Friday, April 19, 2013

MWAKYEMBE-SERIKALI HAITAWAVUMILIA WAKANDARASI WABABAISHAJI

 Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amesema Serikali haitawavumilia makandarasi wababaishaji  na wanaokiuka mikataba yao pindi wanapopata zabuni za kutekeleza miradi mbalimbali  nchini.
Pia, alitoa onyo kwa makandarasi wababaishaji ambapo amesema hatavumilia kuona Tanzania inafanywa kichaka cha watu wanaokuja kuchota fedha za bure na kuondoka pasipo kutimiza majukumu yao, ambayo yanakuwa yameainishwa kwenye mikataba wanayoingia na Serikali.
Waziri Mwakyembe alisema hayo  Dar es Salaam jana wakati akishuhudia   Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) ikisaini mkataba wa ujenzi wa jengo  la tatu la abiria kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA).
Akizungumza katika halfa  hiyo, Mwakyembe alisema ujenzi wa jengo hilo ni faraja kubwa kwa Serikali ya Tanzania, kwani litasaidia kuongeza ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira kwa Watanzania.
Alisema licha ya Serikali kupongeza jitihada hizo za TAA asingependa kuona ujenzi wa jengo hilo ukifanywa chini ya kiwango kwani huu ni wakati wa kuhakikisha kila kitu kinachofanyika nchini kinafanywa kwa viwango vya hali ya juu. Mwakyembe aliiagiza TAA kusimamia mradi huo uweze kumalizika kwa muda uliopangwa na kwamba idhibiti ubadhirifu wowote wa mali zitakazotumika katika mradi huo.
Akizungumza baada ya kutia saini mkataba huo Kaimu Mkurugenzi wa TAA, Suleiman Suleiman alisema ujenzi huo utafanyika kwa awamu mbili na kwamba hadi kukamilika kwa jengo  hilo litakuwa na uwezo wa kuchukua abiria milioni sita. “Jengo la abiria lina uwezo wa kuchukua abiria zaidi ya milioni moja lakini tunapata faraja kwamba pindi ujenzi huu utakapo kamilika uwanja wa JNIA utakuwa na uwezo mkubwa wa kuchukua abiria wengi na kwamba ni faida kwa uchumi wa nchi yetu,”alisema Suleiman.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Bam International Martin Bellamy alisema wamepata faraja kushinda zabuni hiyo na kwamba wao kama wenyeji hapa nchini watahakikisha wanafanikisha mradi huo. Jengo hilo linajengwa na Kampuni ya Bam Inenationali ya Uholanzi kwa gharama ya Sh275 bilioni ambapo hadi kukamilika litakuwa na uwezo wa kuchukua abiria milioni sita.

Chanzo, Mwananchi.

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...