Na Wilfred Lwakatare,
Sina
budi kumshukuru sana mwenyenzi Mungu kwa kunitendea mema na zaidi ya
yote kunipa uhai na afya hadi sasa. Wanasema “shukuruni katika yote” na
mimi nalazimika kushukuru kwa yale yote niliyofunuliwa na kuwa sehemu ya
ushuhuda wangu katika maisha niliyobakiza hapa duniani.
Namshukuru
Mungu muweza wa yote kwa kunirejesha tena uraiani na kwa kuniunganisha
na familia yangu,mke na watoto,wazazi ,ndugu,majirani na
marafiki,viongozi wenzangu na wanachama wa chama kikubwa CHADEMA na
zaidi ya yote watanzania walio wazalendo wanaoipenda na kuipigania nchi
yao.
Ninapojikuta huru nje ya milango ya mninga uliowekewa
makufuli makubwa,madirisha yenye nondo,ukuta uliowekewa waya wenye miiba
mikali na ulinzi wa maaskari wanaonichunga saa 24,inanikumbusha wimbo
mmoja wa mchakamchaka uliokuwa ukiimbwa gerezani kila siku saa 11:00
alfajiri tunapoamshwa uliokuwa na maneno;
“Kama raia!kama raia!kama raia!kama raia!
Iko siku moja nitarudi kwetu kwa baba na mama kama raia!
Iko siku moja nitarudi kwetu kwa ndugu na rafiki kama raia!
Kama raia…….”
Ni
kweli kabisa na wala si hadithi kuwa ‘jela ni MBAYA, jela ni MATESO!’
Lakini zaidi ya hilo, kwangu mimi nimeyaona pia maisha ya gerezani ni
mahala pa mafunzo ya kuijua jamii, kuyajua maisha, kuyaelewa mambo,
kuifahamu nchi n.k.
Nimekubaliana mia kwa mia na maneno ya
mwenyekiti wetu wa CHADEMA-Taifa Freeman Mbowe(MB) aliponitembelea
gerezani Segerea na kuniambia; “hupaswi kulia na kujuta sana;now you are
going to be a PRISON GRADUATE, uhitimu ambao kila mwanasiasa na
mpigania haki mahiri duniani ameupitia.” Kipindi cha siku 92 nilichokaa
ndani nikianzia polisi kituo cha kati, gereza la Keko na kisha kumalizia
Segerea kimenipa uzoefu na ufahamu usio wa kawaida.
Ipo tofauti
kubwa baina ya idara za polisi na magereza,jambo ambalo lilikuwa nje ya
ufahamu wangu kabla.Nina uhakika magereza wakipewa kazi ya kuwasaka
walipua mabomu ,watesaji,wapiga risasi mapadri watawakamata. Nilipata
bahati ya kuitwa na kufanya mazungumzo na wakuu wa magereza ya Keko na
Segerea .
Lakini pia, nilitembelewa na viongozi wakuu wengi wa
jeshi la magereza nchini akiwemo kamishena mkuu Minja.Wakuu hawa wana
weledi mkubwa wa kumpa mtu somo la ‘ushauri nasaha’(counselling).
Wanakufutia fikra zote za uraiani (nyumbani,mitaani na ofisini) na
kukurejesha mahala pa maisha yako mapya ya gerezani na kukujuza taratibu
na kanuni unazopaswa kuzifuata na kuzitii.
Madaktari na manesi
waliweza kuangalia kwa karibu sana afya yangu kiasi cha kulidhibiti kwa
kiasi kikubwa tatizo langu la sukari ambalo limekuwa likinisumbua kwa
miaka 14 sasa.
2: KESI YA UGAIDI.
Ni
kesi ambayo imenifikisha hatua au ngazi nyingine ya maisha yangu kama
mwanasiasa.Naamini wahusika walipoamua kuifungua bila shaka mwelekeo
ulikuwa uleule ambao niliusoma nikiwa chuo kikuu na ninaousoma katika
maandiko mbalimbali kuhusu historia za wanaharakati na wapigania
haki,uhuru na ukombozi waliopita na tulio nao au tunaowasikia hivi sasa
duniani;wakina Nelson Mandela, Martin Luther King Jr n.k. Wakiwa katika
harakati za kuitafuta haki walifunguliwa kesi na wengine kufungwa jela
kwa tuhuma za ugaidi,uhaini na kula njama.
Nilikubaliana na dhana
ya kimtazamo iliyopo au waliyonayo viongozi /watawala wote wadhalimu
duniani kuwa watu wote wanaojitokeza kupambana au kukabiliana na mfumo
kandamizi bila woga, watu wote hao kwao ni magaidi,mahaini,wala njama au
wasaliti.
Ni kipindi kifupi kilikuwa kimepita tangu timu teule
maalumu ilipokuwa imemaliza kikao cha kujitathmini kama CHADEMA
(RETREAT) kuona tumetoka wapi, tuko wapi na kwa mfumo upi na mazingira
yapi ilikuyafikia malengo tuliyonayo.Nakumbuka miongoni mwa mambo
niliyoyasema ni pamoja na nini tutarajie baada ya CHADEMA kuonekana na
kuthibitika kwa watawala kwamba imekua,imeimarika na imejipanga vyema
kiasi cha kuwatia hofu watawala (CCM) kwamba karibu wanaondolewa
madarakani.
Niliwaambia washiriki wenzangu kwamba wajiandae kukamatwa
na polisi mara kwa mara,kutiwa ndani,kufunguliwa kesi nyingi zisizo za
kweli,kubambikiziwa kesi,kuchafuliwa mbele ya jamii,kutishiwa maisha,
kupigwa, kuuwawa, kudhohofishwa kiuchumi n.k.
Nikasema, pindi tukiona
hayo yamekamata kasi kila pembe ya nchi tujue CCM tumeanza kuwashika
pabaya na ushindi utakuwa umekaribia.
Nilishauri tujipange
kisawasawa kimbinu na kimkakati kukabiliana na mambo hayo kwa sababu ni
lazima yatokee.Namshukuru Mungu yameanzia kwangu na kama nilivyomwambia
mwenyekiti Mbowe aliponitembelea gerezani nilimwambia nimekipokea
kikombe hiki na yaliyonitokea tusiyashangae bali yawe changamoto na gia
ya kutusukuma kwenda mbele kwa kasi kubwa zaidi.Ni kukanyaga mafuta
zaidi mpaka kieleweke na hiyo ndiyo itakuwa faraja yangu mimi na wengine
watakaofungwa magerezani.
Tuhuma za ugaidi nilizobambikiziwa
zilinirejesha nyuma mwaka 2002 nilipokuwa bungeni kama mbunge wa jimbo
la Bukoba mjini (CUF) nikiiongoza kambi rasmi ya upinzani iliyokuwa
ikijumuisha wabunge wote wa vyama vya upinzani
TLP,NCCR-Mageuzi,CHADEMA,UDP na CUF.Muswada wa sheria hiyo ya ugaidi
ukiwa ndio umeletwa bungeni kujadiliwa,niliongoza kambi yangu ambayo
miongoni mwao walikuwamo Mh. Mbowe wakati huo akiwa waziri wangu kivuli
wa biashara na viwanda na Dr. Willibroad Slaa akiwa waziri kivuli wa
katiba na sheria kuupinga na kuukataa muswada huo kwa nguvu zote.
Sababu
mojawapo ya kuupinga ikiwa ni mahudhui na malengo ya muswada huo
kutoeleweka na kuwa wazi na kwamba ulilenga zaidi matakwa ya kijasusi ya
nchi za magharibi zikiongozwa na Marekani na kwa hapa kwetu tulitamka
bayana kwamba serikali ya CCM ililenga kuitumia sheria hiyo kuvidhibiti
vyama vya upinzani. Hilo ndilo limetokea sasa na likaanzia kwangu.
Ukiachia
mbali msongo mkali wa mawazo niliokuwa nao nikiwa gerezani juu ya
ugonjwa wa baba yangu mzazi mzee Elias Lwakatare aliyeletwa Dar Es
Salaam kwa ajili ya matibabu,athari za mke wangu kuathirika kimasomo
huko chuo kikuu Mzumbe aliko,mshtuko kwa watoto wangu shuleni na ugumu
wa karo zao za shule,kuwaweka roho juu kaka,dada na ndugu
zangu,kuvurugika kwa kazi za chama ofisini kwangu na mkoani kwangu
Kagera n.k,binafsi nililiona tukio hilo kama nafasi nyingine kwa chama
chetu kujitambua na kujipima udhaifu tulionao,nguvu tulizonazo na fursa
tulizonazo wakati tunapoelekea kuikamata dola.Niliisoma makala mojawapo
ya Mwanakijiji katika toleo mojawapo la Tanzania Daima,niliipenda sana
na niliguswa. Makala hiyo ilikuwa ikituasa CHADEMA kujitathmini. Ukweli
wenyewe ni kama makala hiyo ya Mwanakijiji sisi kama CHADEMA ilituvua
nguo na kutuacha uchi.
Kwanza tuhuma ya ugaidi niliiona kama
kombora la mwisho la serikali ya CCM kukamilisha mkakati wao wa
kuichimbia CHADEMA kaburi ambayo siku zote huwa ni ya pembe nne na
katika kuichimba na kuifukia kawaida koleo lenye umbo la ‘U’ mbele na
mpini wake hutumika.
“U” ya kwanza yenye kutubamkikizia tuhuma za
ufamilia,Ukabila,Uchagga,Ukask azini alikuwa amebebeshwa mwenyekiti
Mbowe zikashindwa. “U” ya pili yenye kuzoa tuhuma za
Udini,Ukatoliki,Upadri alibebeshwa katibu mkuu Dr.Slaa nazo zikakwama
CHADEMA ikapenya. “U” ya tatu yenye kulenga
Uchonganishi,Umbea,Ufitinishaj i na Usongombingo, CCM wakalenga
kumbebesha Naibu katibu mkuu kijana Zitto Kabwe lakini naye akawashtukia
akawaumbua na kuwabwaga. Zitto ameendelea kuhimiza mshikamano mkubwa
ndani ya chama na kuwaacha wapambe nuksi hoi. “U” ya mwisho yenye kubeba
Ugaidi,Uuaji,Utekaji iliyolenga kukifuta kabisa chama vitabuni na
kuwasweka viongozi gerezani, kabambikiziwa Wilfred Lwakatare Mkurugenzi
wa Ulinzi na Usalama CHADEMA.Mungu mkubwa nayo hiyo mahakama kuu yenye
baadhi ya majaji weledi wa sheria na wasiokubali mizengwe wameifutilia
mbali.Hakika CHADEMA haizuiliki na kwa hakika lililobaki ni kulitumia
koleo hilohilo na “U” hizo kuwafukia CCM humohumo kwenye kaburi
walilojichimbia wenyewe. ‘Mchimba kaburi huingia yeye mwenyewe.’
Nashukuru
CHADEMA hivi sasa imejipanga kama taasisi makini inayoongozwa na
kusimamiwa kitaasisi na wala si kwa utashi wa mtu binafsi au kundi
fulani la watu bali vikao vya kikatiba. Mshikamano wa pamoja na fikra
zinazotuelekeza kulenga paala pamoja tulikodhamiria, hivi sasa ndiyo
silaha kubwa na nusuru yetu kichama. Kama CHADEMA inavyoamini ;
“TUNAANZA NA MUNGU, TUNAENDELEA NA MUNGU NA TUNAMALIZA NA MUNGU.”
I AM REALLY PROUD OF BEING IN CHADEMA FAMILY!!!
3: HALI NA TASWIRA YA POLISI MAGEREZA NA VYOMBO VYA KUSIMAMIA HAKI NA USALAMA.
Wakati
nikihojiwa na jopo la maofisa wa makao makuu ya polisi la akina Mhigulu
wakati huo akiwa Kaimu DCI na wenzake akina Obadia,Jonas,Simon
Pasua,Beneth Kipasuka,Nyombi na wengineo baadhi yao niliwapa ujumbe
wamfikishie ‘college mate’ wangu (IGP Said Mwema ) Chuo kikuu cha Dar es
Salaam kuwa naziona jitihada na mbio zao za kuwatafuta hao watu
wanaoitwa magaidi,wateka madaktari na waaandishi,wapiga risasi mapadri
n.k mbio zao haziwezi kufaulu kutokana na namna wanavyoliendesha zoezi.
Niliwaambia
;wakati wao wako ndani ya land rover 109 kilomita arobaini nyuma yetu
sisi tunaokimbizwa na kutuhumiwa kuhusu ugaidi na kupanga njama za
kudhuru watu, wahusika halisi wa mambo hayo wako na Range Rover kilomita
arobaini mbele yetu. Je,ni mwaka gani watawafikia na kuwaweka mbaroni
hao jamaa?Hivi, kikosi cha IGP Mwema ambacho tumeelezwa ni maalum na
kina makachero waliobobea kushindwa kurejesha mrejesho wa maana hadi
sasa kwa angalau hata tukio moja, hivi watanzania hatushtuki tu? JK
haushtuki ? Anyway,tuendelee kuwapa masurufu na kuwatengea mafungu
tutaona! Sijui kama walinielewa au kumfikishia IGP Mwema huo ujumbe
wangu.Na kwa kuwa asiyetaka kujua maana haambiwi maana basi tuendelee
mambo ni kanyaga twende!
Wakili wangu Kichehere niliyekuwa naye
katika mahojiano wakati nikihojiwa kituo cha kati alijaribu kuwapa
changamoto japo chache za kupanua akili zao kuhusu huo unaoitwa ugaidi
dhidi yangu na ‘ka-cd’ kao walikokachota kwenye mtandao wa “You Tube”
(kama walivyotueleza) na kutuonyesha pale kwenye mahojiano. Hawakutaka
kumsikiliza wala kumuelewa juu ya kasoro zilizojidhihirisha moja kwa
moja . Hata pale alipowashauri kuwaita na kuwahoji baadhi ya watu muhimu
walioonekana kuhitajika ili kuondoa walakini usio na sababu tangu
mwanzo wa zoezi, hawakutaka kuuchukua ushauri huo. Wakaona waendelee
kukimbia na hako ‘ka 109’ kao. Mimi naamini upo wakati ambapo mshtukiwa
wa tukio linalochunguzwa aliye mzalendo na nchi yake anaweza kuwa msaada
wa kuinusuru nchi yake anayoipenda endapo anapewa nafasi ya kutoa
ushirikiano kwa njia za kuheshimiana kiutu .
Anyway,sijui mwisho
wa mambo yote haya maana bado tuko safarini na bado nina kesi moja ya
kujibu ya njama ya kumdhuru Denis Msacky kwa sumu (kwa mujibu wa maamuzi
ya mahakama kuu ya jaji Kaduri).Sitaki kuingilia mwenendo wa kesi hiyo
na nikajiibulia mengine.Lakini kaka yangu IGP Mwema endelea kutangaza
bingo la mamilioni labda utafaulu,Inshallah!!
Ukiacha kesi yangu
hiyo ya kutuhumiwa ugaidi, lakini kukaa kwangu pale polisi central
(kituo cha kati),gerezani,keko na Segerea kumenithibitishia vituko na
mambo chungu nzima niliyokuwa nikiyasikia nikiwa uraiani na kufikiria ni
ya uongo. Vitendo vya watu kubambikiwa kesi viko njenje na wenyewe kwa
lugha zao wanaita; “kumpa mtu kichwa! kumpiga mtu armed robbery!
kumpeleka mtu mapumziko!n.k” Nafikiri watu wanaofanya vitendo hivi
wanahitaji kufanyiwa ‘concelling…’ ( kupewa ushauri nasaha) kwani sio
vitendo vya kiutu.
Hivi huu ni utamaduni gani na taifa
tunalipeleka wapi? Hivi kweli inaingia akilini wakati mchezo kama huo
ukiendelea na watu kibao kubambikiziwa kesi kwa ‘kupewa vichwa’ wakati
huohuo mh.JK yuko ‘busy’ kuwatunuku watu nishani za utumishi uliotukuka?
‘This is a typical shame!!’ Sijui kama usalama wa Taifa wapo. Hivi
wanafanya kazi gani kama hawamsaidii mheshimiwa Rais kumjuza
kinachoendelea? Au ni ugonjwa uleule mchanganyiko wa ‘sisiemhosis’.
Naanza kukubaliana na usemi wa mtu mmoja niliyeongea naye gerezani
Segerea aliyesema vyombo vya kulinda usalama huenda ni vya kulinda
usalama wa viongozi walaji,wahujumi wa nchi,mafisadi na mfumo aliouita ;
“chukua chako mapema.”
Na ni vyombo vyenye weledi mkubwa wa
kuchora michoro ya fitina,uongo,wizi,hujuma,kusam baratisha vyama vya
upinzani kuiba kura kutisha watu kutengeneza kesi bandia,kuandaa
mashahidi feki n.k. Matokeo yake watu ambao leo hii wamejaa na
kurundikwa magerezani na mahabusu za polisi,asilimia kubwa wanakuwa
hawana hatia wahalifu wakubwa wako nje wakiendelea kula nchi! Asilimia
kubwa ya kesi zinazopelekwa mahakamani ni feki na ni za kuwachosha
mahakimu na majaji bila sababu kwani kesi hizo huishia kufutwa.
Mrundikano
mkubwa magerezani wa wafungwa na mahabusu unasababisha hata huduma ziwe
mbovu. Wapo wafungwa hawana sare za gereza wanavaa kitu kinachoitwa
‘nusu mlingoti’, kauka nikuvae, sare zilizochanika kiasi cha kutia
aibu.Na kwa kuwa hata sera za uendeshaji magereza nyingi ni zilezile za
‘vichwa vya ki-CCM’ (chama dhaifu,wabunge dhaifu na serikali dhaifu)
hakuna akili inayoweza kubuni namna ya kuitumia kiufanisi nguvu kazi
kubwa iliyojaa magerezani. Ndani ya gereza kuna kila aina ya fani na
vipaji lakini vimelala tu. Kama vile CCM, hawazai na hawana watoto
nyumbani, huwezi kuamini watoto lukuki waliorundikwa Segerea bila
utaratibu mzuri wa kimalezi na kimakuzi hata kama baadhi yao ni wakorofi
na wahalifu. Tutake, tusitake hawa ni taifa la leo na la kesho.Hawa ni
nguvu kazi yetu ya nchi ,hawa wanahitaji kukunjwa wangali wabichi.
Watoto
hawa ambao wengine ni wa umri wa miaka kumi wenye kesi za kuiba embe
tano,kuiba simu, kudokoa pochi zenye elfu 30,000/=n.k,wamo gerezani
wakinyweshwa uji asubuhi,ugali wa dona na mchuzi mwingi wenye maharage
thelathini kwenye bakuli na muda unaobaki kuutumia kufundishana
ngumi,kupiga ‘vice’, na mengine mengi. Kuna kitu kipya ambacho
kimebuniwa na uongozi wa jiji la Dar es Salaam ‘kuusafisha mji’ kwa
kuwaondoa barabarani na mitaani watu wote mafukara na wasio na uwezo
mkubwa wa kipato. Hawa wote wanakusanywa kwa mamia kila siku na
kurundikwa Segerea kwa shtaka moja tu linaloitwa “kesi ya kubughudhi
abiria.”
Uwe umekamatwa unakojoa kichochoroni, unauza maji ya
Uhai barabarani,machinga wa bidhaa,mpiga debe,unayemsubiri jamaa yako
pembeni mwa barabara au kituo cha mabasi Ubungo, uwe ni mama lishe, ni
‘dada poa’ n.k,ukishashindwa kuwakatia elfu kumi au elfu tano jamaa hao
wanaoitwa askari wa jiji au walinzi shirikishi, ujue wewe tayari
unakwenda Segerea kwa kesi ileile inayoitwa ya ‘kubugudhi abiria’.
Wakati huohuo bidhaa zako zote zinakwenda,masufuria na wali wa akina
mama lishe unapelekwa kunusuru familia za wasafisha jiji hao,simu na
pesa yoyote uliyonayo mfukoni inakwenda;yaani ni kiama! Jamani,
waheshimiwa wabunge na madiwani wa jiji la Dar es Salaam hususani wa
CHADEMA chukueni hatua za haraka.
Mzee kikwete upo hapo?
Unakumbuka ahadi zako za hotuba yako ya kwanza bungeni Dodoma na wakati
ulipomaliza ziara yako ya magereza ya Keko na Segerea mwaka 2007? Achana
na hayo yote,sasa njoo gerezani upate picha ‘live’.
Nikiwa
kwenye selo yangu,kwa bahati nzuri niliruhusiwa kuletewa magazeti na
kusikiliza redio . Siku moja wakati nasikiliza kipindi cha Bunge, Naibu
waziri wa mambo ya ndani akijibu hoja za wabunge kuhusiana na hotuba ya
bajeti yao iliyokuwa imewasilishwa na bosi wake Dr.Nchimbi, nikamsikia
akizungumzia swala hilo la upekuzi wa wafungwa na mahabusu kwa utaratibu
unaoonekana kumdhalilisha binadamu. Naibu waziri anasema tatizo hilo
lipo lakini kutokana na ufinyu wa bajeti hawawezi kununua vifaa vya
kisasa vya kufanyia upekuzi. Akasema kutokana na hali hiyo,wataendelea
kutumia njia hizohizo za ‘ubunifu’ mpaka hapo serikali ya CCM
itakapokusanya mapato yanayokidhi bajeti inayoweza kuvinunua vifaa
hivyo.
Wakati wa kupitisha mafungu,jamaa wakapitisha pesa ya
kununua chai,vitumbua,maji ya kunywa,ziara za viongozi,ununuzi wa
magari,semina,warsha,mafunzo ,motisha n.k. Nikajiuliza,hayo mambo ndiyo
kipaumbele kweli hata kuliko kuyanunulia magereza mashine mojamoja za
kufanyia upekuzi? Taasisi mbalimbali za haki za binaadamu ni kweli
zinafanya kazi nzuri kwenye mitandao ,uitishaji semina,uandikaji ripoti
nyingi nzuri zinazotumwa kwa wafadhili ili michuzi izidi kutoka n.k.
lakini nasema haitoshi. Tembeleeni magerezani msiishie kwa bwana Jela ,
ombeni kutembelea maeneo yote na kuongea na wafungwa . Kwa njia hiyo
mtaboresha kazi yenu kwa uzuri zaidi.
4: SALAAM TOKA MAHABUSU, POLISI NA GEREZANI.
Mwenyekiti
Mbowe alipokuja gerezani Segerea kunitembelea akiwa na Mkurugenzi wa
mambo ya Bunge na Halmashauri Bwana John Mrema alinipa kazi ya kukijenga
chama humo humo ndani gerezani . Nitakua namkosea adabu nisipo fanya
mrejesho wa kazi yake. Na kwa kuwa mengi ya yale niliyoyafanya na
kuelezwa na wadau wangu yanatuhusu sisi wote kama viongozi wa CHADEMA,
wanachama na hata wanachama watarajiwa, sio vibaya nikiyaweka hadharani.
Ya Mbowe kama Mbowe nitamuwasilishia yeye mwenyewe kwa muda muafaka.
Wafungwa,
mahabusu, baadhi ya watumishi wa gerezani, mapolisi na wengineo wanatoa
salamu nyingi sana. Wengi wanaipongeza kazi inayofanywa na CHADEMA
ndani na nje ya bunge. Wanasema karibu wote ni CHADEMA japo wengi hawana
kadi. Ili upokelewe vyema gerezani lazima uwe ‘vidole viwili’ ukijitia
‘ukada’ utalijua gereza. Wanasema kamwe wabunge wa CHADEMA msitiwe woga
na tambo za wabunge wa CCM ndani ya bunge kwa kujiona wako wengi
wakifikiria huo wingi upo hata nje ya mjengo. Wanasema katika hilo
‘wamebugi meen!!’. Nje ya Bunge CHADEMA mna mashabiki na wafuasi nyomi!!
Yaonekana kwa hivi sasa Bunge ni uwanja wa nyumbani anaoutumia CCM
kimchezo na ninyi CHADEMA uwanja wenu uko huku uraiani kwa umma.
Wanasema
vitendo vya dada Makinda na mwenzie Job Ndugai wameshavipigia hesabu.
Mwisho wao hauko mbali , ninyi kazi yenu ni kukaza buti bila kulegeza.
Wamenituma niwaambie, maana mjumbe huwa hauwawi!, eti CHADEMA nje ya
Bunge tusiendelee kupoteza muda kuwahubiria watu ufisadi, wizi,
manyanyaso ya vyombo vya dola vya serikali ya CCM, kushindwa uongozi kwa
serikali nzima ya CCM, umaskini mizengwe ya CCM katika kuandikwa kwa
katiba mpya n.k. Wanasema yote hayo wameshayaweka kichwani na wanajionea
wao wenyewe kama waathirika namba moja wanatambua fika kwamba wamo
ndani ya gereza kwa sababu ya mfumo uliosababishwa na kutengenezwa na
CCM.
Wanasema katiba halisi ya watanzania itaandikwa baada ya
CHADEMA kuingia ikulu kwani CCM ni mizengwe mitupu.CCM hawajaanza leo,
kumbukeni yaliyompata Jaji Kisanga na Tume yake walipoambiwa na Mkapa
kwamba wamewasilisha taarifa ya mambo ambayo hakuwatuma. Wanasegerea
wanasema elekezeni nguvu zote kwa kipindi hiki kilichobaki kabla ya
chaguzi za 2014 za serikali za mitaa na ule mkuu wa 2015 kuwapanga
wapiga kura kiuchaguzi .
Lipigwe jaramba na kuwekwa mpango
mahususi utakaowezesha kila aitwaye mtanzania mwenye umri wa kupiga kura
apate uhalali wa kupiga kura. Uwekwe mfumo wa kubanana kuhakikisha watu
wanajipatia vitambulisho vya uraia wanatunza shahada zao au
vitambulisho na wanakwenda kupiga kura. Wanaamini kwa hali ilivyo hivi
sasa, ni binadamu ‘asiye majaliwa’ au wale wachache wasiojaa kiganjani
waitwao ‘CCM maslahi’ watakaothubutu kuelekeza kura zao kwenye rangi ya
kijani- mchicha, kisamvu!
Wamo baadhi ya wafungwa na mahabusu
walionieleza kwamba walikua CCM kufa mtu na walishiriki kwenye hujuma
mbalimbali na hata kuiba kura, lakini hivi sasa wamekoma kwani
wametumika kama karai na kisha kutelekezwa nje ya jumba walilosaidia
kulijenga na ndio maaana wanaozea jela. Baadhi ya mbinu walizokua
wakizitumia kutuibia kura wamenieleza na nimetoka nazo kibindoni.
Wamenituma
niwaeleze, kwa kipindi kilichobaki, ‘chonde! Chonde! acheni kugombana,
kurumbana na kufukuzana. Tumieni kipindi hiki kujenga mshikamano
utakaowezesha kukisuka kikosi cha ‘Real Madrid’ au ‘Manchester United’
ya siasa za Tanzania ili uchaguzi ujao CCM walazwe chali-mwanguko wa
kifo cha mende! Wanasema CCM ni wepesi kama nyama ya maini, wakibanwa
kwenye kumi na nane hawana ujanja wataachia tu , tatu bila!!!
Wameniambia
hivi sasa CHADEMA ni chama kikubwa chenye uwezo wa kubuni njia
mbalimbali mbadala zinazoweza kutumika kuwadhibiti viongozi wowote au
wanachama wanaodiriki kukivuruga chama makusudi au kukihujumu badala ya
kuchukua hatua za kuwafukuza.
Wanampongeza na kumpa heko
Mwenyekiti wa chama kwa umahiri na ubunifu wake uliokifanya chama kikue
na kupanuka kwa haraka. Kwa lugha zao wanasema Mbowe ni jembe na ni
kichwa,anafanya kazi nzuri ya kutengeneza timu kwa lengo la kushinda
mechi. Wanamshauri ajitahidi kuona namna ya kuumudu mchezo ulioko mbele
yetu 2014 na 2015. Iangaliwe karata zitachangwaje? Wanasema ni vyema
tukajifunze namna mchezo wa siasa za Kenya ulivyochezwa dakika za lala
salama za uchaguzi wao. Wanatambua na kupongeza namna CHADEMA
ilivyomuunga mkono Kamarade Odinga na muungano wake wa ACCORD, lakini
kwa msingi wa kujifunza mbinu za kuusaka ushindi , tuangalie na
kujifunza namna Kenyatta alivyoubadili mchezo. Kwanza kwa kumudu kuunda
chama kipya na kukijengea mtandao ndani ya muda mfupi.
Pili
alivyoweza kuwavuta na kuwashawishi waliokuwa mahasimu wake walio muhimu
(kama vile Ruto) ambao bila ya kuwa nao asingeweza kufua dafu kwa
Odinga. Tatu , namna Kenyatta alivyocheza mchezo wa kisiasa kwa
kuzingatia na kutumia kanuni isemayo ‘siasa hazina rafiki wala adui wa
kudumu’ bali ni kuangalia nani anawezesha kupenya vikwazo ili kuwezesha
kufika salama ninakokwenda (kwa maana ya kuingia Ikulu). Ukishaingia
ndani ya mjengo mambo mengine ni akili kichwani, utajua unachemsha vipi
kichwa lakini muhimu kuliko yote si tayari umo ndani na unachezea ndani?
Wanamuomba Mbowe azidi kuzamisha akilli na kuupanga mchezo kwa
“formation” ileile ya Kenyatta, lakini kwa kuongezea na mbinu nyingine
zinazozingatia mazingira yanayotunzunguka KICHADEMA.
5: NIMEKUTANA NA SHEIKH PONDA
Milima
huwa haikutani lakini binadamu wanakutana. Ndivyo sakata la ugaidi
lilivyonifikisha gereza la Segerea na huko nikajikuta nawekwa selo moja
na ‘mjukuu wangu’ Issa Ponda mtoto kutoka Kigoma. Issa Ponda ni kiumbe
wa mwenyezi Mungu wa aina ya pekee. Kwa nchi za wenzetu zilizoendelea
mtu mithiri ya Ponda si mtu wa kuchukulia mzaa kama ninaouona ukichezwa
hapa kwetu. Ni mtu ambaye fikra zake, ubunifu alionao kichwani na katika
vitendo, hulka zake, nasaha zake, ushawishi wake, ujengaji hoja zake,
uchaji wa Mungu wake, uswalihina wake na vingine vingi ni watu wachache
sana unaoweza kukutana nao wakiwa navyo vyote kwa mpigo.
Ponda
tofauti na namna mfumo unavyomchukulia, ni mtu ambaye angetumika vyema
kwa kusikilizwa sehemu kubwa ya mawazo yake na yakafanyiwa kazi
ipasavyo, nina uhakika mambo mengi tunayoyaona yana mitafaruku ya kidini
yasingelikuwepo.
Tatizo wakubwa wanamuangalia kwa taswira ya
upande mmoja ya kumuona ‘mkorofi, mchochezi’. Sijui na ndio maana
nauliza, hivi ni mamlaka gani ya juu na yenye kauli ndani ya nchi hii
imewahi kukaa na Ponda kwa karibu katika misingi ya kuheshimiana kwa
dhati na kusikilizana ili kujua ana mawazo na mitizamo gani kwa masuala
mbalimbali yaliyolalamikiwa na baadhi ya waislamu walio wengi?
Nimeishi
naye zaidi ya siku 60 selo moja kwa masaa 24 karibu kila siku na masaa
mengi tukiwa wawili tu, mimi na yeye. Ni mdadisi wa kupenda kujua, na
ukisha mwelewesha ni mwepesi wa kuelewa na kujenga fikra mpya.
Hivyohivyo siyo mchoyo wa kuyabania maarifa aliyonayo na elimu kubwa ya
kidini aliyobahatika kuipata.
Alinielewesha kuwa kwenye dini ya
kiislamu mtu anapokuwa amefikia kiwango cha kuitwa U-Ustadhi kwa lugha
ya haraka inayoeleweka na wengi ni sawa na U-profesa.Hakika Sheikh Ponda
ni ‘profesa’.
Nilipata fursa ya kujadiliana naye pia mambo ya
msingi yanayolikabili hivi sasa Taifa letu. Moja wapo ni nguvu nyingi
zisizo na sababu zinazotumiwa na polisi kushughulika na watu kama sisi
ambao hata rungu hatuna. Nguvu kubwa inayotumika ya kumpeleka Ponda au
Lwakatare mahakamani ili kesi itajwe tu na kurudi Segerea kulala ni sawa
na kumlipa daktari wa muhimbili mishahara mizuri ya miezi miwili.
Magari nane na mapikipiki kujazwa mafuta,ving’ora barabarani,askari
polisi zaidi ya hamsini kuvunja shughuli nyinginezo kwa siku nzima,
barabara kufungwa na mengine kuzuiwa wakati wa kupita n.k Mikwara yote
hiyo ya nini?
Mfungwa mmoja aliyesoma kwa kiwango fulani
alipoletwa kulala kwenye selo yetu na kuikuta mada hiyo, alichangia
hivi, “kawaida ya mtu yeyote anayelazimisha aonekane mbele ya wakubwa
zake kwamba anafanya kazi ni lazima atengeneze mazingira yanayomfanya
aonekane kweli anafanya kazi”. Kisha kasema hivi “nyie waheshimiwa ili
wale waliowafungulia tuhuma za ugaidi na uchochezi lazima watoe taswira
ya nje kwa umma kuonesha kuwa ninyi ni watu hatari sana na mkipewa
upenyo wowote mnaweza kusababisha maafa makubwa sana wakati wowote kwa
taifa. Kwa ufupi wanataka umma uwahukumu kinadharia kwamba mnahusika na
tuhuma mlizoshtakiwa nazo hata kama mahakama haijazipitia tuhuma zenyewe
kuona zina uzito gani.”
Nilimuelewa vizuri sana na kukubaliana
na huyo mfungwa maana vyombo vyetu hivi vya dola wakati mwingine
vinapenda kutumia nguvu nyingi sana katika jambo dogo sana kwa sababu tu
za kuridhishana na makundi fulani au kulinda nafasi zao za kazi ambazo
hawazimudu.
Jambo jingine lililoangukia katika mijadala yetu ni
hii migogoro ya makundi ya kijamii na hata mauaji na maumizano
yanayojitokeza mara kwa mara. Sheikh Ponda alitoa changamoto moja muhimu
ambayo naona ina mashiko sana. Alisema hivi; huko uswazi (mitaani
wanakoishi watu wengi kwa kubanana) ambako nyumba moja wanapanga na
kuishi zaidi ya watu hamsini, mchanganyiko wa waislamu kwa wakristo,
mbona hakuna ugomvi? Mbona akina mama humo ndani waislamu kwa wakristo
wanaachiana watoto kwenda sokoni? Mbona wanaazimana vijiko na masufuria?
Mbona wanapeana mboga bila kuulizana? Ponda akatumbukiza na utani pia
kuwa “mbona humu selo ukileta chakula alichopika mama Frank siulizi na
wala wewe chakula anachoniletea mama Mariam naona unabugia tu bila
maswali yoyote?
Na mimi nikamwambia mbona ukiamka saa tisa usiku
ukaanza swala zako za sunna mpaka alfajiri wakati wa ‘Azanna’ na kisha
swala zote tano za ‘faradhi’ za siku nzima na lakhai zake mbilimbili
humu humu ndani ya selo havijaingiliana na ibada zangu za ‘Tumwabudu
Mungu wetu?’ Selo yetu ndio msikiti wetu na ndilo kanisa letu. Haya
mambo chanzo na chimbuko lake ni nini? Hayawezi kuwa yanatengenezwa na
kundi maalum la watu kwa malengo maalum?
Swali hili la mwisho
likanikumbusha somo moja tulilowahi kufundishwa kipindi fulani
nilipokwenda Ujerumani kwa mafunzo ya ‘Strategic Planning’. Katika
kipengele kimojawapo cha mafunzo hayo nakumbuka kuna kitu mwalimu
alikiita ‘Power Winning and Maintaining Strategy’, kwa tafsiri nyepesi
‘mkakati wa kuupata utawala na kuulinda’.
Katika mkakati huo
nakumbuka alitwambia, kuna wakati watawala fulani wanapoelemewa na mambo
au jambo wakakosa majibu mbele ya watawaliwa wanaotaka kujua kulikoni
ili kuzima mambo hayo aidha ni kutumia nguvu na fursa zilizopo
kumshughulikia kinara mmoja anayeonekana kimbelembele kuhoji.
Mkisha
mziba mdomo kwa njia zozote zinazowezekana walio nyuma yake wataufyata
tu! Njia nyingine ni kuibua au kufanya jambo fulani kubwa bila
kujulikana linaloweza kusaidia kuwahamisha watu kifikra toka jambo
jingine lililopo ambalo ni hatarishi zaidi kiutawala.
Njia nyingine ni ile iliyotumika tangu ukoloni ya ‘watawanye uwatawale’ (Divide and rule policy).
Ukiwapa
nafasi au fursa watawaliwa wakakaa, wakapanga wakaelewana na nyie
mpompo tu mkiwaangalia, jua siku watakapozua ajenda ya kushughulika na
wewe, ujue umekwenda. Dawa ni kuwafanya siku zote wasielewane kwa
kuwagonganisha vichwa wenyewe kwa wenyewe tena kwa mambo madogo yasiyo
hitaji gharama kubwa na nguvu nyingi. Tulijadiliana sana na kwa urefu na
Sheikh Ponda juu ya mambo haya lakini hatukupata jibu la mwisho na kwa
bahati mbaya au nzuri Mungu akawa amezisikia dua zake na sala zake za
masaa zaidi ya 18 kila siku akawa amechomolewa Segerea na kuniachia
Sello No. 3. Najua Mungu atatukutanisha tena Inshallah! Ila, isiwe tena
Segerea au Keko ili tuhitimishe mada hiyo.
Siku moja kabla ya
kusomewa hukumu yake na Hakimu Nongwa (9/5/2013) tulijadili sana hukumu
yake kwamba inaweza kuwa ya mwelekeo gani na maamuzi yapi. Panga pangua
ilishindikana kueleweka mambo yatakuwaje kutokana na mazingira
yaliyokuwa yakiizunguka kesi yenyewe. Mawakili wake walikuwa wameifanya
kazi yao vyema bila kubakiza punje ya shaka. Lililokuwa likimpa faraja
zaidi na kesi yake ni kusikia kwamba huyo hakimu ni mama mlokole,
ameokoka. Hiyo ilikua ikimpa moyo sana kwamba atahukumiwa na kupewa haki
yake sawa na lile lililozungumzwa na kuwasilishwa mbele ya hakimu
Nongwa.
Nilimuuliza endapo hukumu itamuweka katika mazingira ya
kumkata makali yake ya kazi ya utetezi anayoifanya na wakati huohuo
upande wa pili wa ‘system’ ukamtaka aanze kutoa ‘Ushirikiano’
atafanyaje? Sheikh Ponda aliniambia kuwa haki huwa hainunuliwi wala
kuombwa bali hudaiwa. Alisema atakuwa tayari kutoa ushirikiano kwa
yeyote yule anayezungumzia utoaji na upatakanaji haki.Na akasema mdomo
na nafsi vilivyodhamiria kuzungumzia na kuitafuta haki huwa havifungiki
kwani vikifungika hata hiyo amani haiwezi kuwepo.
Nikiwa ndani ya
selo nilimsikia Sheikh Ponda akimwaga mistari yake redioni baada ya
kuhukumiwa. Kwa mara nyingine nikazidi kumuaminia Sheikh Ponda kwamba ni
mmojawapo ya watu wachache tulio nao hivi sasa nchini wanaoweza
kutembea na kuishi ndani ya maneno yao.
Lipo jambo moja muhimu
ambalo tulikubaliana na Sheikh Ponda tulijadili na kulifanyia kazi kwa
nia ya kuwanusuru watu wanaosota jela bila sababu endapo tungeliachiwa
na kuwa huru uraiani. Namtafuta kwenye simu hayuko ‘reachable’.
Nikishampata tukashauriana na likaonekana linatekelezeka, nitalitoa
hadharani.
6: USHAURI WANGU MDOGO KWA VIONGOZI WETU WA DINI.
Mimi
ni mtu mdogo sana na muumini wa kawaida ndani ya dhehebu la KKKT.
Lakini natambua kanisa ni waumini na wajibu mkubwa wa kila muumini ni
kuhakikisha anatimiza wajibu wake kama kanisa la Mungu linavyoelekezwa
kupitia maandiko matakatifu ya Biblia. Wajibu mmojawapo sisi kama
waumini ni kuonyana ( Ebr. 10:24 – 25).
Nawaombeni viongozi wetu
wa dini zote wakristo kwa waislamu mtimize wajibu wenu mliokabidhiwa na
Mungu, Imeandikwa kwa dini zote kwamba kila mmoja bila kujali wadhifa
wake atahukumiwa sawa na matendo yake. Nawaomba simamieni na kuuzungumza
ukweli(hata kama ni mchungu) mbele ya watawala na hata watawala
watarajiwa.Ninyi mmepewa mamlaka na Mungu ya kuonya, kukemea, kuelekeza
na kubariki na ndio maana watawala wote wanawaogopa na kuwaheshimu.
Wengine huenda ninyi bila ya kuwatambua hutafuta njia za kujikomba kwenu
ili wakipate wanachokitafuta.Yasemeni wazi na kuyahoji hata yale
machache yanayoonekana au kusikika pasipo kificho.
Muulizeni
Mheshimiwa Rais huyo waziri wake anayezungumzwa kila siku kwamba mchana
kweupe alisema anao maadui zake wawili ambao ni waandishi wa habari na
angewashughulikia, Rais analisemaje hilo? Maadam ni ninyi, nina uhakika
Mheshimiwa Rais atajibu na atachukua hatua stahiki.
Binafsi
nawaombeni kwa heshima na taadhima muache kuwa vuguvugu (si moto si
baridi-Ufunuo wa Yohana 3:15-16) Baadhi yenu acheni kuogopa vivuli vyenu
kwa maana ya kuhofia kunyimwa upendeleo au misaada ya serikali (i.e
misamaha ya kodi) na baadhi kuutumia mwanya huo vibaya. Kama maandiko
yanavyosema JIKANENI WENYEWE.
Lazima mtambue hawa jamaa wakati
mwingine huenda wanaitumia fursa hiyo kama chambo cha kuwanasia pindi
wanapokua wana taarifa zenu zote za fursa ya misamaha iliyotumika
vibaya. “Mnapaswa kushuhudiwa mema na watu walio nje…” (1 Tim 3:2-9)
Binafsi
nawaomba msiwalee wala kuwabeba wale wote wenye dhamira chafu na nia
mbaya ya kutaka kuyatumia madhehebu yenu kukidhi matakwa binafsi kwani
wanachafua taswira zenu nzuri za madhehebu yenu mbele ya waumini wenu na
umma kwa ujumla.
Lakini zaidi ya yote ni imani yangu mimi
binafsi kwamba madhehebu yenu ni makubwa na yana mtandao mkubwa na wenye
nguvu ndani na hata nje ya nchi.Kama inawezekana tumieni mtandao wenu
kuisaidia serikali ambayo vyombo vyake vinaelekea kushindwa kuwabaini
wahalifu wachache wanaoelekea kuchafua na kuivuruga amani tuliyoizoea
ndani ya nchi yetu. Kwa bahati nzuri nimesoma na kusikia kwenye vyombo
vya habari kwamba IGP Mwema amezishauri taasisi za kidini kuanzisha
‘ulinzi shirikishi ndani ya misikiti na makanisa’. Kama mambo serikali
ya CCM imeyafikisha hapo, tumieni fursa hiyo kuziomba taasisi makini
mnazozifikia nje na ndani ya nchi.
7: MTIZAMO WANGU WA MBELE BAADA YA SAKATA LA UGAIDI.
Mimi
kama mimi na wakati huohuo Mkurugenzi wa ulinzi na Usalama wa CHADEMA,
kanuni yangu ya maisha ya kila siku huwa ni kutoangalia yale
yaliyokwisha kuniumiza bali ni kuangalia yanayoweza kuniumiza kuanzia
leo na kwenda mbele.
Ushauri wangu wa namna gani twende katika
kukilinda chama kwa ujumla wake nitawasilisha mbele ya mamlaka na vyombo
husika vya Chama.Lakini rahi kwa wanachama wa CHADEMA na wapenda
mabadiliko ya kweli wote nchini, ni kulichukua jukumu la kuzilinda
harakati hizi zinazoendelea kama jukumu letu wote na kila mmoja kujiona
anahusika na anaguswa. Chukua hatua kuyadhibiti yale unayoweza palepale
ulipo na yanayokushinda toa taarifa au tafuta msaada kwa mtandao wa
chama chetu ambao hivi sasa unaendelea kujikita maeneo yote nchini.Asiye
na Uongozi wowote ndani ya chama wala kadi lakini anajisikia kwenye
nafsi kuipenda na kutaka kuitumikia CHADEMA, naomba achukue cheo cha
u-volunteer na aingie kazini kuanzia dakika hii na sisi tutaitambua na
kuienzi kazi yake.
Kwa viongozi wangu wakuu na wale wote
waliopewa dhamana ya kukisimamia na kukiongoza chama katika ngazi na
nyadhifa zozote, Sioni njia ya kutuvusha na kutufikisha haraka
tunakokwenda zaidi ya kuziendesha kazi zetu kwa falsafa ya USIMAMIZI
LAZIMISHI (Lwakatare Theory). Ni kheri ya fedheha kuliko lawama.
Tujitahidi kuyafanyia tafsiri ya kutekelezeka mambo yote tunayoazimia au
kuyapanga kufanyika. Kwa njia hiyo nina uhakika rasilimali zetu
tulizonazo (fedha kidogo watu wengi) zitaweza kutuvusha na kuyashinda
mapambano yaliyo mbele yetu.
Kukaa kwangu mahabusu siku 92
kumenipa fursa ya kuyatafakari mambo mengi kwa kina
yanayonizunguka.Nimeamua NIFUNGUKE. Kufunguka kwangu ni pamoja na
kujitokeza hadharani kwenye mitandao ya kijamii kama hivi sasa
nilivyoamua kufanya jambo ambalo nilikuwa nalikwepa kutokana na watu
wengi kutumia vibaya fursa hii ambayo binadamu ameigundua.
Nilipojiunga
CHADEMA, nilimuuliza mwenyekiti angependa niifanyie nini CHADEMA kama
sehemu ya mchango wangu katika harakati za kutafuta ukombozi
zinazoendelea.Aliniambia kama naweza nitumie uzoefu mdogo niliokuwa nao
kuanzia CUF wa kutengeneza mfumo wa ulinzi na usalama wa chama. Mimi
sijawahi kusomea upolisi, ushushushu wala uanajeshi labda jeshi la
kujenga Taifa mwaka 1982 Makutopora JKT Operesheni wajibu kwa mwaka
mmoja. Lakini pia japo kidogo ujumbe wangu wa muda mrefu ndani ya kamati
ya ulinzi na usalama ya CUF-Taifa, nao unaweza kuwa ulinisaidia kunitoa
tongotongo kwa kiasi Fulani.
Nikiwa gerezani Segerea
nilimshangaa sana ‘bwana mdogo’ Julius Mtatiro-Naibu Katibu mkuu wa CUF
alipozungumza kwenye vyombo vya habari kuwa ;”Lwakatare akiwa CUF
hatukumfundisha ugaidi.” Sikumuelewa hayo maneno alikuwa na maana gani
na alitumwa na nani. Kwanza sijui kipindi hicho nikiwa CUF yeye alikuwa
wapi na sidhani kama kwa wakati huo alifikiria hata kujiunga na hiyo
CUF.Awaulize CUF ‘Original’ kama wapo, Lwakatare alikuwa ni nani ndani
ya CUF.
Hata siku moja haitatokea nibeze uzoefu na msingi wa
kisiasa nilioujenga ndani ya akili zangu na nafsi yangu kutoka CUF. CUF
iliniweka katika ramani ya kisiasa ninayoitumia kutamba hadi leo hii.
CUF ilinijengea nguzo moja kubwa iliyonipaisha kisiasa na inayoendelea
kunisaidia katika kazi niliyokabidhiwa CHADEMA ya ulinzi wa chama hadi
leo ambayo ni UJASIRI WA KUJITOA KWA NAFSI YANGU NA KWA AKILI ZANGU ZOTE
KUIPIGANIA NA KUITAFUTA HAKI BILA KUCHOKA NA KUTOKUBALI DHULUMA NA
UONEVU. ‘HAKI HUWA HULETEWI KWENYE KISAHANI CHA KIKOMBE CHA CHAI, HAKI
HUDAIWA NA KUTAFUTWA.’
Ukisha kuwa na nguzo hiyo, ni silaha tosha
inayoweza kumsaidia mtu yeyote Yule kuyaongoza au kushiriki ipasavyo
katika harakati za kimapambano. Ndio maana leo hii, wapo wanajeshi,
mapolisi, usalama wa Taifa wengi mno ambao serikali ya CCM imewadhulumu
na kuwanyanyasa isivyo kawaida lakini kwa sababu ya kukosa nguzo hiyo
niliyoisema hawathubutu kujitokeza hadharani. Ganzi la CCM la kuwafanya
wawe waoga au wasijitambue limewakolea kwelikweli, hawathubutu
kufurukuta.
Wachache wanaojaribu na kuthubutu kujitokeza
wanapenda wafanye hivyo kwa kutokea mafichoni. Binafsi nawapongeza
angalau hata kwa hilo maana najua ipo siku ambayo haiko mbali, ngoma
itakapokolea watajitokeza hadharani kucheza. Kitendo hiki cha kuvishwa
tuhuma za ugaidi na kikosi cha Mwigulu na CCM wenzake kilitukatisha sana
‘stimu’ ya kazi nyingi tulizokuwa bado tukizipanga. Kwa wahaya
wanasema, “Bampeya ntakamazile…”kwa maana ya kukatishiwa safari kabla ya
kufika mwisho wa safari. Makamanda tukaze buti, tushirikiane kwa dhati
tusonge mbele mpaka kieleweke, neema inakuja.
Afya yangu nikiwa
gerezani imeathirika kidogo na kunilazimisha kufanya vipimo ambavyo
wataalam wamenieleza vinampunguzia mtu maisha yake ya kuishi. Siliogopi
hilo najua tunaye Mungu, hata nikiondoka mimi kesho makamanda wengine
wanaendelea na kazi na kusonga mbele.
Nikiwa gerezani nimezitumia siku zangu 92 kutengeneza andiko la toleo langu la kwanza la kitabu nilichokipa jina;
“USHINDANI NDANI YA MFUMO KANDAMIZI (SAFARI YANGU KISIASA HADI KUTUHUMIWA KUWA GAIDI ASIYE GAIDI).
Nimeona
ni wakati muafaka kwa baadhi ya watu wenye nia nzuri na hata mbaya
wasionijua Wilfred Lwakatare ni nani wanijue maana nikiwa gerezani yuko
mwandishi mmoja wa gazeti la TAZAMA aliandika makala yenye mtazamo wa
kubeza akiuliza, “kwani Lwakatare ni nani?” Maneno yaleyale aliyoyatumia
Waziri Steven Wassira kwa mwandishi Absalom Kibanda.
Naamini
kazi na uzoefu nilioupitia wa uanafunzi hadi chuo kikuu, uafisa utawala
na utumishi serikalini, ujasiliamali, ukulima, ufugaji, uenyekiti wa
mtaa Omukituli Kibeta, uenyekiti wa CUF na CHADEMA mkoa, ubunge wa
jimbo, ukuu wa upinzani Bungeni,uratibu mkuu wa ushirikiano wa vyama vya
CHADEMA, NCCR-Mageuzi, TLP na CUF, unaibu katibu mkuu wa CUF,
ukurugenzi wa ulinzi na usalama CHADEMA, ukuu wa familia ya mke na
watoto wanne na HATIMAYE kujikuta mahabusu nikituhumiwa kuwa GAIDI ASIYE
GAIDI – sio kazi za mchezo. YATAKA MOYO.
Lakini pia nimeona si
vibaya nikaonyesha uzoefu niliopitia kisiasa kwa wengine ili pale
nilipokosea basi wengine wasitumbukie katika makosa yaleyale
niliyoingia. Na kama yapo mazuri ya kujifunza, basi wayachukue na
pengine kuyaboresha zaidi ili yawe chachu ya kuwatengenezea njia katika
kufanikisha malengo yao na hasa ya harakati za kisiasa.Kwa wale
watakaohitaji toleo la kitabu hicho wasisite kuwasiliana nami kwa
kunipigia simu au kutuma ujumbe wa maandishi 0713 237869, 0758 417169,
0786 774697 au barua pepe lwaks62@hotmail.com.
Kwa wale wanaotaka kunisaidia kwa namna moja au nyingine kuhakikisha
toleo hilo linatoka kwa haraka na kwa viwango, nitawashukuru kwa mikono
miwili.
8: USHAURI WANGU WA BURE KWA CCM NA WATANZANIA KWA UJUMLA.
Waswahili
husema ukishikwa, shikamana. Maana tunakoelekea sio siri CCM
wameshashikwa pabaya . CCM hawana namna ya kuyakwepa mabadiliko ya
nyakati. Kukunjwa ni kuzuri kuliko kuvunjwa. “If they can’t change,
changes will change them.”
Watanzania ambao bado wamesinzia tokeni
usingizini. Acheni kugeuzwa mazezeta na CCM kiasi cha kushindwa
kujitambua utu wenu kama watu na ubinadamu wenu kama binadamu wanaoishi
katika Taifa huru. Waache ushamba wa kuendelea kufikiria kwamba bila
kuilamba miguu CCM hawawezi kufanikiwa katika shughuli zao. Ukombozi wa
kifikra ni mkubwa zaidi kuliko ukombozi wa kutoka utumwani.
Wajiulize
wataendelea kuishi maisha ya kila kitu ‘deal’ na uchakachuaji mpaka
lini? Hawaoni kuwa ni utumwa wa kujitakia wenyewe? Naona hata baadhi ya
hizi kesi zinazofunguliwa ni zenye msukumo wa ‘DEAL’. Wafanyakazi na
watendaji ndani ya serikali na taasisi zake nawashauri anzeni kubadilika
na kujipanga kifikra tayari kutumika chini ya utawala wa chama
chochote. Anzeni kujiunga na chama chenu cha AGIP (Any Government In
Power) ambacho sio lazima kisajiliwe wala kutoa kadi.
9: SHUKRANI.
Kipindi
cha kukaa kwangu gerezani kililikua cha mtihani mkubwa kwangu ambacho
kimenipa mafunzo tosha katika maisha. Gerezani sio mahala pa kumuombea
au kuombea mtu kupelekwa . Ni mahala ambapo kwa wengine panakua chanzo
cha familia kugombana, kufarakana, kusambaratika, ndoa kuvunjika na
uadui kujengeka baina ya mtu na mtu, na mengine mengi. Baadhi
nimeyashuhudia mimi mwenyewe kwa macho yangu.
Binafsi nashukuru
kwa ukaribu niliopewa na familia, ndugu, jamaa, marafiki, viongozi wa
chama, wanachama na wanajela wenzangu. Ukaribu wao wa muda wote
uliifanya siku iwe fupi.Sio siri ndugu zangu, unapotembelea ndugu yako
aliyeko gerezani furaha unayomuachia mule ndani haipimiki.
Namshukuru
sana mke wangu Angel Mercy kwa kukikabili kipindi chote hicho kigumu
kwa kunipa huduma, kufuatilia afya yangu, kuiangalia na kuitunza familia
iliyopo nyumbani na watoto walioko mashuleni licha ya yeye mwenyewe
kukabiliwa na masomo chuoni,Mzumbe-Mbeya.
Nawashukuru sana ndugu
zangu kaka, dada zangu, ndugu, marafiki, majirani na watoto wetu wote
kwa misaada waliyonipa kupitia kwa mke wangu lakini kubwa kuliko yote
kitendo chao cha kuja kuniona gerezani. Nikishukuru chama, (CHADEMA) kwa
kunipigania na kunitolea misaada isiyohesabika. Kipekee nimshukuru sana
Katibu Mkuu Dr. Slaa kwa ufuatiliaji mkubwa alioufanya.
Pongezi
na shukrani nyingi kwa jopo zima la mawakili mahiri. Peter Kibatala,
Tindu Lissu, Mabere Marando, Prof. Abdallah Safari na Nyoronyo
kichehere, ambao najua bado tuko pamoja katika ngwe ya pili ya kesi ya
shitaka moja ambalo bado linanikabili na huenda na mazagazaga mengine
yanayoweza kujitokeza.
Nivishukuru kwa namna ya pekee vyombo vya
habari vilivyofuatilia na vinavyoendelea kufuatilia sakata zima la kesi
yangu na kuifahamisha jamii kujua kinachoendelea. Niwape pole na
shukrani nyingi wale wote waliofika gerezani na kushindwa kuniona
kutokana na idadi kuwa kubwa kuliko idadi ya watu walioruhusiwa kuniona.
Kipekee
nimshukuru sana Baba Mchungaji wa usharika wetu wa King’ong’o Kimara na
mke wake. Mr & Mrs Rev Joseph Kyaka walionitembelea na kunijengea
moyo wa imani, matumaini na faraja. Niwashukuru wote waliokuwa pamoja
nami kifikra na kimaombi na ninasema kwa maombi yenu, yote yamewezekana.
Mungu anasikiliza maombi na haachi kujibu.
Nimuombe Mungu azidi kututangulia na kutupa ujasiri wa kukabiliana na adui na kumshinda shetani huku tukidumu katika imani.
IN GOD I TRUST.
IMEANDALIWA NA:
WILFRED MUGANYIZI LWAKATARE
MKURUGENZI WA ULINZI NA USALAMA CHADEMA.
No comments:
Post a Comment