Sunday, August 18, 2013

ALICHOKISEMA ZITTO KABWE LEO.

Katika moja ya maazimio ya Kamati za Bunge za mahesabu ya Umma (Kamati ya Hesabu za Serikali, Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa na Kamati ya Bajeti) iliamuriwa kuwa Serikali ianze utaratibu wa kukusanya maduhuli yake kwa kutoa risiti za kielektroniki. Azimio hilo linasema
“Maduhuli ya Serikali sasa yakusanywe kwa kutumia risiti za elektroniki. Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma yaanze kutumia risiti za eletroniki mara moja ili kudhibiti upotevu wa mapato ya serikali yanayotokea hivi sasa katika kutumia risiti zinazoandikwa kwa mkono. Pia ofisi za serikali zifanye manunuzi yake kwa wafanyabiashara wanaotumia mashine za kielektroniki.”
Nimepitia Mpango wa Serikali wa Mapato (Volume I – Financial Statement and Revenue Estimates 2013/14) na kugundua kuwa mapato yasiyo ya kikodi yamekadiriwa kuwa ni shilingi bilioni 741 kutoka Wizara, Idara na Mikoa na shi...lingi bilioni 383 kutoka kwenye Halmashauri za Wilaya, Miji na Manispaa. Sikuweza kupata mapato ya Mashirika ya Umma maana hayaletwi kwenye Bajeti za Serikali.
Wizara 10 zinazoongoza kwa Mapato (mapato kwenye mabano ni Wizara ya Nishati na Madini ( 220 bn), Wizara ya Fedha (126bn), Wizara ya Ardhi (100 bn), Wizara ya Maliasili (84 bn), Wizara ya Mambo ya Ndani – Uhamiaji (92 bn), Wizara ya Mifugo (19 bn), Wizara ya Mambo ya Nje (16 bn) na Wizara ya Mambo ya Ndani – Polisi (17 bn), kati ya hizi shilingi 16 bilioni ni kutoka idara ya Trafiki (traffic notification fees).
Kutokana na mafanikio ya makusanyo ya VAT ambapo inaonyesha kuwa mapato ya Serikali yameongezeka kwa asilimia 60 (kutoka 500 bn mpaka 800 bn), na kutokana na rekodi mbalimbali za Serikali zinazoonyesha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya makusanyo ya Serikali hayafiki Serikalini, ni dhahiri kuanzishwa kwa makusanyo kwa risiti za kielektroniki kutapandisha mapato ya Serikali zaidi ya mara mbili. Idara ya Usalama barabarani peke yake inasemekana kuwa makusanyo ya sasa ni theluthi tu ya makusanyo stahili kutokana na rekodi za ‘notifications’ barabarani.
Risiti za elektroniki kwa kukusanya maduhuli ya Serikali yanaweza kuongeza mapato ya Serikali maradufu na kuepuka mtindo wa Serikali wa kupandisha kodi kwenye bidhaa muhimu kwa wananchi. Uamuzi wa Kamati za Bunge za Mahesabu wa kuitaka Serikali kukusanya maduhuli yake kwa kutumia risiti za elektroniki unapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania.
 
Zitto Kabwe

No comments:

Post a Comment

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...