Saturday, April 13, 2013

MWANAFUNZI CHUO KIKUU CHA RUAHA (RUCO) AJINYONGA


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Fulgence Ngonyani
WATU wawili wamefariki dunia katika matukio tofauti mkoani Njombe, akiwemo mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), mkoani Iringa kufariki dunia, baada ya kujinyonga kwa kutumia waya wa simu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Fulgence Ngonyani alisema tukio hilo limetokea juzi katika mtaa Iwawa, Makete mjini.

Alimtaja mwanafunzi huyo, kuwa ni Albarth Osward (27), mkazi wa kata ya Iwawa na kwamba mwili wake ulikutwa ukining'inia juu ya mti kando ya mto uliopo mtaa wa Ikuru.

Alisema chanzo cha mwanafunzi huyo kuamua kujiua hakijajulikana kwa madai kuwa hakuacha waraka wowote, na kwamba jeshi hilo linaendelea na uchunguzi.

Katika tukio jingine, mkazi wa Kijiji cha Banawanu Wilaya ya Wanging'ombe, Lutan Mbeni (40) ameuawa kwa kukatwa shoka sehemu mbalimbali za mwili wake, baada ya kuvamiwa na kundi la watu wanaosadikiwa kuwa majambazi.

Kamanda Ngonyani, alisema tukio hilo, limetokea juzi usiku baada ya watu hao kubisha hodi nyumbani kwa marehemu wakijifanya wanaomba msaada.

Alisema baada ya hodi hiyo, mke wa marehemu alifungua mlango akidhani ni watu wema ndipo walipomtaka awaonyeshe alipo mume wake.

Watu hao, walifanikiwa kupora fedha Sh 800,000, kisha kumuua kwa kumkata shoka na kutokomea kusikojulikana.

Alisema jeshi la polisi, linaendesha msako mkali ili kuwakamata watu hao wafikishwe mahakamani.

Habari hii ni kwa mujibu wa Mtanzania

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...