Monday, July 8, 2013

Ndege ya Rais wa Somalia 'yashika moto'


Ndege iliyokuwa inambeba rais wa Somalia, imelazimika kutua kwa dharura mjini Mogadishu baada ya moja ya mabawa yake kushika moto.
Msemaji wa Hassan Sheikh Mohamud, alisema kuwa haijulikani kwa nini injini ya ndege ilisita kufanya kazi.
Rais Hassan Sheikh Mohamud, alielezea kuwa rais hakujeruhiwa lakini wazima moto walifanya kila hali kuzima moto huo.
Bwana Mohamud alichaguliwa kama rais wa Somalia mwaka jana katika mpango ulioungwa mkono na Umoja wa Mataifa, katika hatua za kumaliza vita vya miaka mingi.
Mwandishi wa BBC Mohamed Mwalimu, alisema kuwa magurugumu ya ndege yaliharibiwa vibaya baada ya tukio hilo.
Rais alikuwa anaelekea katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, wakati ndege hiyo ilipolazimika kurejea Mogadishu.
Moja ya ripoti zilizotolewa za mwanzo kuhusu tukio hilo, ilitoka kwa akaunti ya Twitter ya kundi la al-Shabab lakini haikusema kama imeshambulia ndege hiyo.
Wanajeshi wa Muungano wa Afrika pamoja na wale wa Somalia, wanaounga mkono bwana Mohamud wamewaondoa wapiganaji wa al-Shabab kutoka mji mkuu Mogadishu, mwaka jana ingawa kundi hilo bado hufanya mashambulizi ya mara kwa mara ya kuvizia.
Serikali mpya ni ya kwanza kwa zaidi ya miaka 10 kutambuliwa na serikali ya Marekani na shirika la fedha duniani (IMF).

source...BBC

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...