AZAM
FC imelazimishwa sare ya bila kufungana jioni hii na AS FAR Rabat ya
Morocco katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Tatu, Kombe la Shirikisho
Afrika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo
hayo yanaifanya Azam iwe na mtihani mgumu katika mchezo wa marudiano
wiki mbili zijazo Morocco, wakitakiwa lazima kushinda au kutoa sare ya
mabao ili kufuzu.
Pamoja
na sare hiyo, Azam watakumbuka sana mabao matatu ya wazi waliyokosa
kupitia kwa washambuliaji wao wa pembeni, Kipre Herman Tchetche mawili
na Khamis Mcha ‘Vialli’ moja,
Kipre
aligongesha mwamba mashuti mawili katika dakika za 51 pembeni kushoto
katikati na dakika ya 90+1 mwamba wa juu katikati baada ya jitihada za
kuwatoka mabeki wa AS FAR Rabat.
Khamis Mcha naye alimtoka vizuri beki wa pembeni wa AS FAR Rabat dakika ya 52 lakini akapiga nje shuti lake.
Katika
mchezo huo uliochezeshwa na refa Emile Fred wa Shelisheli, aliyesaidiwa
na nduguze Steve Maire na Jean Ernesta pembeni, kipindi cha kwanza Azam
walionekana kucheza kwa tahadhari zaidi na kufanya mashambulizi
machache.
Lakini
kipindi cha pili, walifunguka na kuanza kushambulia moja kwa moja jambo
ambalo liliweka kwenye misukosuko lango la AS FAR Rabat kwa muda mrefu
hadi wachezaji wa timu hiyo kuanza kufanya hila za kupoteza muda ili
kupunguza kasi ya wenyeji.
John
Raphael Bocco ‘Adebayor’ naye alilitia misukosuko mara kadhaa lango la
wageni kila ilipoingizwa mipira ya juu kutokea pembeni hususan kona
japokuwa alikuwa chini ya ulinzi mkali leo.
Kikosi
cha Azam FC leo kilikuwa; Mwadini Ally, Himid Mao, Waziri Salum, David
Mwantika, Joackins Atudo/Luckson Kakolaki dk7, Kipre Balou, Kipre
Tchetche, Salum Abubakar, John Bocco ‘Adebayor’, Humphrey Mieno na
Kahmis Mcha ‘Vialli’/Mwaikimba dk78.
AS
FAR Rabat; Ali Grouni, Mustafa Mrani, Younes Hammal, Younes Belakhdar,
Yassine El Kordy, Abdelrahim Achchakir/Mostafa El yousfi dk74,
Salaheddine Said, Mohamed El Bakkali, Salaheddine Aqqal/Souffiane
Alloudi dk80, Mustafa Allaoui na Hicham El Fathi/Youssef Anouar dk69.
No comments:
Post a Comment