CHAMA cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetishia kuuanika hadharani ushahidi
unaothibitisha polisi kuhusika na mlipuko wa bomu uliotokea katika
mkutano wa kufunga kampeni za udiwani mwezi uliopita na kuua watu wanne
mkoani Arusha, huku kikiamua kuanzisha kambi za mafunzo kwa vijana nchi
nzima kwa ajili ya kuwalinda viongozi wao.
CHADEMA
imesema itauanika hadharani ushahidi huo iwapo Rais Jakaya Kikwete
atakataa kuunda tume ya kimahakama itakayokuwa na jukumu la kusikiliza
shauri hilo.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CHADEMA,
Freeman Mbowe, alisema kikao cha dharura cha Kamati Kuu, kilichoketi
kwa siku mbili jijini humo kimejadili masuala mbalimbali ya kitaifa
ikiwemo siasa, rasimu ya katiba mpya na uanzishaji wa kambi za mafunzo
ya vijana.
Alisema
CHADEMA hawapo tayari kuwasilisha ushahidi wao kwa polisi ambao ndio
watuhumiwa wakuu, bali wanataka Rais Kikwete aunde tume huru ya
kimahakama.
Alisema isipoundwa tume hiyo ya kimahakama, watauweka wazi ushahidi huo kwa wananchi wakati ukifika.
Mbowe
alisema watausambaza ushahidi huo kwa vyama, mashirika ya kiraia ya haki
za binadamu ndani na nje ya nchi pamoja na ofisi za kibalozi za mataifa
rafiki na Tanzania pamoja na jumuiya ya kimataifa.
Alisema
lengo la kufanya hivyo ni kuwataka waishinikize serikali kuunda tume
huru ya kimahakama kuchunguza tukio hilo na mengine yanayofanana na hayo
juu ya mauaji ya kisiasa.
Aliongeza
kuwa serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi, Sera (Uratibu na Bunge)
William Lukuvi imetoa kauli isiyostahili ndani ya Bunge kuwa CHADEMA
wamejilipua kwa ajili ya kutafuta umaarufu.
“Tunalaani
kauli ya serikali kupitia kwa Lukuvi, ni ya kitoto, kijinga na ya
kiuendawazimu. Sisi hatuwezi kutafuta umaarufu kupitia damu za
Watanzania.
“Kama
umaarufu unatufikia kwa kazi tuzifanyazo kwa ajili ya wananchi, serikali
inatafuta pa kushikia baada ya polisi kuhusishwa,” alisema Mbowe.
Alisema ni
jambo la kusikitisha kuona Lukuvi akiwakilisha serikali na kujinadi kuwa
CHADEMA wanahusika na mlipuko pasipo kuuweka hadharani kwa lengo la
kukomesha hatua hiyo.
Mbowe
alisema mlipuko wa bomu uliotokea Arusha katika mkutano wa CHADEMA mwezi
uliopita, umetoa somo kwa chama hicho na sasa wameamua kuanzisha kambi
za mafunzo kwa vijana.
Alibainisha
kambi hizo zitatoa mafunzo kwa vijana ambao watatumika kuwalinda
viongozi wa CHADEMA katika shughuli za kichama na kitaifa.
Mbowe
alisema Jeshi la Polisi limeshindwa kuchukua hatua stahiki kuwalinda
viongozi wa vyama vya siasa, hivyo Kamati Kuu ya CHADEMA imeamua kutoa
mafunzo ya kujilinda.
Alibainisha
kuwa sababu ya kuanzishwa kwa makambi ya ukakamavu ni kwa ajili ya
kuwalinda viongozi wa CHADEMA kwakuwa polisi wameshindwa kufanya kazi
hiyo au wanafuata maelekezo ya viongozi wa CCM.
Alisema
vikundi vya ulinzi vya CCM kwa kushirikiana na wakuu wa wilaya na polisi
wamekuwa wakiendesha zoezi la kuwadhuru wafuasi wa CHADEMA kwa kuwakata
mapanga, kuwachoma visu au kuwapiga marungu pasipo kuchukuliwa kwa
hatua yoyote.
“Tunaonewa
sisi, tunashitaki sisi na tunakamatwa sisi, na sasa kama chama tunasema
hii inatosha. Ni lazima tutafute njia mbadala ya kujilinda, tutakuwa ni
wajinga kuendelea kupiga magoti na kulia,” alisema Mbowe.
Kiongozi
huyo alisema CHADEMA kimewaagiza vijana wa chama hicho waliopo sehemu
mbalimbali nchini kujitokeza kwa wingi ili wapatiwe mafunzo maalumu ya
ukakamavu kwa ajili ya kuwalinda viongozi wao.
“Mafunzo
haya yatatolewa katika kambi maalumu zitakazokuwepo katika mikoa yote
nchini…, kitengo cha ulinzi ndicho kitakachoratibu jambo hili,” alisema.
Msemaji wa
Jeshi la Polisi, Advera Senso akizungumzia mikakati hiyo ya Chedema,
alisema kuwa jeshi hilo lipo kwa ajili ya watu wote, hivyo mtu akienda
kinyume na kuvunja sheria lazima atachukuliwa hatua.
“Nasema
sheria itachukua hatua, polisi ipo na kazi zote zinakwenda vizuri hilo
ndiyo jukumu la msingi la jeshi, nina hakika jeshi ni imara, Watanzania
wote wapo salama,” alisema.
Alisema
jeshi lilianzisha ulinzi shirikishi kwa lengo la kuhakikisha kila
mwananchi anajilinda na kumlinda jirani yake, hivyo sheria za nchi zipo
wazi na majeshi yote yanaanzishwa kwa mujibu wa sheria.
Mlipuko wa Arusha
Mbowe
alisema baada ya kutokea mlipuko wa bomu katika mkutano wa mwisho wa
kampeni ya chama hicho mkoani Arusha na kuua watu wanne na wengine 70
kujeruhiwa, CHADEMA ilitoa tamko kuwa viongozi wake ndio walilengwa
katika shambulio hilo.
Alibainisha
kuwa viongozi wa CHADEMA akiwamo yeye na mbunge wa Arusha Mjini,
Godbless Lema ni miongoni mwa watu waliokuwapo siku ya kufunga kampeni
hizo za udiwani.
Alisema
katika tamko walilotoa walibainisha ushiriki wa moja kwa moja wa Jeshi
la Polisi juu ya mlipuko huo, na kwamba Kamati Kuu imeridhia tamko hilo
baada ya kuelezwa ushahidi uliopo.
Kutokana na
ushahidi huo, Mbowe alisema chama chao kimefedheheshwa na kauli ya
serikali bungeni iliyolenga kulisafisha Jeshi la Polisi kutohusika.
Alibainisha
kuwa serikali inafanya jitihada za makusudi kulihusisha tukio hilo na
CHADEMA wakati inajua polisi ndio waliotenda uovu huo.
“Tunashangazwa
na kitendo cha serikali kupuuza maafa yaliyowafika wananchi wa Arusha.
Nyote mnafahamu rais wetu ni mtu makini katika kuhudhuria misiba na
majanga mbalimbali, lakini katika hili hata kauli ya kutoa pole
haijatoka utadhani waliopata kadhia hiyo si Watanzania,” alisema Mbowe.
Alisema
Bunge ambalo ni taasisi ya kuwawakilisha wananchi lilishindwa kuchukua
nafasi yake ya kusimamisha kwa muda shughuli zake au kutuma wawakilishi
katika tukio hilo na badala yake viongozi wa serikali wamekuwa wakitoa
kauli zenye utata.
Alisema
Kamati Kuu imelitaka Bunge, kuueleza umma kama tukio la kulipuliwa bomu
kwenye mkutano wa CHADEMA, ni tofauti na mengine kama yale ya mlipuko
uliotokea kanisani Olasiti, mabomu Gongo la Mboto au kuzama kwa meli ya
Mv Skargit.
Aliongeza
pia kuwa Kamati Kuu, imelaani vitendo vya fujo, kushambuliwa, kukatwa
mapanga kuchomwa visu na kulipuliwa kwa mabomu viongozi wa CHADEMA.
Alibainisha kuwa licha ya matukio hayo, Jeshi la Polisi limeshindwa kuchukua hatua stahiki kwa watu waliohusika.
Rasimu ya katiba
Mbowe
alisema Kamati Kuu ya CHADEMA, imetambua kazi kubwa iliyofanywa na Tume
ya Mabadiliko ya Katiba katika kukusanya, kuchambua maoni ya wananchi na
kuandaa rasimu.
Alibainisha
kuwa CHADEMA imetambua na kuainisha mapendekezo mengine ya msingi ambayo
yanastahili kuboreshwa zaidi katika rasimu hiyo.
Alisema
msimamo na maazimio ya Kamati Kuu, juu ya rasimu ya katiba mpya
yameainishwa na kuchapishwa katika kitabu maalumu watakachokizindua
katika mkutano wa hadhara watakaoufanya wakati wowote kuanzia sasa.
CC yasikitishwa na Mtwara
Alisema
Kamati Kuu imesikitishwa na hali ya sasa kwa wananchi wa Mtwara
wanaopata madhila makubwa kutokana na vipigo wanavyopata kutoka kwa
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi (JWTZ) huku
serikali ikikaa kimya juu ya hali hiyo.
Aliongeza
kuwa wananchi wa Mtwara kwa sasa wanateswa na kiu yao ya kutaka kujua
watanufaika vipi na gesi inayotoka katika mkoa wao, hali iliyowaingiza
katika kadhia ya kubakwa, kupigwa na hata kuifanya Mtwara ionekane kama
mkoa unaotawaliwa na jeshi.
Alisema hali
hiyo ni hatari kwa mustakabali wa taifa, hasa katika kuhifadhi
demokrasia kwa kile alichoeleza kuwa nguvu ya jeshi inaweza kusambaa
katika mikoa yote na kulifanya Jeshi la Polisi lisiwe na kazi ya kufanya
au nchi kutokuwa na utawala wa kidemokrasia.
Chanzo: CHADEMA Social Media.
No comments:
Post a Comment