LICHA ya
hujuma ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ufanisi mdogo wa Tume ya Uchaguzi
ya Taifa, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeibuka na
ushindi mnono katika uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata nne za jijini
Arusha.
Katika Kata
ya Elerai, mgombea wa CHADEMA Injinia Jeremia Mpinga alimbwaga Emanueli
Laizer wa CCM kwa kura 1,715, dhidi ya 1,239.
Kata hiyo
ilikuwa na wapiga kura 23,797 waliojiandikisha na vituo 55 vya kupigia
kura, lakini idadi kubwa ya wananchi hawakujitokeza.
Matokeo ya
kura yalitangazwa chini ya ulinzi mkali wa askari polisi zaidi ya 40
wenye silaha, na kupokelewa kwa shangwe kubwa na wafuasi na mashabiki wa
CHADEMA.
Katika Kata
ya Kaloleni, mgombea wa CHADEMA, Kessy Emmanuel Miliare alimshinda kwa
mbali mgombea wa CCM kwa kura 1,470 dhidi ya 530, wakati mgombea wa CUF
ameambulia kura 275. waliojiandikisha 12,674 waliopiga kura 2,292. Kura
halali ni 2,277 na zilizoharibika 15.
Akitangaza
matokeo katika Kata ya Themi, Msimamizi wa Uchaguzi, Editha Mboye
alimtangaza mgombea udiwani wa CHADEMA, Mallance Kinabo kuwa mshindi kwa
kupata kura 678, akimwacha mbali mgombea wa CCM Victor Mkolwe aliyepata
kura 326, huku yule wa CUF, Lebora Ndervai akipata kura 313.
Kata ya Kimandolu, CHADEMA pia wameibuka na ushindi mkubwa na kuiacha vibaya CCM.
Mgombea wa CHADEMA, Elishadai Ngowi amemshinda mgombea wa CCM, Edina Sauli kwa kura 2,265, dhidi ya 1,169 za mpinzani wake.
Mara baada
ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Jiji la Arusha lilizizima kwa shangwe na
nderemo, huku idadi kubwa ya watu wakijipongeza kwa ushindi huo mkubwa.
Mwigulu Nchemba atimua
Matokeo hayo
ambayo yameonekana kuwasononesha viongozi na wanachama wa CCM,
yalimfanya Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba, kuondoka kimya
kimya jijini hapa kwa kutumia gari maalumu.
Mwigulu
ambaye aliongoza kikosi cha CCM katika kampeni za kimya kimya, majira ya
jioni alionekana akielekea Moshi, huku wasaidizi wake wakiwemo wabunge
wakitoweka katika vituo vya kuhesabia kura.
Mapema,
wabunge wa CHADEMA na wa CCM tangu asubuhi walikuwa wakizunguka katika
kata hizo, huku Mbunge wa Viti Maalumu, Catherin Mgige (CCM) akitumia
gari ndogo, Salon yenye vioo vya giza alionekana akizunguka kata zote
jana.
Ulinzi mkali wa polisi
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatusi Sabas jana aliongoza kazi ya ulinzi
uliokuwa na idadi kubwa ya askari polisi wenye silaha za moto na mabomu
ya machozi.
Akitumia
gari aina ya Toyota Land Cruiser yenye namba TP 1715, Kamanda Sabas
alionekana akizunguka katika mitaa ya kata zote nne, zilizokuwa
zimesheheni idadi kubwa ya askari, wengi kutoka mkoani Kilimanjaro.
Waangalizi wa kimataifa
Katika tukio
la kwanza la kihistoria, uchaguzi wa kata hizo ulishuhudiwa na
waangalizi wa kimataifa kutoka taasisi ya International Low and Policy
Institute yenye makao makuu yake nchini Norway, na wale wa ndani kutoka
Jukwaa la Katiba.
Kiongozi wa
waangalizi kutoka Norway, Sterling Roop, akiongea na Tanzania Daima
alisema kuwa idadi ndogo ya wapiga kura imejitokeza na uwepo wa dosari
kadhaa umewafanya baadhi ya wananchi kukosa haki yao ya kupiga kura.
Roop alisema
pamoja na wananchi kuwa na shahada halali za kupigia kura na majina yao
kuwepo, lakini hakukuwa na picha zao katika daftari la wapiga kura na
hivyo wakazuiwa kupiga kura.
Katika vituo
vingi, hususani Kata ya Kaloleni dosari kuu ilikuwa ni kukosekana kwa
majina katika daftari la kupiga kura kwa wananchi ambao wana shahada na
pia majina yao kubandikwa katika ofisi za kata kama wapiga kura halali.
Majina ya wapiga kura yatoweka
Dosari kubwa
iliwakumba wapiga kura baada ya majina, picha na maelezo kukosekana
kwenye daftari la wapiga kura karibu katika kata zote.
Makamu
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Hamid M Hamid alikiri tatizo
hilo na kudai kwamba tayari alishawasiliana na wataalamu wake wa mifumo
ya kompyuta (IT) ili washughulikie kasoro hizo kwenye kila kata
iliyokuwa ikiendelea na uchaguzi.
Hata hivyo,
alisema kuwa yeye si mchawi kuweza kubaini chanzo cha hitilafu hizo
zilizojitokeza. Baadhi ya upungufu uliobainika ni baadhi ya watu
kuandikishwa zaidi ya mara moja.
Kata ya
Kaloleni kwenye kituo cha AICC Nursery B, mpiga kura Michael Laurence
alikuwa ameandikishwa mara tatu kwenye daftari la wapiga kura akiwa na
namba 48674955, 444666858 na 13142914.
Hata hivyo
kwenye majira ya saa saba mchana, wataalamu wa kompyuta wa Tume ya
Uchaguzi walifika na kuanza kuwasaidia wananchi waliokuwa wamejazana
kwenye kituo cha kata hiyo.
Mmoja wa
wataalamu hao, Siif Mtezo aliwaeleza waandishi wa habari kuwa tatizo
hilo lilisababishwa na watu kujiandikisha zaidi ya mara moja.
Alisema
kilichowafanya wengi washindwe kuona majina yao ni hofu kama ile
inayowakumba wanafunzi wanaoenda kuangalia matokeo, na kwamba tume
ililazimika kuwapigia simu wananchi wengi waliokuwa wameondoka, na
wakarudi kupiga kura.
Wakala wa
Chama cha Wananchi (CUF), Malik Abbas kwenye kituo hicho aliwaeleza
waandishi wa habari kuwa wananchi wengi walifika, lakini majina yao
hayakuonekana na wakaondoka, huku akionyesha baadhi ya picha ambazo
hazionekani vizuri kutokana na kufifia kwenye daftari hilo.
Mgombea
udiwani wa kata hiyo kwa tiketi ya CUF, Abbas Darwesh alisema wananchi
wengi walishindwa kupiga kura akiwemo mtoto wake Omary Othman ambaye
pamoja na kuwa na kitambulisho chake namba 32479962 jina lake
halikuonekana kwenye orodha.
“Inawezekana
kweli kuna mchezo mchafu umefanyika kubadili daftari la wapiga kura
kama ambavyo tetesi zilikuwa zimezagaa, kwa sababu mtoto wangu mwenyewe
alipiga kura kwenye kituo hiki katika uchaguzi wa 2010, lakini leo
naambiwa jina lake halipo,” alilalamika Darwesh.
Msimamizi wa
uchaguzi Kata ya Kaloleni, Anna Lebisa amekiri kukosekana kwa majina ya
wananchi katika daftari licha ya kuwepo katika mbao za matangazo na
kusema hawakuruhusiwa kupiga kura.
Miongoni mwa
waliokumbwa na kadhia hiyo ni Omari Othmani na mtangazaji wa TBC,
Khalifa Mshana ambaye alilazimika kulifikisha suala lao kwa Makamu
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji mstaafu Hamid Mahmood
ambaye alimuachia ofisa wa tume kulishughulikia.
Mwenyekiti
wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba akiwa na timu yake ya waangalizi wa
uchaguzi huo, alisema kura zimeanza kupigwa taratibu na idadi ndogo ya
watu kujitokeza akidai kumechangiwa na hofu kubwa baada ya kuwepo kwa
askari wengi katika vituo vya kupigia kura.
“Wingi wa
askari wenye silaha za moto katika vituo vya kupigia kura umechangia
kufanya baadhi ya wananchi kutojitokeza kwa hofu ya askari hao,’’
alisema Kibamba.
Wafuasi wa CHADEMA watekwa, wapigwa
Matukio ya kutekwa na kupigwa kwa wafuasi wa CHADEMA yalijiri katika uchaguzi huo jana.
Vijana
wanaoaminika kuwa ni wa CCM, wakiwa ndani ya gari aina ya Land Cruiser
iliyoegeshwa kwenye uwanja wa AICC wa Soweto waliwakamata na kuwapiga
baadhi ya wananchi waliokuwa wakielekea katika vituo vya kupigia kura
eneo la Soweto.
Msimamizi wa
uchaguzi wa Kata ya Kaloleni, Lebisa alikiri kuliona gari hilo majira
ya saa tatu asubuhi. Aliwaelekeza polisi waliokuwa kwenye kituo hicho
kuwafuatilia, lakini waliondoka kabla hawajakamatwa.
Aidha,
mwananchi mwingine, Hassan Noor ambaye alikuwa wakala wa CHADEMA kwenye
kituo cha AICC Nursery alishindwa kufanya kazi hiyo baada ya
kunyang’anywa barua yake na vijana waliokuwa kwenye gari aina ya Land
Cruiser ya rangi ya maziwa ambayo namba zake hakuzishika.
Akiongozana
na wenzake wawili kwenye mzunguko karibu na kituo hicho cha kupigia
kura, Noor aliona gari hilo likisimama karibu yao na kuwataka waondoke
eneo hilo. Aliwaeleza kuwa ni mawakala, ndipo walipomtaka awaonyeshe
barua.
“Nilijua ni
askari, na nilipowapa wakaninyang’anya na kuichana. Kisha wakampiga
mwenzangu Boniface Kimaro. Alipigwa na kitu kama chuma kichwani na
wakaondoka. Tumeripoti Kituo cha Kati cha Polisi,” alisema.
Katika Kata
ya Kimandolu, watu sita walikamatwa wakiwa wamekaa katika gari moja na
kupelekwa polisi kwa mahojiano, hali hiyo ikajitokeza tena katika Kata
ya Kaloleni pia, ambako watu wasiojulikana walikamatwa wakiwa
wamejificha ndani ya gari.
Chanzo:CHADEMA Social Media.
No comments:
Post a Comment