Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ametoa
mipira zaidi ya 1,200 yenye thamani ya dola 30,000 za Marekani kwa vyama
vya mpira wa miguu vya mikoa ya Tanzania Bara na vituo 21 vilivyo hai
vya kuendeleza vijana (academies).
Shirikisho
la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) lilimpa Rais Tenga fedha hizo
ikiwa ni shukrani kwake kwa kushughulikia mgogoro wa uongozi wa mpira wa
miguu nchini Kenya uliodumu kwa miaka miwili; ambapo nchi hiyo kutokana
na mgogoro huo ilikuwa na vyama viwili (KFF na FKL).
Akizungumza
katika hafla ya kukabidhi mipira hiyo kwenye ofisi za TFF, Dar es
Salaam leo (Aprili 22 mwaka huu), Rais Tenga amesema amefanya hivyo kwa
vile anaamini kuwa mipira ndiyo kitu muhimu katika kuinua mchezo huo
mahali popote.
“Dhamira
yangi si kushukuru kwa hafla hii, bali kutoa sababu kwa nini nimefanya
hivi. Ninaamini kwa kuanzia mipira ndiyo muhimu, pili kwa kufanya hivi
itaonekana kweli mipira imegawiwa,” amesema Rais Tenga.
Amesema
amesema mpira wa miguu kwa Tanzania unahitaji sana watu wa kujitolea,
na yeye amefanya hivyo kwa kujitolea kutokana na ukweli shughuli
anazotumwa na FIFA ni za kujitolea.
Rais
Tenga ambaye pia alitumwa na FIFA kutatua matatizo ya uongozi wa mpira
wa miguu katika nchi za Uganda, Zambia na Sudan Kusini amesema anaamini
anapata fursa hizo kutokana na kuwa kiongozi wa TFF, na kwa kuwakumbuka
waliomchagua ndiyo maana hakusita kupeleka fedha hizo kwenye mipira.
Amesema
moja ya ndoto zake wakati anaingia kuongoza TFF mwaka 2004 ameshindwa
kutimiza ni kusaidia mipira, kwani uwezo wa kununua mipira kwa
wanaocheza katika ngazi ya chini hasa watoto haupo.
“Hizi
kelele zote za maendeleo ya mpira wa miguu ni kwa sababu shuleni hakuna
vifaa. Nia yangu ilikuwa shule zote zipate mipira, lakini hiyo ni moja
ya ndoto nilizoshindwa kutekeleza. Vipaji haziwezi kupatikana kama
watoto hawachezi.
“Tunashukuru
sana kwa Serikali kurejesha mpira shuleni. Hata nitakapoondoka
madarakani nikipata nafasi nitaendelea kuomba mipira kwa ajili ya
shule,” amesema Rais Tenga.
Vyama
vya mikoa ambavyo jumla ni 32 (Tanzania Bara na Zanzibar) kila kimoja
kimekabidhiwa mipira 25 (kumi saizi namba tano, 15 saizi namba nne kwa
ajili ya vijana). Kwa academies ambazo ni 21 kila moja imepewa mipira 25
(minane saizi namba tano, na 15 saizi namba nne).
Viongozi
waliohudhuria hafla hiyo ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa
wa Dar es Salaam (DRFA) Almasi Kasongo, Katibu wa Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) Nassib Mabrouk na Katibu wa Chama cha Mpira
wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) Riziki Majala.
Kwa upande wa shule alikuwa Kanali mstaafu Idd Kipingu ambaye ni mmiliki wa shule ya Lord Baden ya Bagamoyo mkoani Pwani.
CHANZO:TFF
No comments:
Post a Comment