Friday, April 19, 2013

MBOWE AHOJI UHALALI WA NEC KUANDAA MFUMO MPYA WA KUHESABU KURA.

 
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amehoji hatua ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuandaa mfumo mpya wa kisasa wa uhesabuji kura bila kuwashirikisha wadau.
Kutokana na hali hiyo, Mbowe aliitaka serikali kusitisha mchakato huo wa NEC hadi sheria itakapotungwa na kushirikisha vyama vya siasa.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani na Mbunge wa Hai, alitoa kauli hiyo jana wakati akiuliza swali katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Akifafanua zaidi, Mbowe alisema kuna taarifa kwamba NEC imeanza kufanya maandalizi ya uhesabuji kura kutumia mfumo wa kisasa kama ule wa Kenya na Ghana.
Alisema mfumo huo wa kisasa wa uhesabuji kura umeshindwa kufanya kazi nchini Kenya na Ghana na kusababisha msumbufu mkubwa.
“Mheshimiwa Spika, mfumo huo ulifanyika nchini Kenya, lakini ulivurugika na kuamua kutumia mfumo wa zamani wa kuhesabu kura. Wadau wasiposhirikishwa katika hatua za awali, hautaweza kuaminika,” alisema.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu, Pinda, alisema ipo mifumo mingi ya uhesabuji kura, lakini hapa nchini kwa muda mrefu mfumo uliokuwa ukitumika ni ule wa kuhesabu kwa mkono.
“Hivi sasa baadhi ya nchi kama Kenya wanatumia mfumo wa kisasa. Nia ya NEC ni nzuri na bila shaka watakuwa na njia mbadala kama huu wa kisasa utashindwa kama walivyofanya wenzetu Kenya,” alisema Pinda.
Akiuliza swali la nyongeza, Mbowe alisema kwa kuwa mfumo huo ulishindwa Kenya na Ghana na kwa kuwa wadau hawakushirikishwa, waziri mkuu atakuwa tayari kutangaza kusitisha mchakato huo hadi sheria itakapopitishwa na kushirikisha wadau?
Akijibu swali hilo, Pinda alisema kuwa swali la Mbowe linatokana na hofu ambayo alisema haipo kwani hata kura zikihesabiwa kwa vidole hofu hiyo ilikuwa kubwa zaidi.
“Mimi nadhani tuamini kabisa kama NEC ina nia njema kwani imesheheni wataalamu wa aina mbalimbali. Ila hili la wadau kushirikishwa nitawasilisha wazo hilo tuone namna ya kuendelea vizuri na jambo hili,” alisema.
Katika hatua nyingine, Pinda alisema kuwa serikali itaruhusu shughuli za kisiasa katika mikoa ya Lindi na Mtwara hadi hapo hali kuhusu mzozo wa gesi itakapokuwa shwari.
Alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Mnyaa (CUF).
Mnyaa alihoji kwanini serikali ilipiga marufuku ziara ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, katika mikoa ya Lindi na Mtwara wakati wengine wanaruhusiwa.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema ziara ya Maalim Seif ilikuwa ya kisiasa na ndiyo maana alizuiliwa na viongozi wengine wote wa kisiasa wamezuiliwa.
“Hali itakapokuwa shwari, shughuli za kisiasa zitarejeshwa hivi karibuni na Maalim Seif na wengine wataruhusiwa kwenda kufanya kazi za kisiasa. Kwa sasa hapana,” alisema.

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...