Mch.Peter Msigwa akichangia bungeni Dodoma. |
Kama
alivyofanya mwaka jana na hata kwenye mikutano yake mingi ya hadhara,
Msigwa alimtaja tena Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, na mkewe,
kwamba anamiliki kampuni ya Sharaf Shipping Co, Ltd ambayo meli yake
inadaiwa kunaswa na kontena la shehena ya meno ya tembo.
Hata hivyo,
hotuba ya Msigwa ilikatizwa kwa mwongozo wa mbunge wa Viti Maalumu, Anna
Abdallah (CCM), akihoji kitendo cha mbunge mwenzake kudai ofisi ya
Spika ni kaburi la kuzika haki. Hata hivyo Spika Anna Makinda aliwataka
wawe wavumilivu kwani yako maneno mengine mengi kama hayo.
Hata hivyo
Msigwa aliendelea kusoma maoni ya kambi ya upinzani kuhusu makadirio ya
matumizi na mapato ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha
wa 2013/14.
Huku wabunge
wa CCM wakimwangalia kwa makini na wengine kutikisa vichwa kumpinga,
Msigwa alimtaja mfanyabiashara na kada wa CCM, Mohsin Abdallah.
Msigwa
ambaye alikuwa akikariri taarifa ya kamati ya waziri wa zamani wa wizara
hiyo, Antony Diallo, aliwataja makada waandamizi wengine wa CCM wenye
maslahi ya aina hii kuwa ni kampuni ya Coastal Wilderness (Tz) Ltd.,
ambayo wakurugenzi wake wanatajwa kuwa ni Napono Edward Moringe Sokoine
na Namelok Edward Moringe Sokoine; Enzagi Safaris (Tz) Ltd., yenye
wakurugenzi Makongoro Nyerere, Muhamed Seif Khatib na Saidi Kawawa; na
Hunting Safaris yenye wakurugenzi, Chande Kawawa na Hassan Kawawa.
Kampuni zingine ni M.S.K. Tours & Hunting Safari Co. ya Muhamed Seif Khatib.
Msigwa
alisema mengi ya makampuni haya yalipewa vitalu vya uwindaji wakati
hayana uzoefu wala mtaji wa kuendesha biashara ya uwindaji wa kitalii
katika vitalu hivyo.
Alisema
matokeo yake ni kwamba makampuni hayo yalishindwa kusimamia uhifadhi wa
wanyamapori katika vitalu vyao na kusababisha tatizo la ujangili
kushamiri katika vitalu hivyo.
Bofya Read more kuendelea.
“Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kutoa kauli mbele ya Bunge lako
tukufu ni kwa nini serikali hii ya CCM imekuwa ikitoa vitalu vya
uwindaji wa kitalii kwa makada waandamizi wa CCM ambao wanajulikana kuwa
hawana weledi wala uwezo wa kibiashara wa kuendesha biashara ya
uwindaji wa kitalii na hivyo kusababisha tatizo la ujangili kuwa kubwa
zaidi na kuleta hasara kwa taifa letu!” alisema.
Akiwa
amerejea bungeni baada ya adhabu ya siku tano, Msingwa alisema serikali
imeanza kufedheheshwa katika mikutano ya kimataifa ya uhifadhi kwa
sababu CCM imeamua kukumbatia makada wake waandamizi aliodai
wanajihusisha na ujangili.
Alitolea
mfano Mkutano wa 16 wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Biashara ya
Kimataifa ya Wanyama Walio Hatarini Kutoweka (CITES) uliofanyika
Bangkok, nchini Thailand mwezi uliopita.
“Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni fedheha ya aina gani kimataifa
itakayoiamsha serikali hii ya CCM katika usingizi wake wa pono ili iweze
kuchukua hatua za kisheria dhidi ya makada wa CCM wa aina hii?”alihoji
Msigwa.
Kuhusu
Kinana, Msigwa alisema kampuni yake ya wakala wa meli ya Sharaf Shipping
Co. Ltd, si tu kwamba imehusishwa na usafirishaji haramu wa pembe za
ndovu kutoka Tanzania bali pia inadaiwa kutoa ajira haramu kwa wageni.
Alisema
wakati shehena ya meno hayo ya tembo inakamatwa nchini Vietnam, nyaraka
zilizoambatana na shehena hiyo zilionyesha kwamba kibali cha kusafirisha
shehena hiyo kilisainiwa na raia wa India anayeitwa Samir Hemani mnamo
Novemba 13, 2008.
Alisema
wakati raia huyo wa kigeni anasaini kibali cha kusafirisha shehena ya
meno ya tembo kwa niaba ya wateja wa Kinana na mkewe, kibali chake cha
kuishi Tanzania kilikuwa kimeisha tangu Mei 7, 2008.
Msigwa
alimshambulia Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, na
kumtaka ajiuzulu kwa madai kuwa ameshindwa kulinda rasilimali za nchi
na kusababisha wanyamapori kutoweka kwa kuuawa na majangili.
Alimshambulia
pia Spika Anna Makinda kuwa Bunge lake limekuwa kaburi la kuzikia
utekelezaji wa maazimio mengi kuhusu kashfa mbalimbali zilizogubika
utendaji wa Ofisi ya Waziri wa Maliasili na Utalii na utekelezaji wa
majukumu yake kisheria.
Nchimbi ajibu mapigo
Hoja za
Msigwa zilimlazimu Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi,
kuomba nafasi ya kwanza kuchangia hotuba ya Waziri Kagaeshiki na hivyo
kutumia muda huo kurusha makombora mazito kwa CHADEMA kwa kuwaita kuwa
ni genge la uongo ndani ya Bunge.
“Kabla
sijaendelea, nitumie nafasi hii kuipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii
kwa kazi nzuri na katika hotuba hii ya Waziri Kagasheki imejidhihirisha
wazi kwa kipindi hiki kifupi kuwa wamekamata watuhumiwa wa ujangili 354
na zipo mahakamani kesi 283, bunduki 435 zimekamatwa.
“Ukiona mtu anasimama na kusema serikali haijafanya kazi, basi upeo wake wa kufikiri ni mdogo,” alisema Nchimbi.
Waziri huyo
alijielekeza kwenye baadhi ya hoja zilizolengwa dhidi ya Kinana ambapo
alisema Msigwa ameamua kusema uongo ili kulipotosha Bunge na Watanzania
kwa ujumla kwamba katibu huyo alikamatwa na meno ya tembo nje.
“Nimejaribu
kufuatilia kwa umakini kujua kwamba kifungu hicho alikimaanisha,
alikielewa, alikitafakari au aliandikiwa tu kisha akaenda kukisoma.
“Baada ya kutafakari kwa kina nimegundua kwamba hakuwa na nia mbaya bali alikuwa ameandikiwa tu na kuisoma,” alisema.
Nchimbi alitumia muda huo kufafanua majumu ya kati ya Shipping Agency na Clearing and Fowarding.
“Kampuni ya
shipping agency duniani kote ni kumwakilisha mwenye meli, agenti hawezi
kuwa mwenye meli ila anamwakilisha mwenye meli, kuna shughuli mbalimbali
zinazofanyika kwenye meli.
“Kuna mambo
ya kuhudumia watumishi kwenye meli, kuwapelekea chakula watumishi,
kufanya usafi, kupelekea mahitaji muhimu lakini wapo watu wanaofanya
‘clearing and fowarding’ na Kiswahili chake ni kupeleka na kutoa.
“Hawa ndio
wanaopeleka mizigo bandarini na kule ndiko kuna utaratibu wa upekuzi kwa
hiyo huko hahusiki mtu wa shipping agency, sina mashaka hata kidogo
kuwa Mchungaji Msigwa analijua hili ila amelifumbia macho kwa makusudi
na kwa maslahi yasiyokubalika kwa taifa,” alisema.
Wakati
akiendelea kuchangia, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu
(CHADEMA), aliomba mwongozo wa Spika kutaka kutoa ufafanuzi, lakini
Spika alikataa.
“Mliposema
ninyi, wenzenu walinyamaza, mtulie hivyo hivyo, naomba uendelee hakuna
cha taarifa, endelea Mheshimiwa Nchimbi na nyie mnanyamaza kama
walivyonyamaza wenzenu,” alisema Makinda.
Nchimbi
aliendelea kusema kumekuwepo uvumi ambao unafanywa kwa Kinana
kwamba anamiliki meli iliyotumika kusafirisha pembe za ndovu.
Alisema
baada ya uchunguzi wa kutosha kuhusu kesi hii, ikabainika na watuhumiwa
wakashtakiwa kwa uhujumu uchumi kwa kufunguliwa kesi namba 3 na 4 ya
mwaka 2006.
Nchimbi aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Eradius Tesha, Shaban Abura, Eric, Issa Abubakar na Omar Hussein.
“Mh Spika,
hawa ndiyo waliopelekwa mahakamani na uchunguzi ulijidhihirisha kuwa
hawa ndiyo watuhumiwa wa kesi hiyo na kambi ya upinzani inalijua hili,”
alisema.
Alisema
wakati kesi iko Kisutu, ulihitajika ushahidi kutoka nchi ya Vietnam na
nchi hiyo imesema haina ushirikiano na Tanzania katika mambo ya jinai.
“Hivi sasa
tunazungumza na ubalozi wa China watupe kibali cha kufanya upelelezi ili
kesi hiyo iweze kuendelea na kwa msingi huo Mahakama ya Kisutu inataka
ushahidi huo ili kesi iendelee na hili wapinzani wanalijua,” alisema.
Source: CHADEMA social media.
No comments:
Post a Comment