KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amesema kuwa Spika wa Bunge, Anne Makinda analiendesha Bunge kidikteta.
Alisema
vurugu na ghasia zinazotokea bungeni wakati wa mijadala mbalimbali
zinatokana na spika na naibu wake Job Ndugai kutaka kuliendesha Bunge
kidikteta kwa maslahi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mbowe ambaye
pia ni Mbunge wa Hai alitoa kauli hiyo jana kupinga uamuzi wa spika wa
kuridhia adhabu iliyotolewa na Ndugai dhidi ya wabunge sita wa CHADEMA.
Wabunge hao
ambao walitolewa bungeni na kuzuiliwa kuhudhuria Bunge kwa siku tano ni
Tundu Lissu (Singida Mashariki), Godbless Lema (Arusha Mjini), Joseph
Mbilinyi (Mbeya Mjini), Highness Kiwia (Ilemela), Ezekiel Wenje
(Nyamagana) na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini).
Awali
akisoma uamuzi wake jana bungeni kufuatia mwongozo alioombwa na Mbowe,
Spika Makinda alisema uamuzi uliofanywa na naibu wake, Ndugai ni sahihi.
Ndugai
aliamuru Lissu atolewe nje kwa kukiuka kanuni ya 60 (12) wakati
aking’ang’ania kutoa mwongozo wakati naibu spika akimzuia.
Makinda
alisema adhabu hiyo ilitokana na kukaidi agizo la kiti la kumtaka kukaa
wakati alipompatia nafasi Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Kiwanga
(CHADEMA).
Alisema
wabunge wengine watano walipewa adhabu hiyo kwa kosa la kuwazuia wapambe
wa Bunge kutekeleza agizo la naibu spika la kutaka kumtoa nje Lissu na
kusababisha fujo.
“Waheshimiwa
wabunge, kanuni zetu na hasa ya 2 (2) na kanuni ya 5(1) ya kanuni za
Bunge imempa mamlaka spika kufanya uamuzi pale ambapo hakuna utaratibu
wa kanuni.
“Aidha
uamuzi unaofanywa na spika ambao unaruhusu uendeshaji bora wa shughuli
za Bunge wa kuleta amani na utulivu bungeni, unaingizwa kwenye kitabu
cha maamuzi ili kuongoza mwenendo wa baadaye wa uendeshaji wa Bunge.
“Kwa kitendo
kilichotokea Aprili 17 bungeni, hakiwezi kupuuzwa kwa kuwa ni kitendo
dhahiri cha kudhalilisha mamlaka ya spika na kilikuwa kitendo cha utovu
wa nidhamu wa hali ya juu. Watanzania wote waliushuhudia na wanalaani
kilichokuwa kinaendelea ukumbini,” alisema Makinda.
Alifafanua kuwa mbunge yeyote aliyekuwa anaongoza Bunge wakati huo, angeweza kutoa uamuzi huo.
“Ninatumia
kanuni ya 5(1) na kanuni ya 2 (2) ya Bunge inayompa mamlaka spika
kufanya maamuzi ambapo jambo ama shughuli yoyote haikuwekewa masharti
katika kanuni hizi.
“Uamuzi
uliofanywa na mheshimiwa Job Ndugai, naibu spika wa kuwatoa nje
Mheshimiwa Tundu Lissu…na kubaki nje kwa kutohudhuria vikao vya Bunge
siku tano ni halali,” alisema na kuongeza:
“Na sasa utaingizwa katika kitabu cha maamuzi ya spika, na mbunge yeyote atakayefanya vitendo hivi apewe adhabu hii.”
Kauli ya Mbowe
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini hapa mara baada ya uamuzi wa Spika Makinda,
Mbowe alisema kama kiti cha spika hakitakuwa tayari kusimamia haki,
wabunge wa CHADEMA hawataacha kusimama kuomba utaratibu wa kuzungumza
kupinga hoja za upotoshaji za mawaziri na wabunge wa CCM na uendeshaji
mbovu wa Bunge.
Alisema
kanuni ya 2(2) na kanuni ya 5(1) ya kanuni za Bunge kweli inampa mamlaka
spika kufanya uamuzi pale ambapo hakuna utaratibu wa kanuni.
“Kosa la
wabunge wetu adhabu yake iko kwenye kanuni. Kanuni aliyotumia inahusu
kwa mfano, wewe mwandishi wa habari umetoka sehemu yako, ukaingia ndani
ya ukumbi wa Bunge na kuanza kupigana.
“Hapo hakuna
kanuni ya kukuadhibu na ndiyo spika anaweza kutumia hiyo kanuni na
kisha kuingiza kwenye kumbukumbu ili iweze kutumika baadaye, lakini sio
katika kosa la wabunge wetu,” alisema Mbowe.
Alisema uamuzi wa spika ni wa kitoto kwani amezidi kukoroga kanuni kwa ajili ya kumlinda naibu wake.
“Hatutangazi
vita na Bunge, lakini kama Bunge halitakubali kufuata haki, wategemee
hali hii kuendelea kujitokeza kwani hatutaogopa kufukuzwa kwa kupigania
haki,” alisema.
Alisema
Lissu alipata adhabu ya kutolewa nje na kufungiwa vikao vitano kwa
sababu alisimama mara nyingi kuomba mwongozo na kutoa ufafanuzi wa hoja
za kupotosha.
“Lissu au
mbunge mwingine yeyote atasimama hata zaidi ya mara 100 kuomba
kuzungumza, na tunafanya hivyo kutokana na wingi wa hoja za hovyo za
serikali na wabunge wa CCM, na hakuna kanuni inayozuia kuzungumza mara
nyingi, na katika hilo tuko tayari kufukuzwa wote,” alisema.
Mbowe
alirejea kauli aliyoitoa juzi wakati akiomba mwongozo kuwa kilichotokea
bungeni ni sintofahamu kati ya wabunge na kiti cha spika ambapo katika
mambo ya msingi, CHADEMA ilitegemea kifungu cha nne cha kanuni za Bunge,
kifungu kidogo cha kwanza kingetumika.
“Kifungu
hicho kinasema hivi: ‘Spika anaweza kutaja jina la mbunge kwamba
amedharau mamlaka ya spika na kisha kupeleka jina hilo kwenye Kamati ya
Haki na Maadili ya Bunge, ikiwa;
Kwa maneno
au vitendo, mbunge huyo anaonesha dharau kwa spika au mbunge huyo
atafanya kitendo chochote cha makusudi cha kudharau shughuli ya Bunge au
mbunge yeyote anayeongoza shughuli hiyo’.
“Kosa la
wabunge wetu linaangukia kwenye kanuni hii kwamba wameonyesha dharau
pale walipokaidi kutoka nje. Kanuni iko wazi kwamba spika atapeleka
majina ya wabunge hao kwenye Kamati ya Haki na Maadili ya Bunge ambako
watapewa nafasi ya kusikilizwa na kutoa ushahidi kabla ya kuhukumiwa,”
alisema.
Mbowe
alieleza kushangazwa na hukumu hiyo kwani hakuna mbunge wala kiongozi
yeyote wa CHADEMA aliyeitwa kusikilizwa, na hata uamuzi wa spika nao
haukuzingatia kuwahoji wahusika.
Aliitaka
jamii kujiuliza kwanini wabunge hao wanapokutana nje ya Bunge ni
marafiki wa karibu, lakini wakiingia ndani ya Bunge vurugu za kurushiana
maneno hujitokeza.
“Huwezi
kukuta wabunge nje wanagombana kwa sababu wanaheshimiana. Ndani ya Bunge
chanzo cha hao wanaopatana nje kurushiana maneno ni kiti cha spika
kushindwa kusimamia haki na kanuni,” alisema.
Hatua za kuchukua
Pamoja na
Spika Makinda kuridhia adhabu ya Ndugai dhidi ya wabunge wa CHADEMA,
Mbowe alisema wanatarajia kukata rufaa kwenye Kamati ya Kanuni kupinga
uamuzi wa spika.
Alisema anajua CHADEMA itashindwa katika kesi hiyo, lakini wanataka kuweka rekodi na kumbukumbu kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Alisema Spika Makinda kama ilivyokuwa kwa Ndugai, amekosea kuridhia adhabu hiyo.
Katika hatua
nyingine, Mbowe alisema kuwa Bunge limenajisiwa kwa kuruhusu watu
wasiotakiwa kikanuni kuingia bungeni kiholela kwa nia ya kutaka kumtoa
Lissu.
Akifafanua,
alisema kisheria wanaoruhusiwa kuingia bungeni ni wabunge, uongozi wa
Bunge na watumishi wao, na kama kuna mtu mwingine anataka kuingia lazima
kanuni itenguliwe.
“Ukiacha
rais ambaye ni sehemu ya mbunge, mtu yeyote haruhusiwi kuingia bila
kutengua kanuni. Juzi Ndugai alivunja kanuni kwa kuruhusu askari kuingia
bungeni wakati siwa iko mbele na hadi sasa hakuna taarifa iliyotolewa,”
alisema.
Chanzo,Mtandao wa kijamii wa CHADEMA .
No comments:
Post a Comment