Friday, July 19, 2013

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KAULI YA CCM JUU YA KODI YA KUMILIKI KADI YA SIMU YA MKONONI/KIGANJANI.

Taarifa iliyotolewa na CCM na kunukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari tarehe 18 Julai 2013 ya kuitaka Serikali inayoongozwa na CCM kuangalia njia nyingine mbadala ya kukusanya kodi na kuachana na hatua yake ya kukusanya kodi ya umiliki wa kadi ya sh. 1000 kila mwezi imethibitisha maneno ya Mwalimu Nyerere kwamba ‘chama lege lege huzaa serikali legelege’.

Aidha, taarifa hiyo ni mkakati legelege wa kujinasua katika malalamiko, kukusanywa kwa saini, kuandaliwa kwa miswada ya sheria, migomo ya kuzima simu kwa muda maalum na maandamano dhidi ya Serikali ya CCM kutokana na chama hicho kushindwa kuwa na sera sahihi na mikakati makini. 

Taarifa hiyo haiwezi kurudisha nyuma hatua ya wananchi kukikataa chama hicho na kuunga mkono mabadiliko ya kweli kupitia CHADEMA kwa kuzingatia kuwa CCM imeshindwa kuhakikisha kwamba Ilani zake za uchaguzi ya mwaka 2005 na 2010 zinatekelezwa. Ikumbukwe kwamba kupitia ilani hizo CCM iliahidi maisha bora kwa kila mtanzania na badala yake maisha ya wananchi yamezidi kuwa magumu kutokana na ongezeko la bei na gharama za maisha.

Ili taarifa hiyo isiwe maneno matupu, Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM ajitokeze na kuagiza utozaji wa kodi hiyo usitishwe kuanzia sasa. Izingatiwe kwamba Muswada huo ambao Rais aliusaini mwanzoni mwa mwezi Julai ulianzisha pia ushuru mwingine na tozo zingine mbalimbali zenye kuongezea mzigo wa gharama za maisha wananchi hususan wa kipato cha chini badala ya kuweka mkazo katika kupanua wigo wa vyanzo mbadala nchini. 

Kadhalika, kwa kuwa chanzo cha hali hiyo ni maamuzi yaliyofanywa katika Mkutano wa kumi na moja wa Bunge uliopitisha Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2013; ufumbuzi lazima uhusishe marekebisho ya sheria kufuta makosa yaliyofanywa na Serikali ya CCM na kupigiwa kura ya ndio na Bunge lililohodhiwa na CCM.

Hivyo, Rais Kikwete awasilishe katika mkutano wa Bunge kwa hati ya dharura muswada wa sheria wa kufuta vifungu vilivyoingizwa kwa marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147 na kuondoa ushuru wa bidhaa kwa kadi za simu (sim card) kwa wamiliki wa simu za kiganjani/mkononi.

Taarifa hiyo isipoambatana na hatua za Rais Kikwete kuagiza Mamlaka ya Mapato (TRA) kuacha kutoza ushuru huo na Rais kuwasilisha muswada bungeni kupitia Waziri wa Fedha itakuwa ‘kiini macho’ kama ilivyokuwa taarifa nyingine kama hiyo iliyotolewa na msemaji huyu huyu wa CCM mwaka 2011.

Taarifa ya Nape Nnauye inapaswa kupuuzwa kwa kuwa alitoa taarifa nyingine kwamba CCM kupitia kikao cha kamati kuu yake Agosti 2011 ‘imeagiza’ Serikali ‘kutafuta njia ya kushusha bei ya mafuta ya taa’ iliyopanda baada ya kuongeza kodi ya mafuta ya taa. 

Badala ya agizo hilo kutekelezwa mafuta ya taa yaliendelea kupanda bei na kinyume na agizo hilo katika mkutano wa 11 wa Bunge mwaka 2013 Serikali hiyo hiyo ya CCM ikawasilisha bungeni muswada wa sheria ya fedha na majedwali ya marekebisho ya kuongeza kodi ya mafuta ya taa kinyume cha agizo hilo.

Taarifa hiyo haiwezi kuinasua CCM dhidi ya kuendelea kukataliwa kwa kuwa imehusika katika maaandalizi ya bajeti ya Serikali na muswada wa sheria ya fedha kabla na wakati wa mkutano wa Bunge uliofanya maamuzi ya kuwaongezea gharama za maisha wananchi. Chama hicho kimeshiriki moja kwa moja kupitia vikao vyake vya kikatiba ikiwemo kamati kuu, sekretariati na kamati ya wabunge wa chama hicho.

Taarifa hiyo imethibitisha madhara ya Serikali ya CCM na wabunge wanaotokana na chama hicho wanavyoshindwa kusimamia maslahi ya umma kwa kuwa iwapo dhamira hiyo ingekuwepo katika hatua za awali wasingewasilisha bungeni mapendekezo hayo. Hata baada ya kuyawasilisha wangeyaondoa katika hatua zote kufuatia kodi hiyo kupingwa na kambi rasmi ya upinzani inayoongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

CCM itambue kwamba wananchi wanakumbuka kuwa kodi hiyo ya simu iliingizwa kwa mara ya kwanza ndani ya ukumbi wa Bunge na Rais kupitia kwa Waziri wa Fedha aliposoma bajeti ya Serikali ya CCM. Ilikuwepo kwenye Hotuba ya maandishi ya Waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa CCM lakini wakati wa kusoma akaruka sehemu hiyo na kutangaza kwamba imefutwa. 

CCM ieleze katika hatua hiyo, wazo hilo lilitoka kwa nani mpaka likaingia katika kitabu cha hotuba ya Waziri na nini maamuzi ya Baraza la Mawaziri ambalo Mwenyekiti ni Rais (ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM) kwenye kikao kilichofanyika siku moja kabla ya yeye kusoma hotuba yake kilichojadili hatua za kikodi (tax measures).

Kifungu hiki kilirejeshwa kwa mara nyingine tena kwenye Muswada wa Sheria ya Fedha kupitia jedwali la Marekebisho lililowasilishwa na Waziri wa Fedha mwenyewe kwa niaba ya Serikali ya CCM na Bunge lenye kuhodhiwa na CCM likakipitisha. CCM iwapo ilikuwa na msimamo wa kuona kwamba kodi hiyo ni mzigo kwa wananchi kwanini haikuwasiliana na wabunge wake ambao ndio wengi katika Bunge kuhakisha kwamba wanaikataa.

Iwapo CCM haitajitokeza kutoa majibu na Rais hataagiza kwamba kodi hiyo isitishwe na muswada kuwasilishwa bungeni kuifuta, natoa mwito kwa wananchi kujitokeza katika mkutano wa hadhara nitakaoshiriki tarehe 21 Julai 2013 katika Uwanja wa Sahara kata ya Mabibo kuanzia saa 8 Mchana mpaka saa 11 Jioni.

Mkutano huo uliandaliwa kwa lengo la kutoa mrejesho kuhusu yaliyojiri bungeni katika mkutano uliopita na kupokea masuala ya kuyawasilisha katika mkutano ujao. Aidha, uchambuzi utafanyika kuhusu rasimu ya katiba sanjari na juu ya mchakato wa katiba mpya. 

Hivyo, kupitia mkutano huo saini zitaendelea kukusanywa kwa ajili ya kutaka kodi hiyo ya kumiliki kadi za simu isitishwe na muswada kupelekwa bungeni kuifuta kodi hiyo yenye kuongeza gharama za maisha kwa wananchi na kuathiri haki ya kupata na kutoa taarifa pamoja na uhuru wa mawasiliano. 

Taarifa hiyo imedhihirisha namna ambavyo tumefika hapa tulipo kutokana na udhaifu wa Serikali ya CCM, uzembe wa Bunge (ambalo limehodhiwa na CCM) na ulegelege wa CCM. 

Hivyo, umma uipuuze na kuendelea kuchukua hatua za kuiunga mkono CHADEMA katika dhamira na dhima yake ya kuleta uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganizesheni thabiti kwa maendeleo endelevu ya Tanzania.

Imetolewa tarehe 18 Julai 2013 na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
Chanzo: CHADEMA Social Media.

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...