Tuesday, April 23, 2013

KIKWETE:AFRIKA TUNAWEZA KUJISIMAMIA,TUMESHAKUA

Rais Jakaya Kikwete, amesema Bara la Afrika limepitia kwenye kipindi kigumu cha kukabiliana na utawala wa kikoloni ulioendesha mambo kwa kuzikandamiza nchi za Kiafrika, lakini sasa bara hilo limepiga hatua na linaweza kuzitafutia ufumbuzi changamoto za kiusalama pasipo kutegemea msaada wa nje.

Rais Kikwete ambaye alikuwa akizungumza wakati akifungua kikao cha siku moja kilichowajumuisha mawaziri wa Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika (AU), alisema kuwa, Afrika imefanikiwa kujitambulisha kwenye duru la kimataifa kuwa ni bara linaloweza kujiamulia mambo yake bila kuingiliwa.

Alisema Umoja wa Afrika utaendelea kuwa mstari wa mbele kutetea masilahi ya wananchi wa Kiafrika hasa katika kipindi hiki ambacho alisema kuwa kiwango cha migogoro kimeanza kupungua.

“ Kwa kweli hadi kufikia hapa Afrika imepiga hatua, tumeweza kuishughulikia na kuitatua migogo mingi iliyolikumba bara letu,tutaendelea kufanya hivyo katika siku za usoni na kwa kweli sasa tumedhamiria kupambana na viongozi wanaoingia madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi” alisema Rais Kikwete.

Alisema yale yanayoendelea kushuhudiwa sasa katika nchi za Mali, Jamhuri ya Kati ni matukio yasiyovumilika na kwamba suala la kutumia nguvu za kijeshi kwa ajili ya kurejesha utulivu na amani ni suala lisiloepukika.

“Nataka niwakumbushe pia wakati nikiwa mwenyekiti wa AU, tulifanikiwa kurejesha utawala wa kidemokrasia nchini Comoro baada ya Kanali Bacar kujaribu kutaka kuteka moja ya kisiwa,na sasa haya tunayoyashuhudia Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati hayawezi kufumbiwa macho pindi itapolazimika sisi kwa umoja wetu tutalazimika kufanya hivyo hivyo “alisema.

Mbali ya kupigana kijeshi kisiwani Comoro, Tanzania inatazamia kushiriki operesheni ya kivita Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa ajili ya kuwafurusha wanamgambo wa kundi la M23 ambao wamedhibiti eneo la Mashariki mwa nchi hiyo.

Tanzania imeitikia wito wa Umoja wa Mataifa ambao hivi karibuni ulipitisha azimio lilitoa fursa kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) kushiriki operesheni ya kivita kama moja ya hatua ya kukabiliana na waasi hao.

Kuhusu hali ya kisiasa nchini Madagascar, Rais Kikwete alisema nchi za Sadc zitaendelea kufuatilia jinsi wanasiasa wa taifa hilo wanavyotekeleza makubaliano yaliyofikiwa baada ya upatanishi wa muda mrefu ulioongozwa na aliyekuwa Rais wa Msumbiji, Joachim Chissano.

Mkutano huo wa mawaziri wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika ulikuwa na agenda ya kujadili hali ya kisiasa nchini Madagascar kabla ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Julai mwaka huu.

CHANZO:MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...