Saturday, June 29, 2013

MAELEZO YA WAKILI KIBATARA JUU YA TUHUMA ZA KIONGOZI WA CHADEMA DAR HENRY J. KILEO.


BAADA ya sintofahamu kuhusu kilichomsibu kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Mkoa wa Dar es Salaam, Henry John Kileo, utata wa Jeshi la Polisi na juhudi za mkewe Joyce Kiria kutaka kujua aliko mumewe, nimeona nitoe kile kilichotokea katika sakata hili.
Kileo alipigiwa simu na maofisa wa polisi makao makuu mnamo tarehe 17/6/2013, wakimuarifu kwamba wanataka kufanya mahojiano naye. Hawakusema ni kuhusu nini.
Mara moja akawasiliana nami kama wakili wa familia yao, nami nikawasiliana na maofisa hao kuwaarifu kwamba kwa kuwa nina majukumu kadhaa ya kimahakama, na kwa kuwa Kileo yuko nje ya mkoa, basi ninaahidi kama wakili kuhakikisha nitampeleka binafsi Makao Makuu Polisi Ijumaa ya tarehe 21/6/2013.
Tarehe 21/6/2013 tuliambatana mimi, Kileo na John Mnyika (MB) hadi Polisi Makao Makuu, kisha Mnyika alituacha na mahojiano yakaanza.
Kwa ujumla walimuhoji Kileo mambo mbalimbali kuhusiana na tukio la kumwagiwa tindikali kijana aitwaye Mussa Tesha katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga mnamo mwaka 2011.
Wakati mahojiano hayo yanafanyika, tayari kulikuwa na kesi ya jinai ikiendelea huko Igunga, mkoani Tabora ambako washitakiwa wanne ambao ni makada wa CHADEMA kutoka maeneo mbalimbali nchini walishitakiwa kama mshtakiwa nambari moja mpaka nne kuhusiana na tukio hilo la Tesha. Walishitakiwa chini ya vifungu vya sheria ya kanuni ya adhabu (Penal Code), na si ugaidi.
Baada ya mahojiano yaliyomalizika kwa Kileo kuandikisha maelezo hadi mnamo saa 11.30 hivi za jioni, polisi walimnyima dhamana, na wakampeleka rumande iliyoko Kituo Kikuu cha Polisi (Central Police Station), akalala huko.
Jumamosi ya tarehe 22/6/2013, mimi Joyce na Mnyika tulifika Kituo Kikuu cha Polisi, ambapo OCS wa hapo alituarifu kwamba amri alizonazo ni kwamba Kileo haruhusiwi kuonana na mtu yeyote.
Kama wakili, nilijadiliana masuala ya kisheria na OCS, ikalazimu kuwasiliana na maofisa wa polisi makao makuu ambao hatimaye waliniruhusu kwa mujibu wa sheria kuonana na mteja wangu.


Tukazungumza na ‘kupeana moyo’, nikahakikisha amekula chakula kilicholetwa na mkewe Joyce ambaye muda wote alikuwa akimuangalia mumewe kwa mbali tu, kwani mazungumzo yangu na Kileo yalifanyika faragha.
Mnamo saa 7.30 hivi tuliondoka sote (mimi, Joyce na Mnyika), na kukubaliana kurudi tena polisi Jumapili ya tarehe 23/6/2013 kumtembelea tena Kilewo, na pia kufahamu mipango hasa ya Jeshi la Polisi kuhusu Kileo kwani hadi tunaondoka si mimi wala mkewe aliyefahamishwa rasmi kuhusu mipango hiyo.
Nikiwa nyumbani, nilipokea simu toka kwa Joyce akiniarifu kwamba amefika Kituo Kikuu cha Polisi jioni ya Jumamosi ya tarehe 22/6/2013 na kuarifiwa tu kwa mkato kwamba Kileo "ameondoka".
Ukweli ni kwamba mkewe alikuwa amechanganyikiwa, na jukumu la kwanza lilikuwa kumtuliza kisaikoilojia kwani nilifahamu kuwa alikuwa amejifungua muda si mrefu huko nyuma;kwa hiyo hali yake ilikuwa ‘delicate’ sana kiafya na kisaikolojia.
Nikapambana kama wakili kwa kutumia uzoefu na ‘contacts’ (P.R -mawasiliano) ili kupata tarifa ya aliko mteja wangu. Niliariwa tu "off record" na maofisa wa polisi kwamba Kileo amesafirishwa kwa ndege ya Precision kuelekea Tabora kupitia Mwanza chini ya ulinzi wa maofisa waandamizi wa polisi ili kule Tabora afunguliwe kesi.
Sikuwa na mawasiliano yoyote na mteja wangu, na hizo taarifa "off record" ndiyo kitu cha pekee tulichokuwa nacho mimi, Joyce na uongozi wa CHADEMA kuhusu nini kimemsibu Kileo.
Niliendelea kupambana kupata taarifa rasmi, na hatimaye Jumapili ya tarehe 23/6/2013 majira ya saa 6 hivi mchana ndipo nilipopigiwa simu na mmoja wa maofisa waliomsindikiza Kileo kuelekea huko Tabora kwa utaratibu ule ule wa "off record", na kuniunganisha nae, ambapo nilizungumza naye kwa kifupi kumjulia hali na kumuhakikishia kwamba tutapigana kwa uwakili wetu wote kwa ajili yake.
Kwa hiyo hadi muda huo hatukuwa bado na uhakika wa asilimia mia moja kwamba Kileo yuko wapi hasa. Kwa wale mawakili wenzangu wanafahamu kwamba huwezi kutegemea taarifa za kusikilizishwa mteja kwenye simu ambazo hata si za kwake. Wala huo si ushahidi wa mahali alipo mtu huyo kisheria.
Lakini ikatubidi ku-"assume" (kisia) kwamba Kileo yuko, atapelekwa Tabora kushitakiwa. Mimi na Profesa Abdallah Safari tukaanza maandalizi ya upesi upesi ya safari kuelekea Tabora kwa gari, kwani ndege kuulekea huko ni Jumamosi na Jumatatu tu.
Tuliondoka kwa gari ya makao makuu ya CHADEMA Jumapili ya tarehe 23/6/2013, majira ya saa 11.30 hivi za jioni. Tulisafiri usiku kucha, na tulichukua "risk" ambazo kwa kawaida tusingechukua, ikiwemo kupita katika mapori maarufu kwa utekaji.
Kilichotusukuma na kutupa moyo ni kwamba Kileo yuko mahali ambapo anatuhitaji sana, na hana tumaini lingine bali sisi mawakili wake.
Tukisafiri usiku kucha na kufika Tabora asubuhi ya Jumatatu tarehe 24/6/2013, majira ya saa 2.30 tukiwa tumechoka hakuna mfano. Tukabadili mavazi upesi upesi na kuvaa suti zetu na kukimbilia Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora. Huko tuliarifiwa kuwa wao hawana taarifa zozote za Kileo. Tukaelekea Makao Makuu ya Polisi Tabora. Jibu likawa ni lile kwamba hawana habari.
Maana yake ni kwamba sisi mawakili wa Kileo, tuko Tabora ambayo ni kubwa hasa na hatujui mteja yuko wapi hasa. Nikafanya juhudi zile zile za "off record", na kufahamishwa kwamba mteja wetu alishikiliwa Kituo cha Polisi cha Nzega, umbali wa saa tatu toka Tabora, na kwamba yuko njiani kuletwa Tabora.
Hatukuwa na uhakika bado, ila ilitulazimu kushikilia hiyo taarifa isiyo rasmi, na kuendelea na maandalizi ya kesi.
Majira ya saa 9 hivi za alasiri ya tarehe 23/6/2013 Kileo akiwa chini ya ulinzi mkali sana wa FFU katika Land Cruisers mbili za polisi waliwasili Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora, akiwa hajala tangu jana yake. Alikuwa yeye na wenzake wanne ambao walikuwa wamefutiwa mashitaka kwa hati ya "Nolle Prosequi" huko Igunga, kisha kukamatwa tena mara moja na kusafirishwa kwa ulinzi mkali sana hadi Tabora.
Ukweli ni kwamba tulivyoonana na Kileo si sisi mawakili wala yeye mwenyewe aliyejizuia kulengwa na machozi; yeye akimshukuru Mungu kwamba tumepambana na yote hadi Tabaora kwa ajili yake kwa kasi vile, nasi kwamba hatimaye tumeonana na mteja wetu.
Tukaingia mahakamani, Kileo na wenzake wakasomewa mashitaka mawili; moja chini ya sheria ya kuzuia ugaidi kwamba walimteka kwa nia ya ugaidi Mussa Tesha huko Igunga, Tabora na la pili kwamba walimdhuru kwa kummwagia tindikali.
Makosa ya ugaidi
Mawakili tulipambana na kutoa hoja za kisheria nne dhidi ya uhalali wa mashitaka yenyewe na utaratibu wa kufungua kesi husika. Tumeoiomba mahakama kufuta mashitaka ya ugaidi, au la iamuru kila mshitakiwa arudishwe kushitakiwa mahali alikokamatwa; mfano Kileo, Dar es Salaam.
Kabla ya kuondoka Tabora, tulipita kumuaga Kileo na wenzake katika gereza la Uyui. Wote wako na kombati zao za chama chao, na wako imara, hasa baada ya kuona mawakili wako imara. Cha msingi ni kuomba Mungu aipe mahakama ujasiri wakati wa kutoa maamuzi hapo Julai 8, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...