ZIARA ya
Rais wa Marekani, Barack Obama hapa nchini, ‘imeivua nguo’ Serikali ya
Tanzania, baada ya vyombo vya habari vya kimataifa kutoa tuhuma nzito za
vitendo vya kikatili vinavyodaiwa kufanywa na vyombo vya dola dhidi ya
raia.
Hatua hiyo
inayodaiwa kujaribu kufichwa kwa nguvu kubwa na baadhi ya watendaji wa
serikali, imekuja kufuatia baadhi ya vyombo vya habari mashuhuri nchini
Marekani, kuibua upya tuhuma za utekaji, upigaji na uuaji wa raia,
waandishi wa habari na wanaharakati nchini Tanzania.
Moja ya
chombo kilichoanika uovu huo, ni gazeti kongwe na mashuhuri
linaloheshimika sio tu Marekani, bali na mataifa makubwa la New York
Times, ambalo Julai 1, 2013, lilichapisha habari isemayo ‘Matukio ya
udhalimu yaongezeka Tanzania, Kisiwa cha Amani Afrika’.
Habari hizo
zilizoandikwa na mwandishi maarufu wa habari za uchunguzi duniani,
Nicholas Kulish zimeeleza tukio la kusikitisha la kutekwa nyara na
kuumizwa vibaya kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk.
Stephen Ulimboka, kama moja ya tukio baya ambalo linadaiwa kuwa na mkono
wa serikali, ingawa Rais Jakaya Kikwete aliwahi kukanusha madai hayo.
Mwandishi
huyo ameeleza namna Dk. Ulimboka alivyotekwa na kupakiwa kwa nguvu
katika gari linaloaminika kuwa la moja ya vyombo vya usalama, kupigwa
kwa kikatili kwa nyaya, kung’olewa kucha, na jinsi watesaji
walivyoshauriana njia ya kumuua ikiwemo kumkanyaga na gari ama sindano
ya sumu.
Mwandishi
huyo, amemnukuu, Dk. Ulimboka akisema namna alivyowasikia watesaji wake,
wakimwambia kuwa ‘atalipa yote aliyotenda’ na kumtaka asali na kumwomba
Mungu wake, kwa sababu hataiona dunia tena.
Aidha,
gazeti hilo limeieleza dunia kutekwa kwa waandishi wa habari na kuuawa
kikatili kwa mwandishi wa habari, Daud Mwangosi aliyeuawa na askari
polisi akiwa kazini, katika Kijiji cha Nyororo, mkoani Iringa, mwaka
jana.
Katika
kuonesha uzito wa tuhuma hizo na namna wananchi wa Marekani wanavyotaka
lishughulikiwe haraka, moja ya taasisi kubwa inayotetea waandishi wa
habari duniani, yenye makazi yake jijini New York, ilimwomba Rais Obama
kumkabili Rais Kikwete watakapokutana katika ziara yake iliyomalizika
jana, juu ya matukio hayo na uhuru wa vyombo vya habari.
Kadhalika,
gazeti hilo limeanika matukio mawili ya mashambulizi ya mabomu
yaliyofanywa jijini Arusha kwenye Kanisa la Katoliki la Olositi na
katika mkutano wa chama cha upinzani, (hawakukitaja) na kusababisha vifo
vya watu saba.
Gazeti hilo
pia limeeleza kwa kirefu namna shambulio la bomu la kurushwa kwa mkono
lilivyotokea katika mkutano wa CHADEMA hivi karibuni huko jijini Arusha,
na shutuma zilizotolewa na chama hicho dhidi ya Jeshi la Polisi
kuhusika na kumtorosha aliyelipua bomu hilo.
Kadhalika,
limenukuu msimamo wa CHADEMA wa kukataa kukabidhi kile kinachosemakana
‘mkanda mzima’ wa tukio hilo kwa polisi, hadi pale itakapoundwa tume
huru kuchunguza tukio hilo.
Msimamo huu
wa New York Times, wa kuichimbua Tanzania na kuyaanika maovu yake yote
unaungwa mkono pia na magazeti mengi nchini Marekani, kama vile USA
Today, ambalo nalo limechapisha habari zenye msimamo kama huo,
likionesha wazi namna ziara ya Rais Obama ilivyotoa fursa ‘kumulikwa’
kikamilifu kwa matukio mabaya yaliyoikumba nchi.
Inadaiwa
kwamba mara baada ya waandishi hawa wa Marekani kupata taarifa kutoka
kwa Wizara ya Nje ya Marekani (State Department), juu ya ziara ya Obama
hapa nchini, walianza kujipanga kufichua maovu yanayotendwa na Serikali
ya Kikwete.
Vyombo
hivyo, vikafichua matukio mabaya yakiwemo uvunjwaji wa haki za
kibinadamu, matukio ya matumizi ya nguvu kupita kiasi kwa upande wa
polisi, kutokamilika kwa uchunguzi kwa matukio ya kihalifu na uhasama
baina wa wafuasi wa chama tawala na wale wa upinzani,
Mbali na matukio hayo, vyombo hivyo, kinyume na vya hapa nchini ambavyo vimesifia ziara ya Obama, vimejikita kuibua uozo uliopo, likiwemo pia suala la kukithiri kwa uchafu katika Jiji la Dar es Salaam.
Mbali na matukio hayo, vyombo hivyo, kinyume na vya hapa nchini ambavyo vimesifia ziara ya Obama, vimejikita kuibua uozo uliopo, likiwemo pia suala la kukithiri kwa uchafu katika Jiji la Dar es Salaam.
Chombo kingine kilichoandika mabaya ya Tanzania ni wavuti ya eTurbroNews ambayo inaandika kuhusu masuala ya utalii.
Watuti hiyo,
Julai 1, 2013, iliibua habari za uchafu uliokithiri jijini Dar es
Salaam, na kulitaja kuwa mojawapo ya majiji yanayosifika kwa uchafu
likishika nafasi ya 12 duniani.
Habari hiyo
imeushutumu uongozi wa jiji kwa kuamka dakika za majeruhi kufanya usafi
na kujiuliza ilikuwaje wasubiri hadi ziara ya Obama kufanya kazi hiyo.
Aidha,
habari hiyo imezungumzia kero ya kunguru weusi, na kushauri pengine
ianzishwe kampeni ya watu kutoka nje kuja kuwawinda na kuwaangamiza
kabisa, kama mchezo wa uwindaji, kwani sasa idadi ya kunguru hao
waharibifu inazidi milioni moja.
Chanzo:CHADEMA Social Media.
No comments:
Post a Comment