Thursday, March 28, 2013

NAIBU WAZIRI ATETEA VITI MAALUM VISIONDOLEWE

Naibu Waziri wa  Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu, ametilia shaka pendekezo la kuondolewa kwa nafasi ya Viti Maalumu Katiba Mpya.
Alisema kitendo hicho kinaweza kukwamisha malengo ya milenia  na yale ya itifaki ya jinsia na maendeleo katika  nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) ya kuwa na uwakilishi wa asilimia 50  ya wanawake  bungeni.
Naibu  waziri huyo alisema kama  nafasi hizo zitatolewa, kuna ulazima wa katiba kutamka wazi namna ambavyo itahakisha kuwa wanawake wanapata nafasi za uongozi katika ngazi zote za serikali. Alitolea mfano katiba ya Kenya ambayo inaeleza bayana namna viongozi wanawake wanavyopatikana katika nchi hiyo.
Alisema hayo katika kongamano la waandishi  wa habari na mashirika yasiyokuwa  ya kiserikali yanayojihusisha na  masuala ya kijinsia, jijini Dar es Salaam jana.
Kongamano hilo  lilikuwa na lengo la kutathimi itifaki ya  malengo 28 ya kijinsia ya Sadc ifikapo 2015.
Naibu waziri huyo aliwataka waandishi wa habari na wanaharakati, kuhakikisha kuwa masuala ya ujinsia yanafafanuliwa kwa kiasi kikubwa katika rasimu ya Katiba Mpya inayotarajiwa kuwasilishwa juni mwaka huu na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Pia aliwataka waandishi kutumia  wanawake kama vyanzo vya  habari  kwa sababu takwimu zinaonyesha  ni asilimia 21 tu wanawake ndio wanatoa sauti katika vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini.

Habari hii ni kwa hisani ya Mwananchi.

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...