Saturday, June 29, 2013

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUKANUSHA BAADHI YA MATANGAZO KATIKA MITANDAO YA KIJAMII.

Katibu wa Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi wakati akizungumza na wandishi wa Habari Ofisini kwake kuhusu maswala mbalimbali ya Ofisi yake. Kulia kwake ni Naibu Katibu Idara ya Ajira Bw. Lucas Mrumapili.

 

Taarifa ya Kukanusha Baadhi ya Matangazo katika Mitandao ya Kijamii

Ndugu Wandishi wa Habari, kwanza niwashukuru kwa kuitikia wito, nimewaita hapa kwa mambo mawili.
Awali ya yote nianze kwa kuwapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya katika kuelimisha umma  juu ya masuala mbalimbali yakiwemo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii licha ya changamoto mbalimbali mnazokumbana nazo katika utekelezaji wa majukumu yenu.

Baada ya kusema hayo, nianze kueleza nilichowaitia hapa nikitambua umuhimu  wa nafasi yenu katika jamii hususan katika kuelimisha umma kupitia vyombo vyenu.   Moja ya kazi za msingi za taasisi yetu kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ni kutangaza nafasi wazi za Ajira kwa mujibu wa mahitaji.

Napenda kutoa rai kupitia  kwenu na kwa wadau wetu wote watambue kuwa ni kosa kwa mtu au taasisi yoyote kuchukua matangazo ya Sekretarieti ya Ajira bila idhini na kuyafanyia marekebisho.  Vile vile ni kosa kwa mujibu wa sheria kuandaa  matangazo mbalimbali yanayohusiana na Mchakato wa Ajira katika Utumishi wa Umma kwa lengo la kupotosha umma ilhali wakijua wazi kuwa taarifa hizo wanazozichapisha au kuziandika katika baadhi ya mitandao ya kijamii siyo halali na hazijatolewa na Sekretarieti ya Ajira.

Sote tunajua kuwa suala la Ajira ni nyeti  na linavuta hisia za watu wengi.  Nimefikia hatua ya kutoa tamko hili kutokana na baadhi ya taarifa zinazohusu Mchakato wa Ajira katika Utumishi wa Umma hususan matangazo ya nafasi za kazi yaliyoko katika baadhi ya mitandao ya kijamii yakionyesha kuwa Katibu wa Sekretarieti ya Ajira ndiye  ametoa matangazo hayo kitu ambacho siyo kweli.  Miongoni mwa matangazo hayo ya kughushi na yenye nia ya kupotosha umma ni yale yaliyoko katika tovuti inayojulikana kwa www.eastafricajobscareer.com.
Tovuti hii imetoa matangazo yenye kichwa cha habari kinachosomeka “Kazi Utumishi Julai 2013 jobs in Tanzania” ambalo linaonyesha ”Mwisho wa kupokea barua za maombi ni tarehe 14 Julai, 2013” na lingine ni lenye kichwa cha habari  kinachosomeka  “Kazi Utumishi August 2013 Jobs in Tanzania” ambalo “Mwisho wa kupokea barua za maombi ni tarehe 10 Agosti, 2013” Pamoja na mengine.  Huu ni upotoshaji mkubwa kwa kuwa matangazo hayo yanasababisha usumbufu mkubwa kwa umma.

Ni vyema wananchi wote wakafahamu kuwa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ndicho chombo pekee kilichoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Na.8 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na.18 ya mwaka 2007 Kifungu 29(1), pamoja na marekebisho yaliyofanyika katika Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 1998 Toleo Na.2 la mwaka 2008 ambapo katika Vifungu Na.4.6 na 6.6 vya Sera hiyo vimetamka kuwepo kwa chombo maalum cha kushughulikia Mchakato wa masuala ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Sekretarieti ya Ajira inafahamu kuwa matangazo hayo ya kughushi yamesababisha usumbufu mkubwa kwa wadau wetu hususan waombaji wa fursa za Ajira, wengi wao wamekuwa wakiyasoma na kutuma  maombi ya kazi kupitia matangazo hayo.  Kwa kuwa baadhi ya waombaji wa fursa za Ajira hawafahamu ukweli huu ambapo walituma maombi na Sekretarieti ya Ajira haikuweza kuyashughulikia kulizua malalamiko makubwa na shutuma kwetu kuwa hawajaitwa kwenye usaili.

Nitoe rai kwa wadau wote wanaotafuta fursa za Ajira katika Utumishi wa Umma pindi wanapoona matangazo yanayohusu Ajira Serikalini katika vyombo mbalimbali vya habari, ikiwemo mitandao ya kijamii wajaribu kujiridhisha kwa kuthibitisha taarifa hizo kama ni za kweli kwa kutembelea tovuti ya Sekretarieti ya Ajira ambayo ni www.ajira.go.tz kwa taarifa sahihi au kupiga simu namba 255-687624975 ili kupata ufafanuzi zaidi.

Aidha, naomba kuufahamisha umma kuwa Sekretarieti ya Ajira haiwajibiki na wala haitawajibika kwa taarifa ama matangazo yanayohusu  Mchakato wa Ajira katika Utumishi wa yaliyotolewa kwa njia ya udanganyifu na mitandao hiyo ya kijamii kama www.eastafricajobscareer.com.  Nawataka wale wote wanaoendelea kutoa matangazo hayo ya uongo/kughushi yenye lengo la kupotosha umma ilhali wakijua matangazo hayo si ya kweli kuacha mara moja kwani tutakapombaini mhusika ama taasisi yenye kumiliki chombo hicho cha habari ama mtandao huo wa kijamii hatutasita kuwachukulia hatua za kisheria.

Nitoe taarifa  kwa umma pia kuwa Sekretarieti ya Ajira kama chombo cha Serikali kinaendeshwa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu.  Aidha, matangazo ya ajira yanayotolewa na chombo chetu, yanatolewa kwenye magazeti au tovuti ya Sekretarieti ya Ajira au nyingine za Serikali ambazo hutanguliwa na majadiliano na makubaliano na taasisi husika kabla ya kutoa tangazo.

Pili, baada ya kusema hayo niongelee kidogo kuhusu mchakato wa usaili wa tangazo la kazi lililotolewa tarehe 26 Machi, 2013 kwa lugha ya Kiswahili kwa Kada mbalimbali ambalo usaili wake unatarajiwa kufanyika muda wowote kuanzia mwezi Julai, 2013.  Napenda niwafahamishe wale wote ambao walituma maombi yao kuwa ratiba na majina ya waliokidhi vigezo yatatolewa katika mtandao wa Sekretarieti ya Ajira wiki ya kwanza ya mwezi Julai, 2013, hivyo watembelee mtandao wetu wakati huo ili kufahamu sehemu na siku ya usaili husika maana baadhi ya saili hizo zitaendeshwa mikoani kwa wale wote waliotumia anuani za mikoani hususan kada za chini ambazo siyo za Maofisa.

Mwisho, nawataka waombaji  kazi Serikalini kutambua kuwa fursa za Ajira ni za ushindani unaozingatia sifa na uwezo wa mwombaji, maana wahitimu hivi sasa ni wengi kuliko miaka ya nyuma, na wanahitajika  watumishi wenye uwezo wa kitaaluma na kiutendaji  katika kuwahudumia Watanzania kwa ufanisi zaidi, hivyo ni vyema kwa wahitimu wanapoomba nafasi za kazi wasome tangazo na kulielewa ili waweze kuzingatia vigezo na masharti yaliyowekwa na pindi wanapoitwa kwenye usaili wawe wamejiandaa vya kutosha ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata Ajira husika.

Nimalizie kwa kuwashukuru nyote  kwa  kunisikiliza.
Ahsanteni sana.

Imetolewa 27 Juni, 2013

Katibu,

Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma
Barua pepe: katibu@ajira.go.tz Tovuti:  www.ajira.go.tz
Kwa maelezo zaidi: wasiliana na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kwa barua pepe: gcu@ajira.go.tz, www.facebook.com/sekretarieti ya ajira au Simu: 255-687624975

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...