Mchugaji Peter Msigwa. |
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI MHE. MCHUNGAJI PETER MSIGWA, (MB) WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, KUHUSU MAKADIRIO YA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014. (Yanatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) toleo la mwaka 2013)
1.0 UTANGULIZI.
Mheshimiwa Spika, sisi kama wabunge bila kujali CHADEMA, CUF,TLP,UDP CCM au NCCR MAGEUZI tunaamini kwa dhati tunajua kipi ni chema kwa watu wetu na kwa ujumla kushawishika katika uendelevu wa maliasili zetu, haya hayawezi kufikia kwa kutetea maslahi ya sisi binafsi na vyama vyetu pasipo kujifanya kuingiwa na upofu na kutenda kile tunachokiamini.
UTEKELEZAJI WA BAJETI YA 2012/2013
Mheshimiwa Spika,Taarifa za wizara juu ya utekelezaji wa bajeti ya 2012/2013 mbele ya kamati na vile zinavyoonekana katika randama ya mapato na matumizi, inaonesha wazi jinsi wizara na serikali ilivyoweka nyuma swala la miradi ya maendeleo na ulinzi wa rasilimali asili za kitanzania hasa kwa manufaa ya Taifa.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2012/2013 bunge lilipitisha na kuidhinisha fedha za miradi ya maendeleo kutoka katika mapato ya ndani na nje, na hadi kufikia February 2013 wizara ili pokea sehemu ya fedha za nje tuu na hakuna fedha za ndani zilizoelekezwa katika miradi ya maendeleo, pamoja na kupata fedha za nje ambazo ni shilingi 360,002,100 kati ya shilingi 12,712,682,390 bado fedha hizo zilizopokelewa na wizara zinajumuisha fedha za mwaka 2011/2012 shilingi 3,288,835,448/- huu ni uthibitisho dhahiri wa serikali kutoweka kipaumbele miradi ya maendeleo na kuweka rehani kwa wahisani swala la kuendeleza Taifa.
Mheshimiwa Spika,Pamoja na wizara kutoa taarifa imeainisha changamoto zilizopo katika utekelezaji ikiwa ni pamoja na kukabiliana na ujangili,uhaba wa fedha, viendea kazi hafifu, je changamoto kuelezea chanagamoto hizi kwa serikali inayotangaza kukabiliana na tatizo la ujangili pasipo kutenga fedha za kuiwezesha wizara ni nia ya dhati kwa serikali kudhibiti ujangili unaofanywa na mitandao yenye kutumia fedha nyingi?
Mheshimiwa Spika, katika miradi saba iliyopangwa kutekelezwa na wizara ni pamoja na miradi ya idara ya wanyamapori na idara ya misitu na nyuki kama ilivyoanishwa katika kasma namba 2001 na 3001, na serikali kutoipatia wizara fedha za ndani mpaka sasa ni dhahiri serikali kutotambua na kutoona wazi tatizo la ujangili na uharibifu wa misitu katika nchi yetu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kupitia ahadi zake za kutokomeza ujangili ni vema sasa ikatekeleza kwa vitendo, hivyo basi hatuwezi tegemea wahisani kulinda rasilimali zetu huku taarifa kuonesha uhusikaji mkubwa wa mitandao ya ujangili kutoka nje ya nchi.
HISTORIA YA UHIFADHI KATIKA JAMII ZA WAFUGAJI
Mheshimiwa Spika, uhifadhi wa wanyamapori katika historia tangu utawala wa kikoloni sera na sheria zilizotumika kwa miaka mingi hususani maeneo ya hifadhi ya Ngorongoro, mfumo uliopo sasa pamoja na kutishia mustakabali wa wanyamapori nchini pia umekuwa ikidhoofisha usalama wa nchi na umiliki wa rasilimali za wafugaji wa Kimasai.
Mheshimiwa Spika, taasisi za uhifadhi wa wanyamapori zilizoongozwa kwa misingi ya kikoloni, hazikumtenganisha mtu kutoka katika mazingira yake ya asili, kwa kutozingatia yale yaliofanywa na Serikali za kikoloni katika hifadhi hizi mambo ya ulinzi dhidi ya mtu kutozingatiwa na kusababisha binadamu kutengwa na makazi yao moja kwa moja hususani jamii za kimasai katika maeneo ya Ngorongoro na raslimali zao za asili kuchukuliwa na wao kuachwa pasipo kupewa ardhi mbadala kwa matumizi ya shughuli zao za ufugaji.
Mheshimiwa Spika,wakati hoja ya kuundwa kwa maeneo ya hifadhi kama vile Eneo la hifadhi ya Ngorongoro (NCA) kipindi cha utawala wa kikoloni ni dhahiri serikali ya kikoloni ilipata kigugumizi cha kufanya maamuzi ya kutowashirikisha wamasai katika mchakato,lakini waliweza kuwashirikisha wanajamii ya kimasai na kuamua kwa pamoja juu ya uanzishwaji wa eneo la hifadhi pasipo kuwepo malumbano na serikali ya kikoloni, hivyo tofauti tunayoiona sasa ni jinsi serikali ya kikoloni ilivyotii na kuheshimu jamii za kimasai na kuwaacha wakiendelea na maisha yao.
BOFYA READ MORE KUENDELEA
ATHARI ZA MFUMO USIOSHIRIKISHI KWA JAMII ZA UHIFADHI
Mheshimiwa Spika,hasara ya aina muhimu ya wanyamapori imeendelea kuwepo kwa kiwango kikubwa, kwa kuwepo kwa idadi kubwa ya majangili haramu kutoka nje ya maeneo ya hifadhi, kwa matokeo ya mambo kama haya kuna haja ya haraka zaidi ambayo itakuwa endelevu kuchunguza upya fikra na sera na mazoea ambayo imedumu kwa zaidi ya nusu karne sasa katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro baada ya kupuuza mfumo uliokuwepo enzi za ukoloni wa kuwashirikisha wananchi katika uhifadhi yaani Community based Natural Resource Management System(CBNRMS).
Mheshimiwa Spika, nchi yetu imepita katika historia yenye taswira ya ukoloni kufanya vitendo visivyo rafiki kwa wananchi wa Tanganyika kwa wakati huo na Zanzibar, tafsiri iliyowajengea watanganyika kuwa mbaya dhidi ya wakoloni kwa vitendo vyao vya unyanyasaji, pamoja na kufanya vitendo hivyo bado taarifa zinaonesha wakoloni walijali sana maslahi ya jamii za wafugaji katika maeneo yao kwa kuingia mikataba na wafugaji katika maeneo yao yenye kuziwezesha jamii za wafugaji kuendelea kuishi katika maeneo yao na kufanya shughuli zao pasipo kuingiliwa.
Mheshimiwa Spika, serikali ya kikoloni mnamo mwaka 1958 iliingia na kusaini mkataba na jamii za kimasaikwa kuthibitisha kuwa haki za Kimasai juu ya ardhi katika nchi yao zitaendelea kulindwa pasipo kuingiliwa hadi kuwepo kwa makubaliano, pamoja na mapendekezo ya Kamati ya Nihill, serikali ya kikoloni ilikwenda kupata ridhaa ya Wamaasai ya kuhama kutoka Serengeti na kwenda eneo la hifadhi ya Ngorongoro katika makao mapya, katika makubaliano kati ya serikali ya kikoloni na viongozi wa jadi wa jamii ya Wamasai (Laigwanak) kumi na mbili na Makamishna wa Majimbo,Wilaya na Mkoa wa Kaskazini kwa pamoja, Wamasai walikubaliana kuachana na madai yao dhidi ya eneo la Serengeti.
Mheshimiwa Spika,pamoja na makubaliano hayo serikali ya kikoloni iliwaahidi wanajamii wa kimasai kuruhusiwa kufanya marekebisho ya jinsi ya kuendesha maisha na kufanya shughuli za uwindaji katika eneo la hifadhi ya ngorongoro, pia jamii ya kimasai kupewa fidia ya kusambaziwa huduma ya maji katika makazi yao mapya, vivyo hivyo katika hotuba yake wakati akifungua Kikao cha 34 cha Baraza la Kutunga Sheria mwezi Oktoba 14, 1958, Gavana wa serikali ya kikoloni alisema“Najisikia furaha kuchukua fursa hii ya kusisitiza kwamba kwa misingi yote ya usawa na imani nzuri hakuna Serikali itakayo tafakari kuwaondoa Wamasai kutoka maeneo yote ya hifadhi za wanyama za Serengeti na Nyanda za juu za kreta” pia alitoa wito kwa waheshimiwa kuzingatia maoni ya mijadala ya miaka mitatu iliyopita kwa kuwakumbusha mnamo mwaka 1956 serikali ilichagua nyanda za juu kama hifadhi mpya ya taifa kutokana na msuguano kutoka kwa jamii na maoni ya kisayansi yaliyoambatana na mabadiliko ya sera.
Mheshimiwa Spika, swala la uhifadhi wa eneo la Ngorongoro kujengwa kwa kuzingatia maslahi ya wakazi wake katika maeneo ya hifadhi yaliwekwa wazi zaidi katika hotuba aliyoitoa Gavana wa Kimasai wa Halmashauri ya Wilaya Agosti 1959, kwa kusema yafuatayo. Nataka kuweka wazi kwenu wote kwamba ni nia ya Serikali kuendeleza Crater kwa maslahi ya watu na matumizi yake,wakati huo huo Serikali inakusudia kulinda hifadhi ya wanyama katika eneo hilo, pamoja na kuwepo kwa mgongano wa jamii na serikali bado serikali inathamini na kuheshimu shughuli za jamii na haitaingilia shughuli za wafugaji wa kimasai, ni wazi kwamba mkataba ulionesha dhamira ya kutosha ya utawala wa kikoloni kuhakikisha Wamasai wanapata haki zao katika ardhi yao.
Mheshimiwa Spika , mwaka 2009, waziri wa wakati huo Ezekiel Maige aliunda timu ya wataalamu wa ardhi na hifadhi kwenda loliondo kuangalia umuhimu wa uhifadhi ambayo yanafaa kuombwa kwa wananchi ili yaweze kulindwa kama hatua za awali ya kuanzisha pori tengefu. Timu hiyo baada ya kufanya kazi ilipendekeza kuwa eneo muhimu la kiuhifadhi ni lile la ushoroba wa kilomita za mraba 1500 ambalo liko pembezoni mwa eneo la hifadhi la Ngorongoro, Serengeti na Masai mara nchini Kenya. Eneo hili ni mapito ya wanyama migration route na pia ni chanzo cha maji cha mito mingi inayotiririsha maji kuingia hifadhi ya Serengeti ikiwemo mto grumeti ambacho ni chanzo cha maji kwa maelfu wa wanyama ndani ya hifadhi ya serengeti na pori la akiba la grumeti.
Mheshimiwa Spika, mapendekezo ya ripoti hiyo iliwasilishwa kwa wananchi kupata maoni yao, na kabla ya mchakato huo uliokuwa unafuata sheria haujakamilika, yakatokea mabadiliko ya uongozi katika wizara ya maliasili na utalii na ndipo waziri wa sasa Khamis Kagasheki akazuka na msimamo wa kibabe wa kutangaza eneo hilo la km1500 kuwa ni pori tengefu na kupotosha umma kuwa wananchi wameachiwa kilomita za mraba 2500 jambo ambalo si kweli kwani ukweli ni kwamba waziri ameamua kujitwalia ardhi kimabavu ili kuilinda kampuni ya uwindaji ya Otterlo Business Corporation (OBC) ya mwana mfalme Brigadia Mohamad Al-Ali iliyoruhusiwa kuwinda ndani ya vijiji vya tarafa vya loliondo na sale.
Mheshimiwa Spika, katika taarifa yake kwa umma, waziri kagasheki alisema kwamba “..serikali ipo tayari kuangalia upya eneo kubwa alilopewa OBC na ikibidi litapunguzwa..”.Kimsingi OBC ipo katika eneo tengefu la Loliondo tena ndani ya vijiji mahalia kwa kibali cha kuwinda tu na si umiliki wa ardhi, wala hawajawahi kupewa ardhi ambayo Waziri anadai walipewa. Ama kwa kujua au kutokujua inaonesha kuwa zipo njama za kimakusudi (pengine) zinazoongozwa na Waziri wa Maliasili na utalii wa kutaka kumpatia OBC ardhi ya Loliondo, tena kinyume na sheria ya ardhi na sheria ya uwekezaji inayokataza wageni kumiliki ardhi isipokuwa kwa kuwekeza tu.
Mheshimiwa Spika, tumeona na kusikia mgogoro wa wananchi wa Loliondo ulivyoshika kasi hivi karibuni na watu kujiuliza kulikoni kwa yanayotokea? Wakati waziri wa maliasili na utalii Mheshimiwa Balozi Hamis Kagasheki (Mb) alipokwenda na kutaka ardhi ya wananchi wa Loliondo apewe mwekezaji, na wakati huohuo timu ya Chama Tawala chini ya Naibu Katibu Mkuu wake Mwigulu Nchemba kwenda na kupingana na maelekezo au uamuzi wa Serikali inayoongozwa na chama chake. Tafsiri nzuri ni kwamba serikali na chama chake ni kukosa mwelekeo inapofika katika utoaji wa maamuzi inafanya sanaa kwa wananchi wakati maisha ya wananchi yanateketea.
Mheshimiwa Spika, katika kuweka kumbukumbu sawa ni kwamba Mhe Rais ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri ambalo Mhe Waziri Kagasheki ni Mjumbe, na Pia Rais huyo huyo ndiye Mwenyekiti wa Chama kinachotawala (CCM) ambapo Mwigulu Nchemba ni Naibu Katibu Mkuu wake. Katika hali hiyo ni nani mwenye mapungufu?
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sheria ya mwaka 1974 ya wanyamapori kifungu cha 6 kiliainisha maeneo ya vijiji ambapo maeneo hayo yalikuwa na wanyama wengi, sheria hiyo iliyatambua maeneo hayo kama mapori tengefu ambayo ni kama ifuatavyo,Wilaya nzima ya Longido, Zaidi ya 80% ya ardhi yote ya Wilaya ya Monduli hususani maeneo ya Mto wa mbu, Makuyuni Minjingu, Lolksale n.k,Wilaya yote ya Siha, Wilaya ya Hai ikiwemo KIA,Wilaya yote ya Simanjiro, Sehemu kubwa ya wilaya ya Kiteto ikiwemo Kibaya, Wilaya za Kilombero na Ulanga eneo la ramsa ya Kilombero.Wilaya ya Mbarali hususani Bonde la Usangu,Wilaya ya Igunga eneo la Wembere,Wilaya ya Ngorongoro hususani tarafa ya LOLIONDO.
Mheshimiwa Spika, pamoja na ongezeko la watu kwa sasa bado vijiji hivyo vimekuwepo kwa mujibu wa sheria ya mwaka 1974, lakini dhana ya waziri wa maliasili ya kuuaminisha umma kuwa waziri wa ardhi alitoa hati za vijiji kimakosa mnamo mwaka 1994 katika vijiji vya Loliondo na Ololosokwan ni kutotambua ni sheria ipi ilitumika kwa wakati huo.
Mheshimiwa Spika,Kufuatia kukua kwa mahitaji ya ardhi ilitungwa sheria ya wanyamapori mwaka 2009, ambapo katika sheria hiyo namba 5 ya 2009, kifungu cha 16, kinamtaka waziri wa Wanyamapori kuyatambua maeneo ya mapori tengefu na kuyatangaza upya, pamoja na kuyatangaza upya sheria inasisitiza, katika vifungu 16 (4) na 16 (5) kuwa, katika kufanya zoezi hilo, hakuna ardhi ya kijiji itakayoangukia ndani ya pori tengefu jipya (baada ya kutambuliwa) na kuwa wananchi wa maeneo hayo lazima washirikishwe.
Mheshimiwa Spika, hapa tulipofikia ni dhahiri serikali inafanya kazi kwa kusukumwa na wananchi kwani kama wananchi wangethubutu kutii maagizo ya mwanzo kwa kuiogopa serikali ni dhahiri haki yao ingekuwa imepotea bila ya wao kusikilizwa, pia kwa serikali kufanya kazi kwa kujaribu msimamo wa wananchi ni dhahiri sasa serikali inahitaji kujisahihisha na kutambua wananchi hawako tayari kufanyiwa sanaa katika maisha yao. Naomba kutoa wito tena kwa watanzania haki inadaiwa sio inaombwa hivyo waendelee kuunga mkono juhudi za CHADEMA kudai haki zao.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwekwa mara kadhaa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilihoji na kushauri serikali juu ya migogoro iliyopo katika jamii za wafugaji, wawindaji wa asili, warina asali, wakusanya matunda (wahdzabe na Waakire/ Ndorobo) pamoja na kuzitambua jamii husika pia kuitaka serikali kufanya marekebisho ya sheria ya wanyamapori Na 5 ya mwaka 2009, pia kamati ya bunge ya ardhi, maliasili na mazingira, pamoja na ushauri huo muhimu kwa serikali bado serikali imeendelea kuuma maneno kwa kutoa majibu yasiyo na matumaini kwa jamii hizo, kuwa yataangaliwa badala ya kutekeleza, Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inayoongozwa na CHADEMA inaitaka serikali kutoa msimamo wake ni jinsi gani italinda maslahi ya jamii za wafugaji hasa zile zilizohamishwa kutoka Serengeti kama zilivyokubalina na Utawala wa Kikoloni enzi hizo.
Mheshimiwa Spika, UKUSANYAJI WA MADUHULI Mheshimiwa Spika, katika ukusanyaji wa maduhuli ndani ya idara mbalimbali kumekuwepo na baadhi ya takwimu zinazoashirioa ubadhirifu wa rasilimali za umma kwa kuzingatia viwando vinavyotakjwa kwenye makadirio ya makusanyo,ukisoam katika randama ya wizara iliyowasilishwa ndani kamati kifungu namba 1001-idara ya utawala na usimamizi wa rasilimali watu kinatoa kiasi cha fedha zinazotarajiwa kukusanywa kutokana na vyanzo vya mapato kwa mwaka 2013/2014.
Mheshimiwa Spika,kwa mfano taarifa inaonesha makusanyo katika mauzo ya vifaa chakavu ni shilingi 1,000 (Elfu moja)mapato yatokananyo na mauzo ya vifaa sh 1,000 (Elfu moja), Masurufu ambayo hayajarejeshwa sh 1,000 (Elfu moja) pia katika kifungu cha 2001 mapato mengine sh 1,000 (Elfu moja) kwa kutokuwa makini na watendaji wa wizara na kutumia mbinu chafu kuiba rasilimali za umma kwa kuweka viwango vidogo vya makadirio ya ukusanyaji huku takwimu hizi kutokuakisi uhalisia ni dhahiri taifa litaendelea kutafunwa na baadhi ya watendaji wasio waamininfu.
Mheshimiwa Spika, kwa akili ya kawaida wizara haiwezi kufanya kazi ya kukusanya shilingi elfu moja kwa mwaka mzima na huu ni mfano wa maeneo machache kwa kuonesha tabia hii kukithiri ndani ya serikali kwa wahujumu na kujificha katika mgongo wa serikali kutopata mapato ya kutosha huku mapato yakipatikana kwa kiwango kikubwa na bila taarifa zake kuwekwa wazi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kutolea ufafanuzi hujuma hii inayofanywa na watendaji na ni kwa vipi wizara inbadhibiti taarifa za makadirio ya maduhuli kwa kuhakiki ili ziwe na uhalisia zaidi kuliko hivi sasa.
Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha mwaka 2012 serikali imeendelea kutoa vibali vya kuendelea na uwindaji kwa kampuni zilizokuwa na malimbikizo ya madeni, mfano kampuni saba za uwindaji: M/S Malagarasi Hunting Safaris, Mwanahuta & Company Limited, Usangu Ltd, Rana Tours & Safaris Ltd,Coastal Wilderness (T) Ltd, Kilimanjaro Game Trails Ltd na Said Kawawa Hunting Company Ltd kampuni hizi kwa jumla zikidaiwa na wizara jumla ya dola za kimarekani 973,493.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kutoa maelezo ya kina juu ya sababu za kutoa vibali pamoja na kampuni hizi kushindwa kulipa maduhuli kwa wakati na kuendelea kuruhusiwa kufanya uwindaji.
Mheshimiwa Spika, pia wawindaji halali waliopewa leseni wamekuwa wakifanay shughuli za uwindaji na kufikia mwisho wa mwaka 2012 bado serikali haikukusanya maduhuli yenye jumla ya dola za kimarekani 216,000 na kuisababishia hasara serikali, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inachelea kulithibitishia bunge kuwa ni vitendo vya rushwa vinavyoifanya serikali ikose mapato na mapato hayo kuingia mifukoni mwa watumishi wasio waaminifu ndani ya wizara.
SEKTA NDOGO YA UTALII
Mheshimiwa Spika,Taatrifa za upotevu wa mapato ya serikali imeendelea kuonekana katika sekta ya utalii kupitia ada ya Utalii isiyokusanywa, Dola za Kimarekani 158,000 kwa mujibu wa Kanuni Na. 4 ya Kanuni za Utalii (ada na tozo) za mwaka 2009inaeleza kuwa“ada ya leseni kwa kila daraja italipwa kilamwaka kwa kiasi ambacho kimeainishwa katika Jedwali la Pilila Kanuni hizo”.Mapitio ya makusanyo ya mapato yatokanayo na Leseni zaUendeshaji wa Huduma za Utalii katika Wizara ya Maliasili naUtalii kwa mwaka wa fedha 2011/2012 yameonyesha kuwepokwa Kampuni zilizojiingiza kwenye biashara ya kutoa hudumaya utalii lakini hawajalipa ada ya Leseni za Utalii yenye jumlaya Dola za Kimarekani 158,000.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano, malengo ya kiutendaji ni kuboresha mfumo wa makusanyo ya mapato yatokanayo na shughuli za utalii. Kambi ya Upinzani inauliza kama mambo yaliyowazi ya ukusanyaji yanashindikana, huo mfumo utaboreshwa vipi wakati hujuma inafanywa kwa ushirika na watendaji?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kutoa maelezo ya kina ni kwa jinsi gani imehakiki ili kutorudiwa kwa matatizo haya ya kupoteza mapato. Aidha, inaishauri serikali kuchukua hatua kwa watendaji wasiozingatia sheria na kanuni katika kutimiza majukumu yao maana utaratibu huu ni hujuma inayofanywa na wafanyabiashara na watendaji wasio waaminifu kwa umma.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa mpango wa maendeleo, unaonyesha kuwa kwa mwaka huu wa fedha uwekezaji kwenye sekta ya utalii ni shilingi bilioni 43.968 wakati kitabu cha bajeti fedha za maendeleo inaonyesha zimetengwa jumla ya shilingi bilioni 1 tu sawa na asilimia 2 tu,. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza kwa nini hili limekuwa hivi? Na ni tafsiri ya kuwa na mapango wa maendeleo wa taifa kama hatuwezi kuutekeleza? ni kweli sekta hii itaweza kuwa shindani na wenzetu katika jumuiya ya Afrika ya Mashariki au tupo tukisubiri miujiza? Kama si dharau kwa ofisi ya rais idara ya mipango ni nini hiki?
SEKTA NDOGO YA MISITU NA NYUKI
Mheshimiwa Spika, Katika hotuba ya waziri mkuu aliainisha moja ya vipaumbele vya ofisi yake ikiwa ni pamoja na Ufugaji Nyuki,na kueleza mwenendo wa sekta ya nyuki nchini, pamoja na maelezo ya waziri mkuu bado sekta hii ipo nyuma pamoja na matamshi ya kuonesha kuwepo kwa juhudi kubwa katika kuiwezesha sekta hii kukua na kuwa na tija kwa uchumi wan chi na jamii husika, Ufugaji wa Nyuki ni shughuli ya kiuchumi inayoweza kuwaongezea Wananchi wetu kipato na kuwaondolea umaskini. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita 2009 - 2012, uzalishaji wa Asali ulifikia Wastani wa Tani 8,747 na Nta Tani 583 kwa mujibu wa taarifa ya Waziri mkuu bungeni katika hotuba ya makadirio ya bajeti ya 2013/2014,
Mheshimiwa Spika, swala la kipaumbele chochote cha serikali si kufanya kwa malengo ya kutangaza nia kwa wananchi kwa maslahi ya kisiasa, kuna haja ya serikali kuhakiki inatekeleza vipaumbele kwa kuonesha utendaji halisi hasa kuifanya sekta ya nyuki kuwa na manufaa kwa wananchi wanaoingia katika biashara hiyo, takwimu zinazotolewa na taarifa za serikali juu ya kuiwezesha sekta ya ugfugaji nyuiki si za kuridhisha kutokana na rasilimali nyuki tulionayo nchini.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inatoa rai kwa serikali juu ya uwekezaji katika sekta ya nyuki kwa kuendeleza sekta hiyo kuweza kuwafanya wananchi waweze kuuza bidhaa za nyuki na sio bidhaa ghafi.
Mheshimiwa Spika, taarifa za mauzo yatokanayo na bidhaa za misitu,licha ya ukweli kwamba bidhaa za misitu zimekuwa kianzio kikubwa cha mapato kwa Wizara ya Maliasili na Utalii,wizara inaendelea kukiri katika taarifa zake kwa uwazi kwamba hakuna udhibiti wa kutosha kwenye eneo la misitu,hivyo kusababisha makusanyo yamaduhuli sawana asilimia 40 kutokusanywa kwa kutokana na changamoto mbalimbali hususani kuingiliwa na wanasiasa, maslahi madogo kwa watumishi wasimamizi wa misitu,ulegevu katika usimamizi wa sheria na Kutoeleweka vizuri kwa vianzio vya kodi na wakusanyaji mapato kama vilivyoainishwa kwenye kifungu 49 cha sheria ya misitu ya mwaka 2002 (Act No 14 of 2002).
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka serikali kuona umuhimu wa kuboresha maslahi ya watumishi wa umma ili kuwapa motisha na kulinda rasilimali za taifa, pia kuzingatia sheria katika utekelezaji wa mipango ya serikali hivyo itaweza kudhibiti siasa kuingilia utendaji. MAMLAKA YA HIFADHI YA NGORONGORO Mheshimiwa Spika,sheria ya uanzishaji wa mamlaka ya hifadhi za ngorongoro imeonekana kuwa na udhaifu katika baadhi ya maeneo hivyo kutolewa maoni juu ya kuiboresha sheria hiyo kwa manufaa ya umma, na ni dhahiri upo uhitaji mkubwa kwa sasa mamalaka kutakiwa kisheria kuwasilisha sehemu ya mapato katika mfuko mkuu wa serikali, hivo Kambi rasmi ya upinzani bungeni inaitaka serikali kufanya marekebisho ya sheria katika kifungu kidogo cha kifungu cha 14 cha Sheria iliyoanzisha Mamlalaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ili kuitaka mamlaka ilazimike kisheria kuwasilisha asilimia fulani ya mapato yake kwenda Mfuko Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, Kumekuwepo na maoni mbalimbali juu ya ada zinazotozwa kwa magari ya kibiashara yanayoingia katika hifadhi ya ngorongoro kutokana na miongozo iliyopo kutokidhi huduma itolewayo na mamlaka, Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inaitaka serikali kutoa taarifa ya jinsi ilivyoweza kufanyia kazi maoni haya na kuweza kufanya marekebisho ya ada zinazotozwa magari ya kibiashara kuingia eneo la hifadhi ya Ngorongoro.
SEKTA NDOGO YA WANYAMAPORI-
Mheshimiwa Spika, Shoroba (corridor za wanyama –Mapitio ya Wanyama) zote za wanyama nilazima zilindwe kikamilifu, hii ni kutokana na ukweli kuwa wanyama huwa wanaendelea kupita njia ile ile wakati wote wa maisha yao na katika mapito hayo ndio pia hupata muda wa kuzaliana. Mbali na hilo ni pia katika shoroba hizo majangili ndipo hutumia mwanya huo kuwauwa.
Mheshimiwa Spika, Aidha, pamoja na umuhimu wa Corridor hizi za wanyama serikali imekuwa ya kwanza kuziharibu na mfano ni ushoroba uliopo Mvomero ambako yalikuwa ni mapito ya Tembo serikali imejenga jengo la Mkuu wa Wilaya na Halmashauri kwenye eneo hilo, na ni hivi majuzi tu Tembo aliyekuwa anapita eneo hilo iliamriwa auwawe na maaskari wa wanyama pori baada ya kukwama njiani kutokana na kukosa njia eneo hilo, pia upo mfano wa shoroba iliyopo kati ya Tarangire na Manyara inayopitia njia ya Mijingu nayo imevamiwa na kaya za watu wasiozidi 22 na kufunga njia hiyo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ambayo inasema kuwa inahifadhi uhalisia wa mazalia ya wanyama pori wetu, inakuwaje wataalam wetu na Serikali badala ya kulinda wanakuwa ndio waharibifu wakubwa? Mheshimiwa Spika, Hifadhi ya Taifa Rubondo, hifadhi hii ambayo ni Kisiwa kinachoundwa na visiwa tisa vidogo vidogo ambapo kisiwa hiki cha Rubondo ni makazi na mazingira muafaka ya kuzaliana Samaki wakiwemo Sato na Sangara wenye ukubwa wa uzito wa kilo hadi 100. Wanyama wanaopatikana katika hifadhi hiyo ni pamoja na Viboko,Pongo, Nzohe, Fisi maji, Mamba na Pimbi, wanabadilishana makazi na wanyama wengine waliohamishiwa katika hifadhi hii kama Sokwe, Tembo, Mbega weusi na weupe na Twiga.
Mheshimiwa Spika, kukosekana kwa shoroba za kuwafanya wanyama waweze kutoka na kurudi katika hifadhi ni tatizo kubwa kijenetik, kutokana na utafiti uliofanyika unaonyesha kuwa kitendo cha wanyama kukaa eneo moja kwa muda mrefu na kuzaliana wenyewe kwa wenyewe kunaweza kuadhiri wanyama hao. Hili linatokana na ukweli wa kibailojia kuwa uzaliano wa kindugu (In breeding) una madhara makubwa kwa jamii kwani kama kwenye familia ina magonjwa ni dhahiri kuwa familia nzima itakuwa na magonjwa hayo na vivyo hivyo, kwa hifadhi ambazo wanyama wake wametengwa na kufungiwa sehemu moja. Hii ni hatari kwa muendelezo mahiri wa hifadhi hiyo.
TAASISI YA UTAFITI WA WANYAMAPORI-TAWIRI
Mheshimiwa Spika, uwekezaji katika tafiti umeendelea kuwa ni vigumu kwa serikali yetu hususani katika sekta ya wanyamapori kutokana na kutokuwa moja ya vipaumbele vya serikali, nah ii ni kutokana na dhana ya serikali kutotambua umuhimu wa rasilimali hizi kwa maendeleo ya uchumi wa nchi,taasisi ya utafiti wa wanyamapori ambayo ni TAWIRI na inafanyakazi zake lakini kutokana na kutokupatiwa fedha za kutosha za kufanya tafiti zake kwenye sekta ya wanyamapori kumepelekea taarifa muhimu na za maana kutokupatikana hapa kwetu kwa maendeleop ya sekta ya wanyamapori, badala yake tafiti muhimu kwenye sekta hii zinafanyika kwa ufadhili toka nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuwa huu ni udhaifu kwa nchi ambayo inapata mapato mengi kupitia sekta hii na kutowekeza zaidi katika utafiti wa sekta hii,kwa mfano kwa mwaka wa fedha 2011/2012 makusanyo sekta wanyamapori yalikuwa kiasi cha shilingi 15,074,053,972.10 na kwa mwaka wa fedha 2012/2013 makisio yalikuwa shilingi 25,175,381,917.00 Hizi ni fedha nyingi kwa sekta ambayo uwekezaji katika sekta hiyo ni karibia na hakuna, kuna haja ya serikali kuona umuhimu wa kujitathmini zaidi na kuona ni muhimu zaidi kwa maendeleo ya sekta ya wanyamapori kuwa na fungu maalumu kwa ajili ya kuwezesha tafiti mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, kuna taasisi ambayo imepewa dhamana ya kuratibu na kuwezesha tafiti mbalimbali hapa nchini ambayo ni COSTECH, lakini cha ajabu ni kwamba taasisi hii imekuwa haitoi kipaumbele kwa watafiti ambao wanafanya utafiti kwenye sekta hii ya wanyama na badala yake utafiti unaegemea sana fedha za mashirika ya nje ambayo yanakuwa na haki zote za takwimu husika. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuweka vipaumbele kwa kuangalia mchango wa sekta kwenye uchumi husika ambako tafiti zitafanyika.
MTANDAO WA UJANGILI WA WANYAMAPORI
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na taarifa mbalimbali kuhusiana na ujangili wa maliasili. Pembe za ndovu zenye uzito wa tani 4 kutoka nchini Tanzania na Kenya zimeripotiwa kukamatwa na vyombo vya usalama vya mamlaka ya jiji la Hong Kong hivi karibuni, huku zile zilizoibwa kutoka Tanzania zikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.5; meno za ndovu zilizokamatwa wilaya ya Biharamulo; pembe za ndovu zilizokamatwa kwenye gari iliyosemekana ya serikali maeneo ya mto wa mbu; watu watatu waliokamatwa masasi kwa kusafirisha pembe za ndovu; Haya ni matukio machache tu ambayo yaliweza kuripotiwa na jeshi la polisi yanayotoa taswira ya tatizo kubwa la ujangili hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa mtandao wa ujangili dhidi ya wanyama pori ni mtandao wa kimafia ulio mkubwa na hatari ambao unahusisha baadhi ya watumishi wa jeshi la Polisi, jeshi la wananchi, usalama wa Taifa na baadhi viongozi wa Chama Cha Mapinduzi. Tumeshuhudia watuhumiwa wengine wa ujangili ambao Ikulu imediriki kuwapatia nafasi kubwa uongozi wa Taifa hili licha ya kutajwa katika ripoti ya uchunguzi kuhusiana ujangili. Wakati akihojiwa, Mkurugenzi wa TANAPA, Allan Kijazi alikiri kuwa mtandao wa ujangili ni mkubwa sana, unaotumia silaha za kisasa kuliko za TANAPA. Alikiri TANAPA kutumia fedha nyingi katika kuwalinda na kukabiliana na ujangili, lakini wahalifu wanapokamatwa wamekuwa wakiachiwa kinyemela hata pale ambapo kuna ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani.
Mheshimiwa Spika, mtandao wa ujangili ni mkubwa sana kwani upo katika uuaji, usafirishaji, masoko, polisi, TRA na mahakama. Uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya mahakimu wa mahakama za wilaya katika mikoa ya Mara, Simiyu, Shinyanga na Kigoma ni sehemu ya mtandao huo kwani watuhumiwa wengi wanaokamatwa na nyara zikiwemo silaha hupewa dhamana na hawarudi mahakamani. Mfano, mtuhumiwa aliyekamatwa kwa tuhuma za kuwinda faru, nyani na ngiri ndani ya hifadhi ya serengeti mwaka 2010, madubu Masunga Dusara (33) mkazi wa Ng'walali haonekani mahakamani baada ya hakimu mkazi wa mahakama ya shinyanga, Lydia Ilunda kumpa dhamana kwa masharti nafuu.
Kambi rasmi ya upinzani inaitaka serikali itoe taarifa kwanini wale waliotajwa katika ripoti ya ujangili wameweza kupewa nafasi kubwa ya uongozi wa nchi hii? Biashara ya pembe za ndovu inamilikiwa na nani? Usafirishaji wa pembe hizo na nyaraka nyingine unaratibiwa na magenge gani katika bandari na viwanja vya ndege? Ni kwa kiasi gani vyombo vya serikali kama jeshi la Polisi, usalama wa taifa na mamlaka ya mapato nchini (TRA) vinahusika?
Mheshimiwa Spika, Mwezi Disemba shehena yenye tani 1.3 ya meno ya Tembo iliyofichwa kwenye magunia ya Alizeti ilikamatwa na Maafisa wa Forodha wa HongKong, Shehena hii ilikuwa na thamani ya dola za kimarekani milioni moja na nusu, pia wiki mbili kabla ya hapo takribani tani nne za meno ya Tembo zilikamatwa huko huko HongKong,Kwa matukio haya mawili, hawa ni sawa na Tembo 900 waliouwawa.
Mheshimiwa Spika, Pia katika mwezi Desemba 2012 Polisi mkoani Arusha walikamata nyara nyingi za Serikali katika eneo la Kisongo, zikiwemo ngozi za Simba na wanyama wengine, pembe za ndovu na wanyama wengine na vichwa vya wanyama. Nyara hizi zilikuwa tayari kwa kuuzwa nje ya Nchi, vivyo hivyo mkoani Katavi walikamatwa majangili kadhaa na kuachiwa huru kwa amri kutoka juu kwa mujibu wa taarifa za maafisa wa wanyama pori.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya upinzani bungeni katika mjadala wa makadirio ya bajeti ya mwaka 2012/2013 ilizungumza sana juu ya hali tete iliyopo katika usalama wa wanyamapori kwa ushahidi wa kutosha ili kuweza kuisaidia serikali katika kulinda rasilimali asiri ya wanyamapori kambi rasmi ya upinzani ilichoambulia kwa serikali ni kubezwa na kudhalilishwa na sio kupokea maoni yetu na kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika,Itakumbukwa mwaka 2009 meli ya kampuni ya Sharaf Shipping Agency inayomilikiwa na Abdurahamani Kinana ambae ni katibu mkuu wa CCM ilikamatwa nchini China ikiwa na shehena ya nyara za serikali ikisafirisha makontena ya nyara za serikali kuelekea hong kong, sakata la kukamatwa kwa nyara hizo za serikali zilizosafirishwa na kampuni ya Sharaf Shipping Agency ilithibitika kuwa hati ya kusafirisha makontena hayo mawili yaliyokuwa yamesheheni pembe za ndovu ilisainiwa na mfanyakazi mwenye asili ya India wa kampuni hiyo Samir Hemani,Nyaraka zote zilionyesha kuwa kilichokuwa ndani ni plastiki zilizorudufiwa, wakati baada ya makontena kukamatwa, walikuta yamesheheni pembe za ndovu.
Mheshimiwa Spika,Taarifa zilionesha kibali cha kusafirishwa kontena hilo kilisainiwa 13 Novemba 2008 na Meneja wa Fedha na Utawala wa Kampuni hiyo,wakati Hemani anasaini nyaraka hizo, kibali chake cha kuishi nchini tayari kilikuwa kimeshaisha muda wake,Kibali cha Hemani kiliisha 7 Mei 2008.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni pamoja na juhudi zake kutoa ushauri ni vema sasa watanzania wakatambua kuwa vitendo hivi si tu kuwa vinalenga kupoteza rasilimali za taifa na kuwatajirisha viongozi walio madarakani, bali ni mkakati unaotekelezwa na serikali kuendesha shughuli za ujangili na ndio maana imekuwa ni vigumu kwa serikali kuchukua hatua dhidi ya mitandao ya ujangili ambayo inaendeshwa na viongozi kama hawa ndani ya Chama Cha Mapinduzi na serikali.
Mheshimiwa Spika, wakati hivi karibuni nchini Kenya watetezi wa hifadhi waliishinikiza serikali kuanzisha sheria kali dhidi ya ujangili ili kuwepo na adhabu stahiki, pili idara ya wanyamapori ya kenya (KWS) na wahifadhi maliasili kutangaza teknolojia mpya ambayo itasaidia kupambana na ujangili kam ilivyotangazwa na Daily Nations ya tarehe 26 March 2013, na tatu serikali ya Kenya kuongeza askari zaidi ya 1,000 ili kukabiliana na ujangili, haya yote yakifanyika Kenya kukabiliana na ujangili, Serikali ya Tanzania inaendelea kujikita kupiga vijembe kwa chama cha demokrasia na maendeleo na kuendelea kulinda majangili ambao taarifa zao zimekuwa zikizifikia mamlaka zilizo chini ya serikali.
Mheshimiwa Spika, kambi rasmi ya upinzani bungeni inapenda kutoa rai kwa serikali, pamoja na kejeli na udhalilishaji kwa kambi yetu ya kuashiria kuwa na chuki ya wazi na CHADEMA, hili halina tija kwa wananchi waliowachagua, ni vema wakarejea kuwa na uzalendo kwa nchi yetu na kuona umuhimu wa kulinda rasilimali zetu na kuwafanya watanzania wanufaike na rasilimali hizo.
Mheshimiwa Spika, tafiti mbalimbali zinaonesha wazi juu ya ulegevu wa utekelezaji wa sheria na adhabu kwa watuhumiwa wa ujangili, kutokana na kutokuwepo kwa uwajaibikaji katika sekta ya wanyamapori imepelekera kuongezeka kwa kasi ya vitendo vya ujangili nchini na kupelekea kuendelea kupungua kwa baadhi ya wanyamapori katika mbuga za taifa.
Mheshimiwa Spika, kutokana na taarifa za kanzidata ya mfumo wa taarifa za biashara ya tembo, Elephant Trade Information System (ETIS) kwa kipindi cha mwaka 2002 hadi 2012 Tanzania katika matukio ya kukamatwa kwa shehena za pembe za ndovu kwa matukio 23 sawa na asilimia 28% ya shehena zote kubwa duniani, kwa takwimu hizo imethibitika kuwepo mauaji ya tembo 24,000 kwa shehena zilizokamatwa za pembe za ndovu, hivyo Tanzania kuwa ni nchi inayotoa pembe za ndovu kwa wingi duniani.
Mheshimkiwa Spika,kwa mwaka 2012 tu shehena zilizokamatwa nchini Hong Kong zenye uzito wa kilo 1,330 pia kwa mfululizo kuwepo kwa shehena zilizokamatwa kwa nyakati tofauti nchini Vietnam kilo 6,232 mwezi March 2009 na 2005. 6 mwezi August, pia nchini Ufilipino (Philippines) kilo 3,346, mwaka 2011, Malaysia, na nchi nyingine duniani, kwa matukio haya baadhi na kutokuwepo kwa hatua zozote zinazochukuliwa ni dahahiri Dola imekuwa ni mhusika mkubwa wa kulinda tatizo hili la ujangili na hivyo kuendelea kuwa na walakini na kutokuhusika kwa dola kuchochea tatizo la ujangili kuendelea kuwa kubwa.
Mheshimiwa Spika, kama nchi inapata madhara makubwa ya kiuchumi kutokana na mauaji makubwa ya tembo yanayoendela nchini hadi hivi sasa, hususani uchumi kutokua kutokana na sekta ya utalii kuathirika kimapato, pia pamoja na nchi kuwa na tatizo kubwa la ajira kwa vijana bado tatizo la ujangili linakweza zaidi tatizo la ajira kwa kuondoa fursa za vijana kuingia katika shughuli za utalii wa tembo kutokana na kutoweka kwa kivutio hicho kwa watalii.
Mheshimiwa Spika, ni matarajio hasi kwa nchi kwa takribani miaka saba ijayo Tanzania itakuwa na historia ya kuwa na akiba ya tembo, ikiwa tafiti za mwenendo wa mauaji ya tembo kuonesha kukua na kuashiria mauaji kufikia 10,950 kwa mwaka huu wa 2013, ni dhahiri juhudi za kutokomeza ujangili zilizopo zitatufikisha mwaka 2020 tukiwa hatuna akiba ya tembo tena.
Mheshimiwa Spika, tunaposema kuwa serikali inakumbatia majangili tunamaanisha kuwa, ikiwa mtu ambaye taasisi za kiitelijensia za kimataifa zimemtaja kama jangili wa kimataifa na kisha hapa nchini kupewa vitalu vya uwindaji inatoa tafsri gani? Hivi karibuni taasisi ya Envronmental Investigation Agency ilimtamja Ndugu Shein ambaye aliwahi pia aliwahi kuwa mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM kama jangili wa kimataifa ambaye anajishughulisha na biashara na mtandao wa pembe za ndovu. Ni jambo linalojulikana kuwa jangili huyo yupo karibu na baadhi ya viongozi wakuu na waandamizi wa serikali ya CCM.
Mheshimiwa Spika, hatua ya Katibu Mkuu wa CCM Abdurahiman Kinana kuwa na kukiri ni wakala wa meli zilizo kamatwa zinasafirisha pembe za ndovu zinaashiria jinsi gani mtandao huu unahusisha vigogo wakubwa wakiwemo wa Chama Cha Mapinduzi. Serikali itoe tamko kuwa imechukua hatua gani dhidi ya mmiliki wa meli hiyo kwani taasisi ya Enviromental Investigation Agency katika uchunguzi ulibaini mtandao mkubwa wa majangili huhusisha pia wasafirishaji wa pembe za ndovu ambao hujua njia za panya kuweza kufikisha pembe hizo kwenye masoko ya Asia.
Mheshimiwa Spika, kambi rasmi ya upinzani bungeni inapenda kutoa rai kwa serikali kama ilivyotoa katika hotuba ya bajeti ya mwaka jana, kwamba kuna haja ya kuangalia upya mfumo mzima wa ulinzi wa wanyamapori kama kweli serikali inayo nia ya dhati ya kukabiliana na taizo la ujangili nchini.
Kwanza Mheshimiwa Spika, kabla ya kuanza kuchukua hatua dhidi ya tatizo la ujangili kwa nia ya kizalendo kwa nchi, ni vema sasa serikali ikaanza kujitathmini yenyewe na viongozi ndani ya serikali na chama cha mapinduzi juu ya tuhuma zilizopo kwa viongozi wake kuhusishwa na ujangili ili kuweza kutoka nje kwa ujasili kushughulikia tatizo hilo baada ya kuwajibisha viongozi wahusika na kuacha watendaji na viongozi safi ndani ya serikali na chama watakao shughulikia pasipo haya.
Mheshimiwa Spika, piakambi rasmi ya upinzani bungeni inaitaka serikali kuona umuhimu wa kurejea sheria ya adhabu kwa kosa la ujangili na kuifanyia marekebisho na kuweza kuongeza adhabu ili kudhibiti tatizo la ujangili ambao umekuwa ukiendelea kutokana na adhabu ndogo zilizopo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni pia inaitaka serikali kushirikisha wadau wa ulinzi hususani jeshi la Wananchi (JWTZ) kushiriki katika ulinzi wa wanyamapori kutokana na mamlaka za hifadhi na jeshi la polisi kuzidiwa nguvu na mitandao ya ujangili ambayo imekuwa ikitumia silaha kubwa za kivita katika shughuli za ujangili.
SEKTA NDOGO YA MISITU
Mheshimiwa Spika, mwanamazingira mmoja duniani aliwahi kusema hivi, naomba kunukuu,”To be poor and be without trees, is to be the most starved human being in the world”, Hakuishia hapo na akasema tena “To be poor and have trees, is to be completely rich in ways that money can never buy” mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika, tatizo la uharibifu wa misitu bado limeendelea kuwepo nchini na kuathiri juhudi za utunzaji wa misitu nchini, itakimbukwa mnamo tarehe imezungumzwa ndani ya bunge hili kuwa magogo yamekuwa yakisafirishwa nje ya nchi kupitia bandari ya Dar es Salaam katika maswali kwa mawaziri huku tatizo la madawati kwa wanaunzi likiwa halijapata suluhu,swali linakuja je pamoja na majibu ya waziri kuwa serikali imekwisha piga maruku usafirishaji wa magogo nje ya nchi ni sahihi kuwa hali iliyopo sasa inathibitisha utekelezaji wa katazo la serikali?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani haihitaji kujua nani alitoa taarifa zilizo sahihi kati ya mbunge na waziri, lakini jambo kubwa hapa ni kusimamia sera na taratibu rasmi za serikali katika kulinda misitu nchini, itakumbukwa kuwa takwimu zinaonesha kuwa ni asilimia 4 tuu ya misitu yetu ambayo huvunwa kwa vibali halali na asilimia 96 ni kwa njia isiyo halali.
Mheshimiwa Spika, kutokana na ubadhirifu huo katika sekta ya misitu serikali inakosa mapato yatokanayo na uvunaji wa misitu, pia wananchi wa pembezoni mwa misitu wanashindwa kujikwamua katika umaskini, kwa kurejea taarifa ya shirika la mazingira la TRAFFIC ya mwaka 2007 ilitoa takwimu zilizoonesha hasara inayoipata serikali kwa mwaka kutokana na biashara haramu ya misitu ikiwa ni shilingi bilioni 75, pamoja na kuonesha hasara hiyo ya mapato ya serikali pia ilieleza uhusikaji wa viongozi wa serikali katika ubadhirifu huo.
Mheshimiwa Spika, kambi rasmi ya upinzani bungeni inaitaka serikali kuona umuhimu wa misitu katika kukuza uchumi na kuwaondoa wananchi katika wimbi la umaskini, hivyo kuweka kipaumbele katika swala la usimamizi wa misitu iliyopo.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na nguvu hadi wakati huu. Napenda kushukuru viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo kwa msaada mkubwa ambao wamekuwa wakinipatia katika kutekeleza majukumu yangu ya kibunge na uwaziri kivuli wa maliasili na utalii. Napenda kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Iringa mjini kwa kunipa nguvu, msaada na ushirikiano tangu wanichague niwe Mbunge wao hadi wakati huu. Nawaambia kwamba nawapenda na nitaendelea kuwatumikia kadri ya uwezo wangu wote.
Mwisho lakini kwa umuhimu mkubwa ni kwa familia yangu, kwa uvumilivu mkubwa kwa kipindi chote ninachokuwa sipo nyumbani.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani naomba kuwasilisha.
______________________________ _______
Mchungaji Peter Msigwa (Mb) Iringa Mjini
Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani
Wizara ya maliasili na Utalii
Chanzo:Mtandao wa kijamii wa CHADEMA.
No comments:
Post a Comment