa Mamlaka ya Chakula na Dawa.
Mheshimiwa Spika, Katika
kaguzi za huduma za afya nchini, ripoti zinaonesha kuwa kumekuwepo na
udanganyifu wa sifa na ujuzi kwa watumishi wa kada ya wauguzi na wahudumu
pamoja na watumishi wengine kupata mshahara bila ya kufanya kazi. Pamoja na
mikakati ya wizara katika kukabiliana na changamoto hii, kwa kuwahimiza waajiri
kuthibitisha sifa za wataalamu wao kwenye mabaraza ya kitaaluma bado mfumo
uliopo nchini, haujaweza kudhibiti vitendo vya kugushi sifa za kitaaluma hivyo
kufanya zoezi zima la kudhibiti ongezeko la vitendo hivyo kuwa gumu. Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka majibu kutoka kwa waziri kutoa kwa kutoa
kiujumla idadi ya watumishi ambao wamegushi sifa na ujuzi wao na majibu ya
hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha kuwa mapungufu haya
hayajitokezi katika sekta ya afya ukizingatia kuwa Sekta ya Afya nchini, ni
sekta muhimu hivyo kuwa na watu waliogushi ujuzi na sifa stahiki katika utoaji
wa huduma za afya ni kuhatarisha maisha na kuziweka rehani afya za wananchi.
9.0 TATIZO LA DAWA
BANDIA ZA KUPUNGUZA MAKALI YA UKIMWI (ARVs) NCHINI
Mheshimiwa Spika, taarifa kwamba watu 5,358
wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (VVU) waliokuwa kwenye matibabu wameacha kutumia
dawa za kupunguza makali ya ugonjwa Huo (ARVs), mkoani Dodoma. Taarifa kupitia
vyombo vya habari na taasisi mbalimbali kuhusu
watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) kuacha kutumia dawa,
zimekuja kipindi ambacho Wananchi na wadau wa UKIMWI wakitafakari hatma ya
uchunguzi wa sakata la kutengenezwa Dawa
bandia za ARVs.
Mheshimiwa Spika, Dawa hizo aina ya TT--‐VIR toleo namba (batch number oc.01.85) zilisambazwa
katika mikoa ya Mara, Tanga na Dar es Salaam tangu Mei, 2011. Kuwepo kwa ARVs
bandia na taarifa juu ya WAVIU kuacha kutumia dawa kunadhihirisha Udhaifu uliopo
ndani ya mifumo na mamlaka za serikali zilizopewa kusimamia ubora, Uwepo na upatikanaji
wa dawa. Inaaminika, kuwepo kwa uhusiano wa karibu kati ya uwepo wa dawa hizo bandia
nchini Na WAVIU hao kuingiwa hofu na kuacha kutumia dawa.
Tunaamini hayo kwa kuzingatia
ukweli kwamba suala la mgonjwa kutumia dawa kwa kiasi kikubwa Linategemea imani na utayari wa mhusika.
Mheshimiwa Spika, uwepo wa dawa bandia ama zisizo na ubora unapunguza
imani na hivyo kuweza kusababisha mgonjwa kuacha kuzitumia na kupelekea kuathirika
zaidi.
Sakata la kuwepo kwa ARVs
Bandia lililochukua takribani miezi nane sasa, limekuwa na sura tofauti Hususan
juu ya nani anahusika moja kwa moja baada ya kiwanda kinachodaiwa kutengeneza
dawa Hizo Tanzania Pharmaceticals Industry (TPI) kukanusha kuhusika na
utengenezaji huku Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Bohari Kuu ya Dawa (MSD)
wakisisitiza kuwa dawa hizo zimetoka kiwandani hapo.
Mheshimiwa Spika, Pamoja
na kuwa uchunguzi unaendelea kuhusu dawa hizi lakini waathirika wa ugonjwa wa
UKIMWI waliopata madhara ya dawa hizi wengine wameshapoteza maisha, wengine
wameendelea kudhoofika na pia imefanya idadi kubwa ya waathirika kupuuzia dawa
nyengine za ARVs kwa kuhofia kuwa zitaleta madhara zaidi. Pamoja na yote hayo
bado Serikali kwa kupitia timu ya wataalamu iliyoundwa kwa lengo la kufuatilia
tiba na matunzo kwa wagonjwa wa UKIMWI, imetoa matokeo ya awali ya ufuatiliaji
wa madhara ya dawa hiyo ya bandia ya TT-VIR 30 toleo Na. OC.01.85 kuwa
hayakubaini wagonjwa waliodhurika kwa kutumia kwa kutumia dawa hiyo. Kambi
Rasmi inapingana na matokeo haya ya awali kwa kuwa inao ushahidi kuwa wapo
watanzania, wenzetu walioathirika kwa matumizi ya dawa hizo za bandia.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa taarifa
kutoka ofisi ya DPP, jalada la kesi ya ARVs bandia limepokelewa na
linashughulikiwa ili kupata muelekeo wa nani ahusishwe na kwa kosa gani kabla
ya kuachia mamlaka husika jukumu la uchunguzi wa kina. Kwa maelezo ya ofisi
hiyo, Suala la ARVs bandia limechukua muda mrefu (zaidi ya miezi miwili),
tofauti na muda wa kawaida wa siku 14 unaotumiwa na ofisi ya DPP kushughulikia
kesi mbalimbali zinazofikishwa hapo, kutokana na uzito/unyeti wa suala hilo.
Mheshimiwa Spika, Wakati taratibu hizo za
kitaalamu na kisheria zikiendelea, tunaishauri Serikali kutoa taarifa rasmi kwa
wananchi juu ya dawa bandia (makopo 4,000) ambazo hazijakusanywa. Je, ziko
vituoni au zilishatumiwa na wananachi? Kama zilishatumiwa, je serikali ina
taarifa zozote Juu ya waliozitumia dawa hizo? Je, kuna madhara yoyote
waliyopata kutokana na kuzitumia?
Kwa kutoa taarifa sahihi,
serikali itasaidia kuwatoa mashaka wanaotumia ARVs na kuwajengea imani
waendelee kuzitumia bila kuathiri afya zao.
Mheshimiwa Spika, Mwaka
2010, mkoani Arusha iliripotiwa kuwa kuna dawa ambazo ziliisha muda wake wa
matumizi za kupunguza makali ya UKIMWI ambazo zilileta madhara kwa watumiaji
ambazo zilikua zikitolewa na kituo cha Matibabu cha Arusha Lutheran Medical
Centre. Ndugu Joseph Lukumay, ambaye ni mkazi wa kata ya Kioga, Meru pamoja na
wengine walilalamikia kupewa ARVs aina ya Efavirenz zilizotengenezwa na Aurobindo
Pharma Limited ya India. Pamoja na muda wa kutengenezwa dawa ilikua ni Januari
2008 na zilitakiwa zitumike kabla ya Disemba 2009, ALMAC ilianza kuzitoa hizo
dawa kuanzia Januari 2010 na kuendelea. Pamoja na wagonjwa hawa kulalamika kuwa
dawa hizo zimekwisha muda wake, walipata majibu toka ALMAC kuwa dawa hizo
hazitaleta madhara ikiwa zitatumika ndani ya miezi sita ya kwanza baada ya siku
yake ya matumizi kuisha. Baada ya kutumia ndani ya miezi mitatu, dawa hizo
zilianza kumletea madhara Ndugu Lukumay kwa kumbabua ngozi, kumtoa vidonda na malengelenge ambapo pamoja na kuripoti
ALMAC, alipewa vitisho na kusitishiwa matibabu yake.
Mheshimiwa Spika, Ingawa
pamoja na maelekezo ya Serikali ya kuagiza dawa zote za matibabu lazima
ziagizwe na kusambazwa na MSD, baadhi ya vituo vyenye mrengo wa kiimani vimekua
vikitumia mianya iliyopo katika kuingiza dawa na vifaa kinyume na taratibu
zilizowekwa kwa kuwa huwa wanapata misaada kutoka mashirika ya nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua mkakati ambao umewekwa na Wizara kwa
mwaka 2013/2014 kwa ajili ya kuhakikisha kuwa vituo vya afya vinavyopata
misaada toka kwa mashirika ya nje ya nchi yanatimiza taratibu za kuingiza
nchini misaada ya kitiba hapa nchini. Aidha, tunataka Serikali itoe kauli juu
ya tuhuma zilizotolewa dhidi ya ALMAC ili kuweza kuwasaidia waathirika wa
UKIMWI katika kupata haki zao hasa pale inapotokea madhara yanayosababishwa na
uzembe wa vituo vya afya katika matibabu yao.
10.0 MWENENDO WA
TIBA ASILIA NA TIBA MBADALA NCHINI
Mheshimiwa Spika, TANZANIA ina idadi kubwa ya miti ya aina nyingi
inayoweza kutumika kama tiba ya maradhi mbalimbali.Inakadiriwa kuna aina 15,000
za miti inayotumika kama dawa nchini, lakini Watanzania hawafaidiki na mauzo ya
dawa zenyewe, yanayokadiriwa kuingiza Dola za Marekani bilioni1.6 kwa mwaka.
Mheshimiwa
Spika, umuhimu wa dawa za
zinazotokana na miti, unajionyesha hasa kwa kuwa asilimia 60 ya Watanzania
hutegemea tiba asili kwa matibabu yao. Tanzania
inayo nafasi kubwa ya kujitajirisha kwa kuuza dawa asilia. Kati ya vigezo vya
soko la dawa hizo kuwa ni dawa kuwa na virutubisho vinavyotakiwa, ziwe
zimetafitiwa kisayansi ili kuonekana kama hazina sumu na kuweka mbinu za
biashara kwa dawa hizo.Kwa Tanzania, dawa za miti hutathminiwa na kusajiliwa na
Mamlaka ya Chakula na dawa (TFDA) kabla ya kuanza kuuzwa. Lengo la kuhakiki na
kusajili ni kuhakikisha usalama, ubora kwa ajili ya matumizi ndani ya nchi.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na umuhimu wa
tiba asilia, Serikali ilitunga sheria namba 23 ya mwaka 2002 ili kuratibu
utendaji mzima wa sekta hii. Wizara ya Afya itoe takwimu kuna watabibu wangapi
waliosajiliwa na wangapi bado kusajiliwa kulingana na matakwa ya sheria hii.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani
inaitaka Serikali iwaeleze wadau katika sekta hii imeweka mkakati gani wa
kuielimisha jamii juu ya tofauti za waganga wa kienyeji, waganga wa tiba asili,
waganga wa jadi na watibabu wa Tiba mbadala. Utaratibu gani umewekwa kisheria
kuwasajili waganga wa tiba asili, kwani usajili wa wahusika unatakiwa uanzie
ngazi ya mtaa hadi taifa. Hivi ni chombo gani kina hakikia uhalisia wa
wanaosajiliwa, aidha, kuna tatizo pale waganga wa tiba asilia wanapoambiwa
wachangie kiasi cha Shilingi 80,000 hadi 200,000/- za kikao. Je, ni kweli
utaratibu huu unasaidia kuimarisha huduma za afya zitolewazo na tiba asili.
Mheshimiwa Spika,
kutokana na kukua kwa soko la tiba asili duniani na nafasi ambayo Tanzania
inayo katika kunufaika na soko hilo, ambalo nchini Cameroon peke yake kwa
kutumia soko la tiba asili iliweza kuingiza Dola milioni 40 mwaka 1993 kwa kuuza mti ujulikanao kwa jina la ‘Prunus Africana’
na mbegu za ‘Voacanga Africana’ unaoaminika kutibu magonjwa ya uzee, pekee.
Hivyo kambi rasmi ya upinzani bungeni, inaitaka Serikali kwa kupitia kwa waziri
mwenye dhamana ya wizara ya afya na
ustawi wa jamii, alieleze bunge lako tukufu, ni mikakati ipi ambayo imewekwa
kwa mwaka huu wa fedha wa 2013/2014 katika kuhakikisha kuwa taifa linanufaika
kwa soko la miti ya tiba asilia.
Mheshimiwa
Spika, Kambi rasmi ya Upinzani
Bungeni, inajua kuwa licha ya kuwepo kwa soko kubwa la dawa hizo na kuwa na
sheria kama vile Sheria ya NIMR namba 23 ya 1979, sheria ya dawa za jadi na
nyinginezo na sheria iliyoanzisha TFDA ya mwaka 2003, bado Tanzania haifaidiki
na soko hilo. Kati ya mambo ambayo yanaleta changamoto katika uendelezaji wa
tiba asili nchini ni udhaifu wa tafiti nchini, ampapo taasisi kama NIMR, ITM,
TAFORI na TAWIRI hazipati misaada ya kutosha katika tafiti zake.
Mheshimiwa
Spika, kuna tatizo kubwa kwani
Serikali imeshindwa kusimamia sheria hii, kwani dawa zinasambazwa kiholela kila
mtu anajiita mganga wa tiba asilia. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali iwathibitishie watumiaji wa huduma hii usalama wa madawa hayo?
Mheshimiwa Spika, Kutokana
na kukua kwa soko la tiba asili duniani na nafasi ambayo Tanzania inayo katika
kunufaika na soko hilo, ambalo nchini Cameroon peke yake kwa kutumia soko la
tiba asili iliweza kuingiza Dola
milioni 40 mwaka 1993 kwa kuuza mti ujulikanao kwa jina la ‘Prunus Africana’ na mbegu za
‘Voacanga Africana’ unaoaminika kutibu magonjwa ya uzee, pekee. Hivyo kambi
rasmi ya upinzani bungeni, inaitaka Serikali kwa kupitia kwa waziri mwenye
dhamana ya wizara ya afya na ustawi wa
jamii, alieleze bunge lako tukufu, ni mikakati ipi ambayo imewekwa kwa mwaka
huu wa fedha wa 2013/2014 katika kuhakikisha kuwa taifa linanufaika kwa soko la
miti ya tiba asilia.
Mheshimiwa
Spika, kuna watu wanaotoa
uchawi maarufu kama rambaramba ambao kutokana na taarifa zisizo rasmi kuwa
mratibu wake anajulikana na vyombo vya dola. Watu hawa wamesababisha hujuma na
hasara kubwa sana kwa jamii kwa nyumba kuchomwa moto, watu kupoteza maisha.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa kauli kuhusiana na mtandao huo
ambao mratibu wake ni maarufu kwa vyombo vya dola.
11.0 KIKOMBE CHA
BABU WA LOLIONDO
Mheshimiwa Spika, Kati
ya jambo ambalo lilileta gumzo katika sekta ya afya ni pamoja na tiba ya asili
maarufu kama 'Kikombe cha Babu wa
Loliondo' iliyokua ikitolewa na Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la
Kiluteri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapila.
Mheshimiwa Spika, Viongozi
waandamizi wa Serikali, walifurika Loliondo kwa babu na hivyo kuzidisha imani
kwa wananchi kuwa tiba ile ilikua ni sahihi na ya kuaminika. Wananchi wengi,
wakiwemo wabunge walikimbilia Loliondo kwa kuwa Serikali iliingilia
"uvumbuzi wa kiboko ya magonjwa' na wagonjwa kupuuza matibabu ya
hospitali. Safari ya kwenda Loliondo ilizua matumaini mengi kwa wananchi, huku
Serikali kabla ya kufanya utafiti wa kina wa
ubora wa dawa hii katika kutibu magonjwa sugu. Pamoja na majibu haya ya
Serikali ya 'kikombe cha babu' kuashiria kuwa haina madhara, haikutoa majibu ya
kitaalamu ya uwezo wa dawa ile kwa wakati ule katika tiba ya magonjwa sugu
ambapo hata wakati ule kuna mawaziri waliofuata ‘tiba’ hiyo ya Babu ambao nao
walichangia mno kuwaaminisha mamilioni ya Watanzania kuwa tiba hiyo ya Babu ni
ya kweli. Leo hii, kuna watu wengi ambao wamefariki kutokana na 'kikombe cha
babu'. Kuna waliofariki wakiwa njiani kuelekea kwa babu, kuna waliofariki
wakiwa kwa babu, na kuna waliofariki hata baada ya kunywa 'kikombe cha babu'. Na
kwa mujibu wa aliyekuwa waziri wa afya na ustawi wa jamii, Mh. Dr. Haji Mponda, alisema
kuwa jumla ya watu 116 walifariki kutokana na sababu mbalimbali wakiwa kijijini
Samunge au wakitoka kituo cha Arusha kupitia Mto wa Mbu na Bunda kupitia
Serengeti wakielekea kwa Babu kupata kikombe. Mpaka leo Serikali haijasema
chochote kuhusu uchunguzi wa dawa ya babu. Mpaka leo Serikali haijatoa kauli
yoyote na wala kuchukua hatua yoyote dhidi ya Mzee Masapila ambaye Februari hii
alitoa kauli nyengine juu ya ugunduzi wa dawa nyengine.
Mheshimiwa Spika, Timu
ya uchunguzi iliyoundwa mpaka mwezi machi 2011 ilikuwa imeandaa kukamilisha taratibu, ili kufuatilia maendeleo ya
kiafya ya wagonjwa 200, ambao wamekubali kwa ridhaa yao wenyewe, kushiriki
katika utafiti huu, ili kuona maendeleo yao kiafya, baada ya kunywa dawa ya
Mchungaji mstaafu Ambilikile Masapila, kwa maradhi walionayo, kwa kufuata
vigezo vyote vya Kitaifa na Kimataifa.
Mheshimiwa
Spika, naomba
kutoa nukuu ya Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya
Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Charys Ugullum, na timu ya wataalamu iliyoanza
utafiti wake wa awali Machi 7, 2011, timu
hiyo ilijumuisha wataalamu kutoka Wizara ya Afya, TFDA, Taasisi ya Utafiti wa
Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Mkemia Mkuu wa Serikali na Taasisi ya Utafiti wa
Dawa za Asili ya Chuo Kikuu cha Afya ya Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS),
kwamba; "Serikali imesema imeridhishwa na dawa
inayotolewa na Mchungaji Ambilikile Mwasapila wa Kijiji cha Samunge, Loliondo
ikisema haina madhara yoyote kwa matumizi ya binadamu,”
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inatoa ushauri kwa serikali kwa kuanzisha taasisi ya kitaifa
itakayoweka takwimu za dawa za asili na kuibua mipango itakayohamasisha
wananchi katika tiba asili pamoja na kujengewa uwezo na kuwezeshwa katika sekta
hii; pia kuongezwa kwa viwanda vitakavyozifanya dawa hizo kuwa za kibiashara,
na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na zile za umma; kufanya
uchambuzi yakinifu na tafiti za kuinua sekta ya miti ya tiba asili kwa
kuainisha mikoa na sehemu ambazo zina miti ya tibaasili itakayoenda sambamba na
upandaji wa miti ya dawa kwa ajili ya biashara kama vile milonge, Artemisia
annua; kuwepo kwa mipango mikakati ya kuinua
teknolojia na uwekaji ubora wa dawa hizo na kuitunza miti hiyo ya dawa.
Tukifanya hivyo, dawa za asili zitaleta ajira na kukuza uchumi wa nchi yetu.
12.0 USIMAMIZI
WA FEDHA KWA MIRADI MISONGE
Mheshimiwa Spika, Serikali
kwa kupitia wizara hii ilianzisha mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji wa
taarifa za mapato na matumizi ya fedha kwa miradi misonge ambayo ni Mradi wa
Kifua Kikuu, UKIMWI na Malaria kwa mwaka 2011/2012. Mfumo huu unawezesha kutoa
ripoti kwa wakati kulingana na mahitaji, hivyo utatumika pia kwenye miradi
mingine. Aidha, Hospitali za Rufaa Mbeya na KCMC zimeanza kutumia mifumo
ya aina hiyo katika shughuli mbalimbali za ukusanyaji wa taarifa za hospitali;
zikiwemo taarifa za fedha, huduma za wagonjwa pamoja na za kiutawala. Kambi
rasmi ya Upinzani inataka takwimu rasmi ya jumla na idadi ya hospitali zenye
miradi misonge iliyopo sasa na mafanikio na changamoto za mfumo huo na mikakati
ya Wizara kwa mwaka huu wa fedha wa 2013/2014 katika kuhakikisha kuwa mfumo huu
wa kielektroniki unasambaa nchi nzima.
13.0
HOSPITALI ZA MIKOA
Mheshimiwa
Spika, ni vizuri fedha zinazotengwa kwa ajili ya afya
zikatumika ipasavyo kwani afya ndo msingi bora wa maisha ya watanzania, kwa
mwaka wa fedha 2013/14 fedha
zilizotengwa kwa ajili ya hospitali za mikoa ni bilioni 65 ikilinganisha na
kiasi cha bilioni 68 zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na kwa ajili
ya fedha za maendeleo.Kambi ya upinzani inahitaji majibu ya kutosha kutoka
serikalini ni kwa nini fedha zinatengwa kidogo kwenda kwenye mikoa ili hali ndo
sehemu ambazo watanzania wengi wanaishi na kufanya shughuli zao za maendeleo.
Mheshimiwa
Spika,Kwa mwaka wa fedha 2013/14 fedha zilizotengwa
kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za mikoa ni takribani kiasi cha bilioni tatu
fedha hizi zimetengwa kwa ajili ya mikoa ya singida pwani na manyara. Kambi ya upinzani inashauri
ujenzi wa hospitali za mikoa zitengewe fedha nyingi na kwa wakati il;I kuweza
kufanikisha ujenzi kwa haraka na wananchi waweze kupata hudumu kwa wakati
muafaka .Kukamilika kwa wakati kwa ujenzi wa hospitali za mikoa zitasasidia
kupunguza mzigo mkubwa wa wagonjwa unaozikikumba hospitali za wilaya hivyo kufanya watu wengi kukimbilia
hospitali kuu za kitaifa kama muhimbili ili hali matatizo yao yangeliweza
kutatuliwa katika ngazi ya mkoa.
14.0
AFYA NA USAFI WA MAZINGIRA
Mheshimiwa
Spika, ni wazi kuwa pamoja na kuendeshwa kwa mashindano
ya afya na usafi wa mazingira yanayohusisha Halmashauri zote nchini, tatizo la
uchafu wa mazingira ambao ni hatarishi kwa afya za wananchi. Pamoja na kuwa
mashindano hayo kuwa na zawadi mbalimbali katika kila kundi ili kuhamasisha
wadau mbalimbali katika shughuli za usafi wa mazingira kwa washindi wa kila
kundi lakini Serikali kwa kupitia wizara hii inashindwa kuelewa kuwa,
changamoto si kutoa zawadi kwa washindi wa mashindano ya usafi wa mazingira
bali ni nini kinafanyika kwa halmashauri zinazoshindwa katika utunzaji na usafi
wa mazingira. Ni jambo la ajabu kuwa mashindano yanafanyika kuwazawadia wasafi
lakini hakuna adhabu kwa halmashauri chafu jambo linalofanya usafi wa mazingira
kuonekana si kipaumbele kwa halmashauri.
15.0 MWENENDO WA
BAJETI YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
Mheshimiwa
Spika, Kama ilivyo kawaida hali ya bajeti imekuwa
katika sura ileile ya kutengewa fedha kidogo ambazo hazikidhi mahitaji.Hakika
bila ya kuwa na afya ya kutosha huwezi kuwa na mipango yoyote endelevu. Bado
bajeti yetu haijakidhi hata kidogo azimio la Abuja la kutenga kiasi cha 15% ya fedha
zetu za ndani kwa ajili ya bajeti ya afya. Kwa miaka mitatu mfululizo bajeti ya
afya imekuwa imetengewa kama ifuatavyo; kwa mwaka wa fedha wa 2010/2011 (12.1%),
2011/2012 (10.4%), na 2012/2013 (10.4%)
Mhesimiwa
Spika, Bajeti ya wizara ya afya na ustawi wa jamii
imeongezeka kutoka kiasi cha shilingi 576 bilioni hadi kiasi cha shilingi
bilioni 748 hili likiwa ni ongezeko la asilimia 29.9 lakini ukiangalia kwa makini utagundua
kuwa kuwa bajeti ya afya imekuwa
tegemezi kwa kiasi kikubwa. Kwa mwaka wa fedha 2013/14 Serikali imetenga
bilioni 36 tu kwa fedha za maendeleo ilhali tukitegemea kiasi cha bilioni 435
kutoka kwa wahisani. Kambi Rasmi ya upinzani inahitaji majibu ni kwa nini kila
mara utegemezi unakuwa mkubwa hali inayoweka maendeleo ya afya na ustawi wa
nchi yetu rehani endapo wahisani watajitoa katika kufadhili miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa
Spika, Japokuwa, tumekua tukitenga fedha kwa ajili ya
Wizara ya Afya na ustawi wa jamii bado fedha tunazotenga hazitolewi kwa wakati
na hivyo kufanya wizara kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Mwaka wa
fedha 2012/13 bunge lako liliidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 581 kwa ajili
ya wizara lakini cha kushangaza hadi mwezi Machi mwaka huu kiasi cha bilioni
325 zilipokelewa na wizara ikiwa ni asilimia 66.6 ya fedha zote zilizotengwa.
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inahitaji maelezo ni
kwa nini Serikali inashindwa kutoa fedha zilizoidhinishwa kwa mwaka 2012/13. Serikali
ilitenga kiasi cha bilioni 19 kama mchango wake katika fedha za maendeleo
lakini hadi Machi 2013, Serikali ilitoa tu kiasi cha bilioni 12 tu; hiki ni kitendo cha kustaajabisha.
Hata hivyo Serikali yetu, sikivu, imeshindwa kutoa fedha za maendeleo kwa
wakati na sasa tunahoji tunapeleka wapi mustakabali wa afya na ustawi wa taifa
letu.
Mheshimiwa
Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi
ya Upinzani, naomba kuwasilisha.
……………………………………..
Dr.
Antony G. Mbassa (Mb)
Msemaji
Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
08.05.2013
Chanzo:CHADEMA social media.
No comments:
Post a Comment