Monday, June 3, 2013

MAPENDEKEZO YA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA HAYA HAPA.

Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini Tanzania, imependekeza wawepo wagombea huru katika ngazi za uchaguzi mbalimbali . Hayo ni miongoni mwa mapendekezo yaliyotangazwa jijini Dar es salaam na Mwenyeketi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba wakati wa uzinduzi wa Rasimu ya Kwanza ya Katiba Mpya.
Jaji Warioba amesema pia wapo wananchi waliopendekeza kwamba, wagombea huru waruhusiwe kugombea nafasi zote isipokuwa nafasi ya urais. Jaji Warioba amesema tume ilipitia maoni hayo na kupendekeza kwamba, wagombea huru waruhusiwe kugombea nafasi zote kuanzia ngazi ya Mwenyekiti wa Mtaa hadi nafasi ya Urais.
Kadhalika Jaji Warioba amesema, Tume pia imependekeza kwamba, mgombea yeyote wa Urais ili athibitike kuwa ni mshindi atalazimika kupata zaidi ya asilimia hamsini ya kura, na kwamba endapo mgombea hatafanikiwa kupata asilimia hamsini uchaguzi utarudiwa kwa kuangalia wagombea wawili waliopata kura nyingi.
Mapendekezo mengine yaliyotangazwa na Tume ni pamoja na kuwepo kwa serikali tatu yaani ya Bara,Zanzibar na ile ya Muungano.
Pia tume imependekeza kuwa, Bunge la Muungano liwe na jumla ya Wabunge 75, hamsini kutoka Bara, ishirini kutoka visiwani na watano wateuliwe na Rais kutoka makundi maalum ya walemavu.
Mapendekezo mengine ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni pamoja na Rais kubakia na madaraka yake ya uteuzi wa viongozi wa ngazi za juu, lakini uteuzi wa ngazi za chini uachiwe Tume ya Utumishi.
Imeeleza kwamba, Rais mara baada ya kufanya uteuzi wa viongozi wa ngazi za juu wakiwemo, mawaziri, manaibu waziri, jaji mkuu na naibu jaji mkuu, viongozi hao watalazimika kuthibitishwa na Bunge.

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...