Tuesday, April 2, 2013

RUFAA YA SERIKALI DHIDI YA ZOMBE KUANZA KUSIKIRIZWA APRILI 22.


Abdallah Zombwe akihamaki
RUFAA ya kupinga kuachiwa huru kwa aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe na wenzake, inatarajiwa kusikilizwa mfululizo kuanzia Aprili 22 na 23 mwaka huu.

Rufaa hiyo imepangwa kusikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani ambao ni Jaji, Edward Rutakangwa, Jaji Mbarouk Mbarouk na Jaji Bernard Luanda.

Mbali na Zombe, wajibu rufani wengine ni polisi Christopher Bageni, Ahmed Makele, Jane Andrew, Koplo Emmanuel Mabula, Michael Shonza, Abeneth Saro, Rajabu Bakari na Festus Gwasab.

Serikali ilikata rufani hiyo kupinga hukumu iliyotolewa Agosti 17, mwaka 2008 na Jaji Salum Massati wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.

Jaji Massati katika hukumu hiyo aliwaachia huru Zombe na wenzake waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini wa mkoani Morogoro na dereva teksi.

Zombe na wenzake walikuwa wakidaiwa kuwa Januari 14, mwaka 2006 waliwaua wafanyabiashara watatu wa madini wa wilayani Ulanga mkoani Morogoro; Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe na dereva teksi, Juma Ndugu, mkazi wa Dar es Salaam.

Katika hukumu hiyo, Jaji Massati alisema upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha mashitaka bila ya kuacha shaka yoyote na hivyo mahakama iliwaona washitakiwa hawakuwa na hatia na kuwaachia huru.

Alisema mahakama hiyo ilibaini wauaji halisi walikuwa hawajafikishwa mahakamani na hivyo mashitaka dhidi ya washitakwa yasingeweza kutengenezeka. Aliuagiza upande wa Jamhuri iwasake na kuwafikisha mahakamani wahusika.

Baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Mkurugenzi wa Mashitaka wa Serikali (DPP) aliamua kukata rufaa Mahakama ya Rufani, iliyosajiliwa na kupewa namba 254/2009 kupinga hukumu hiyo akidai hakuridhika nayo.
Katika rufani hiyo, DPP aliwasilisha hoja 11 za sheria kupinga hukumu hiyo akidai kwamba kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, washitakiwa wote walikuwa na hatia.

Miongoni mwa sababu nyingine, DPP anadai kulikuwa na upungufu katika hukumu hiyo kwa kila mshtakiwa.

Anadai Jaji Massati alipotoka na kushindwa kutafsiri sheria na kanuni mbalimbali zinazohusu mashitaka ya jinai na kwamba alijichanganya katika hukumu hiyo.

DPP anadai kushangazwa na Jaji Massati kushindwa kuwatia hatia washitakiwa wote ikizingatiwa ulikuwapo ushahidi wa dhahiri na wa mazingira wa kutosha kuwatia hatiani.

Habari hii ni kwa hisani ya Mtanzania.

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...