Thursday, April 11, 2013

MAWAZIRI SASA HAWARUHUSIWI KUTOA SHUKRANI NA POLE BUNGENI

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni za Bunge na Naibu Spika, Job Ndugai
KUANZIA sasa Bunge limepitisha kanuni za kuwabana mawaziri kutoa salamu za pongezi, shukrani na pole pindi wanapokuwa wakizungumza bungeni. Pia Mawaziri hao wamezuiwa kutaja majina ya wabunge waliochangia bajeti zao kwa kuwa kufanya hivyo ni kutumia vibaya muda wa Bunge.
Kauli hiyo, ilitolewa bungeni jana na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni za Bunge ambaye pia ni Naibu Spika, Job Ndugai, alipokuwa akiwasilisha Azimio la Marekebisho ya Kanuni za Bunge.

Pamoja na mambo mengine, Naibu Spika alitoa kauli hiyo alipokuwa akifafanua kauli ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), aliyeonyesha kutoridhishwa na jinsi Spika wa Bunge anavyotumia Kanuni za Bunge juu ya matumizi ya muda.

Katika mazungumzo yake alipokuwa akichangia marekebisho ya kanuni hizo za Bunge, Lissu alimshutumu Spika wa Bunge, Anne Makinda, kwamba anachangia kwa wabunge na mawaziri kupoteza muda kwa sababu wanapokuwa wanazungumza bungeni, husema maneno ambayo hayana msingi wowote bungeni.

Kwa mujibu wa Lissu, kitendo cha mawaziri na wabunge kutoa pole, kutoa pongezi na kushukuru bungeni, ni maneno yasiyokuwa na maana na kwamba kitendo cha Spika kuyaruhusu kinakiuka Kanuni ya 154 ya Bunge.

“Mheshimiwa Spika, pamoja na kusema hayo, naomba niseme jambo hili na nalielekeza kwako moja kwa moja na hili linahusu matumizi ya muda.

“Kiti chako kina nguvu sana na baadhi yetu tunaona kama kiti chako kitatumia vizuri Kanuni za Bunge, tunaweza kuokoa muda mwingi unaopotea bila sababu.

“Huu utaratibu wa mheshimiwa kusimama na kutoa pole, kutoa pongezi unapoteza muda bure na unakiuka kanuni za Bunge. Kwa hiyo, naomba tuweke utaratibu ili ikiwezekana Spika ashukuru au apongeze kwa niaba ya Bunge na Waziri Mkuu apongeze kwa niaba ya Serikali.

“Naamini kama tukifanya hivyo, wabunge watapata muda wa kuchangia badala ya huu utaratibu wa sasa ambapo muda unapotea bila sababu,” alisema Lissu.

Akitoa ufafanuzi wa kauli hiyo, Naibu Spika aliungana na Lissu na kusema kuwa japokuwa siyo busara Spika kumkatisha mbunge asizungumze, wabunge na mawaziri wanatakiwa kutumia muda vizuri kwa kujielekeza kwenye hoja moja kwa moja.

“Marekebisho haya ninayowasilisha hapa, yanalenga kuitendea haki bajeti ya Serikali, kwani wabunge sasa wanapata muda wa kujadili bajeti za wizara kabla ya ile bajeti kuu.

“Kuhusu suala la muda wa kuchangia, marekebisho haya mapya yanasema mbunge atakuwa akichangia kwa dakika 10, wakati wa Bunge la Bajeti na atakuwa akitumia dakika 15 wakati wa Bunge la kawaida.

“Lakini, chama kinaweza kuomba zile dakika kumi zigawanywe kwa wabunge wawili ili kila mmoja achangie kwa dakika tano. Juu ya hili suala la wabunge na mawaziri kutoa pongezi, shukrani na kutoa pole na mawaziri kutaja majina ya waliochangia bajeti zao, kuanzia sasa halitaruhusiwa na nawashauri wabunge kila mnaposimama mwende kwenye hoja na kama unajijua huna hoja, tafadhali usisimame kuzungumza,” alisema Naibu Spika.

Awali katika mazungumzo yake, mbali na kutoridhishwa na jinsi muda unavyotumiwa bungeni, Lissu alilisisitiza Bunge, kwamba kilichokuwa kimewasilishwa na Naibu Spika kilihusu sehemu ya tisa ya Kanuni za Bunge, inayohusu masuala ya fedha na kwamba isije ikatafsiriwa kwamba marekebisho hayo yamegusa na maeneo mengine.

Kuhusu muda wa wabunge kuchangia, aliunga mkono kila mbunge atumie dakika kumi badala ya 15 zilizokuwa zikiruhusiwa kikanuni kwa kile alichosema kuwa, mabadiliko hayo yatawafanya wabunge wengi wazungumze.

Pamoja na hayo, alisema kuna haja Bunge kuangalia upya kanuni ya 96, kifungu cha pili, cha tatu na cha nne kinachompa waziri mamlaka ya kuweka ukomo wa bajeti yake.

Naye, Mbunge wa Viti Maalum, Anna Abdallah (CCM) na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), waliunga mkono kwa nyakati tofauti marekebisho hayo na kusema yanalenga kulipa nguvu Bunge. Pamoja na mjadala huo, Bunge lilipitisha marekebisho hayo.

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...