Tuesday, July 23, 2013

WATU 9 WAUAWA NCHINI MISRI.


Watu tisa wameuawa mjini Cairo, Misri katika makabiliano yaliyodumu usiku kucha kati ya wafuasi na wapinzani wa rais aliyengo'lewa mamlakani Mohammed Morsi.
Maafisa wanasema kuwa , ghasia zilitokea wakati wa maandamano yaliyofanywa na wafuasi wa Morsi.

Familia ya Bwana Morsi imetuhumu jeshi kwa kumteka nyara kiongozi huyo wa zamani.
Rais huyo wa zamani amezuiliwa na jeshi katika sehemu isiyojulikana bila ya kufunguliwa mashtaka yoyote, tangu mkuu wa majeshi Generali Abdul Fattah al-Sisi, kutangaza kung'olewa mamlakani kwa Morsi tarehe 3 Julai.
Chama cha Bwana Morsi cha Muslim Brotherhood kimekataa kutambua serikali ya kijeshi huku kikifanya maandamano karibu kila siku kote nchini Misri.
Ghasia hizo zimesababisha vifo vya zaidi ya watu 60 tangu kuondolewa mamlakani kwa Morsi.
Siku ya Jumatatu mtu mmoja alifariki na wengine wengi wakijeruhiwa wakati wa maandamano mjini Cairo, kwa mujibu wa maafisa wa afya.
Televisheni ya taifa iliripoti kuwa wafuasi wa Morsi waliokuwa wanaandamana walikamatwa kwa umiliki haramu wa silaha.
Vifo zaidi vimeripotiwa katika makabiliano mengine tofauti katika mkoa wa Qalyubiya Kaskazini mwa Cairo.
Wakati huohuo, familia ya Morsi ilisema hawajawasiliana kamwe na Morsi, na ikathibitisha kuwa wanaitaka mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita kuanzisha uchunguzi juu ya kupinduliwa kwake.
Nchi kadhaa ikiwemo Marekani zimetaka Morsi aachiliwe.
Lakini maafisa wa kijeshi wanasisitiza kuwa anazuiliwa katika eneo salama.

Source: BBC

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...