Thursday, April 11, 2013

CHADEMA NA JUKWAA LA KATIBA KUJITOA KWENYE MCHAKATO WA KATIBA MPYA.

Mwenyekiti wa kambi rasmi ya upinzani Bungeni Mh.Freeman Mbowe.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kitajitoa katika mchakato wa Katiba Mpya endapo mambo muhimu mawili hayatapatiwa ufumbuzi hadi kufikia Aprili 30, mwaka huu.

Wakati Chadema wakisema hayo, Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), limesema uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba uliomalizika siku tatu zilizopita katika maeneo mbalimbali nchini haukuwa huru na ni batili, huku likipendekeza urudiwe katika maeneo yote yaliyokumbwa na kasoro.

Katika hoja zake, Chadema kimesema kinataka kufutwa kwa uteuzi/uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza ya Wilaya ya Katiba uliofanywa na Kamati za Maendeleo za Kata na badala yake wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya wachaguliwe moja kwa moja na wananchi wa Kata husika bila kuchujwa na Kamati za Maendeleo za Kata (WDC).
Msimamo huo ulitolewa na Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe wakati akisoma hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2013/14 huku akiitaka Serikali kuwasilisha muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba ili maeneo kadhaa yafanyiwe marekebisho.

“Katika Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba tunataka marekebisho ya vifungu vyote vinavyohusu uwakilishi katika Bunge Maalumu la Katiba wa taasisi zilizoainishwa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Pia vifungu vyote vinavyohusu ushiriki wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka Zanzibar katika mijadala inayohusu mambo yasiyokuwa ya Muungano.”

Jukwaa la Katiba
Kwa upande wake, Jukwaa la Katiba limesema Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatakiwa kubadili mwenendo wake kuanzia katika utaratibu wa kuwapata wajumbe hao hadi uundwaji wa Bunge la Katiba na wananchi kupiga kura za maoni. Limesema isiporekebisha utaratibu huo, litakwenda mahakamani kusitisha mchakato mzima wa Katiba.

Kumalizika kwa uchaguzi huo kunaashiria kuanza kwa mabaraza ya Katiba Mei mwaka huu, ambayo yatakuwa yakijadili rasimu ya Katiba ambayo imetokana na maoni mbalimbali yaliyotolewa na wananchi.

Mwenyekiti wa Jukata, Deus Kibamba alisema uchaguzi huo ulikuwa na kasoro zaidi ya 15, ambazo ni itikadi za vyama na udini, rushwa, uchakachuaji, upendeleo, ubaguzi wa makundi ya watu wenye ulemavu na kukosekana kwa mwongozo timilifu wa uchaguzi huo.

Baadhi ya mikoa iliyokumbwa na kasoro hizo ni Dar es Salaam, Arusha, Mara, Singida na Dodoma. “Pia kulikuwa na vurugu katika uchaguzi huu, kukataliwa kwa barua za maombi za baadhi ya waombaji, kutokuwa na tarehe rasmi ya uchaguzi, uandikishaji bandia wa wapigakura, kukosekana kwa orodha ya majina ya wagombea katika mitaa na vijiji.”

Habari na Mwananchi

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...