HOTUBA YA MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI WIZARA YA NISHATI
NA MADINI JOHN JOHN MNYIKA (MB) KUHUSU MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI
JUU YA MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2012/2013 NA MAKADIRIO
YA MATUMIZI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014
(Inatolewa chini ya kanuni ya 99(9) toleo la mwaka 2013)
A:
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Ofisi
ya Waziri wa Nishati na Madini ilianzishwa kwa mujibu wa kipengele cha 21 cha
Nyongeza ya Waraka wa Rais uliochapishwa kama Tangazo la Serikali Na. 494 la tarehe 17 Desemba 2010. Majukumu ya
Ofisi hii yameainishwa katika Tangazo la
Ukasimishaji wa Majukumu ya Kiuwaziri la mwaka 2010 (The Ministers [Assignment
of Ministerial Functions] Notice, 2010) lililochapishwa katika Gazeti la Serikali kama Tangazo la Serikali Na. 494A la tarehe 17
Desemba 2010.
Mheshimiwa Spika, Katika
kujadili Mapitio ya Utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2012/2013 na Makadirio ya
Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2013/2014
naomba tuyatafakari maandiko ya katika muktadha wa uongozi wetu wa leo na hatma
ya sekta hizi mbili muhimu za nishati na madini.
Mheshimiwa Spika,
Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha TUJISAHIHISHE katika ukurasa wa pili tutafakari kwamba, naomba kumnukuu ‘ukweli una tabia moja nzuri sana. Haujali
mkubwa wala mdogo; haujali adui wala rafiki. Kwake wote ni sawa. Pia ukweli
unayo tabia ya kujilipiza kisasi kama ukipuuzwa.Ukiniona nataka kulipiga teke
jiwe kwa kuwa nafikiri kuwa ni dongo au mpira, natumaini utanionya. Lakini
nikilipuuza onyo lako kwa sababu eti wewe ni mdogo au kwa sababu sikupendi,
nitalipiga teke, basi litanivunja dole japo ningekuwa nani. Ukweli haupendi
kupuuzwapuuzwa.
Mheshimiwa Spika,
Tuendelee kutafakari maandiko ya Nyerere kwamba
‘Wakati mwingine, mtu tunayempinga huwa anamakosa kweli, lakini hoja
tunazozitoa ni za kinafsi na hazihusiani kabisa na hoja zake.Nikisema mbili na
tatu ni sita, nakosa. Lakini ni bora kunionyesha kwamba pengine nifikiri
tunazidisha kumbe tunajumlisha.Ni kweli mbili mara tatu ni sita;lakini mbili na
tatu ni tano, siyo sita. Lakini ukijaribu kuwashawishi wenzetu wakatae mawazo
yangu na kukubali yako kwa kusema kuwa meno yangu ni machafu ,au natoa kamasi
daima, utakuwa unatumia hoja ambazo hazina maana, Huu ni mfano wa upuuzi;
lakini mara nyingi hoja tunazozitumia kuwashawishi watu wakatae mawazo ya wale
tusiowapenda,au kukubali mawazo yetu, huwa haziuhusiani kabisa na mambo
tunayojadili’.
Mheshimiwa Spika, Tutafakari
maandiko ya Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha UONGOZI WETU NA HATIMA YA TANZANIA uk. 50, nanukuu “Rais
Mwinyi ni mtu mwema na mpole, lakini ni kiongozi dhaifu; au upole wake na
udhaifu wake unatumiwa na watu ambao wala si wema wala wapole kuhatarisha umoja
na amani ya nchi yetu, Kipindi chake cha pili kinakaribia kwisha”.
Mheshimiwa Spika, Tutafakari
maandiko mengine ya Mwalimu Nyerere kwamba “lakini
hatulazimiki kuendelea na uongozi mbovu wa chama na Serikali. Wala tukiendelea
na hali hii, bila kubadili uongozi wa Chama na Serikali, sina hakika kama
tutafika huko salama.Masuala muhimu ya nchi yetu hayatashughulikiwa.Viongozi
wetu wataendelea na matendo yao ya kuvuruga muungano. Matatizo ya kweli ya
muungano hayatashughulikiwa, maana hatuna serikali ya kuyashughulikia.Na
masuala mengine muhimu ya uchumi, huduma za umma, rushwa,chuki za uzawa na
ukabilana udini yataachwa yajitatue yenyewe.Nasema , katika hili kama hiyo sina
hakika kama tutafika salama;na tukifika “salama”,tukiwa na uongozi huu huu wa
chama na serikali , mbele yetu kutakuwa ni giza tupu.Majuto ni mjukuu, huja
baadaye.Tunaweza tukafikishwa mahali tukilinganisha uongozi wa rais Mwinyi na
wa rais wa kesho tukaona kuwa chini ya Ndugu Mwinyi, Pamoja na udhaifu wake
wote, tulikuwa peponi”!
Mheshimiwa Spika,
Mwalimu Nyerere anaendelea kuandika kwamba “Waingereza wana msemo “Nature abhors vacuum”, “hulka huchukia ombwe” . Hata siasa huchukia
ombwe. Kama uongozi ni mbovu, upo kama haupo au upo kwa masilahi ya wenyewe,
watatokea watu waujaze uwazi uliopo;hauwezi kuachwa wazi hivi hivi.Lakini
uongozi mbovu ni kama mzoga, unatabia ya kukaribisha mafisi na mainzi.
Tusidhani kuwa hulka ya siasa yetu ni tofauti na hulka ya siasa ya watu
wengine; kwamba sisi tunaweza kuvumilia uongozi mbovu na tusivune matunda ya
hulka ya uongozi mbovu”.
Mheshimiwa Spika,
Mwalimu Nyerere alikuwa akiandika wakati wa awamu ya Rais Mwinyi kuhusu masuala
yanayohusu Muungano; sisi tutafakari maandiko haya katika muktadha wa uongozi
wa sasa wa taifa letu na mustakabali wa sekta nyeti kwa uchumi wa nchi na
maisha ya wananchi za nishati na madini.
1.0 MAPITIO UJUMLA YA UTEKELEZAJI KWA
MWAKA 2012/2013 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2013/2014
Mheshimiwa Spika, tarehe
27 Julai, 2012 niliwasilisha Bungeni maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/2012 na makadirio ya
matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Kufuatia
maoni hayo, yapo masuala machache ambayo Serikali imeyazingatia kwenye
utekelezaji na mengine mengi ambayo Serikali haikuyazingatia pamoja na umuhimu
wake kwa maslahi ya nchi na maisha ya wananchi.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani ilitaka kiwango cha bajeti ya Wizara ya Nishati na
Madini kuongezwa, miongoni mwa masuala ambayo serikali imetekeleza ni pamoja na
kuongeza bajeti ya wizara hii kwa kupanga kutumia kwa mwaka 2013/2014 jumla ya
shilingi 1,099,434,031,000/= ikilinganishwa
na mwaka 2012/2013 ambako kiasi cha shilingi 641,269,729,000/= kilipangwa kutumika. Aidha napenda kuikumbusha serikali kuzingatia vipaumbele vya
miradi ya maendeleo ambavyo Kambi Rasmi ya Upinzani ilipendekeza katika Hotuba
zake za 2011 na 2012 ili kuweza kuleta maana ya ongezeko hili la bajeti kwa
maana ya kuvipatia vipaumbele uzito unaostahili kwa Kuwekeza fedha za kutosha
kwenye sekta ya umeme na Gesi ili kumaliza kabisa tatizo la nishati ya Umeme na
kupunguza gharama za maisha kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika,
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilishauri kuwepo kwa mfumo thabiti wa
kuhakikisha maoni na maazimio yanatekelezwa kwa wakati na kwa ukamilifu. Lakini
serikali imeendelea kupuuza mapendekezo hayo na kutoa ahadi ambazo haikuwa
tayari kuzitekeleza, mathalani ahadi ya Mhe Waziri Mkuu aliyotoa wakati
akiahirisha bunge la bajeti 2011/2012 ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima
ili kuongeza pesa wizara ya Nishati na Madini lakini tofauti na ahadi yake,
Serikali ikaamua kuja na mpango wa kukopa fedha katika taasisi za fedha ili
kulinusuru shirika la umeme Tanzania TANESCO, ambao nao haujatekelezwa kwa
ukamilifu.
Mheshimiwa Spika,
pamoja na hali hiyo ninatambua maoni
machache ambayo yalizingatiwa kuhusu gesi asili, ikiwemo kuendelezwa kwa
mchakato wa kuwa na sera na sheria ya gesi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inayoongozwa na CHADEMA ikaitaka Serikali ieleze hatua ilizochukua juu ya maoni
ya kambi rasmi ya Upinzani Bungeni ambayo hayakuzingatiwa na mengine yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya
Bunge na michango ya Wabunge kwa nyakati mbalimbali mwaka 2011 na 2012.
Aidha,
ni Kwa bahati mbaya kabisa serikali haikupenda kufanyia kazi maoni na ushauri
iliyopewa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,kamati ya Bunge na wabunge
mbalimbali kwa nyakati tofauti na ambayo kama yangezingatiwa kikamilifu yangeweza kuliepusha taifa na matatizo yaliyotokea
katika mikoa ya Lindi na Mtwara na ambayo bado yanaendelea mpaka sasa.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2012/2013 makadirio ya mapato na matumizi ya kawaida yanaombewa jumla ya
shilingi 107,221,286,000/= kati ya
fedha hizo kiasi cha shilingi 11,612,542,000/=
ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi
wa wizara na taasisi zilizochini yake na kiasi cha shilingi 95,608,744,000/= ni kwa ajili ya
matumizi mengine (OC). Matumizi haya
yanaonekana ni pungufu ya kiasi cha shilingi 2,857,582,000/= kwenye
bajeti ya mwaka jana katika fungu hili la matumizi ya kawaida.
Mheshimiwa Spika, upungufu
huu, unaacha maswali, Kambi rasmi ya upinzani Bungeni inaitaka serikali
kuwaeleza watanzania sababu za kupungua kwa bajeti ya mishahara ya wizara na
taasisi zilizokochini yake, ambayo katika mwaka wa fedha 2012/2013 Wizara ya
Nishati na Madini ilitengewa shilingi 17,292,347,000/=
na kwa mwaka huu wa fedha 2013/2014 serikali inaomba kiasi cha shilingi 11,612,542,000/= ikiwa ni pungufu
ya shilingi 5,679,805,000/= Kambi Rasmi
ya Upinzani inataka majibu kwa kuwa wakati wafanya kazi wakitarajia kupandishwa
madaraja na ongezeko la mishahara kutokana na kupanda kwa gharama za maisha
pamoja na mfumko wa bei, bajeti ya mishahara kwa Wizara na taasisi zilizochini
yake inapunguzwa.
Mheshimiwa Spika,Kambi
Rasmi ya Upinzani inataka maelezo iwapo punguzo hilo ni kutokana na kubana
matumizi au ni udhaifu katika maandalizi ya bajeti na nini athari zake kwenye
ufanisi wa wizara na taasisi zake? Au wizara imebaini mianya ya ufisadi ambayo
ilikuwepo katika bajeti zilizopita kuhusiana na fungu la mishahara?
Mheshimiwa Spika,
Serikali hii ya CCM inaonekana kuziba masikio katika kupunguza matumizi yasiyo
ya lazima pamoja na Kambi rasmi ya upinzani Bungeni, wananchi na wadau wa
maendeleo kulipigia kelele swala hili. Jambo hili limejirudia kwa upande wa
matumizi ya kawaida, ambapo serikali iliomba kiasi cha shilingi 92,786,521,000/= katika Bajeti ya mwaka
2012/2013 na mwaka huu wa fedha 2013/2014 serikali inaomba kiasi cha shilingi 95,608,744,000/= ikiwa ni ongezeko la
shilingi 2,822,223,000/=.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa rai kwa wabunge na Bunge kuungana pamoja kabla
ya kupitisha matumizi haya makubwa na kuitaka Wizara ya Nishati na madini
kubana matumizi kwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ili tupate fedha za
kuwekeza kwenye nishati .
Mheshimiwa Spika,
katika kuendelea kuonyesha udhaifu na uwezo mdogo wa wizara katika kusimamia
sheria za nchi, kwa mujibu wa taarifa ya CAG ya Juni 2012 nchi imepoteza kiasi
cha dola za kimarekani 12,634,354.61 sawa na shilingi bilioni 19.71. Hizi ni
fedha ambazo hazikukusanywa kutoka kwa makampuni ya madini kwa kufuata sheria
mpya ya madini ya mwaka 2010, kifungu cha 87(1) kuwa mrahaba wa 4% utozwe kabla
ya makato na badala yake mrahaba ukawa
ni 3% na kutozwa baada ya makato kama sheria ya zamani ilivyokuwa.
Mheshimiwa Spika,katika
kipindi cha utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/2012 na 2012/2013, iliathiriwa
kwa kiwango kikubwa na mvutano baina ya Watendaji Waandamizi wa Wizara ya
Nishati na Madini na Taasisi zake kwa upande mmoja na baadhi ya wabunge kwa
upande mwingine katika mvutano ambao uliambatana na kutuhumiana hadharani
kupitia vyombo vya habari juu ya tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya
madaraka. Baadhi yakiwa yamejidhihirisha kufuatia chunguzi na ripoti
zilizofanyika na kubaini kasoro kubwa za kiutendaji hususan kupitia ukaguzi
maalum uliofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Shirika la
Umeme (TANESCO).
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA, inataka Serikali ieleze hatua
iliyofikiwa katika uchunguzi juu ya ununuzi wa mafuta mazito kama ambavyo
tulipendekeza ufanyike. Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kwamba Mamlaka ya
Ununuzi wa Umma (PPRA) nayo iliwahi kueleza kwenye vyombo vya habari kuwa imeanza
uchunguzi ambao ulipaswa kukamilika mwaka 2012; hivyo tunataka taarifa ya
uchunguzi iwekwe hadharani na Serikali ieleze hatua ilizochukua dhidi ya madai
ya ufisadi na matumizi ya madaraka kupitia mianya ya dharura ya umeme.
2.0
Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge
2.1 Maazimio kuhusu uhalali wa
uchangishaji (‘Sakata la Jairo’).
Mheshimiwa Spika,
kwa kipindi cha mwaka 2011/2012 Bunge lako lilishuhudia mambo kadhaa yaliyokiuka
miiko ya uongozi, ambalo yalilazimu bunge kuunda kamati teule kuchunguza
uhalali wa uchangishaji uliofanyika katika Wizara ya Nishati na Madini (‘Sakata
la Jairo’) na baadhi ya mapendekezo yake ambayo yalipitishwa kuwa maazimio yalikuwa;
(1). Kamati
Teule inapendekeza kwamba Serikali ichukue hatua za kinidhamu kwa Ndugu David
Kitundu Jairo kwa matumizi mabaya ya madaraka, kukusanya na kutumia fedha za
Serikali kinyume cha Sheria, Kanuni na Taratibu za Fedha za Umma na kuruhusu
matumizi mabaya ya fedha za Umma.
(2)Vile
vile Serikali iwachukulie hatua za kinidhamu, kwa mujibu wa Sheria, watumishi
wote wa Wizara ya Nishati na Madini waliotajwa kwenye Taarifa hii kushiriki kwa
namna mbalimbali katika mchakato wa uchangishaji na matumizi ya fedha hizi za
umma. Aidha, kwa kuwa kwa mujibu wa Mwongozo wa Baraza la Mawaziri Waziri ndiye
Msimamizi Mkuu wa Wizara, hivyo suala la uchangishaji halikupaswa kufanyika bila
yeye kufahamu,
(3).
Kamati Teule inapendekeza Serikali ichukue hatua zinazofaa kwa Waziri wa
Nishati na Madini, Mhe. William Ngeleja, (Mb.)
(4).,………..
Kamati Teule inapendekeza Serikali ichukue hatua zinazofaa kwa Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa upotoshaji huo.. ,
(5).
…… Kamati Teule inapendekeza Serikali ichukue hatua zinazofaa kwa Katibu Mkuu
Kiongozi.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inahoji ni kwanini hadi sasa
Bunge hili limeshindwa kuhakikisha kwamba maazimio haya yametekelezwa na
Serikali? Hakika huu ni uzembe wa wazi wa Bunge
kushindwa kutimiza majukumu yake ya kuisimamia serikali kwa mujibu wa
katiba .
Aidha,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge hatua za utekelezaji
wa maazimio hayo ya Bunge, kwani baadhi ya wahusika bado wapo ma-ofisini wakiendelea
na kazi na wengine wakiendelea kuteuliwa kushika nafasi zingine katika uongozi
na utumishi wa umma kama vile hakuna liliowahi kutokea.
2.2 MAAZIMIO YA RICHMOND
Mheshimiwa Spika: Itakumbukwa
kwamba taarifa mbili za serikali kuhusu utekelezwaji wa maazimio haya ziliwasilishwa
Bungeni na Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda, tarehe 28 Agosti, 2008 na tarehe 11
Februari, 2009 . Taarifa moja ilikabidhiwa na kujadiliwa na Kamati, ambazo
zililitaarifu Bunge kuwa utekelezaji wa Maazimio 10 kati ya 23 yaliyotolewa na
Bunge, yalifanyiwa kazi hadi mwezi Februari, 2009 na Maazimio 13 bado yalikuwa
hayajakamilika.
Mheshimiwa
Spika; Bunge liliazimia kwamba taarifa za utekelezaji wa
maazimio yaliyobaki ziwasilishwe kwa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama
ambayo hata hivyo katika mwaka 2011, 2012 na mpaka mabadiliko ya muundo wa
Kamati yalipofanyika kamati hiyo haikuwasilisha taarifa yoyote bungeni ya
kueleza kukamilika kwa utekelezaji wa maazimio husika hali ambayo inahitaji
bunge kuingilia kati kuweza kuisimamia Serikali kwa mujibu wa Katiba ya Nchi
Ibara ya 63 (2) na (3).
Mheshimiwa
Spika, katika hali inayozua maswali kuhusu umakini wa Bunge
katika kusimamia maazimio yake mwaka 2011, Mbunge wa Monduli Mheshimiwa Edward
Lowassa; aliyekuwa Waziri Mkuu na kujiuzulu kufuatia kashfa hiyo ya Richmond
alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na
Usalama iliyopewa dhamana na Bunge kufuatilia utekelezaji wa maazimio kuhusu
mkataba kati ya TANESCO na Richmond. Katika hali hiyo, haishangazi kwamba kwa
miaka miwili toka wakati huo, mpaka mabadiliko ya Kamati za Bunge
yalipofanyika; Kamati hiyo katika Taarifa zake zote bungeni haijawahi
kuisimamia Serikali kuhakikisha maazimio husika ya Bunge yanatekelezwa. Huu
ndio uwajibikaji, ndani ya Serikali na uongozi wa Bunge; vyote vikiongozwa na
CCM.
Mheshimiwa
Spika, sasa inajulikana wazi kuwa Mkataba wa TANESCO na
Richmond ulirithishwa kinyemela kwenda kwa Dowans kama inavyoonekana katika
nyaraka za mahakama ambapo Dowans na Richmond zilidaiana huko Marekani; na kuwa
hilo lilifanyika bila kuitaarifu TANESCO kinyume na kifungu cha 15:12 cha
Mkataba huo.
Mheshimiwa
Spika, Kutokana na hukumu ya Dowans ushahidi umepatikana na
kuwa mashahidi mbalimbali walioitwa mbele ya Kamati Teule ya Bunge na wakiwa
chini ya kiapo walitoa taarifa za uongo kuwa mkataba kati ya Richmond na
Tanesco ulihamishwa kwenda Dowans Disemba 23, 2006 na hivyo wahusika hao
mbalimbali – wakiwemo wamiliki wa Richmond – walidanganya au kuficha ukweli
mbele ya Kamati Teule na hivyo kuonesha dharau dhidi ya Bunge.
Mheshimiwa
Spika; Masuala haya ni muhimu yakajadiliwa sasa ili kupata
undani wa wahusika wanaopaswa kubeba mzigo wa fidia kwa kampuni ya Dowans
badala ya kubebesha mzigo huo TANESCO na umma wa watanzania. Kushindwa
kuwashughulikia kwa ukamilifu mafisadi wa Richmond na kukwepa kutumia mianya ya
sheria za kimataifa kukana mikataba iliyoingiwa kwenye mazingira ya ufisadi kwa
mara nyingine tena kunaelekea kuligharimu taifa hivyo wakati umefika sasa wa
Bunge kuingilia kati kwa niaba ya wananchi.
Mheshimiwa Spika; Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Wizara ya Nishati na Madini na Serikali kwa ujumla
kutoa majibu bungeni juu ya hatma ya maazimio 10 yaliyobaki: Nambari
3,5,7,8,9,10,11,13,14 na 18 ili bunge liweze kuishauri na kuisimamia serikali
kuhakikisha maazimio husika yanatekelezwa kwa ukamilifu na kwa haraka.
Kambi Rasmi ya Upinzani, inataka Taarifa
ya utekelezwaji wa Maazimio tajwa yaliyotolewa na Bunge juu ya Mkataba baina ya
TANESCO na Kampuni ya Richmond Development Company LLC badala ya kuwasilishwa
kwenye Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ambayo kwa sasa haipo, sasa
iwasilishwe kwenye Bunge zima ili yaweze kujadiliwa na hatima yake iweze
kujulikana.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ieleze kwanini mpaka sasa
haijatekeleza maazimio hayo na bunge
liweke muda wa ukomo wa kutekeleza Maazimio yote ya Bunge yaliyokuwa yamesalia
katika sakata hili la Richmond ili mara moja na daima sakata hili la Richmond
limalizwe na kufungwa baada ya maazimio yote kutekelezwa kwa ukamilifu. Ikiwa
maazimio ya mwaka 2008 utekelezaji wake haujakamilika mpaka mwaka 2013 kwa miaka
mitano, nini kitalihakikishia taifa kwamba maazimio mengine mapya
yaliyopitishwa 2011 na 2012 yatatekelezwa kwa wakati na kwa ukamilifu?
Mheshimiwa Spika:
Azimio Na. 3, ambalo liliagiza kwamba “Mkataba kati ya TANESCO na
Richmond Development Company LLC (uliorithiwa na Dowans Holdings S.A.) na
ile kati ya TANESCO na IPTL, SONGAS, AGGREKO na Alstom
Power Rentals, ipitiwe upya mapema iwezekanavyo kama ambavyo Mikataba ya
Madini ilivyopitiwa upya na Serikali”. Iwapo Azimio hili lingetekelezwa kwa
ukamilifu wake, gharama za uzalishaji TANESCO na serikali kwa ujumla
zinazotokana na matatizo katika mikataba zingepungua.
(1) Mheshimiwa
Spika, Azimio Na. 5 Mkataba
kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC na sasa Dowans Holdings S.A
umesheheni makosa mengi ya kisheria yanayoashiria udhaifu mkubwa wa kitaalamu
katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali au ukosefu wa umakini ama ubinafsi
katika kuiwakilisha Serikali. Kwa mfano, kushindwa kutambua ukosefu wa sifa za
kikampuni za Richmond Development Company LLC; kushindwa kuishauri
Serikali kuifanyia kampuni hiyo ukaguzi
wa awali (due deligence) au ukaguzi
baada ya uteuzi (post qualification); kushindwa kutambua tofauti kati ya consortium agreement na proprietary information agreement;
kushindwa kuona dosari kisheria za proprietary
information agreement; kushindwa kuona tofauti kisheria kati ya Richmond
Development Company LLC, RDEVCO,RDVECO na RDC, majina ambayo wamiliki wa
Richmond Development Company LLC walikuwa wanayatumia kwa kubadilisha badilisha
(interchangerbly) kwa makusudi;
kushindwa kuwashauri Wajumbe wa GNT kwamba business
card si mbadala wa hati mahsusi kisheria; kushindwa kuishauri Serikali
kuhakikisha kuwa muhtasari wa majadiliano kati ya Kamati ya Serikali ya
Majadiliano (GNT) na Richmond Development Company LLC ambao ulizingatia baadhi
ya maslahi ya nchi, uwe sehemu ya Mkataba kati ya TANESCO na Richmond
Development Company LLC; kushindwa kuishauri Serikali kutumia fursa iliyokuwepo
wazi ya kuvunja Mkataba baada ya Richmond Development Company LLC kushindwa
kutekeleza sehemu yake ya Mkataba; kushindwa kuhudhuria idadi kubwa ya vikao
muhimu vya majadiliano;n.k. Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye katika
majadiliano yake na Kamati Teule alionyesha kutokuelewa kabisa kilichokuwa
kinatendeka na wasaidizi wake, na mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Wakili wa Serikali Donald Chidowu, ambaye ushiriki wake katika GNT haukuwa na
tija yeyote, wawajibishwe na Mamlaka ya juu ya nchi kwa kuchangia kuiingiza
nchi katika mkataba wa aibu.
(2) Mheshimiwa
Spika, Azimio Na. 7 lilikuwa “
Kamati Teule inapendekeza kuwa Wajumbe wote wa GNT ambao ni maafisa waandamizi
wa Serikali wawajibishwe mara moja kwa kushindwa kutumia elimu na ujuzi wao
kulinda maslahi ya Taifa”.
Aidha,
Azimio namba 9 lilikuwa linataka mabadiliko
ya haraka ya uongozi wa taasisi ya TAKUKURU.
Mheshimiwa
Spika, Azimio Na. 13 “ Kamati Teule inatoa wito kwa Kamati
zote za Bunge zihakikishe kuwa zinapitia mikataba mikubwa na ya muda mrefu ya
kibiashara chini ya sekta zao ili kuliondolea Taifa mizigo isiyo ya lazima.
Pale ambapo upatikanaji wa mikataba hiyo unakwamishwa kwa urasimu usio wa
lazima Kamati zitumie utaratibu uliotumiwa na Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na
Biashara ya kuunda Kamati Teule yenye ufunguo wa mikataba iliyofichika”.
Mheshimiwa Spika,
Azimio Na. 14 “Kamati Teule inapendekeza kwamba Waziri wa Nishati na Madini wa
wakati huo Mhe. Dk. Ibrahim Msabaha (Mb) na Katibu Mkuu Ndugu Arthur Mwakapugi
wachukuliwe hatua kali za kinidhamu kwa kuliingiza Taifa kwa makusudi kwenye
mkataba na kampuni ya mfukoni ambao umesababisha hasara kubwa kwa nchi. Aidha
Kamishna wa Nishati Ndugu Bashir Mrindoko naye achukuliwe hatua za kinidhamu
kwa kushindwa kumshauri Katibu Mkuu mpya wa Wizara kuhusu udhaifu wa Richmond
Development Company LLC ambao ulijulikana dhahiri na Wizara toka mwaka 2004
kwenye mkataba wa Bomba la Mafuta. Ndugu Mrindoko ndiye aliyeiandikia barua
kampuni hiyo kusitisha mkataba wake na Serikali mwezi mmoja tu kabla ya
mchakato wa zabuni ya umeme wa dharura haujaanza”.
2.3 Kamati ya wataalamu wa Ofisi ya
Spika.
Mheshimiwa
Spika, mbali na maazimio hayo pia kuna uchambuzi uliofanywa na
kamati ya wataalam wa Ofisi ya Spika, kuhusiana na makampuni yanayouza umeme
kwa TANESCO ambayo mikataba yake haipishani na ule wa RICHMOND, taarifa hiyo iliwasilishwa
Bungeni wakati Mhe Harrison Mwakyembe akiwasilisha Taarifa yake ya Kamati Teule
ya RICHMOND ili Waziri atoe ufafanuzi ni kwa kiwango gani mapendekezo yake
Serikali imeyafanyia kazi;
(a) “Uhalali
kisheria wa Kampuni ya Aggreko (legal status)
Kwa mujibu wa maelezo
yaliyomo kwenye Mkataba, Kampuni ya Aggreko International Projects Limited ni
Kampuni iliyosajiliwa chini ya Sheria za nchi ya Scotland. Uchambuzi na utafiti
wetu haukuweza kuthibitisha kuwa Kampuni hiyo kweli imesajiliwa kisheria huko
Scotland ili kubaini kama kulikuwa na udanganyifu kama ule uliofanywa na
Kampuni ya RICHMOND, yaani kutoa taarifa za uongo kuhusu uhalali kisheria wa
Kampuni.
(b) Malipo
ya Kodi
Kama ilivyo katika Mkataba wa Kampuni
ya Richmond, Kifungu cha 3.4 cha Mkataba wa AGGREKO kinatamka kwamba, kodi zote
na malipo mengine yanayotokana na uingizaji nchini na utoaji nchi za nje ya
nchi wa Mitambo ya uzalishaji wa umeme, ikiwa ni pamoja na vipuri na vifaa
vingine vinavyohusika na uendeshaji wa Mtambo huo italipwa na TANESCO. Aidha,
Kifungu hicho kimeweka pia sharti kwamba, pale ambapo bodi au malipo yoyote
yatadaiwa na Mamlaka yoyote ya kodi kutoka kwa AGGREKO, Kampuni hiyo
italijulisha Shirika la TANESCO ambalo litalipa kodi au malipo hayo kwa mamlaka
husika au litairejeshea AGGREKO fedha ambazo itakuwa imelipa kwa Mamlaka hiyo
katika kipindi cha siku 14.
(c) Malipo
Kwa mujibu wa Vifungu vya 4.2 na 4.3
vya Mkataba, Shirika la TANESCO linawajibu wa kuilipa Kampuni ya Aggreko malipo
yafuatayo:-
i. ‘Capacity Charge’ – Dola za Marekani
35.928 kwa Kw kwa mwezi [Tazama Kiambatanisho C cha Mkataba].
ii. Malipo ya Umeme (energy purchase price)
– Dola 4.99 kwa Kwh [Tazama tafsiri ya interim energy purchase price katika uk.
wa 3 wa Mkataba]
(d) Fidia
kwa Ucheleweshaji wa Kuzalisha Umeme.
·
Kwa
mujibu wa Kifungu cha 4.4.2 cha Mkataba, Aggreko inawajibika kulipa kwa TANESCO
Dola ya Marekani 0.5 kwa Kw kwa siku kwa wiki 4 za kwanza za ucheleweshaji, na
baada ya hapo’ kama ucheleweshaji wa uzalishaji umeme utaendelea, anawajibika
kulipa Dola ya Kimarekani 1 kwa Kw kwa siku.
·
Hata
hivyo, malipo hayo ya fidia (liquidated damages) yamewekewa ukomo chini ya
Kifungu cha 10.3 (a) na (c) ambapo hayatazidi Dola za Kimarekani 350,000 na
kwamba, malipo hayo kwa ujumla wake chini ya Mkataba huo hayatazidi Dola za
Kimarekani 500,000.
·
Aidha,
Kifungu cha 8.8 cha Mkataba wa Richmond kinachoiruhusu TANESCO kuendesha
Mitambo ya Richmond pale ambapo Kampuni hiyoi itaitelekeza (abandon) Mitambo
hiyo, kimeondolewa kwenye mkataba wa AGGREKO.
(c) Nyongeza ya Mkataba
·
Mkataba
huo una Nyongeza (Addendum) au (Amendment No.2) ya Januari, 2007 ambayo
imebadilisha formula ya kupata ‘capacity payments’, ambapo muda uliopotezwa na
TANESCO kutokana na matatizo ya upatikanaji wa gesi na pia kutokana na TANESCO
kutoomba kupewa umeme kutoka AGGREKO umepigiwa hesabu kwa ajili ya AGGREKO
kulipwa na TANESCO.
·
Nyongeza
hiyo pia imebadilisha bei ya Umeme unaotolewa na AGGREKO ambapo, bei mpya sasa
ni Dola za Kimarekani 0.0499 x 1000 kwa kila Mwh.
4.1.1
Mkataba Kati ya TANESCO na ALSTOM POWER
RENTALS ENERGY LLC
(b)
Tarehe ya Kusainiwa kwa Mkatab
Mkataba
huo ulisainiwa tarehe 27 Oktoba, 2006
(c)
Madhumuni ya Mkataba (Subject
Matter)
Mkataba
huo ni kwa ajili ya uzalishaji na usambazji wa
umeme wa dharura kutoka kwenye Kinu cha dizeli cha kuzalisha umeme
(emergency supply of power from a diesel – based generating plant in Mwanza
with a capacity of 40 Mw).
(c)
Muundo (form) wa Mkataba
Kama
ilivyo kwa Mikataba iliyotangulia, Mkataba huu upo katika muundo wa ‘Standard
Power Off-take Agreement’
(d)
Muda wa Mkataba
Muda
wa Mkataba huo ni miezi kumi na mbili (12) kwa mujibu wa Kifungu cha 2.1 cha
Mkataba.
(e)
Uhalali Kisheria wa Kampuni ya
Alstom Power Rentals Energy LLC
Kwa
mujibu wa maelezo yaliyomo kwenye Mkataba hususan kwenye Kifungu cha 5.1 (a) na
(b), Kampuni ya Alstom Power Rentals Energy LLC imesajiliwa chini ya Sheria za
Florida, Marekani.
(f)
Malipo ya Kodi
Kifungu
cha 3.4 cha Mkataba kinatamka kwamba, TANESCO itatumia juhudi za kibiashara
kuhakikisha kwamba Serikali ya Tanzania inatoa msamaha kwa Alstom wa kutolipa
‘import duties’ na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kuhusiana na Mtambo au
utekelezaji wa majukumu ya Alstom, chini ya Mkataba huo.
Aidha,
Kifungu hicho kinatamka pia kuwa, pale ambapo kodi hizo zitadaiwa, Alstom
itaiomba TANESCO ilipe kodi hiyo au kama italipwa na Alstom, TANESCO
itarejeshea Alstom malipo hayo ya kodi.
(g)
Kutii Sheria za Mazingira
Kifungu
cha 3.9 cha Mkataba huu kinamtaka Alstom kuhakikisha kwamba, hatafanya kitendo
chochote ambacho kitasababisha kuwepo kwa hali ya mazingira ambayo inakiuka
Sheria za Tanzania.
(h)
Malipo ya Umeme
Kwa
mujibu wa Kifungu cha 4.3 cha Mkataba, TANESCO inawajibika kulipa malipo ya
‘capacity charge’ kwa kiasi cha Dola za Marekani 43.8 kwa Kw kwa mwezi.
(i)
Malipo ya Fidia kwa Ucheleweshaji
wa Kuzalisha Umeme
Kwa
mujibu wa Kifungu cha 4.4 na cha 10.1(a) cha Mkataba, Alstom anawajibika kulipa
kwa TANESCO kiasi cha Dola za Kimarekani 400,000 kama kiwango cha mwisho cha
malipo ya fidia (damages) kwa ucheleweshaji wa kuzalisha umeme na kiasi cha
Dola za Kimarekani 600,000 kama kiwango cha mwisho cha malipo yote ya fidia
(damages).
(j) Dhamana ya Malipo kwa Alstom
Kifungu
cha 4.6 cha Mkataba kinaitaka TANESCO kufungua ‘Letter of Credit’ ya kiasi cha
Dola za Kimarekani 3,500,000 kwa kipindi chote cha Mkataba, kama dhamana ya
malipo kwa Alstom.
Aidha, Kifungu cha 4.7 cha Mkataba
kinaitaka TANESCO kufungua ‘Standby Letter of Credit’ ya kiasi cha Dola za
Kimarekani 14,000,000 kwa ajili ya malipo ya miezi minane (8) ya Mkataba.
(k) Mafuta (fuel)
Kifungu
cha 6 cha Mkataba kinatamka kuwa, TANESCO itawajibika kulipia mafuta ya dizeli
yatakayotumika kuendeshea Mtambo wa Alstom wa kuzalisha Umeme.
(l) Kutolipa Malip ‘Capacity Charges’ Wakati
wa Majanga
Kwa
mujibu wa Kifungu cha 13.1 cha Mkataba, malipo ya ‘Capacity Charges’
yanayotakiwa kulipwa na TANESCO yatasitishwa kwa siku 30 iwapo litatokea janga
lolote ambalo litasababisha Alstom kutelekeza majukumu yake ya kuzalisha na
kusambaza umeme.
(m)
Kuhamisha (assign) Majukumu
Kwa
mujibu wa Kifungu cha 15.12 cha Mkataba, Alstom au TANESCO inaweza
kuhamisha (assign) sehemu au majukumu
yote yaliyomo kwenye Mkataba kwa Kampuni Tanzu, baada ya kutoa taarifa kwa
mhusika wa pili uuzaji uhamishaji huo wa majukumu. Hata hivyo, mhusika yeyote
anayehamisha majukumu atabaki na wajibu wa kuhakikisha kuwa majukumu hayo
yanatekelezwa ipasavyo na yasipotekelezwa, atawajibika.
4.1.2
Mkataba Kati ya TANESCO na WARTSILA
FINLAND OY
(a) Tarehe ya Kusainiwa kwa Mkataba
Mkataba
huo ulisainiwa tarehe 20 Juni, 2006.
(b)
Madhumuni ya Mkataba (Subject
Matter)
Mkataba huo ni kwa ajili ya uzalishaji
na usambazaji wa umeme wa dharura
kutoka kwenye Kinu cha gesi cha kuzalisha umeme (Energy Purchase Contract for
Procurement of Emergency 100 Mw Gas-based Power Generation Plant at Ubungo, Dar
es Salaam.)
(c) Muundo (form) wa Mkataba
Tofauti na Mikataba yote iliyotangulia
kufanyiwa uchambuzi hapo juu, Mkataba huo upo katika muundo uliowekwa na Kanuni
ya Ununuzi wa Umma [The Public Procurement (Goods, Works, Non-Consultant
Services and Disposal of Public Assets by Tender) Rgulations, G.N. No.97 of
15/4/2005] zilizotungwa chini ya Kifungu cha 88 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma
Na.21 ya Mwaka 2004 [The Public Procurement Act, 2004 (No.21 of 2004)].
Kanuni ya 115(1) ya Kanuni za Ununuzi
wa Umma za Mwaka 2005, Taarifa ya Serikali Namba 97 ya Mwaka 2005 inaelekeza
kama ifuatavyo:-
“Kwa kadri inavyowezekana, kila
jitihada itafanywa kutumia miundo ya rasimu za mikataba iliyotayarishwa na
Mamlaka ya Ununuzi wa Umma.” Tafsiri na msisitizo ni wetu.
Ili kuondoa tatizo la tafsiri, Kanuni
hiyo iliyoandikwa kwa lugha ya Kingereza inasomeka kama ifuatavyo:-
“Every effort shall be made to utilize
as for as possible, the sample Standard Contract documents prepared by the
Authority.”
(d) Muda wa Mkataba
Muda wa Mkataba (contract period) ni
miezi 21, kwa mujibu wa Kifungu cha G.C.C 1.1 (aa) na GCC 8.1[Tazama Uk.1 na 2
wa ‘Special Conditions of Contract]
(e) Uhalali kisheria wa
Kampuni ya WARTSILA FINLAND OY
Kwa mujibu wa maelezo yaliyomo kwenye Mkataba, Kampuni
hiyo imesajiliwa chini ya Sheria za Finland. Hatukuweza kufanya utafiti wa kina
kuthibitisha kuwa maelezo hayo ni sahihi, isipokuwa tumefanya hivyo kwa Kampuni
moja tu ya RICHMOND.
(f) Malipo (Contract Price)
Kwa mujibu wa Kifungu cha 2.1 cha Mkataba, TANESCO
anawajibika kulipa kiasi cha Euro 57,550,000/= kama malipo ya huduma ya
kupatiwa umeme wa Megawatt 100 kutoka kwenye Kinu cha kuzalisha umeme cha
WARTSILA.
(g) Utaratibu wa malipo
Kwa mujibu wa Kifungu cha 2.2 cha Mkataba, TANESCO
anawajibika kufanya malipo ya huduma ya umeme kwa kufungua ‘Letter of Credit’
ya kiasi cha Euro 51,795,000/= kwa jina la WARTSILA.
(h)
Dhamana ya Utekelezaji (Performance
Bond)
Chini ya Kifungu cha 3.1 cha Mkataba, WARTSILA
anawajibika kutoa dhamana ya utekelezaji wa kazi (Performance security/bond) ya
kiasi cha 10%ya malipo anayostahili kulipwa, kabla ya kuanza kazi.
(i) Malipo ya Kodi
§ Kwa mujibu wa Kifungu cha 14.4 (GCC),
uk. wa 3 wa Special Conditions of Contract, kodi zote ambazo WARTSILA anapaswa
kulipa zitasamehewa (be exempted) au zitalipwa na TANESCO.
§ Aidha, chini ya Kifungu hicho pia, kodi
na malipo yote yanyohusu mishahara ya watumishi wa kigeni wa Kampuni ya
WARTSILA zinapaswa kulipwa na TANESCO.
(j)
Taratibu za Usuluhishi
Chini ya Kifungu cha 6.2.3 taratibu zitakazotumika wakati
wa Usuluhishi ni za Mahakama ya Kimataifa ya usuluhishi ya London, chini ya
Sheria za Uingereza.
Tunadhani kifungu hiki si kwa manufaa na maslahi ya
TANESCO.
(k)
Malipo ya bonus
Chini ya Kifungu cha 26.3 cha Mkataba (Taz. Uk. wa 5 wa
SCC malipo ya bonus hayaruhusiwi.
(l) Kipindi cha Matengenezo (Defect liability
period)
§ Kwa mujibu wa Kifungu cha 27.2 cha
Mkataba (Uk. wa 5 wa SCC), kipindi cha matengenezo ni miaka miwili (2) baada ya
kukamilika kwa ufungaji wa Mtambo.
§ Tunadhani kwamba, Kifungu hiki ni kwa
manufaa na maslahi ya TANESCO.
4.1.3
Mkataba Kati ya TANESCO na SONGAS
LIMITED
(a) Tarehe ya Kusainiwa kwa Mkataba
Mkataba
huo umesainiwa tarehe 11 Oktoba, 2001.
(b) Madhumuni ya Mkataba (Subject Matter)
Mkataba huo ni kwa ajili ya uzalishaji
na usambazji wa nishati ya umeme kutokana na gesi ya Songosongo (Power purchase
relating to the Songosongo gas-to-electricity)
(c) Muundo (form) wa Mkataba
Mkataba huo upo katika muundo wa
‘Standard Power Purchase Agreement’.
(d) Muda wa Mkataba
Kwa mujibu wa Kifungu cha 4.1 cha
Mkataba, muda wa Mkataba ni miaka ishirini (20), na unaweza kuongezwa kwa
makubaliano kati ya TANESCO na SONGAS.
(e) Uhalali Kisheria wa Kampuni ya SONGAS
LIMITED
Kampuni ya SONGAS LIMITED ni Kampuni ya kitanzania
iliyosajiliwa chini ya Sheria ya Makampuni, Sura 212, Toleo la 2002 [The
Companies Ordience (Cap.212) of the Laws of Tanzania, R.E, 2002] (Tazama
Kifungu cha 5.1 cha Mkataba)
(f) Malipo ya Kodi
Kwa mujibu wa Kifungu cha 15.1 cha Mkataba, SONGAS
LIMITED inatakiwa kulipa kodi kulingana na masharti yaliyomo kwenye Mkataba wa
Utekelezaji (Implementation Agreement) ulioingiwa kati yake na Serikali ya
Tanzania.
(g) Malipo ya Umeme
Kwa mujibu wa Kifungu cha 2.1(a)(i) na (ii) cha Mkataba,
kikisomwa pamoja na Vifungu 9.2 na 9.5, TANESCO anawajibika kulipa malipo
yafuatayo kwa SONGAS:- ‘Capacity Charge’ – Dola za Kimarekani 6,638,600 ‘Energy
Charge’ – kwa kiasi kitakachotokana na ‘formula’ iliyowekwa na Kifungu cha 5
cha Nyongeza F ya Mkataba.
(h) Usuluhishi
§ Kifungu cha 3.10 cha Mkataba kinatamka
kwamba, TANESCO na SONGAS wamekubaliana kutotekeleza masharti na matakwa ya
Kifungu cha 20(2) cha Sheria ya Umeme, Sura 131, Toleo la 2002 [Electricity
Act, (Cap.131) of the Laws of Tanzania, R.E 2002], na badala yake kusuluhishwa
migogoro baina yao kwa kutumia utaratibu uliowekwa na Mkataba.
§ Kwa kuwa kinahusu makubaliano ambayo
yanavunja sheria, Kifungu hicho hakina uhalali wowote wa kisheria.
(i) Kuvunjwa kwa TANESCO
Kwa mujibu wa Kifungu cha 4.3(a) cha Mkataba, kikisomwa
pamoja na Kifungu cha 17.12, TANESCO haiwezi kuvunjwa kwa Sheria au kuhamisha
majukumu yake yaliyoainishwa kwenye Mkataba, isipokuwa tu kwa kuzingatia
masharti yaliyowekwa na Kifungu cha 8.7 cha Mkataba wa Utekelezaji
(Implementation Agreement).
(j) Uuzaji Umeme wa SONGAS
Kwa mujibu wa Kifungu cha 4.1(b), iwapo TANESCO watakataa
kuongeza muda wa Mkataba baada ya muda wa awali wa miaka 20 kumalizika, SONGAS
wataruhusiwa kuingia Mkataba na mtu yoyote anayetaka kuuziwa umeme.
(k) Haki ya Kununua Mradi
Chini ya Kifungu cha 4.8 cha Mkataba, TANESCO na T.P.D.C
wamepewa haki ya kununua Mradi huo wa SONGAS iwapo SONGAS atakiuka masharti ya
Mkataba.
Mapendekezo Mengine
Pamoja
na mapendekezo ya hapo juu, tunashauri na kupendekeza pia kuwa, kuna ulazima
kwa Mikataba mikubwa ambayo inahusu maslahi na manufaa ya Taifa kama vile
Mkataba wa IPTL kuwasilishwa Bungeni, kwa utaratibu wa dhana ya demokrasia ya
uwajibikaji (accountability in a Parliamentary democracy) kwa ajili ya ushauri
wa Bunge.
Tunapendekeza
na kushauri vilevile kuwa, pale ambapo kuna ulazima wa kutumia rasimu ya
Mkataba ambayo ni tofauti na ile iliyotayarishwa na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma,
mabadiliko muhimu yafanywe katika rasimu hiyo ili masharti yaliyomo ambayo
hayafai yaondolewe na yale ambayo ni kwa manufaa ya Taifa letu yawekwe.
Wanasheria watumike katika kuitekeleza jambo hili.
Tunashauri
na kupendekeza vilevile kuwa, Mikataba yote ya umma ifanywe kwa kuzingatia
misingi ya kibiashara na si vinginevyo, na kwamba, Taasisi na Mashirika yote ya
Umma lazima yatekeleze na kufuata utaratibu, masharti na matakwa yaliyowekwa na
Sheria ya Ununuzi wa Umma, Namba 21 ya mwaka 2004, pamoja na Kanuni
zilizotungwa chini ya Sheria hiyo.
Aidha,
tunapendekeza na kushauri kwamba utoaji Mikataba utumike kama njia au chombo
cha kutekeleza Sera za Taifa na malengo ya jamii, badala ya kutumika kama
chombo cha kuchota rasilimali za Taifa na kuongeza umaskini wa wananchi wa nchi
hii.
Aidha,
tunashuri pia kwamba, pale inapotokea ukiukwaji wa masharti ya Mkataba
unaofanywa na Mwekezaji basi hatua mwafaka zichukuliwe, ikiwa ni pamoja na
kudai malipo ya fidia iwapo kuna kifungu cha Mkataba kinachotoa haki hiyo.
Kwa
kuzingatia kuwa Mikataba mibovu kati ya TANESCO na Makampuni mbalimbali ambapo
Makampuni hayo yanalipiwa kodi yote na TANESCO imekuwa ni chanzo cha bei kubwa
za umeme katika nchi yetu, na kwa kuzingatia kuwa Mikataba hiyo inasababisha
Sera muhimu za Taifa, kama vile, Sera ya Kupiga vita Umaskini, Sera ya Huduma
Bora kwa Jamii, Sera ya Taifa ya Nishati inayolenga kusambaza nishati ya bei
nafuu vijijini n.k. kutotekelezeka, tunashauri kuwa Mikataba hiyo ipitiwe upya
ili irekebishwe, kwa maslahi na manufaa ya Taifa letu.
Mwisho,
kwa kuzingatia ukweli kwamba, Mikataba hiyo mibovu, kwa kiasi kikubwa
inadidimiza uchumi wa nchi yetu, tunapendekeza Serikali ichukuwe hatua muafaka
zinazofaa ili kuondoa hali hiyo ambayo
inalipeleka Taifa letu ‘shimoni’[1].
Mheshimiwa Spika,
hali hiyo ya kuachwa kutekelezwa kwa maazimio ya Bunge la Tisa ya Mwaka 2008,
hayahusu tu Richmond bali pia juu ya Kashfa ya Mgodi wa Kiwira aliyomgusa Rais
Mstaafu Benjamin Mkapa na baadhi ya mawaziri kama ambavyo hotuba hii itaeleza
kwa ufupi wakati wa kutoa maoni kuhusu sekta ya madini. Serikali wakati
inaendelea kuchukua hatua kuhusu kashfa hii ni muhimu ikarejea maelezo ya ziada
na vielelezo zaidi vilivyotolewa wakati wa kusomwa kwa orodha ya mafisadi (List
of Shame) Septemba 15 mwaka 2007 katika uwanja wa Mwembe Yanga.
Mheshimiwa Spika, Aidha,
matokeo ya Bunge kuzembea kuisimamia Serikali kukamilisha utekelezaji wa
maazimio ya Bunge ya mwaka 2008 yamesababisha udhaifu wa Serikali katika
kutekeleza maazimio ya Bunge ya mwaka 2011 kuhusu “Sakata la Jairo” kama
nilivyoeleza katika Hotuba hii lakini pia kuhusu uchunguzi juu ya Sekta ndogo
ya Gesi Asili na Mpango wa Dharura wa Umeme kama nitakavyoeleza wakati
nawasilisha maoni kuhusu sekta ya gesi ya nishati.
C. NISHATI
3.0 SEKTA NDOGO YA GESI ASILIA TANZANIA
Mheshimiwa Spika,
sekta ndogo ya gesi asilia ni sekta ambayo kutokana na ukubwa wa hazina
iliyokwishapatikana na inayokisiwa kuwepo itakuwa ni kubwa sana katika shughuli
za uchumi kwa nchi yetu. Lakini Sekta ya gesi asilia imegubikwa na utata mwingi
ambao kwa njia moja au nyingine unatokana na kutokuwepo kwa sera na sheria
mahususi ya gesi. Na hivyo kusababisha utendaji wake kutokuwa na mdhibiti
(regulator) wa kuhakikisha maslahi ya taifa, mwekezaji na mlaji yanaangaliwa.
Mheshimiwa Spika, Utafutaji na uzalishaji wa mafuta
na gesi( Upstream); shughuli zote za utafutaji wa mafuta na gesi nchini
unatawaliwa na Sheria ya Utafutaji na Uzalishaji Mafuta ya mwaka 1980 (The
Exploration Act,1980). Shughuli ya usafirishaji na uuzaji (down stream) hii
hutawaliwa na sheria ya EWURA sura 414 kwa kuwa kwa sasa sheria ya gesi nchini
haipo. Hivyo basi, makubaliano katika mkataba baina ya wadau hutakiwa
kuwasilishwa EWURA kwa mapitio tu, na baada ya kujiridhisha EWURA hupanga bei za gesi.
Mheshimiwa
Spika, mkataba wa ubia ndiyo mwongozo mkuu wa mahusiano yote yanayohusu
uzalishaji na ugawanaji wa mapato ya gesi baina ya TPDC na mbia yeyote. Lakini
kwa makusudi wabia na TPDC wamekuwa hawafuati matakwa yaliyomo kwenye PSA na
mfano mzuri ni Pan African Energy[2].
Mheshimiwa Spika,
utakumbuka moja ya mapendekezo ya kamati ndogo iliyoundwa na Bunge lako tukufu
toka kwenye iliyokuwa kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini ilipendekeza na
Bunge kukubali, kuwa nina nukuuu ‘’ipo
haja ya kudurusu Sera ya Nishati, kuandaa Muswada wa gesi asili wenye kutoa
majibu ya maswali magumu ya Watanzania wa leo na wa miaka 50 ijayo…
Majukumu kati ya asasi moja na asasi
nyingine yaainishwe bayana na kutenganishwa kwa lengo la kuleta ufanisi na
kuongeza tija. Aidha, mipango mkakati na kabambe iandaliwe ili kuibua miradi ya
miundombinu na mahitaji ya rasilimali. Taifa likichelewa kuweka nyenzo hizi
muhimu, likaruhusu majadiliano na mikataba kuchukuwa nafasi, kipindi si kirefu
yatashuhudia manun’guniko kuwa nchi imeuzwa na mivutano kati ya wananchi na
wawekezaji na ya wananchi na Serikali yao itajitokeza kwa nguvu sana jambo
ambalo ni vyema likaepukwa mapema[3]’’
Mheshimiwa Spika,
mapendekezo haja yalitolewa Bungeni Novemba 17, 2011. Sasa ni mwaka mzima na
miezi sita, hadi tunashuhudia maandamano
na malalamiko ya wazi toka maeneo ambapo gesi asili imegunduliwa.
Mheshimiwa Spika,
Licha ya ukweli kwamba gesi asili ilianza kutafutwa toka mwaka 1952 na
iligunduliwa kwa mara ya kwanza nchini mwaka 1974 na baadae mwaka 1982, wakati
wote huo hakuwahi kuwa na sera mahususi ya gesi mpaka mwishoni mwa mwaka 2012
zaidi ya miaka 30 baadae ndipo serikali imeanzisha mchakato wa kutunga sera ya Taifa
ya gesi asili.
Mheshimiwa Spika,
Serikali imedhihirisha udhaifu mkubwa wa kisera kwa kuzingatia kuwa mikataba
kadhaa ya uchimbaji na utafutaji wa gesi imeshatiwa saini kati ya serikali na
wawekezaji bila kuwa na sera wala sheria inayotoa mwongozo juu ya namna Taifa
linavyopaswa kuthibiti rasilimali hii adhimu. Uwepo wa sera ya gesi asilia
ungetoa mwelekeo juu ya namna gani serikali ingeshirikiana na wakazi wa maeneo
yaliyogunduliwa gesi, pamoja na wadau wengine katika kutafuta,kugundua na
kuvuna, kusafirisha, kununua na kutumia gesi asilia.
Mheshimiwa Spika,
Serikali bila uwepo wa sera na sheria hiyo, tayari imefunga mkataba na kampuni
ya Statoil, Ophir, British Gas, Artumas, Shell, Texaco, Agip, PetroBras na
kadhalika. Ni wazi kwamba mikataba husika imeingiwa bila muongozo wowote wa
kisera wala kisheria mahususi. Aidha, licha ya makosa hayo na wakati mchakato
wa sera uko karibu kukamilika Serikali imefunga mkataba mwingine kwa Kampuni
nyingine kufanya utafutaji kwenye Ziwa
Tanganyika. Jambo hili linazidisha wasiwasi kama kweli Serikali ina nia ya
dhati ya kuhakikisha sekta hii ya gesi inanufaisha Taifa na watu wake.
Kitendo
cha Serikali kuendelea kuingia mikataba na makampuni ya kutafuta gesi asilia
bila ya kukamilisha kwanza sera na sheria ni sawa na kuweka mkokoteni mbele ya
punda.
Mheshimiwa Spika; Waziri
Mkuu akiwa ndiye msimamizi na mdhibiti wa shughuli za kila siku za Serikali
ndani na nje ya Bunge, anapaswa kutoa maelezo kuhusu hali inayoendelea hivi
sasa katika sekta ndogo (sub sector) muhimu kwa nchi yetu ya gesi asili kuhusu
mazungumzo yanayoendelea na makampuni mbalimbali ya kimataifa na mikataba
inayozidi kusainiwa huku kukiwa na ombwe la kisera na udhaifu wa kiuongozi
katika sekta hizo nyeti hali ambayo itakuwa na athari za muda mrefu sana kwa
taifa.
Mheshimiwa Spika,
Ucheleweshwaji wa sera na sheria katika sekta ya gesi asilia unachangiwa na
wizara yenyewe kwa watendaji wake kuwa na udhaifu katika kuweka mifumo ya
kuifanya sekta hiyo kuwa endelevu na yenye manufaa kwa nchi. Hili linathibitishwa
na ukweli kwamba TPDC imeshindwa kusimamia kwa ukamilifu sekta hii ya gesi
asilia kwani hata mikataba iliyopo
inayotaka kampuni inayofanya utafiti baada ya muda Fulani kuchimba kisima
kipya; lakini hadi sasa kwa mfano tangu Kampuni ya Songas kuchukua visima
vilivyochimbwa na TPDC haijawahi kuchimba kisima kipya.
Mheshimiwa Spika,
mfano mwingine ni kampuni ya Pan African
Energy Tanzania (PAT) kukosa sifa za uaminifu ambapo Kamati ilishauri Mkataba
wa Pan African Energy Tanzania (PAT) usitishwe. Aidha, utekelezaji wa kuvunja
mkataba huu ulipaswa kwenda sambamba na kuhakikisha kuwa taratibu za kisheria
na za kimkataba zinazingatiwa, uwepo wa usalama wa visima na mitambo na uwepo
wa uhakika wa huduma ya upatikanaji wa gesi nchini. Hili lilikuwa ni pendekezo
namba 4 la kamati iliyochunguza uendeshwaji wa sekta ndogo ya gesi asilia hapa
nchini na baadae kuwa azimio la Bunge. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge ni kwanini mpaka sasa Serikali
haijatekeleza azimio hilo? Aidha, ni lini Bunge litachukua hatua ili kuepusha
uzembe kwa upande wa chombo hili muhimu?
Mheshimiwa Spika, kuhusu
gesi asilia, tarehe 15 Julai, 2011 Kambi Rasmi ya Upinzani ilieleza kuwa, nchi
yetu imejaliwa utajiri wa gesi asilia katikati ya lindi la umaskini wa wananchi
na kwamba Taifa letu lina fursa ya kuwa nchi kiongozi katika gesi Afrika na
kushindana Kimataifa ikiwa tutaweka mstari wa mbele uzalendo,upeo, umakini na
uadilifu katika sekta ya nishati kuepusha laana ya rasilimali.
Mheshimiwa Spika, hata
hivyo, mapitio ya utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2011/2012, yalionesha Serikali
kutochukua hatua thabiti kushughulikia ufisadi na udhaifu wa kiuongozi katika
sekta ndogo ya gesi asili.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilitaka hatua za haraka kuchukuliwa
katika mwaka wa fedha 2012/2013 ili kuepusha
rasilimali kuwa chanzo cha migogoro na kuhatarisha pia usalama wa nchi
lakini kwa sababu ya udhaifu wa serikali hii kutosikiliza ushauri kitendo hicho
kilisababisha vurugu na uharibifu wa mali kwa mikoa ya Lindi na Mtwara.
Mheshimiwa Spika,
ushahidi wa hili unapatikana katika ushauri ambao serikali ilipewa kwa nyakati
mbili tofauti lakini ikashindwa kuzuia vurugu za Lindi na Mtwara. Tarehe 27
Julai 2012 nikiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu mapitio na
makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya nishati na madini nilishauri “Mapitio
ya utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2011/2012, yanaonekana bado serikali
haichukui hatua thabiti kushughulikia ufisadi na udhaifu wa kiuongozi katika
sekta ndogo ya gesi asili hivyo hatua za haraka zisipochukuliwa katika mwaka
2012/2013 na kuendelea rasilimali inaweza kuwa chanzo cha migogoro na
kuhatarisha pia usalama wa nchi”. Lakini pamoja na angalizo hili
serikali haikuchukua hatua yeyote na matokeo yake sote tunayafahamu.
Mheshimiwa Spika, wakati
wa mchakato wa kutoa maoni juu ya rasimu ya gesi , pamoja na kwamba mchakato
huo haukufanyika katika maeneo mengine muhimu kama Chuo Kikuu cha Dar es salaam(UDSM)
ambacho kina kozi mbalimbali za masuala haya na ambako tungepata ushauri mzuri
na wa kitaalamu kutokana na wadau hao kutokujua na hivyo kutokujitokeza .
Mheshimiwa Spika,
miongoni mwa wananchi waliojitokeza kutoa maoni ni pamoja na wananchi
waliofunga safari kutoka Mtwara hadi Dar es salaam kuja kutoa maoni yao juu ya
rasimu ya gesi. Miongoni mwa mapendekezo aliyotoa mwananchi huyo (jina linahifadhiwa)
mbele ya viongozi wa serikali alishauri
serikali kujua matatizo yanayotokea katika sekta ya madini ili tuhusianishe na
gesi asilia.
Mheshimiwa Spika,
Pamoja mwananchi huyo kuwakilisha mikoa ambayo ndiko hasa nishati hiyo
inakopatikana, mwananchi huyo alipendekeza kutengwa kwa asilimia kumi (10%) ya
mapato yatokanayo na gesi kwa ajili ya kuboresha maeneo rasilimali hiyo inapopatikana.
Akapendekeza kijengwe Chuo Kikuu Mtwara kitakachofundisha watanzania elimu ya
gesi na pia vijengwe viwanda vitatu kwa faida ya wana mtwara. Mapendekezo ambayo pia yamewahi kutolewa na
Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA
kwa mwaka 2011 na 2012, katika hali
kama hii ya kushindwa kutimiza wajibu na kusababisha migogoro, Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali ikiri kuwa imeshindwa kuiongoza sekta hii .
Mheshimiwa Spika, Kamati
ya kudumu ya bunge ya nishati na madini ilitoa mapendekezo ya kukamilishwa kwa
sera na sheria ya gesi kwa haraka na umakini mkubwa. Kamati pia ilishauri
serikali kuonyesha katika sera na sheria hiyo ya gesi asilia jinsi ambavyo
mapato yanayotokana na gesi asilia yatakavyo simamiwa, mapendekezo hayo ya
kamati yalizingatia wingi wa upatikanaji wa nishati hii kwa sasa katika nchi
yetu.
Mheshimiwa Spika,
katika hali ya kushangaza serikali imeendesha mchakato mzima wa kutengeneza
rasimu ya gesi asilia bila kuwa na ushiriki mkubwa wa wananchi kinyume na
mapendekezo ya kamati ya kudumu ya Bunge.
Mheshimiwa Spika,
hakukuwa na uhamasishaji wa kutosha kwa wananchi katika kutoa maoni juu ya
rasimu ya kwanza ya gesi iliyotolewa na Wizara ya Nishati na Madini na ndio
maana mahudhurio katika sehemu ambako mijadala iliendeshwa yalikuwa madogo sana.
Kwa mfano katika ukumbi uliopo Makumbusho ya Mwalimu Nyerere waliohudhuria siku
ya kwanza hawakufika hata 25 na siku ya pili hawakuzidi watu 30. Pia katika Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), wanafunzi na wadau wa gesi kutoka taasisi hiyo
muhimu ya elimu ya juu hawakujitokeza kwa sababu ya uhamasishaji hafifu na
hivyo kupelekea kuahirishwa kwa zoezi hilo katika suala la msingi linalohusu
uchumi wa watanzania. Lakini pia suala hili kwa wakati huo lilitakiwa liwe ni
mjadala wa kitaifa ndani ya vyuo vikuu vingi nchini na jamii kwa ujumla
ikihusisha pia mikoa yote ambako kuna uvunaji au utafutaji wa gesi asilia ili
kupanua dhana ya kuwashirikisha wananchi katika maswala yanayohusu rasilimali
za Taifa kinyume na uhalisia wenyewe.
Mheshimiwa Spika,
Kufuatia kasoro zilizoanza kubainishwa na wabunge na wadau mbalimbali katika
toleo la tatu la rasimu ya gesi; Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kutoa maelezo ni kwanini haikuzingatia baadhi ya maoni muhimu ya wadau
yaliyotolewa mara baada ya kutolewa kwa rasimu ya kwanza ya Sera hiyo. Aidha,
Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inataka mchakato wa kupitia
rasimu ya tatu ya sera hiyo upanue wigo wa ushirikishwaji wa wananchi katika
mikoa yote ambayo utafutaji wa gesi asilia umeanza au unatarajiwa kuanza pamoja
na mikoa yote itakayofikiwa na miradi ya uendelezaji wa gesi asilia.
Ikumbukwe
kwamba udhaifu wa Serikali katika kuwezesha ushirikishwaji wa wananchi katika
mipango na miradi ya maendeleo na matumizi mabaya ya muda mrefu ya rasilimali
za nchi ni kati ya sababu zilizochangia migogoro katika maeneo ambayo
uendelezaji wa miradi ya gesi asilia umeanza hususani katika mikoa ya Lindi na
Mtwara.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuwashirikisha wananchi na kutoa
taarifa za kutosha na kwa wakati juu ya suala hili la gesi asilia na rasilimali
nyingine za taifa ili kuondoa mkanganyiko unaojitokeza kwa wananchi juu ya
mchakato mzima wa uwekezaji kwenye
rasilimali za Taifa.
Mheshimiwa spika,
kwa mujibu wa michango mbalimbali iliyotolewa na wabunge wakati wa mjadala wa
kuchangia bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini 2012/2013 waheshimiwa wabunge
pia walitaka kujua kama taifa mipango ambayo serikali imeweka kufuatia
kugundulika kwa kiasi kikubwa cha gesi, kama rasilimali watu kwa maana ya
wataalamu waliobobea, idadi ya wataalamu tunaowaandaa kwenda sambamba na
uhalisia wa uhitaji wa wataalamu wenyewe katika sekta ya gesi. Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inarudia kuitaka serikali kufanya maandalizi ya kutosha ya
kuwekeza katika suala la rasilimali watu
ili kuondoa matatizo yanayoweza kujitokeza hivi karibuni kutokana na uhaba wa wataalamu katika fani
hiyo.
3.1 Ugawaji wa Vitalu vipya vya
utafutaji wa gesi na mafuta.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara
kwa mwaka 2012/13, baada ya kupokea ushauri wa Kamati kuhusu kusitisha ugawaji
wa vitalu vya utafutaji gesi, Serikali iliahidi kwa kusema kuwa “zoezi
la kugawa vitalu vipya kwa ajili ya utafutaji wa mafuta umesitishwa mpaka hapo sera ya Gesi Asilia na
sheria ya Gesi Asilia nchini itakapokamilika na kuanza kutumika”
Mheshimiwa
Spika, Jambo la kushangaza ni kwamba wakati sera ya Gesi
Asilia ipo kwenye rasimu na ndio kwanza wabunge tumeletewa kutoa maoni,
Serikali tayari imetangaza kwa mujibu wa vyombo vya habari na tamko la
TPDC tarehe 18.5.2013 kuanza mzunguko mwingine wa leseni za
utafutaji Mafuta na Gesi kwenye Bahari kuu na Ziwa Tanganyika Kaskazini. Kutoa
leseni kwenye kitalu ya utafutaji ni hatua ya kuelekea kutoa mkataba wa
uvunaji.
Zabuni hii mpya ya leseni
za vitalu vya utafutaji imetolewa wakati kuna maamuzi ya Bunge kuzuia ugawaji
huu mpya mpaka sera ya Gesi Asilia na Sheria ya Gesi vikamilike. Haraka hii ya
serikali kugawa vitalu bila sera wala Sheria inatoka wapi.
Mheshimiwa
Spika, uharaka huu unaifanya Kambi Rasmi ya Upinzani iwe na
mawazo kwamba Wizara iliidanganya Kamati ya Kudumu ya Bunge, je ilifanya hivyo
kwa maslahi ya nani? Tunamtaka Mheshimiwa Waziri alieleze Bunge sababu za
kuidanganya kamati inayofanyakazi kwa niaba ya Bunge.
Wizara ya Nishati na Madini
imekuwa ikitoa ufafanuzi potofu kwamba tangazo la sasa halina athari kwa kuwa
maamuzi ya utoaji wa leseni yatafanyika mwaka 2014 baada ya kuwa na sera na
sheria. Hata hivyo, ufafanuzi huu wa Wizara hauzingatii ukweli kuwa, hata zabuni
ya maombi ikiwemo vigezo, utaratibu na masuala mengine ilipaswa kutolewa kwa
kuzingatia misingi mipya inayopaswa kuwekwa kupitia mchakato wa katiba mpya na
maandalizi ya Sera na Sheria ya Gesi Asili.
Katika muktadha huo, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutengua tangazo hilo mpaka baada ya
kukamilika kwa mchakato wa katiba mpya na maandalizi ya sera na sheria mpya sio
tu kwenye sekta ndogo ya gesi asilia bali katika sekta nzima ya nishati ikiwemo
juu ya masuala yanayohusu mafuta.
Vinginevyo, watanzania
wataamini kwamba hatua hiyo imefuatia msukumo uliotokea baada ya ziara ya Rais
wa China nchini Tanzania; hasa kwa kuzingatia namna ambavyo, pamoja na vitalu vilivyotangazwa kwenye zabuni ili
kutolewa kwa ushindani, vipo vitalu ambavyo vimebakishwa mikononi kwa TPDC
ambavyo mazingira ya mchakato wa utolewaji wake yanaacha maswali.
Mheshimiwa
spika, Katika hatua ya sasa Wizara ya Nishati na Madini
ijielekeze katika kusimamia mikataba ambayo tayari nchi yetu imeingia mpaka
sasa kwa maslahi ya nchi na kupitia upya mikataba mibovu. Aidha, katika
kutekeleza azma hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inaitaka
Wizara ya Nishati na Madini kutoa kwa Bunge taarifa ya uchunguzi wa mikataba
hiyo iliyokamilika toka mwaka 2012 lakini imeendelea kufanywa kuwa siri mpaka
hivi sasa.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inaitaka pia serikali kuweka wazi kwa watanzania wote mikataba hiyo na mingine
ambayo serikali imeisaini inayohusu rasilimali za Taifa hili. Aidha inatoa
mwito kwa wananchi kuhakikisha kwamba masuala ya uwazi katika mikataba yanapewa
kipaumbele katika katiba mpya, sera na sheria.
Mheshimiwa spika, Kitendo
ambacho serikali ilikuwa inakifanya kupitia Shirika la Maendeleo ya Petrol
(TPDC) cha kugawa vitalu vipya nane vya gesi wakati bado sera na sheria ya gesi
haijakamilika ni ushahidi tosha kuwa kuna watu wachache katika serikali
wameanza kulichukulia suala hili la gesi asilia kwa manufaa ya watu binafsi.
Mheshimiwa spika, Wizara
ya Nishati na Madini katika bajeti yake ya miaka iliyopita imekuwa ikitenga
fedha nyingi kwa ajili ya mishahara na posho kitengo cha sheria cha Wizara.
Jambo hili la kugawa vitalu vipya nane vya gesi wakati sera na sheria kuhusu
gesi havijakamilika linadhihirisha siyo tu udhaifu katika idara hii ya ushauri
wa kisheria bali pia mazingira yanayoashiria mianya ya matumizi mabaya ya
raslimali za umma katika zoezi hili. Kambi Rasimi ya Upinzani Bungeni
inalichukulia jambo hili kuwa ni udhaifu ambao hauwezi kuvumilika hata kidogo
na tunaitaka wizara ieleze sababu hasa za kuendesha zoezi hili kinyume na maoni
na mapendekezo ya kamati ya kudumu ya Bunge.
Mheshimiwa Spika, Mwalimu
Nyerere aliwahi kusema kwamba chama lege lege huzaa serikali legelege; udhaifu
huu wa wizara unaweza kutafsiriwa kwamba unachangiwa na ushiriki wa Chama cha
Mapinduzi (CCM) kupewa na kukubali hisa toka kwa moja ya makampuni
yanayojihusisha na utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini, kampuni ya Ophir energy . Kwa mujibu wa taarifa
rasmi za Bunge za tarehe 08.11.2012 ni kuwa wakati CCM ikipewa hisa wapo pia
baadhi ya watanzania ambao waligawiwa sehemu ya hisa hizo kwa ajili ya CCM
Aidha,Katibu
Mkuu wa CCM Abdurahaman Kinana anatajwa na vyanzo mbalimbali kwamba amewahaki
kuwa Mjumbe wa Bodi ya wakurugenzi ya kampuni ya Artumas ambayo iliingia
mkataba na Serikali wa kuzalisha Mega Watt- 300 za umeme Mtwara eneo la Mnazi
Bay. Mkataba huo ulikuwa wa misingi ya mabadilishano ya gesi kwa nishati ya
umeme (gas for power). Kwamba Artumas ingechimba na kuuza gesi asilia na
kuilipa serikali kwa pamoja na mambo mengine kuizalishia umeme wa 300MW. Baadae
mwaka 2010 Artumas baada ya kufaidika vya kutosha kutokana na uvunaji na
uuzaji iliacha kuendeleza mradi huo kwa
kisingizio cha madai ya mdororo wa Uchumi mwaka 2009 na kuuza hisa zake kwa
kampuni ya Wentworth ya Ufaransa.
Mheshimiwa Spika,Ushiriki
huu wa viongozi waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi na chama hicho kwenye
shughuli ambazo zinaitia hasara serikali unazua mazingira ya kwamba CCM
inasababisha unyonywaji wa Taifa na wananchi, na hivyo ni dhahiri si mwafaka
kuendelea kuongoza nchi hii. CCM na
baadhi ya viongozi wake wamekuwa wakifaidika kutokana na ombwe la kisera na kisheria katika
sekta hii na nyingine muhimu. Katika hali kama hii, maneno ya Mwalimu Nyerere
yanapaswa kuongezewa nukuu mpya kwamba “chama cha mafisadi huzaa serikali ya
mafisadi”.
3.2 Haki ya Wananchi kumiliki
rasilimali asilia
Mheshimiwa
Spika, Wakati Katiba yetu inatambua haki ya kumiliki mali na hifadhi ya
mali hiyo na inakataza unyang'anyi wa mali kwa lengo la kuitaifisha au kwa
malengo mengine, haki za wananchi kumiliki rasilimali zao za asilia kama ardhi,
madini, mafuta, gesi asilia, misitu na wanyama pori, uvuvi, n.k., zimekuwa
haziheshimiwi na mamlaka za kiserikali kwa hoja kwamba rasilimali asilia hizo
ni mali ya umma.
Mheshimiwa Spika, Dhana
ya mali ya umma ni dhana yenye asili yake katika ukoloni. Ni dola ya kikoloni
ya Kijerumani ndio ilikuwa ya kwanza kutangaza kwamba mali asilia zote katika
koloni lao la Tanganyika ni mali ya Mfalme wa Kijerumani. Baada ya Wajerumani
kushindwa Vita ya Kwanza ya Dunia na kunyang'anywa makoloni yao ya Afrika, dola
ya kikoloni ya Waingereza iliyokabidhiwa Tanganyika, walitangaza kwamba
rasilimali asilia zote ni mali ya umma chini ya mamlaka na udhibiti wa Gavana
wa kikoloni. Dhana hii ilipokelewa bila mabadiliko yoyote ya msingi baada ya
uhuru na ndio imekuwa msingi mkuu wa sera za rasilimali asilia za nchi yetu kwa
muda wote wa uhuru wetu. Jambo hili ni hatari kwani mali ya umma maana yake ni
mali isiyokuwa na mwenyewe, na ndio maana wenye nguvu wanatumia mwanya huo
kupora wasio na nguvu.
Mheshimiwa Spika,
Kama ilivyokuwa wakati wa ukoloni, utekelezaji kivitendo wa dhana ya mali ya
umma wakati wote wa uhuru umekuwa ni kuwanyang'anya wananchi rasilimali asilia
zilizoko kwenye maeneo yao na kuzimilikisha mamlaka za Serikali (wakati wa
miaka ya uchumi-dola), au kuzimilikisha kwa wawekezaji wa kigeni katika zama
hizi za soko holela kwa kisingizio cha huria.
Mheshimiwa Spika,
Matokeo ya mfumo huu ni kwamba milki na mamlaka ya maamuzi juu ya matumizi ya
rasilimali asilia yameondolewa mikononi mwa wananchi na kuhamishiwa kwenye
mikono ya warasimu wa Serikali. Sio hio tu, wananchi wamejikuta wakiondolewa
kwa nguvu kutoka kwenye maeneo yao ili kuwapisha wamiliki wapya wa rasilimali
hizo, yaani wawekezaji wa kigeni au wa ndani. Kwa sababu hiyo, uchumi wa
wananchi umeanguka, umaskini umeongezeka na matukio ya ukiukwaji wa haki za
binadamu yameongezeka.
Mheshimiwa Spika,
Dhana ya mali ya umma katika umilikaji wa rasilimali asilia imehakikisha kwamba
maeneo yenye rasilimali asilia hayapati faida na manufaa yanayotokana na uwepo
wa rasilimali hizo katika maeneo yao. Mrahaba, kodi na tozo nyingine
zinazotokana na matumizi au mapato ya rasilimali hizo yanapelekwa kwenye
mamlaka za Serikali Kuu. Kwa upande mwingine, madhara yanayotokana na matumizi
ya rasilimali hizo Kama vile uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya matumizi ya
rasilimali husika, yanawaangukia wananchi wa maeneo ziliko rasilimali hizo.
Mheshimiwa Spika, naomba
nieleze mtazamo na msimamo wa Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA
kuhusiana na umiliki pamoja na uendelezaji wa Raslimali zetu asilia,ni kwamba:
- Wananchi hawatanyang'anywa rasilimali zao asilia na mamlaka za Serikali kwa ajili ya matumizi na watu au taasisi nyingine bila kwanza Wananchi watakaoathiriwa na unyang'anyi au matumizi hayo kutoa ridhaa yao baada ya kupatiwa taarifa zote na kamili zinazohusu matumizi yanayotarajiwa ya rasilimali hizo na athari za matumizi hayo kwa mazingira, kiuchumi na kijamii (the right of prior informed consent). Wananchi Kama wamiliki wa msingi wa rasilimali asilia, watakuw
ii.Wananchi
wana haki ya kulipwa mrahaba kwa ajili ya matumizi ya watu au taasisi nyingine
ya rasilimali asilia za Wananchi, wakati mamlaka za Serikali za mitaa, Majimbo
na Serikali Kuu zitakuwa na haki ya kutoza kodi mapato yatakayotokana na
matumizi ya rasilimali hizo.
3.4 BOMBA LA GESI TOKA MTWARA HADI DAR ES SALAAM
Mheshimiwa Spika, Pamoja
na ushauri wa kambi rasmi ya upinzani bungeni wakati wa kuwasilishwa kwa bajeti
ya wizara 2012/2013 kuitaka Serikali kuwasilisha Bungeni na kuweka wazi kwa
umma mkataba wa mradi husika ili Bunge liweze kuishauri na kuisimamia Serikali
kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 63; kuanzia
katika hatua za awali kuhakikisha kwamba maslahi ya Taifa yanalindwa katika
hatua zote na pia wananchi wananufaika kutokana na fursa za uwekezaji huo
mkubwa lakini bado serikali haikutilia maanani ushauri huu. Matokeo yake siyo
tu kusababisha mkanganyiko kwa wakazi wa Lindi na Mtwara bali pia kuacha
maswali mengi kwa watanzania juu ya nini hasa nia ya serikali kwa kuficha
mikataba inayohusu rasilimali hizi za Taifa kwa wananchi wake na hata kwa
chombo cha kuwakilisha wananchi kama Bunge.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali isiendelee na
ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara mpaka Dar Es Salaam hadi kwanza; Mosi,
iweke wazi kwa Bunge mikataba yote inayohusu uendelezaji wa gesi asilia ikiwemo
ya ujenzi wa Bomba hilo. Pili, ikutane na wananchi kuwashirikisha na
kuhakikisha manufaa kwa taifa na kwao.
Kambi
Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA imeshangazwa na hatua ya Waziri wa
Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo tangu kuibuka kwa mgogoro huo
amejikita zaidi katika kutoa kauli kupitia vyombo vya habari badala ya kwenda
kukutana na wananchi hatua kwa hatua na kuwezesha ufumbuzi kupatikana. Aidha,
manufaa kwa wananchi wa Lindi na Mtwara ambayo taarifa yake imechapwa kwenye
vyombo vya habari yaletwe kama taarifa rasmi bungeni ikiwa na ulinganisho baina
ya shughuli za kijamii zilizofanywa na makampuni tajwa pamoja na miradi
iliyotekelezwa na Serikali kufuatia mapato katika sekta hii tangu mwaka 2004 na
thamani halisi ya mapato ambayo makampuni tajwa na Serikali wamepata.
Mheshimiwa Spika,
pamoja na ujenzi wa mitambo miwili ya kusafishia gesi asili Mnazi Bay na Songo
Songo kama sehemu ya mradi huo, Kambi Rasmi ya Upinzani inarudia kuitaka
Serikali kueleza ni miradi ipi
iliyotengewa fedha inayoambatana na mradi huo ambayo imepangwa
kuwanufaisha wananchi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara na imetengewa kiasi gani cha
fedha katika mwaka huu wa fedha 2013/2014 ili kuharakisha msukumo wa maendeleo
kwa mikoa hiyo ya Kusini ambayo imesahaulika kwa siku nyingi na hivyo siyo tu
kuharakisha maendeleo kwa mikoa ya Kusini bali pia kuhakikisha usalama wa mradi
huo mkubwa kwa manufaa mapana ya jamii ya kitanzania.
Mheshimiwa Spika,
kuanza kwa ujenzi wa mitambo ya kusafisha gesi asilia pamoja na bomba la
kusafirisha gesi hiyo hadi Dar es salaam na usambazaji wa umeme katika vijiji
52 vinavyopitiwa na bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Lindi haikidhi wala kujibu
kilio cha wananchi wa Mtwara na Lindi cha kutaka ugunduzi wa gesi asilia katika
mikoa hiyo uweze kunufaisha mikoa hiyo kimaendeleo kutokana na kuwa nyuma
kimaendeleo miaka 52 baada ya uhuru wa Taifa hili.
Mheshimiwa Spika,
wakati waziri akiwasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2012/2013 ya Wizara ya
Nishati na Madini tarehe 27-07-2012 aliliambia bunge hili kuwa, kusainiwa kwa
mkataba wa mkopo kati ya Tanzania na China kwa ajili ya kusafirisha Gesi asili
na ujenzi wa Bomba la kusafirishia gesi toka Mnazi BAY hadi Dar es saalam na
kusainiwa kwa mikataba mingine mitano (5) na mkataba wa uzalishaji na
ugawanyaji wa mapato ya mafuta na Gesi asili kuwa ni miongoni mwa jitihada
ambazo serikali imechukua katika jitihada za kukabiliana na tatizo sugu la
umeme hapa nchini, hata hivyo kama ulivyo utaratibu wa serikali mikataba hii
inaendelea kuwa siri.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali na Wizara ya Nishati na Madini
kuainisha miradi hiyo na kuitengea fedha ili wananchi wa mikoa ya kusini waweze
kunufaika na rasilimali hiyo kwani kwa muda mrefu sana wamekuwa wavumilivu
wakisubiria utekelezwaji wa ahadi za kuwapelekea maendeleo kwa miaka mingi bila
kuyaona wala kuyapata.
Kambi rasmi ya Upinzani , inaitaka
serikali isitishe ujenzi wa Bomba hilo kwanza iende ikajadiliane na wananchi wa
mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani na wakubaliane jinsi ya kuendelea na mradi huo ndipo
ujenzi wa bomba hilo uweze kuendelea , kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeamua
kumaliza tatizo la msingi kwani serikali ikiendelea bila kujali madai ya
wananchi hawa na kuamua kutumia mabavu kujenga hakuna atakayekuwa mshindi kati
ya serikali na wananchi hawa. Ni rai yetu kuwa serikali itaweza kuiona busara
hii ili gesi iweze kuwanufaisha watanzania wote yaani wa Mtwara na wale wa
maeneo mengine.
4.0 MAFUTA
4.1 MFUMO WA UAGIZIAJI MAFUTA KWA
UFANISI
Mheshimiwa Spika, Marekebisho
ya Sheria ya petrol (Petroleum Supply Act 2008) kifungu cha 33(1) kinatamka
kuwa uagiziaji wa bidhaa za petroli lazima ufanyike kwa ufanisi na kwa kigezo
cha unafuu mkubwa wa gharama na kufafanuliwa zaidi na kifungu cha 33(2) ambacho
kinaeleza ufanisi wenyewe ikiwa ni pamoja na :-
a)
Uagiziaji wa pamoja wa kushirikiana (Joint
Procurement)
b)
Uagiziaji
wa ushindani (Compitative Procurement)
c)
Uagiziaji wa shehena kubwa (Bulk
Procurement)
d)
Kwa kutumia fursa ya viwango vya kiuchumi (Taking
advantage of economic Scale). Pia Sheria imetoa fursa ya kubadili kwenye aina
nyingine za uagiziaji utakao onekana unatija zaidi.
Mheshimiwa Spika,
sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (EWURA) sura ya 414
pamoja na Petroleum Conservation Act (cap 392) zimeongeza majukumu ya kudhibiti
na kuratibu uagiziaji mafuta kutoka nje. Pia mfumo wa ununuzi na usafirishaji wa mafuta kwa pamoja
umependekeza kuwa na mratibu (Petroleum Importation Co-ordinator - PIC) wa kukusanya taarifa za mahitaji na
kutayarisha zabuni.
Mheshimiwa Spika,
Kampuni hii , iliratibiwa na EWURA lakini ilisajiliwa kwa masharti ya sheria ya
makampuni na hivyo kuifanya kuwa kampuni binafsi inayomilikiwa na Umoja wa
Makampuni yanayoagiza na kusafirisha mafuta nchini (TAOMAC). Uendeshwaji wa
Kampuni hiyo upo chini ya bodi na Mwenyekiti wa bodi uteuliwa na mkutano wa
wanahisa.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani imekuwa ikieleza jinsi gani Wizara inavyoshindwa kusimamia
mambo ya msingi kwa mujibu wa sheria na kanuni za uwepo wake. Mfano dhahiri ni
kitendo cha Mhe Waziri kuteua Mwenyekiti wa Bodi ya PIC kwa kutumia Nafasi yake
na mbaya zaidi kumteua Ndugu James Andindile ambaye ni Kamishna msaidizi-Wizara
ya Nishati ni dhahiri kuwa Wizara itashindwa kufanyakazi yake ya usimamizi.
Kambi
Rasmi ya Upinzani inamtaka Mhe.Waziri alieleze Bunge ni kwa vipi ana uwezo wa kuingilia
utendaji wa Kampuni Binafsi kwa kuteua Mwenyekiti wa Bodi? Ni mfumo gani umewekwa wa kuhakikisha Wizara
inafanya usimamizi?
Mheshimiwa Spika, ili
kuepusha watanzania kubebeshwa mzigo wa gharama kubwa ya mafuta katika Kikao
cha Arobaini na Mbili – Tarehe 9 Agosti, 2011,kulitolewa hoja ya dharura kuhusu
uhaba wa mafuta baada ya michango kadhaa ya waheshimiwa wabunge na hatimae
Serikali ilitoa kauli yake. Baada ya mjadala huo Bunge lilifanya uamuzi. Hata
hivyo hakukuwa na ufuatiliaji wa karibu baada ya maazimio. Hali hii ni moja
katika kasoro kubwa ambayo kuanzia mwaka huu Kambi Rasmi ya Upinzani
inayoongozwa na CHADEMA ilitaka irekebishwe. Katika Kamati zote zilizopo za
sekta hakuna Kamati ambayo inafuatilia maazimio yote ya Bunge ili Serikali kusimamiwa kwa zile
ahadi au maazimio tuliyoyapitisha hapa
Bungeni.
Mheshimiwa
Spika, Kamati ya Nishati na Madini ya Bunge la Tisa iliweza
kupendekeza kwa
Serikali mara nyingi sana kuhusu suala la TPDC kupitia kampuni tanzu ya
COPEC kuanzisha biashara ya mafuta. Kamati ya Nishati ya Bunge
la Tisa ikazungumzia pia Bulk Procurement
pia Strategic Reserve.
Masuala yote haya yamehojiwa na Kambi Rasmi ya Upinzani mwaka 2011 na 2012
Mheshimiwa
Spika, baada ya kushindwa kuchukua
hatua hatimaye Serikali ikaleta ahadi nyingine, nanukuu “leo hii tarehe 9 Agosti, 2011, Serikali
kupitia EWURA imeipa leseni
Kampuni ya COPEC ambayo ni
Kampuni Tanzu ya Serikali kupitia TPDC
kuanza kufanya biashara ya mafuta mara moja.
Naomba kurudia. Leo hii tarehe 9
Agosti, 2011 Serikali kupitia EWURA imeipa
leseni COPEC ambayo ni Kampuni
Tanzu ya Serikali kupitia TPDC kuanza
kufanya biashara ya mafuta mara moja”.
Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka 2011/2012 wa fedha Wizara ya Nishati na Madini, COPEC ilikuwa imepangiwa
shilingi milioni 20 tu kwa ajili ya kampuni hiyo kuanza kufanya biashara.
Ukweli ni kwamba kampuni hiyo haikuwa na miundombinu yoyote ya kuiwezesha
kufanyabiashara kama Serikali ilivyoagiza.
Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ilieleze Bunge toka ilipopatiwa leseni ya
biashara hadi sasa COPEC imeongeza tija ipi katika biashara ya mafuta kwa
watanzania?
Mheshimiwa Spika,
Waziri aliahidi mbele ya bunge kuanza kwa mpango wa utekelezaji uingizaji wa
mafuta wa pamoja (Bulk procurement) mwezi January 2012. Wizara ieleze kuanza
kwa utaratibu huu umeokoa kiasi gani cha pesa kilichokuwa kinapotea kabla ya
kuanza kutumika kwa utaratibu huu mpya na sababu za mpango huo kushindwa
kushusha bei ya mafuta kinyume na ahadi za Serikali.
5.0 UMEME
Mheshimiwa Spika,
Bado kunaendelea kuwepo na utata kuhusu mgawo wa umeme katika maeneo mengine ya
nchi huku serikali ikikanusha kuhusu mgawo wakati watanzania wakiendelea kupewa
nishati hiyo kwa mgawo. Aidha Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini
akiwasilisha makadirio ya Bajeti ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka 2012/1013 aliliambia bunge lako tukufu kuwa “hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Juni 2012
lengo la kuondoa mgao wa umeme lilifikiwa kwa asilimia 100”. Kambi Rasmi ya
Upinzani bungeni inalitaka shirika la
umeme Tanzania (TANESCO) na Wizara ya Nishati na Madini kuwaambia ukweli
watanzania kuhusu mgawo wa umeme kwa kuzingatia hali mbaya ya shirika hilo
kifedha ambayo imeripotiwa na vyombo vya habari hivi karibuni.
Mheshimiwa Spika,
kitendo cha kutowaambia wananchi ukweli kuhusu mgawo wa umeme wakati wananchi
wakipata nishati hiyo kwa mgawo huku wakipewa sababu ambazo zinaonekana hazina
ukweli kinazidi siyo tu kushusha heshima na hadhi ya serikali kwa wananchi wake
bali pia kinadhihirisha udhaifu uliopo katika mfumo wa kiutendaji wa serikali pamoja
na mashirika yake likiwemo shirika la umeme Tanzania (TANESCO).
Mhesimiwa Spika,
mradi wa kuboresha mifumo ya umeme katika jiji la Dar es salaam ambayo imekuwa
ndio kisingizio kikubwa cha mgawo wa umeme hali ambayo inazua maswali mengi kwa
watanzania. Hii ni kutokana na ukweli kwamba
kazi hiyo ilianza katika bajeti ya 2011/2012 na mpaka sasa tatizo la kukatika kwa umeme
bado linaendelea kitendo ambacho kinatafisiriwa kuwa kazi hiyo bado
haijakamilika miaka miwili tangu kuanza
kwa kazi hiyo iliyogharimu shilingi billion 120. Watanzania wanapenda kujua ni
lini hasa kazi hii itakamilika ili kupunguza kero ya mgawo wa umeme kwa Dar es
salaam na Tanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika,
kitendo cha serikali kutoa ahadi hewa zisizo tekelezeka na kutochukua hatua
stahiki dhidi ya watumishi wa serikali wanaoihujumu TANESCO imekuwa ndio chanzo
cha kuzorotesha ufanisi wa shirika hili na kufanya liendelee kuendeshwa kwa
hasara. Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni imekuwa ikishauri mara kadhaa juu ya
kufikishwa mahakamani kwa watumishi wote wa serikali na mafisadi wote
wanaohujumu uchumi wakiwemo wale wa TANESCO, Kiwira, Meremeta, Richmond
n.k lakini inaonekana kuwa ni utaratibu
wa serikali hii au udhaifu wa serikali katika kushughulikia watuhumiwa hao
wa uhujumu uchumi.
Mheshimiwa Spika,
kutokana na udhaifu wa Serikali ya CCM katika kuchukua hatua, kama ilivyokuwa
katika kusamehe naadhi ya wezi wa EPA
na
kuzimwa kwa sakata la Richmond lililosababisha hasara ya mabilioni ya fedha.
Hali hiyo imechangia kuzaliwa kwa sakata jipya la DOWANS linalopelekea TANESCO
kutakiwa kuilipa kampuni hii ya DOWANS ambayo ilirithi mkataba wa kampuni hewa
ya Richmond zaidi ya shilingi 97,000,000,000 kuna zidi kulipatia taifa mzigo
mkubwa. Hii ni kwa sababu kodi za wananchi
na malipo ya wateja zinazotumika katika kashfa zote hizo na
kuwasababishia wavuja jasho wa taifa hili kuwa na ugumu wa maisha pamoja na kwamba waliahidiwa
maisha bora kwa kila mtanzania.
Mheshimiwa spika,Kambi
Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka serikali kutoa taarifa kwa Bunge lako tukufu
ikieleza sababu zinazowafanya wasimfikishe Mahakamani aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu
wa Tanesco Eng. William Mhando, siyo tu kwa matumizi mabaya ya ofisi
yaliyosababisha TANESCO hasara ya zaidi ya bilioni 6,000,000,000 kwa kila mwezi
baada ya kukatisha mkataba wa ununuzi wa mafuta kwa ajili ya IPTL kutoka kwa BP
waliokuwa wakiuza kwa bei nafuu na kuanza kununua kwa kampuni za Oryx na Camel
oil ambayo gharama yake ilikuwa juu bali pia kwa kukiuka miiko ya maadili ya
viongozi wa umma?
Mheshimiwa spika, katika
mjadala wa bajeti ya mwaka 2012/2013 kulijitokeza pia wasiwasi wa namna TANESCO
inavyojiendesha. Bunge liliiomba
Wizara ya Nishati na Madini ichunguze kwa kina suala la mapato ya TANESCO na
jinsi yanavyotumika. Ilionekana TANESCO kwa mwezi inapata takribani Billion 60
au Billion 70. Mishahara ya wafanyakazi wa TANESCO peke yake ni takribani
Billion kumi na moja. TANESCO inatumia fedha nyingi sana kununua umeme kutoka
makampuni yanayotumia umeme hususan wa dharura su kukodisha mitambo ya kufua
umeme wa dharura. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kupitia
wizara ya Nishati na Madini itoe majibu juu ya uchunguzi unaohusu uendeshaji wa
shirika hili.
Mheshimiwa spika,
Mnamo tarehe 18 Julai, 2011 serikali kupitia Waziri Mkuu Mizingo Pinda iliahidi
kupunguza matumizi yasiyo ya msingi ya serikali ilikupata fedha ambazo
zilitegemewa kuliongezea Shirika la Umeme la TANESCO ili liweze kutekeleza
mpango wa umeme wa dharura na kuliongezea shirika hilo uwezo wa kujiendesha.
Hata hivyo ahadi hiyo ilichukua sura mpya baada ya serikali kushindwa
kutekeleza tamko lake la kwanza na kutoa ahadi nyingine tena ya kupata fedha
kwa kukopa ambayo mpaka sasa utekelezaji wake bado unasuasua.
Mheshimiwa spika,
Mnamo 13 Agosti, 2011 serikali ilitoa ahadi ya kuisaidia TANESCO kuweza kukopa
bilioni 408 kutoka kwenye mabenki, lakini mpaka sasa ni jumla ya dola za
marekani milioni 65 ambazo ni sawa na billion 104 tu ndizo TANESCO imeweza
kukopa tena kwa kuchelewa. Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya serikali kama
ilivyoainishwa na Wizara katika ripoti yake ya utekelezaji kwa Kamati ya
Nishati na Madini TANESCO ilipokea fedha hiyo mwezi Januari mwaka huu (2013).
Ahadi hizi zisizotekelezeka zimekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo ya sekta hii
muhimu ya umeme ndiyo maana mpaka sasa ni sehemu ndogo sana ya Watanzania
wameunganishwa na huduma hii muhimu ya umeme.
Mheshimiwa spika,katika
mwaka wa fedha 2012/13 kamati ya kudumu ya bunge ya nishati na madini ilitoa
mapendekezo kazaa kwa lengo la kuboresha sekta ya umeme, mapendekezo hayo ya
kamati pamoja na yale yaliyotolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni mengi hayajafanyiwa kazi na serikali na hata
yale ambayo yamefanyiwa kazi utekelezaji wake ni kwa kiwango kidogo. Aidha mapendekezo
ambayo hayajafanyiwa kazi ni kama ifuatavyo:
(i) kuanzishwa kwa mfuko wa kuendeleza nishati ya
umeme nchini kwa lengo la kutumia mfuko huo kama mtaji (Equity) ili fedha zake
zitumike katika kuboresha huduma ya upatikanaji wa umeme nchini na pia kukopa
kutoka vyombo vingine vya fedha.
(ii).
Kamati pia ilishauri wizara kutenga fedha za kutosha katika uzalishaji,
usambazaji na usafirishaji wa umeme kwani vinategemeana. Cha kushangaza katika
bajeti ya serikali ya mwaka 2013/2014 haijatengwa fedha yoyote ile kwa ajili ya
kuboresha njia za usafirishaji umeme mbali ya kuwepo kwa asilimia 22.5 ya
upotevu wa umeme unaozalishwa inayosababishwa na miundombinu chakavu ya umeme.
(iii). Kamati baada
ya kuona ugumu na gharama ambayo TANESCO itapata katika kusafirisha mafuta toka
bandarini kwenda Nyakato Mwanza ilishauri tangu kwenye bageti ya mwaka
2011/2012 na kurudia ushauri huo katika bajeti 2012/2013 kwamba mradi huu
uhamishiwe sehemu ambayo yatapatikana mafuta ya uhakika na mitambo hiyo itumie
mafuta ya dizeli ili kuweza kunusuru gharama
ambazo nchi itaingia baadaye na kupelekea ufanisi wa mitambo hiyo kuwa
mdogo.
(iv)
Pia Kamati iliitaka serikali kuiwezesha
TANESCO kumiliki mitambo yake badala ya kutegemea mitambo ya kukodi ambayo
inaligharimu shirika hilo fedha nyingi linazolipa kwa makampuni yanayomiliki
kama capacity charge.
Mheshimiwa
Spika, Katika hoja hii Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inaamini
kwamba kamati ilifanya uchunguzi wa swala hili kabla ya kutoa ushauri kwa
serikali. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kutoa mchanganuo
wa gharama ambazo TANESCO itazipata katika kusafirisha mafuta mazito ya mitambo
ya kufua umeme inayo jengwa Nyakato Mwanza.
Mheshimiwa spika,
katika hoja hii serikali imejaribu kueleza jitihada yake ya kujenga mitambo
mbalimbali ya kufua umeme wa gesi ikiwemo ile ya Kinyerezi, Ubungo na Mwanza.
Mheshimiwa spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kueleza bayana namna mitambo hii
inayojengwa itakavyokuwa mbadala wa mitambo ya kukodi kuliko kuendelea
kijisifia inajenga mitambo wakati kuna baadhi ya mitambo imekamilika lakini
bado mitambo ya kukodi haipungui na TANESCO inazidi kulipa capacity charge.
Mheshimiwa spika, umeme
vijijini, zaidi ya bilioni50 ambazo
REA imetengewa, kiasi hiki ni kikubwa,
hivyo kitendo cha Wizara kutenga fedha kwa ajili ya kupeleka umeme
vijijIni bila kutaja idadi na majina ya vijiji vitakavyonufaika na miradi ya
fedha hizo linatoa mwanya wa kutumia vibaya fedha za serikali. Hali hii
imejitokeza pia katika Taarifa za Serikali za mwaka wa fedha 2012/2013 ambapo
hakuna vijiji vya kutosha vilivyooneshwa kunufaika na hivyo kuleta mkanganyiko
mkubwa katika utekelezaji wa miradi hii vijijini.
Mheshimiwa Spika,
pia tunamtaka Waziri aelezee juu ya mradi uliotengewa fedha na Serikali katika
bajeti mwaka wa fedha 2011/2012 mradi uliohusu taa za mwanga bora vijijini
ambao ulitakiwa kutekelezwa Bukombe, Kahama, Biharamulo na Chato. Kambi Rasmi
ya Upinzani inaitaka Serikali itoe majibu kwa nini mradi huo haukutekelezwa
wakati fedha za mradi huo zilitengwa? Pamoja na majibu hayo Kambi Rasmi Bungeni
pia inaitaka Wizara kueleza juu ya mradi mwingine ambao ulifahamika kwa jina la
“TANZANIA AFFORDABLE RURAL ELECTRIFICATION PLAN” ambao ulitakiwa utekelezwe
Bukombe na Kibondo, hasa juu ya hatua iliyofikiwa hadi sasa.
Mheshimiwa
Spika, TANESCO imefika hapo ilipo sasa kutokana na kutokuwa
makini katika uingiaji wa mikataba mbalimbali na makampuni yanayoiuzia umeme.
Kamati ya wataalam wa sheria ya Bunge wakati wa sakata la RICHMOND ilishauri
yafuatayo kuhusiana na mikataba: “kuna ulazima kwa Mikataba mikubwa ambayo
inahusu maslahi na manufaa ya Taifa kama vile Mkataba wa IPTL kuwasilishwa
Bungeni, kwa utaratibu wa dhana ya demokrasia ya uwajibikaji (accountability in
a Parliamentary democracy) kwa ajili ya ushauri wa Bunge kuwasilishwa Bungeni…..
Aidha, Kwa kuzingatia kuwa Mikataba mibovu kati ya TANESCO na Makampuni
mbalimbali ambapo Makampuni hayo yanalipiwa kodi yote na TANESCO imekuwa ni
chanzo cha bei kubwa za umeme katika nchi yetu, na kwa kuzingatia kuwa Mikataba
hiyo inasababisha Sera muhimu za Taifa, kama vile, Sera ya Kupiga vita
Umaskini, Sera ya Huduma Bora kwa Jamii, Sera ya Taifa ya Nishati inayolenga
kusambaza nishati ya bei nafuu vijijini n.k. kutotekelezeka, tunashauri kuwa
Mikataba hiyo ipitiwe upya ili irekebishwe, kwa maslahi na manufaa ya Taifa
letu”.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Mheshimiwa Waziri alieleze Bunge katika
ufanyaji kazi wake ni mikataba mingapi ya uzalishaji wa umeme na kuiuzia
TANESCO, Madini au Gesi imefungwa bila ya kuzingatia ushauri au mapendekezo
yaliyokwishatolewa Bungeni? Kama imefanyika je jukumu la Bunge kuisimamia
Serikali kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 63 ina maana gani?
Mheshimiwa
Spika, matumizi mabaya ya raslimali za umma hayako katika
mikataba ya kukodi mitambo ya umeme tu, bali katika ununuzi wa huduma za
kisheria. Hivyo, narudia kutoa mwito kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali aeleze ni
kiasi cha fedha kilichotumika kwenye kuendesha kesi za Dowans na IPTL mpaka
sasa na hatua zilizochukuliwa dhidi ya mawakili wa TANESCO na makampuni binafsi
yanayotuhumiwa kusababisha mzigo mkubwa wa gharama za kesi ambazo serikali
inashindwa kwa nyakati mbalimbali.
Mheshimiwa
Spika, Izingatiwe kuwa
kwa mwaka wa fedha 2011/2012 pekee jumla ya shilingi bilioni 10 zimetumika kwa
ajili ya gharama za kuendesha kesi hizo kwa kuilipa kampuni ya Rex Attorneys na
Makampuni mengine ambayo kwa nyakati mbalimbali yamekuwa yakiiwakilisha
serikali na TANESCO na kushindwa katika mahakama za kitaifa na kimataifa.
Mheshimiwa
Spika, kufuatia mfululizo wa TANESCO kushindwa mahakamani
huku mabilioni ya walipa kodi na wateja wake yakitumika, Kambi Rasmi ya
Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inapendekeza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa
Hesabu za Serikali (NAO) na Mamlaka ya
Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) wachunguze tuhuma za ufisadi na ubadhirifu
kwa Shirika la Umeme (TANESCO) kwenye matumizi ya mabilioni katika idara ya sheria na ununuzi
wa huduma za kisheria kutoka makampuni binafsi unaofanywa na TANESCO.
Ukaguzi na uchunguzi huo
ufanywe kuhusu matumizi na ufanisi wa huduma za kisheria ambazo TANESCO imekuwa
ikizipata kutoka kwenye makampuni binafsi katika kesi kubwa za kimataifa
ikiwemo ya Dowans na IPTL kwa kurejea pia maoni niliyoyawasilisha bungeni
tarehe 27 Julai 2012.
Mheshimiwa
Spika, katika hotuba ya Kambi Rasmi bungeni mwaka jana
ilitaka Serikali kutoa maelezo ya kina kuhusu matumizi ya kifungu cha 1005 cha
Kitengo cha Sheria ambacho kina kasma ya 229900 ambayo kwa mwaka wa fedha
2012/2013 kimetengewa kiasi cha Shilingi Bilioni 4 kama
gharama za utetezi wa Serikali katika kesi ya IPTL ikiwemo kwa ajili ya
kuilipa kampuni ya Mkono & Co. Advocates.
Aidha, Kambi Rasmi ya
Upinzani iliitaka Serikali kueleza jumla ya fedha zilizotumiwa na Wizara kati
ya mwaka 1995 mpaka 2011 kwa ajili ya kulipa makampuni binafsi ya uwakili
kwenye kesi kubwa za kitaifa na za kimataifa pamoja na kutaja orodha ya
makampuni hayo.
Mheshimiwa
Spika, pia Serikali ilitakiwa ieleze mkakati wa kudhibiti
ongezeko la gharama za kisheria ambazo ni mzigo mkubwa kwa mashirika ya umma na
wananchi walipa kodi kwa kuwa yamekuwepo mazingira ya kesi kuendelezwa kwa muda
mrefu na kugeuzwa kuwa vitega uchumi vya watu wachache. Nilitaja Mifano ya kesi
zilizodumu kwa muda mrefu ni ya IPTL ambayo Serikali inawakilishwa na Mkono and
Co. Advocates na ile ya Dowans ambayo Serikali imekuwa ikiwakilishwa kwa
nyakati mbalimbali na Rex Attorneys.
Mheshimiwa
Spika, Waziri wa Nishati na Madini na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali wanapaswa kulieza Bunge sababu za kuacha kutoa majibu kuhusu suala
hilo mpaka hivi sasa. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua hatua ambazo
Serikali imechukua juu ya matumizi hayo.
Mheshimiwa
Spika, mwaka 2011 Benki ya Standard Hong-Kong ambayo ni mdeni
mkuu katika sakata la IPTL ilifungua kesi ya madai katika mahakama ya Kimataifa
ya Usuluhishi (ICSID case Na. ARB/10/20) inayodai kiasi cha dola za Kimarekani
milioni 225, pamoja na riba katika kuendesha kesi hiyo. Kampuni ya uwakili ya
Mkono (inayomilikiwa na Nimrod Mkono Mbunge wa CCM) ilipewa zabuni ya kuitetea
Serikali katika shauri hilo, na kwa kujiamini iliishauri Serikali kuwa kesi
hiyo tutashinda pamoja na wanasheria wengine kuwa na maoni kinzani kuhusu suala
hilo. Kampuni ya Mkono imekuwa
ikiishauri Serikali isifanye usuluhishi nje ya mahakama ya ICSID wakati wadai
kupitia kwa Mfilisi wa Mali na Madeni za IPTL (RITA) wanakubali kusuluhishwa
nje ya mahakama. Je, mpaka lini Serikali itaendelea kuingia gharama hizo na ni
kiasi gani Serikali imelipa kwa kampuni hiyo na zingine mpaka hivi sasa?
5.1 MPANGO WA UMEME WA DHARURA
Mheshimiwa spika,
itakumbukwa kuwa Bunge lako tukufu lilipitisha mpango wa umeme katika mkutano
wake wa nne. Serikali ililiambia Bunge hili usafirishaji wa gesi kutoka Songosongo
hadi, Somanga hadi Dar es salaam ungeongezwa ndani ya miezi kumi na mbili ili
majenereta yaliyokuwa yamenunuliwa kutumika katika mfumo wa gesi yafanye kazi
ndani ya miezi kumi na mbili. Aidha ilikusudiwa pia kuwa mpango huo ulilenga
kushusha gharama za uzalishaji wa umeme hapa nchini. Ikiwa sasa ni mwaka mmoja
na zaidi umepita fedha zinazidi kutengwa kwa ajili ya kununulia mafuta mazito
ya kuendeshea majenerata, kwa sehemu kubwa ikiwa ni kwa ajili ya mitambo ya
kufua umeme.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kutoa kauli kuhusu sababu za
ucheleweshaji katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na kushindwa kubadilisha mfumo wa majenereta kutumia gesi
badala ya mafuta, na kama kweli dharura iliyokuwepo bado ipo au imekwisha?
Mheshimiwa Spika,
miongoni mwa miradi ya dharura iliyotakiwa kuwa imekamilika ni pamoja na mradi
wa Jacobsen awamu ya pili ambao ulitakiwa kutekelezwa kuanzia mwezi Januari
hadi disemba 2012 ambao ungezalisha mega-watt 150 na kuendeshwa na fedha za
mkopo. Tunapenda kupata ufafanuzi kuhusu miradi hii ya umeme wa dharura miradi
mingapi imekamilika, kiasi gani cha pesa kimetumika na kama taifa tunadaiwa
kiasi gani cha fedha ambazo hadi sasa zimekopwa kwa ajili ya miradi ya umeme
kwa vile ni miongoni mwa maeneo ambayo nchi hii imekuwa ikiingia gharama kubwa
lakini ikishindwa kumaliza tatizo hili na kuchangia katika deni la Taifa ambalo
sasa linafika trilioni 22.
Aidha Mheshimiwa Spika,
moja ya mambo ambayo serikali iliahidi kuyafanyia kazi katika mpango wa umeme
wa dharura ni kununua mitambo yake, napenda kunukuu maneno ya mheshimiwa waziri
mkuu “Mheshimiwa spika ushauri mlioutoa
ni wa msingi sana, moja mumesema serikali nunueni mitambo, ”Kambi Rasmi ya Upinzani
bungeni inaitaka serikali kuliambia bunge hadi sasa tangia kupitishwa kwa
mpango wa umeme wa dharura ni mitambo mingapi ya kuzalisha umeme ambayo inenunuliwa
na tayari imeshaanza kuzalisha umeme. Pia serikali iliambie bunge lako tukufu
ina mpango gani kuhusu mitambo ambayo tumekuwa tunakodi kwa maana ya mitambo ya
Symbion miaka miwili, na mitambo ya Aggreko ambayo yote tumekuwa tunalipa
capacity charge, je serikali imeandaa njia gani mbadala zaidi ya ambayo
tumekuwa tukitumia?
Mheshimiwa Spika
katika mpango wa umeme wa dharura, mashirika ya mifuko ya jamii kama NSSF nayo yaliruhusiwa kuwekeza katika
sekta hii ya umeme, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kupata ufafanuzi kuhusu
mipango inayoendelea juu ya nia hiyo ya mifuko ya jamii kuwekeza katika sekta
ya umeme hapa nchini.
5.2
SYMBION POWER AFRICA LLC, TANESCO NA KUANZISHA
KAMPUNI MPYA YA UMEME KUSINI MWA TANZANIA (SECO).
Mheshimiwa Spika, kutokana
na andiko la kinadharia ‘conceptual proposal’ la kujenga mtambo wa kufua umeme
katika mji wa Mtwara na usambazaji wake
lililoandikwa na kuwasilishwa
Wizara ya Nishati na Madini ,TANESCO na TPDC mnamo tarehe 07 Septemba 2012 na
baada ya andiko hilo kupitiwa kwa kina na TANESCO kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, mnamo
tarehe 12 Februari 2013 Symbion Power Africa LLC waliandaa /waliwasilisha MOU
baina yao na Tanesco ili iweze kusainiwa kwa ajili ya kuanzisha kampuni ya
kuzalisha umeme chini ya kinachoitwa ‘Special Purpose Company’ (SPC), Kampuni hiyo itajulikana kama “Southern Electric Company” (SECO)
ambayo inaanzishwa chini ya utaratibu wa PPP .Kwa mujibu wa MOU ni kuwa
Kampuni
hii itakuwa ni kwa ajili ya kujenga ,kumiliki na kuendesha mitambo
inayotumia gesi kuzalisha umeme 600 MW katika miji ya Mtwara
na Dar Es Salaam.
Aidha
,kampuni hiyo ‘mpya’ ya SECO
itajenga ,kumiliki na kuendesha mtandao wa usafirishaji na usambazaji wa umeme
kutoka kusini mwa Tanzania kwenda kwenye Gridi ya Taifa , Kaskazini mwa Msumbiji
na Malawi ( ….AND to build,own and operate transimission and distribution networks
that will link power plants in the south to the Tanzania grid, northern
Mozambique and Malawi (“the project”))
Mheshimiwa Spika,
MOU hii iliingiwa baada ya Symbion kufanya mazungumzo na Shirika la umeme la
Msumbiji ‘Electricite de Mozambique’ (EDM) kwa ajili ya kuwauzia umeme
eneo la kaskazini mwa Msumbiji katika maeneo ya Pemba na Nacala, hii ni
baada ya EDM kuonyesha kuwa watakuwa tayari kununua umeme kutoka Symbion Tanzania.
Aidha
kwa mujibu wa MOU hiyo ni kuwa tayari Symbion wameshasaini makubaliano na
Wizara ya Nishati ya Malawi kwa ajili ya kuanzisha uchunguzi kuhusiana na mradi
huo wa umeme kutoka nje , kipengele E cha MOU kinasomeka hivi, nanukuu “Symbion has signed an agreement with the
Ministry of Energy in Malawi that provides for the investigation of a cross
border project”
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa MOU kipengele cha 2.1 ni kuwa Symbion ndio
watakuwa na jukumu la kufanya upembuzi yakinifu kwa gharama zao wenyewe na
kuwasilishwa TIC kupitia kampuni ya ‘Special
Purpose Company’ (SPC) kwa ajili
ya kupatiwa hati ya PPP. Aidha, kampuni ya Special
Purpose Company (SPC) itapewa hadhi ya kuwa ‘mwekezaji wa kimkakati’
‘strategic Investor’ .
Aidha , kwa mujibu wa kipengele
cha 2.2 cha MOU ni kuwa umpembuzi yakinifu huo utahusisha pia kuhusiana na
mtaji unaohitajika kuwekezwa na SPC kwa ajili ya mtambo wa kuzalisha 300MW kwa
kutumia gesi pamoja na mtambo wa kuzalisha 300MW Kinyerezi DSM kwa kutumia
gesi.
Mheshimiwa
Spika, kipengele cha 2.4 cha MOU kinasema kuwa upembuzi
yakinifu huo utahusisha pia uwezekano wa kuhamisha mara moja baadhi ya mitambo
ya kuzalisha umeme kutoka mtambo wa kuzalisha umeme wa Symbion Ubungo na
kupelekwa Mtwara,lengo likiwa ni kuongeza ufanisi kwa muda mfupi huko Mtwara.
Kwa mujibu wa kifungu cha
2.5 ni kuwa upembuzi yakinifu huo pia utahusisha utoaji wa mafunzo ya kina
kuhusiana na uendeshaji wa mitambo ya kisasa ya uzalishaji,usafirishaji na
usambazaji wa umeme nchini Marekani kwa ajili ya utawala wa baadae wa SPC .
Mheshimiwa
Spika, kambi rasmi ya upinzani inasikitishwa sana na tabia ya Serikali hii ya
CCM kutokana na tabia yake ya kuendelea kupuuza maazimio ya Bunge hili ,kwani
itakumbukwa kuwa Moja ya maazimio ya Bunge kuhusiana na Richmond ilikuwa ni
kuhusisha Kamati za Bunge katika kuingia mikataba na makampuni ya kuzalisha
umeme , sasa hapa sio kuzalisha tu bali ni kuanzisha kampuni nyingine .
Aidha,
tunataka kujua ni kwanini serikali hii ya CCM imeamua kusaini MOU ya aina hii
bila kuishirikisha kamati ya Bunge au Bunge, tena huu ni mkataba wa kwenda
kuuza umeme nje ya nchi wakati sisi tuna shida kubwa ya umeme. Je, hii haiwezi
kwenda kuwa Richmond nyingine?
5.3
MIRADI
MIKUBWA YA UMEME NCHINI 2013/2014
5.3.1 Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Mheshimiwa Spika,
wakala huyu alianzishwa kwa sheria Na 8 ya mwaka 2005 na alianza kazi rasmi oktoba
mwaka 2007, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka
2003. Lengo likiwa ni kuwapatia wananchi waishio vijijini nishati bora. Pamoja
na umuhimu wa wakala huyu bado serikali haijaonyesha kwa vitendo kuwa ina nia
ya kusaidia wakala huyu ili aweze kutimiza majukumu yake kikamilifu na hasa
linapokuja suala la kuupatia fedha kama zinavyoombwa na zinavyopitishwa na
Bunge hili.
Mheshimiwa Spika,
Takwimu zinaonyesha kuwa serikali imekuwa haitimizi wajibu wake wa kuipatia REA
fedha kama zinavyotengwa na kuidhinishwa na Bunge hili , kwa mfano mwaka
2008/2009 zilipitishwa shilingi bilioni
20.00 ila zilitolewa shilingi bilioni
12.06 sawa na asilimia 60. Mwaka 2009/2010 zilipitishwa shilingi bilioni 39.55, zilizotolewa ni bilioni
22.14 sawa na asilimia 56. Mwaka 2010/2011 zilipitishwa bilioni 58.883, zilizotolewa zilikuwa bilioni 14.652 sawa na asilimia 25. Mwaka
2011/2012 zilipitishwa bilioni 71.044,zilitolewa
bilioni 56.748 sawa na asilimia 80
na mwaka 2012 /2013 zilipitishwa bilioni
53.158, zilitolewa bilioni 6.757
sawa na asilimia 13.
Mheshimiwa Spika,
kwa mwaka huu wa fedha 2013/2014 wakala unahitaji kiasi cha shilingi bilioni 366.9 kwa ajili ya kutekeleza miradi sita ya
nishati vijijini ambayo ni pamoja na awamu ya pili ya kusambaza umeme vijijini bilioni 200, mradi wa kupunguza gharama
za miundombinu na usambazaji wa umeme
vijijini bilioni 10, kupeleka umeme
katika makao makuu ya wilaya mpya 13 bilioni
70, mradi wa kusambaza umeme kwenye maeneo yaliyopitiwa na njia kuu bilioni 75, mradi wa Global Village
Energy Partinership bilioni 10.4 na mradi wa kuhamasisha na
kuongeza matumizi ya nishati jadidifu bilioni
1.5.
Kambi rasmi ya Upinzani, inaitaka
serikali kutenga fedha kama zilivyoombwa na wakala yaani bilioni 366.9 kwa mwaka huu wa fedha na sio kutenga kiasi cha
shilingi bilioni 91 za ndani na bilioni 62 za nje, kama Kifungu 3001, kasma
3113 zinavyoonyesha, kwani wakala huyu asipopewa fedha kulingana na mipango
ilivyo atashindwa kufikia lengo la kusambaza umeme kwa asilimia 30 Vijijini
Aidha,
Kambi rasmi ya Upinzani, inataka kujua fedha zilizotengwa kwa ajili ya REA
2012/2013 asilimia 87 zimeenda wapi ? Mbona hazikupelekewa REA kama Bunge lilivyokuwa
limeamua?
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA, haikubaliani na pendekezo la Waziri
aliloliwasilisha mbele ya kamati ya Bunge (randama uk 22) la kuongeza tozo ya
shilingi 100 kwenye kila lita moja ya mafuta ya petrol kwa ajili ya nishati
Vijijini kwani huku ni kumwongezea mwananchi mzigo wa gharama za maisha, badala
yake tunaendelea kusisitiza kuwa fedha zilizoongezwa kwenye kila lita moja ya
mafuta ya taa mwaka 2011/2012 kwa hoja kwamba ni kuzuia uchakachuaji shilingi
bilioni 600 kwa mwaka zipelekwe zote REA kwani watumiaji wakuu wa mafuta ya taa
wapo vijijini na nusu zipelekwe TANESCO. Aidha makampuni ya madini yalipe kodi
na tozo za mafuta wanayosafirisha na wanayotumia.
5.3.2
Thermal Power Operation Bilioni 273.207
Mheshimiwa Spika,mradi
huu ni kwa ajili ya kuhudumia vituo vya uzalishaji umeme ambavyo vimeungwa
kwenye Gridi ya Taifa na kununua vipuri vyake wakati kina cha maji kwenye
mabwawa ya kufua umeme kitakapopungua kutokana na ukame. Kwa mwaka huu fedha
zilizotengwa ni kwa ajili ya kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya dharura ya
kufua umeme na kununua umeme kutoka kwa wazalishaji hao binafsi.
Mheshimiwa Spika,
Mnamo tarehe 28.07.2012 Naibu Waziri wa Nishati na Madini (nishati)
Mhe.Simbachawene wakati akiwasilisha maoni juu ya hotuba ya bajeti alisema kuwa
tatizo la mgao wa umeme nchini ni la kupangwa mezani, nanukuu (hansard uk.488) ‘………..lakini
kila unapokaa siku mbili unaombwa kukubaliana na mgawo wa umeme na mkizungumza
mezani mgawo unatoweka .Kumbe umeme wa Tanzania ni suala la kuzungumza mezani
halafu mnakubaliana kuwa unakuwepo mgao au haupo;hii haikubaliki’
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya upinzani inaona kuwa hata
suala la kutenga fedha nyingi kiasi hiki kwa ajili ya mafuta ya kuendeshea
mitambo binafsi ya kuzalisha umeme wa mafuta nalo ni jambo la kupangwa mezani,
kwani kama tukiamua kuwekeza kwenye vyanzo vingine vya umeme hakika tusingekuwa
tunatumia fedha nyingi namna hii kwa ajili ya umeme wa mafuta nchini tena
kutoka kwa wazalishaji binafsi.
Mwenendo
wa wizara hii ni kutenga mabilioni ya fedha kila mwaka , Kwa mfano mwaka
2011/2012 zilitengwa bilioni 204.643, mwaka jana 2012/2013 tulitenga bilioni
51.3 (lakini serikali ikatumia kiasi cha
shilingi bilioni 242.96 randama uk.4) na mwaka huu wa fedha tunatenga
bilioni 273.207 kwa ajili ya kununulia mafuta ya mitambo ya kuzalishia umeme.
Yaani kwa miaka 3 tu taifa limeunguza
fedha kiasi cha shilingi bilioni
720.81.kwa ajili ya kulipa makampuni binafsi, hivi Mchuchuma,Liganga,
Stiglersgorge, inahitaji uwekezaji wa kiasi gani?
5.3.3 MRADI WA UMEME IGUNGA
Mheshimiwa Spika,
kutokana na mradi wa umeme ambao unaendelea katika Wilaya ya Igunga kumekuwepo
na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wa vijiji vya Mbutu, Mwamakona, Bukama,
Igunga na vijiji vingine ambavyo mradi huu unapita kutokana na kutokuridhishwa
na kiwango cha fidia ambacho walilipwa ili kuweza kupisha na kuachia ardhi yao,
nyumba zao na mazao yao kwa manufaa ya mradi huo .Wapo waliolipwa shilingi laki
sita, milioni moja nk
Kambi rasmi ya upinzani, imepokea
malalamiko ya wananchi juu ya viwango vidogo vya fidia kwani na madai yao ya kutoona tathimini iliyofanywa
kulingana na mali zao na pia hawakulipwa kwa njia ya hundi pamoja na kutakiwa
kufungua akaunti bali walilipwa kwa fedha taslimu. Hivyo, tunataka kujua juu ya
yafuatayo;
i.
Ni lini wananchi hawa watalipwa kiasi halisi
kulingana na ardhi na mali zao?
ii.
Ni kwanini wananchi hawa walilipwa fedha
taslimu na sio kwa njia ya hundi kama ulivyo utaratibu wa malipo wa serikali?
5.3.4 SERIKALI NA MADENI YA SHIRIKA LA
UMEME TANZANIA (TANESCO)
Mheshimiwa
Spika kambi rasmi ya upinzani bungeni, inaishangaa serikaLi
hii ya CCM kwa kukosa dira ya kuongoza nchi hii, hali hii inatokana na serikali
yenyewe kuwa sehemu ya kudhoofisha Shirika lake yenyewe huku ikitaka
kuwaaminisha watanzania kwamba inashughulikia matatizo ya kupatatikana kwa
umeme nchini.
Mheshimiwa
Spika miongoni mwa matatizo yanayokwamisha shirika la umeme
Tanzania kujiendesha ni pamoja na madeni ambayo yamekuwa sugu kutoka kwa
makampuni mbalimbali, watu binafsi , mashirika , katika hali ya kushangaza
idara za serikali zikiwemo pia Wizara za
Serikali ambayo inajinadi kuweka mpango wa kumaliza tatizo la umeme wakati
ikishindwa kulipia hata bili zake za umeme.
Taasisi za serikali ambazo zinaonekana
kuwa ni wadaiwa sugu hadi kufikia mwazi Januari 2013 ni pamoja na Zanzibar
State Fuel inayo daiwa kiasi cha shilingi 46,136,823,543/=, Jeshi la wananchi
wa Tanzania (TPDF) linadaiwa shilingi 13,839,849,487/=, Jeshi la Polisi
linalodaiwa shilingi 8,994,752,654/= Wizara ya maji inadaiwa shilingi
4,997,245,027/= DAWASA inadaiwa shilingi 4,114,828,175/= na Jeshi la
MAGEREZA linalodaiwa shilingi
3,530,850,068/= pamoja na mifano hii
michache wadai wengine ni pamoja na Regional Water Engineers, Muhimbili Medical
Centre, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Hospitali za serikali, Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii pamoja na Radio Tanzania.
Kwa mjibu wa taarifa rasmi za TANESCO
zilizopo ni kuwa shirika linadai jumla ya Tsh
83,773,824,632/= hadi mwezi januari 2013 kutoka kwa wadaiwa ambao ni wizara na taasisi za Serikali hii ya
CCM .
Kambi
rasmi ya upinzani bungeni, inaitaka serikali kueleza sababu za
kulihujumu shirika la umeme Tanzania kwa kutolipa bili za umeme, lakini pia
ikumbukwe kuwa kila mwaka bunge hili Tukufu linapitisha bajeti kwa Wizara
husika zenye vifungu vya matumizi mengine (0C) ambayo hutumika kufanyia
shughuli nyingine zikiwemo kulipia bill za umeme na gharama za wizara husika ,
tunataka wakati wa majumuisho serikali itoe maelezo kwanini imeshindwa kulipa
hadi sasa, fedha hizo zinafanya kazi gani na lini serikali italilipa shirika la
umeme Tanzania ili kuepukana na matatizo ambayo serikali inayasababisha
yenyewe.
6.0
MADINI
Mheshimiwa Spika,
sekta ya madini ni miongoni mwa sekta ambazo, kama serikali ikiamua kutumia
vizuri rasilimali hii ni miongoni mwa rasilimali ambazo kama zikitumika kwa
masilahi ya Taifa zinaweza kulitoa taifa katika lindi hili la umasikini. Hata
hivyo inaonekana kuwa bado sekta hii kama ilivyo kilio cha watanzania walio
wengi na wenye mapenzi mema na taifa hili bado haijaweza kuchangia pato la
Taifa kwa kiwango kinachotakiwa.
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali hazina ya
madini iliyothibitika hadi sasa ni pamoja na Dhahabu tani 222, Nikel tani
milioni 209, shaba tani milioni13.65, chuma tani milioni 103, Almasi tani
milioni 50.9, Limestone tani milioni 313, magadi soda tani milioni109, chuma tani
milioni 103, jasi tani milioni 3,
phosipahate tani milioni 577, na makaa ya mawe tani milioni 911. Lakini pamoja
na kuwepo kwa hazina hii mchango wa sekta hii katika uchumi wa Taifa na
maendeleo ya jamii haukidhi matarajio ya wananchi. Aidha miongoni mwa vitu
vinavyofanya sekta hii kutochangia vyema ukuaji wa uchumi ni pamoja na misamaha
katika ulipaji wa kodi ya madini. Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni inaishangaa serikali hii ya CCM kwa kushindwa kufuta
misamaha inayotoa kwa makampuni ya uchimbaji wa madini hapa nchini licha ya
kwamba jambo hili limekuwa linapigiwa kelele na wadau walio wengi. Kama taifa
tunajiuliza na kutaka majibu toka kwa serikali ni nini nia hasa siri ya
serikali katika kuendelea kutoa misamaha hii ya kodi.
Mheshimiwa Spika, Kwa
mujibu wa ripoti ya kodi katika madini iliyotolewa na shirika la International
Centre for Tax and Development (ICTD) iliyotolewa mwezi April 2013
inaonesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zinapata pato dogo la
mapato ya ndani yanayotokana na madini kwa wastani wa 1:1.3 ikilinganishwa na
nchi ya Botswana ambayo inawastani wa 1.32:1 ikifuatiwa na nchi ya Chile. Aidha
ripoti hiyo inaonesha kuwa Tanzania ingeweza kufikia kiwango cha nchi ya Chile
kama ingekuwa na viwango vya kutoza kodi kama nchi ya Chile kwa sekta ya madini
na kuchangia kukua kwa pato la Taifa
endapo ongezeko ya kodi ya thamani, kodi ya kusafirisha na kodi ya mapato
zinazotokana na madini zingechangia kupanda kwa pato la Taifa (GDP).
Mheshimiwa Spika,
Swala la mrahaba limeonekana kutopatiwa jawabu halisi kwani kiwango cha
asilimia 4% kinachotozwa kwa sasa baada
ya kufanyika marekebisho bado ni kidogo. Pamoja na kwamba kamati ya Jaji Mark Bomani
kupendekeza kuwa tozo la mrahaba lizingatie ukokotoaji kwa kigezo cha gross value badala ya net back value pendelezo hilo
halitekelezwi kwa ukamilifu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali
kuboresha mazingira ya utoaji wa mrahaba pamoja na kodi, ikizingatiwa kuwa
baadhi ya makampuni hayafuati sheria ya mpya ya madini ya mwaka 2010 inayotaja
kiwango kipya cha mrahaba (Royalty), na kuchukua hatua nyingine za ziada kwa
kuzingatia mapendekezo tuliyotoa 2011 na
2012 hapa Bungeni.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ieleze kwanza ni makampuni gani
ambayo hayajaanza kutumia sheria hii mpya, pili ni hatua gani imechukuliwa
dhidi ya suala hili lakini pia viwango vya kodi na mrahaba vinavyotozwa
vilingane na viwango vinavyotozwa katika nchi nyingine kama Botswana.
Mheshimiwa Spika, kwa
upande wa mchango wa sekta ya madini katika maendeleo na huduma za jamii
(Corporate social responsibility); Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini
kuwa sekta ya madini inayo kazi ya kuhakikisha maendeleo na huduma za jamii. Katika
kufanikisha adhima hii ripoti ya Jaji Mark Bomani ilipendekeza miongoni mwa
mambo mengine ni pamoja na wawekezaji kutoa huduma za jamii ili kuimarisha
uhusiano na jamii zinazozunguka migodi, wawekezaji washiriki katika mashauriano
ya mashauri ili wajue vipaumbele na mirahaba inayokwenda halmashauri itumike
katika kuboresha huduma za jamii.
Mheshimiwa Spika,
pamoja na mapendekezo hayo lakini hali ya halmashauri ambako makampuni ya uchimbaji
wa madini yanakopatikana bado ni wilaya maskini sana. Halmashauri za Kahama,
Geita, Tarime hazifanani na thamani ya madini yanayopatikana katika maeneo yao.
Pamoja na hayo kuna mkanganyiko katika sheria ya Local Authority Finance Act dhidi
ya mikataba na kusababisha halmashauri kukosa haki zake. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
serikali kueleza hatua zaidi za makusudi ambazo inachukua kuhakikisha wananchi
wa maeneo hayo na watanzania kwa ujumla wananufaika na rasilimali za nchi hii
kwa maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kushughulikia mkanganyiko huo wa kisheria.
Mheshimiwa Spika,
naomba kunukuu tulichokisema mwaka 2011/2012 kuhusiana na ujanja wa makampuni
makubwa ya madini “Mheshimiwa Naibu
Spika, Ili kuongeza kiwango cha mapato ikiwemo ya kodi kutokana na uchimbaji wa
madini; Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutekeleza mikakati ya
kupenya kuta za umiliki na mitaji (capital
and ownership structures) zilizojengwa
kwa muda mrefu na makampuni ya kimataifa kwa kutumia mianya ya udhaifu wa kisheria
na ushawishi wa kifisadi uliosababisha mikataba mibovu katika sekta ya madini
nchini. Mheshimiwa Naibu Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kueleza bayana hatua ambazo imechukua kufuatia Ripoti ya Tume/Kamati mbalimbali
ambazo ziliundwa na Serikali kwa nyakati mbalimbali kwa kutumia fedha nyingi za
walipa kodi lakini mapendekezo yake bado hayajatekelezwa kwa ukamilifu wake.
Mathalani ripoti za karibuni za Kamati ya Masha na ile ya Bomani (2008)
zilieleza bayana namna ambavyo makampuni makubwa ya madini yamekuwa yakitumia
sehemu kubwa ya uwekazaji wao kama mkopo (debt
financing). Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kwamba makampuni hayo
yamekuwa yakitumia mianya hiyo ya kisheria na kimikataba kuwezesha wamiliki na
wanahisa kupata faida mapema kuliko kuweka mtaji kwa kuwa riba ya mikopo
huondolewa katika kukokotoa kodi. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Serikali
iwaeleze Watanzania ni trilioni ngapi za mapato tumezikosa kati ya mwaka 1995
mpaka 2010 katika kipindi cha miaka 15
ya kuachia mianya ya upotevu wa mapato kwa kuruhusu asilimia kubwa ya mikopo
kuwa mitaji. Aidha, ni hatua gani zimechukuliwa kwa waliohusika kuliingiza
Taifa katika mikataba mibovu iliyoruhusu makampuni hayo kujitangazia hasara
kila mwaka huku yakipata faida kubwa”.
Mheshimiwa Spika, matatizo
ya wachimbaji wadogowadogo wa madini, kimekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa
taifa hili. Kwa mujibu wa mapendekezo ya kamati ya Jaji Bomani kuhusu namna ya
kuboresha mazingira ya wachimbaji wadogowadogo wa madini, kamati ilishauri muda
wa leseni kuongezwa kufikia miaka 10 ili kuwawezesha wachimbaji hao waweze
kupata mikopo kutoka taasisi za fedha. Wachimbaji kusaidiwa mbinu kwa ajili ya
kupata mtaji wa kufanya shughuli za uchimbaji, kuchangia katika mfuko wa
wachimabji wadogowadogo, kuwekwa kwa utaratibu wa kisheria kwa ajili ya
kuwakatia bima wafanyakazi wao na kuanzisha taasisi za fedha kwa ajili ya
mikopo kupitia SACCOS zao.
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa taarifa ya kamati ya kudumu ya bunge ya Nishati na Madini kuhusu
utekelezaji wa majukumu ya wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha
2011/2012 pamoja na makadirio ya mapato
na matumizi kwa mwaka wa fedha 2012/2013, kamati ilithibitisha matatizo ya
wachimbaji wadogowadogo kuwa ni pamoja bajeti ndogo inayotengwa kwa wachimbaji,
elimu kutotolewa kwa wachimbaji, uhaba wa maeneo ya uchimbaji kwa vile maeneo
yao yamechukuliwa na wawekezaji wakubwa, ukosefu wa masoko ya kuuzia bishaa zao
na kodi kubwa, Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka serikali kueleza hatua
ilizofanya katika kutekeleza mpango mkakati wake hususan katika matatizo
yafuatayo;
(a)
Serikali imeongeza kiasi gani cha fedha
kwenye bajeti ya wachimbaji wadogowadogo,
ni utaratibu gani umewekwa ili fedha hizo ziwafikie walengwa?
(b)
Kuna mkakati gani wa kuhakikisha wachimbaji
hao wanapata mafunzo ya uchimbaji na masuala yanayolenga kuongeza thamani ya
madini yao?
(c)
Maeneo
gani na kanda zipi ambapo wachimbaji hawa wametengewa maeneo kutokana na maeneo
yao kuchukuliwa na wawekezaji wakubwa?
(d)
Serikali imeweka mfumo gani katika kuhakikisha
mchango wa uchimbaji mdogo unajulikana kwenye pato la Taifa?
(e)
Ili kuongeza thamani ya madini, kuna mkakati
gani wa wa kuhakikisha kazi hii inafanyika hapa nchini na kuongeza siyo tu
thamani bali ajira kwa watanzania?
(f)
Hatua
gani zimefanywa na serikali kuhakikisha soko na bei ya madini inakuwa imara na
mikakati gani imewekwa ili kuhakikisha umeme unapatikana katika maeneo ya
wachimbaji wadogowadogo?
Mheshimiwa Spika,
sasa ni takriban miaka sita toka
kuwasilishwa kwa ripoti ya
Mheshimiwa Jaji Mark Bomani kwa Rais. Baada ya kuwasilishwa pia hapa Bungeni na
Kamati husika na Bunge likaijadili na mapendekezo yake yakawa ni maazimio ya
Bunge. Lakini hadi sasa maazimio ya Bunge bado hayatekelezwa kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, Katika
mapendekezo ya tume ya Jaji Bomani ambayo pia yaliridhiwa na Bunge lako tukufu
na kupitishwa kama Azimio la Bunge ni pamoja na kufutwa misamaha ya kodi, kwa
badiliko alilotoa Waziri wa Fedha la kufuta utekelezaji wa GN 99 kuanzia Julai 2009 kwa makampuni.
Marekebisho haya yanahusu kampuni za madini zilizoingia mkataba na Serikali
kuanzia July 2009. Kwa nini ufutaji wa
misamaha hii usiyaguse makampuni yaliyokuwepo kabla ya kamati ya Jaji Bomani
haijaanza kazi?
Mheshimiwa Spika, ukweli
ni kwamba msamaha ambao unaendelea kutolewa hadi sasa kwa makampuni hayo ya
mafuta unaukosesha mfuko wa barabara mabilioni ya fedha na huko makampuni hayo
ndiyo yanaharibu kwa kiasi kikubwa barabara zetu. Kambi Rasmi ya Upinzani
inamtaka Mhe Waziri alieleze Bunge ni kwanini maazimio ya Bunge hadi leo hii
hayajatekelezwa kikamilifu?
Aidha,
Mheshimiwa Spika, mapendekezo
mengine ya kamati ya Mheshimiwa Jaji Bomani yalikuwa ni:
1.
Serikali kumiliki hisa ndogo kama kwa
kampuni ya Williamson Diamonds Limited ambapo Serikali ina hisa 25%, hali
ambayo si sawa kwa umiliki wa kigeni. Upo umuhimu wa ushiriki wa kutosha wa
watanzania katika umiliki wa hisa za kampuni za uchimbaji mkubwa.
2.
Shughuli zote za uchimbaji wa vito, na Kampuni
za uchimbaji wa kati wa madini mengine, zimilikiwe ama kwa 100% au kwa kiasi
kisichopungua 50% na wananchi wa Tanzania.
3.
Shughuli zote za wachimbaji wadogo
zimilikiwe na kuendeshwa na watanzania tu.
Mheshimiwa
Spika, ni matarajio ya Kambi Rasmi ya Upinzani, Serikali
itawaeleza watanzania utekelezwaji wa maazimio hayo ya Kamati ya Mhe.Jaji
Bomani ambayo yaliridhiwa na Bunge yametekelezwa kwa kiwango.
Mheshimiwa Spika, Utaratibu unaotumika
katika kuingia mikataba ya uchimbaji wa madini umewekwa wazi katika Sheria ya
Madini ya mwaka 2010. Sehemu ya 23 ya Sheria hiyo inaelezea kuhusu kuanzishwa
kwa bodi itakayojulikana kama Bodi ya Ushauri ya Sekta ya Madini. Bodi hii
inamshauri Waziri anayesimamia madini kuhusu masuala ambayo yako chini ya
Sheria ya Madini ya mwaka 2010 ambayo yanatakiwa kufikishwa kwenye Bodi.
Mheshimiwa Spika, Wizara
ya Nishati na Madini imeonyesha udhaifu wa kumnyima hata Mkuguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG) kuhakikia mikataba ambayo Serikali imefunga na wachimbaji ili
“kubainisha taratibu ambazo zinafuatwa na
Wizara katika kutekeleza matakwa ya sheria hii kwa vile mikataba hii ya
Uchimbaji ni ya watu binafsi na ni siri kwa watu wengine wasiokuwa sehemu ya
mikataba hiyo. Kutokana na usiri huo, sikupewa haki ya kuipitia mikataba hiyo
na hivyo kuzuia wigo wa ukaguzi wangu”[4].
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaliomba Bunge katika mjadala huu utakaoendelea kupitisha
azimio mahususi kuilazimisha Wizara kuwajibika kwa kuendelea na utekelezaji wa
mikataba yote ambayo, kwa njia moja au nyingine imekiuka sheria na pia imekiuka
maazimio na ushauri unaotolewa na Bunge. Kwa njia hii tutakuwa tumetimiza
wajibu wetu wa Kikatiba wa Kuisimamia na kuishauri Serikali.
Mheshimiwa spika, mchango
wa sekta ya madini katika pato la taifa bado ni mdogo mno ukilinganisha na
jinsi nchi yetu ilivyojaliwa rasilimali hii na uchimbaji unaoendelea sehemu
mbalimbali katika nchi yetu. Kwa ujumla madini tuliyojaliwa hayawafaidishi
watanzania kwa kiwango kilichotegemewa zaidi ya kuwaingiza kwenye matatizo ya
uchafuzi wa kimazingira ugumu wa maisha.
6.1 STAMICO
Mheshimiwa
Spika, Shirika la Madini (STAMICO) linaimarishwa
upya na serikali baada ya kuondolewa kutoka kwenye orodha ya mashirika ya umma
yanayotakiwa kufutwa mwezi Machi, 2009. Hivyo lilipewa majukumu makuu manne,
ambayo ni:
a. Kuwekeza katika utafutaji,uendelezaji na uchimbaji
wa madini
b. Kusimamia hisa za serikali katika migodi
c. Kuratibu uendelezaji wa wachimbaji wadogo nchini, na
d. Kutoa huduma za kibiashara katika sekta ya madini,
huduma hizo ni uchorongaji wa miamba, utafutaji wa madini na utoaji ushauri
katika masuala ya madini.
Mheshimiwa
Spika, taarifa ya shirika
liyowasilishwa kwenye kamati ya madini na nishati, inaeleza kuwa Bodi ilimaliza
muda wake mwezi Juni, 2012. Hivyo basi
shirika hilo halina bodi hai. Kwa mujibu wa taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti
ameongelea kitendo cha Mwenyekiti wa Bodi kuingilia moja kwa moja utendaji wa
shirika hilo kiasi kwamba, shirika limekuwa likimlipa posho ya mafuta
Mwenyekiti huyo sawa na lita 100 za mafuta kila wiki, asilimia 40 ya posho ya
mafuta kama fedha za matengenezo kila wiki na shilingi 500,000/= kwa mwezi kama
fedha za mawasiliano.
Mheshimiwa
Spika, msuguano huu wa kiutendaji
kati ya mkurugenzi mtendaji na Mwenyekiti wa bodi kwa kiasi kikubwa inadumaza
utendaji wa shirika. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kuwachukuliwa hatua za kinidhamu Wenyeviti wenye tabia kama hii kwani malipo
hayo ni aina nyingine ya matumizi mabaya ya raslimali za umma ambayo yanapaswa
kudhibitiwa.
Mheshimiwa
Spika, STAMICO ndiyo yenye dhamana ya
uendelezaji wa Mgodi wa Buhemba, kwani tangu mwezi Julai, 2011 shirika lilipewa
leseni ya utafutaji wa madini juu ya eneo la mgodi wa zamani wa dhahabu wa
Buhemba, mkoani Mara kwa kumiliki asilimia 40 za mgodi huo.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na ukweli kwamba
mgodi huu wa Buhemba ndio uliokuwa ukimilikiwa na kampuni ya MEREMETA kampuni
ambayo mbali ya kuiingiza nchi kwenye kashfa bali pia iliwaacha wananchi/
wachimbaji wadogo wa eneo la Buhemba wakiwa na malalamiko ya kutokulipwa fidia
kwa kutwaliwa maeneo yao. Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kuelewa je STAMICO
inamkakati gani wa kwanza kuchukua mali zilizokuwa zinamilikiwa na MEREMETA? Na
pili madai ya wananchi wanayalipa vipi kwa pamoja na mbia wake?
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa ushauri ulipotolewa
na Mkaguzi kuhusu ushiriki wa Sekta ya Umma na Sekta binafsi kugubikwa na
mapungufu makubwa ambapo faida inakuwa kwenye upande wa pili zaidi na Serikali.
Mfano ni ubia wa SONGAS Ltd, IPTL ltd, Kiwira Coal Mines (TANPOWER LTD), TICTS
na kadhalika. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali iwahakikishie
watanzania ni kwa kiwango gani ubia huo wa STAMICO na MANJARO RESOURCES Pty
Ltd kutoka Australia utakuwa na tija
kwa taifa?
6.2 WAKALA WA
UKAGUZI WA MADINI-TMAA
Mheshimiwa Spika, wizara ya nishati na madini 08
desemba, 2011 ilitoa taarifa kwa umma kuhusu maendeleo ya sekta ya
madini.
Mrabaha uliolipwa na migodi mikubwa ya dhahabu katika kipindi
hicho cha kuanzia mwaka 1998 hadi 2010 ilikuwa
ni Shilingi Bilioni 341.57, wakati hadi
kufikia mwaka 2010 kulikuwa na Watanzania 6,129 walioajiriwa rasmi kwenye
migodi mikubwa 6 ya dhahabu. PAYE wanayolipwa ya kati ya asilimia 14 mpaka
30 kutegemea kiwango cha malipo.
Mheshimiwa Spika, ili kufanya ulinganisho ulio sahihi wa kama kweli mchango wa sekta ya
madini kwenye kodi unatokana na mrahaba au kodi ya PAYE wanayolipa waajiriwa
hao 6,129 ilitakiwa tuambiwe ni kiasi gani, kwani kuna uwezekano mkubwa PAYE
inazidi kwa mbali fedha inayoingia itokanayo na mrahaba.
Mheshimiwa
Spika, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) ndiye mwenye
dhamana katika kudhibiti uzalishaji wa madini na ukusanyaji maduhuli yatokanayo
na mrahaba kwa kampuni za uchimbaji madini. Hata hivyo, TMAA haina udhibiti
wowote katika uzalishaji na uthamanishaji wa madini kwa wachimbaji wadogo na wa
kati ambao wameachwa kueleza wenyewe kiasi cha madini wanachozalisha.
Mheshimiwa Spika,
kutokana na ukweli huo, ni kwa vipi Wizara inataka kuliaminisha Bunge kuwa
takwimu za madini hasa dhahabu
zilizozalishwa hapa nchini kuwa ni sahihi?
Mheshimiwa Spika,
mapungufu haya kwa kiasi kikubwa yanatokana na ukweli kwamba “control
mechanism” kwa wachimbaji wadogo wakati wa kutoa leseni umegubikwa na matumizi
mabaya na udanganyifu ambapo watu wachache wamehodhi maeneo mengi na kuajiri wachimbaji
wadogo na kinachopatikana kutokana na machimbo hayo Serikali inanyimwa taarifa.
Pia kushindikana kwa udhibiti ni viwanja vidogo vya ndege vilivyotapakaa hapa
nchini ambavyo TMAA haina udhibiti navyo.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa hiyo ni kwamba Serikali imechukua hatua
zingine za kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini ni pamoja na:
1. Kutenga maeneo maalum ya wachimbaji
wadogo;
2. TANSORT kuhamishia rasmi shughuli zake
hapa nchini kutoka Uingereza mwezi Agosti, 2010;
3. Upigaji marufuku
wa usafirishaji nje ya nchi madini ghafi ya Tanzanite yenye ukubwa unaoanzia gramu
moja na kuendelea mwezi Aprili, 2010;
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ilieleze Bunge tangu kitengo hicho
cha kuchambua almasi kirudishwe hapa nchini toka Uingereza ni kiasi gani cha
fedha kimepatikana kutokana na kazi zake hizo?
Mheshimiwa Spika, yamekuwepo
madai ya wachimbaji wadogo wadogo ambao ndiyo wazawa kunyimwa leseni katika
maeneo yao ya uchimbaji na maenea yao kugawiwa kwa wanaojiita wawekezaji na wao
wakihamishwa hamishwa pasipo kupatiwa maeneo mbadala.
Mheshimiwa Spika, Kuna
matatizo mengi ya wachimbaji wadogo wadogo katika maeneo ya Kalalani Tanga,
Mgusu, Nyarugusu, Mtakuja Geita, Winza Mtakanini Mpwapwa, Simangulu Chamwino,
North Mara, Rwamgasa, Kasema,Kilindi Nyamongo na kadhalika. Hivi karibu ni
wachimbaji wapatao 400 wa kijiji cha Nkongilangi wanaochimba eneo la Machimbo
ya Sekenke-Iramba Magharibi, ambao toka mwaka 1982 wamekuwa wakiomba leseni
lakini hawapatiwi majibu ya maombi yao. Mwaka 2007 waliomba tena na kuambiwa
leseni imetolewa kwa kampuni ya WASEKE, kwa mshangao mkubwa mwaka 2011 alikuja
mtu anayedai kuwa ndiye mmiliki wa eneo hilo la uchimbaji mdogo la kijiji cha
Nkongilangi aitwaye “JOHN BINA”. Na hapo ndipo matatizo na unyanyasaji
ulipoanzia na kusababisha uporaji na vifo kutokea[5].
Mheshimiwa Spika,
katika mazingira kama hayo, wachimbaji wadogo wapatao 3000 kwa ushirika wao wilayani
Maswa baada ya kulipia ada ya maombi yao imechukua takriban miezi minne baadae
wakajibiwa kuwa eneo hilo tayari lilikuwa na mmiliki toka mwaka 2002. Lakini baada ya kuangalia coordinates zilizosemwa
kwenye barua na zile zilizoko kwenye ramani, ni kwamba leseni PL 4233/2007
ambayo mmiliki wake ni SAVANNAH EXPL. Ltd iliyotolewa tarehe 02/05.2007 na eneo
lake liko Luguru na Luguru ni kijiji kilicho ndani ya wilaya ya Bariadi na sio
Maswa. Huu ni mkakati unaotumiwa na watendaji Idara ya Madini kwa kushirikiana
na wenye dhamana katika Serikali kuwanyima haki wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwaeleza wachimbaji fedha zilizotengwa
kiasi cha shilingi bilioni moja kama
kianzio cha Mfuko wa kuendeleza Wachimbaji wadogo nchini, kama hotuba ya Waziri
Mkuu Mhe. Mazengo Pinda alivyosema Bungeni wakati akiwasilisha mapitio na
makadirio ya matumizi ya fedha yake na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2010/2011
zilipewa wachimbaji wadogo wa wapi?
Mheshimiwa
Spika, aidha, kwa mujibu wa maneno ya Mhe Naibu Waziri
Madini wakati akijibu swali tarehe 22
April 2013 alisema “SERIKALI inatarajia kukamilisha taratibu za Mfuko rasmi wa
kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini, ili kuwawezesha kupata mikopo, ikiwa
ni pamoja na kuwapatia mikopo ya vifaa vya kuchimbia kwa kanda zote nane
zinazochimba madini nchini”.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza mfuko huo ambao umekwisha tengewa
fedha na hapa Naibu Waziri anasema inatarajia kukamilisha taratibu rasmi za mfuko huo, hii maana yake nini? Na
mfuko huo utaendeleza wachimbaji gani wakati ambapo maeneo mengi wana
malalamiko ya leseni na wanafukuzwa ovyo kama mifano ambayo tumeitoa hapo juu.
Mheshimiwa Spika, Kwa
wale walio na maeneo ya kuchimba madini wamekuwa wakifanya kazi katika
mazingira magumu kutokana na kuwa na mtaji mdogo unaowafanya washindwe kupata
zana bora kwa ajili ya uchimbaji. Aidha, watoto wa walalahoi wamekuwa
wakiajiriwa katika migodi mbalimbali nchini mbali ya kuwa na sheria inayopinga
ajira kwa watoto hususan katika maeneo ya migodini.
Mheshimiwa spika, Kitendo
cha serikali kupandisha kodi mara kawa mara kwa wachimbaji au wawekezaji wadogo
wadogo ni kufanya wawekezaji wadogo wasimudu kushiriki kikamilifu katika
kuwekeza ndani ya sekta ya Madini wakati serikali inajigamba kuwasaidia
wawekezaji hao huku serikali ikipandisha kodi kutoka 80,000/= hadi 1,000,000/=
kwa wachimbaji hao.
Mheshimiwa spika,
Jambo hili ambalo pia lililalamikiwa na wabunge wengi limeonekana limetafsiriwa
kuwa ni mkakati wa makusudi wa kuwafukuza wawekezaji wadogo wadogo katika sekta
hii na kutoa mianya kwa wawekezaji wenye pesa zao kuendelea kuwekeza katika
sekta hii ya madini. Kambi rasmi ya
upinzani bungeni inaitaka serikali kieleze kwa kina ni kwa jinsi kani
itawasaidia wachimbaji wadogo kama gharama za uendeshaji wa migodi hiyo
zinapanda bila kuzingatia hali halisi ya wachimbaji hao. Hii ni hatari sana
kwani tunafanya wazawa washindwe kunufaika na sekta hii moja kwa moja.
Mheshmiwa spika, Katika
kuboresha sekta hii ya madini kamati ilishauri mambo yafuatayo yafanyike:
Ø Serikali
kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kushiriki katika shughuli za kutoa huduma(supply)mbalimbali
migodini
Ø Sheria
ya ajira kwa watoto isimamiwe ipasavyo
Ø Migodi
mikongwe ilipe kodi(corporate tax)
Ø Kuwepo
kwa soko la pamoja la madini
Ø Kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo katika
kila kanda na kusimamia vizuri zoezi la ugawaji wa leseni
Ø Serikali
iwasaidie wachimbaji wadogo iliwaweze kapata mikopo ya kuwawezesha kuanzisha
viwanda vidogo vitakavyowasaidia kuongeza thamani ya madini yao
Ø Serikali
kukomesha biashara haramu ya madini
Hata
hivyo serikali haijayafanyia kazi kwa ukamilifu mapendekezo hayo ya kamati
katika mwaka wa fedha 2012/2013 na bado sekta hii inakumbwa na hali ileile na
kuifanya iendelee kutokuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.
Mheshimiwa spika, Taarifa
ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa fedha za serikali ulioishia 30 Juni, 2012 inaonesha kuwa Wizara
ya Nishati na Madini imeliingizia taifa hasara ya zaidi ya shilingi
20,000,000,000 katika sekta ya madini. Hasara hiyo kama ilivyooneshwa kwenye
taarifa ya CAG ilisababishwa na malimbikizo
ya maduhuli ambayo hayakuonyeshwa Sh.1,645,582,899.Taarifa za fedha
zilizowasilishwa na Wizara hazikuonyesha malimbikizo ya maduhuli yenye jumla ya
Sh. 1,645,582,899/- kama ilivyotakiwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za
Serikali
Mheshimiwa
spika, Kambi Rasmi ya Upinzani
bungeni inashangaa ni kwa sababu gani hasa bado sheria ya zamani inaendelea
kutumika wakati tayari sheria ya mwaka 2010 imeshaanza kufanya kazi. Aidha Kambi
Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka Wizara ieleze kwanini hali hiyo
imejitokeza na hatua gani inachukua dhidi ya watendaji waliohusika katika
kulipatia hasara hiyo?
Kambi
Rasmi ya Upinzani pia inaitaka
serikali kutumia sheria mpya ya kukusanya mrahaba katika kampuni za madini na
hivyo makampuni yote yaliyolipa mrahaba huo kwa kutumia sheria ya zamani yalipe
sehemu iliyobakia kwa mujibu wa sheria mpya.
Pamoja na hayo tunaitaka serikali ilitaarifu bunge
lako tukufu kuhusu malimbikizo ya maduhuli ambayo hayakuoneshwa kwenye taarifa
za mahesabu ya wizara hii, tunataka tujue serikali inampango gani na fedha hizi
ambazo ni zaidi ya 1,000,000,000/=.
Mheshimiwa
spika, mambo mengine yanayo
sababisha hasara katika sekta ya madini ni pamoja na kutokuwa na udhibiti wa
mapato ya wachimbaji wadogo wa madini na kutokuwa na udhibiti katika viwanja
vya ndege. Udhibiti mdogo katika sekta hii ya madini kumesababisha kupotea kwa
mapato mengi ambayo nchi ingeyapata kutokana na madini yanayosafirisha bila
kulipa kodi na biashara haramu ya madini inayoendelea nchini.
Mheshimiwa
Spika, Pia kwa mujibu wa taarifa ya
CAG hukuna ushirikianao kati ya wizara na TRA na hivyo kodi nyingi zinashindwa
kukusanywa kutokana na TRA kukosa taarifa sahihi juu ya vyanzo vya mapato vya
wizara hiyo.
Mheshimiwa spika, utekelezaji
wa ahadi nyingine za Waziri wa Nishati
na Madini katika bajeti ya 2012/2013; Waziri
wa Nishati na Madini katika majumuisho yake aliahidi Bunge kuwa kuna madini ya
VANADIUN na PGE yanayopatikana katika madini ya Copper na Nickel. Hilo atalifanyia
kazi suala la wawekezaji wanaochukua leseni ya Copper na Nickel kwani kuna
upatikanaji wa madini ya VANADIUM na PGE ambayo inasemekana kuwa yanathamani
kubwa kuliko Copper na Nickel. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka
serikali kueleza juu ya utekelezaji wa suala hili kama waziri alivyoahidi
bungeni wakati wa kuhitimisha hotuba ya bajeti ya wizara yake ya mwaka wa fedha 2012/2013
Mheshimiwa
spika, katika suala la mkopo wa billion 8.9 kwa wachimbaji wadogo kwamba ni
kwa vipi wachimbaji wadogo wangepewa mikopo hiyo wakati kwa wakati huo leseni
nyingi na maeneo yote wamepewa wawekezaji wakubwa, Mh. Waziri aliliambia bunge
kuwa lesini hizo zinaisha muda wake, na zikiisha muda wake wawekezaji wakubwa
wanaacha nusu ya eneo walilokuwa wanamiliki na hivyo maeneo haya wanapewa
wachimbaji wadogo wadogo.
Mheshimiwa spika,
katika suala hilohilo la wachimbaji wadogo wadogo ilijitokeza pia hoja kutoka
kwa wabunge, waliomuuliza Waziri wa Nishati na Madini jinsi gani mkopo wa
billion 8.9 uliopangwa kuwanufaisha wachimbaji wadogo wadogo nchini utagawiwa
kwa wachimbaji husika. Waziri alijibu wanatakiwa waunde vyama vyao kila mkoa na
wawe na chama chao kitaifa ambako ndiko mkopo huu utaelekezwa.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inaitaka serikali itupe takwimu sahihi mpaka sasa tathmini ikoje juu ya leseni
za wawekezaji wakubwa kuisha muda wake na wawekezaji wadogo kupewa maeneo
husika na je mkopo wa billion 8.9 umewanufaisha wachimbaji wadogo wadogo
wangapi mpaka sasa? Na Kama wachimbaji wadogo hawajanufaika na mkopo huu
serikali itueleze fedha hizi zilizotengwa katika mwaka wa fedha 2012/2013 kwa
ajili ya kazi hii zimefanyiwa nini?
Mheshimiwa spika,
kuhusu madeni ambayo wawekezaji katika sekta ya madini wanadaiwa na serikali, Naibu
Waziri Wa Nishati na Madini wakati wa mjadala wa bageti ya mwaka 2012/2013 alipokuwa
anajibu hoja ya madeni ambayo wawekezaji katika sekta ya madini walikuwa
wanadaiwa tangu mwaka 1997 hadi mwaka 2005 aliliahidi bunge kwamba kampuni ya
BARRICK ambayo ndiyo kampuni pekee iliyokuwa inakataa kulipa deni lake
atalifanyia kazi swala hilo na kuhakikisha wanalipa.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka serikali ieleze kama madeni yote yamelipwa
kwa kuzingatia sheria mpya ya madini ambayo pamoja na mambo mengine inataka
mirahaba kulipwa kwa asilimia nne [4%] kabla ya makato ya makato ya Kodi. Na kama kuna makampuni hayataki kutii sheria
hii mpya ya madini kwa nini serikali isiyafutie leseni ya kufanya kazi za
uchimbaji wa madini nchini ? Kwa sababu nchi haiwezi ikavumilia wawekezaji
ambao hawatii sheria za nchi.
Mheshimiwa spika,
Pia Naibu Waziri alikiri mbele ya bunge lako tukufu kuwa mgodi wa BUZWAGI
haujalipa kodi ya kampuni yaani (Corporate tax), na kuahidi kuwa mgodi wowote
mpya utaoanza kuanzia wakati huo serikali itaanza kuwa na share ya 15% kama
hisa za kubeba (free carried interest).
Tunaitaka
serikali ilieleze bunge lako tukufu na umma wa watanzania kwa ujumla wake kama
mgodi huo umelipa kodi hiyo na serikali imejipangaje kumiliki hisa kwenye
migodi inayotegemewa kuanzishwa na hii ambayo imeanzishwa kwa ajili ya kuwa na
udhibiti wakati kwa kuzingatia masharti
ya sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo inatoa haki hiyo ya Serikali kuwa na
hisa.
6.3 UCHIMBAJI MADINI AINA YA URANI
Mheshimiwa Spika,
Kwa kuwa swala la uchimbaji na utafutaji wa madini ya aina yeyote lipo chini ya
wizara ya nishati na madini , na kwa kuwa swala la uchimbaji wa madini ya aina
ya urani kama taifa tunahitaji kuwa na angalizo kubwa ikiwa ni pamoja na
kutochimba madini hayo ya aina ya urani kutokana na uhatari wake kwa maisha ya
binadamu, na kwa kuwa kambi rasmi ya upinzani kwa mara kadhaa ndani ya bunge
hili imekuwa ikitoa maoni yenye nia njema na maisha ya watanzania na viumbe
vingine na kwa kuwa tatizo la serikali kutokubali kufanya maamuzi ya kubadili
mtazamo wa kutegemea uchumi wa urani na kujikita katika uchumi wa rasilimali
mbadala ambazo taifa letu limebarikiwa kuwa nazo.
Mheshimiwa Spika,
katika eneo la mbarang’andu katika wilaya ya Namtumbo ambapo kampuni ya Game
Frontiers iliyojipatia kitalu hicho kwa ajili ya uwindaji kwa mujibu wa sheria
imeamua kufanya biashara ya kuruhusu utafiti wa uchimbaji madini aina ya urani
kinyume na taratibu za uendesahji wa vitalu vya uwindaji.
Mheshimiwa Spika,katika
bunge hili mnamo Tar 28/07/2012 zilitolewa taarifa hapa ndani ya bunge hili kwa
vielelezo kutoka kwa msemaji wa kambi rasmi ya upinzani bungeni kuhusu maswala
ya ardhi Mhe. Halima Mdee juu ya kampuni ya Game Frontiers kukodisha kitalu
chake cha uwindaji kwa ajili ya utafutaji wa madini ya urani katika eneo la
mbarang’andu katika wilaya ya Namtumbo.
Mheshimiwa Spika, lakini
pia msemaji wa kambi rasmi ya upinzani alitaka kupata ufafanuzi kwa Waziri juu
ya maagizo yaliyotolewa na Naibu Spika wakati wa majumuisho ya Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, maagizo husika yalitaka Wizara ya Nishati na
Madini, wakati wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi itoe maelezo juu ya
mkataba ulioingiwa tarehe 23 Machi, 2007 kati ya Uranium Resources PLC na
Western Metals Limited na Game Frontiers of Tanzania Limited.
Mkataba ambao, pamoja na mambo mengine una ihalalishia Game Frontiers
Limited kupata malipo toka kwa makampuni yanayofanya utafiti katika kitalu
cha uwindaji katika kijiji cha Mbarang‘andu.
Mheshimiwa Spika,
majibu ya waziri yalikua kama ifuatavyo nanukuu …..“Mheshimiwa Spika, lingine lililoulizwa na Kambi ya Upinzani hasa
Mheshimiwa Mdee, huu mkataba wa siri, kweli tumeufuatilia mkataba wa siri, ule
wa uchimbaji wa uranium”…. Kuonesha
waziri alikiri mbele ya bunge na kuahidi kulitafutia ufumbuzi swala hilo, na
kuwa ataleta taarifa kwa mtoa hoja.
Mheshimiwa Spika,kwa
mara nyingine tena kambi rasmi ya upinzani bungeni inataka kujua ni vipi wizara
ya nishati na madini imeshughulikia swala la kampuni ya uwindaji ya Game
Frontiers kukodisha kitalu chake cha uwindaji kwa ajili ya utafutaji wa madini
ya urani katika eneo la Mbarang’andu wialayani Namtumbo, lakini pia serikali
iwaambie watanzania kwa hatua ilizochukua za kuchimba urani ni vipi itaweza
kuwalinda dhidi ya madhara ya uchimbaji wa madini hayo?
6.4
MGODI WA KIWIRA
Mheshimiwa
Spika, kati ya kashfa ambazo
ziliikumba serikali ya awamu ya tatu ya Rais Mkapa ilikuwa ni pamoja na
kubinafsishwa kwa mgodi huu wa Kiwira
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa kumbukumbu za bunge lako tukufu, bunge
lilipitisha maazimio yake juu ya taarifa ya kamati ya Nishati na Madini kuhusu
ubinafisishaji wa mgodi wa kiwira kufuatia mapendekezo yaliyokuwa yameelekezwa
serikalini kwa ajili ya hatua stahiki, miongoni mwa maazimio ya bunge ambayo
hayakufanyiwa kazi na serikali yalikuwa ni pamoja na;
i.
Urejeshwaji wa vifaa na mali ambavyo
vimeibiwa au kuhamishwa kutoka kwenye miundombinu ya mgodi wa kiwira
ii.
Bilioni 17 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ukarabati wa miundomninu ya
mgodi, serikali ilitakiwa kufanya ukaguzi wa matumizi ya fedha hizo kupitia kwa
Mthibiti na Mkaguzi wa Hesabu za serikali ili kujua matumizi halisi na halali
ya fedha za umma
iii.
Serikali kufuatilia uchunguzi uliofanywa na
TAKUKURU wa shilingi milioni 50 zilizotolewa kutoka mfuko wa Consolidated
Holdings Corporation
iv.
Kuwalipa wafanyakazi wa mgodi wa Kiwira mafao yao na stahiki zao kwa wafanyakazi
ambao CAG alithibitisha kuwa hawakulipwa
v.
Serikali kukamilisha haraka zoezi la kukabidhiana
mgodi huo
vi.
Serikali kueleza kigezo kilichotumika
kuwalipa viongozi waandamizi kiasi cha
shilingi milioni 80 wakati wafanya kazi wa kati walilipwa kati ya shiligi milioni 8 na wafanya kazi wa
chini wakilipwa shilingi milioni moja na
nusu.
Mheshimiwa
Spika, jambo lingine ambalo halijafanyiwa kazi lilikuwa ni
hili la malipo yaliyolipwa mara mbili, kwa mjibu wa hansard za bunge , maoni ya
wabunge yalikuwa ni … “niligusie hili la dola milioni nne na laki nane na
sitini na tano ambazo ni sawa na bilioni tano na laki sita, serikali
imekiri…imefanya double payment jambo ambalo ni kosa la jinai, … mwenzangu
anadai tuachane nayo, haiwezekani” lakini katika hali ya kustaajabisha hadi
hivi leo haijulikanai hatima ya fedha hizo zilizolipwa mara mbili. Ni maoni ya
kambi rasmi ya upinzani kuwa serikali ihakikishe maoni yote yanafanyiwa kazi ,
fedha za walipa kodi haziwezi kupotea hivihivi kwa wajanja wachache.
Kambi rasmi ya Upinzani,
inataka maelezo ya kina kuhusiana na mambo yafuatayo;
i.
Fedha za mwaka jana zilitengwa Bilioni 40 na
zilitumika Bilioni 28 kulipa fidia, je fedha hizo alilipwa nani na zilikuwa ni
kwa ajili gani?
ii.
Mwaka huu tumetenga tena bilioni 20 je, ni
kwa ajili ya kuendelea kufidia ufisadi huu ? au ni kwa ajili ya kazi gani?
7.0 HITIMISHO
Mheshimiwa
Spika, Maoni yetu juu ya mapitio ya utekelezaji wa Bajeti kwa
mwaka 2012/2013 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2013/2014
yanaonyesha kwamba chanzo cha hali tuliyonayo hivi sasa ni cha muda mrefu.
Bunge la tisa likiongozwa na Spika Samuel Sitta halikuweza kukamilisha
kurekebisha hali hiyo, ikiwemo kukwepa kukamilisha kwa wakati maazimio ya Bunge
ya mwaka 2010. Bunge la kumi, likiongozwa na Spika Anna Makinda katika kipindi
chake cha kwanza cha miaka miwili na nusu, halijaweza kukamilisha utekelezaji
wa maazimio ya mwaka 2008 na maazimio yake ya mwaka 2011 na 2012. Bunge hili,
bado linalo nafasi ya kurekebisha hali hii kuanzia sasa katika kipindi chake
cha miaka miwili na nusu iliyobaki.
Mheshimiwa
Spika, mwalimu nyerere katika kitabu chake cha TUJISAHIHISHE
ukurasa wa pili (2) aya ya 4 kinasema nanukuu “Makosa yetu mengine hutokana na woga; woga unaotuzuia kumlaumu mkubwa
japo tunajua kuwa kakosa,au kumtetea mdogo anayelaumiwa na wakubwa japo tunajua
kuwa hana makosa. Na msingi wa woga pia ni unafsi. Pengine twaweza kuwa hatuna
cheo cochote ambacho tunaogopa kupoteza; pengine huwa hatuna wala tama yoyote
ya kupata cheo Fulani. Lakini woga unaweza kutokana na tamaa ya kila bindamu
kupendwa na binadamu wenzake. Sisi wote tunayo tama hii, au sivyo tusingekuwa
binadamu. Woga huu huweza ukamfanya mtu kuvumilia maovu, hasa kama maovu yale
yanatendwa na walio wengi kwa walio wachache, au yanatendwa na wakubwa kwa
wadogo. Kwa kuogopa kuwaudhi wengi tunawaacha watende makosa bila
kuwasahihisha, wasije wakatuchukia. Huu ni unafsi mbaya sana. Ni kweli kwamba
demokrasia haiwezi kudumu ikiwa wachache hawatakubali matakwa ya wengi, lakini
matakwa ya wengi hujulikana katika majadiliano au mazungumzo ya wazi wazi.
Mheshimiwa
Spika, lakini pia katika ukurasa wa tatu (3) aya ya pili
anasema nanukuu “Kadhalika, matakwa ya
wachache hujulikana katika majadiliano na na mazungumzo. Bila wale wachache
kusema wazi wazi matakwa yao, majadiliano hayana maana. Wakati mwingine, hata
baada ya majadiliano, wachache japo wamekubali kutii uamuzi wa wengi wanaweza
kuendelea kuamini kwamba mawazo yao ni sawa, na ya walio wengi yamepotoka.
Democrasi inawapa haki, na ukweli unawapa wajibu wa kuendeleza mawazo yao mpaka
wengi waone kuwa ni ya kweli.Bila hivyo maendeleo katika mawazo hayawezekani,
kwani mara nyingi wazo zuri hutokana na mtu mmoja tu. Mwanzo laweza likapigwa,
pengine kwa nguvu kabisa,na walio wengi, lakini hatimaye wengi hulikubali. Huu
ndio msingi wa maendeleo katika mawazo ya binadamu”.
Mheshimiwa
Spika, Katika
sekta za Nishati na Madini, kama ilivyo katika sekta nyingi nchini; tumefika
hapa tulipo kwa sababu ya udhaifu wa Serikali inayoongozwa na Rais Kikwete,
uzembe wa Bunge na ulegelege wa CCM. Kambi Rasmi ya upinzani inayoongozwa na
CHADEMA inataka kama taifa; TUBADILIKE, TUWAJIBIKE, TUJISAHIHISHE.
Mshimiwa Spika, Naomba kuwasilisha.
John
John Mnyika (Mb)
Msemaji
Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-
Wizara
ya Nishati na Madini
22.05.2013
No comments:
Post a Comment