Monday, November 26, 2012

KUNGURU WEUSI KUANGAMIZWA MOROGORO



KUNGURU WEUSI KUANGAMIZWA MOROGORO 
Ni mikakati mizuri iliyowekwa na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kuangamiza kunguru weusi katika mikoa ya Pwani.
Hawa ndege ni wasumbufu sana hasa upande wa jikoni kiasi kwamba ukizubaa tu chakula unachopika mnakigawana.
 




 Nimefurahi kuona tangazo la serilaki la kuwaangamiza hawa kunguru weusi Mjini Morogoro,naona tutapumua wakazi wa Morogoro.
 


 Na tangazo la serikali ni hili hapa.

KUNGURU WEUSI KUANGAMIZWA MOROGORO


Wizara ya Maliasili na Utalii itaendesha zoezi la kuwaangamiza Kunguru Weusi katika Manispaa ya Morogoro kuanzia tarehe 16 Novemba hadi 15 Desemba 2012.
Kunguru weusi watauwawa kwa kutumia sumu tulivu aina ya DRC 1339 ambayo haina madhara makubwa kwa binadamu. Hata hivyo tahadhari inatolewa kuwa watoto wasichezee mizoga ya kunguru iliyoanguka barabarani na mitaani.
Wananchi wametakiwa kutoa ushirikiano kwa kikosi kazi kinachoendesha zoezi hilo kwa kutoa taarifa kuhusu maeneo yenye idadi kubwa ya Kunguru weusi. Aidha, taarifa zitolewe endapo mizoga ya kunguru itaonekana katika makazi ya watu na barabarani.
Lengo la operesheni hii ni kupunguza idadi ya kunguru weusi ambao wanasababisha kero na adha kwa wananchi katika makazi yao. Pia kunguru hao wamekuwa wakiua viumbe wa asili wakiwemo ndege pamoja na kueneza vimelea vya magonjwa kama vile kuhara na mdondo kwa kuku.
Zoezi hili ambalo limeshafanyika katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga litaendeshwa Morogoro kwa mara ya mwisho kabla ya kurudi tena Dar es Salaam kukamilisha zoezi katika sehemu ambazo zitakuwa na kunguru weusi waliosalia.
Kuanzia mwezi Julai 2010 hadi Oktoba 2012 Jumla ya kunguru weusi 856,831 wameshauawa kwa kutumia sumu hiyo ya DRC 1339 na mitego katika Jiji la Dar es salaam, Pwani na Tanga.
Katika Manispaa ya Morogoro taarifa kuhusu Kunguru Weusi zitolewe katika ofisi za Maliasili, pamoja na kupiga simu kwa: Meneja mradi – 0754498957 au 0716129120 na Mtaalamu wa sumu – 0757 – 585358.              
George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
16 Novemba 2012
Simu: 0784 468047

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...