Wachezaji
wawili kutoka Tanzania wamechaguliwa miongoni mwa 50 waliofanyiwa
majaribio nchini Uganda kwa ajili ya kuingia katika kituo cha kuendeleza
vipaji (centre of excellence) kilichoko Doha nchini Qatar kupitia
mpango wa kukuza vipaji wa Aspire Football Dream.
Abdulrasul
Tahir Bitebo (15) ambaye ni mshambuliaji kutoka Kituo cha Uwanja wa
Karume, na Martin Omela Tangazi (14) ambaye ni beki kutoka Kituo cha
Ukonga ndiyo waliochaguliwa kutoka Tanzania kuingia katika kituo ambapo
watakaa kwa mwezi mmoja kabla ya kusaini mkataba rasmi wa kuendelezwa.
Wachezaji wengine walikuwa wakitoka katika nchi za Uganda na Kenya.
Mchezaji mwingine aliyefuzu katika nafasi tatu zilizokuwepo ni kutoka
nchini Kenya.
Mpango wa Aspire Football Dream unafadhiliwa na Mtoto wa Mfalme wa
Qatar katika nchi 16 duniani, na kwa hapa nchini uko chini ya Idara ya
Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
TFF ina jumla ya vituo 14 vya kuendeleza vipaji kupitia mpango huo wa
Aspire Football Dream. Vituo hivyo ni Karume, Kigamboni, Tandika, Kawe,
Ukonga, Kitunda, Mbagala, Magomeni, Makongo, na Tabata vilivyo katika
Mkoa wa Dar es Salaam. Vingine ni Bagamoyo kilichopo mkoani Pwani,
Morogoro, Arusha na Moshi mkoani Kilimanjaro.
Kituo kingine cha kuendeleza vipaji (centre of excellence) cha Aspire kipo Dakar nchini Senegal.
No comments:
Post a Comment