UAMUZI wa
Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kukataa
kuwasilisha ushahidi wa mauji ya mlipuko wa bomu uliotokea jijini
Arusha, umeliweka njia panda Jeshi la Polisi na hivyo kushindwa kuchukua
hatua.
Licha ya jeshi
hilo kumhoji Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, na kumtaka
awasilishe ushahidi huo, kiongozi huyo amekataa agizo hilo akisema kuwa
wamekubaliana kuutoa ushahidi huo kwa tume huru ya majaji endapo Rais
Jakaya Kikwete ataiunda kama walivyomuomba.
Chanzo chetu
ndani ya jeshi hilo, kimedokeza kuwa msimamo huo wa CHADEMA umeliweka
njia panda na hivyo kushindwa kuchukua hatua za kuwabaini watuhumiwa wa
tukio hilo na kuwafungulia mashtaka kutokana na mkanganyiko wa taarifa
zinazotolewa.
Jeshi hilo
linadaiwa kuwa awali lilitaka kujiegemeza kwenye kauli za kisiasa za
baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na serikali ili
kuonyesha kuwa CHADEMA ilisababisha mlipuko huo yenyewe kwa ajili ya
kuwahadaa wafuasi na kujitafutia umaarufu.
Hata hivyo,
mbinu hiyo ya kutaka kuwasakama baadhi ya viongozi na wafuasi wa CHADEMA
inadaiwa kufifishwa na tamko la Mbowe pamoja na mbunge wa Arusha Mjini,
Godbless Lema, kwamba chama kina ushahidi unaoonyesha kuwa tukio hilo
lilifanywa na polisi.
“Hapa kuna
mkanganyiko hasa baada ya Mbowe kudai wanao ushahidi wa video ya tukio
hilo. Wakubwa wetu wamegawanyika na kujikuta wakitoa kauli za kukinzana
maana wanahofia wakiwafungulia kesi watu wengine mashtaka halafu CHADEMA
ikaonyesha ushahidi tofauti itakuwa ni aibu,” kilisema chanzo chetu.
Kwa mujibu wa
chanzo hicho, jeshi hilo mkoani Arusha lilikuwa limewakamata watu wawili
raia wa kigeni likiwatuhumu kuhusika na mlipuko huo lakini baada ya
Mbowe kugoma kupeleka ushahidi huo, watuhumiwa hao hawakuweza
kufunguliwa mashtaka.
Pia katika
hali ya kushangaza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, alikaririwa
na baadhi ya vyombo vya habari kuwa makachero wa Taasisi ya Uchunguzi ya
Marekani (FBI) wamefika mkoani Arusha kuchunguza jambo hilo.
Hata hivyo
taarifa kutoka ubalozi wa Marekani zilikana FBI kuingia nchini
kuchunguza jambo hilo hivyo kusababisha mkanganyiko wa tukio hilo
lililovuta hisia kubwa ndani na nje ya nchi.
CHADEMA mara
kwa mara imekuwa ikilituhumu jeshi la polisi na makada wa CCM kuendesha
harakati za kukidhoofisha kwa kutumia matukio mbalimbali yanayofanywa na
chama hicho cha upinzani.
Mmoja wa
viongozi wa CHADEMA ameliambia Tanzania Daima, kuwa polisi walikuwa
wamepanga kuwatumia FBI kuuhabarisha umma kuwa CHADEMA ilihusika na
ulipuaji huo bomu lakini kutokana na mazingira yaliyopo wameshindwa
kutekeleza uovu huo.
“Unajua hila
za polisi na CCM kila siku zinabadilika lakini kwa bahati mbaya hawajui
kuwa wananchi wanajua kinachofanyika, kuna askari hawaridhiki na uovu
unaofanywa na wenzao,” alisema kiongozi huyo.
Tanzania
Daima, iliwasiliana na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert
Manumba, kuhusu sakata hilo ambapo alikataa kulizungumzia akidai msemaji
wa jeshi hilo Advera Senso anayo majibu.
Hata hivyo
Senso hakuwa tayari kulizungumzia akisema kuwa alikuwa eneo baya na
akitoka eneo hilo angelijulisha gazeti hili lakini mpaka tunakwenda
mitamboni hakutimiza ahadi hiyo.
Mlipuko huo
ambao ulisababisha vifo vya watu wanne na wengine zaidi ya 60
kujeruhiwa, ulitokea Juni 15 mwaka huu wakati wa kuhitimisha kampeni za
uchaguzi mdogo wa madiwani jijini humo, zikiwa zimepita dakika chache
baada ya Mbowe kumaliza kuhutubia na kutelemka katika jukwaa
lililokokuwa limeelekezwa bomu hilo.
Siku moja
baada ya tukio hilo, serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, ilitoa taarifa
tata bungeni ikionyesha kulikingia kifua jeshi la polisi na kuwatwisha
lawama viongozi wa CHADEMA.
Lukuvi alisema
kuwa mkutano wa CHADEMA ulikuwa na ulinzi wa polisi wenye magari mawili
waliosimama upande wa kaskazini ya uwanja na mrushaji wa mlipuko huo
akiwa upande wa mashariki ya uwanja huo na kurusha kuelekea magharibi.
“Jaribio la
askari kutaka kumfuata aliyerusha mlipuko huo zilizuiliwa na makundi ya
wananchi ambao walianza kuwashambulia askari kwa mawe na kuwazomea na
hivyo polisi kulazimika kuanza kujiokoa badala ya kumsaka mhalifu huyo.
“Hivi karibuni
zimekuwepo jitihada za makusudi za baadhi ya vyama vya siasa, makundi
ya kijamii na watu binafsi kupandikiza chuki ya raia dhidi ya vijana
wetu wa polisi, kuwafanya raia wawachukie, wasiwaamini, wasiwape
ushirikiano na kuifanya nchi isitawalike,” alisema Lukuvi.
Aliliongeza
kuwa kufanikiwa kutoroka kwa mhalifu wa tukio hilo ni matokeo ya
uchochezi unaofanywa kwa makusudi na baadhi ya wanasiasa dhidi ya
serikali na polisi na hivyo kuwafanya wananchi wajenge chuki dhidi ya
polisi.
Siku chache
baadaye viongozi wa CCM pamoja na baadhi ya mawaziri kana kwamba
wanafahamu mlipuaji wa bomu hilo, waliitwisha lawama CHADEMA wakidai
ilihusika na tukio hilo ingawa hadi leo hakuna aliyehojiwa na polisi
kati yao kuthibitisha tuhuma hizo badala yake Mbowe pekee ndiye
anaandamwa awapelekee ushahidi.
Makada hao ni
Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), Mwigulu Nchemba, na Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),
Hawa Ghasia, ambao walidai kuwa CHADEMA ndiyo imekuwa ikihusika na
vurugu zote zinazohusisha mauaji nchini.
Kauli za
viongozi hao zilitplewa baada ya Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya
Chama cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kudai kuwa
wanao ushahidi wa kutosha kuwa CHADEMA iliandaa na kuratibu shambulio
hilo.
“Ni lazima
tuwaze na kuvuka mipaka, kuna mambo ambayo yanawezekana kabisa yakawa
yamejificha pale. Watu wanaangalia, wanaojitoa ufahamu wanafikiria CCM
inaweza kushiriki.
“Mimi
niwaambie CCM hata bila kushiriki ni moja kwa moja inawekwa kwenye
lawama jambo kama hilo likitokea. Ila CCM haina ushiriki katika jambo
kama hili kwa sababu ndio watu wake kupitia serikali yake wanatakiwa
kuwahakikishia usalama,” alisema.
Mwigulu ambaye
pia ni mbunge wa Iramba Magharibi aliongeza kuwa hata video ya mauji ya
Arusha iliyowekwa kwenye mtando wa You tube inaonesha wazi kuwa
yalipangwa.
“Yule
aliyekuwa anachukua video eti hakushtushwa kabisa na lile bomu,
aliendelea kufuatilia kama vile ni mkanda wa harusi. Iliwahi kutokea
wapi mchukua video kwenye mkutano wa hadhara kitu ambacho hakikupangwa
kimelipuka, kinaua watu, yeye anendelea kama anachukua send off?”
alihoji.
Ghasia naye
alidai kuwa CHADEMA wamechochea vurugu Mtwara, Mwanza, Mbeya, Morogoro
na sasa Arusha ili maeneo hayo yasipate maendeleo.
Kutokana na
mlipuko huo, CHADEMA ilitangaza kuanza mpango wa kutoa mafunzo kwa
vijana wake kwa ajili ya kulinda mikutano na viongozi wake lakini CCM,
polisi na Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, walikionya chama
hicho wakidai kuwa hatua hiyo ni kinyume cha sheria za nchi, Katiba na
sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992.
Hata hivyo
hoja zao zilipingwa vikali na baadhi ya wadau wa siasa na wananchi
wakihoji walikuwa wapi kwa kutoionya CCM ambayo ina kikundi cha vijana
cha Green Guard ambacho kinapewa mafunzo ya kijeshi na matumizi ya
silaha za moto.
Julai 17 mwaka
huu, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, alimwandikia
Mbowe barua na kumwamuru awasilishe ushahidi wa video aliyodai kuwa nayo
ikiwaonesha baadhi yao walivyoshiriki kwenye tukio la mlipuko wa bomu
Arusha kabla ya Julai 23 mchana saa nane.
Katika hatua
ya kuchanganyana, jeshi hilo Juni 20 mwaka huu, kupitia kwa Mkuu wa
Mafunzo na Operesheni, Paul Chagonja, aliwaeleza wanahabari kuwa Mbowe
anapaswa kuwa mkweli na kuacha kuuchezea umma kwa alichowaeleza polisi
ni tofauti kwani hana ushahidi huo.
Lakini katika
hatua ya kushangaza Chagonja huyo huyo ndiye amemwamuru Mbowe kupeleka
tena ushahidi huo polisi akitamba kuwa baada ya kukaidi kufanya hivyo,
polisi inao makachero wake wanaojua jinsi gani ya kuendelea na kazi
hiyo.
Pamoja na
polisi kudai Mbowe hana ushahidi, Julai 10 mwaka huu usiku wa manane
askari kadhaa wakiwa na silaha walifika nyumbani kwake wamkisaka bila
mafanikio wakitaka awapatie video hiyo.
Hata hivyo,
kesho yake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alidai
hana taarifa za askari wake kufika nyumbani kwa Mbowe.
Muda aliopewa
Mbowe umemalizika bila kuwasilisha ushahidi huo, akidai kuwa hawezi
kwenda kinyume na msimamo wa chama kwani jeshi hilo ni watuhumiwa kwenye
tukio hilo la Arusha.
Juzi jeshi
hilo lilimtaka Mbowe kuwasilisha msimamo huo wa utetezi wake kwa
maandishi leo ambapo kiongozi huyo wa upinzani alisema mwanasheria wa
chama hicho ataandaa maelezo hayo.
Chanzo:CHADEMA Social Media.
No comments:
Post a Comment