Wednesday, March 20, 2013

MVUA ZASABABISHA MITAMBO YA KUSAFISHA NA KUTIBIA MAJI KUZIMWA MOROGORO

Maji yakiwa yanamwagwa eneo la kutibia maji Mafiga.
 Mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha wataalam katika kituo cha kutibu na kusafisha maji Mfiga iliyochini ya Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Morogoro (MORUWASA) kuzima mitambo na kumwaga maji yaliyokuwa yanaingia mitamboni hapo kutoka katika bwawa la Mindu kutokana na maji hayo kuwa machafu sana kwa kujaa tope.
Sampuli ya maji yaliyokuwa yanatoka bwawa la Mindu na kuja sehemu ya kutibia maji Mafiga.
 Hali hii ilizidi zaidi kutokana na mvua iliyonyesha jana jioni hadi usiku iliyoingiza tope jingi sana kwenye mdomo wa bomba la kuchukulia maji katika bwawa la Mindu.Hata hivyo wataalamu hao wamesema watawasha mitambo tu mara hali ya maji itakaporejea katika hali yake ya kawaida.
Kuzimwa kwa mitambo hiyo kumeathiri wakazi wa Maorogoro wanaotegemea chanzo cha Mindu kukosa maji ambao ni zaidi ya 70%.
Bi.Getrude Salema Afisa Uhusiano wa MORUWASA.
 Akiongea na Blogu hii Afisa Uhusiano wa MORUWASA Bi. Getrude Salema amesema hali hii ni changamoto kwa MORUWASA. Hata hivyo amewasihi wakazi wa Morogoro kuwa wawe wavumilivu na kuwa maji yatakayowafikia yatakuwa salama pale tu watakapokuwa wamewasha hiyo mitambo na kuruhusu maji yaanze kuingia na kutibiwa.
Mkondo wa maji ya mvua unaongiza tope bwawa la Mindu.
Blogu hii imefanya ziara hadi Mitambo ya kutibia maji Mafiga, Bwawa la Mindu na Sehemu ambako maji ya mvua yanavuka barabara ya Iringa na kuingia bwawa la Mindu.Kilichoonekana ni uchimbaji wa madini karibu na bwawa,mifugo kutifua ardhi pamoja na kilimo ndo sababu zilizochangia tope kuwa jingi.
Maji ya mvua yakiwa yametuama kando kando ya barabara ya Iringa eneo la Mindu
Hata hivyo,kando kando ya barabara ya Iringa kumeonekana madimbwi mengi ya maji yakiwa yametuama kutokana na makaravati yanayopitisha maji ya mvua kuziba kiasi cha kusababisha maji kukaa kwa muda mrefu na mvua zinaponyesha zinasomba hayo maji hadi bwawa la Mindu.

Wafanyakazi wa MORUWASA wakiwa wameenda kujionea halihalisi ya mikondo inayoingiza maji ya  mvua bwawani.

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...