Monday, August 19, 2013

TAMKO LA VODACOM KUHUSU KUKOSEKANA KWA HUDUMA ZA MAWASILANO NCHINI.

 
Wapendwa wateja wetu na jamii kwa ujumla;

Tunaomba radhi kwa dhati kabisa kwa kutoweza kuwapa huduma za mawasiliano za mtandao wa Vodacom kuanzia jioni ya siku ya Ijumaa Agosti 16 mpaka Jumamosi asubuhi Agosti 17, 2013....

Hali hii ilisababishwa na moto uliozuka katika jengo lenye kitovu cha kuendesha (switch) mitambo yetu lililopo Dar es Salaam . Moto huo ulipelekea kuzimika kwa mtambo wetu na kukata huduma zetu zote nchini na hivyo kuwaathiri wateja wetu wa ndani na nje ya nchi pamoja na jamii kwa ujumla.

Tunatambua na kuelewa usumbufu uliosababishwa na kukosekana kwa huduma zetu, na tunapenda kuwashukuru kwa uvumilivu na uaminifu wenu kwa Vodacom katika kipindi hiki kigumu.

Tutawarejeshea gharama za vifurushi vya bidhaa zetu hususan, muda wa maongezi, SMS na huduma za intaneti , mlivyovinunua siku ya Ijumaa Agosti 16, na ambavyo hamukuweza kuvitumia kikamilifu kutokana na kutokuwepo kwa mawasiliano. Zoezi hili litakamilika Jumatatu Agosti 19, 2013.

Ninaomba niwahakikishie wateja wetu kwamba Vodacom ina dhamira ya dhati kabisa ya kuendelea kutoa huduma zenye ubora wa hali ya juu hapa nchini.

Aidha, ninaomba pia kuwashukuru wafanyakazi na washirika wetu wote waliofanya kazi bila kuchoka ili kuhakikisha kuwa huduma zetu zinarejea katika hali yake ya kawaida kufikia asubuhi ya Agosti 17, 2013. Kwa hakika jitihada zao, kujituma kwao na utendaji kazi wao kwa bidii, vilitoa mchango mkubwa sana katika zoezi hili.

Kwa mara nyingine ninaomba niwatake radhi kwa usumbufu na kuwashukuru kwa uvumilivu wenu.

Rene Meza
Mkurugenzi Mtendaji

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...