VITUKO na
matukio ya hatari kwenye mikutano ya CHADEMA vimeendelea kushika kasi.
Jana Mbunge wa
Ubungo, John Mnyika alinusurika kupigwa na bomu la machozi lililorushwa
na polisi waliokuwa wakizuia kufanyika mkutano ulioitishwa na chama
hicho.
Tukio hilo
lilitokea katika eneo la Mabibo kwenye viwanja vya Sahara ambapo bomu
hilo lilimpata mtu aliyekuwa karibu na Mnyika anayeitwa Thomas Jerome,
aliyejeruhiwa sehemu ya paja.
Baada ya
kurushwa kwa bomu hilo, polisi walitaka kumchukua majeruhi huyo ili
wamweke kwenye gari lao apelekwe hospitalini, lakini Mnyika aliwaelekeza
wafuasi wa CHADEMA kumchukua kwa madai kitendo kilichofanywa na askari
hao kililenga kuficha ushahidi wa jambo hilo.
Polisi
waliokuwemo eneo la tukio waliamua kukubaliana na matakwa ya wafuasi wa
CHADEMA waliomchukua Jerome na kumpeleka hospitali ambako hali yake
inadaiwa inaendelea vizuri.
Akielezea hali
ilivyokuwa akiwa katika mkutano mwingine uliofanyika Ubungo, Mnyika
alisema polisi walifika katika viwanja vya Sahara wakiwa na magari
matatu kwa lengo la kutawanya wafuasi wa CHADEMA wasifanye mkutano
wakidai haukuwa na baraka za jeshi hilo.
Mnyika alisema
polisi hao walisema sababu ya kuuzuia mkutano huo ni uwepo wa ziara ya
Makamu wa Rais katika Wilaya ya Kinondoni, hivyo walikuwa wameelekeza
nguvu zao katika ziara hiyo, kwamba hawakuwa na uwezo wa kuulinda
mkutano wa CHADEMA.
“Nikiwa
nimejiandaa kupanda jukwaani ndiyo polisi walikuja kusema tuache
tusifanye mkutano, nilisogea karibu na gari kumlalamikia ofisa wa polisi
kwani kitendo cha kuahirisha mkutano kwa barua waliyoileta saa sita
mchana siku ya mkutano wakati sisi tuliwapa taarifa siku nne zilizopita
ilikuwa sio haki.
“Nilimwambia
ofisa huyo wa polisi kuwa nilikuwa najadiliana kwa simu na viongozi
wakuu wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Inspekta
Jenerali wa Polisi Said Mwema kumlaumu kutumika vibaya kwa Jeshi la
Polisi.
“Nilipokuwa
bado najibizana naye bila fujo zozote, bomu lilirushwa kutoka ndani ya
gari ya polisi na kupita karibu na mimi likamjeruhi mtu aliyekuwa karibu
yangu, ki ukweli nimeshangazwa sana na matumizi mabaya ya silaha za
moto,” alisema.
Aliongeza kuwa
katika purukushani zilizotokea baada ya bomu kupigwa, alipoteza nyaraka
mbalimbali alizokuwa amebeba kama ushahidi kuwaonyesha wafuasi wa chama
hicho hasa jinsi serikali ya CCM na wabunge wake walivyopitisha kodi ya
huduma za simu, na kodi ya laini za simu.
Slaa
anena
Aidha katika
mkutano huo ambao awali ulitangazwa kuwa ungehutubiwa na Katibu Mkuu wa
chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, haukuweza kuhutubiwa naye kwa kile
alichosema kuwa watu wake wa usalama walimwambia mapema hali si salama
kwenye mkutano huo.
“Nilipata
taarifa kutoka vyanzo vyangu kuwa polisi walikuwa na mpango wa kuleta
fujo, hivyo nikaona kwa kuwa wanatuwinda nisingeenda kuhutubia, pengine
bomu lililomkosa Mnyika lilikusudiwa kwangu au kwa mwingine,” alisema
Dk. Slaa alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu baada ya
kutoonekana mkutanoni.
Jeshi la
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, jana liliahirisha mkutano huo wa
CHADEMA kabla viongozi hao kupanda jukwaani.
Liliwapelekea
barua ya zuio CHADEMA inayosomeka: “Kumbuka barua ya tarehe 17 Julai,
yenye kumb. CHADEMA/MKT/UBUN/015/2013 uliyomwandikia Kamishna wa Polisi
Kanda Maalumu Dar es Salaam. Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam amezuia kufanyika kwa mkutano huo tarehe 21 Julai 2013 katika
viwanja vya Sahara, Mabibo kwa sababu siku mliyoomba kufanya mkutano
wenu wa hadhara, Wilaya ya Kinondoni ina mapokezi ya ugeni wa ziara ya
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Hata hivyo
Mnyika alipinga sababu hiyo ya polisi kwa madai CHADEMA wamepeleka
taarifa kwa Jeshi la Polisi tangu Julai 17 kwamba wangefanya mkutano
katika viwanja hivyo Julai 21, lakini jeshi hilo halikuwajibu hadi
walipokuwa wanaenda mkutanoni.
CHADEMA
wabadili mbinu
Kutokana na
kuzuiwa kufanya mkutano kwenye viwanja vya Sahara, CHADEMA waliamua
kuufanyia Ubungo kutokana na kuomba vibali viwili kwenye maeneo tofauti.
Baada ya
kuzuiliwa Mabibo, kibali cha Ubungo kilikuwa halali, hivyo Mbunge wa
Ubungo aliyekuwa amefika Sahara kwa ajili ya kuhutubia, aliandamana kwa
miguu na wafuasi wa chama hicho hadi Ubungo, huku kukiwa na makachero
wengi wa polisi waliofuatilia maandamano hayo.
Akizungumza na
wananchi katika mkutano uliofanyika Ubungo, Mnyika alisema polisi
walifanya kitendo cha kikatili, kusubiri watu wamalize maandalizi,
wakusanyike uwanjani ndipo wanaleta barua ya kupiga marufuku mkutano kwa
kisingizio kuwa katika Wilaya ya Kinondoni kulikuwa na ziara ya makamu
wa Rais katika Jimbo la Kawe na Kindondoni.
“Sisi tupo
Ubungo, Makamu wa Rais yupo Kawe na Kinondoni, sasa suala la kuzuia
mikutano isifanyike lilikuwa na maana gani? Kama Jeshi la Polisi
walisema hawana askari wa kutosha kulinda mkutano wetu mbona katika
kuutawanya wamekuja na magari matatu?” alihoji.
Mnyika
alitumia muda mwingi kulilaumu Jeshi la Polisi, kwanza kwa kuahirisha
mkutano muda mfupi kabla ya viongozi kupanda jukwaani, lakini pia
kitendo cha kurushwa bomu mahali ambapo hakukuwepo fujo zozote.
Madudu
zaidi ya CCM
Mwenyekiti wa
CHADEMA, Freeman Mbowe ameendelea kuanika madudu ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), safari hii akitoa nyaraka za mikakati ya chama hicho tawala
kufundisha vijana kukabiliana na wapinzani.
Akihutubia
mkutano wa hadhara juzi katika Viwanja vya Mahakama ya Mwanzo, Nguzo
Nane, mjini Shinyanga, Mbowe alisema kuwa ili kujilinda dhidi ya vitendo
alivyodai wanafanyiwa na vijana wa Green Guards - kikosi cha vijana wa
CCM, chama chao kitaendelea na mipango ya kuwapatia vijana wao mafunzo
ya ukakamavu.
Mbowe
alionyesha nyaraka mbili za CCM zinazoonyesha kuwa chama hicho tawala
kupitia wanachama wa Jumuiya ya Vijana (UVCCM) kimekuwa kikitoa mafunzo
ya ukakamavu kwa vijana wake, huku nyaraka moja ikionyesha kuwa moja ya
malengo ya mafunzo hayo ni kukabiliana na upinzani.
“Tunashambuliwa,
watu wetu wanapigwa, wanateswa, wanatekwa na wengine kuuawa, kwa sababu
tu wanataka mabadiliko na wanapenda CHADEMA, majuzi mlisikia Waziri
Mkuu Pinda anasema wamechoka...sasa tunasema Pinda kama umechoka ondoka
upishe ofisi ya umma hiyo, upishe kwenye ofisi ya watu kama umechoka,
maana kuchoka huko ni kuchoka kwa CCM. Pisheni ofisi sio za kwenu hizo,
ni za Watanzania.
“Wananchi hapa
mkononi nimeshika nyaraka mbili za CCM, moja ni cheti cha kuhitimu
mafunzo na nyingine hapa juu imeandikwa ‘Sera za Msingi za CCM’, sasa mi
sitawasomea, naomba aje hapa jukwaani mtu yeyote anayejua kusoma,
awasomee mjue tunaposema CCM wamekuwa na kikundi kinachoshambulia,
kupiga, kutesa, kuteka na hata kuua Watanzania wenzao eti tu kwa sababu
wanaunga mkono CHADEMA, huwa tunamaanisha nini,” alisema Mbowe.
Mmoja wa
wananchi aliyehudhuria mkutano huo wa hadhara, ambao ulikuwa ni sehemu
ya shughuli za ukamilishaji wa kuzindua Kanda ya Ziwa Mashariki (mikoa
ya Shinyanga, Simiyu na Mara), alipewa kabrasha kubwa na kusoma sehemu
inayozungumzia majukumu ya jumuiya za chama hicho.
Gazeti hili
pia lilifanikiwa kuona kabrasha hilo kwa karibu, ambapo kifungu cha 9.1
kinachozungumzia UVCCM, kinasomeka hivi;
“(i) Umoja wa
vijana wa CCM unapaswa kuwajenga vijana katika itikadi, ukakamavu na
mafunzo yatakayowafanya wajiamini, wawe vijana wenye ari ya kutimiza
wajibu wao wakiwa walinzi wa chama, viongozi na wagombea wa CCM.
“(i) Utaratibu
wa kuandaa makambi ya vijana usimamiwe kwa dhati. Chama kiwe na mipango
mizuri ya kutafuta na kuwateua wakufunzi watakaofaa kuwapatia vijana
mwelekeo unaotakiwa ikiwa ni pamoja na elimu ya uchaguzi/uraia. Mafunzo
ya makambi ya vijana, mbali ya kujifunza nyimbo za hamasa yatilie mkazo
pia mafunzo ya ukakamavu kwa lengo la kukabiliana na vitendo vya kihuni
vya baadhi ya vijana wa vyama vya upinzani.”
Mbowe pia
aliwaonyesha wananchi waliofurika kwenye mkutano huo cheti cha mmoja wa
watu waliohitimu mafunzo ya makambi ya vijana wa CCM ambacho kilionyesha
mhusika alianza mafunzo Juni 27, 2009 na kumaliza Julai 4, 2009, mkoani
Dodoma.
Cheti hicho
kimesainiwa na watu wawili, mmoja mwenye jina la Jumanne Kitundu, akiwa
na nafasi ya Katibu wa UVCCM, Dodoma mjini na mwingine, Robert Mwinje,
Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Wilaya ya Dodoma mjini.
Cheti hicho
kinaonyesha mhusika (jina linahifadhiwa) alihitimu mafunzo ya masomo ya
kanuni ya umoja wa vijana, wajibu wa vijana katika chama, ulinzi na
usalama, ujasiriamali, ukakamavu, wajibu wa vijana katika uchaguzi,
rushwa, ukimwi, historia ya TANU na ASP pamoja na maadili.
Msimamo
wa CHADEMA
Mbowe
alisitiza kuwa CHADEMA kitasimamia azimio la kikao cha Kamati Kuu ya
chama hicho juu ya kuimarisha kitengo chake cha ulinzi na usalama
ikiwemo kuanzisha makambi ya mafunzo ya ukakamavu kwa vijana wa chama
hicho watakaokuwa na jukumu la kulinda viongozi wao.
Ingawa msimamo
huo umekuwa ukipingwa na wadau mbalimbali likiwemo Jeshi la Polisi,
Msajili wa Vyama vya Siasa na CCM, Mbowe amesisitiza kuwa hawatarudi
nyuma juu ya mpango huo utakaoimarisha ulinzi.
Kodi
ya laini za simu
Hoja ya tozo
ya simu imekuwa ajenda kubwa kwenye mikutano iliyofanywa na viongozi
mbalimbali wa CHADEMA.
Mwenyekiti wa
Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA), John Heche alisema kama wananchi
wasingeipa ushirikiano CHADEMA na kupinga maovu mbalimbali, CCM ingekuwa
imeshauza nchi na wananchi wake.
Alisema tozo
la laini za simu lilipitishwa wakati wabunge wa CHADEMA walipokwenda
Arusha kushiriki maombolezo na mazishi ya marehemu wa tukio la bomu,
hivyo serikali ikaona ipeleke jambo hilo lililobarikiwa na wabunge wengi
wa CCM.
“Maana yake ni
nini? Kodi hii kwanza mwananchi maskini kabisa ambaye amedunduliza na
kununua simu, atakuwa analipa sawa sawa na matajiri wakubwa, yaani wewe
hapa utakuwa unalipa kodi sawa na Reginald Mengi...lakini kama hiyo
haitoshi, ukipiga mahesabu utakuwa unalipa kodi takriban shilingi 12,000
kwa mwaka.
“Serikali hii
ya CCM inayowaletea kodi ya sh 12,000 kwa mwaka ndiyo ililazimika
kuondoa na kufuta kodi ya kichwa, baada ya CHADEMA kuwa imefanya hivyo
kwenye halmashauri zake, kwa kuanza na Hai ambako Mwenyekiti Mbowe
alikuwa ni mbunge na Karatu kwa Dk. Slaa. Sasa walifuta kodi ya
manyanyaso ya kichwa kwa maelekezo ya CHADEMA iliyokuwa sh 3,000 kwa
mwaka, ambapo watu walikuwa wanakimbia nyumba na kujificha maporini,
wengine wakaliwa na wanyama, sasa wanataka mlipe kimya kimya, sh 12,000
kwa mwaka. Ni matokeo ya kushindwa kwa sera za CCM,” alisema Heche.
Mkutano
wa Geita
Wabunge wa
CHADEMA wanaotoka Kanda ya Ziwa na viongozi wa chama hicho nao
waliendelea kufanya mikutano katika maeneo mbalimbali huku wakilalamikia
tozo la laini za simu pamoja na mapendezo ya rasimu ya katiba mpya
yaliyotolewa na CCM hivi karibuni yakipinga mambo mengi yaliyopendezwa
na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Jana, wabunge
hao wa viongozi walifanya mikutano ya hadhara katika mji wa Kasamwa huko
Geita na Sengerema mkoani Mwanza ambako walisema CCM imekosa sifa ya
kuongoza ndiyo maana maisha ya Watanzania yamezidi kuwa magumu kadiri
siku zinavyokwenda mbele.
Wabunge hao
pamoja na viongozi na makada wa CHADEMA ambao wapo kwenye msafara wa
kuimarisha chama katika kanda hiyo, ni pamoja na Ezekiel Wenje (Mbunge
wa Nyamagana), Profesa Kulikoyela Kahigi (Bukombe), Dk. Anthony Mbasa
(Biharamulo Magharibi) na Conchesta Rwamlaza (Viti Maalumu – Kagera).
Viongozi na
makada wengine ni pamoja na mjumbe wa Baraza Kanda ya Ziwa Magharibi,
Anwar Kashaga, katibu wa CHADEMA Manispaa ya Bukoba, Lenatus Kilongozi
pamoja na Mwenyekiti wa Wilaya ya Biharamulo Magharibi, George Kasaiza.
Akizungumza
kwenye mikutano hiyo, Wenje alisema CHADEMA inatarajia kuunda mabaraza
ya wananchi kuhusu muundo wa serikali tatu, na wanatarajia kukusanya
saini za Watanzania kupinga tozo ya kodi mpya ya laini za simu
iliyopitishwa hivi karibuni bungeni.
Alisema kwa
sasa CCM wametoa mapendekezo ya kutaka kusiwepo uwazi wa mikataba,
maadili ya umma na haki za binadamu kwenye katiba mpya, na inataka Spika
wa Bunge lazima atokane na mbunge, jambo aliloliita ni kuendeleza
ukandamizaji kwa wananchi.
“Wakati
CHADEMA tunataka spika na mawaziri wasitokane na wabunge, CCM wao
wamependekeza viongozi hao watokane na wabunge ili waendelee
kuwakandamiza Watanzania. CHADEMA tunataka nchi iwe na mawaziri saba tu,
na siyo 15 wa pendekezo la tume na 64 waliopo sasa.
“Si hilo tu,
ibara ya 22 hadi 23 ya rasimu ya katiba mpya, CCM kwa mapendekezo yao
wanataka haki za binadamu zisiwepo kwenye katiba mpya ijayo, bali ziwepo
kwenye sheria tu. CCM haitaki kuwepo malengo ya taifa kwenye katiba
mpya!
“Tutakusanya
saini milioni 10 za wananchi kuhusu mapendekezo ya katiba mpya. Pia
tutakusanya saini milioni tano za wananchi kutaka tozo ya laini za simu
ifutwe,” alisema Wenje huku akisisitiza uundwaji wa serikali tatu;
Tanganyika, Zanzibar na Shirikisho.Mbunge wa Biharamuro Magharibi, Dk.
Mbasa, mbunge Conchesta, Katibu wa CHADEMA Manispaa ya Bukoba, mjumbe wa
Baraza Kanda ya Ziwa Magharibi, Anwar pamoja na mwenyekiti wa chama
hicho Biharamulo Magharibi, Kasaiza waliishutumu serikali kwa kushindwa
kuwaondolea umasikini wananchi wake.
Walisema kwa
sasa Watanzania walio wengi wanalazimika kuvaa viatu vya ‘yebo yebo’ kwa
sababu ya umasikini unaotokana na kushindwa kwa Serikali ya CCM
kuwatumikia wananchi wake kwa kuwanufaisha na rasilimali zilizopo hapa
nchini.
“Serikali ya
chama tawala imekosa sifa ya kuwaongoza wananchi. Tunahitaji tuungane
wote kuiondoa CCM mwaka 2015. CHADEMA ni mkombozi wa Watanzania na ndiyo
maana wabunge na viongozi wake wanapambana usiku na mchana kutwa
kupigania maendeleo ya wananchi,” alisema Dk. Mbasa.
Chanzo: CHADEMA Social Media.
No comments:
Post a Comment