Wednesday, June 19, 2013

MAHAKAMA YA RUFAA YATAKA MAJALADA YA LWAKATARE.

Mahakama ya Rufaa imeagiza  kupelekwa majalada yote ya kesi inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare na mwenzake Lodvick Joseph.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na shitaka la kula njama kutaka kumnywesha sumu Mhariri wa Gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky.
Kwa Mujibu wa Msajili wa Mahakama Kuu, Projest Kahyoza, amepokea amri ya Mahakama ya Rufani kuitisha jalada la Lwakatare lililopo Mahakama Kuu pamoja na Kisutu na kuunganishwa kwa pamoja na kupelekwa mahakamani hapo.
 
Hatua hiyo imefuatia Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) kuwasilisha ombi la marejeo ya kutaka kuitishwa majalada ya kesi hiyo ili kuona uhalali wa uamuzi wa Mahakama Kuu wa kumfutia mashitaka ya ugaidi Lwakatare. 
 
Machi 8, mwaka huu, Lwakatare na mwenzake walipandishwa kizimbani mahakamani hapo na kusomewa mashitaka manne likiwemo la ugaidi.
 
Hata hivyo, Mei 8, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilimfutia Lwakatare mashtaka matatu ya ugaidi yaliyokuwa yanamkabili na kubakiwa na shitaka moja la kula njama kumnywesha sumu Msacky.
 
Uamuzi huo ulitolewa na Jaji wa Mahakama hiyo, Lawlance Kaduri baada ya kupitia maombi yaliyowasilishwa na  Mawakili wa Lwakatare na kusema kuwa DPP hakuwa na uhalali wa kufuta kesi ya awali iliyofunguliwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Machi 18, mwaka huu na muda mfupi kuirudisha mahakamani hapo kwa hakimu mwingine.
 
Source: CHADEMA's social media.

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...