Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo(CHADEMA) |
NAIBU Waziri wa Nishati na Madini,
George Simbachawene, amekiri kuwapo kwa tatizo la umeme katika Kanda ya
Kaskazini hususan Mkoa wa Kilimanjaro, kwamba hali hiyo imetokana na
mtandao wa umeme katika mkoa huo kuwa mkubwa.
Simbachawene alitoa kauli hiyo jana
bungeni alipokuwa kijibu swali la Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon
Ndesamburo(CHADEMA), ambaye alitaka kujua serikali ina mkakati gani wa
kutatua tatizo hilo la umeme.
Katika swali lake Ndesamburo alisema
kuwa Kilimanjaro kuna mtandao mkubwa wa umeme wa gridi ya taifa, lakini
umeme unaopatikana ni hafifu sana ambao haufai kutumika hata kuwasha
mshumaa.
Kutokana na hali hiyo, Ndesamburo
alitaka serikali ieleze ina mkakati gani wa kurekebisha umeme huo ili
uwe umeme wa ukweli tofauti na ilivyo sasa.
Akijibu swali hilo, Simbachawene alisema
kuwa ni kweli kuna matatizo mbalimbali ya umeme katika Kanda ya
Kaskazini hasa mkoani Kilimanjaro kutokana na ukweli kwamba mtandao wa
umeme katika mkoa huo ni mkubwa na ni wa muda mrefu.
Alisema kuwa hali hiyo inasababisha
kuzidiwa kwa gridi ya taifa kwa upande mmoja, na kuzidiwa kwa vituo
vyote vya kupoozea umeme, hivyo kusababisha kukatika kwa umeme mara kwa
mara na kuwa na umeme hafifu kwenye mfumo.
Kutokana na hali hiyo serikali kupitia
TANESCO inatekeleza mradi mkubwa wa TEDAP katika mikoa ya Kilimamjaro na
Arusha ili kutatua matatizo ya umeme hafifu.
Simbachawene alieleza kuwa miradi hiyo
ya kuimarisha umeme katika mikoa hiyo inahusisha ujenzi wa nijia kubwa
ya kupoozea umeme ya msongo wa Kv 66 kutoka Kiyungi hadi Mkuyuni.
Chanzo, Mtandao wa kijamii wa CHADEMA
No comments:
Post a Comment