Friday, July 19, 2013

TAMKO LA WAZIRI KIVULI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI MHE. VINCENT JOSEPHAT NYERERE (MB) KUHUSU UDHAIFU WA SERIKALI KATIKA KUKOMESHA BIASHARA HARAMU YA MADAWA YA KULEVYA NCHINI.

 
Ndugu wanahabari, kwanza kabisa napenda kuwashukuru kwa kuitikia wito wangu, ili niweze kuzungumza na watanzania kupitia kwenu kuhusu hatari kubwa inayolikumba taifa ya madawa ya kulevya.

Biashara haramu ya dawa za kulevya imekua kwa kasi sana hapa nchini miaka ya hivi karibuni licha ya kuwa na vyombo lukuki vya ulinzi na usalama na licha ya kuwa na Tume maalumu ya kudhibiti madawa ya kulevya chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda, iliyosomwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera Uratibu na Bunge Mhe. Wiliam Lukuvi tarehe 26 Juni, 2013 siku ya maadhimisho ya kitaifa ya kupiga vita dawa za kulevya huko Dodoma ni kwamba katika kipindi cha mwaka 2008 hadi 2012 watuhumiwa 10,799 walikamatwa kwa kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya hapa nchini. Aidha, watanzania wapatao 240 walikamatwa na madawa ya kulevya katika nchi za Brazil, Pakistan na Afrika ya kusini na hivyo kutia doa taswira ya Tanzania katika jumuiya ya kimataifa. Kutokana na kukithiri kwa biashara hii haramu, Serikali kupitia maadhimisho hayo ya siku ya kupiga vita madawa ya kulevya duniani ilitangaza kuwa biashara ya dawa za kulevya kuwa ni janga la taifa. 

Mtakumbuka pia kwamba hivi majuzi, muda mfupi baada ya Serikali kutangaza kuwa biashara ya dawa za kulevya ni janga la taifa , walikamatwa wasichana wawili ambao ni watanzania huko Afrika ya kusini wakiwa na kilo 150 za madawa ya kulevya yenye thamani ya zaidi ya randi milioni 42.6 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 6 za kitanzania.

Ndugu wanahabari, matukio yote haya yametokea ndani ya kipindi cha miaka sita tu ya utawala wa Serikali ya awamu ya nne ambapo kuna viongozi wa juu Serikalini ambao waliwahi kusema kuwa wanawajua watu wanaojishughulisha na biashara haramu ya dawa za kulevya lakini mpaka sasa hawajawataja wahusika na wala hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi ya wahusika.

Ndugu wana habari, miongoni mwa viongozi wa serikali na taasisi nyingine waliosema kuwa wanawafahamu wafanya biashara ya madawa ya kulevya ni:-

Rais Jakaya Kikwete, ambaye alipiga hatua kubwa zaidi na kusema anawajua hata viongozi wa dini wanaofanya biashara hiyo. Licha ya maaskofu na viongozi wengine wa dini kumtaka Rais awataje wahusika hao wa madawa ya kulevya ili kuuweka ukweli wazi, Rais hajafanya hivyo mpaka sasa.

Kamishna wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya: huyu alisema anayo majina ya vigogo (kwa maana ya viongozi) wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya lakini hajaweka majina hayo hadharani na wala haijulikani kama wahusika hao wamechukuliwa hatua yoyote hadi sasa.

Mbunge wa Mwibara – Kange Lugola alisema katika bunge la bajeti 2013/2014 kuwa kama Rais na Kamishna wa tume ya kudhibiti dawa za kulevya wanawajua “kwa majina” watu wanaojihusisha na biashara za dawa za kulevya na hawataki kuwataja watu hao wala kuwachulia hatu yamkini watu hao ni miongoni mwa mawaziri ndio maana kuna kigugumizi cha kuwataja na kuwachukulia hatua. Tangu Mhe. Kange Lugola alihusishe baraza la Mawaziri na kashfa hiyo ya kuhusika na biashara ya dawa za kulevya hakuna hatua yoyote ilivyochuliwa na Serikali kuthibitisha au kubatilisha kauli hiyo.

Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Bw. Reginald Mengi aliwahi kutoa taarifa ya wazi kuwa kuna kundi la matajiri wanaoshirikiana na viongozi wa Jeshi la Polisi waliokuwa wanapanga njama za kumwekea mtoto wake dawa za kulevya ili wambambikizie kesi ya dawa za kulevya na hivyo kuchafua heshima ya Bw. Mengi na familia yake. Ndugu mengi alisisitiza katika taarifa yake kwamba yuko tayari kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi na mamlaka nyingine zinazohusika ili kubaini njama hizo na kuchukua hatua stahiki kwa wahusika lakini mpaka leo Ndugu Mengi hakuhojiwa ili kuthibitisha kauli yake jambo linaloashiria kwamba kuna ukweli katika kauli yake.

Baada ya matukio yote haya na baada ya Serikali kukaa kimya kuhusu matukio hayo, mimi kama Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi na kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ninatoa tamko kama ifuatavyo:

Rais Jakaya Mrisho Kikwete awataje na kuwachukulia hatua watu aliosema anawafahamu wanaojishughulisha na biashara ya dawa za kulevya la sivyo akubali kubeba shutuma kwamba Serikali yake ndio Mratibu Mkuu wa biashara ya dawa za kulevya ndio maana anashindwa kuchukua hatua.

Kamishana wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya awajibike kwa kutoa maelezo kwa umma juu ya hatua alizochukua dhidi ya wahusika wa biashara ya dawa za kulevya aloiosema anawafahamu la sivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni italazimika kuwashawishi wananchi kuamini kwamba yamkini na yeye yumo katika mtandao wa wafanya biashara haramu ya dawa za kulevya ndio maana anasita kuwachukulia hatua wahusika hao ambao alishakiri kuwa anawafahamu. 

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege awajibike kwa kutoa maelezo kwa umma kuwa ni tatizo gani linaloikabili mamlaka yake hadi kufanya viwanja vya ndege vya Tanzania kuwa ndio njia rahisi ya kuingiza na kusafirishia madawa ya kulevya katika ukanda wa Afrika Mashariki?

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini na Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi wawajibike kwa kutoa maelezo kwa umma kuwa ni kazi ipi wanayofanya ikiwa madawa ya kulevya yanaingizwa nchini na kusafirishwa nje ya nchi kwa kasi kubwa zaidi?

HITIMISHO: Ni vema kama taifa tukatambua madhara ya madawa ya kulevya kwa vijana wetu ambao ndio nguvu kazi ya taifa. Kupuuzia na kutochukua hatua kwa wahusika wa dawa za kulevya ni kuangamiza nguvu kazi ya taifa. Nguvu kazi ya taifa ikishaharibiwa na dawa za kulevya hatuna taifa tena. Hivyo Serikali ifahamu kwamba kuendelea kulifumbia macho jambo hili kwa manufaa ya mafisadi wachache ni kulihujumu taifa na huo ni usaliti dhidi ya kiapo ilichokula cha kulitumikia taifa na kusimamia usitawi wa wananchi wa Tanzania. Aidha, Serikali itambue pia kwamba kuendelea kukaa kimya bila kuchukua hatua yoyote juu ya jambo hili kunatoa dalili kwamba yamkini ya yenyewe inahusika na biashara hiyo.

MUHIMU: IKIWA SERIKALI ITAENDELEA KUPUUZIA JAMBO HILI AMBALO LINALIANGAMIZA TAIFA, BASI KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI ITAENDESHA OPERESHENI NCHI NZIMA ILI WANANCHI WAPIGE KURA KWA WAHUSIKA WAKUU WA BIASHARA YA DAWA ZA KULEVYA, NA BAADA YA ZOEZI HILO, TUTAANIKA HADHARANI (KWA KUWATAJA MAJINA) WAHUSIKA WA BIASHARA HARAMU YA DAWA ZA KULEVYA.

MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
NA WAZIRI KIVULI WA MABO YA NDANI YA NCHI
Imetolewa leo, tarehe 16 Julai, 2013
 
Source: CHADEMA Social Media.

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...