Rais mstaafu wa Marekani, George W. Bush na mkewe, Laura, wanatarajiwa
kuwasili nchini mwezi ujao ambapo watahutubia kongamano litakalojadili
wajibu wa wake za marais katika kuinua wanawake duniani.
Taasisi ya George Bush ndiyo imeandaa kongamano hilo litakalofanyika Dar es Salaam kuanzia Julai 2 hadi 3.
Taarifa iliyotolewa jana na taasisi hiyo kwa vyombo vya habari, ilisema
kongamano hilo, litahudhuriwa pia na mke wa Rais Barack Obama wa
Marekani, Michelle na muasisi wa Taasisi ya Wanawake ya Cherie, Cherie
Blair ambaye ni mke wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair.
Wake wengine wa marais wa Afrika watakaohudhuria ni Mama Salma Kikwete,
Chantal Campaore wa Burkina Faso, Roman Tesfaye wa Ethiopia, Maria da
Luz Dai Guebuza (Msumbiji), Penehupifo Pohamba (Namibia), Sia Nyama
Koroma (Sierra Leone), Janet Museveni (Uganda) na Christine Kaseba wa
Zambia.
Kongamano hilo litajikita zaidi katika kujadili masuala ya kuwekeza kwa
wake, kuimarisha Afrika lakini pia wajibu wa wake za marais kuhamasisha
wanawake katika maeneo ya elimu, afya na kuwakwamua kiuchumi.
“Kongamano hili litakutanisha pamoja wake za marais, maofisa wa
Serikali, mashirika binafsi, Asasi Zisizo za Serikali (AZISE) na wasomi
kujadili mambo muhimu ya kuchukuliwa hatua ili kunufaisha wanawake,”
ilisema taarifa hiyo.
Aidha, mada zitakazowasilishwa na kujadiliwa katika kongamano hilo ni
kuinua wajasiriamali wanawake kiuchumi kupitia mafunzo na teknolojia,
kupatia fursa wanawake wakulima kwa kupewa mafunzo ya kilimo cha kisasa,
mafunzo kuhusu saratani ya matiti na umuhimu wa elimu kwa wanawake.
Kongamano hilo linafanyika sambamba na ujio wa Rais Obama anayetarajiwa kuwasili nchini mwanzoni mwa mwezi ujao.
Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo kiongozi huyo atazuru
katika ziara itakayoanza Juni 26 hadi Julai 2. Nchi nyingine ni Senegal
na Afrika Kusini.
Ziara za kiongozi huyo na Bush, inafanya Tanzania mwaka huu kushuhudia
ugeni wa watu mashuhuri mfululizo, baada ya Rais Xi Jiping wa China
Machi 28, ambapo Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza kutembelea Afrika tangu
achaguliwe kuwa Rais Machi 14.
Amani, utulivu na uimara wa mfumo wa demokrasia ni miongoni mwa mambo
yanayotajwa kuvutia viongozi hao wa kimataifa kuja nchini.
Wapo wengine ambao katika maoni yao juu ya ujio wa viongozi hao,
wamekuwa wakisema ugunduzi wa rasilimali za asili kama vile gesi, mafuta
na madini ya urani ni sababu nyingine ya Tanzania kutembelewa.
Hata hivyo, Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt alikaririwa hivi
karibuni akifafanua, kwamba ziara ya Obama haina ajenda yoyote ya
kuchukua rasilimali za Tanzania, bali ni ya uhusiano wa kiuchumi kati ya
nchi hizo.
Source:CCM Social media.
No comments:
Post a Comment