BAADA ya
sintofahamu kuhusu kilichomsibu kiongozi wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo CHADEMA Mkoa wa Dar es Salaam, Henry John Kileo, utata wa
Jeshi la Polisi na juhudi za mkewe Joyce Kiria kutaka kujua aliko
mumewe, nimeona nitoe kile kilichotokea katika sakata hili.
Kileo
alipigiwa simu na maofisa wa polisi makao makuu mnamo tarehe 17/6/2013,
wakimuarifu kwamba wanataka kufanya mahojiano naye. Hawakusema ni kuhusu
nini.
Mara moja
akawasiliana nami kama wakili wa familia yao, nami nikawasiliana na
maofisa hao kuwaarifu kwamba kwa kuwa nina majukumu kadhaa ya
kimahakama, na kwa kuwa Kileo yuko nje ya mkoa, basi ninaahidi kama
wakili kuhakikisha nitampeleka binafsi Makao Makuu Polisi Ijumaa ya
tarehe 21/6/2013.
Tarehe
21/6/2013 tuliambatana mimi, Kileo na John Mnyika (MB) hadi Polisi Makao
Makuu, kisha Mnyika alituacha na mahojiano yakaanza.
Kwa ujumla
walimuhoji Kileo mambo mbalimbali kuhusiana na tukio la kumwagiwa
tindikali kijana aitwaye Mussa Tesha katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la
Igunga mnamo mwaka 2011.
Wakati
mahojiano hayo yanafanyika, tayari kulikuwa na kesi ya jinai ikiendelea
huko Igunga, mkoani Tabora ambako washitakiwa wanne ambao ni makada wa
CHADEMA kutoka maeneo mbalimbali nchini walishitakiwa kama mshtakiwa
nambari moja mpaka nne kuhusiana na tukio hilo la Tesha. Walishitakiwa
chini ya vifungu vya sheria ya kanuni ya adhabu (Penal Code), na si
ugaidi.
Baada ya
mahojiano yaliyomalizika kwa Kileo kuandikisha maelezo hadi mnamo saa
11.30 hivi za jioni, polisi walimnyima dhamana, na wakampeleka rumande
iliyoko Kituo Kikuu cha Polisi (Central Police Station), akalala huko.
Jumamosi ya
tarehe 22/6/2013, mimi Joyce na Mnyika tulifika Kituo Kikuu cha Polisi,
ambapo OCS wa hapo alituarifu kwamba amri alizonazo ni kwamba Kileo
haruhusiwi kuonana na mtu yeyote.
Kama wakili,
nilijadiliana masuala ya kisheria na OCS, ikalazimu kuwasiliana na
maofisa wa polisi makao makuu ambao hatimaye waliniruhusu kwa mujibu wa
sheria kuonana na mteja wangu.
Tukazungumza na ‘kupeana moyo’, nikahakikisha amekula chakula kilicholetwa na mkewe Joyce ambaye muda wote alikuwa akimuangalia mumewe kwa mbali tu, kwani mazungumzo yangu na Kileo yalifanyika faragha.
Mnamo saa
7.30 hivi tuliondoka sote (mimi, Joyce na Mnyika), na kukubaliana kurudi
tena polisi Jumapili ya tarehe 23/6/2013 kumtembelea tena Kilewo, na
pia kufahamu mipango hasa ya Jeshi la Polisi kuhusu Kileo kwani hadi
tunaondoka si mimi wala mkewe aliyefahamishwa rasmi kuhusu mipango hiyo.
Nikiwa
nyumbani, nilipokea simu toka kwa Joyce akiniarifu kwamba amefika Kituo
Kikuu cha Polisi jioni ya Jumamosi ya tarehe 22/6/2013 na kuarifiwa tu
kwa mkato kwamba Kileo "ameondoka".
Ukweli ni
kwamba mkewe alikuwa amechanganyikiwa, na jukumu la kwanza lilikuwa
kumtuliza kisaikoilojia kwani nilifahamu kuwa alikuwa amejifungua muda
si mrefu huko nyuma;kwa hiyo hali yake ilikuwa ‘delicate’ sana kiafya na
kisaikolojia.
Nikapambana
kama wakili kwa kutumia uzoefu na ‘contacts’ (P.R -mawasiliano) ili
kupata tarifa ya aliko mteja wangu. Niliariwa tu "off record" na maofisa
wa polisi kwamba Kileo amesafirishwa kwa ndege ya Precision kuelekea
Tabora kupitia Mwanza chini ya ulinzi wa maofisa waandamizi wa polisi
ili kule Tabora afunguliwe kesi.
Sikuwa na
mawasiliano yoyote na mteja wangu, na hizo taarifa "off record" ndiyo
kitu cha pekee tulichokuwa nacho mimi, Joyce na uongozi wa CHADEMA
kuhusu nini kimemsibu Kileo.
Niliendelea
kupambana kupata taarifa rasmi, na hatimaye Jumapili ya tarehe 23/6/2013
majira ya saa 6 hivi mchana ndipo nilipopigiwa simu na mmoja wa maofisa
waliomsindikiza Kileo kuelekea huko Tabora kwa utaratibu ule ule wa
"off record", na kuniunganisha nae, ambapo nilizungumza naye kwa kifupi
kumjulia hali na kumuhakikishia kwamba tutapigana kwa uwakili wetu wote
kwa ajili yake.
Kwa hiyo
hadi muda huo hatukuwa bado na uhakika wa asilimia mia moja kwamba Kileo
yuko wapi hasa. Kwa wale mawakili wenzangu wanafahamu kwamba huwezi
kutegemea taarifa za kusikilizishwa mteja kwenye simu ambazo hata si za
kwake. Wala huo si ushahidi wa mahali alipo mtu huyo kisheria.
Lakini
ikatubidi ku-"assume" (kisia) kwamba Kileo yuko, atapelekwa Tabora
kushitakiwa. Mimi na Profesa Abdallah Safari tukaanza maandalizi ya
upesi upesi ya safari kuelekea Tabora kwa gari, kwani ndege kuulekea
huko ni Jumamosi na Jumatatu tu.
Tuliondoka
kwa gari ya makao makuu ya CHADEMA Jumapili ya tarehe 23/6/2013, majira
ya saa 11.30 hivi za jioni. Tulisafiri usiku kucha, na tulichukua "risk"
ambazo kwa kawaida tusingechukua, ikiwemo kupita katika mapori maarufu
kwa utekaji.
Kilichotusukuma
na kutupa moyo ni kwamba Kileo yuko mahali ambapo anatuhitaji sana, na
hana tumaini lingine bali sisi mawakili wake.
Tukisafiri
usiku kucha na kufika Tabora asubuhi ya Jumatatu tarehe 24/6/2013,
majira ya saa 2.30 tukiwa tumechoka hakuna mfano. Tukabadili mavazi
upesi upesi na kuvaa suti zetu na kukimbilia Mahakama ya Hakimu Mkazi
Tabora. Huko tuliarifiwa kuwa wao hawana taarifa zozote za Kileo.
Tukaelekea Makao Makuu ya Polisi Tabora. Jibu likawa ni lile kwamba
hawana habari.
Maana yake
ni kwamba sisi mawakili wa Kileo, tuko Tabora ambayo ni kubwa hasa na
hatujui mteja yuko wapi hasa. Nikafanya juhudi zile zile za "off
record", na kufahamishwa kwamba mteja wetu alishikiliwa Kituo cha Polisi
cha Nzega, umbali wa saa tatu toka Tabora, na kwamba yuko njiani
kuletwa Tabora.
Hatukuwa na uhakika bado, ila ilitulazimu kushikilia hiyo taarifa isiyo rasmi, na kuendelea na maandalizi ya kesi.
Majira ya
saa 9 hivi za alasiri ya tarehe 23/6/2013 Kileo akiwa chini ya ulinzi
mkali sana wa FFU katika Land Cruisers mbili za polisi waliwasili
Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora, akiwa hajala tangu jana yake. Alikuwa
yeye na wenzake wanne ambao walikuwa wamefutiwa mashitaka kwa hati ya
"Nolle Prosequi" huko Igunga, kisha kukamatwa tena mara moja na
kusafirishwa kwa ulinzi mkali sana hadi Tabora.
Ukweli ni
kwamba tulivyoonana na Kileo si sisi mawakili wala yeye mwenyewe
aliyejizuia kulengwa na machozi; yeye akimshukuru Mungu kwamba
tumepambana na yote hadi Tabaora kwa ajili yake kwa kasi vile, nasi
kwamba hatimaye tumeonana na mteja wetu.
Tukaingia
mahakamani, Kileo na wenzake wakasomewa mashitaka mawili; moja chini ya
sheria ya kuzuia ugaidi kwamba walimteka kwa nia ya ugaidi Mussa Tesha
huko Igunga, Tabora na la pili kwamba walimdhuru kwa kummwagia
tindikali.
Makosa ya ugaidi
Mawakili
tulipambana na kutoa hoja za kisheria nne dhidi ya uhalali wa mashitaka
yenyewe na utaratibu wa kufungua kesi husika. Tumeoiomba mahakama kufuta
mashitaka ya ugaidi, au la iamuru kila mshitakiwa arudishwe kushitakiwa
mahali alikokamatwa; mfano Kileo, Dar es Salaam.
Kabla ya
kuondoka Tabora, tulipita kumuaga Kileo na wenzake katika gereza la
Uyui. Wote wako na kombati zao za chama chao, na wako imara, hasa baada
ya kuona mawakili wako imara. Cha msingi ni kuomba Mungu aipe mahakama
ujasiri wakati wa kutoa maamuzi hapo Julai 8, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment