Tuesday, April 2, 2013

RAIS KIKWETE AKUTANA NA NAIBU RAIS WA KENYA WILLIAM RUTO.

Rais kikwete akiongea na Naibu Rais Mteule wa Kenya Mh.William Ruto
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete leo (jana) Aprili 1, 2013 amekutana na Naibu Rais mteule wa Kenya Mhe William Kipchirchir Samoei arap Ruto  ambaye alikuwa nchini kwa mapumziko ya Pasaka.
Akiongea na mgeni huyo katika hoteli ya Seronera iliyoko katika mbuga ya wanyama ya Serengeti  mkoani  Mara, Rais Kikwete  amempongeza Mhe Ruto na Rais mteule wa Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta, kwa ushindi wao kwenye uchaguzi mkuu nchini Kenya.
Mhe Rais pia alimueleza Mhe Rutto furaha yake pamoja na kuridhishwa  na jinsi  uchaguzi ulivyofanyika kwa amani katika nchi hiyo.
Alielelezea  matumaini yake ya kuwa  urafiki uliopo kati ya Tanzania na Kenya  utadumishwa  pamoja na kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mhe Rutto, ambaye aliwasili Mkoani  Mara wiki  iliyopita akiwa na mke wake na watoto, ameondoka  leo baada ya chakula cha mchana alichoandaliwa na mwenyeji wake.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...